09-08-2021, 04:13 PM
Kiswahili ni kati ya lugha nne za taifa la DRC. Rais wa DRC, Joseph Kabila, anaongea Kiswahili sanifu. Kwa vile rais wa nchi anaongea Kiswahili sanifu, hii itakuwa chachu ya kukiboresha Kiswahili cha DRC, na kukieneza kwenye nchi zinayoizunguka DRC, kwa upande wa kaskazini. Kiswahili ni lugha ya taifa la Tanzania, Uganda na Kenya. Ingawa Kiswahili, si lugha ya taifa la Rwanda na Burundi, lakini vita vya maziwa makuu vimekifanya Kiswahili kuzungumzwa karibu na watu wote wa Rwanda na Burundi. Mipango iko mbioni kukifundisha Kiswahili kwenye shule za msingi za Rwanda na Burundi. Msukumo huu unatokana na nchi hizi mbili kuomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Kwenye miaka ya themanini, Kenya ilifanya jitihada nyingi kukiendeleza Kiswahili. Kiswahili lilifanywa somo la lazima kwenye shule za sekondari. Matokeo yake yameanza kujitokeza miongoni mwa kizazi kipya cha Kenya, kwa kuongea Kiswahili sanifu kuliko kile Kiswahili cha kizazi cha miaka ya nyuma. Pia ongezeko la vyuo vikuu nchini Kenya vimeongeza ufanisi wa Kiswahili, kila mwaka zaidi ya vijana 2000 wanaokifahamu vizuri Kiswahili wanahitimu vyuo vikuu. Hii itachangia kuwapata walimu wazuri wa kufundisha lugha ya Kiswahili na wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili. Ingawa magazeti ya Kiswahili hayajaongezeka kwa kasi kubwa, lakini uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili uko juu zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania. Kenya inatoa vitabu vingi vya Kiswahili na usambazaji wake ni mzuri kuliko wa Tanzania. Pia Wakenya wanasoma vitabu kuzidi watanzania. Bidii ya Kenya, katika kukikuza Kiswahili itachangia kwa kiasi kikubwa kuieneza lugha hii katika nchi zinazopakana nayo upande wa kaskazini, kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia. Tukizingatia kwamba wakimbizi wengi kutoka katika nchi hizi wamekuwa wakiishi nchini Kenya. Hizi ni dalili za kukipanua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima!
Tofauti na Tanzania, ambapo Kiswahili, karibu kinatumika kila sehemu katika jamii, Kenya Kiswahili kinatumika kama lugha ya siasa, dini na wasomi. Ingawa hii inaonyesha picha hasi ya kukiendeleza Kiswahili katika jamii nzima ya Wakenya, lakini pia kwa njia hii Kiswahili kinaweza kuongeza kasi ya kuongea lugha ya kisayansi na kiteknolojia na kujikita katika utandawazi kwa haraka zaidi ya Tanzania.
Kwenye miaka ya Sabini, Iddi Amin, alikitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa ya Uganda. Lakini waganda na hasa “Baganda” hawakukipokea Kiswahili kwa vile wanaipenda sana lugha yao ya “Luganda”. Sababu nyingine ni kwamba wanajeshi wa Iddi Amin, walitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi. Matendo maovu ya jeshi la Iddi Amin na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo, yalikipaka matope Kiswahili na kuwafanya watu wa Uganda, kukichukie. Pia waganda walimchukulia mtu anayeongea Kiswahili kuwa ni “Mswahili” mjanja mjanja na mtu asiyeaminika. Lakini pia waganda wengine walikihusisha Kiswahili na Uislamu, maana Waislamu walikitumia kama lugha ya dini kwa kukichanganya Kiswahili na Kiarabu, au kutafsiri Kiarabu katika kistahili. Kwa nchi kama Uganda, ambayo imepitia migongano na michafuko mikubwa ya kidini, kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kuamsha vita kati ya Wakristu na Waislamu.
Jeshi la Museveni, na Museveni mwenyewe walitumia Kiswahili. Hadi leo hii Kiswahili ni lugha ya jeshi la Uganda. Hii haikuwavutia waganda waliokuwa wamechoka na utawala wa kijeshi. Hivyo Kiswahili ilibaki ni lugha ya jeshi na biashara ya magendo kati ya Uganda, Tanzania na Kenya.
Kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo waganda wanaiona ina faida kubwa kuliko hasara, wameanza kuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili. Serikali ya Uganda imepitisha kwamba kuanzia mwaka kesho Kiswahili litakuwa somo la lazima katika shule za msingi na sekondari. Huu utakuwa ni msaada mkubwa wa kukikuza Kiswahili na kukipatia picha ya kuwa lugha ya Afrika ya Mashariki na hatimaye Afrika nzima.
Kwenye makala iliyopita nilielezea jinsi Tanzania, ilivyofanikiwa kukisambaza Kiswahili nchi nzima na kuifanya lugha hii kuwa ya taifa ingawa haikutangazwa kisheria. Hivyo sirudii haya kwenye makala hii. Labda kutaja tu hapa kwamba Mwalimu Nyerere, kukubali Dar-es-Salaam, kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi za kusini mwa Afrika, kulisaidia kukisambaza Kiswahili katika nchi hizo za Kusini mwa Afrika.
Mpango wa IPP Media Group wa kuanzisha gazeti la Kiswahili liitwalo Afrika ya Mashariki, utakuwa mchango mkubwa katika kukifanya Kiswahili lugha pana inayoweza kukubalika Afrika nzima. Huu unaweza kuwa uwanja wa kuzua malumbano na majadiliano ya kuelekea kukikomaza Kiswahili kama enzi zile washairi wa Afrika ya Mashariki walivyokuwa wakijibizana na kulumbana katika uwanja wa ushairi. Bado kuna ushahidi wa kutosha jinsi mashairi yalivyosaidia kukikuza Kiswahili.
Vita vya ukombozi kusini mwa Afrika, vimekifanya Kiswahili isiwe lugha ngeni katika nchi za Zimbabwe, Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika ya kusini. Lakini pia wakimbizi wa Sudan, Somalia na Ethiopia, walioishi Kenya na Uganda wamesaidia kukisambaza Kiswahili hadi kwenye nchi zao. Wafanyabiashara wa Kisomali ambao hufanya kazi ya kusafirisha mizigo kwenye magari ya mizigo kwenye maeneo yote ya Afrika ya Mashariki, Kati na kusini wamekuwa mabalozi wa kuisambaza lugha ya Kiswahili.
Ingawa kuna lugha zingine za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi kama Kihausa. Kiswahili kinachomoza zaidi kwa sababu si lugha inayofungamana na kabila au taifa Fulani. Mfano ni tofauti na Kihausa. Ingawa Kihausa kinazungumzwa na watu wengi wa Afrika ya Magharibi, kinafungamana na kabila kubwa la Wahausa ambalo limekuwa kwenye migogoro na mapigano na makabila mengine kwa muda wa miaka mingi. Lengo lolote la kutaka kukifanya Kihausa kuwa lugha ya Afrika nzima, ni lazima litaamsha chuki miongoni mwa makabila makubwa ya Afrika magharibi ambayo nayo yangependa lugha zao zichukue nafasi ya kwanza.
Profesa Mulokozi, kwenye mada yake: “Kiswahili as a National and International Language” Anaelezea kisa alichosimuliwa na Kanyama Chiume, pale Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, mwaka 2002; kwamba mwaka 1959, wapigania uhuru wa Afrika walikuwa na mkutano ulioitishwa na Sekou Toure, katika mji wa Conakry, Guinea, ili kupanga harakati za kudai uhuru. Mkutano huu ulihudhuriwa na watu kutoka nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza na Kifaransa. Tatizo kubwa lililojitokeza katika mkutano huo ni lugha ya kutumia. Wajumbe walikaa wakitafakari zaidi ya masaa mawili juu ya lugha ya kutumia katika mkutano huo ili wote waweze kusikilizana na kuchangia hoja. Waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza hawakufahamu Kifaransa na wale waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kifaransa hakukifahamu Kiingereza. Huu ulikuwa mtindo wa wakoloni, wakutaka kufundisha lugha zaidi ya lugha yao. Baada ya muda mrefu wa kutafakari namna ya kuendesha kikao hicho kigumu, Kanyama Chiume, ndiye aliyeokoa jahazi. Alipendekeza: Kwa vile yeye alifahamu Kiswahili na Kiingereza, na Patrice Lumumba, alifahamu Kiswahili na Kifaransa, mkutano ungeweza kuendelea kwa wajumbe waliokuwa wakitumia Kiingereza, kuongea kwa Kiingereza na Kanyama Chiume, kutafsiri yote kwa Kiswahili ili Patrice Lumumba, aweze kutafsiri Kiswahili kwa Kifaransa. Vilevile na wale wa upande wa Kifaransa waliongea kwa Kifaransa na Patrice Lumumba, alitafsiri kila kitu kwa Kiswahili ili Kanyama Chiume, aweze kutafsiri kwa Kiingereza.
Kufuatana na maelezo ya Kanyama Chiume, mkutano huo uliendelea kwa ufanisi mkubwa ingawa ulikuwa wa kuchosha. Lakini wajumbe walielewana vizuri kwa msaada wa Lumumba na Kanyama Chiume waliokuwa wakikifahamu Kiswahili. Ndiyo kusema Kiswahili kiliwaunganisha Waafrika katika mkutano huo. Na kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Kiswahili ni tofauti na Kihausa au lugha nyingine maana si lugha ya Kabila Fulani au taifa Fulani. Mfano katika mkutano huu wa Conakry wa mwaka 1959, Patrice Lumumba alitokea Congo na Kanyama Chiume, alitokea Malawi! Kiswahili, haikuwa lugha ya kabila la Lumumba na wala haikuwa lugha ya kabila la Kanyama Chiume. Tunaweza kusema Kiswahili ilijitokeza kama lugha ya Waafrika katika mkutano huo. Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri, kama si uvivu na kutojali kwa watu wanaojiita chimbuko la Kiswahili, kama vile watanzania, leo hii Kiswahili, kingekuwa kimepiga hatua kubwa katika Bara zima la Afrika na duniani kote.
Mfano mwingine anautoa Profesa Mulokozi, ni ule wa mwanamapinduzi Che Guevara, wakati akiongoza harakati za mapambano ya vita vya msituni kuikomboa Congo, akiwa bega kwa bega na Laurent Kabila, alilazimika yeye na wapiganaji kutoka Cuba, kujifunza Kiswahili, hadi yeye Che Guevara, akabatizwa jina la Kiswahili la Tatu! Waligundua kwamba hii ndio lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha Waafrika waliokuwa wakipigana msituni na kwamba adui aliyeongea Kiingereza na Kifaransa asingeweza kufuatilia nyendo zao katika mawasiliano. Che Guevara, ni mwanamapinduzi anaheshimika duniani kote na historia yake imejaa mvuto wa pekee na kati ya mvuto huu ni lugha ya Kiswahili!
Lakini kitu kinachokifanya Kiswahili kionekane kuwa ni Lugha ya Afrika, wale wanaoisukuma mbele si watu wa Afrika Mashariki na wala si watu wanaotoka kwenye nchi ambazo zinaaminika kuwa ni nchi za Kiswahili kama Tanzania na Kenya. Tumeona mfano wa Kanyama Chiume na Lumumba. Mfano mwingine ni wa Chisano kutoka Msumbiji kwenye nchi inayoongea Kireno, na lugha nyingine za Kiafrika ambazo ni kubwa pia, kuwa rais wa kwanza wa Afrika, kuhutubia Umoja wa nchi za Afrika, kwa lugha ya Kiswahili.
Mkutano wa viongozi na wataalam wa maziwa makuu uliofanyika Aprili 2002 kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ulitoa mwito wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mataifa ya maziwa makuu.
Katika miaka ya sitini Mwandishi Maarufu wa Nigeria Wole Soyinka , alitoa mwito wa kukitangaza Kiswahili kuwa ni lugha ya Afrika nzima. Nigeria, kuna lugha kubwa za Kiafrika, lakini Wole Soyinka, aliguswa na lugha ya Kiswahili! Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.
Mwito huu ulirudiwa tena na mwandishi mwingine wa Ghana, Ayi Kwei Armah, mnamo mwaka wa 1985, yeye alikiona Kiswahili kama lugha ambayo inaweza kuingiza maneno mengi kutoka kwenye lugha nyingine za Kiafrika na kukifanya Kiswahili kuwa tajiri kwa msamiati. Ayi Kwei Armah, aliishi na kufanya kazi Tanzania. Alifundisha kwenye Chuo cha Walimu Chang’ombe. Kitabu chake “Te Beautiful Ones Are Not Yet Born” kimetafsiri katika Kiswahili: “Wema Hawajazaliwa”.
Kiswahili kilitumika kwenye mkutano mkuu wa UNESCO, Parish, Ufaransa. Hizi ni dalili kwamba Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha kubwa kutoka Afrika.
Mwanzoni mwa miaka ya themanini, UNESCO iliamua juzuu nane (8-volume) za historia ya Afrika zitafsiriwe kwenye lugha zaidi ya tatu za Kiafrika, Ukiondoa Kiarabu, lugha nyingine zilizopendekezwa ni Hausa,Fulfulde na Kiswahili. Juzuu za Kiswahili zimekamilika na kuchapishwa. Huu ni mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika historia ya Afrika. Kwa wale wanaofikiri kwamba Kiswahili si lugha ya kisomi, juzuu hizi ni changamoto kubwa kwao. Na huu ni ushahidi kwamba Kiswahili ni lugha ya Afrika.
Kwa vile utandawazi unatishia kuzimeza nchi za ulimwengu wa watu na hasa Afrika, kwa karibu kila kitu, ni vyema na Afrika itafute kitu cha kuuza kwenye utandawazi. Tukishindwa kuuza vitu vingine kama utamaduni, kazi za mikono na bongo zetu, basi tuuze lugha zetu na hasa zile zinazoelekea kukubalika Ulimwengu mzima kama vile Kiswahili.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
Mwl Maeda