Massamba, D.P.B na wenzake (2001:26-28) Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu. TUKI.Dar es Salaam
Katika sehemu ya 1.1 tulisema kwamba lugha ya Kiswahili ndiyo lugha muhimu sana katika eneo lote la Afrika Mashariki na kati. Tulisema vile vile kwamba lugha hii ina nafasi ya pekee katika nchi ya Tanzania na Kenya. Hii ni kwa sababu lugha hii ni lugha ya taifa na pia lugha rasmi katika nchi zote mbili. Wananchi wengi wa Afrika mashariki wanajua na huitumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao. Kwa hiyo ina maana kwamba lugha hii ina nafasi ya pekee katika mambo muhimu kama utamaduni, siasa na uchumi. Pengine yafaa kufafanua kidogo jambo hili.
Wataalamu wengi wa masuala ya utamaduni hukubaliana kwamba kwa kiasi kikubwa lugha ni kielelezo cha utamaduni. Ukweli huo hujidhihirisha katika lugha yenyewe. Ukiichunguza kwa makini lugha yoyote iwayo utagundua kwamba ina vipengekele mbalimbali vya utamaduni vya wasemaji wa lugha hiyo ambavyo vinajitokeza ndani mwake. Mfano mdogo tu ni kwamba wakati kwa Mswahili ndugu wa kiume wa baba ni baba na ndugu wa kike wa mama ni mama kwa mzungu sivyo, kwani Mzungu ana baba (father) mmoja tu na mama (mother) mmoja tu; Mzungu ana dhanna za half-brother (nusu-kaka?) na half-sister (nusu-dada?), ambazo hazimo katika lugha ya Kiswahili. Mswahili akiamua kutumia lugha ya Kiingereza atashindwa kuvieleza vipengele hivi vya utamaduni; hivyo itakuwa njia moja wapo ya kumomonyoa utamaduni. Kwa hiyo basi, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Afrika Mashariki yataendelea kuudumisha utamaduni wetu.
Nafasi ya lugha ya Kiswahili katika masuala ya siasa ni jambo ambalo halihitaji kupigiwa ngoma. Tumekwishaona jinsi lugha hii inavyotumika kama chombo muhimu sana cha kuunganisha watu na kuleta umoja, Kwa kuwa lugha hii ndiyo itumiwayo na watu wengi katika Afrika mashariki ndiyo lugha peke yake inayoweza kuleta uelewano katika masuala ya kisiasa kwa wananchi wa eneo hili, siyo lugha nyingine. Aidha, lugha ya Kiswahili ndiyo lugha muhimu iwaunganishayo wananchi wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Kwani katika maeneo haya kuna lugha mbalimbali zinazotumika, lugha peke yake inayotumika kote ni Kiswahili.
Lugha ya Kiswahili ni lugha muhimu sana katika Afrika Mashariki kwa upande wa masuala ya uchumi. Lugha ambayo inafahamika kwa watu wengi ndiyo lugha ifaayo kutumiwa katika mambo na mawasiliano ya kibiashara. Tangu zamani wananchi wa Afrika Mashariki wamekuwa wakiitumia lugha hii katika shughuli zao za kibiashara. Kiswahili kinamwezesha Mkenya kwenda Tanzania, hata vijijini akafanya biashara bila wasiwasi wowote; halikadhalika Mtanzania anaweza kwenda Kenya vijijini akaendesha shughuli zake za kibiashara bila tabu ya kutafuta mkalimani. Na kwa hakika hii si kwa Tanzania na Kenya tu; hali ni hiyo hiyo kwa upande wa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kwa kiasi fulani hata katika Rwanda na Burundi pia.
Kwa ujumla lugha ya Kiswahili ni lugha muhimu katika harakati zozote za wananchi wa sehemu za Afrika Mashariki na Kati. Kwa misingi hiyo, lugha hii haina budi kukuzwa na kuendelezwa zaidi ili matumizi yake yazidi kuwa mapana na toshelevu kwa kiwango kinachotakiwa katika sehemu zote hizi.