KATIKA kitabu chake cha tawasifu “MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI” Shaaban Robert anasimulia dhiki, adha na udhalili alioupitia, pengine kwa sababu ya Uafrika wake, kipindi cha ukoloni akiwa katika safari ya kikazi kama mtumishi wa serikali;
ABIRIA CHEO CHA PILI
DARAJA yangu katika kazi sasa ilikuwa imeniwezesha kusafiri kama abiria wa cheo cha pili katika gari moshi. Mapendelea haya yanayotamaniwa yalinijia baada ya miaka kumi na nne ya kazi serikalini. Julai 13, 1944, nilichukua tikiti, na baada ya kuagana na marafiki, nikasafiri kwenda Mpwapwa. Nilishuka Korogwe kungoja safari ya lori. Karibu ningalilala nje Korogwe kwa ukosefu wa malazi kwa abiria Waafrika., lakini mtu mmoja aliyenijua zamani alinichukua kwake akanipa malazi mema. Asubuhi nilionyesha tikiti zangu za safari kwa msimamizi wa safari. Mtu huyu alinitupia jicho kwa haraka kisha akaamuru nijipakie katika lori.
Palikuwa na malori manne tayari kwa safari siku ile. Nilikwenda nikajipakia katika lori la abiria cheo cha pili. Mimi nilikuwa msafiri wa kwanza kujipakia. Dakika chache baadaye loro letu lilijaa abiria. Abiria Waafrika tulikuwa mimi na watoto wangu tu. Wengine wote walikuwa ni Wahindi. Karibu na dakika ya mwisho kusafari pakaja Wahindi wanne wengine. Kuwapa watu hawa wanne nafasi katika lori nililojipakia mimi ilipasa watu wanne waliokuwa wamekwisha kuingia washuke. Msimamizi wa safari, Mhindi vilevile, hakuona mtu mwingine wa kushuka ila mimi. Baridi ina mzizimo siku zote kwa kondoo mwenye manyoya haba. Kwa maneno ya karaha alinilazimisha kushuka chini nikajipakie katika lori la abiria wa cheo cha tatu au la mizigo. Nilimkumbusha msimamizi wa safari kuwa mimi ni abiria wa cheo cha pili ambaye nilikuwa nikisafiri kwa kazi ya serikali; nilitangulia kujipakia mahali nilipostahili kukaa; alikuwa hana haki ya kuniteremsha; iwapo ililazimu kutenda atakavyo ililazimu vilevile yeye kunipa stashahada ya kuonyesha namna ilivyosafiri kutoka Korogwe. Kwa maneno hayo ulimi wa msimamizi wa safari ulianza kupotoka akadai kuwa aliweza kuzuia kusafiri lori nililoingia.
Kundi kubwa la watazamaji lilikuwepo. Karibu watu wengi katika kundi lile walicheka kwa maneno ya msimamizi wa safari. Kivumo cha kicheko kilichemsha hasira yake akaamuru niteremshwe chini kwa nguvu. Matarishi waliokuwa chini ya amri yake walitii wakawa tayari kunijia wanikamate na kunitupa chini kama mtumba, lakini kitu gani sijui kiliwafanya kusita kutimiza amri ya bwana wao. Halafu nilisikia kuwa desturi ya matarishi wale ilikuwa kutii na kutimiza kila amri njema waliyopewa, na kuacha mbali kila amri mbaya hata katika hatari ya kutolewa kazini mwao. Nilifurahi sana kusikia habari hii. Idadi ya watu wema ni kubwa siku zote kuliko jumla ya watu wabaya.
Siku zangu zilikuwa zikihesabiwa. Sikutaka kuchelewa bure pale Korogwe. Niliita watu kuja kushuhudia mwamale niliotendewa na tabia ya msimamizi wa safari. Watu wengi walikuwa tayari kunipa sahihi za mikono yao kuwa walishuhudia yote yaliyotokea. Kisha mimi na watoto wangu tulishuka na kujipakia katika gari jingine. Nafasi iliyokuwa imebaki mle garini ilikuwa si kubwa. Basi tulikaa juu ya mizigo yetu. Kutoka Korogwe tulikwenda Morogoro. Mchana wote ulituishia njiani. Hii ilikuwa siku ya pili ya safari yangu, nikafurahi kushuka katika gari.
Saa mbili na nusu usiku nilijipakia katika gari moshi lililotoka Dar es Salaam hata saa tisa usiku nikashuka Gulwe. Kutoka Gulwe nilichukuliwa na lori la Idara ya Utunzaji wa Wanyama kwenda Mpwapwa. Saa kumi alfajiri nikawa Mpwapwa. Mwisho wa safari yangu ilikuwa ni Kikombo, lakini niliambiwa nikae juu ya gari hata saa moja asubuhi wakati mwendeshaji wetu alipoingia nyumbani kwake kulala. Nje kulikuwa kukizizima sana kwa baridi na umande na lori letu lilikuwa wazi. Taya za watoto wangu zilitingishika na meno yakagongana kwa kipupwe. Julai ni mwezi wa kipupwe kikali pande zile za dunia. Mbwa hafi maji akiona ufuko, na sisi kwa kuwa sasa tulikuwa karibu kufika mwisho wa safari yetu jaribu la baridi halikutufadhaisha sana. Tulikuwa na mablanketi yaliyoweza kuzuia mzizimo wake kutudhuru. Tulijifunika mablanketi yetu tukasaburi kuche polepole.
Saa moja na nusu asubuhi nilikuwa mbele ya msimamizi wa Afisi ya Idara ya Utunzaji wa Wanyama. Huyu alikuwa ni Mzungu. Hakuwa tayari kushikana mikono na mimi kama nilivyozoea kuona Wazungu wengine. Labda mimi nilikuwa si kitu mbele yake lakini tuliongea vema. Alisema kuwa nitapata nyumba lakini kwa namna maneno yalivyotamkwa niliweza kufahamu kuwa idara ilikuwa na dhiki ya makao mema. Dhiki hii ilikuwa imeenea duniani wakati ule. Bati na simenti vilikuwa adimu kupatikana kwa sababu ya Vita Kuu Na. 2. Hii ilikuwa ni Jumapili, siku ya tatu ya safari yangu. Nilipewa ruhusa nikapumzike nihudhurie kazini Jumatatu asubuhi.
*** Vitabu vya sheikh Shaaban Robert vimerejewa kuchapwa upya, na sasa vinapatikana kwa wingi madukani, hususani jijini Dar es Salaam. Ni uzalendo wa kujivunia kwa kila Mswahili kumiliki na kuzisoma nakala za vitabu vya gwiji huyu na “baba wa Kiswahili”.
ORODHA YA KAZI ZA FASIHI ALIZOANDIKA SHAABAN ROBERT
1. MWAFRIKA AIMBA (1969), Nelson. Nairobi
2. ALMASI ZA AFRIKA (1971), Nelson, Nairobi
3. KOJA LA LUGHA (1969), Oxford, Nairobi
4. INSHA NA MASHAIRI (1967), Nelson, Nairobi
5. ASHIKI KITABU HIKI (1968), Nelson, Nairobi
6. PAMBO LA LUGHA (1968), Oxford, Nairobi
7. KIELEZO CHA FASILI (1962), Nelson, Nairobi
8. MASOMO YENYE ADILI (1959), Art&Literature, Nairobi
9. MAPENZI BORA (1969), Nelson, Nairobi
10. TENZI ZA MARUDI MEMA NA OMAR KHAYYAM (1973), TPH, Dar-es- salaam
11. UTENZI WA VITA VYA UHURU (1961), Oxford, Nairobi
12. ALMASI ZA AFRIKA NA TAFSIRI YA KIINGEREZA (1960), Art&Literature, Nairobi
13. MASHAIRI YA SHAABAN ROBERT (1971), Nelson, Nairobi 14. SANAA YA USHAIRI (1972), Nelson, Nairobi. Na vitabu vya nathari vya Sheikh Shaaban Robert ni:
15. KUFIKIRIKA (1968),Oxford, Nairobi
16. WASIFU WA SITI BINTI SAAD (1967), Art&Literature, Nairobi 17. MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI (1949), Nelson, Nairobi
18. KUSADIKIKA (1951), Nelson, Nairobi
19. ADILI NA NDUGUZE (1977), TPH, Dar-es- salaam
20. UTU BORA MKULIMA (1968), Nelson, Nairobi
21. SIKU YA WATENZI WOTE (1968), Nelson, Nairobi
22. KIELELEZO CHA INSHA (1954), Witwatersand, Nairobi
23. BARUA ZA SHAABAN ROBERT 1931- 1958, (2002), TUKI, Dar- es- salaam
24. MITHALI NA MIFANO YA KISWAHILI (2007), TUKI, Dar-es- salaam