Marahaba, Bwana Rwaka. Nakushukuru kwa kuniuliza swali hilo, kutokana na makala yangu kuhusu neno "Mwanamajumui", uliyoyasoma kwenye ukurasa wa mtandaoni wa Kiswahili Kina Wenyewe. Na namshukuru Sheikh Khamisi Mataka kwa kunisaidia kulijibu, kabla ya mimi kupata nafasi ya kulijibu. Natumai umetosheka na maelezo yake mazuri. Kwa hivyo, sitakuwa na mengi ya kuongeza isipokuwa haya machache yafuatayo.
Umeniuliza maswali mawili. Mosi, hilo neno "harufu" ulilolisoma kwenye makala hayo (ambalo kwa Kiswahili Sanifu huandikwa "herufi") ni la lahaja ipi? Umeeleza kuwa neno hilo ni jipya kwako, kwa sababu ulijualo wewe ni hilo "herufi". Na, pili, umeniuliza kwenye lahaja hiyo neno "harufu" lenye maana ya "smell" kwa Kiingereza, huandikwaje?
Naanza kwa kulijibu swali la pili. Jawabu yake ni kwamba huandikwa vivyo hivyo - "harufu".
Na jawabu ya swali lako la kwanza ni: hilo "harufu" si neno la lahaja yoyote fulani ya Kiswahili, bali hivyo ndivyo lilivyokuwa likiandikwa na Waswahili wa sehemu zote za Uswahilini. Ukitaka kulithibitisha hilo, tafuta maandishi ya zamani ya Kiswahili - kwa mfano, ya barua za watu binafsi au ya nyaraka rasmi - zilizokuwa zikiandikwa kwa hati za Kiarabu. Baadhi ya hati hizo za Kiarabu zilifanyiwa marakibisho na Waswahili wenyewe ili zilingane na sauti za maneno ya Kiswahili. (Miongoni mwa lugha nyengine zilizoanza kuandikwa kwa kutumia hati za Kiarabu zilizorakibishwa na wenye asili na lugha hizo ili zilingane na matamshi ya lugha zao ni Kiurdu, (Pakistan ya leo), Kifursi (Iran ya leo), na Kihausa (Nigeria)). Natumai waelewa kwamba hati za Kiarabu ndizo zilizotumiwa na Waswahili kwa karne nyingi kuandikia lugha yao, kabla ya hizi hati za Kirumi (Kilatini) kutumiwa huku katika karne ya 19.
Hili neno "herufi", kama liandikwavyo katika hichi kiitwacho Kiswahili Sanifu, ni matokeo ya baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa na hao Wazungu (wengi wao maafisa wa kikoloni) waliojipa madaraka ya kuiwekea lugha hii kanuni za kisarufi na za kimaandishi, mara nyingi bila ya kuwahusisha au kuwataka shauri wenye lugha yao (au hata Mwafrika mwengine yoyote yule) kwa zaidi ya miaka kumi ya mwanzo.
Kutokana na urathi huo wa kikoloni wa kulazimishwa kuzifuata hizo kanuni, ambazo wenyeji hawakuwa na kauli au hiari nazo, ndipo leo katika Kiswahili Sanifu kukawa kwaandikwa "herufi" badala ya "harufu". Mifano mengine ya maneno waliyoyabadilisha jinsi
ya kuandikwa kwake ni ilimu (elimu), hishima (heshima), hishimu (heshimu), hikima (hekima), tafauti (tofauti), sharia (sheria), hisabu (hesabu), sirikali (serikali), rakibisha (rekebisha), marakibisho (marekebisho), na mengi mengineyo. Na hivi leo atokeapo mtu akayaandika au akayatamka maneno kama hayo kama yalivyokuwa yakitamkwa na kuandikwa na wenyeji wenyewe, huonekana ni kitushi kikubwa, au amefanya madhambi makubwa!!
Najua kwamba, kwa sababu zao mbalimbali, si watumiaji wote wa Kiswahili hivi leo watakaokuwa tayari - hata kwa kufikiria tu - kukubali kuyatamka au kuyaandika kama hivyo yalivyokuwa yakitamkwa na kuandikwa na wenyeji wa lugha hii, kabla ya mwaka 1930 kilipobuniwa Kiswahili Sanifu. Najua pia kwamba si rahisi kurudi tulikotoka, au kujikomboa kiakili na kuyang'oa yaliyokita mizizi katika mabongo ya baadhi yetu kuhusu hichi tukiitacho Kiswahili Sanifu.
Swali ambalo huwa najiuliza ni hili: Ikiwa tulipigania kuzikomboa nchi zetu kisiasa (ingawa bado hatujafaulu), na ikiwa twajitahidi tuzikomboe nchi zetu kiuchumi (ingawa bado hatujafanikiwa kuwa na mikakati madhubuti), basi kwa nini twaona uzito kukikomboa Kiswahili kutokana na baadhi ya minyororo ya kikoloni? Kama nilivyotangulia kueleza, haitawezekana kurudi tulikotoka - kwa sababu mbalimbali. Lakini naamini kuwa sote tukitumiao Kiswahili sasa twafaa kuanza kujadiliana kuhusu hii fikira ya kwamba ni lazima kuwa na aina moja tu ya Kiswahili Sanifu. Na hili litakuwa si bina kwa Kiswahili. Kwa mfano, hakuna aina moja ya Kiingereza Sanifu: Waingereza wana chao, Wamarekani wana chao, Waaustralia wana chao. Kwa nini, basi, tusikubaliane kuwa maneno "hishima", "ilimu", "tafauti", na hayo mengineyo, ni Kiswahili Sanifu pia?
- Abdilatif Abdalla
Hamburg, Ujerumani
15 Aprili, 2021
Assalaamu alaykum tena, Prof. Abdulaziz Lodhi. Katika maoni yako uliyoniandikia kuhusu "wimbo" na "nyimbo" ulinieleza kwamba "...baadhi ya wasemaji wa jadi wa Kiswahili hawatafautishi baina ya vitenzi vya 'ku-kua' na 'ku-wa'. Badala ya kuandika k.m. 'Alikuwa amelala wanaandika 'Alikua amelala' ".
Kama tujuavyo, katika kanuni za uandishi za Kiswahili Sanifu, maneno haya mawili huendelezwa kwa namna mbili tafauti ili kutafautisha maana zake. Kwa hivyo, "kua" likawa na maana ya _grow_ na "kuwa" likawa na maana ya _to be_. Lakini wasanifishaji hao walioyawekea kanuni hiyo maneno hayo hapo mwaka 1930, hawakuifuata kanuni yao hiyo katika maneno mengine ili kutafautisha maana zake. Kwa mfano, katika Kiswahili Sanifu kwaandikwa "ua" kwa maana ya _kill_, _flower_ na _fence_; au "jua" kwa maana ya _know_ na _sun_; au "pua" kwa maana ya _nose_ na aina ya madini ya chuma.
Lakini tukitizama jinsi maneno hayo (kwa maana zake zote) yalivyokuwa yakiandikwa na Waswahili wenyewe kwa harufu za Kiarabu, kabla ya Kiswahili kuandikwa kwa hizi harufu za Kilatini, tutaona yalikuwa yakiandikwa hivi: "kuwa" (كُوَ), "uwa" (اُوَ), "juwa" (جُوَ), na "puwa" (پُوَ). Kwa ufupi, maneno yote kama hayo yalikuwa yakimalizika kwa -*wa* (وَ) na hayakuwa yakimalizika kwa -*a* (اَ) pekee. Mtu aweza kuyaona haya akizitizama nyaraka za kale, au hata za hivi karibuni, zilizoandikwa kwa harufu hizo.
Kuhusu hayo maneno mengine uliyoyataja yanavyoandikwa leo katika Kiswahili Sanifu, nakuletea haya maoni yangu hapa chini?niliyoyaandika zaidi ya mwaka mmoja unusu uliopita kulijibu swali nililoulizwa kwenye kikundi kimojawapo cha Kiswahili cha WhatsApp.
Abdilatif Abdalla: Kwa ruhusa ya rafiki yangu, Prof. Abdulaziz Lodhi, hapa chini nawaletea maoni yake aliyoniandikia baada ya mimi kumpelekea yale maelezo yangu niliyoyaleta kwenye ukumbi wetu huu kuhusu matumizi ya maneno "wimbo" na "nyimbo." Natumai maoni yake hayo aliyoniandikia, pamoja na jawabu zangu, yatasaidia kuuendeleza mjadala huo.?
Abdilatif Abdalla: Ustaadh 'Atifu, Nakutakieni nyote Mwaka Mpya Mwema!
Shukran kwa maelezo yako ya kitaaluma kuhusu "wimbo/nyimbo" n.k..
Katika matumizi ya Kiswahili chetu cha Kijiweni (kilahaja cha Kimjini, cha Kiunguja Mjini) twasema k.m. "nyimbo nzuri moja yake" na "nyimbo nzuri mbili zake" (Nomino za Ngeli za 9/10. Hoyo ni Kifasaha. Ndivyo nimelelewa nacho Kiswahili cha kwetu. Na hata jamaa zetu wa Mwambao walikuwa wanasema hivyo.
Lakini skuli tulifundishwa "wimbo mzuri mmoja wake/nyimbo nzuri mbili zake" n.k. (Nomino za Ngeli za 11/10). Hiyo ni Kisanifu.
Pili, watu wengi, hata baadhi ya wasemaji wa jaddi wa Kiswahili, hawatafautishi baina ya vitenzi vya "ku-kua" na "Ku-wa". Badala ya kuandika k.m. "Alikuwa amelala." wanaandika "Alikua amelala."
Yako na makosa mengineyo (kama "rekebisha" badala ya "rakibisha" na "hutuba" badala ya "hutuba" ambayo nitayaeleza kesho au kesho kutwa.
Wasalaam!
Abdulaziz Lodhi
Uppsala, Uswidi.
Abdilatif Abdalla: Assalaamu alaykum. Ahsanta (ahsante) sana, Prof. Abdulaziz Lodhi, kwa salamu za mwaka mpya wa 2022. Allah Aujaaliye uwe na kheri nasi kuliko ulivyokuwa mwaka uliopita.
Nimefurahi mno kupata maoni yako kuhusu niliyoyaandika jana. Hii ni hishima kubwa kwangu: kwamba uliziweka kando shughuli zako muhimu
na kuniandikia. Nakushukuru mno.
Nakubaliana nawe kwamba wako wasemao "nyimbo" kwa hali ya umoja na kwa wingi pia - kama nilivyoeleza katika hayo maoni yangu ya jana. Na nakubaliana nawe pia kwamba wako hata baadhi ya "jamaa zetu wa Mwambao" walitumiao neno hilo hivyo. Bali kwa jinsi idadi ya walitumiao neno "nyimbo" kwa umoja na kwa wingi inavyoongezeka sana, huenda baada ya miaka michache hilo "wimbo" likapotea kabisa! Hata hivyo, kwa hivi sasa hatufai kulinyima haki yake, maadamu wako walitumiao - wangawa wachache.
Naona kama nakukosea adabu (na nakuomba uniwie radhi) nisemapo kwamba, kama ujuavyo, kuna tafauti za matumizi, matamshi na maana, za baadhi ya maneno hayo hayo ya Kiswahili fasaha - hata miongoni mwa "jamaa zetu wa Mwambao". Kwa vile wewe ni msomi wa miaka mingi mno na ni mwanataaluma mbobezi wa isimu na lugha ya Kiswahili(kinyume na mimi ambaye si mwanataaluma wala si msomi, bali nimeokotezaokoteza kichache tu barabarani) huhitaji kuelezwa nami tafauti hizo. Lakini kwa madhumuni ya kujirahisishia mimi mwenyewe haya maelezo yangu, kwa mifano michache ya haraka haraka, kuna "jamaa zetu wa Mwambao" ambao katika Kiswahili chao fasaha husema nipa, amkua (ambalo kwa wengine "amkua" lina maana ya ita); inua, ufuo, embe hili, (maembe haya); ilhali wengine wa Mwambao husema nipe, amkia, nyanyua (neno ambalo kwa hao wa mwanzo lina maana ya kuchana au kurarua), ufukwe au ufuko (neno ambalo kwa hao wa mwanzo lina maana ya sehemu inayochimbwa ndani ya nyumba, chini ya kitanda cha kuoshea maiti, ili maji anayooshewa maiti yaingie humo); na embe hii (embe hizi).
Kwa hivyo, hilo neno "nyimbo" kutumiwa na baadhi ya watu kwa umoja na kwa wingi pia, laweza kutiwa kwenye mkumbo wa tafauti kama hizo za Kiswahili fasaha kitumiwacho na "jamaa zetu wa Mwambao".
Umenieleza katika hayo maoni yako kwamba neno "wimbo" kuwa ni umoja wa "nyimbo" ulifundishwa skuli; kwa hivyo, kwa maoni yako, ni athari ya Kiswahili Sanifu. Mimi nami tangu nilipokuwa mtoto mdogo nilikuwa nikilisikia neno "wimbo" likitumiwa nyumbani kwetu na wazazi na wazee wangu wengine, kuwa ni umoja wa "nyimbo. Na wao hawakupata kusoma skuli. Kwa hivyo, hawakuwa wakilitumia hivyo kutokana na athari za skuli au Kiswahili Sanifu. Hata ile misemo miwili niliyolitolea ushahidi neno "wimbo" (yaani "Wimbo hutokea ngomani" na "Wimbo muwi hauongolewi mwana") ni misemo ya kale sana ya Kiswahili, ambayo ikitumika kabla ya kubuniwa hicho Kiswahili Sanifu mwaka 1930.
Kwa mara nyengine tena, nakushukuru sana ndugu yangu kwa kuniandikia na kunipa maoni yako.
Wassalaamu alaykum.
Panga lilokata shina, kukata tawi katiti
Usivimbe na kutuna, kwa kuwekwa juu ya mti
Mpanga yote Rabana, usinajisi bahati
Waziviza zako hati, kulumba yaso maana
Kiburi si maungwana, hapa nazikaza nati
Nasema niloyaona, sisemi ya hatihati
Aliye hai mchana, usiku ndiye maiti
Nanena nao umati, nami mumo pasi kona
Vikombe vinagongana, viwapo kwenye kabati
Nakuambiya bayana, na vi tele vizibiti
Lililo m’bwaga jana, mgema ni lile kuti
Ola chako kizingiti, na mazoea achana
Pokea yangu semina, usinilipe senti
Ni ada kukumbushana, katika hizi nyakati
Nataka tujezikana, sisi wa moja baiti
Endeleza harakati, ulitunze lako jina
Kwa kheri ya kuonana, naivua helmeti
Tambua utu hazina, na matendo hasanati
Na changi kuchangizana, njoo tukutane kati
Usinipige manati, siyo vyema kugombana