WACHAGA
Usuli
Wachaga ni kabila la watu wenye asili ya Kibantu lakini pia mchanganyiko wa damu, hasa ya Kikushi wanaoishi kaskazini mwa Tanzania chini ya mlima Kilimanjaro, mkoani Kilimanjaro.Shughuli kubwa ya Wachaga ni biashara, kilimo na kazi za ofisini.Wachaga ni kabila la tatu kwa ukubwa nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2003 zinaonyesha kuwa idadi ya Wachaga ni watu 2,000,000.
Vikundi vya Wachaga
Wachaga wana historia ndefu ya asili yao na ya maingiliano yao na makabila mengine. Kabila la Kichaga ni mkusanyiko wa makabila madogomadogo (ya Kichaga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia mashariki (Tarakea, Rombo) hadi magharibi kwa Kilimanjaro (Siha, Machame).
Makabila ya Kichaga ni Wa-Rombo, Wa-Vunjo ambao wanajumuisha watu wa Mwika, Mamba, Marangu, Kilema na Kirua ambayo ndio inajulikana na wengi kama Kirua Vunjo. Ukipenda unaweza kuwagawa watu hawa wa Vunjo kama Wa-Mwika, Wa-Mamba ,Wa-Marangu,Wa-Kilema,na Wakirua.Makabila mengine ni Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, na Wa-Machame, Wa-Uru, na Wa-Siha.
Lugha ya Kichaga
Lugha ya Kichaga inabadilika kuanzia unapotoka Tarakea mpaka unapofika Siha magharibi mlima Kilimanjaro.
Kutokana na tofauti hizo Kichaga kimegawanyika katika Kirombo (ambacho nacho kinatofautiana kadiri unavyotoka eneo moja hadi jingine; mfano Kisseri, Kimashati, Kimkuu, Kimengwe, Kimahida), Kivunjo, Kimarangu, Kirombo, Kioldimoshi, Kingassa, Kiuru, Kikibosho, Kimachame na Kisiha.
Lugha hizo zinakaribia kufanana kadiri makabila hayo yalivyopakana. Kwa mfano, Kivunjo kinafanana na Kioldimoshi. Vile vile Kisiha kinafanana sana na Kimachame ambacho pia kinafanana kidogo na Kikibosho.
Baadhi ya Wamachame walihamia sehemu za Meru, Arusha, na kuchanganyikana na Waarusha, hivyo lugha yao ikabadilika kidogo na kuwa Kimeru. Kwa sababu hiyo Wameru wanasikilizana sana na Wamachame ingawa lafudhi zao zinatofautiana kidogo.
Koo za Kichaga
Majina ya kiukoo ya Kichaga pia huashiria wanatoka sehemu gani ya Uchaga, japo si lazima kuwa hivyo: kwa mfano, familia maarufu za Kichaga nchini Tanzania ni kama ukoo wa akina Mushi, Mmasy Kimaro, Swai, Massawe, Lema, Urassa, Nkya, Ndosi, Meena hutoka Machame.
Akina Temu, Mlaki, Mlay, Lyimo, Moshiro, Mselle, Kamnde, Kileo, Kimambo, Tesha, Msaki, Assey, Kyara, Kessy, Ndanu, Macha, Mbishi, Kombe, Njau wanatoka Old Moshi na Vunjo.
Majina mengine ya Old Moshi ni kama yafuatayo: Mmari, Macha, Mshiu, Kyara, Moshi, Massamu, Kimambo, Mboro, Mlngu, Saule,Tenga, Njau, Malisa, Maro, Maeda, Ringo,Olomi, Ngowi, Lyatuu na mengine mengi.
Kavishe, Mariki, Tarimo, Laswai, Mallya, Mrema, Mkenda, Massawe, Silayo, Lyaruu, Makyao, Mowo, Lamtey, Tairo, Masue, Maleto, Mramba, Kauki wanatoka Rombo.
Sawe, Usiri, Shayo, Kiwelu, Makundi, Urasa, Mtui, Moshi, Meela, Minja, Njau,Mtei wanatoka Marangu na Kilema.
Rite, Makule, Minja, Mashayo, Chao, Shao, Makawia, Ndesano, Kimario, Tilla, Mariale, Tarimo, Mafole, Kituo, Mrosso, Lyakundia, Kessy, Mmbando, Matemba, Ndenshau, Morio, Akaro, Matowo, Towo, Mkony, Temba, Foya, Munishi, Kilawe, na kadhalika hutoka Kibosho.
Ukoo wa akina Teri wako Mamba, Chami, Chuwa, Kiria Owoya na wachache Sango, Old Moshi na wengine walihamia Maji ya Chai, Mkoa wa Arusha.
Utawala wa jadi wa Wachaga
Watawala wa Kichaga waliitwa “Mangi”. Hawa walihodhi mashamba, ng’ombe na waliheshimiwa kama viongozi wa kikabila. Walikuwa na nguvu za kisiasa na utajiri. Baadhi ya Ma-mangi mashuhuri katika historia ni kama Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (Wajerumani), Mangi Sina wa Kibosho na Mangi Horombo wa Keni – waliojulikana kwa uhodari wao wa vita katika kupigana na Wamachame na kupora ng’ombe na mazao yao, hata mpaka leo makabila ya Kimachame na Kikibosho hayaoani kwa urahisi, na Mangi Marealle wa Marangu na Vunjo. Mangi Meli huyu alikuwa mangi wa waoldmoshi ambaye alipigana na wajerumani na aliishia kukatwa kichwa na mpaka sasa kichwa chake kipo ujerumani alizikwa kiwiliwili tuu baada ya kumnyoga na mti aliyonyongewa upo mpaka sasa sehemu ya oldmoshi bomani karibu na kolila sekondari .
Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na viongozi hawa wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia ndugu na watoto wa Ma-mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika serikali za kwanza. Hawa pia wanaaminika walikuwa kama mabepari wa kwanza wa kijadi, maana walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao Ma-mangi wamekaa kuhesabu mali zao.
Usemi maarufu wa “u-Mangi-meza” nadharia inawezekana kuwa umetokana na watawala hawa wa Kichaga.
Elimu kati ya Wachaga
Wachaga wanajulikana kwa uwezo wao mkubwa katika uwanja wa elimu, hususani katika masomo ya sayansi na hisabati. Moshi ni maeneo ya mwanzo ambayo wamisionari wa Ukristo walijenga makanisa na shule.
Sababu hii imefanya Wachaga kuwa kabila namba moja lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa (elimu ya juu) na mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania. Kulingana na takwimu za elimu mkoa huo una shule za sekondari zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.
Shule nyingi za sekondari ziko katika mkoa huu kwa sababu zifuatazo: 1) Hali ya hewa na vivutio vya kitalii katika mkoa huu viliwavutia zaidi walowezi na wakoloni na kuweka makazi yao hapo. Hivyo wamisionari walijenga shule za kwanza wakifuatiliwa na serikali za wakoloni 2) Serikali ya Tanzania ilirithi shule zilizojengwa na wakoloni 3) Wachaga waliobahatika kupata fedha binafsi baadaye waliwekeza kwenye ujenzi wa shule binafsi kama kitega-uchumi, wakati wakazi wa mikoa mingine kadhaa walisubiri serikali iwajengee shule. 4) Ukichanganya sababu 1, 2 & 3 utagundua shule katika mkoa wa Kilimanjaro zimezidi sana idadi ya shule katika mikoa mingine yote.
Ni vema pia kusema kuwa shule hizo huvutia wanafunzi kutoka Tanzania nzima, haziwasomeshi Wachaga tu.
Ardhi
Ingawa ardhi ni msingi wa maendeleo kwa watu wote, kwa Wachaga, ardhi ni mali sana kwa sababu kilimo chao ni cha mazao ya kudumu kama kahawa na ndizi hukaa shambani kwa muda wa miaka mingi.
Mojawapo ya urithi wapewayo watoto ni “kihamba”. Hii ni sehemu ya ardhi ambayo mtoto anategemewa atajenga na kuanzisha familia yake. Bahati mbaya watoto wa kike walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawanaji wa vihamba. Uhabawa ardhi huko Uchaga ulipelekea Wachaga wengi kuhamia mikoa mingine. Hivi leo utakuta Wachaga wakiishi Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya n.k. wakiwa wamepanda migomba yao na kuendesha biashara za maduka ya vyakula.
Ukienda kwenye mikoa hiyo utakuta wamejenga jamii zao na vyama vyao vya kusaidiana wakati wa sherehe au matatizo. Aidha hata pombe ya mbege utaweza kuikuta kwenye makusanyiko ya Wachaga katika mikoa mbalimbali.
Kilimo na chakula
Wachaga hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, maharagwe, viazi, ndizi, ulezi na mboga mbalimbali. Pia mazao ya biashara kama vile kahawa, nyanya na vitunguu.
Ndizi za Wachaga
Ingawa Wachaga wa leo wanakula vyakula mbalimbali kama vile ugali, wali na viazi, chakula kikuu cha Wachaga ni ndizi.
Kuna ndizi za aina mbalimbali na kwa matumizi tofauti. Mfano ndizi sukari ni fupi na huachwa hadi ziive na huliwa mbivu kama tunda.
Ndizi mshale hukatwa zikiwa mbichi na kupikiwa vyakula mbalimbali pamoja na nyama ya ng’ombe, kondoo au mbuzi. Mara nyingine hupikwa na maharage, choroko, kunde au hata maziwa ya mtindi. Vyakula vya ndizi huja kwa ladha tofauti kama vile ndizi nyama, mtori, machalari, kiburu na kadhalika.
Aina nyingine ni ndizi ng’ombe ambazo huachwa ziive halafu humenywa na kutumiwa kutengenezea pombe maarufu iitwayo mbege. Mbege hutengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, maji, na ulezi.
Aina nyingine ni ndizi mzuzu. Hizi zikikomaa huachwa zianze kuiva kidogo halafu huchomwa na kuliwa kama kitafunwapamoja na chai au pombe. Ukipita mitaa ya Dar es Salaam utaona ndizi mzuzu zikichomwa sambamba na muhogo au kuku vumbi au kiti moto.
Wachaga na muhogo
Inasemekana kuwa “Mchagga halisi hali muhogo – akila muhogo atakufa”. Usemi huu umetokana na historia ya mababu kuwa Wachaga waliopanda mihogo Kilimanjaro enzi za kale walikufa baada ya kuila. Historia hiyo yaweza kuwa ya ukweli kwa sababu aina nyingi za mihogo zinajenga sumu ya sianidi ndani yake; watu waliozoea kutumia mihogo huwa na njia za kuondoa sumu kwa kuiloweka mihogo katika maji kwa muda. Lakini kama Wachaga wale wa zamani, hasa wa Machame, walifanya jaribio bila kujua mbinu ya kuondoa sumu, ajali iliweza kutokea. Cha kushangaza ni kwamba hukohuko Kilimanjaro, majirani na watani wa Wachaga, yaani Wapare, walikuwa wameshazoea mihogo na ilikuja kuwa moja ya chakula chao kikuu.
Ulaji kiti-moto
Pamoja na kilimo cha mazao, Wachaga hupendelea sana kufuga nguruwe. Tabia ya kula nyama ya nguruwe ijulikanayo leo kwa jina la “kiti moto” ni moja ya mambo yaliyoenezwa na Wachaga. Ulaji wa “kiti moto” haukuwa pendeza baadhi ya wenyeji wa Pwani kama Dar es Salaam ambapo Wachaga walihamia, kwani wakaaji wengi wa Pwani ni Waislamu kwa hiyo nguruwe kwao ni haramu. Wakazi wa Dar es Salaam watokao makabila mengine na wasiyo Waislamu kwao kula nguruwe ilikuwa “ruksa”.
Maoni juu ya Wachaga
Ingawa wanaume wa Kichaga hupendelea kufanya kazi mbali na kwao, wake zao hukaa nyumbani (Moshi) na hufuga ng’ombe na kazi za shambani. ila kwa sasa kutokana na ugonjwa wa ukimwi tabia hii imepungua miongoni mwao.
Wanawake wa Kichaga (hasa kutoka Machame) hujulikana kama wafanyakazi hodari. Huchangia sana katika mapato ya nyumbani na chakula.
Ingawa kipato cha Wachaga ni kikubwa kulingana na cha makabila mengine, takwimu zinaonyesha watoto wa mkoa wa Kilimanjaro kuongoza kwa utapiamlo. Sababu kubwa ya watoto kuwa na utapiamlo ni wazazi kujali zaidi kazi kuliko muda wa kuwahudumia watoto.
Wengi wa watoto hao ni wale ambao wazazi wao ni watu wa pombe na kipato chao kinaishia kilabuni. Utaona kwamba Uchagga una vilabu vingi vya pombe na vinaongezeka kwa sababu imekuwa biashara kubwa. Karibu kila kaya kumi na tano kuna kilabu cha pombe na kiwango cha chini kabisa cha pombe inayouzwa kwa siku katika vilabu hivyo si chini ya madebesita au lita mia moja. Pombe ni sababu moja ya watoto kuwa na utapiamlo.
Hii inawezekana kuwa matunda ya wazazi kutowalisha watoto wao chakula cha kutosha au chakula bora. Kuna sehemu nyingine za Uchagga kama Old Moshi na Kibosho ambapo watoto wadogo hupewa pombe ya mbege asubuhi, mchana na jioni.
Sababu nyingine ni kazi; mama wa Kichaga anaweza kushinda shambani kutwa na hana desturi ya kubeba watoto mgongoni kwenda nao shambani, hivyo wanakuwa nyumbani ama wenyewe au na mayaya. Mfano ulio dhahiri ni nyakati za asubuhi na mapema kwenye vyombo vya usafiri karibu robo tatu ya abiria ni wanawake wakienda katika shuguli za biashara na kilimo na vivyo hivyo nyakati za jioni wakirudi majumbani. Hao ni nje ya wale wanaotumia usafiri wa miguu ambao ni wengi zaidi.
Pia baadhi ya kina mama wa Kichaga wanawajali waume zao zaidi kwani nyama nzuri ni ya baba. Kuepuka gharama baba ataandaliwa chakula kizuri, tofauti na chakula walichoandaliwa watoto, japo ni chakula kilekile.
Pia Wachaga wamekuwa na desturi ya kuwaenzi wazee wao waliotangulia mbele za haki kwa kuwatambikia kwa pombe na nyama za mbuzi pale tu wanaporudi nyumbani ifikapo mwezi Desemba. Hili limekuwa suala la kawaida sana na halipingiki. Wengi wao huwa wanarudi na magari, ndiyo sababu utaona ya kwambwa kila ifikapo mwezi Desemba kila mwaka foleni za magari zimekuwa zikiongezeka kutokana na Wachaga kurudi nyumbani msimu wa sikukuu. Wengi wao wamekuwa wakitoka sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.
Wachaga wengi hupenda kurudi nyumbani kipindi cha Krismasi, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu.
Ingawa wengi hudhani kwamba Wachaga wamepokea sana dini [imani] ya Ukristo kwa kuwa wengi wao ni Wakristo na hiki huwa ni kipindi cha likizo kwao, inaaminika pia kuwa kurudi kwao Uchagani wakati wa Krismasi ni pamoja na kutembelea ndugu zao na kujumuika pamoja katika kuumaliza mwaka baada ya kazi nyingi za kutafuta pesa mwaka mzima.
Pia imekuwa kama desturi wanaukoo kukaa pamoja na kujadiliana mambo jinsi yalivyokwenda katika kipindi kizima cha mwaka na wakati mwingine inakuwa sehemu ya kwenda kuwatambulisha watoto kwa bibi na babu zao, hasa wale waliozaliwa mijini.
Dola Ya Wachaga
Wakati wazungu wanagawana bara la Afrika, walipokuja walikuta baadhi ya maeneo kuna tawala zenye nguvu, zilizokua na mfumo rasmi wa uongozi. Wao waliziita tawala za jadi (Chiefdoms).
Moja ya tawala iliyokua na nguvu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ni dola ya Wachaga (Chagga state). Zilikuwepo nyingine zenye nguvu kama Himaya ya Sultani wa Zanzibar, Dola ya Buganda, Nyamwezi, Ngoni, Haya, Hutu, Tutsi na Hehe,
Dola ya Wachaga imetamalaki eneo la pembezoni mwa mlima Kilimanjaro kuanzia maeneo ya Rongai hadi Siha.
Eneo hili lilikua na mtawala mkuu mmoja (aliyeitwa Mangi Mkuu). Huyu alikua kama Rais ama Mfalme wa jamii hiyo. Chini yake walikuwepo watawala wakuu wawakilishi wa majimbo. Hawa waliitwa ‘Mangi Waitori’. Chini yao walikuwepo watawala wa wa maeneo madogo, hawa waliitwa Mangi kama vile Mangi Meli wa Old Moshi, Mangi Sina wa Kibosho, Mangi Salakana wa Useri.
Kwa mfano eneo kama Rombo lilikuwa na Mangi wengi. Alikuwepo Mangi wa Keni, Mangi wa Mashati, Mangi wa Mengwe nk. Lakini wote waliunganishwa na Mangi Mwitori wa Rombo.
Vivyo hivyo katika maeneo ya Kibosho, Machame, Siha, Old Moshi, Marangu nk.
Mangi mdogo aliripoti kwa Mangi Mwitori. Mangi Mwitori naye aliripoti kwa Mangi Mkuu aliyeunganisha Wachaga wote.
Kwa mfano kufikia mwaka 1953 Mangi Mwitori wa Vunjo alikua Petro Itosi Marealle, Mangi Mwitori wa Hai alikua Abdiel Shangali, Mangi Mwitori wa Rombo alikua James Selengia Kinabo kabla ya kustaafu mwaka 1952 na John Maruma kuchukua nafasi yake.
Mangi Mwitori alichaguliwa na wamangi wadogo. Kisha wamangi wadogo na wamangi waitori waliunda baraza kuu la uongozi (Supreme council) ambalo lilimchagua Mangi Mkuu.
January 1952 kulifanyika uchaguzi wa kumchagua Mangi Mkuu wa Wachaga. Wagombea walikua watano. Abdieli Shangali wa Machame, Jackson Kitali wa Mbokomu (Old Moshi), Petro Marealle wa Vunjo, John Maruma wa Rombo, na Thomas Marealle wa Marangu.
Baada ya kila mgombea kunadi sera zake, hatimaye kura zilipigwa na Mangi Thomas Marealle kutangazwa mshindi, akifuatiwa kwa mbali na ndugu yake Mangi Petro Itosi Marealle, aliyekuwa Mangi Mwitori wa Vunjo.
Mangi Mkuu ndiye aliyekuwa Kiongozi mkuu wa dola ya Wachaga. Baraza la uongozi (Supreme council) ndicho kilikua chombo cha juu kinachosimamia utendaji wa serikali.
Kwahiyo Mangi mkuu alijitahidi sana kushirikiana mangi waitori na mangi wadogo kuhakikisha jamii nzima ya Wachaga inajiletea maendeleo.
Kila Mangi alikua na baraza lake la ushauri lililojulikana kama ‘baraza la wachili’, ambalo lilifanya kazi kama baraza la mawaziri kwa sasa.
Ushirikiano huu ulifanya dola ya Wachaga kupiga hatua kubwa kimaendeleo kuliko jamii nyingi za wakati huo.
Kwa mfano kufikia mwaka 1920 dola ya Wachaga ilikua ya kwanza kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kuanzisha na kumiliki gazeti lake (Komkya). Miaka 10 baadae dola ya Buganda (Buganda Kingdom) nayo ilianzisha gazeti lake (Buruuli) na mwaka 1940 Himaya ya Sultani wa Zanzibar (Zanzibar Sultanate) nayo ikaanzisha jarida lake (Imperial).
Si hivyo tu, huduma za maji, umeme, miundombinu ya barabara, hospitali na shule vilifika mapema kulinganisha na maeneo mengine ya nchi. Ikulu ya kisasa ya Mangi Mkuu wa Wachaga, iliyojengwa karibu miaka 100 iliyopita ndiyo inayotumika hadi sasa kama Ikulu ndogo ya Rais kwa mkoa wa Kilimanjaro.
Zilizokuwa ofisi za watendaji wa serikali ya Mangi mkuu (eneo la KDC Moshi) ndio ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Moshi kwa sasa.
Maendeleo haya na mengine mengi, Wachaga waliamini yalitokana na elimu. Kwahiyo mwamko wa elimu ulikua mkubwa hasa baada ya wamisionari kujenga shule na huduma za afya kila walipojenga kanisa. Vitu hivi vitatu viliambatana. Kanisa, Shule, na Kituo cha afya.
Kwahiyo hata kwenye kuchagua viongozi, yule aliyekuwa na elimu nzuri ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda ikiaminika kwamba elimu yake itachochea kasi ya maendeleo. Na hii ni moja ya sababu iliyomfanya Thomas Marealle kushinda kiti cha umangi mkuu mwaka 1952, kwani kati ya wagombea wote yeye ndiye aliyekua na shahada ya uzamili (masters degree) kwa wakati huo.
Kabla ya uhuru kulikua wachumi wawili tu wazawa ambao ni Thomas Marealle na mzee Fredrick Mchauru ambaye walisoma pamoja London School of Economics, kabla ya Marealle kupata ufadhili Cambridge University (Trinity College).
Iliaminika pia kwamba Uingereza ilitaka dola ya Wachaga ijitenge kutoka Tanganyika na itafute uhuru wake yenyewe, kama Rwanda na Burundi zilivyojitenga kutoka Tanganyika baada ya vita vya kwanza vya dunia, wakati huo zikiitwa Ruanda-Urundi.
Hata hivyo mpango huo ulishindikana kwa kuwa Tanganyika ilikua ‘Trusteeship colony’ ya Umoja wa mataifa, na Uingereza alikabidhiwa tu aisimamie hadi iweze kujitawala. Kwahiyo hoja ya Muingereza ilitupwa kwa maelezo kwamba wakati wa kugawanya bara la Afrika pale Berlin mwaka 1984/85 hakuna nchi inayoitwa ‘Chagga state’ iliyogawanywa. Hivyo uhuru unaopaswa kuwa wa Tanganyika kwa ujumla na sio wa jamii moja moja.
Baada ya jaribio hilo kushindwa, inadaiwa shirika la ujasusi la Uingereza (M16) lilimpendekeza Mangi Thomas Mareale kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika baada ya uhuru.
Katika moja ya barua za Richard Turnbull (Gavana wa mwisho wa Uingereza) kwenda kwa shirika la ujasusi la nchi hiyo (M16) ilieleza mapendekezo hayo kwa Thomas Mareale.
Sehemu ya nyaraka hiyo iliyoandikwa mwaka 1958 ilisema ‘I consider Thomas Marreale an outstanding Chagga leader. I dont know him personally but he would be the leader of Tanganyika if British had to leave. However he lack support from other tribes’.
Turnbull alikua akiwaelezea M16 kuhusu Mangi Thomas Marealle na umahiri wake katika uongozi. Hata hivyo alionesha hofu kuwa Marealle hakuwa na ushawishi mkubwa kwa makabila mengine nje ya Wachaga.
Na hii ni moja ya hofu kubwa aliyokua nayo Mwalimu Nyerere wakati wa kudai uhuru. Alipofika uchaggani alikuta dola ya Wachaga ina mamlaka kamili. Ilikua na ‘well defined leadership structure’, bendera yake, wimbo wake, na askari wake.
Nyerere alisema ili Tanganyika iwe uhuru lazima dola ya Wachaga ife kwanza, kwa sababu hatuwezi kuwa na taifa moja ndani ya taifa jingine. Mwaka 1961 Nyerere aliagiza bendera ya Tanganyika isipandishwe kabla bendera ya Wachaga haijashushwa kwanza. Tarehe 8 December 1961 saa 5 usiku bendera ya Wachaga ilishushwa katika Ikulu ndogo ya Moshi, na muda mfupi baadae (saa 6 usiku, December 9) bendera ya Tanganyika ikapandishwa.
Hata hivyo hofu ya Nyerere haikua na mashiko kwa sababu Mareale mwenyewe alimpa ushirikiano mkubwa wakati wa kudai Uhuru. Na ili kuonesha kwamba hakuwa na mpango wowote wa kumhujumu, aliamua kujiuzulu nafasi yake ya umangi mkuu mwaka 1960, na kuruhusu askari wake kujiunga na jeshi la Tanganyika.
Pichani ni wagombea watatu kati ya watano walioshiriki uchaguzi wa Mangi Mkuu mwaka 1952. Kutoka kushoto ni Mangi Thomas Mareale aliyeshinda uchaguzi huo), Mangi John Maruma (Mangi Mwitori wa Rombo), na Abdieli Shangali (Mangi Mwitori wa Machame).
Kwanini Wachaga hupenda kwenda kwao mwishoni mwa mwaka?
Kumekuwa na dhana nyingi potofu juu ya Wachaga kwenda kwao kipindi cha mwisho wa mwaka, maarufu kama “kwenda kuhesabiwa”.
Je ni kweli Wachaga huenda kuhesabiwa? Jibu ni Hapana.. si kweli. Wachaga hawaendi kuhesabiwa.
SWALI; Sasa kama hawaendi kuhesabiwa neno “kuhesabiwa” limetoka wapi na kwanini litumike kwao tu sio kwa Wasukuma, Wamasai, Wayao au Wamakonde?
JIBU; Neno “kuhesabiwa” limetoholewa kutoka neno la Kiebrania “מִפקָד אוֹכלוּסִין” linalomaanisha Wana wa Israel kurudi kwao kwa ajili ya kuhesabiwa.
Mara nyingi Waisrael walikua wanarudi kipindi cha mwisho wa mwaka wa Kiyahudi katika mwezi uitwao “Adar Beit” ambao kwa mujibu wa Kalenda ya Kiyahudi huo ndio mwezi wa mwisho wa mwaka. Na hukaa huko hadi mwezi wa kwanza wa mwaka ambao kwa kiyahudi huitwa “Nissan”.
Utamaduni huu ulitumika katika Israel ya zamani (Ancient Jews) japo kwa sasa haupo tena. Katika kipindi hiki Waisrael walikua wakikutana nyumbani na kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kuhesabiwa ili kujua idadi yao kutokana na kutawanyika katika mataifa mengi duniani.
Tangu enzi za Musa miaka zaidi ya 4,000 kabla ya Kristo; Waisrael walikua na utamaduni wa kurudi kwao kuhesabiwa.
Katika kitabu cha 1Nyakati 23:2-3 Biblia inasema “Akawakusanya wakuu wote wa Israeli, pamoja na makuhani na Walawi. Nao wakahesabiwa Walawi wenye miaka thelathini na zaidi; na jumla yao kwa vichwa, mtu kwa mtu, ikapata thelathini na nane elfu.”
Huu ni udhibitisho wa kuhesabiwa kwa Wana wa Israel zamani hizo. Lakini pia kitabu cha Hesabu 3:14-15 kinasema “Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia, Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu.”
Maandiko yanayoeleza juu ya kuhesabiwa kwa wana wa Israel ni mengi na unaweza kuyasoma baadae katika (Kutoka 12:37, Waamuzi 20:14, 1 Samweli 11:8, Ezra 2:64).
Kwa hiyo kuhesabiwa ni agizo la Mungu na utamaduni huu wa wana wa Israel kurudi kwao kwenda kuhesabiwa ni utamaduni uliokua maagizo ya Mungu mwenyewe (Jehovah).
Sasa je ikiwa Wachaga hawaendi kuhesabiwa iweje wafananishwe na WaIsrael?
Sababu mbili hufanya Wachaga kufananishwa na utamaduni huu wa Israel wa kuhesabiwa.
SABABU YA KWANZA ni kitendo cha Wachaga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka (December) na kukaa huko hadi mwanzoni mwa mwaka mpya (January). Ikumbukwe wana wa Israel nao huenda kwao mwishoni mwa mwaka wa Kiyahudi (Adar Beit) na kurejea mwanzoni mwa mwaka mpya (Nissan). Ufanano huu wa majira hufanya Wachaga nao waonekane kuwa wanaenda “kuhesabiwa” kama waIsrael.
SABABU YA PILI ni mtawanyiko wa jamii hizi mbili. Wana wa Israel wametawanyika katika mataifa mbalimbali duniani. Kutokana na ufinyu wa nchi yao wamejikuta wakisambaa nchi mbalimbali ambapo wanaishi na kufanya kazi huko. Wengine ni wahandisi, madaktari, majemadari wa vita etc. Wana wa Israel wametawanyika mataifa yote ya Ulaya, America na baadhi ya nchi za Asia na Afrika. Pamoja na kutawanyika huku lakini mwisho wa mwaka hukumbuka kurudi kwao.
Kwa upande wa Wachaga nao wametawanyika sana katika mikoa mbalimbali nchini. Mtawanyiko wao unafananishwa na ule wa wana wa Israel kwa sababu mbili. Kwanza eneo lao la makazi (Kilimanjaro) ni dogo na haliwatoshi, sawa na Israel ilivyo ndogo na isivyotosha watu wake. Pili ni “nature” ya mtawanyiko wao. Wachaga kama Waisrael wametawanyika sehemu mbalimbali za nchi na hata nje ya nchi.
Hakuna mkoa au Wilaya yeyote unaweza kwenda nchini ukamkosa Mchagga. Wametapakaa kila kona ya nchi wakifanya shughuli mbalimbali hususani biashara. Mtu mmoja aliwahi kutania kuwa “ukienda eneo la nchi hii ukakosa Mchagga ondoka haraka maana hapafai kuishi”.. Hii ina maanisha Wachaga wanaweza kuishi katika mazingira yoyote na hali yoyote.
Mtawanyiko wa Wachaga katika maeneo mbalimbali ya nchi hufananishwa na mtawanyiko wa Waisrael katika maeneo mbalimbali ya dunia, na hivyo basi kitendo cha Wachaga kurudi kwao mwishoni mwa mwaka hufananishwa na kitendo cha Waisrael kurudi kwao mwishoni mwa mwaka wa kalenda ya kiyahudi. Tofauti ni kuwa Waisrael huenda kuhesabiwa lakini Wachaga hawaendi kuhesabiwa.
Kama Wachaga hawahesabiwi, wanaenda kufanya nini?
Pengine hili ndio swali la msingi ambalo wengi wanajiuliza. Ikiwa Wachaga hawaendi kuhesabiwa kama ilivyo kwa waisrael, Je wanaenda kufanya nini?
Ukweli ni kwamba Wachaga wanakwenda kwao kwa sababu mbalimbali. Leo nitaainisha kwa uchache sababu 10 zinazorudisha Wachaga kwao kila mwisho wa mwaka. Zipo nyingi zaidi ila kwa kifupi ni kama ifuatavyo;
- 1. Kuna wanaokwenda kwao kwa ajili ya kuonana na familia zao na kuwaona wapendwa wao na kujumuika nao kwa ajili ya kufurahia sikukuu za mwisho wa Mwaka huhusani “Krismasi” na “Mwaka mpya”.
Kwa mfano wazazi wako (baba na mama) au ndugu zako wengine (babu, bibi, kaka, dada, shangazi, wajomba etc) hujawaona kwa kipindi cha mwaka mzima. Mmekuwa mkiwasiliana tu kwa simu. Hivyo basi December huwa ni kipindi kizuri cha kurudi nyumbani na kuwaona na kuwajulia hali.
- 2. Pia kipindi hiki hutumika kupanga mipango ya maendeleo ya familia kama vile kujenga. Kwa kuwa watoto wote wa familia hukutana kipindi hiki basi huweka mipango ya maendeleo kwa familia yao. Wanaweza kupanga kujenga nyumba kwa ajili ya wazazi wao ambao ni wazee, kuweka umeme, maji etc.
Uchaggani ni mojawapo ya maeneo nchini ambako kuna nyumba nyingi za kisasa vijijini na ni mkoa uliofanikiwa kupiga vita nyumba ya Nyasi tangu mwaka 1996.
Ni jambo la Kawaida kukutana na maghorofa ya kisasa kule “Machame Uswaa, Kibosho Kirima, au Mamba Komakundi”.. au ukipita “Uru Mawela, Rombo Mamsera au Kilema Poffo” nyumba zote unazokutana nazo ni self-contzined za kisasa, lakini wanaishi wazee. Watoto wao wapo Shinyanga, Dar, Kigoma, Mwanza etc wanatafuta maisha. Mipango hiyo ya kujenga na kuhudumia wazazi hupangwa msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
- 3. Msimu huu wa sikukuu hutumika kupatanisha ndugu, jamaa au marafiki waliokosana. Wazee huitwa na kuzungumza na pande zote mbili kisha kuwapatanisha. Mkikubali kuelewana basi huchinjwa mbuzi kama ishara ya furaha ambapo jamii yote hujumuika kwa kula na kunywa.4. Kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ndio kipindi kizuri ambacho vijana hukitumia kutambulisha wachumba zao nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na umepata mchumba wa Morogoro. Lakini ndugu zako wametawanyika. Wengine wapo Tabora, wengine Mwanza, wengine Mbeya. Huwezi kupita na mchumba wako kote huko kumtambulisha. Kwahiyo “option” nzuri ni kusubiri msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ambapo ndugu zako wote watakuwepo nyumbani ndipo umpeleke mchumba wako kumtambulisha, na kupanga mipango ya ndoa.5. Kuwaleta watoto wafahamu ndugu zao na wafahamike nyumbani. Unaweza kuwa unaishi Dar na familia lakini ndugu zako wanaishi na familia zao maeneo mengine ya nchi, watoto wenu hawafahamiani maana hawajawahi kuonana. Hivyo mkikutana nyumbani msimu wa sikukuu ni kipindi kizuri cha watoto wenu kufahamiana na kufahamu asili yao.
Pia ikiwa umejaliwa mtoto ukiwa huko unakofanyia shughuli zako lakini wazazi wako hawajamuona mjukuu wao, hiki ni kipindi kizuri cha kuwapelekea wazazi wako mjukuu wao wamuone na kumpa baraka.
- 4. Kushiriki shughuli za kijamii (charity work). Wachaga wengi ni waumini wazuri sana wa dini iwe ukristo au uislamu. Hivyo kipindi cha msimu wa sikukuu hutenga muda wa kutembelea wagonjwa, Yatima na Wasiojiweza na kuwapa misaada mbalimbali. Kwa wale Wakristo huita “sadaka ya Epifania”.7. Kipindi hiki hutumika pia kufanya usafi na kurekebisha maeneo waliyopumzika wapendwa wetu (makaburi). Wachaga kama ilivyo binadamu wengine hutenga maeneo maalumu ya kuzikia ndugu zao; na mara nyingi kila familia ina eneo lake.
Kwa hiyo ikiwa kuna ndugu amefariki na akazikwa basi msimu huu huwa ni kipindi kizuri cha kujengea makaburi kama kumbukumbu ya sehemu walipopumzika wenzetu.
Bahati mbaya wapo watu wanaohusisha utamaduni huu na matambiko. Kwanza ieleweke kujengea makaburi si dhambi na si matambiko. Hata Yakobo alipofia kule Misri alipoenda kwa mwanae Yusufu alizikwa kwenye Kaburi lililojengewa (Matendo 7:15-16). Hivyo basi ni vizuri ikaeleweka kuwa kujengea makaburi si dhambi.
Na mara nyingi uchaggani kabla ya kujengea Kaburi kiongozi wa dini huitwa na kufanya sala, kabla ya shughuli ya ujenzi haijaanza. Kwahiyo hakuna nafasi ya matambiko.
Ikiwa kuna mchagga anafanya matambiko wakati wa kujengea makaburi ichukuliwe kuwa ni tabia ya mtu binafsi na isihuhishwe Wachaga wote. Kwani wapo watu wa makabila mengine hufanya matambiko pia lakini huwezi kusema jamii yote hutambika.
- 5. Msimu huu wa sikukuu ni kipindi kizuri ambacho Wachaga hukitumia kupanga na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii yao kama vile mashule, hospitali, Maji, barabara n.k
Kwa mfano zipo barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi wenyewe kwa kuamua kujichangisha bila kusubiri serikali ifanye. Barabara ya Uru Kusini ni mojawapo. Mipango hii hupangwa msimu huu wa sikukuu.
- 6. Msimu huu hutumika kwa ajili ya mapumziko ya familia baada ya mahangaiko ya mwaka mzima. Ni wakati wa familia kutulia pamoja kutafakari mipango ya mwaka uliopita na kuweka mipango mipya ya mwaka unaofuata.
Ndugu na jamaa hukutana pamoja na kufurahia sikukuu za “Krismasi” na “mwaka mpya” kwa kula na kunywa hasa vyakula vya asili kama “kisusio, faya, supu ya mbuzi iliyopikwa kiasili kwa kuchanganywa na majani aina ya “mahombo” na vyakula vingine bila kusahau kinywaji aina ya mbege.
- 7. Kipindi hiki hutumiwa kujenga na kukarabati nyumba za ibada. Ni wazi kuwa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna nyumba nzuri na za kisasa za Ibada.
Kanisa kubwa na la kisasa kama la KKKT Old-Moshi Rau, au La RC Kristu Mfalme, Au TAG Kilimanjaro Revival, au Msikiti wa kisasa kama wa Riadha, ni nadra kuvipata mahali pengine. Au Kanisa la kale kama la KKKT Old-Moshi Kidia lililojengwa mwaka 1843 utalipata wapi kwingine?
Mipango ya ujenzi wa nyumba hizi za ibada za kisasa na kukarabati zile za zamani hufanywa msimu huu wa sikukuu.
Pia Wachaga wengi hupenda kwenda kwao kwa kuwa ibada zote katika msimu huu huongozwa kwa kichagga. Yani kuanzia usomaji wa misa, mahubiri hadi nyimbo huimbwa kwa kichagga, wakati huo nyumba za ibada zimepambwa kwa mapambo ya asili kama “Makurera, makangachi, migomba imechimbiwa vichumini (njia za kwenda nyumbani)” etc.
Hii huongeza nakshi na kufanya mtu ajisikie kupungukiwa kitu ikiwa hatakuwepo Nyumbani msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Utamaduni huu wa Wachaga ni mzuri sana, na kuna mengi jamii nyingine zinaweza kujifunza kupitia Wachaga kama ambavyo Wachaga wanaweza kujifunza kupitia jamii nyingine.
Bendera Ya Wachaga
Halmashauri ya Uchaga ilikuwa na bendera yake ambayo ipo hadi leo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, yenye nembo tano kuu:
1. Mlima Kilimanjaro uliochorwa katikati ya bendera ukionyesha mandhari nzuri ya kilele cha Kibo. Kilele cha Kibo kinatoa maji safi na ni kielelezo cha umoja wao.
2. Chini ya kilele cha Kibo, upande wa kushoto wa bendera kuna mgomba wenye ndizi. Hiki ni chakula kikuu cha Wachaga.
3. Upande wa kulia wa bendera ni tawi la mbuni ukiwa na matunda yake. Kahawa ni zao lililowaletea maendeleo.
4. Bendera imezungukwa na matawi ya ‘sale’ lenye matawi mawili (draceana plant). Matawi haya yamefanya mduara kuzunguka kilele cha Kibo, mgomba wa ndizi na tawi la zao la kahawa. Masale ni mmea unaoheshimiwa sana na Wachaga wote.
Ni alama ya amani. Masale hutumika katika sherehe na shughuli zote za kimila zinazofanywa na Wachaga. Majani yake ni kijani kibichi yanayoonyesha jinsi Kilimanjaro ilivyo na rutuba nzuri inayostawisha mazao ya kila aina.
5. Juu kidogo ya kilele cha Kibo yupo chui ambaye amejipumzisha. Chui ni alama kuu ya mamlaka ya Wachaga.
Hapo awali kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro walikuwepo chui wengi wa rangi nyeusi lakini kutokana na ongezeko la watu pamoja na uharibifu wa mazingira chui hawa wametoweka.
|