Welcome, Guest |
You have to register before you can post on our site.
|
Online Users |
There are currently 103 online users. » 0 Member(s) | 102 Guest(s) Bing
|
Latest Threads |
Buy Vilitra 60 Mg |【Get E...
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Kieth_winsett
04-24-2023, 11:45 AM
» Replies: 0
» Views: 0
|
How to take Cenforce50?
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Kieth_winsett
04-19-2023, 12:59 PM
» Replies: 0
» Views: 0
|
About the Vidalista 60 Mg...
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Kieth_winsett
04-04-2023, 04:07 PM
» Replies: 0
» Views: 0
|
What Is Vidalista 60?
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Kieth_winsett
04-03-2023, 10:49 AM
» Replies: 0
» Views: 0
|
How to take Cenforce 100 ...
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Kieth_winsett
03-29-2023, 02:37 PM
» Replies: 0
» Views: 66
|
How is Vidalista 10 Mg us...
Forum: Watunzi wa Kiswahili
Last Post: Kieth_winsett
03-27-2023, 01:26 PM
» Replies: 0
» Views: 117
|
Obtain Thesis Paper Assis...
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Minny02
03-24-2023, 03:01 PM
» Replies: 0
» Views: 200
|
SEO services for sports f...
Forum: Historia ya makabila ya kibantu
Last Post: Maria Poland
03-17-2023, 01:51 PM
» Replies: 1
» Views: 223
|
NUKUU ZA KISWAHILI DARASA...
Forum: Nukuu
Last Post: MwlMaeda
01-15-2023, 05:31 PM
» Replies: 0
» Views: 788
|
NECTA K4 2022
Forum: Mitihani
Last Post: MwlMaeda
01-15-2023, 05:25 PM
» Replies: 0
» Views: 403
|
|
|
Historia ya mswahili wa Zanzibar (VIDEO) |
Posted by: MwlMaeda - 09-09-2021, 07:04 AM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Historia ya mtu anayeitwa Mswahili inaonekana kutotiliwa maanani sana na wataalamu wengi kiasi cha kuibua hofu miongoni mwa waswahili kuwa pengine ipo njama ya kuwameza na kuwapoteza waswahili katika historia ya jamii za Mwambao.
|
|
|
UHAKIKI WA SERA YA LUGHA KATIKA ELIMU YA TANZANIA |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 04:55 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
ELIMU AU MAIGIZO?
Uhakiki wa Sera ya Lugha Katika Elimu Tanzania
Z.S.M. Mochiwa katika Kioo cha Lugha 2,1996/97:41-58
Z.S.M.Mochiwa katika kuhakiki sera ya elimu katika Tanzania anaeleza yafuatayo:
Utangulizi
Katika wimbo wa Taifa la Tanzania, hekima, umoja na amani hutamkwa kuwa ngao za Watanzania. Aidha, nembo ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam imesogeza falsafa hii hatua moja mbele kwa kutangaza kuwa: Hekima ni uhuru. Hainipitii akilini mwangu kuwa kuna mtu-hadhiri wa nafsi yake anayeweza kusema matamko haya ni mufilisi. Mimi, binafsi yangu, ninayahesabu kuwa miongoni mwa vito vichache tulivyo navyo katika taifa hili.
Kwa bahati mbaya, sijapata kusikia majadiliano yanayomulika jinsi vito hivi vinavyorutubishwa ndani ya jamii. Penyenye peke yake niliyoona ni ile inayotokana na matumizi ya kito kimoja ndani ya nembo ya Chuo Kikuu. Kwa kuwa Chuo Kikuu ni taaisis ya elimu, hapana shaka kuwa nemno ile inahusisha elimu na hekima. Kwa maana hiyo, ndani ya elimu, hekima hukua na inapokua, hekima humpa aliye nayo uhuru.
Tukiyaondoa hayo yote, bado taifa halielekei kujiuliza kwa dhati kabisa, hekima, umoja na amani hukuzwa na kuendelezwa vipi. Hata wataalamu wa Chuo Kikuu, pamoja na kudai kuwa hekima ni uhuru, hawaelekei kuionesha imani hii kwa vitendo kwa kubainisha na kutumia mbinu zinazokuza hekima. Aidha, mtu anapohakiki safari ya taifa hili tangu lizaliwe hadi hivi leo, na hususan miaka kumi hivi iliyopita, inadhihirika wazi kuwa kuna kupuuzwa kwa virutubisho vya vito hivi.
Inawezekana kuwa mwenendo wa kupuuzwa kwa virutubisho hivi si wa makusudi. Linaloelekea kuwa dhahiri kwangu, ni kule kutotambua vizuri virutubisho hivyo ni vipi na vina umuhimu gani. Mathalan, baada ya uhuru, Tanzania ilianzisha wizara ya Utamaduni-kirutubisho cha kwanza cha hizo ngao za taifa-lakini wizara hii haikuweza kudumu na nafsi yake. Kisa cha kupachikwa pachikwa kwa wizara hii kila mahali-mara utamaduni ni sehemu ya Wizara ya kazi, mara vijana, ningethubutu kusema, ni taswira yake yenye uvumilivu mbele ya wahandisi wanaoanzisha wizara katika Jamhuri. Hali hii ya uvumilivu wa taswira ya wizara huakisika pia katika mgao wa mafungu ya fedha. Hali hii hujirudia kwenye taasisi za wizara hii, kama vile, BAKITA. Kwa ufupi taifa halijapambaukiwa kwamba utamaduni ndiyo nyenzo pekee ya kurutubishia vito vya taifa.
Katika makala haya ninakusudia kudai kuwa Tanzania haikupiga hatua kubwa kielimu na kimaendeleo kwa ujumla kwa sababu ya kuweka kipaumbele chake katika mambo ambayo, kwa maoni ya makala haya, si ya msingi. Kuitelekeza lugha ya Kiswahili ikabaki kuwa lugha ya kuuzia nyanya sokoni, kumeleta maafa makubwa kielimu, kijamii na kiuchumi, ima kwa neno moja kiutamaduni. Ikisemwa vinginevyo, kwa kupuuza lugha ya Kiswahili na kuikumbatia ya Kiingereza, Tanzania imekubali kujiweka katika hali ya kutojitegemea. Matokeo ya mwenendo huu ni kwamba kila kinachofanyika ni maigizo tu. Hali hii hailiruhusu taifa kuishi kwa nafsi yake isipokuwa kwa nafsi ya kuazima. Kabla ya kuanza mjadala huo hapana budi kuelekeza makini yetu kwenye dhana muhimu, nazo ni taifa, utamaduni, maendeleo ya kijamii, elimu na lugha.
Taifa
Inaposemwa kwamba Tanzania ni taifa, ina maana ni kundi la watu ambao wana nduni mahususi. Kwanza kundi hilo lina kipande cha ardhi ambacho wote kwa pamoja wanadai kuwa ni chao; ni nchi yao. Watanzania, kwa mfano, huishi Tanzania, na Wakenya huishi Kenya. Pili, ili wawe taifa, ni lazima watu hao wawe na mambo kadhaa yanayofanana. Miongoni mwa mambo hayo ni historia, mila na desturi. Tunaposema, mila na desturi, tunasema taifa haliwezi kuwa taifa bila ya kuwa na utamaduni wake. Nduni hizi ndizo zinzorutubisha umoja wao.
Watu wenye mila na desturi au, kwa neno moja, utamaduni unaofanana wana kongamano kubwa la rai, mtazamo na hisia. Hukumu zao kuhusu masuala na matukio mbalimbali hufanana. Kwa misingi hii watu wa namna hii wana umoja wa aina fulani katika mienendo na hukumu kuhusu vilivyo na visivyo. Pamoja na kuzikubali nduni hizi, Gerth na Mills (1954:197) wanaongeza kuwa kundi hilo lina uwezo wa kujiundia chombo cha uongozi kikawa serikali yao. Kwa kuwa moja ya nduni za taifa ni utamaduni wake, tujipe wasaa wa kuifasili dhana hii.
Utamaduni
Kwa watu wa kawaida, utamaduni unafasiliwa kwa namna nyingi kwa kutegemea muktadha. Utamaduni unanasibishwa na uganga au mazingaombwe, uchawi, michezo au ngoma au mambo yote ambayo, kwa macho ya sasa, yamepitwa na wakati. Mifano halisi ya mikanganyiko hiyo ni pamoja na jina la wizara yenyewe inayosimamia masuala ya utamaduni nchini ambayo inaitwa Wizara ya Elimu na Utamaduni. Kutenganisha Elimu na Utamaduni ni kudai kuwa Elimu huweza kuangaliwa pekee bila ya kuhusisha Utamaduni. Jina la Wizara halidokezi kuwa Utamaduni ni elimu na elimu ni utamaduni. Aidha, inapotokea kuwa watu huiita Wizara hii kuwa ya michezo, kwa sababu tu wao ni washabiki wa michezo, hii ni dalili ya ufahamu nusu nusu wa dhana nzima ya utamaduni. Hali hii, kwa maoni yangu, inatia hofu kwa sababu utamaduni, kwa sehemu kubwa, unaonekana kuwa mambo ya jana na si ya leo. Ni mambo ambayo hayana mchango wa moja kwa moja katika uhai wa jamii hivi leo. Aidha, fasili hizi zinaelekea kudokeza uwezekano wa utamaduni kuwa kikwazo katika maendeleo ya jamii badala ya kuwa suluhu au mashine yenyewe ya maendeleo hayo.
Chanzo cha mikanganyiko hii ni upana wa dhana yenyewe. Karibu kila kitu katika jamii kinanasibika na utamaduni. Kutokana na mikanganyiko hii, hata wataalamu wameelekea kufasili dhana hii kwa kutaja ‘orodha’ ya vitendo, matukio na mienendo ya jamii. Goodenough (1957:167), kwa mfano, anasema:
Quote:Utamaduni wa jamii ni mkusanyiko wa yote ambayo mwanajamii ni lazima ajue au aamini kama sharti la kukubalika kwa mwenendo wake kwa wanajamii wenzake…..(tafsiri ya mwandishi).
Maneno ‘mkusanyiko wa yote’ katika fasili husisitiza kuwa dhana ya utamaduni ni ‘kapu’ la kubebea yote yaliyo ndani ya jamii. Pamoja na upana wake, fasili hii ni maarufu kwa wataalamu wengi kama Wardhaugh (1992) na Baker (1995). Baker, kwa mfano, zaidi ya kutumia mkusanyiko wa yote, anaorodhesha vipengee kama fasili yake inavyoonesha:
Quote:Utamaduni ni mwenendo mzima wa maisha ya jamii, maono ya jamii, mpangilio wao wa uzoevu, taratibu za matazamio, mahusiano ya kijamii, kaida za mienendo, sayansi na teknolojia, n.k (uk. 28) (tafsiri ya mwandishi)
Udhaifu wa fasili hizi ni kwamba unaifanya dhana hii iwe ngumu kufumbatika kiakili. Aidha fasili hii inashindwa kuhusisha channzo na matokeo na badala yake kushikilia matokeo. Mienendo ya jamii, mpangilio wa uzoevu, matazamio na mahusiano kati ya wanajamii, ngoma, michezo n.k. peke yake si utamaduni. Utamaduni ni muunganiko wa haja ya jamii kupata nusura na jitihada zao za vitendo vya kuipatia nusura hiyo. Yote yanayoorodheshwa yanatokana na haja iliyo ndani ya nafsi ya kila mwanajamii ya kutaka kunusurika. Nusura hii ndiyo inayofasilika kuwa mfumo wa maitikio yote ya wanajamii katika kukabiliana na changamoto zilizomo ndani ya mazingira ya jamii yenyewe. Mbinu za kujiruzuku, kujihami, kujifurahisha, kujenga mahusiano kati ya wanajamii ni mkusanyiko wa jitihada za wanajamii ambazo zinakidhi haja ya kupata nusura.
Fasili hii, inatuwezesha kuona nafsi ya kubadilikabadilika kwa michomozo ya nusura. Ingawa haja ya kunusurika haibadiliki lakini mbinu zinazotumika ili kuipata hubadilika kutokana na mabadiliko ya mazingira. Tuchukue mfano wa burudani. Kuburudika ni kipengee muhimu kinachodhihirisha utashi wa mwanajamii wa kujipatia nusura. Lakini kwa kadiri miaka inavyobadilika jamii imeshuhudia kuingia na kutoka kwa aina mbalimbali za burudani. Ni nani, kwa mfano anajua Mserego au beni ni nini hivi leo? Kutoweka kwa ngoma kama hizi hakuna maana ya kupotea kwa haja ya burudani. Kilichotokea ni kwamba wanajamii hupata burudani wanayohitaji kutokana na ngoma, michezo au shughuli nyingine mpya.
Fasili kama hii inatusaidia kuusawiri mwanzo wa utamaduni ndani ya heba ya mwanajamii badala ya kuuona kuwa nje ya heba hiyo. Aidha fasili hii itatuzuia kuuona utamaduni kuwa gwanda ambalo mtu anaweza kuvaa au kuvua. Ingawa mtu hazaliwi nao, lakini mbegu ya utamaduni imo ndani ya nafsi yake. Utamaduni kwa mtazamo huu ni mfungamano wa nafsi ya mwanadamu ya kutaka nusura na maitikio yake ya changamoto za mazingira yake. Kutokana na mfungamano huo, utamaduni huifumbata heba yake. Kwa vyovyote itakavyofasiliwa, hapana budi dhana ya utamaduni iungane na heba ya jamii. Utamaduni ndiyo nafsi; ni dhati ya jamii.
Mjadala huu unatufanya kuuona utamaduni kuwa na nyuso mbili. Uso mmoja ambao umo ndani ya heba ya mwanajamii katika sura ya utashi wake wa nusura. Utashi huu wa nusura ndio unajidhihirisha katika mkusanyiko wa mbinu mbalimbali za kuutafutia nusura. Uso huu ulio ndani ya heba ndio unaoukilia vipengele vyote vinavyoorodheshwa. Aidha, uso huu ndio unaomsukuma mwanajamii mpya kufanya jitihada ya kujifunza huu uso wa nje. Uhusiano wa usababisho kati ya utashi wa nusura na mbinu za maisha zinazodhihirika ni kitu cha msingi katika kuchochea, kuimarisha na/au kuhamasisha maendeleo ya jamii. Kwa maneno mengine, ncha mbili hizi zinazokamilisha fasili zinasaidia kuona uhusiano wa karibu kati ya utamaduni na maendeleo ya jamii.
Maendeleo ya jamii
Tunapochukulia kuwa utamaduni una nyuso mbili, yaani utashi wa nusura na mbinu za kuipata nusura hiyo, inawezekana kusema maendeleo ya jamii yoyote ni mabadiliko ya utamaduni wake, na hasa, kwa usahihi zaidi, ni mabadiliko ya mbinu za kupatia nusura. Mabadiliko ya mbinu hizo huanzia kwenye utashi. Huanza na hisia za kutosheleza kwa mbinu hizo za kuipatia jamii nusura yake. Baada ya kuridhika kuwa mbinu zinazotumika zina udhaifu, jamii hufanya bidii ya kuondoa zile zilizochakaa na kuingiza mpya. Mbinu mpya zinapoingia katika jamii, ndipo jamii inayohusika inasemekana kuwa imepiga hatua ya maendeleo.Kwa maana hii, jitihada zozote za kuiletea jamii maendeleo huanza na tathmini ya kina ya utamaduni wa jamii inayohusika, hususan, mbinu za maitikio ya changamoto za mazingira zinakidhi kwa kiasi gani haja ya jamii hiyo ya kujitafutia nusura. Tathmini hii itaelekeza ni vipengee gani katika ‘mashine’ ya maendeleo vimechakaa na kwa hivyo vinahitaji kubadilishwa. Mbinu mpya za utunzaji wa mazingira, kwa mfano, huibukia ndani ya utamaduni wa jamii kuhisi kuwa maitikio ya zile za zamani ya changamoto hizo hayaleti tija inayolingana na mahitaji.
Jambo la msingi hapa ni kwamba ni lazima jamii ihisi kwamba kuna tatizo. Endapo jamii, kwa macho yake ya utamaduni, haihisi kuwa liko tatizo, jitihada zote za kuleta maendeleo hukwama. Mathalan, sina hakika kama heba ya Tanzania inahisi kuwa uzazi wa watoto wengi ni tatizo. Mradi wa Uzazi wa mpango utafanikiwa ikiwa heba ya jamii itagundua na kukubali kuwa, kuwa na watoto wengi katika familia ni tatizo.
Umuhimu wa kuangalia maendeleo ya jamii kwa mwanga huu umetiliwa mkazo katika Mkutano Mkuu wa sera za utamaduni ulimwenguni (1982). Mkutano huo wa Mexico ulidhihirisha kwa kauli moja haja ya kuweka mnasaba kati ya maendeleo na utamaduni. Mkutano ulizingatia na kutangaza kwamba:
Quote:Maendeleo ya kweli ni yale yanayotokana na hisia na dhamira za mabadiliko za wanajamii. Kwa maana hiyo maendeleo ya jamii yatakuwa matokeo ya juhudi za wanajamii. (uk. 18). (Tafsiri ya mwandishi)
Kwa kuangalia kampeni nyingi za nchi, ni rahisi kuona kuwa, yaliyo matatizo kwa wenzetu, yamefanywa kuwa matatizo kwetu. Aidha, kwa kuwa suala la utamaduni halina kipaumbele, nchi imejitumbukiza katika miradi mbalimbali ambayo mara nyingi haielekei kukabili changamoto halisi za mazingira ya jamii. Kampeni kama Twende na wakati na Uzazi wa mpango, zinafungamana zaidi na heba za jamii za nje kuliko heba ya Tanzania Ni dhahiri kuwa, Tanzania haitafuti maendeleo ya kijamii kwa kurekebisha heba yake bali kwa kujilinganisha na kujifananisha na heba nyingine. Kujiangalia na kujirekebisha kwa kioo cha nje, au tuseme, kwa kutumia vigezo vya tamaduni za nje, kuna matokeo ya kutelekeza utamaduni wetu ambao, ndio mashine ya maendeleo ya kweli.
Elimu na lugha
Zinapokubalika, fasili za utamaduni na maendeleo ya jamii zinadokeza kwa nguvu, umuhimu wa elimu na lugha katika maendeleo. Ikiwa ndani ya utamaduni mna mfumo wa maarifa au mbinu mbalimbali zinazoleta arabuni ya utashi wa nusura ya jamii, na ikiwa maendeleo ya jamii ni mabadiliko ya utamaduni, ni dhahiri kuwa elimu na lugha ni muhimu katika uhai wa mfumo wenyewe pamoja na maendeleo ya jamii. Mfumo huo hauwezi kuendelea kuwako bila ya kuwako kwa taratibu za kuurithisha kwa kizazi kipya. Taratibu hizo za kuurithisha mfumo wa maarifa na mbinu za nusura ndizo zinazoingia katika ajenda ya elimu.
Elimu kwa rai ya makala haya, iwe ya asili au ya kisasa, ina kazi kuu mbili. Zaidi ya kuwa mchakato wa kurithishia vipengee mbalimbali vya mfumo wa nusura ya jamii, lakini pia, mchakato huu humpatia kila mwanajamii fursa ya kugundua na kukuza vipawa vyake. Ni mfumo unaokuza akili ya mpokeaji hadi imepata uwezo wa kutanzua tata, kudadisi na/au kupata stadi za ubunifu. Elimu hii ndiyo ile ile inayofasiliwa na Nyerere (1967) kuwa mchakato wa kukuzia udadisi na wa kujengea fikra angavu.
Freire (1970) anaifasili elimu hii kuwa kitendo cha kitamaduni chenye kumleta mpokeaji kwenye uhuru. Kauli ya Freire inaobesha wazi kuwa Elimu ni utamaduni na utamaduni ni elimu. Tanzania kuwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni ni kuonesha kuwa dhana ya utamaduni haijaeleweka. Aidha, kwa mujibu wa Freire, kitendo hicho cha kitamaduni kitakuwa hakina maana ikiwa hakimpi mpokeaji kujua na badala yake humpa kukariri mambo tu.
Elimu, na hasa ile ambayo ni chipukizi la utamaduni wa jamii, ni mchakato muhimu na wenye nguvu za kusukuma gurudumu la maendeleo. Lakini kama wanavyodai Costa na Garmston (1994) elimu hiyo ni sharti iwe na makusudi mahususi. Hapana budi iwe na ‘mtu wa ndoto’ anayeaniwa nayo;
Quote:Ni lazima elimu ikuze uwezo wa kufikiri kwa unyofu na uangavu. Impe mpokeaji uwezo wa kuunganisha chanzo na sababu za matukio na kutoa maamuzi razini (uk 77) (Tafsiri ya mwandishi)
Haya, kwa kiasi kikubwa, ndiyo yanayotajwa na Nyerere anapofafanua mtu wake wa ndoto kielimu (mtajwa). Yeye pamoja nao wote wanasisitiza kuwako kwa falsafa ambayo itaongoza mchakato mzima wa elimu. Kutokuwako kwa falsafa ya elimu iliyo hai nchini kumesababisha matatizo ya aina mbalimbali ambayo yanaelekea kuunyima mchakato wa elimu Tanzania uwezo wa kumuumba mtu wa ndoto tuliyemtaja.
Mchakato wa elimu wenye uwezo wa kutoa bidhaa ya aina iliyoelezwa, ni ule ambao unatumia lugha inayoruhusu makusano (interaction) baina ya walimu na wanafunzi, walimu na walimu na wanafunzi na wanafunzi. Matumizi ya lugha ya Kiingereza katika elimu ya sekondari yametunyima bidhaa hii. Walimu na wanafunzi hawaonani kifikra, hawakusani wala hawajadiliani. Kwa miaka mingi, Kiswahili kwa macho ya serikali Tanzania hakistahiki na wala hakiwezi kumudu mawasiliano ya kitaalam. Viongozi na watu wengine wanalitamka jambo hili bila ya ‘ashakum’ wala ‘astaghafiru’. Kinachoumiza roho ni kwamba, kama tutakavyoona hivi punde, dai hili si sahihi kabisa. Aidha, hata kama lingalikuwa kweli, lisingalitangazwa kwa mikogo hiyo. Kwa kuwa lugha huakisi akili ya jamii nzima, inaposemwa lugha yake haimudu hili au lile ni kifani cha kusema akili ya jamii hiyo ni ndogo kuliko ya jamii nyingine. Sina hakika kama jamii hii iko tayari kujipuuza hivi ili iendelee kupuuzwa. Vinginevyo tunajitia katika ushahidi kuwa mnyonge huanza kujinyonga mwenyewe.
Lugha ya kufundishia
Kwa muongo mzima huu, kuanzia 1987 hadi 1997, taifa kwa sehemu kubwa, limeendelea kutoelewa vipengee vya msingi vinavyosukuma mbele gurudumu la maendeleo. Hakuna dalili zozote zinazoonesha nafasi ya utamaduni, na hususan lugha, katika kurutubisha vito vya taifa kwa upande mmoja na kwa maendeleo ya taifa kwa upande wa pili. Taifa limeshindwa, hadi sasa, kugundua ubadhirifu wa vipawa vya taifa shuleni. Ingawa Kiingereza hakijulikani, bado serikali imeshikilia kidinindi kiendelee kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari. Inatia huzuni, na pengine aibu, kuona kuwa Tanzania inaamini kuwa mtoto wa nchi hii atakuwa amesharabu Kiingereza baada ya kupewa saa 800 za kujifunza lugha hiyo katika shule ya msingi (ang. Mochiwa 1991).
Kutojulikana kwa Kiingereza si suala la utafiti tena. Wataalam mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wamelieleza taifa hili kwamba lugha hii haijulikani kwa kiwango cha mawasiliano katika elimu ya sekondari (ang. Mlama na Matteru, 1977, Criper & Donald 1984, Rubagumya 1990). Isitoshe, tume ya Rais (1982) ilipendekeza kitumike Kiswahili badala ya Kiingereza lakini, serikali ililifumbia macho pendekezo hilo.
Hali hii inaonesha kuwa serikali ya Tanzania haiendeshi mambo yake kisayansi badala yake inafuata ushauri wa kihisia usiozingatia hali halisi. Ushauri huo wa kihisia unaelekea kuitisha serikali kwa kutangaza matatizo makubwa yatakayoikumba nchi endapo itaamua kuingiza Kiswahili ndani ya madarasa ya sekondari. Baadhi ya matatizo ni ya hhakika na mengine ni ya kufikirika. Tujipe fursa ya kuyaangalia.
Matatizo ya kutumia Kiswahili
Matatizo au vikwazo vinavyotajwa sana tunaposhauri kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili katika uhai wa taifa hili ni mengi. Aidha, sababu za kushikilia matumizi ya Kiingereza katika shule za sekondari ni nyingi. Lakini Maghimbi (1995) angepata nafasi ya kutangaza sababu za kushikilia Kiingereza na kutupilia mbali Kiswahili – mwenyewe sababu hizo anaziita Tasinifu – ametaja 25. Baadhi ya tasnifu hizo ni: kuogopa kuwa wa kwanza katika mabadiliko, ukosefu wa vitabu vya taaluma, gharama, kuanguka kwa viwango vya elimu nchini, kuvunjika kwa mashirikiano ya kitaalam na uchanga wa Kiswahili. Kwa makusudi ya makala haya matatizo haya yatawekwa katika matapo makuu mawili: nafsi ya lugha yenyewe na utekelezaji wa sera ya Kiswahili sekondari. Tutaanza na nafsi ya lugha.
Nafsi ya lugha
Hofu kubwa ambayo inasambazwa na washauri ina mwega ndani ya Kiswahili chenyewe. Kiswahili, inadaiwa, hakina msamiati. Ingawa dai hili ni kweli lakini inasaliti udhaifu wa aina tatu. Mosi, inaelekea wanaotangaza dai hili kwa pumzi zote, hawajui lugha ni nini. Kwa nafsi yake, lugha ni sarufi yake na si msamiati wake. Hawajui kwamba asilimia kubwa ya msamiati wa Kiingereza – lugha inayotukuzwa kupita kiasi – si wake; ni wa kusharabu. Hivyo basi, matumizi ya Kiswahili katika nyanja za elimu hayawezi kuleta matatizo kwani, ikiwa kitapungukiwa na msamiati, Kiswahili kinaweza kuchukua/kutohoa maneno kama ilivyofanyika katika ukuaji wa Kiingereza. Kinachotakiwa kubadilika si msamiati bali sarufi. Wanafunzi shuleni hawashindwi kwa sababu ya msamiati mgumu bali wanashindwa na sarufi ngumu ya Kiingereza.
Pili, njia ya kuondoa tatizo la msamiati, washauri wanasema, ni kuahirisha kwanza matumizi ya Kiswahili ili uundwe msamiati kwanza, Ushauri huu hudhihirisha kutojua kuwa lugha, kama ulivyo utamaduni, hujirekebisha kwa kulingana na mahitaji mapya. Isitoshe, maana ya ushauri huu ni kutaka Tanzania itayarishe Kiswahili kwa matumizi yatakayotangazwa baadaye. Ushauri huu, zaidi ya kuhuzunisha, unapingana na maumbile. Maneno na semi hujengwa na wazungumzaji wenyewe katika hizo shughuli zao. Mkemia atazua maneno kwa kulingana na kile anachokiona akilini mwake au tuseme katika taaluma yake. Wasio na utaalamu wa kemia hawawezi kuratili hali halisi ya taaluma hiyo. Kwa maana hii, tunapozungumzia mabadiliko ya lugha ya kufundishia, tunatangaza changamoto kwa wataalamu wote – wakemia, wafizikia, wahandisi n.k – wajenge msamiati na semi mwafaka kwa taaluma zao. Kwa mantiki hii hata kesho Kiswahili kingeweza kuingia katika maabara ya shule ya sekondari maadam walimu ni Watanzania.
Tatu, washauri hao wanasahau kuwa vinavyoelea vimeundwa. Ikiwa lugha yetu ina kasoro zozote ni juu yetu sote kusimama kidete kuirekebisha katika hima ya kujiletea maendeleo yetu. Kuijenga lugha hii ikawa chombo chenye uwezo wa kuchanuza mikondo yote ya fikra za wanajamii ni hatua muhimu katika maendeleo.Aidha, ikiwa lugha ni miongoni mwa mbinu za jamii za utashi nusura, kwa kufanya hivyo, jamii hujijengea mtandao wa mawasiliano utakaolea changilizi ya maarifa. Taifa ambalo watu wake wamegawanyika kimawasiliano hawana changilizi ya maarifa. Maana, inagawa Kiswahili kinazungumzwa na wote, lakini fikra na mijadala ya kitaalamu, hivi sasa, haina mikondo katika lugha hii. Hivyo, kama Waaarabu wa Pemba, Kiingereza ndicho kilemba cha wasomi na asiye na kilemba hicho hafaidiki na mazungumzo yao.
Hofu nyingine maarufu iliyoenea na inaendelea kusambazwa na washauri inahusiana na kukosekana kwa vitabu vya kitaaluma. Wataalamu wetu – pengine pamoja na sisi wenyewe – wanagwaya wanapoichungulia maktaba ya Kiswahili ilivyosinyaa. Wanadai kwamba, vitabu vyote vya kitaaluma vimeandikwa kwa Kiingereza. Hivyo haitakuwa busara wala kwa faida yetu endapo tutaacha Kiingereza kitoke madarasani mwetu. Hofu hii nayo ni imara kwa kiasi fulani cha masafa. Lakini ikiangaliwa kwa jicho la karibu, itaonekana kuwa hoja hii inalegalega na inatia kiinimacho katika tatizo. Hii, kwa upande mwingine, ni hoja inayodai kuwa jambo linalotafakariwa haliwezekani mpaka Kiswahili kiwe na vitabu vyake vya kitaaluma. Kila mtu anajua kuwa kutokuwako kwa vitabu vya taaluma ni jambo la hakika. Lakini kama ilivyokuwa katika suala la msamiati, matatizo ya kukosekana kwa vitabu ni changamoto kwa wataalamu wetu. Wataalamu wetu wataanza kuandika vitabu vya taaluma zao baada ya kujua kuwa kuna wasomaji na/au wanunuzi.
Utaratibu wa kuanza kutumia Kiswahili katika sekondari, ninathubutu kusema, ndio ambao utajenga mwega wa usomi wenye manufaa. Sasa hivi wasomi wengi hawafikirii kuandika vitabu kwa sababu wanaweza kufanya kazi zao kwa kutegemea vitabu vya jamii nyingine. Hivyo kitendo cha kuanzisha mijadala ya kitaalam kwa Kiswahili kitaanza kutengua mihimili ya utegemezi wa kisomi.
Swali ambalo linakuja akilini haraka ni lile linalohusu vitabu vya kutumiwa wakati vya Kiswahili vinaandikwa. Aidha, kutokuwako na vitabu vya taaluma si suala la kuzua au la kukichukia Kiswahili. Namna ya kulikabili suala hili ni kukifanya Kiswahili kifundishie kwa sauti, Kiingereza kifundishie kimya kimya. Maana ya tamko hili ni kwamba Kiswahili kiendeshe majadiliano darasani na Kiingereza kiwapatie wasomi wetu maarifa kutoka vitabuni. Kwa maneno mengine Kiingereza kiendelee kuwa lugha ya maktaba. Utaratibu huu usiwe wa muda bali uwe wa kudumu katika jamii. Utaratibu huo utawataka wanafunzi wasome vitabu na marejeo mbalimbali kwa Kiingereza lakini ufundishaji, majadiliano, mazoezi na tathmini vifanyike kwa Kiswahili. Aidha, huu ndio utaratibu unaotumika katika ufundishaji wa Isimu katika Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu.
Utaratibu wa kumlazimisha mwanafunzi aeleze maarifa yake kwa lugha asiyoijua, kama ilivyo sasa, hutupotezea watu wengi wenye vipawa. Katika makala fulani, (Mochiwa 1991:15) niliuliza swali: ikitokea kwamba mwanafunzi ameulizwa: What is ice? na akajibu kwa Kiswahili: ni maji yaliyoganda: tutasema amekosa au amepata? Tukisema amekosa, amekosa nini? Haya ni miongoni mwa matatizo yanayodhihirisha udhaifu wa sera yetu ya lugha katika elimu. Kwa sera hii wasio na vipawa vya kujifunza lugha hupotea hata kama wanavyo vingine ambavyo vingeleta tumaini jipya katika jamii. Kwa hekima ya Tanzania, mpaka sasa, kujua ni kujua Kiingereza na /au kwa Kiingereza.
Suala lililojadiliwa hivi punde ni suala la uhusiano wa lugha na elimu. Tumezoezwa kuchanganya elimu na lugha. Mtu anayemwaga Kiingereza vizuri hufikiriwa kuwa ana akili, tena amesoma sana. Maana, kama Whiteley (1971) alivyopata kutamka, kwetu, Kiingereza ni elimu, na elimu ni Kiingereza. Katika miaka kumi hii iliyopita, kigezo kikuu cha tathmimi ya watu ya kuanguka kwa kiwango cha elimu nchini ni udhaifu wa wanafunzi katika Kiingereza. Inadaiwa kuwa, watoto wanafika kidato cha nne bila uwezo wa kuandika barua ya mistari miwili ya Kiingereza. Kitu ambacho wangezingatia ni kwamba Kiingereza kimemzuia mwanafunzi asikuze uwezo wake wa kufikiri na kutanzua tata. Lakini badala ya kulizingatia tatizo hili wazazi wengi wanasikitika kuwa watoto wao wanajua Kiswahili tu, eti hii ni hasara!Wazazi wanaosema kuwa watoto wao wamepata hasara kwa kujua Kiswahili wanaendeleza fikra ya usawa wa Kiingereza na elimu. Lakini kinyume cha bahati, watoto wao hata hicho Kiswahili hawakijui! Aidha, kujua Kiingereza fasaha si usomi wala akili. Lugha ni suhula tu (facility) ya kuchanuzia yale tunayofikiri. Hivyo, katika tathmini ya elimu haitoshi kupima uwezo wa kusema tu bila ya kupima uzito wa lile linalosemwa pia. Tathmini sahihi ya viwango vya elimu ni lazima izingatie jinsi Kiingereza kilivyosahilisha au kuleta pingamizi katika uelewa wa wanafunzi. Kiingereza ni chanzo cha kuanguka kwa viwango vya elimu kwa sababu hakifai kwa matumizi ya lugha ya kufundishia.
Gharama
washauri wetu wameshikilia kidinindi kuwa kukiingiza Kiswahili katika madarasa ya sekondari kuna gharama kubwa na za namna mbalimbali. Miongoni mwa gharama hizo ni ile ya matayarisho. Watu wengi wanafikiri au ni ubinu wao wa kuchelewesha utekelezaji wa matumizi ya Kiswahili sekondari – ni lazima vitabu vyote, vya kiada na ziada, vifasiriwe kwa Kiswahili. Mradi huo utaligharimu taifa mabilioni ya fedha. Baadhi ya washauri, Maghimbi (1995) kwa mfano, wanatangaza kwa midomo mipana kwamba Kiswahili hakiwezi kuwa lugha ya kufundishia mpaka vitabu vyote vya kitaaluma vimefasiriwa na kuchapishwa. Kwa kweli ikiwa Tanzania inafikiri haiwezi kutumia Kiswahili katika shule za sekondari mpaka vitabu vyote vya taaluma vifasiriwe ni kana kwamba inasema Kiswahili hakitafundishia elimu ya sekondari.
Kwa nchi maskini kama yetu, kuamua kubadilisha lugha ya kufundishia ni ujuba ikiwa, mradi wa kufasiri vitabu ni muhimu kiasi hicho. Ilivyokuwa hakuna haja ya kufasiri kitabu chochote, hakuna sababu ya kuchelewesha hatua ya kukiingiza Kiswahili katika madarasa ya sekondari. Mabadiliko ya lugha ya kufundishia ni hatua muhimu na ya kwanza kabla ya kuingia katika mchakato wa maendeleo ya kijamii. Kwamba hadi leo tumo katika majadiliano ni dalili kuwa bado hatujapafahamu pa kuanzia safari yetu ya maendeleo.
Gharama nyingine kubwa iliyojizonga akilini mwa washauri wetu ni ule uwezekano wa kutoka kwenye kambi ya wasema Kiingereza. Itakumbukwa kwamba nchi za Kiafrika zimo katika makambi ya lugha za wale waliozitawala. Tanzania na nchi nyingine zilizotawaliwa na Waingereza ni za kambi ya Anglophone. Zilizotawaliwa na Wareno zimo katika kambi ya Lusophone na za Wafaransa ni za kambi ya Francophone. Kwa mtazamo huo washauri, kama Maghimbi (1995) wanafikiria haitakuwa salama kama tutatoka kwenye kambi ya Waingereza. Msingi wa rai hii uko mara mbili. Kwa upande mmoja, washauri wanalinda mazoea na kwa upande wa pili wanafirki kwamba Watanzania watakuwa wameandalika kwa masomo nchi za nje. Pengine inasemekana kuwa kuendeleza mtindo huu kunawapatia Watanzania uwezo wa kuwasiliana na watu wa nje.
Tathmini yagharama hizi inaonesha kuwa ushauri unaelekeza kwenye haja ya uanachama wa u-anglophone bila kujiuliza kama upo uwezekano wa kuupata. Isitoshe ushauri haukuzingatia kwamba kazi kubwa ya lugha katika elimu si kutufutia uanachama. Ushauri umeendelea kulifumbia macho suala la kutojulikana kwa Kiingereza nchini Anayetumia lugha kwa masomo au kutafuta urafiki ni yule anayejua lugha yenyewe. Je, ni nani ambaye, hadi sasa, hajui kwamba Kiingereza hakijulikani nchini kwa kiwango cha kuendeshea mawasiliano yanayoweza kuonesha fikra pevu?
Zaidi ya kufumbia macho suala la kutojulikana kwa Kiingereza, kuna ule ushauri wa kuwaandaa Watanzania kwa masomo ya nje ambao ni dhaifu. Hii ni kwa sababu, kwa hali ilivyo sasa hivi, si sahihi kufikiri kila penye asasi ya elimu patazungumzwa Kiingereza. Watanzania wamekwenda China, Japani, Ujerumani na sehemu nyingine nyingi mbalimbali ambazo hazitumii Kiingereza. Ke bado watu wale wamesoma. Pengine ingekuwa bora kwa Mtanzania kujifunza lugha yoyote kule inakozungumzwa na wazawa wake kuliko tunavyofikiri tunajifunza Kiingereza hapa ambapo hakina wazungumzaji wazawa.
Hasara ya kung’ang’ania Kiingereza
Baada ya mjadala wa ushauri wa kutelekeza Kiswahili, kikabakia lugha ya kuuzia karanga kwa muda wote huu, ni vyema tutafakari kidogo hasara au tuseme, gharma ya kung’ang’ania Kiingereza. Gharama kubwa tunayobeba ni kuendeleea kwa kutenguka kwa elimu. Kiingereza kinaendelea kuzuia makusano kati ya walimu na wanafunzi na kwa hivyo umaizi wa ubongo wa mtoto haupati nafasi ya kuongezeka. Kwa maana hii, mchakato wa elimu mpaka sasa haujaweza kuwasaidia wanafunzi kujifunza kufikiri, na hasa kufikiri haraka haraka. Ingawa sina ushahidi wa kisayansi kuhusu jambo hili, lakini ninahisi kwamba, kwa kuwa hatukimiliki ipasavyo, tunapokitumia, Kiingereza kinapunguza kasi ya kufikiri. Kama Powell (1997) anavyosema, kujifunza lugha ni kupata mamlaka ya kutawala mazingira na kutawala ulimwengu wa uzoevu. Wanafunzi wasiojua Kiingereza watatarajiwa vipi kutawala mazingira yao au taaluma zao?
Kung’ang’ania Kiingereza katika kuendeshea maisha ya taifa hili kunawanyima wanajamii haki za msingi za binadamu. Nitachukua mifano kutokana na kuchungua sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inahusu haki ya kuishi duniani. Hospitali zimesambazwa nchini kuhakikisha kuwa kila mwanajamii anapata huduma anapougua ili apone. Wahudumu wetu wamejifunza huduma hiyo kwa Kiingereza. Ikiwa sote tunajua kuwa Kiingereza hakifahamiki vizuri, tuna hakika gani kuwa Madaktari na Manesi wao wanaelewana? Lini taifa litagundua hatari ya unasibu wa lugha? Unasibu wa lugha ndio uliosababisha neno moja la Kiarabu lipokewe kwenye Kiingereza kuwa ‘risk’ kitu au tukio la hatari na katika Kiswahili ‘riziki’ kitu cha kukidhi haja! Ingawa sina takwimu,- na si rahisi kuzipata-lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuwako kwa vifo ambavyo vimetokana na mawasiliano butu kati ya Daktari na Nesi, au kutoiva kikamilifu kwa Daktari au Nesi mwenyewe.
Sehemu ya pili inahusu sheria. Ninaambiwa mpaka leo, waheshimiwa wanasheria huweka kumbukumbu zao kwa lugha ya Kiingereza, hata kama washitaki na washitakiwa wametumia Kiswahili au lugha nyingine. Wao wameaminiwa kuwa ‘wafasiri’ wasiojikwaa! Lakini kwa mujibu wa ninavyojua dhati ya lugha, unasibu wake pamoja na matatizo yanayofafanuliwa katika nadharia za tafsiri (ang. Nida 1964), ninahisi kwa nguvu kuwa wako watu ambao wamezama magerezani kwa kutokana na mabadilikobadiliko haya ya lugha. Kosa la tafsiri linaumba hatia ya mshitakiwa. Jambo kama hili linapotokea, kuna mwanajamii mmoja ambaye atakuwa amenyimwa haki yake ya kimsingi. Ni dhahiri kwamba jamii inashindwa kulinda haki za watu.
Sehemu ya tatu inahusu haki ya kujiendeleza. Tanzania ilikuwa maarufu duniani kwa kuweka kipaumbele katika maendeleo ya elimu ya watu wazima. Kinyume cha bahati, jitihadi za mtu anayeanza kujielimisha haziwezi kuvuka elimu ya msingi. Hii ni kwa sababu akipita kiwango cha shule ya msingi hawezi kusonga mbele kwa kuwa hajui lugha ya Kiingereza. Jambo hili linazidi ugumu kwa kuwa mhitimu wa kisomo chenye manufaa atajiendeleza nje ya mazingira ya shule. Sasa ikiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, wenye miaka kumi na nne au kumi na tano, wanashindwa kujifunza Kiingereza mbele ya mwalimu wao, mtu aliyeanza kisomo cha manufaa na miaka arobaini ataweza kujifunza Kiingereza chini ya mwembe? Ikiwa hana Kiingereza, mwanakisomo atajiendelezaje? Kwa utaratibu wa sasa, matumizi ya Kiingereza yanazuia mienendo ya elimu nchini. Hivyo elimu si ya wote bali ni haki ya wachache, tena, wenye kipawa madhubuti cha lugha.
Suala hili lililojadiliwa hivi punde halimwathiri mtu mmoja mmoja tu, bali jamii nzima. Jamii inawazuia watu ambao, kama wangepata nafasi ya kujiendeleza, wangekuwa wabunifu na watundu wa manufaa kwa taifa. Ama, hali hii nayo inahuzunisha. Huenda taifa halipati wasiwasi kwa imani kuwa wavumbuzi au wagunduzi watapatikana Chuo Kikuu. Lakini, kwamba rai hii imepotoka, inaonekana kwa kusoma kwenye magazeti kuwa kuna watu vijijini wanaweza kutengeneza vitu vya kisasa kama silaha. Aidha, labda kwa sababu ya imani ileile ya wavumbuzi kuwa watu wa Chuo Kikuu, watu hawa wanapogundulika hupata misukosuko. Isingekuwa hivyo, watundu hawa wangepewa kipaumbele. Watu hawa, kwa kuonekana umuhimu wao kwa taifa, wangeengwaengwa na kubembeslezwa wajiunge na jeshi ili taifa lifaidike.
Makusudi yangu hapa ni kwamba si siku zote wavumbuzi watatoka vyuoni. Kuendelea na matumizi ya Kiingereza katika elimu ya juu ni kuziba uwezekano wa kupatikana kwa watu walio na vito muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Pamoja na umaarufu wake – kwa herufi na harufu-Tanzania haiwezi kukipa Kiingereza kiti kikakaa hapa nchini kwa makusudi ya kuongeza ukuzaji wa umaizi wa Watanzania. Hii haina maana kuwa Kiingereza hakifai au hakitakiwi nchini. Haya si makusudi ya makala. Bali kinachokusudiwa hapa ni kwamba, kwa mazingira tuliyo nayo, upeo wa ufundishaji, muda na mbinu za ufundishaji, si rahisi kukifundisha kikajulikana ganda na kiini. Aidha, wataalamu wengi (Qorro, et al 1987, Trappes – Lomax et al (eds) 1982) wameonesha wazi kuwa Kiingereza hakiwezi kufundishwa hadi aliyefundishwa akafikia kiwango cha umilisi wa kuchambua fikra au viumbile dhahania. Ziko sababu nyingi zinazosababisha hali hii, lakini hapa tutachambua mbili: Muda na mazingira. Tutaanza na muda.
Muda
Tanzania haina budi kuelewa kuwa kufundisha na hasa kujifunza lugha kunataka muda mrefu. Kujua kuwa hivyo ndivyo, tujiulize mtoto mchanga anayejifunza lugha yake ya maziwa anahitaji muda gani. Mtaalam mmoja (ang. Hammerly 1982) alidai kuwa mtoto anatumia saa 18,000 za kujifunza lugha hiyo ya kwanza. Kwa kuwa suala hili halikutiwa ndani ya mizani zetu sawasawa, Tanzania inaona kuwa saa 800 za kujifunza Kiingereza (soma. Mochiwa 1991) katika shule ya msingi zinatosha. Baya zaidi ni kwamba, ilihali anapojifunza lugha ya kwanza mtoto anakutana nayo kwa wakati mwafaka, wakati ambao ubongo na hisia havijui kukataa wala kudharau, lakini mtoto wa shule ya msingi anakutana na Kiingereza kwa wakati usio mwafaka. Anakuwa amekwisha vuka umri wa kawaida wa kujifunza lugha.
Tunapoendelea kuwalinganisha watoto wawili hawa, tunaona kwamba anayejifunza lugha ya mama hana ratiba yoyote ya shughuli. Yeye hatumwitumwi na wala halazimishwi kujifunza kipengee fulani kilichomo mwenye muhtasari. Lakini huyu aliye shuleni hupewa hizo saa 800 za Kiingereza ndani ya ratiba ya masomo mengine. Kana kwamba hii haitoshi, hizo saa mia nane zimetawanywa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia darasa la tatu hadi la saba. Yule mtoto aliye nyumbani ana saa nyingi na haziingiliwi na mambo mengine isipokuwa usingizi tu.
Tunapolinganisha muda huu mrefu wa kusharabu lugha, itakuwa hatuangalii mambo kiuhakikifu (objectively) kama tutatarajia Kiingereza kijengeke katika akili ya mtoto kwa muda huu mfupi. Ikiwa tunataka Kiingereza kijengeke basi inabidi ratiba ya shule isogelee hizo saa 18,000. Lakini hii ina maana kwamba, kwa muda wa miaka isiyopungua mitatu, Watanzania hawana budi wazamishwe kwenye programu ya Kiingereza. Kwa rai yangu hatua ya namna hii haiwezekani kwa sababu nyingi, lakini kubwa, ni gharama yake ya mali na muda.
Mazingira
Mtoto anapojifunza lugha ya kwanza anafunikwa na lugha anayojifunza. Mtoto anayejifunza Kiingereza shuleni hana bahati hiyo. Kwake, Kiingereza hakisikiki, maana hakitumiki kuongoza maisha ya kila siku. Hivyo, dafaa za kukisikia Kiingereza ni chache sana. Ni lugha ambayo itasikika darasani na si muktadha utakaomfanya mtoto aone jinsi lugha yenyewe inavyofanya mambo yaende.
Mazingira ya ufundishaji wa Kiingereza ni ya kuigiza heba ambayo haipo katika jamii. Maadamu ‘Kiingereza’ maana yake ni ‘kwa namna’ au kwa ‘mila ya’ au ‘mwenendo wa’ Waingereza, Kiingereza ndani ya mazingira ya Kiswahili kinahitaji jitihada kubwa za kukifanya kimee. Kujifunza namna au mwenendo wa Kiingereza kunahitaji uamuzi na nidhamu ya kisaikolojia. Heba hiyo hiyo iliyosisitizwiwa umuhimu wa kujivunia. Uswahili, Uafrika ndiyo hiyo hiyo inayoingizwa katika majaribu ya kuenenda naau kujifasili kwa Kiingereza. Migongano ya aina hii ndiyo inayosababisha elimu nchini Tanzania kuwa maigizo na si maisha.
Mwisho
Mchakato wa elimu katika Tanzania hauna tofauti na maigizo kwa sababu mbili. Kwanza, ingawa unatakiwa umfanye mpokeaji awe ‘huyo mtu wa ndoto’ lakini kwa kutokana na sera ya lugha iliyopo, mchakato wa elimu unamfanya mpokeaji awe KAMA ‘huyo mtu wa ndoto’ Mtu huyo wa ndoto si Mtanzania bali ni Mwingereza. Ilivyokuwa haiwezekani, Mngoni kuzaa Mzigua, vivyo hivyo Mtanzania hawezi kuzaa Mwingereza. Kwa mantiki hiyo, mchakato wa elimu unampeleka mtanzania kuzaa ‘Kizuu cha Mwingereza’ au Mmarekani, mpokeaji wa elimu ya Tanzania atakuwa anaingiza heba ya Kiingereza na/au Kimarekani kwa mwenendo wa fikra na msemo. Mpokeaji huyo hataishi kwa heba ya kwao bali ataishi kwa heba ya kuazima.
Pili, mpokeaji wa elimu hii atakuwa ana utapia elimu mkubwa kwa sababu ya pingamizi la lugha ambalo humkabili katika mchakato mzima. Hatapata kiwango cha weledi sawa na mtu wa ndoto ambaye Tanzania imemwekea. Katika mazingira haya, mfumo wa elimu unakuwa mchakato wa kuingia utumwani na si wa kumpatia uhuru kama unavyotarajiwa na Nyerere na Freire (op.cit). Anapoumaliza mfumo wa elimu, mpokeaji hatalingana na Mwingereza kwa uwezo wa kuchambua, kuwaza, kusasanya mambo wala kusasanyua. Kutokana na kuung’amua ukweli huu, mhitimu atasema moyoni mwake ‘Wazungu,wazungukeni!’
Zaidi ya kuufanya kuwa mchakato wa kuvuruga mfumo wa kujiamini wa mpokeaji sera ya lugha inamnyima mpokeaji haki za msingi za kibinadamu. Haki hizo ni pamoja na ya kujielimisha, ya mazingira ya kupata tiba isiyo na madhara kwake na ya kupata haki mbele ya sheria. Watanzania hawana hakika ya kukuza akili zao, ya kupata matibabu sahihi wala ya kutendewa haki wanapokabiliwa na daawa. Yote haya ndiyo matokeo ya maigizo ya kielimu yanayosababishwa na matumizi ya Kiingereza katika elimu. Wanaonufaika katika vurumai hii ni watu wenye kipawa cha lugha tu. Aidha vurumai hii hunufaisha sana mataifa ya nje kwa sababu kwao Watanzania ni ‘wateja’.
|
|
|
NAFASI YA KISWAHILI KATIKA JAMII YA AFRIKA MASHARIKI, KATI NA KUSINI |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 04:47 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Massamba, D.P.B na wenzake (2001:26-28) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. TUKI.Dar es Salaam
Katika sehemu ya 1.1 tulisema kwamba lugha ya Kiswahili ndiyo lugha muhimu sana katika eneo lote la Afrika Mashariki na kati. Tulisema vile vile kwamba lugha hii ina nafasi ya pekee katika nchi ya Tanzania na Kenya. Hii ni kwa sababu lugha hii ni lugha ya taifa na pia lugha rasmi katika nchi zote mbili. Wananchi wengi wa Afrika mashariki wanajua na huitumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao. Kwa hiyo ina maana kwamba lugha hii ina nafasi ya pekee katika mambo muhimu kama utamaduni, siasa na uchumi. Pengine yafaa kufafanua kidogo jambo hili.
Wataalamu wengi wa masuala ya utamaduni hukubaliana kwamba kwa kiasi kikubwa lugha ni kielelezo cha utamaduni. Ukweli huo hujidhihirisha katika lugha yenyewe. Ukiichunguza kwa makini lugha yoyote iwayo utagundua kwamba ina vipengekele mbalimbali vya utamaduni vya wasemaji wa lugha hiyo ambavyo vinajitokeza ndani mwake. Mfano mdogo tu ni kwamba wakati kwa Mswahili ndugu wa kiume wa baba ni baba na ndugu wa kike wa mama ni mama kwa mzungu sivyo, kwani Mzungu ana baba (father) mmoja tu na mama (mother) mmoja tu; Mzungu ana dhanna za half-brother (nusu-kaka?) na half-sister (nusu-dada?), ambazo hazimo katika lugha ya Kiswahili. Mswahili akiamua kutumia lugha ya Kiingereza atashindwa kuvieleza vipengele hivi vya utamaduni; hivyo itakuwa njia moja wapo ya kumomonyoa utamaduni. Kwa hiyo basi, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Afrika Mashariki yataendelea kuudumisha utamaduni wetu.
Nafasi ya lugha ya Kiswahili katika masuala ya siasa ni jambo ambalo halihitaji kupigiwa ngoma. Tumekwishaona jinsi lugha hii inavyotumika kama chombo muhimu sana cha kuunganisha watu na kuleta umoja, Kwa kuwa lugha hii ndiyo itumiwayo na watu wengi katika Afrika mashariki ndiyo lugha peke yake inayoweza kuleta uelewano katika masuala ya kisiasa kwa wananchi wa eneo hili, siyo lugha nyingine. Aidha, lugha ya Kiswahili ndiyo lugha muhimu iwaunganishayo wananchi wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Kwani katika maeneo haya kuna lugha mbalimbali zinazotumika, lugha peke yake inayotumika kote ni Kiswahili.
Lugha ya Kiswahili ni lugha muhimu sana katika Afrika Mashariki kwa upande wa masuala ya uchumi. Lugha ambayo inafahamika kwa watu wengi ndiyo lugha ifaayo kutumiwa katika mambo na mawasiliano ya kibiashara. Tangu zamani wananchi wa Afrika Mashariki wamekuwa wakiitumia lugha hii katika shughuli zao za kibiashara. Kiswahili kinamwezesha Mkenya kwenda Tanzania, hata vijijini akafanya biashara bila wasiwasi wowote; halikadhalika Mtanzania anaweza kwenda Kenya vijijini akaendesha shughuli zake za kibiashara bila tabu ya kutafuta mkalimani. Na kwa hakika hii si kwa Tanzania na Kenya tu; hali ni hiyo hiyo kwa upande wa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kwa kiasi fulani hata katika Rwanda na Burundi pia.
Kwa ujumla lugha ya Kiswahili ni lugha muhimu katika harakati zozote za wananchi wa sehemu za Afrika Mashariki na Kati. Kwa misingi hiyo, lugha hii haina budi kukuzwa na kuendelezwa zaidi ili matumizi yake yazidi kuwa mapana na toshelevu kwa kiwango kinachotakiwa katika sehemu zote hizi.
|
|
|
KISWAHILI NI LUGHA YA AFRIKA |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 04:34 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Kiswahili ni kati ya lugha nne za taifa la DRC. Rais wa DRC, Joseph Kabila, anaongea Kiswahili sanifu. Kwa vile rais wa nchi anaongea Kiswahili sanifu, hii itakuwa chachu ya kukiboresha Kiswahili cha DRC, na kukieneza kwenye nchi zinayoizunguka DRC, kwa upande wa kaskazini. Kiswahili ni lugha ya taifa la Tanzania, Uganda na Kenya. Ingawa Kiswahili, si lugha ya taifa la Rwanda na Burundi, lakini vita vya maziwa makuu vimekifanya Kiswahili kuzungumzwa karibu na watu wote wa Rwanda na Burundi. Mipango iko mbioni kukifundisha Kiswahili kwenye shule za msingi za Rwanda na Burundi. Msukumo huu unatokana na nchi hizi mbili kuomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Kwenye miaka ya themanini, Kenya ilifanya jitihada nyingi kukiendeleza Kiswahili. Kiswahili lilifanywa somo la lazima kwenye shule za sekondari. Matokeo yake yameanza kujitokeza miongoni mwa kizazi kipya cha Kenya, kwa kuongea Kiswahili sanifu kuliko kile Kiswahili cha kizazi cha miaka ya nyuma. Pia ongezeko la vyuo vikuu nchini Kenya vimeongeza ufanisi wa Kiswahili, kila mwaka zaidi ya vijana 2000 wanaokifahamu vizuri Kiswahili wanahitimu vyuo vikuu. Hii itachangia kuwapata walimu wazuri wa kufundisha lugha ya Kiswahili na wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili. Ingawa magazeti ya Kiswahili hayajaongezeka kwa kasi kubwa, lakini uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili uko juu zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania. Kenya inatoa vitabu vingi vya Kiswahili na usambazaji wake ni mzuri kuliko wa Tanzania. Pia Wakenya wanasoma vitabu kuzidi watanzania. Bidii ya Kenya, katika kukikuza Kiswahili itachangia kwa kiasi kikubwa kuieneza lugha hii katika nchi zinazopakana nayo upande wa kaskazini, kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia. Tukizingatia kwamba wakimbizi wengi kutoka katika nchi hizi wamekuwa wakiishi nchini Kenya. Hizi ni dalili za kukipanua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima!
Tofauti na Tanzania, ambapo Kiswahili, karibu kinatumika kila sehemu katika jamii, Kenya Kiswahili kinatumika kama lugha ya siasa, dini na wasomi. Ingawa hii inaonyesha picha hasi ya kukiendeleza Kiswahili katika jamii nzima ya Wakenya, lakini pia kwa njia hii Kiswahili kinaweza kuongeza kasi ya kuongea lugha ya kisayansi na kiteknolojia na kujikita katika utandawazi kwa haraka zaidi ya Tanzania.
Kwenye miaka ya Sabini, Iddi Amin, alikitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa ya Uganda. Lakini waganda na hasa “Baganda” hawakukipokea Kiswahili kwa vile wanaipenda sana lugha yao ya “Luganda”. Sababu nyingine ni kwamba wanajeshi wa Iddi Amin, walitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi. Matendo maovu ya jeshi la Iddi Amin na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo, yalikipaka matope Kiswahili na kuwafanya watu wa Uganda, kukichukie. Pia waganda walimchukulia mtu anayeongea Kiswahili kuwa ni “Mswahili” mjanja mjanja na mtu asiyeaminika. Lakini pia waganda wengine walikihusisha Kiswahili na Uislamu, maana Waislamu walikitumia kama lugha ya dini kwa kukichanganya Kiswahili na Kiarabu, au kutafsiri Kiarabu katika kistahili. Kwa nchi kama Uganda, ambayo imepitia migongano na michafuko mikubwa ya kidini, kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kuamsha vita kati ya Wakristu na Waislamu.
Jeshi la Museveni, na Museveni mwenyewe walitumia Kiswahili. Hadi leo hii Kiswahili ni lugha ya jeshi la Uganda. Hii haikuwavutia waganda waliokuwa wamechoka na utawala wa kijeshi. Hivyo Kiswahili ilibaki ni lugha ya jeshi na biashara ya magendo kati ya Uganda, Tanzania na Kenya.
Kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo waganda wanaiona ina faida kubwa kuliko hasara, wameanza kuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili. Serikali ya Uganda imepitisha kwamba kuanzia mwaka kesho Kiswahili litakuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari. Huu utakuwa ni msaada mkubwa wa kukikuza Kiswahili na kukipatia picha ya kuwa lugha ya Afrika ya Mashariki na hatimaye Afrika nzima.
Kwenye makala iliyopita nilielezea jinsi Tanzania, ilivyofanikiwa kukisambaza Kiswahili nchi nzima na kuifanya lugha hii kuwa ya taifa ingawa haikutangazwa kisheria. Hivyo sirudii haya kwenye makala hii. Labda kutaja tu hapa kwamba Mwalimu Nyerere, kukubali Dar-es-Salaam, kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, kulisaidia kukisambaza Kiswahili katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika.
Mpango wa IPP Media Group wa kuanzisha gazeti la Kiswahili liitwalo Afrika ya Mashariki, utakuwa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili lugha pana inayoweza kukubalika Afrika nzima. Huu unaweza kuwa uwanja wa kuzua malumbano na majadiliano ya kuelekea kukikomaza Kiswahili kama enzi zile washairi wa Afrika ya Mashariki walivyokuwa wakijibizana na kulumbana katika uwanja wa ushairi. Bado kuna ushahidi wa kutosha jinsi mashairi yalivyosaidia kukikuza Kiswahili.
Vita vya ukombozi kusini mwa Afrika, vimekifanya Kiswahili isiwe lugha ngeni katika nchi za Zimbabwe, Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika ya kusini. Lakini pia wakimbizi wa Sudan, Somalia na Ethiopia, walioishi Kenya na Uganda wamesaidia kukisambaza Kiswahili hadi kwenye nchi zao. Wafanyabiashara wa Kisomali ambao hufanya kazi ya kusafirisha mizigo kwenye magari ya mizigo kwenye maeneo yote ya Afrika ya Mashariki, Kati na kusini wamekuwa mabalozi wa kuisambaza lugha ya Kiswahili.
Ingawa kuna lugha zingine za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi kama Kihausa. Kiswahili kinachomoza zaidi kwa sababu si lugha inayofungamana na kabila au taifa Fulani. Mfano ni tofauti na Kihausa. Ingawa Kihausa kinazungumzwa na watu wengi wa Afrika ya Magharibi, kinafungamana na kabila kubwa la Wahausa ambalo limekuwa kwenye migogoro na mapigano na makabila mengine kwa muda wa miaka mingi. Lengo lolote la kutaka kukifanya Kihausa kuwa lugha ya Afrika nzima, ni lazima litaamsha chuki miongoni mwa makabila makubwa ya Afrika magharibi ambayo nayo yangependa lugha zao zichukue nafasi ya kwanza.
Profesa Mulokozi, kwenye mada yake: “Kiswahili as a National and International Language” Anaelezea kisa alichosimuliwa na Kanyama Chiume, pale Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, mwaka 2002; kwamba mwaka 1959, wapigania uhuru wa Afrika walikuwa na mkutano ulioitishwa na Sekou Toure, katika mji wa Conakry, Guinea, ili kupanga harakati za kudai uhuru. Mkutano huu ulihudhuriwa na watu kutoka nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza na Kifaransa. Tatizo kubwa lililojitokeza katika mkutano huo ni lugha ya kutumia. Wajumbe walikaa wakitafakari zaidi ya masaa mawili juu ya lugha ya kutumia katika mkutano huo ili wote waweze kusikilizana na kuchangia hoja. Waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza hawakufahamu Kifaransa na wale waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kifaransa hakukifahamu Kiingereza. Huu ulikuwa mtindo wa wakoloni, wakutaka kufundisha lugha zaidi ya lugha yao. Baada ya muda mrefu wa kutafakari namna ya kuendesha kikao hicho kigumu, Kanyama Chiume, ndiye aliyeokoa jahazi. Alipendekeza: Kwa vile yeye alifahamu Kiswahili na Kiingereza, na Patrice Lumumba, alifahamu Kiswahili na Kifaransa, mkutano ungeweza kuendelea kwa wajumbe waliokuwa wakitumia Kiingereza, kuongea kwa Kiingereza na Kanyama Chiume, kutafsiri yote kwa Kiswahili ili Patrice Lumumba, aweze kutafsiri Kiswahili kwa Kifaransa. Vilevile na wale wa upande wa Kifaransa waliongea kwa Kifaransa na Patrice Lumumba, alitafsiri kila kitu kwa Kiswahili ili Kanyama Chiume, aweze kutafsiri kwa Kiingereza.
Kufuatana na maelezo ya Kanyama Chiume, mkutano huo uliendelea kwa ufanisi mkubwa ingawa ulikuwa wa kuchosha. Lakini wajumbe walielewana vizuri kwa msaada wa Lumumba na Kanyama Chiume waliokuwa wakikifahamu Kiswahili. Ndiyo kusema Kiswahili kiliwaunganisha Waafrika katika mkutano huo. Na kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Kiswahili ni tofauti na Kihausa au lugha nyingine maana si lugha ya Kabila Fulani au taifa Fulani. Mfano katika mkutano huu wa Conakry wa mwaka 1959, Patrice Lumumba alitokea Congo na Kanyama Chiume, alitokea Malawi! Kiswahili, haikuwa lugha ya kabila la Lumumba na wala haikuwa lugha ya kabila la Kanyama Chiume. Tunaweza kusema Kiswahili ilijitokeza kama lugha ya Waafrika katika mkutano huo. Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri, kama si uvivu na kutojali kwa watu wanaojiita chimbuko la Kiswahili, kama vile watanzania, leo hii Kiswahili, kingekuwa kimepiga hatua kubwa katika Bara zima la Afrika na duniani kote.
Mfano mwingine anautoa Profesa Mulokozi, ni ule wa mwanamapinduzi Che Guevara, wakati akiongoza harakati za mapambano ya vita vya msituni kuikomboa Congo, akiwa bega kwa bega na Laurent Kabila, alilazimika yeye na wapiganaji kutoka Cuba, kujifunza Kiswahili, hadi yeye Che Guevara, akabatizwa jina la Kiswahili la Tatu! Waligundua kwamba hii ndio lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha Waafrika waliokuwa wakipigana msituni na kwamba adui aliyeongea Kiingereza na Kifaransa asingeweza kufuatilia nyendo zao katika mawasiliano. Che Guevara, ni mwanamapinduzi anaheshimika duniani kote na historia yake imejaa mvuto wa pekee na kati ya mvuto huu ni lugha ya Kiswahili!
Lakini kitu kinachokifanya Kiswahili kionekane kuwa ni Lugha ya Afrika, wale wanaoisukuma mbele si watu wa Afrika Mashariki na wala si watu wanaotoka kwenye nchi ambazo zinaaminika kuwa ni nchi za Kiswahili kama Tanzania na Kenya. Tumeona mfano wa Kanyama Chiume na Lumumba. Mfano mwingine ni wa Chisano kutoka Msumbiji kwenye nchi inayoongea Kireno, na lugha nyingine za Kiafrika ambazo ni kubwa pia, kuwa rais wa kwanza wa Afrika, kuhutubia Umoja wa nchi za Afrika, kwa lugha ya Kiswahili.
Mkutano wa viongozi na wataalam wa maziwa makuu uliofanyika Aprili 2002 kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ulitoa mwito wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mataifa ya maziwa makuu.
Katika miaka ya sitini Mwandishi Maarufu wa Nigeria Wole Soyinka , alitoa mwito wa kukitangaza Kiswahili kuwa ni lugha ya Afrika nzima. Nigeria, kuna lugha kubwa za Kiafrika, lakini Wole Soyinka, aliguswa na lugha ya Kiswahili! Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.
Mwito huu ulirudiwa tena na mwandishi mwingine wa Ghana, Ayi Kwei Armah, mnamo mwaka wa 1985, yeye alikiona Kiswahili kama lugha ambayo inaweza kuingiza maneno mengi kutoka kwenye lugha nyingine za Kiafrika na kukifanya Kiswahili kuwa tajiri kwa msamiati. Ayi Kwei Armah, aliishi na kufanya kazi Tanzania. Alifundisha kwenye Chuo cha Walimu Chang’ombe. Kitabu chake “Te Beautiful Ones Are Not Yet Born” kimetafsiri katika Kiswahili: “Wema Hawajazaliwa”.
Kiswahili kilitumika kwenye mkutano mkuu wa UNESCO, Parish, Ufaransa. Hizi ni dalili kwamba Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha kubwa kutoka Afrika.
Mwanzoni mwa miaka ya themanini, UNESCO iliamua juzuu nane (8-volume) za historia ya Afrika zitafsiriwe kwenye lugha zaidi ya tatu za Kiafrika, Ukiondoa Kiarabu, lugha nyingine zilizopendekezwa ni Hausa,Fulfulde na Kiswahili. Juzuu za Kiswahili zimekamilika na kuchapishwa. Huu ni mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika historia ya Afrika. Kwa wale wanaofikiri kwamba Kiswahili si lugha ya kisomi, juzuu hizi ni changamoto kubwa kwao. Na huu ni ushahidi kwamba Kiswahili ni lugha ya Afrika.
Kwa vile utandawazi unatishia kuzimeza nchi za ulimwengu wa watu na hasa Afrika, kwa karibu kila kitu, ni vyema na Afrika itafute kitu cha kuuza kwenye utandawazi. Tukishindwa kuuza vitu vingine kama utamaduni, kazi za mikono na bongo zetu, basi tuuze lugha zetu na hasa zile zinazoelekea kukubalika Ulimwengu mzima kama vile Kiswahili.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
|
|
|
Katiba itambue Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 04:26 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Mjumbe wa Tume ya Katiba, Mohamed Yusuf Mashamba akifafanua jambo wakati wa ukusanyaji wa maoni katika Kijiji cha Kitere, Halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani hapa juzi.Kushoto ni Mjumbe mwingine wa Tume hiyo, Dk.Sengondo Mvungi. Picha na Abdallah Bakari
Kwa ufupi
“Wenyeviti wa vijiji, vitongoji walipwe mishahara, wazee umri wa miaka 60 walipwe posho ya uzeeni kila siku” alisema Singa.
Abdallah Bakari, Mtwara
DIWANI wa Kata ya Ziwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani hapa, Mohamedi Mkiwa (72) amependekeza katiba ijayo itamke kuwa Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na shughuli zote za nchi zitaendeshwa kwa lugha hiyo.Akitoa maoni yake juzi mbele ya Tume ya Katiba ilipofanya mkutano wa kukusanya maoni ya wananchi hao katika kijiji cha Madimba, Ziwani na Msangamkuu, diwani huyo alisema katiba ya sasa haitambui Kiswahili kama lugha ya Taifa.
Alisema kukosekana kwa kipengele hicho kunasababisha kupuuzwa kwa lugha ya Taifa na watendaji wa serikali wanaotumia lugha za kigeni katika shughuli za kila siku za utendaji wa serikali.
“Katiba itambue kuwa Kiswahili ni lugha ya Taifa na itamke wazi kuwa shughuli zote za kiserikali zitaendeshwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili” alisema Mkiwa.
Aidha diwani huyo alipendekeza Rais kuongezewa madaraka kwa kuitwa Rais mtendaji badala ya sasa ambapo shughuli za kiutendaji zipo chini ya Waziri Mkuu.
Mkazi mwingine wa Ziwani Hassan Singa (76), alipendekeza viongozi wa vitongoji na vijiji walipwe mishahara kwa kuwa wanatumia muda wao mwingi kuhudumia wananchi.
“Wenyeviti wa vijiji, vitongoji walipwe mishahara, wazee umri wa miaka 60 walipwe posho ya uzeeni kila siku” alisema Singa.
Naye Mkazi wa Madimba,Abdallah Lina (54) alipendekeza siku ya kupiga kura wapiga kura wote walipwe posho kwa sababu wanatumia muda wa siku nzima kushinda kwenye foleni wakisubiri kupiga kura.
Maoni hayo yalihojiwa na Mjumbe wa Tume hiyo, Mohamedi Mashamba, aliyehoji iwapo haoni kwa kufanya hivyo wananchi watakuwa wameuza haki yao, swali ambalo lilijibiwa na Lina kuwa “Viongozi wamegeuza uongozi kuwa mtaji basi ni heri na sisi tukaambulia japo kidogo”
Mashamba alimweleza Lina kuwa iwapo maoni yake yatapitishwa kutakuwa na hatari kubwa ya nchi kutawaliwa na mafisadi, kwa kuwa wataweza kuwalipa wapiga kura.
Awali Mwenyekiti wa mkutano huo, Dk. Sengondo Mvungi aliwataka wananchi hao kuwa wawazi kutoa maoni yao ili watunge Katiba itakayoondoa matatizo yao.
Mvungi alisema ni vema kwa wananchi wakaelewa kuwa Katiba waitungayo itadumu kwa zaidi ya miaka 50 ijayo na kwamba ni muhimu matatizo yao wakayapa kipaumbele ili yapatiwe ufumbuzi na katiba yao.
“Katiba ndiyo maisha yako ya kila siku, sema unataka iweje, msiwe na hofu maoni yote yatachukuliwa, kwa maandishi, vinasa sauti na video” alisema Dk. Mvungi. Chanzo>>>>>
|
|
|
KISWAHILI NI LUGHA YA AFRIKA |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 04:13 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Kiswahili ni kati ya lugha nne za taifa la DRC. Rais wa DRC, Joseph Kabila, anaongea Kiswahili sanifu. Kwa vile rais wa nchi anaongea Kiswahili sanifu, hii itakuwa chachu ya kukiboresha Kiswahili cha DRC, na kukieneza kwenye nchi zinayoizunguka DRC, kwa upande wa kaskazini. Kiswahili ni lugha ya taifa la Tanzania, Uganda na Kenya. Ingawa Kiswahili, si lugha ya taifa la Rwanda na Burundi, lakini vita vya maziwa makuu vimekifanya Kiswahili kuzungumzwa karibu na watu wote wa Rwanda na Burundi. Mipango iko mbioni kukifundisha Kiswahili kwenye shule za msingi za Rwanda na Burundi. Msukumo huu unatokana na nchi hizi mbili kuomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Kwenye miaka ya themanini, Kenya ilifanya jitihada nyingi kukiendeleza Kiswahili. Kiswahili lilifanywa somo la lazima kwenye shule za sekondari. Matokeo yake yameanza kujitokeza miongoni mwa kizazi kipya cha Kenya, kwa kuongea Kiswahili sanifu kuliko kile Kiswahili cha kizazi cha miaka ya nyuma. Pia ongezeko la vyuo vikuu nchini Kenya vimeongeza ufanisi wa Kiswahili, kila mwaka zaidi ya vijana 2000 wanaokifahamu vizuri Kiswahili wanahitimu vyuo vikuu. Hii itachangia kuwapata walimu wazuri wa kufundisha lugha ya Kiswahili na wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili. Ingawa magazeti ya Kiswahili hayajaongezeka kwa kasi kubwa, lakini uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili uko juu zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania. Kenya inatoa vitabu vingi vya Kiswahili na usambazaji wake ni mzuri kuliko wa Tanzania. Pia Wakenya wanasoma vitabu kuzidi watanzania. Bidii ya Kenya, katika kukikuza Kiswahili itachangia kwa kiasi kikubwa kuieneza lugha hii katika nchi zinazopakana nayo upande wa kaskazini, kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia. Tukizingatia kwamba wakimbizi wengi kutoka katika nchi hizi wamekuwa wakiishi nchini Kenya. Hizi ni dalili za kukipanua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima!
Tofauti na Tanzania, ambapo Kiswahili, karibu kinatumika kila sehemu katika jamii, Kenya Kiswahili kinatumika kama lugha ya siasa, dini na wasomi. Ingawa hii inaonyesha picha hasi ya kukiendeleza Kiswahili katika jamii nzima ya Wakenya, lakini pia kwa njia hii Kiswahili kinaweza kuongeza kasi ya kuongea lugha ya kisayansi na kiteknolojia na kujikita katika utandawazi kwa haraka zaidi ya Tanzania.
Kwenye miaka ya Sabini, Iddi Amin, alikitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa ya Uganda. Lakini waganda na hasa “Baganda” hawakukipokea Kiswahili kwa vile wanaipenda sana lugha yao ya “Luganda”. Sababu nyingine ni kwamba wanajeshi wa Iddi Amin, walitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi. Matendo maovu ya jeshi la Iddi Amin na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo, yalikipaka matope Kiswahili na kuwafanya watu wa Uganda, kukichukie. Pia waganda walimchukulia mtu anayeongea Kiswahili kuwa ni “Mswahili” mjanja mjanja na mtu asiyeaminika. Lakini pia waganda wengine walikihusisha Kiswahili na Uislamu, maana Waislamu walikitumia kama lugha ya dini kwa kukichanganya Kiswahili na Kiarabu, au kutafsiri Kiarabu katika kistahili. Kwa nchi kama Uganda, ambayo imepitia migongano na michafuko mikubwa ya kidini, kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kuamsha vita kati ya Wakristu na Waislamu.
Jeshi la Museveni, na Museveni mwenyewe walitumia Kiswahili. Hadi leo hii Kiswahili ni lugha ya jeshi la Uganda. Hii haikuwavutia waganda waliokuwa wamechoka na utawala wa kijeshi. Hivyo Kiswahili ilibaki ni lugha ya jeshi na biashara ya magendo kati ya Uganda, Tanzania na Kenya.
Kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo waganda wanaiona ina faida kubwa kuliko hasara, wameanza kuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili. Serikali ya Uganda imepitisha kwamba kuanzia mwaka kesho Kiswahili litakuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari. Huu utakuwa ni msaada mkubwa wa kukikuza Kiswahili na kukipatia picha ya kuwa lugha ya Afrika ya Mashariki na hatimaye Afrika nzima.
Kwenye makala iliyopita nilielezea jinsi Tanzania, ilivyofanikiwa kukisambaza Kiswahili nchi nzima na kuifanya lugha hii kuwa ya taifa ingawa haikutangazwa kisheria. Hivyo sirudii haya kwenye makala hii. Labda kutaja tu hapa kwamba Mwalimu Nyerere, kukubali Dar-es-Salaam, kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, kulisaidia kukisambaza Kiswahili katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika.
Mpango wa IPP Media Group wa kuanzisha gazeti la Kiswahili liitwalo Afrika ya Mashariki, utakuwa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili lugha pana inayoweza kukubalika Afrika nzima. Huu unaweza kuwa uwanja wa kuzua malumbano na majadiliano ya kuelekea kukikomaza Kiswahili kama enzi zile washairi wa Afrika ya Mashariki walivyokuwa wakijibizana na kulumbana katika uwanja wa ushairi. Bado kuna ushahidi wa kutosha jinsi mashairi yalivyosaidia kukikuza Kiswahili.
Vita vya ukombozi kusini mwa Afrika, vimekifanya Kiswahili isiwe lugha ngeni katika nchi za Zimbabwe, Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika ya kusini. Lakini pia wakimbizi wa Sudan, Somalia na Ethiopia, walioishi Kenya na Uganda wamesaidia kukisambaza Kiswahili hadi kwenye nchi zao. Wafanyabiashara wa Kisomali ambao hufanya kazi ya kusafirisha mizigo kwenye magari ya mizigo kwenye maeneo yote ya Afrika ya Mashariki, Kati na kusini wamekuwa mabalozi wa kuisambaza lugha ya Kiswahili.
Ingawa kuna lugha zingine za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi kama Kihausa. Kiswahili kinachomoza zaidi kwa sababu si lugha inayofungamana na kabila au taifa Fulani. Mfano ni tofauti na Kihausa. Ingawa Kihausa kinazungumzwa na watu wengi wa Afrika ya Magharibi, kinafungamana na kabila kubwa la Wahausa ambalo limekuwa kwenye migogoro na mapigano na makabila mengine kwa muda wa miaka mingi. Lengo lolote la kutaka kukifanya Kihausa kuwa lugha ya Afrika nzima, ni lazima litaamsha chuki miongoni mwa makabila makubwa ya Afrika magharibi ambayo nayo yangependa lugha zao zichukue nafasi ya kwanza.
Profesa Mulokozi, kwenye mada yake: “Kiswahili as a National and International Language” Anaelezea kisa alichosimuliwa na Kanyama Chiume, pale Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, mwaka 2002; kwamba mwaka 1959, wapigania uhuru wa Afrika walikuwa na mkutano ulioitishwa na Sekou Toure, katika mji wa Conakry, Guinea, ili kupanga harakati za kudai uhuru. Mkutano huu ulihudhuriwa na watu kutoka nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza na Kifaransa. Tatizo kubwa lililojitokeza katika mkutano huo ni lugha ya kutumia. Wajumbe walikaa wakitafakari zaidi ya masaa mawili juu ya lugha ya kutumia katika mkutano huo ili wote waweze kusikilizana na kuchangia hoja. Waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza hawakufahamu Kifaransa na wale waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kifaransa hakukifahamu Kiingereza. Huu ulikuwa mtindo wa wakoloni, wakutaka kufundisha lugha zaidi ya lugha yao. Baada ya muda mrefu wa kutafakari namna ya kuendesha kikao hicho kigumu, Kanyama Chiume, ndiye aliyeokoa jahazi. Alipendekeza: Kwa vile yeye alifahamu Kiswahili na Kiingereza, na Patrice Lumumba, alifahamu Kiswahili na Kifaransa, mkutano ungeweza kuendelea kwa wajumbe waliokuwa wakitumia Kiingereza, kuongea kwa Kiingereza na Kanyama Chiume, kutafsiri yote kwa Kiswahili ili Patrice Lumumba, aweze kutafsiri Kiswahili kwa Kifaransa. Vilevile na wale wa upande wa Kifaransa waliongea kwa Kifaransa na Patrice Lumumba, alitafsiri kila kitu kwa Kiswahili ili Kanyama Chiume, aweze kutafsiri kwa Kiingereza.
Kufuatana na maelezo ya Kanyama Chiume, mkutano huo uliendelea kwa ufanisi mkubwa ingawa ulikuwa wa kuchosha. Lakini wajumbe walielewana vizuri kwa msaada wa Lumumba na Kanyama Chiume waliokuwa wakikifahamu Kiswahili. Ndiyo kusema Kiswahili kiliwaunganisha Waafrika katika mkutano huo. Na kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Kiswahili ni tofauti na Kihausa au lugha nyingine maana si lugha ya Kabila Fulani au taifa Fulani. Mfano katika mkutano huu wa Conakry wa mwaka 1959, Patrice Lumumba alitokea Congo na Kanyama Chiume, alitokea Malawi! Kiswahili, haikuwa lugha ya kabila la Lumumba na wala haikuwa lugha ya kabila la Kanyama Chiume. Tunaweza kusema Kiswahili ilijitokeza kama lugha ya Waafrika katika mkutano huo. Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri, kama si uvivu na kutojali kwa watu wanaojiita chimbuko la Kiswahili, kama vile watanzania, leo hii Kiswahili, kingekuwa kimepiga hatua kubwa katika Bara zima la Afrika na duniani kote.
Mfano mwingine anautoa Profesa Mulokozi, ni ule wa mwanamapinduzi Che Guevara, wakati akiongoza harakati za mapambano ya vita vya msituni kuikomboa Congo, akiwa bega kwa bega na Laurent Kabila, alilazimika yeye na wapiganaji kutoka Cuba, kujifunza Kiswahili, hadi yeye Che Guevara, akabatizwa jina la Kiswahili la Tatu! Waligundua kwamba hii ndio lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha Waafrika waliokuwa wakipigana msituni na kwamba adui aliyeongea Kiingereza na Kifaransa asingeweza kufuatilia nyendo zao katika mawasiliano. Che Guevara, ni mwanamapinduzi anaheshimika duniani kote na historia yake imejaa mvuto wa pekee na kati ya mvuto huu ni lugha ya Kiswahili!
Lakini kitu kinachokifanya Kiswahili kionekane kuwa ni Lugha ya Afrika, wale wanaoisukuma mbele si watu wa Afrika Mashariki na wala si watu wanaotoka kwenye nchi ambazo zinaaminika kuwa ni nchi za Kiswahili kama Tanzania na Kenya. Tumeona mfano wa Kanyama Chiume na Lumumba. Mfano mwingine ni wa Chisano kutoka Msumbiji kwenye nchi inayoongea Kireno, na lugha nyingine za Kiafrika ambazo ni kubwa pia, kuwa rais wa kwanza wa Afrika, kuhutubia Umoja wa nchi za Afrika, kwa lugha ya Kiswahili.
Mkutano wa viongozi na wataalam wa maziwa makuu uliofanyika Aprili 2002 kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ulitoa mwito wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mataifa ya maziwa makuu.
Katika miaka ya sitini Mwandishi Maarufu wa Nigeria Wole Soyinka , alitoa mwito wa kukitangaza Kiswahili kuwa ni lugha ya Afrika nzima. Nigeria, kuna lugha kubwa za Kiafrika, lakini Wole Soyinka, aliguswa na lugha ya Kiswahili! Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.
Mwito huu ulirudiwa tena na mwandishi mwingine wa Ghana, Ayi Kwei Armah, mnamo mwaka wa 1985, yeye alikiona Kiswahili kama lugha ambayo inaweza kuingiza maneno mengi kutoka kwenye lugha nyingine za Kiafrika na kukifanya Kiswahili kuwa tajiri kwa msamiati. Ayi Kwei Armah, aliishi na kufanya kazi Tanzania. Alifundisha kwenye Chuo cha Walimu Chang’ombe. Kitabu chake “Te Beautiful Ones Are Not Yet Born” kimetafsiri katika Kiswahili: “Wema Hawajazaliwa”.
Kiswahili kilitumika kwenye mkutano mkuu wa UNESCO, Parish, Ufaransa. Hizi ni dalili kwamba Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha kubwa kutoka Afrika.
Mwanzoni mwa miaka ya themanini, UNESCO iliamua juzuu nane (8-volume) za historia ya Afrika zitafsiriwe kwenye lugha zaidi ya tatu za Kiafrika, Ukiondoa Kiarabu, lugha nyingine zilizopendekezwa ni Hausa,Fulfulde na Kiswahili. Juzuu za Kiswahili zimekamilika na kuchapishwa. Huu ni mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika historia ya Afrika. Kwa wale wanaofikiri kwamba Kiswahili si lugha ya kisomi, juzuu hizi ni changamoto kubwa kwao. Na huu ni ushahidi kwamba Kiswahili ni lugha ya Afrika.
Kwa vile utandawazi unatishia kuzimeza nchi za ulimwengu wa watu na hasa Afrika, kwa karibu kila kitu, ni vyema na Afrika itafute kitu cha kuuza kwenye utandawazi. Tukishindwa kuuza vitu vingine kama utamaduni, kazi za mikono na bongo zetu, basi tuuze lugha zetu na hasa zile zinazoelekea kukubalika Ulimwengu mzima kama vile Kiswahili.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
|
|
|
KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI: Wakati wa Kubadili fikra ni huu |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 03:57 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
Nimekutana na maoni ya mzalendo mmoja kuhusu matumizi ya lugha ya kiswahili nikaona nishirikiane nanyi kupata anachosema: maoni yake nayaweka hapa chini:
KILA NCHI INATOA ELIMU KWA KISWAHILI
Mzee Nimejifunza yafuatayo na siyo vibaya tukichangia:
(1) Kule Mbeya, Bukoba, Moshi, Iringa na sehemu nyingi zenye baridi watu wanakunywa zaidi CHAI ya kahawa. Wakati sehemu za joto joto kama Dar hawana chaguo maalumu, hata CHAI ya siturungi, milo, cocoa, zote zinanywewa bila mpangilio wowote.
(2) Yule NYERERE wa Msumbiji aliyekuwa akiitwa SamoraMasheli alikufa kwa ajali ya ndege na wala siyo gari.Na NYERERE wa Libya, Gadafi huenda akawa ndiyekiongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa muda mrefu. Somali wao hawana NYERERE bado, hii ni kwa ajili yamachafuko ya kivita.
(3) Kila nchi duniani hutumia lugha ya KISWAHILI kuunganisha jamii zao za makabila mbalimbali na kufundisha katika ngazi na nyanja zote za elimu. Mfano, Uganda, Malawi, Zambia, n.k., wao hutumia KISWAHILI cha Kiingereza. Gabon, Congo, Senegal, n.k.wao hutumia KISWAHILI cha Kifaransa; England, Wales,Marekani na Scotland hutumia KISWAHILI cha Kiingereza;Misri, Libya, Tunisia, n.k. wao ni KISWAHILI chaKiarabu; Uchina nasikia ni KISWAHILI kinachoitwa Mandarin; Arjentina, Kolombia, Chile, n.k. niKISWAHILI cha Kiispania, Urusi ni Kirusi, Ureno naBrazili na Angola ni Kireno, n.k. n.k.?
(4) Nchi yetu Tanzania ambayo KISWAHILI chake ni Kiswahili, ndiyo nchi pekee duniani ambayo imetumia KISWAHILI kuunganisha watu wake wa makabila mbalimbali halafu maajabu imekataa kutumia KISWAHILI hicho hicho katika kutoa na kupokea elimu mashuleni na vyuoni mwake !!!!!!!!!!!!. Hii inamaanisha kuwa kinachofundishwa mashuleni kwetu siyo elimu bali mahudhurio ya semina ndefu ndefu tulizozibatiza majina; Form IV, IV na madigirii.Nadhani vyeti vyake sahihi vingeitwa VYETI VYA MAHUDHURIO YA SEMINA YA FORM IV, n.k. na siyo vyeti vya ELIMU. Neno elimu ni pana na kubwa. Hivyo lisitumike pasipostahili. Vinginevyo ni sawa na kudai kuendesha kilimo cha minazi wakati shamba zima umepandikiza makuti mabichi!! Na misingi ya kukataa kutoa elimu kwa KISWAHILI ndiyo chanzo cha umaskikini wetu pamoja na kuwa matajiri wenye raslimali lukuki:watu takribani milioni 40, ardhi yote yenye rutuba,maji hadi kiama – yawe chumvi au baridi, hali ya hewa murua – hakuna vimbunga-matetemeko ya ardhi-baridi na joto zinazoua, madini kila aina nchi nzima, mbuga za wanyama duniani hakuna na lugha ya KISWAHILI iliyo pevu. Nchi zote duniani zinapotoa elimu kwa KISWAHILI chake,siyo wapumbavu, hivyo na sisi tuanze leo. Anayedai lugha haijakuwa bado, mwambie akupangia lugha ya kwanza hadi ya mwisho kama ataweza, hawezi, kwani hakuna kitu kama lugha changa. Anayesema tutafsiri kwanza vitabu kutoka lugha za kigeni – muulize mbona tunatumia maneno kama motokaa, oksijeni, pasipoti,kompyuta, redio na wenzetu nao wanatumia maneno yetu kama panga, shamba, safari, kimeharibika nini?. Anayedai hatutatambulika duniani – kwanza, waulize duniani kuna nchi ngapi zisizotumia hiyo lugha ya kigeni tunayoikumbatia – na wanatambulika zaidi yetu??pili wafahamishe kiswahili kinasambaa kama moto wa mbugani. Wasikilize Wakongo, Waburundi na Rwanda,Wakenya, Wamsumbiji, n.k. wanavyokiongea. Tatu waombe wasikilize redio Ujerumani, Peking, Sauti ya Amerika,BBC, n.k. Mwisho waelimishe kuwa wanapodai kuwa lugha haijakuwa, hatutatambulika, n.k huwa wanamaanisha,tena bila kujitambua wala aibu, kuwa wao ni wanyonge,dhaifu, wasiojiamini, wasioweza kujiendesha wenyewe,watumwa – haswa haswa huko vichwani mwao na wasiotakakuelimika.
Kwaheri,
Kiswahili chema,
|
|
|
KIMTANG’ATA MJINI TANGA |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 03:52 PM - Forum: Maendeleo ya Kiswahili
- No Replies
|
|
KIMTANG’ATA MJINI TANGA
Katrin Bromber
1. Utangulizi
Mnamo mwaka 1955 Wilfred Howed Whiteley eneo kusini mwa mji wa Tanga ili kuchungua lugha iliyozungumzwa pale. Matokeo ya utafiti wake aliyahifadhi katika kijitabu chake KI-MTANG’ATA. A dialect of the Mrima coast – Tanganyika kilichotolewa mwaka 1956. Lunga aliyoifafanua katika kitabu hicho ni lahaja moja ya Kiswahili ya kusini ambayo ilifanana na lahaja nyingine za eneo hilo – hasa Kivumba. Whitely aliipa lahaja hiyo jina la Kimtang’ata kufuatana na kijiji cha Mtang’ata. Maelezo yake yanaonesha kwamba Kimtang’ata kilikuwa
kikizungumzwa pwani kati ya Mwambani na Kigombe. Aidha aligundua kwamba matumizi ya lahaja hiyo yanaendelea kupungua. Hasa ni wanawake ndio watumiaji wa lahaja hiyo (Whiteley 1956: 3-5). Zaidi ya miaka thelathini Derek Nurse na Thomas Hinnebusch walifanya utafiti wa kiisimu katika eneo hilo mara nyingine. Waliwakuta wazee wachache tu waliozungumza lugha iliyofanana na Kimtang’ata kilichofafanuliwa na Whiteley (Nurse na Hinnebusch, 1993: 521). Wote watatu walieleza kupungua kwa hadhi ya lahaja hiyo kwa ongezeko la matumizi ya Kiunguja. Waliendelea kusema kwamba sifa za lahaja hiyo huonekana katika kiwango cha kileksika zaidi kuliko viwango vingine vya lugha. Kwa vyovyote, matokeo ya uchambuzi mwingine uliofanyika mwezi wa tatu mwaka 1996 mjini Tanga yanaonesha hali tofauti kidogo. Wahojiwa walitumia sifa za kiwango cha mofolojia zaidi kuliko zile za kileksika.
Maelezo ya makala haya yanahusu Kiswahili kitumiwacho na watu ambao husafiri mara nyingi kati ya vijiji vya Mwambani na Tongoni, ambapo lahaja ya Kimtang’ata ilitumiwa wakati wa uchambuzi wa Whiteley, na mji wa Tanga. Sehemu ya pili inahusu mazingira ya uchambuzi. Sehemu ya tatu mpaka ya tano zinatoa maelezo juu ya sifa za kilahaja katika viwango vya fonetiki, mofolojia na msamiati. Makala inamalizia kwa kufikiria uhai wa Kimtang’ata.
2. Mahojiano
Mahojiano yalifanyika mwezi wa tatu mwaka 1996. Marehemu Mwl. Pera Ridhiwani, aliyeheshimiwa sana na watu wa Tanga na watafiti wa lugha na fasihi ya Kiswahili, alikuwa ameshafanya miadi na wanawake kutoka Mwambani na Tongoni. Mwl. Pera alimfahamisha mhoji na wahojiwa. Alihudhuria kila mahojiano lakini hakuingilia mwenyewe hata mara moja. Wahojiwa walikuwa wanawake wane wenye umri uliozidi miaka sitini. Walieleza kwamba husafiri mara nyingi kati ya vijiji vyao na mji wa Tanga ili kuwatembelea jamaa zao. Kawaida yao ya kusafiri ilipunguza uwezekano wa kupata “lahaja safi”. Zaidi ya hayo mhoji alizungumza Kiunguja tu na kuonesha kwamba yeye mwenyewe hajui kutumia Kimtang’ata.
Walipoulizwa kusimulia vigano katika lahaja ya Kimtang’ata wanawake hao hawakufahamu. Kutumia kwa neno la Kimtang’ata ili kutaja yao ya mama kilikuwa kigeni kwao. Hali hii ingeonesha kwamba wanawake hao hawakujua kwamba kilugha chao ni tofauti na Kiswahili kizungumzwacho mjini au Kimtang’ata kimeshakufa kabisa.
Mahojiano na wanawake kutoka Mwambani yalifanyika ndani ya nyumba bila ya kuhudhuriwa na watu wengine. Kila mmoja alisimulia vigano viwili bila ya kuingiliwa na mtu yeyote. Mfumo wa matini hizo ni wa usimulizi tu. Mahojiano na wanawake waliotoka Tongani yalifanyika hadharani katika ua wa nyumba ya jamaa yao. Hivyo wote waliotaka kusikiliza walipata nafasi hiyo. Wasikilizaji wa kike na wa kiume umri mbalimbali waliingilia masimulizi kwa kutoa maoni yao ama juu ya habari zilizoelezwa au juu ya matumizi ya lugha. Zaidi ya hayo wanawake wawili hawa walifanana kihadhi na kitabia na kusahihishana waliposikia ulazima wa kufanya hivyo. Mahojiano yalitoa matini zenye sifa za masimulizi na za mazungumzo.
3. Fonetiki
Tofauti za kifonetiki zilitokea nadra tu. Kimsingi ilitokea ukaakaishaji wa fonimu /k/ mbele ya fonimu /i/ katika upatanifu wa ngeli ya saba. Matini zinaonesha sifa hii katika vimilikishi tu. Whitely (1956: 18) alitaja kipengele hicho kwa kiambishi awali cha nomino pia.
(1) Kigano kyangu kikeshilia hapo. (Kigano cgangu kikeshilia hapo)
4. Mofolojia
Sifa nyingi zaidi zilitokea katika kiwango cha mofolojia kuliko viwango vingine vya kiisimu. Katika kitabu chake Whiteley (1956: 22) alieleza juu ya mifululizo miwili ya viambishi awali kiima vya umoja. Mfululizo wa Kiunguja ni-, u-, a- hutumika sawasawa na mfululizo wa Kimtang’ata si-, ku-, ka- ambao pia hutokea katika lahaja ya jirani Kivumba. Matini za 1996 zinaonesha wazi matumizi ya mifululizo yote miwili. Kwa vyovyote, mfululizo si-, ku-, ka- unaambatana na mahali timilifu. Whitely alitoa mifano ambapo mfululizo huo ulitumiwa pamoja na njeo zote nyingine.
1. Baba sinarudi. Kunarudi, wee
(Baba nimesharudi. Je, umesharudi?)
2. Yule bwana kanakaa juu ya kiti.
(Yule bwana amekaa juu ya kiti.)
Kwa vile mazungumzo yalinaswa sauti mifano ya mpumuo wa /kh/ ili kuonesha ukanushaji wa nafsi ya pili na tatu ya umoja yaliyotokea. Nurse (1982: 173) na Nurse na Hinnebusch (1993: 365) wanaeleza mifano kama (4) na (5) kuwa ukanushaji wa kimsingi na unyambuaji wa /*nka/.
(4) Ebu khuolo wakezo? (Ebu huoni wakezo?)
(5) Lakini kila apatacho kikubwa khakimtoshi wala kidogo khakimtoshi. (Lakini kila apatacho kikubwa hakimtoshi wala kidogo hakimtoshi.)
Zaidi ya hayo mfano (4) unaonesha tangamano irabu katika silabi ya mwisho wa kitenzi. Kwa namna hii ukanushaji unasisitizwa mara mbili. Tangamano irabu ilitokea mara moja katika matini simulizi tu lakini mara nyingi katika matini mazungumzo yenye kitenzi –ona (simwono – simwoni) na –oga (sogo – siogi). Kinyume cha lahaja ya kaskazini ambazo zinatumia mpumuo kwa kuonesha tofauti za kisarufi, kazi hii imepunguzwa katika lahaja za kusini. Hivyo ukanushaji unaoneshwa kwa njia mbili katika matini: Kwanza kwa mpumuo na pili kwa tangamano irabu.
Katika vitenzi kiambishi awali kiima yu- badala ya Kiunguja a- kinachoashiria nafsi ya tatu umoja hutokea katika matini zote. Aidha kiwakilishi nafsi cha nafsi ya kwanza uwingi ni siswi badala ya sisi. Whitely (1956) na Nurse na
Hinnebusch (1993) hawakutaja maumbo hayo kuwa sehemu ya sarufi ya Kimtang’ata. Inawezekana kwamba yaliingia kutoka lahaja za kaskazini, hasa Kivumba. Zaidi ya hayo Meinhof (1905: 54) alieleza siswi kuwa kiwakilishi nafsi katika lugha ya Kidigo inayozungumzwa katika eneo la Tanga.
Kuhusu mofimu ya wakati, hali na namna (TAM) matini zilionesha sifa ya kilahaja moja tu, maana yake matumizi ya –na badala ya Kiunguja –me- kutaja hali timilifu. Nurse (1982: 176) na Nurse na Hinnebusch (1993: 420) wakieleza kipengele hicho kwa lahaja za jirani Kivumba, Kipemba na Chichifundi pia.
Matini simulizi zinataja vitenzi zenye kisaidizi –(e)vu na kitenzi chenye mofimu –ki- zinazolingana na Kiunguja –likuwa na –ki-. Kazi ya mifumo hiyo ni kuonesha sharti au tendo lifululizalo. Nurse (1982: 178) alitaja tungo hizo kuhusiana na Kivumba na Kitumbatu.
(6) Na baba kevu akanga
(Na baba alikuwa akianga)
Upanuaji wa kitenzi unaonekana katika kitenzi –chukua kitungwapo katika kauli ya kutendewa tu, maana yake –chukulibwa badala ya –chukuliwa. Kitenzi hicho ni dalili ya pekee ya uviringishaji katika tungo ya kauli ya kutendewa. Kihusishi kinachounganisha kitenzi na mtendaji ni kitenzi shirikishi ni badala ya kihusishi na.
Kuhusu kirai nomino matini zinaonesha tofauti mbili zikilinganishwa na Kiunguja. Kwanza,wahojiwa walitumia kimilikishi –akwe (taz. Mfano (7)) sawasawa na –ake. Sacleux (1909: 116) na Burt (1910) walikuwa wameshataja –akwe kuwa kimilikishi kwa lahaja za kaskazini. Whitely (1956: 18) hakueleza unasibu katika matumizi ya tungo hizo mbili. Alitaja –akwe tu. Kama isemavyo mwanzoni mwa makala haya Kiunguja kimeathiri haswa lahaja jirani.
(7) Huyo ng’ombe aliyekuwa na nafsi yakwe khanashiba.
(Huyo ng’ombe aliyekuwa na nafsi yake hakushiba)
Sawa na lahaja nyingine pamoja na Kiunguja majina ya wajamaa huunganishwa na vimilikishi kimsinyao. Sifa maalumu katika matini za Kimtang’ata ni usilimisho mbele ya irabu ya mwisho /a/ hugeuza /i/ mbele ya nusu-irabu /y/. Mifano kama (8) na (9) ilikuwa imeshaelezwa na Sacleux (1909: 118) kwa jumla lakini hakutaja matumizi ya usilimicho mbele kwa Kimtang’ata.
(8) Babiye ana mazizi ya ng’ombe mengi
(Baba yake ana mazizi ya ngombe mengi)
(9) Sasa amwuliza mamiye.
(Sasa anamwuliza mama yake)
Sifa ya pili katika kirai nomino ni mifano ya viwakilishi oneshi mbali vyenye mfumo h+upatanivu+le. Mieche (1979: 145) anaelez kazi ya mfumo huo kuwa ni kutilia mkazo. Mfano (10) unasaidia ufafanuzi huo.
(10) Baada ya kumwoa mkewe, siku hiile yule bwana asomesha somesha moja kwa moja mpaka usiku wa saa nne, saa tano.
(Baada ya kumwoa mkewe, siku ile yule bwana asomesha somesha moja kwa moja mpaka usiku wa saa nne, saa tano.) kazi ya kutilia mkazo itakuwa wazi katika hadithi yenyewe. Mke wa mwalimu huyo alikasirishwa na bidii ya mume wake kadiri alimtamkia kuishi na jamii.
5. Msamiati
Kwa ujumla msamiati wa matini zinazozungumziwa katika makala haya unafanana na ule wa Kiunguja. Sifa mbili zilizotokea ni vitenzi –ola na –uya. Nurse na Hinnebusch (1993) walifahamisha –ola (Kiunguja –ona) kuwa neno la Kimtang’ata na Kivumba. Whitely hakulitaja kabisa. Kitenzi -uya kinachofanana kikazi na -rudi liliingizwa na Whiteley katika orodha ya maneno ya Kimtang’ata (1956: 63). Sacleux (1939: 988) alieleza -uya kuwa linatokana na lugha ya kizamani iliyoacha maneno machache katika lahaja za kaskazini. Ili kusaidia maelezo yake alitoa ubeti mmoja wa Fumo Liyongo.
6. Hitimisho
Lengo la makala haya lilikuwa kutafiti sifa za lahaja ya Kimtang’ata katika matini simulizi na matini za mazungumzo. Matini hizo ni mifano ya lugha ya wanawake wanaotoka vijijini ambapo, kufuatana na Whiteley, Nurse na Hinnebusch, Kimtang’ata kilitumiwa. Lugha ya wahojiwa ilichambuliwa katika viwango vya fonetiki, mofolojia na msamiati. Msingi wa ulinganisho ulikuwa Kiunguja, maana yake Kiswahili Sanifu.
Uchunguzi umebainisha kwamba sifa za kilahaja zilitokea nadra tu na matini zinaeleweka kwa watu wanaojua Kiunguja. Tofauti zilitokea haswa katika kiwango cha mofolojia. Hivyo matokeo ya utafiti huo yanahitilafiana na maelezo ya Whiteley, Nurse na Hinnebusch ambao walisisitiza sifa za Kimtang’ata haswa katika kiwango
cha msamiati. Hitilafu hizo zinaweza kuelezwa na sababu kwamba msamiati ni sehemu ya lugha ambayo hubadilika upesi zaidi kuliko zote. Zaidi ya hayowanawake hao husafiri mara nyingi kati ya vijiji vyao na mji wa Tanga. Ongezeko la usafiri linaelekea hali ambapo sifa chache za mofolojia zitakuwa kumbukumbu za mwisho za Kimtang’ata.
Uchunguzi juu ya mahojiano ulionesha kwamba wahojiwa walisahihishana lugha zao. Hali hii ingedokeza kwamba hawana uhakika tena kuhusu lugha zao za vijijini. Zaidi ya hayo hawakujua kwamba lahaja yao huitwa Kimtang’ata. Hivyo ni lazima kuuliza kama lahaja hiyo ilikuwa hai kweli wakati uliopita au kama Kimtang’ata ni mfano mzuri wa kubuni kwa kitaaluma. Mtu lazima ajiulize kwa nini Charles Sacleux aliyeishi jirani na kuandika kitabu kizima juu ya lahaja za Kiswahili hakutaja Kimtang’ata hata mara moja? Mohling (1995: 44) alisawazisha Kimtang’ata na Kimrima. Lakini Kimrima ni Kiswahili kisemwacho kati ya ghuba ya Vanga na Rufiji, yaani Kimrima ni istilahi inayojumlisha matumizi ya Kiswahili katika eneo linalohitaji ufafanuzi wa kiisimu zaidi. Mradi wa pamoja wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na Chuo Kikuu cha Helsinki wa kuchambua matumizi ya Kiswahili kusini mwa Dar es Salaam, Unguja, Pemba, Tumbatu na Mafia ni mwelekeo mzuri wa kudhihirisha hali ya Kiswahili katika eneo hilo (Hurskainen 1998).
Kwa kumaliza inapaswa kusisitiza tena kwamba matini zilizokuwa msingi wa utafiti huu ni mifano ya lugha ya mjini. Wahojiwa na jamaa zao walisema kwamba vijijini kusini mwa Tanga watu wanatumia lugha tofauti kabisa. Lakini hawakuwa na uhakika kama lugha hiyo ni Kiswahili au lugha nyingine ya Kibantu. Hivyo, uchambuzi katika eneo hilo ungeweza kutoa matokeo tofauti.
Marejeleo
Kioo cha Lugha 2, 1996/97:15-21
|
|
|
ULAHAJIA NI NINI? DHANA YA ULAHAJIA INAFAA VIPI KATIKA KUELEZEA UTENDAJI? |
Posted by: MwlMaeda - 09-08-2021, 02:59 PM - Forum: Maswali na majibu
- No Replies
|
|
Swali hili limegawanyika katika sehemu ‘a’ na sehemu ‘b’. Na katika kulijibu swali hili tukianza na kipengele ‘a’ tutajadili dhana ya ulahaji kutokana na wataalamu mbalimbali huku tukitoa fasili yetu kwa ujumla. Pia katika kipengele ‘b’ tutajadili kuhusu dhana ya utendi kwa mujibu wa wataalamu, pia tutajadili maana mazungumzo huku tukitoa fasili yetu. Na katika kujadili kiini chetu cha swali tutajadili dhana ya ulahajia jinsi inavyotumika katika kuelezea utendaji wa lugha na mwishoni tutatoa hitimisho la kazi yetu.
Dhana ya ulahajia imefasiliwa na wataalamu mbalimbali ambao wameifafanua dhana hii kama ifuatavyo:-
Crystal, D (2000) anafasili ulahajia kuwa ni taaluma inayohusu mfumo wa lahaja za kimkoa.
Wikipedia wanasema kuwa, ulahajia ni tawi la isimu linalojihusisha na taaluma ya lahaja.
Kwa hiyo dhana ya ulahajia hufafanuliwa kuwa ni taaluma inayojihusisha na uchunguzi wa lahaja za kimkoa.
Taaluma hii huchunguza utofauti wa lahaja kati ya mkoa mmoja na mkoa mwingine. Zamani taaluma hii ilijikita zaidi katika kufanya uchunguzi kwa wazee walioishi sehemu moja bila kuhama tangia kuzaliwa kwao, lakini kwa sasa taaluma hii uchunguzi wake umejikita zaidi katika maeneo ya mjini kutokana na kuchanganyika kwa makundi ya watu tofauti tofauti kutoka mikoa tofautitofauti.
Dhana ya utendi imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali ambao wamefasili dhana hii kama ifuatavyo:-
Wikipedia wanafasili utendi kuwa ni uzungumzaji wa lugha katika muktadha halisi, nini hasa mzungumzaji husema kwa kuzingatia makosa ya kisarufi.
Kwa hiyo utendi huweza kufasiliwa kuwa ni utumiaji wa lugha katika mazingira halisi. Lugha inayotumika lazima iendane na mazingira yaliyopo.
Vile vile mazungumzo yamefasiliwa na Oxford (2004) kuwa ni jambo linalojadiliwa na watu au kikundi cha watu kwa lengo fulani. Kwa mfano maongezi.
Halliday (1990) anasema mazungumzo huweza kuwa na makosa mbalimbali katika mpangilio wa sentensi au katika mtindo wa matamshi. Vile vile Halliday anasema lugha ya mazungumzo inasifa zake bainifu ambazo ni tofauti na zile sifa za lugha ya maandishi.
Kwa hiyo tunaweza kufasili mazungumzo kuwa ni jambo fulani linalojadiliwa na watu wawili au kundi la watu kwa lengo fulani.
Baada ya kujadili dhana hizo, sasa tunaweza kujadili ni kwa jinsi gani dhana ya ulahajia inavyoweza kuelezea utendaji wa lugha hususani katika lugha ya mazungumzo kwa kuzingatia lugha ya Kiswahili.
Utofauti wa matamshi. Ulahajia huchunguza matamshi ya wazungumzaji wa lugha kutoka mikoa tofauti tofauti. Kwa mfano wazungumzaji kutoka mikoa ya kanda ya ziwa. Mfano wahaya kutoka mkoa wa Kagera katika matamshi yao hawana kitamkwa ng’ kwa hiyo wanapotamka maneno kama vile ng’ombe wao hutamka ngombe, neno ng’ang’ania hutamka ngangania, neno ung’amuzi wao hulitamka kama ungamuzi. Vile vile watu kutoka mkoa wa Mara ambao ni wakurya hutumia kitamkwa r badala ya l kwa mfano neno kula wao hulitamka kura, neno kulala hulitamka kurara, kulalamika wao hulitamka kuraramika. Pia wazungumzaji kutoka mikoa ya kusini mfano kutoka mkoa wa mtwara na lindi ambao ni Wamakonde wao hutumia kitamkwa n badala ya m kwa mfano mtoto hutamka kama ntoto, msichana hutamka kama nsichana, mchana hutamka nchana. Vile vile wazungumzaji kutoka mkoa wa mbeya ambao ni wanyakyusa wao hutamka f badala ya v kwa mfano neno viatu vyangu hutamka kama fiatu fyangu, uvivu hutamka ufifu, viazi hutamka fiasi. Wazungumzaji wa kutoka mikoa ya kaskazini mfano wapare kutoka mkoa wa moshi hutumia kitakmwa th badala ya s kwa mfano badala ya kusema sisi sote ni wasichana wao hutamka thithi thote ni wathichana. Kwa hiyo tofauti hizo za kimatamshi zinatokana na athari za lahaja za mikoa waliyotoka.
Msamiati. Dhana ya ulahajia huweza kutumika katika kuchunguza msamiti mbalimbali wa wazungumzaji wa lugha moja kutoka mikoa tofauti tofauti. Kwa mfano watu kutoka Zanzibar wao hutumia msamiati tofauti na wazungumzaji wa mikoa ya bara, kwa mfano husema neno tungule kwa kumaanisha nyanya, neno malikiti humaanisha sokoni, mferejini humaanisha bombani, vile vile kabila la Wamakonde kutoka mkoa Mtwara hutumia neno kumaanika kwa kumaanisha kudharirika, kwa hiyo wazungumzaji hawa hutumia msamiati wa lahaja zao kutokana na athari za lahaja hizo.
Muundo wa sentensi, vile vile dhana ya ulahajia huweza kuelezea utendaji wa lugha kwa kuchunguza muundo wa sentensi wa wazungumzaji wa lugha moja, kwa kuchunguza muundo wa sentensi utaweza kubaini kuwa wazungumzaji wa lugha hii wanatokea mkoa gani, kwa mfano wazungumzaji wa mkoa wa Tabora hutumia wingi mahala pa nomino ya umoja wakiashiria heshima. Kwa mfano husema baba wanakuja badala ya kusema baba anakuja, mmefika salama? Badala ya kusema umefika salama?. Kwa hiyo mtu wa heshima kwao hutumia nomino ya wingi na hii yote ni kutokana na kuathiriwa na lahaja za mikoa watokayo.
Kiimbo. Ulahajia huweza kuchunguza kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya wazungumzaji wa lugha, kwa mfano kabila la Waluguru kutoka mkoa wa Morogoro wao huzungumza kwa kupandisha na kushusha mawimbi ya sauti. Kwa mfano, “baba amekuja”. kwa hiyo athari hizo zimetokana na lahaja ya mkoa waliotokea.
Mkazo, mkazo ni kule kutumia nguvu zaidi katika kutamka maneno au sentensi. Yaani ni hali ya neno au silabi katika neno kusikika kuwa na nguvu zaidi kuliko silabi au maneno mengine. Kwa hiyo ulahajia huweza kuelezea utofauti wa mkazo uliopo katika baadhi ya wazungumzaji wa lugha moja. Kwa mfano kabila la Wasukuma kutoka mkoa wa Mwanza huweka msisitizo katika mazungumzo, kwa mfano “baba anakujaa”, pia wanaongeza vitamkwa ambavyo si vya msingi katika maneno yanayojitosheleaza. kwa mfano neno amekuja wao huongezea kitamkwa ga, = amekujaga, neno ameenda + ga, = ameendaga, hakuna + ga.=hakunaga.
Kwa hiyo mtu huweza kuwa na umilisi wa lugha fulani lakini asiwe mtendaji hususani katika lugha ya mazungumzo na hii ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuathiriwa na lahaja ya mkoa atokao, athari hizi hujidhihirisha zaidi katika lugha ya mazungumzo kama tulivyojadili hapo juu, lakini katika lugha ya maandishi athari hizi huweza kujidhihirisha kwa kiasi kidogo sana au zisitokee kabisa.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa dhana ya ulahajia huweza kuelezea utendaji wa lugha husasani katika lugha ya mazungumzo kwani ndio rahisi sana kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha moja watokao sehemu tofauti tofauti, ambayo ni tofauti sana na kuelezea utendaji wa lugha katika lugha ya maandishi kwani ni vigumu sana kubainisha makosa ya kisarufi kama vile matamshi, kiimbo, mkazo, msamiati na hata muundo wa sentensi. Mara nyingi maandishi huandikwa kwa ufasaha zaidi ukilinganisha na mazungumzo na ndio maana ulahajia huweza kuelezea utendaji wa lugha hususani katika lugha ya mazungumzo.
MAREJELEO
Crystal, D. (2002). The Cambridge of Encyclopedia of Language: Second edition. London.Cambridge University Press.
Halliday, M.A.K. (1990). Spoken and Written Language. London. Oxford University Press.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu, (2004). Nairobi. Oxford University Press.
Chanzo>>>>>[url=http://tunuzakiswahili.blogspot.com/p/blog-page_6.html][/url]
|
|
|
|