LAZIMA NIMUACHE
Ni aheri Gari kweche, jukumu tabeba fundi
Mke tabia ni chehe, nyumba kaingia bundi,
Ni lazima nimuache, kukerwa mimi sipendi,
Kujitowa kwenye kundi, mahaba yake machache.
Si Nguo nimfikiche, tajitaidi siundi,
Maudhi ni kechekeche, nikimwacha sikondi,
Ni busara nimkache, mimi siziwezi ndondi,
Kujitowa kwenye kundi, mahaba yake machache.
Wazi sitaki nifiche, hiki si kile kipindi,
Baadhi leo vicheche, wataka pesa ndindindi,
Kama mfuko ni peche, mtaishi nyondi nyondi,
Kujitowa kwenye kundi, mahaba yake machache
Hassan Msati Dar es Salaam.
*USIKURUPUKE*
Hasan Kaka Hasani, maneno yangu pulika,
Kuacha sio utani, si Daladala kushuka,
Uuze moyo uneni, ushauri ukitaka,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Alinidhani bandia, mwenzio alitamka,
Kaacha akarudia, kulala peke kachoka,
Watu wakamuambia, kiko wapi Bwana Kaka,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Kuacha kwataka kunga, si mchezo wa vidaka,
Usije kawa mkunga, unga ukapukutika,
Utashinda kwa waganga, na fedha zitakutoka,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Vinono vina gharama, si Jahazi kwenda tweka,
Kuvitunza ni nakama, si mchezo hekaheka,
Faida utayochuma, ni moyo kufurahika,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Eti mahaba machache, sababu umetamka,
Mbona yale mambo fiche, ugani unayaweka,
Sema kweli usifiche, kipi hasa kimetuka,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Tamati nitamatile, beti zimetamatika,
Ukisikie kelele, sauti nje zatoka,
Kama si hili ni lile, furaha au mashaka,
*Siache huku wataka, alinidhani bandia.*
Kanga au leso ni vazi ambalo asili yake imefungamana na utamaduni wa waswahili wanaoishi katika pwani ya Afrika Mashariki. Katika makala ya “asili na tamaduni” tunaangazia asili ya kanga na matumizi yake katika jamii ya waswahili.
Makala haya yamegawika sehemu
mbili. Sehemu ya kwanza inachungua mawazo ya Shaaban Robert aliyoyatoa katika
vitabu vyake viwili: Adili na Nduguze
na Wasifu wa Siti Binti Saad. Sehemu ya
pili yatumia mawazo hayo kupimia vitendo na maisha ya Shaaban kama
alivyotueleza yeye mwenyewe katika vitabu viwili vingine vilivyokusanywa
pamoja: Maisha Yangu na Baada ya Miaka
Hamsini.
Nionavyo mimi, Shaaban Robert
amechukua nafasi ya kuandika vitabu vyake hivi viwili vya mwanzo ili aweze
kutoa mawazo na maoni yake kuhusu mambo mabaya na mazuri, yapi ya kufuata na
yapi ya kuepuka katika dunia yenye maisha mbalimbali. Baada ya kuvisoma vitabu
hivyo kwa makini, nimekatikiwa kuwa Shaaban alikuwa na mawazo yasiyo tafauti na
siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Amefikiria kuishi kwa ujamaa katika kitabu
chake cha Adili na Nduguze na katika Wasifu wa Siti Binti Saad ametoa mawazo
yake kuhusu maisha ya kujitegemea; na bila shaka ana lengo halisi katika kutoa
mawazo hayo. Pengine alipenda kueleza na kufafanua, au kupanua zaidi, yasemwayo
katika Injili Takatifu, yaani ‘umpende jirani yako kama nafsi yako’, na mapenzi
hayo ndiyo msingi wa wema, matendo safi, na juhudi ya kazi ziletazo faida kwa
watu wote.
Kwa kuwa vitabu viwili hivi
vimetumiwa kama vyombo vya kuelezea aina mbili za mawazo na maoni ya mtungaji,
naona ni vema nisivichanganye katika uchambuzi huu bali nivichukue kimoja
kimoja. Ebu nianze na kile kilichotangulia kutoka. Kimoja kilitoka mara ya
kwanza katika jarida la 1958 (Nambari 28/1) la Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki, na kingine kilitoka mara ya kwanza kama kitabu kamili mnamo 1952,
nacho ni Adili na Ndiguze ambacho
ndicho tutakachoanzia.
Nimesema kwamba mawazo ya Shaaban
Robert yana lengo au kiini fulani. Katika Adili
na Nduguze lengo lake ni upendo, yaani watu wapendane na kuishi kiujamaa-na
upendo huo ndio alioufungulia kitabu chenyewe alipoandika mwanzoni:
‘Kwa marafiki zangu
Wazawa wa Afrika
Pamoja na Wazungu
Wapendao afrika’.
Shaaban Robert amekianza kitabu
chake kwa maelezo juu ya Mfalme Rai. Mawazo yenyewe, nionavyo mimi, ni sawa nay
ale yasemwayo na Azimio la Arusha kwamba, ili kuleta mafanikio na maendeleo ya
nchi, vihitajiwavyo ni ardhi, watu, uongozi bora na siasa safi.
Kiini cha kumuanzia Rain i kutaka
kueleza kwamba, hata kama ardhi na watu wapo, jambo la kwanza linalotakiwa ni
uongozi bora wenye msingi ufananao na tabia ya Rai. Pengine ardhi na watu wa
Ughaibuni walifanikiwa na kuendelea kwa sababu ya uongozi mzuri wa Rai. Mawazo ya
Shaaban ni kuwa uongozi mzuri wa nchi ni kama ule wa Rai ambao kiini chake
kilikuwa upendo. Alikuwa na mapenzi na wanaadamu, nao wakampenda;alifuata
msingi wa kidini wa zamani ambapo Daudi aliwapenda wanyama na Sulemani akatiiwa
na majini.
Mawazo ya Shaaban juu ya kiongozi
bora wa nchi yoyote yameelezwa katika wasifu wa Rai, ukurasa wa pili. Hapo uongozi
bora unaonekana unahitajia uadilifu, wema, kufanya kazi ndogo na kubwa au kutoa
amri zifanywe, kusaidia na kushiriki katika maendeleo ya nchi, kutolazimisha
watu mambo bali kuwashawishi tu (kama uhitajivyo ujamaa wa kweli), kuvuta mioyo
ya watu ili kusiwe na wavivu, magoigoi wala waoga.
Kwa namna hii Shaaban Robert atoa
mawazo kwamba viumbe wote wangefurahia sifa ya kiongozi wa namna hiyo-tangu
malaika mbinguni hadi ndege angani, watu duniani, samaki majini, na hata majini
na mashetani popote pale wafikiriwapo wapo. Upendo na ujamaa wa kweli ni
kufanya urafiki na viumbe mbalimbali pamoja na kuwajali watu wote. Baada ya
upendo ni matendo. Na hapa ndipo Shaaban aliposema: ‘Tendo hukidhi haja
maridhawa kuliko neno.’ Yaani, tendo huleta haja upesi lakini neno huichelesha;
na neno tu si njia ya kuleta mapinduzi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Katika kuhukumu mwandishi
aonekane ana machache ya kueleza. Itolewapo hukumu inatakikana kiongozi awe
imara, asipendelee bali watu wote wawe sawa mbele ya sheria. Hiyo ndiyo
demokrasi halisi-demokrasia ya kiujamaa. Uongozi bora ni ule ufuatao haki ya
watu na wanyama pia, na ule ufanyao uchunguzi wa matukio yote-mazuri na
mabaya-kwa raia. Na, katika uchunguzi wa Rai kuhusu kasoro iliyotokea Janibu,
ndimo Shaaban Robert anamoeleza mawazo yake kuhusu tabaka kwa tabaka za maisha
ya kiujamaa nay ale yasiyo ya kiujamaa. Na juu ya huo uchunguzi Shaaban
anasema, ‘Mambo katika maisha yambo katika mwnedo huu siku zote. Hayajulikani mpaka
yamechunguzwa na kuthibitishwa kwanza.’ Kiongozi bora kama Rai huwa mtu arifu
wa mwendo huu!
Tunaambiwa vile vile kuwa si
kiongozi tu atakikanaye kuwa mtu wa kufaa bali watu wote walio na wajibu na
mamlaka chini yake, kama vile Rai alivyokuwa na Maarifa (Waziri Mkuu) na
Ikibali (Mshauri). Na kazi lazima ipokezanwe kwani kiongozi hawezi kufanya kazi
zote peke yake. Juu ya Ikibali, ambaye alikuwa na wajibu wa kwenda Janibu
kuchungua mambo ya kodi, tunayaona mawazo mengi ya mwandishi kuhusu njia nzuri
ya mtu kuiweza kazi yake kwa urahisi. Zaidi ya kuwa na maarifa mengi, kuchuana
na watu kwahitaji tabia njema ambayo
ndiyo inayomkamilisha mtu. Tabia njema kwa viongozi wa nchi ndiyo alama ya ‘jembe’
au ‘nyumba’ ambayo Shaaban anataka watu waiangalie wanapoteua viongozi wao, na
ndiyo sifa inayowapa watu kuwaamini na kuwapenda.
Sura ya kwanza ni fupi; lakini
mwandishi ameitumia kutolea mawazo mengi kuhusu uongozi bora wa watu na utumiaji
bora wa ardhi, kuhusu raia, serikali, mawaziri, siasa safi na mifano bora ya
viongozi. Sehemu yote iliyosalia-na ni kubwa-anaitumia kutolea mawazo yake
kuhusu umma na jinsi ya kuishi kwa mapenzi na ujamaa. Na sura zote kumi na nne
zifuatazo, hadi kufikia mwisho, ni maoni juu ya ‘machimbo na hazina zake’, ‘biashara
na faida yake’, ‘safari na manufaa yake’, ‘utajiri na Baraka yake’, ‘hali na
heshima yake’ na juu ya ndugu, watu, jamaa na matendo yao-mambo yahsuyo dunia
nzima. Kwanza kabisa amekwisha kutoa maoni yake kuhusu ardhi na mimea yake na
mifugo na mazao yake, kwamba ni hazina za urithi wa watu wote. Hebu basi
tuangalie ni nini awazacho mtungaji huyu juu ya ujamaa na upendo kati ya watu.
Katika sura ya pili, mwandishi
anatoa maoni yake kuhusu mgeni Ikibali aliyekuwa na hulka ya kuwapendeza watu
waliokutana naye na ambaye usoni aling’aa kwa kicheko; na aliyekuwa na fadhila
na shukrani. Katika kwenda kwake Janibu, Ikibali anakutana na Adili, Liwali wa
mji huo ambaye mtungaji anamtumia kuelezea mawazo yake kuhusu namna nzuri na
mbaya ya kuishi na ndugu na watu mbalimbali. Ikibali alipotaka kurudi
Ughaibuni, Adili alimwomba akae Janibu kwa muda wa siku tatu zaidi ili wazidi
kutafaraji pamoja. Ikibali akakubali, kwani ‘waungwana hawanyimani neno’. Kwa hiyo
tunaona vile vile kuwa penye upendo pana kujitolea na subira pia.
Twafahamu kwamba subira mara
nyingi huvuta heri, basi Ikibali naye katika kusubiri kwake alivuna heri-na heri
yenyewe ilikuwa ni kule kuona kuwa kuna kitu fulani kibaya ambacho ilimlazimu
Adili kukitenda bila furaha. Juu ya habari hii ya Adili, Shaaban
anatutanabahisha tusimchukulie mtu kwa hali yake ya nje tu, tukafikiri yakuwa
mtu kama Adili-Liwali mzima-ati hana jambo linalomuondolea furaha. Mtu kama
huyo, tunapogundua ana tatizo, inafaa tumsaidie-si katika mambo ya kikazi tu
bali hata mambo yake mwenyewe binafsi. Hii ndiyo sababu Ikibali akaazimia
kumsaidia mwenziwe ingawa hilo jambo la kusaidiwa lilikuwa ni la siri: siri ambayo
ilibidi ifichuliwe ili msaada upatikane. Ndipo Ikibali akaitoboa siri hiyo, ya
Adili na manyani wake, na baadaye akenda naye mbele ya Rai, si kwa ajili ya
kumuaibisha bali kumfanya Rai ayasikilize maelezo ambayo huenda yakawa ndio
ufunguo wa furaha. ‘Aonae kosa akitoa hana lawama’, ndivyo asemavyo mwandishi. Na
kusaidiana ni dalili ya upendo nan i ujamaa.
Katika sura ya tatu, mawazo ya
mwandishi ni kuwa vitendo ni mapinduzi. Tunaambiwa kwamba busara nyingi humjia
mtu baada ya jambo kufanyika. Hivyo, Adili hakumkasirikia Ikibali kwa kumtolea
siri yake kwa Rai. Inaonekana kwamba wazo la mtungaji ni kusema kuwa itukiapo
ajabu, au jambo la kushangaza, huenda kukawa na sababu maalumu na kwamba, jambo
lenyewe likichunguzwa, huenda sababu yenyewe ikaonekana. Ajabu ya wale manyani
waliopanda farasi na kumfanyia mfalme ishara inapochunguliwa ndipo sababu yake
inapofahamika. Katika kusikiliza shauri la Adili na manyani kuna wazo kwamba ‘waungwana
hawasemi uongo’. Kwa hivyo ingawa Adili ameshtakiwa kwamba anawatesa manyani,
tunaona anawageukia manyani wale wale na kuwataka wayathibitishe ayasemayo.
Kuhusu malezi ya Hasidi, Mwivu na
Adili, mtungaji atoa wazo kwamba kumlea mtoto ni kumtunza mwili, kumfundisha
mawaidha na kuzipanua fikra zake, na zaidi ya yote ni kumfundisha ‘wema’ wa
moyoni. Moyo ndio makao ya upendo ambao ndio msingi wa ujamaa.
Kuhusu madeni inaonekana kwamba,
ili kutengeneza maisha ya upendo na kujitegemea, kukopa si jambo zuri na
kwamba, kama imekuwa lazima kulipa kabla ya kudaiwa. Na yule anayekukopesha
naye asiwe na lazima ya kudai kwa kero au inda.
Shaaban anamtumia Adili kueleza
kuwa, ingawa yeye alikuwa kitinda mimba, aliweza kuwa na busara na subira zaidi
ya wakubwaze. Busara yake ilimfanya afaulu katika biashara kwani aliweka
daftari ya mapato, kwa hivyo mali yake haikupotea bila ya kuelewa vile
ilivyopotea. Wazo la mtungaji ni kuwa biashara au shamba lahitaji mpango ambao
usipokuwepo patapatikana hasara. Kwa kuwa ndugu zake Adili hawakuwa na mpango
walifilisika baada ya mwaka mmoja tu. Na hivi ndivyo watu wengi duniani
wafanyavyo: hupata mali wakafanyia pupa kwa kutaka kuchuma zaidi bila mpango,
mara wakapata hasara. Lakini mtu kuvumilia na kusamehe ndugu zake ndilo jambo
linalohitajia, na hapa mtungaji anazidisha sana wazo lake la ukarimu. Kwa ajili
ya upendo, Adili aliwagawia tena mali nduguze ili wafanye tena biashara na
wajitegemee, wasimnyonye. Katika safari waliyoifanya wote watatu, Shaaban
anachukua nafasi ya kueleza faida za safari kwa kusema kuwa safari huleta ‘kufarijika
kkatika hamu, kujua namna ya kuendesha maisha, kupata elimu mpya, kuelewa tabia
za watu mbalimbali, kukutana na marafiki wa kweli kushinda ndugu, na mtu mwenye
bahati mbaya kwao huweza kupata bahati njema ugenini.’
Katika sura ya sita mwandishi
aeleza tena kwamba upendo ndiyo jambo muhimu duniani, kwani Adili ‘aliwapenda
ndugu zake kama pumzi ya maisha yake mwenyewe’. Pendo huleta huruma, na huruma
hii ndiyo iliyomwezesha Adili kumwokoa yule tandu aliyetaka kuangamizwa na
nyoka. Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba jema hulipwa na jema. Yule tandu,
ambaye alijigeuza msichana, aliahidi kumlipa wema Adili na akamwombea dua
njema. Sura hii inaonesha kwamba ujasiri unatakiwa sana katika kufanya mambo
yaonekanayo kuwa magumu. Kwa ujasiri wake, Adili alipata maji, na safari ya
pili akajitolea peke yake kwenda mji wa Mawe kutafuta tena maji ya kunywa.
Sura ya saba haina mawazo mengi
ya mtungaji ila kusema kwamba duniani kuna mali nyingi lakini ni vigumu mtu
kuipata ikiwa amejificha. Watakaoipata ni wale wajasiri tu wenye nia ya
kuipata. Sura ifuatayo yasema hivyo hivyo: bahati ya turufu humwendea mchezaji,
na ndivyo ilivyokuwa bahati ya Adili, hata sasa akawa na bahati ya kukaribishwa
humo mjini na msichana mrembo.
Mawazo ya uongozi bora yarudiwa
tena katika sura ya tisa. Katika ukurasa wa 35, tunaelezwa jinsi kiongozi
ahitajiwavyo kuwa katika maingiliano yake na watu na vile vile na dini ya kweli
ya Mungu. Mrefu alimwangamiza Mfalme Tukufu na enzi yake yote (ila bintiye,
Mwelekevu) kwa sababu kiongozi huyo alimdharau Mungu akawa anaamini mizimu na
uimamu wa Kabwere. Rehema za Mungu huwafikia wanaomtii, na hivi ndivyo
Mwelekevu alivyojaaliwa kukipata kile kitabu kitakatifu pamoja na ule
mkomamanga. Mizimu na kutomjali Mungu ni kinyume cha ustawi wa moyo.
Maelezo yafuatayo yanahusu wivu. Mtungaji
anatwambia kwa njia hii hii ya hadithi kuwa wivu haufai. Mwenye kupata kitu kwa
jasho lake aachwe kufurahia mapato yake. Katika ukurasa wa 40, mtungaji
anahubiri juu ya mambo machafu na hila mbovu kama za wale ndugu zake Adili
ambao kila mmoja wao aling’ang’ania kutaka kumwoa Mwelekevu na baadaye
wakaonelea kuwa yule binti awe mke wa wote-jambo ambalo ni chafu sana. Na hapo
ndipo atoapo mawazo yake kuhusu ndoa yenye msingi kamili, kuwa ndoa si jambo la
watu wote; ni la watu wawili tu-mume na mke. ‘Mwanamume hakukusudiwa kuwa
fahali wa kila mtamba, wala mwanamke kuwatembe wa kila jogoo’. Mafanikio ya
Adili yaliwakata maini nduguze, kwa hivyo maoni ya Shaaban hapa ni kwamba watu
wafanikiwao ni lazima wawe macho, watahadhari na kijicho wanachoonewa, kwani si
watu wote wapendao au wanaofurahia mafanikio yao. Tena nduguze Adili, waliokuwa
hawapendi Adili, wakamtosa majini kwa wivu. Tunaoneshwa kuwa, kwa upande
mwingine, pendo likitoka upande mmoja tu katika maisha ya ujamaa basi huwa
halina msingi imara, na maisha yake huwa si marefu. Pendo lazima litoke pande
zote mbili sawa kwa sawa.
Adili alitoswa majini lakini ile
dua ya msichana-tandu ikamuokoa. Mtenda mema mara ntingi hulipwa mema, na
mtenda mabaya naye pia hupata kadiri ya ule ubaya wake. Basi Adili akapata mali
zaidi, na nduguze walio na wivu wakaadhibiwa wakageuzwa manyani na kupigwa
mijeledi kila siku.
Sura ya kumi na nne na ya mwisho
zaonesha mambo mawili hasa: wajibu wa kiongozi kuwaangalia wafuasi wake kwa
shida zao-kama vile Rai alivyojishughulisha kumpatia Adili ushahidi kutoka kwa
babake Huria, Kisasi-na mafundisho kuhusu hali ya binadamu na vitendo vyake. Mawazo
haya ya Shaaban yasemwa na Rai kuwaambia nduguze Adili: ‘Weavivu walijitahidi
kuwa hodari, ilikuwa kinyume hodari kuwa wavivu; kama waovu walitaka kuwa wema,
ilichukiza wema kuwa waovu; kama maskini walitafuta utajiri, ilikuwa ujinga
matajiri kufuja walichokuwa nacho; kama mbegu kidogo iliongezwa mchanga,
ilikuwa uharabu mtu kuua ndugu yake; pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri
kutenda maovu.’
Kwa hiyo, ni dhahiri yakuwa
katika Adili na Nduguze Shaaban
afundisha watu waishi kwa kupendana chini ya uongozi bora, na wajisaidie
kiujamaa badala ya kujiangamiza na kuoneana wivu ambao hauna faida-si kwa hao
wenye wivu tu, bali kwa nchi nzima. Vile vile anawaambia wale wenye busara na
werevu kwamba dunia ni kubwa na imejaa mali na vitu vizuri ambavyo vitakuwa ni
vya kila avitoleaye jasho na mwenye wema moyoni na akili kichwani.
Wasifu wa Siti Binti Saad zaidi unaonesha pendo kuliko ujamaa,
lakini kiini chake ni ‘kujitegemea’. Kama Bwana Waziri Juma asemavyo katika
dibaji ya kitabu hicho (uk. vii), ni sawa kama mwandishi awatia moyo wasichana
na wanawake wengi wa Kiafrika wanaojibidiisha kwa shughuli mbalimbali kwa ajili
ya maisha yao.
Shaaban Robert ana nia ya kueleza
kwamba ni lazima mtu ajitegemee kwanza ndipo atakapofanikiwa kupata yale
ayatakayo. kule kuwa mwanamke, au kutosoma, au kutokuwa na fedha, au kutozaliwa
na kukaa mjini, au kutokuwa na sura nzuri, hayo yote si kitu kwani kujiamini,
kuwa na nia, na kuwa na subira na juhudi kunaweza kuleta mafanikio mengine
makubwa yasiyoweza kufikiriwa hata kidogo hapo mwanzoni. karibu kitabu chote
kinazungumza habari za mtu mmoja tu, na hakisemi mengi juu ya watu wengine ila
kuonesha tu yakuwa wapo wengine waliomuonea wivu Siti wakastahili kupewa jibu
la kuwatia vidaka vya midomo. kwa hivyo inaonekana kwamba maelezo yaliyomo humu
ni kama safari ya barabara moja yenye vipingamizi, na mtungaji anaonesha vile
msafiri mmoja anavyoendelea na safari yenyewe. na hata huyu msafiri mwenyewe, Siti,
ametumiwa na mtungaji ili awe mfano kwa wanawake wengine wanaojidharau na kuona
kwamba hakuna lolote hapa duniani wawezalo kulifanya. Lakini hivyo sivyo;
ulimwenguni ni mpana.
Shaaban Robert anataka kuonesha
kuwa katikati ya vizuizi mtu anaweza kusimama na kufanya kazi kwa bidii hata
akajipatia sifa. Siti hakuwa na bahati njema ya kuviepuka ‘vipingamizi’ vile vilivyotajwa
hapo juu (kutokuwa na sura nzuri na kadhalika), lakini vivyo alianza safari
yake katika maisha. alijua kuwa wazazi wake ni maskini, kwa hivyo aliendelea na
biashara yao ya kuuza vyungu. hakuna mtu aliyepata vyote au aliyekosa vyote. Mtumwa-jina
la Siti la hapo mwanzo-alikosa sura nzuri, lakini alifadhiliwa sauti ya kuvutia
kweli kweli. Fimbo iliyo mkononi ndiyo iuayo nyoka; kwa hivyo Siti aliifanya
sauti yake ndiyo fimbo yake, na akaitumia vilivyo. Hapa Shaaban anachukua
nafasi ya kutueleza kuwa sura nzuri si kitu cha kukiangalia sana maishani mara
kwa mara, wala si kizima kiu cha mapenzi. Mawazo yake ni kuwa inambidi mtu aikubali
hali yake kwanza, kisha ndipo atakapoweza kuona ni wapi anapofaa ili aweze
kufanya jambo atakalo kwa kadiri ya uwezo wake. na haya yote yawezekana, si ya
ajabu.
Lakini, katika kukata shauri juu
ya jambo la kutekeleza, mtu mara nyingi humbidi kuyatoa mhanga mambo yake
fulani aliyokuwa nayo kama vile Siti ilivyombidi kukiacha kijiji chao Fumba,
mumewe, mtoto wake na maisha ya utulivu yasiyo na ghasia, akakata shauri
kukidhihirisha kipawa chake kwa kuimba katika taarab mjini Unguja. Alihitajia
sana subira, juhudi, kujiamini na kujitegemea katika maisha mapya ya mjini
yaliyokuwa na vipingamizi vingi. kimojawapo cha vipingamizi hivyo kilikuwa ni
kushindwa kuimba siku ya kwanza alipotokea hadharani. Alikuwa hajazoea. Lakini
baadaye alifaulu kwani ‘alishikilia kazi yake kwa bidii’, akawa na dhamira na
nia ya kufaulu.
Kipawa bila ya ujasiri, dhamira
na nia ni bure tu. Maisha ya mjini ni magumu na hasa kwa mwanamke ambaye ni
mgeni tena ni mtu mzima ambaye hapo alipokuwapo hakuwa na mume. Lakini Siti
hakuwa muhuni. Aliweza kukaa imara kwani alikwenda mjini kwa kusudi maalumu; na
palimfaa kwalo. Hakwenda mjini kutafuta fedha, kwani tunaambiwa yakuwa Siti
hakupenda fedha, lakini kazi yake ilikusudiwa kumletea sifa na umaarufu. Hakuwa
mnyang’anya watu fedha kwa sababu ‘alikuwa mcha Mungu wa sala na saumu. Alisali
vipindi vitano kila siku, akafunga faradhi na suna katika maisha yake yote’.
Maoni ya mwandishi hapa ni kuwa mtu awe wa ibada saa za ibada, na mlimwengu
wakati wa mambo ya kilimwengu.
Pia inaonekana mwandishi
anafikiri kwamba Siti alifanikiwa kwa sababu ya ukarimu wake na Baraka kuliko
kuwa ni kwa sababu ya masharti ya mikataba na mapatano katika kazi yake.
Mafanikio, kwa wale wajuao wayafanyayo ni kama moto wa mbugani. Mara watu
wakawa wanamfuatafuata Siti, watribu wakamzunguka kwa vinanda ili awaimbie,
wapiga picha na wapiga chapa nao wakamwendea, watu wa santuri pia wakawa
wanamfuata, na kwa njia hii sifa za mwanamke huyu zikatapakaa hata nje ya Afrika
Mashariki. Mafanikio mengi ya Siti, asema Shaaban, ni kwa sababu alikuwa
mtanashati, hana majivuno, mwenye adabu na mlahaka kwa watu wote.
Ni kweli kabisa kwamba ‘jina
kubwa lolote halipatikani duniani bila vizuizi kadha wa kadha’ kwa maana kuna
mfano wa Siti ambaye, mara tu alipoanza kupata sifa kwa kuimba, watu walianza
kumwonea wivu na kumdharau na hata kumtukana. Kuhusu mambo haya yote, maoni ya
mwandishi ni haya: mtu lazima awe na subira, bidii na uvumilivu katika kazi
yake; aende mbele bila ya kuangalia nyuma.
Safari ya Siti katika maisha
ilifanikiwa kwa ramani ya maneno. Mwenye busara hujiwekea maneno ya kumwongoza.
Katika kuwajibu waliokuwa wakimtia ila na kumtukana, Siti alisema:
Si hoja uzuri, na sura jamali
Kuwa mtukufu, na jadi kubeli
Hasara ya mtu, kukosa akili
Huu ndio wimbo uliowakomesha
wapinzani wake. Na yaonesha kwamba mtu yambidi kujitetea anaposhambuliwa na
binadamu wenziwe, lakini si kujitetea kishenzi kama mnyama wa porini.
Kama kawaida, mwandishi
anajiuliza kwa nini Siti alifanikiwa hivyo? Maoni yake ni kwamba, kwanza, Siti
alifahamu sana tabia za watu, alikuwa na adabu na alijua kuchukuana nao (wazo
lililomo katika kitabu cha Adili na
Nduguze pia); na pili aliwapenda sana wasikilizaji wake. Hapa upendo
waonekana kuwa ndio msingi wa mafanikio. Hata hivyo, Siti hakujisifu mwenyewe.
Baada ya kueleza kwamba Siti
alizidi kusonga mbele, na kuviruka vipingamizi vingi, mwandishi anatoa mawazo
yake kwamba hayo hayakuwa mambo ya ajabu; matendo yake yanaweza kuigwa. Siti
alikuwa ni mtu kama watu wengine. Katika ukurasa wa 49 yapo mawazo mazuri ya
Shaaban yanayosema:
‘Fikiri kama na wewe umepata
kutenda neno lolote la fadhili kwa watu au nchi yako. Kama hujalifanya bado,
lifanye sasa. Yamkini una marafiki. Wafurahishe kwa fadhili yoyote uwezayo
kutenda. Haikosi una washindani. Wape sababu ya kukuajabia kwa unyofu ulio nao….Maisha
yalikuwa matendo, sio usingizi’.
Tangu mwanzo mpaka mwisho wa sura
ya nane Shaaban ameacha kutuzungumzia mtu wake. Hapa anasimama na kutoa mawazo
yake juu ya jambo moja muhimu sana kwa wanaadamu. Nalo ni tabia njema. Anasema
tabia njema imo katika ukweli na mapenzi ya moyoni. Tabia njema haifuati elimu,
wala utajiri, wala kuwa na cheo. ‘Tabia ilikuwa kama njia panda kuu katika
maisha yaliyogawa watu kwenda pande mbalimbali za dunia.’ Watu hutengana kadiri
ya tabia. Hata Mungu anawagawa watu kwa kufuata tabia zao. Ni vizuri kuwa na
tabia nzuri ambayo Shaaban Robert anafikiri ina amani na upole, saburi na
unyenyekevu, uungwana na uaminifu kwa watu wote-hiyo ni johari. Mwandishi
anahubiri juu ya tabia njema itakiwayo, akitoa mfano wa Siti, na anamalizia
kitabu chake vizuri sana kwa kutaja waziwazi kiini hasa cha mawazo na maoni
yake juu ya maisha.
Kama nilivyosema hapo awali,
Shaaban Robert katika Wasifu wa Siti
Binti Saad anaonesha jinsi mtu, hata akiwa katika hali ya chini, awezavyo
kujitahidi hadi akaweza kustawi na kujitegemea. Sura ya mwisho inatilia mkazo
neno kuu la kitabu hiki, ‘kujitegemea’. ‘Kujikimu ni kujiruzuku. Kujiruzuku ni kujitegemea kwa chakula, nguo na
masurufu mengine katika maisha.’ Na hapa ndipo tutakapokomea kutoa mawazo ya
mtungaji wa kitabu hiki.
Baada ya kuhakiki Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, na pia nikiyapima mawazo ya marehemu
Shaaban Robert katika fasihi zake nyingine kama mashairi yake Masomo Yenye Adili, Kusadikika, na Kufikirika, naona vigumu sana kuuepa
ukweli kwamba marehemu aliandika vitabu vyake kwa nia ya kufundisha watu;
alitoa fasihi yake iwe kioo cha watu kujiangalia ili waone jinsi wanavyoishi na
wanavyotaka kusihi, na vile vile waone jinsi ambavyo yeye mwenyewe Shaaban
Robert angependelea watu waishi. Kwa sababu hii, maandishi yake yote yanang’aa
kwa ilani isemayo, ‘Maisha ya mtu ni msingi wa maendeleo ya nchi.’ Maneno haya
ndiyo ufunguo uliomo mwanzoni kabisa mwa Maisha
Yangu na Baada ya Miaka Hamsini-kitabu ambacho kwacho Shaaban ametueleza na
kutuonesha sehemu ya maisha yake.
Kingwana ni lahaja ya Kiswahili inayozungumzwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hasa upande wa mashariki.Chanzo chaKingwana ni Kiswahili cha wafanyabiashara na askari kutoka pwani ya Bahari Hindi (leo nchini Tanzania) walioingia katika Katanga kwa biashara ya watumwa na pembe za ndovu wakati ya karne ya 19 kabla
ya ukoloni. Lugha ikaendelea ilipokuwa chombo cha mawasiliano katika mchanganyiko wa watu wa makabila mbalimbali walioelekea kutafuta kazi katika migodi ya Katanga na Kongo ya
Mashariki. Mfano wa Kingwana
HABARI NJEMA KAMA YOHANA ALIANDIKA
Ku mwanzo Neno alikuwa, na Neno alikuwa pamuya na Mungu, na Neno alikuwa Mungu. 2 Ye njo alikuwa ku mwanzo pamoya na Mungu. 8 Vitu yote zilifanywa na ye; na haiko na ye, kitu haikufanywa ile ilifanywa. 4 Ndani yake ilikuwa uzima; na uzima ilikuwa nuru ya watu. 5 Na nuru inangala ku iza; na iza haikusinda ye. 6 Mutu moya alitokea, alitumwa kutoka ku Mungu, jina yake Yohana. 7 Ye njo alikuya sahidi, asuhudie nuru, watu yote waamini kwa sababu yake. 8 Hakukuwa nuru ile, lakini alikuya asuhudie nuru. 9 Nuru ile ilikuwa nuru ya kweli, ile inapatisa nuru kila mutu ile anakuya ku ulimwengu. 10 Alikuwa ku ulimwengu, na ulimwengu ilifanywa na ye, na ulimwengu haikuyua ye.
Nyimbo za harusi huimbiwa bwana na bibi harusi kuwapongeza na kuwapa heko kwa kufunga ndoa yao. Aidha nyimbo hizi huwapa wawili hao mawaidha ya kutunza familia na watoto wao ili waishi pamoja.
Nyimbo za Jandoni/Tohara
huimbwa na vijana wanapopashwa tohara. Nyimbo hizi huonyesha ushujaa, na kuashiria kutoka kwamba anayetahiriwa amekuwa mtu mzima sasa.
Hodiya/Wawe
Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na watu wanapofanya kazi ili kuwatia bidii wafanye kazi bila kuhisi machofu.
Kimai
Nyimbo za Mabaharia – Hizi ni nyimbo za wanabahari wanaposafiri baharini.
Nyimbo za Mazishi/Huzuni/Simanzi
Hizi ni nyimbo za kuliwaza na kuwapa pole walioachwa na marehemu. Nyimbo hizi huwapa matumaini waombolezaji.
Nyimbo za Kidini
Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa kumsifia Mungu, kuomba au kutoa mafunzo ya kidini.
Nyimbo za Kisiasa
Hizi ni nyimbo za kuwasifia viongozi wa kisiasa
Nyimbo za Kizalendo
Nyimbo za huonyesha uzalendo kwa kusifia taifa/nchi
Nyimbo za Mapenzi
Katika nyimbo za mapenzi, mwimbaji huimba kwa kumsifia mpenzi wake hasa kwa urembo na tabia zake.
Nadharia huchukuliwa kuwa dira ya kumwongoza mtafiti au mchambuzi kulikabili na kulielezea vyema jambo fulani kwa tazamao unaotazamiwa kuwa imara zaidi kuliko ule wa nadharia nyingine. Nadharia hutoa mwongozo katika utatuzi wa jambo fulani ambalo halijaweza kuhakikishwa ukweli wake. Ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kutatua au kutekeleza jambo fulani, kwa upande wetu jambo la kifasihi simulizi.
HISTORIA YA NADHARIA YA FASIHI SIMULIZI
Historia ya nadharia ya fasihi simulizi ilianza katika elimu ya ushairi, balagha n.k. ya Wagiriki toka karne ya 18. Katika karne ya 20 nadharia hii imekuwa ni mkabala mkubwa katika usomaji wa matini. Kuna nadharia mbalimbali za kifasihi kama vile Umuundo, Umarksi, Ufeministi nk.
Hivyo, tunaweza kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi simulizi ni chombo kinachotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani. Hii ina maana kwamba ni mwangaza unaoimulika jamii juu ya mazingira na fikra zake. Kwa hali hiyo basi, nadharia hii haina budi kuzibainisha sifa na ushirikiano wa jamii husika.
Kuingia kwa ukoloni mamboleo kumefanya fikra na maarifa kutoka nje zitukuzwe na kuabudiwa huku fikra za ndani zikidumazwa kila kukicha. Kwa kufanya hivyo nadharia hizi zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo. Kwa mfano; utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, jando na unyago, nk zimebadilika baada ya kuingia kwa ukoloni mamboleo.
Hata hivyo, wahakiki wa Magharibi na Kiafrika wameangalia mambo mengi yaliyoikabili fasihi simulizi ya Kiafrika kama tutavyoona katika nadharia za fasihi simulizi tutakazopitia.
Nadharia za Fasihi simulizi tutakazojadili katika kozi hii ni hizi zifuatazo:
1: Nadharia za kitandawazi
Nadharia ya Ubadilikaji Taratibu (Evolutionalism Theory)
Nadharia ya Msambao (Diffusionism Theory)
Nadharia ya Kisosholojia (Sociological Theory)
2: Nadharia za kitaifa
3: Nadharia Hulutishi
1. Nadharia za Kitandawazi
Ubadilikaji Taratibu “Evolutionalism”
Mfuasi wa nadharia hii ni Charles Darwin (1809-1882) ambapo hoja zake zilikuwa na ushawishi mkubwa kwa wanafunzi waliokuwa wakijifunza kuhusu utamaduni kama vile Edward Burnet Tylor (1832-1917) na James George Frazer (1854-1941). Wote hawa waliamini juu ya misingi anuwai kuhusu kanuni zinazoongoza asili na maendeleo ya utamaduni wa mwanadamu.
Kundi hili liliona kuwa dhana ya ubadilikaji taratibu misingi yake mikuu ni viumbe hai. Wanaona kwamba viumbe hai vyote vinakuwa katika mchakato wa mabadiliko mbalimbali hadi kufikia maumbo vilivyonayo sasa.
Wanaedelea kusema kuwa kuna kanuni ambazo ni muhimu sana zinazochangia makuzi ya kanuni za binadamu. Wakaona kuwa kuna ukoo, akili au asili au jamii moja ambayo imezagaa ulimwenguni kote, na kama uchunguzi utafanywa wa kuchunguza jamii mbili kiutamaduni katika kipindi kilekile cha mabadiliko, itabainika kuwa elimu zao zina tabia zinazofanana.
Wanaendelea kusema kwamba, ili kuelewa jamii moja kwa ujumla ni vyema kulinganisha na jamii nyingine ya aina hiyo kwa kipindi kilekile cha ukuaji. Kwa mfano kuchunguza ngano za kijadi katika makabila mbalimbali ya Kusini kama vile uchawi na miviga na kulinganisha na jamii za Kiafrika.
Kwa ujumla katika nadharia hii tunabaini kuwa nadharia hii ilitawaliwa na mbinu linganishi (comparative methods).
Kwa mfano Frazer (kazi yake ni The Golden Bough ambayo ilikuwa katika majuzuu 13), alitafiti sanaa jadi ya Waitalia. Katika utafiti wake yeye alijihusisha na kutafiti chimbuko la matambiko ya uchawi na dini huko Italia. Alichokuwa anataka kuthibitisha kuhusu jamii ya Waitalia ni kwamba asili ya dini inapatikana katika magical rites za mtu wa kale.
Pamoja na watafiti wenzake, walikuja kama watawala na kuchunguza mila na desturi za Kiafrika ili kuzilinganisha na utafiti kama huo aliokuwa akiufanya huko kwao. Walitafiti na kuchunguza jamii ndogo ndogo za Kiafrika na kisha kufanya ulinganishi. Kwa ujumla wataalamu hao walikusanya, walitathimni fani mbalimbali za Kiafrika kama vile ngano, nyimbo, vitendawili, methali na aina nyingine, za FS katika jamii mbalimbali za Kiafrika. Baadhi ya watawala wataaluma wa kikoloni walitafiti kuhusu fasihi simulizi ya Kiafrika chini ya usimamizi wa Frazer ni pamoja na;
John Roscoe ambaye alitafiti jamii ya Baganda- Uganda.
Edwin Smith & Andrew Dale ambao walitafiti jamii ya Ila- Zambia.
Reverend Henri Junod- Tonga, Afrika Kusini
Robert Rattray- Akan-Ghana, pia Hausa- Nigeria
P. Amaury Talbot- Ekoi- Nigeria (Southeastern Nigeria)
H. Chatelain- Angola. Chatelain akichunguza kuhusu ngano za Angola na za Afrika kwa jumla, aligundua kuwa ngano za Kiafrika ni tawi toka mti mmoja wa ulimwengu.
Mwisho, wote kwa pamoja walihitimisha kuwa watu wa Afrika ni sawa na watu wengine popote pale ulimwenguni.
CHANGAMOTO
Dhana hii ya ubadilikaji taratibu iliathiri mbinu na matokeo ya utafiti wao kwa njia tofautitofauti kama vile:
Ø Kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi kilihesabika kama masalia ya zamani au mabaki ya fasihi zilizotangulia.
Ø Kadri fani hizo zilivyorithishwa kwa njia ya mdomo toka kizazi kimoja hadi kingine ndivyo zilivyozidi kupoteza sifa mahsusi za ubora, zilichuja na kuchujuka
Ø Chochote kilichosalia lazima kitakuwa na dosari fulani tofauti na kitu halisi cha zamani
Ø Walijihusisha mno na maudhui na kamwe hawakujihusisha na sifa za kifani kama vile miundo na mitindo ya fani husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba lengo lao lilikuwa ni kufahamu hali halisi ya utamaduni wa jamii za watu wasiostaarabika na historia yao. Ili kuyafahamu haya waliona kuwa ni bora kupata muhtasari tu wa maudhui yanayojadiliwa ndani ya fasihi simulizi ya jamii husika na sio kujihusisha na fani ya fs hiyo
Ø Hawakuoa umuhimu wa fanani na mtambaji: “no creator, no author of such tales,…….as a product of joint or communal authorship.”
Ø Pia waliziona kazi za fasihi simulizi za Kiafrika kwamba hazina mwenyewe kwa kuwa ni mali ya jamii nzima. Walisema kwamba, ijapokuwa fasihi simulizi ni mali ya jamii, lakini sio kwa kiwango hicho walichokisema wao. Walisisitiza kuwa si kila mzungumzaji anaweza kuwa fanani wa fasihi simulizi. Wao walilipuuza suala la upekee wa muktadha.
HITIMISHO
Kimsingi, ilikuwa vigumu sana kupata matokeo sahihi katika uchunguzi ulioongozwa na misingi ya kiuibukaji. Hii ni kutokana na mbinu batili zilizotumika pamoja na kuongozwa na malengo muflisi na finyu kuhusu umbile la jamii za Kiafrika kwa jumla. Leo hii nadharia hii haitumiki tena katika mijadala ya fasihi simulizi. Wakoloni waliitumia kama njia ya kuhalalisha suala la uvamizi na ukoloni barani Afrika.
Nadharia ya Msambao “Diffusionism Theory”
Iliongozwa na mawazo na ushawishi wa Grimms na Thompson
Ni nadharia iliyopingana na nadharia ya ubadilikaji taratibu tuliyoona hapo juu. Wana ubadilikaji taratibu waliamini kuwa;
Ikiwa ngano mbili kutoka katika jamii mbili tofauti zimeonyesha kufanana kwa namna fulani za kimuundo au kimaudui ni kwa sababu wanadamu ulimwenguni kote wanamkondo mmoja wa mawazo na kufikiri kwao ni kwa namna moja, na kwamba ngano hiyo inasawiri hatua sawa za maendeleo ya kiutamaduni katika jamii husika.
Tofauti na wanaubadilikaji, wanamsambao wangeamini kuwa;
Pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea, sababu ya msingi ya kuwapo kwa mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani sana jamii hizo mbili ziliwahi kukutana kwa namna fulani, makutano baina ya jamii hizo yalisababisha hali ya kuazimana kwa baadhi ya mila na tamaduni (mawazo) mojawapo ya jamii husika.
Watafiti hawa waliangalia mila na desturi za jamii zilivyokuwa zikikua na kusema kuwa zilikua kutokana na msukumo wa asili na lugha za Ulaya. Walikubaliana kwa sehemu kubwa kuwa asili ya mila, desturi na aina nyingine za utamaduni zinapatikana India, na walitaka kutafiti ni kwa kiasi gani utamaduni huu wa Indo-European ulikuwa umesambaa duniani.
Wana msambao nao walitumia mbinu ya ulinganishi kama walivyofanya wanaubadilikaji taratibu. Kazi ya utafiti ilihimizwa na wajerumani ambao ni Jacob na Wilhelm Grimm ambao walikusanya ngano nyingi kutoka India na kutoka katika nchi yao.
Jacob na Wilhelm Grimm: Walitafiti ngano kutoka India na Afrika, na walihitimisha kwamba, kuna kufanana kwa ngano za India na Ulaya. Wakatoa maamuzi ya kwamba, hadithi za Kiafrika ni chimbuko kutoka kwa wazazi wenye asili na utamaduni wa India na Ulaya. Hivyo, dhana yao hiyo waliifikia kutokana na kuifanyia kazi dhana potofu, kwani kila bara lina utamaduni, mila na desturi zake. Aidha waliliona bara la Afrika kama bara ambalo halijastaarabika.
Stith Thompson: Yeye aliwaunga mkono akina Jacob na Wilhelm. Katika kitabu chake cha The Folktale (1946:438)anapendekeza kuwa panapotokea kufanana kati ya ngano/hadithi za Ulaya na za Afrika, zinaweza kuelezewa kuwa huenda hadithi/ngano hizo zililetwa na Wazungu wakati wa utumwa.
Mawazo yao kwa ujumla ni kuwa;
Ø Utamaduni unaweza kusambaa tu kutoka katika jamii imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea kwenye utamaduni wa jamii iliyo kinyume chake “from superior to an inferior people)
Ø Ikiwa kulikuwa na kufanana kwa namna yoyote katika ngano zilizopatikana Afrika na Ulaya kwa mfano, lazima moja kati ya jamii hizo ni dhaifu kuliko nyingine, na jamii dhaifu….Afrika, ilihali jamii imara… ulaya
Ø Yote haya yangeweza kuelezwa tu kwa misingi ya ukweli kuwa jamii za Ulaya zilileta mambo hayo Afrika kutokea Ulaya kipindi cha biashara ya Watumwa (Thompson 1946:438)
Tafiti ziliendelea kufanyika baada ya Jacob, Grimm na Thompson ambapo bara la Afrika lilionekana kuwa bara lenye giza na hivyo kukaonekana haja ya kuanzisha dini ya Kikristo na teknolojia ya Ulaya barani Afrika ili Afrika iondokane na giza hilo.
Kwahiyo tunaweza kuona namna kila kitu cha Afrika ikiwemo fasihi simulizi yake vilivyodidimizwa na watawala hawa wa kikoloni.
Mapungufu
Tunaweza kusema kwamba, ingawa walijitahidi kuipa hadhi fasihi simulizi kwa kusisitiza upekee wa muktadha, hawakuchunguza kwa undani sifa za kisanaa za fasihi simulizi. Pia walijishughulisha na muhtasari tu wa simulizi walizochunguza, na hivyo ni dhahiri kwamba kuna vipengele vingine muhimu vya Fasihi Simulizi ya Kiafrika ambavyo havikutiliwa maanani..
Hitimisho
Ø Bado tafiti za namna hii hapa Afrika zinaendelea lkn mkabala na malengo ni tofauti
Ø Ule upendeleo uliokuwepo hapo zamani sasa umeondoka
Ø Sasa wanajihusisha na kutafiti msambao wa ngano na vipengele (units) vyake ndani ya tamaduni mbalimbali, katika bara la Afrika. Kama vile asili ya ngano za Kiafrika zinazosimuliwa katika Marekani ya Kusini na Kaskazini
Nadhari ya Sosholojia ‘Sociological Theory’
Mihimili ya Nadharia hii
(a) Umahsusi na sio umajumui
· Ilikuwa mahususi zaidi kuliko nadharia zilizotangulia: badala ya kujikita katika taaluma ya sanaa jadi kwa ujumla (maumbile ya mwanadamu na utamaduni wa mwanadamu) kama walivyofanya wanadharia wa zamani, nadharia ya usosholojia ilijikita katika jamii peke yake.
· Hii ilikuwa baada ya kugundua dosari zilizofanywa hapo kabla; dosari za kutoa matamko ya juu juu na ya kijumla zaidi
Ø Kauli hizo mara nyingi zilitupilia mbali vipengele fulani vya maisha kmv lugha na mienendo mingine….. hakika viliitofautisha jamii moja dhidi ya nyingine
Ø Kwao, tofauti zilizokuwepo baina ya jamii moja na nyingine zilikuwa na maana zaidi kuliko kufanana kulikokuwepo
· Kwa hiyo wanasosholojia waliazimia kuchunguza kila jamii kwa wakati na nafasi yake, kwa kurekodi kila kilichopatikana katika jamii husika (sanaa jadi yao).
· Wataalamu mbalimbali walioongoza jitihada hizi ni pamoja na hawa wafuatao
Ø Bronislaw Malinowski na A.R. Radcliffe-Brown (Uingereza)
Hawa walichunguza jamii mbalimbali katika Pasifiki, na waliandika mengi kuhusu jamii hizo. Jamii hizo ni pamoja na visiwa vya Trobriand na Andaman mutawalia
Ø Franz Boas (Marekani)
Huyu alichunguza jamii za wenyeji wa Marekani
· Wapo pia wataalamu wengi waliofanya utafiti wao, na kuandikia kuhusu jamii za Kiafrika ambao ni pamoja na hawa wafuatao
i. E.E. Evans-Pritchard………Nuer (Sudani)
ii. Geoffrey Lienhardt……..Dinka (Sudani)
iii. William Boscom…….Yoruba (Nigeria)
iv. S.F. Nadel………..Nupe (Nigeria)
v. Marcel Griaule……….Dogon (Burkina Faso)
Ingawa hata kabla ya wataalamu hawa, kulikwishakuwepo wataalamu wengine waliotafiti na kuandika kuhusu FS ya kiafrika lakini wataalamu hao waliongozwa na mawazo ya kiubadilikaji taratibu zaidi
(b) Mkazo katika Utendaji
-Tofauti na ilivyokuwa kwa wananadharia wa nadharia zilizotangulia ambao hawaku…. “They were not interested in studying the performers of oral tradition” wanasosholojia waliweka msisitizo katika kuchunguza PERFORMERS/watendaji wa fani mbalimbali za FS. Kutokana na msisitizo wao huu imebainika kuwa
*Fanani wa FSwanaujuzi na ustadi wa kiutendaji katika sanaa husika (ubunifu wao ni mkubwa sana).Jambo hili… limetusogeza mbele kidogo ktk kuielewa FS
*Wanasosholojia walidiriki na kuthubutu kudokeza kuhusu sifa za ndani za kimtindo katika FS ya kiafrika
Ø Tofauti na ilivyokuwa imedhaniwa hapo mwanzo kuwa FS ni mabaki tu ya zamani na kwamba hayakuwa na umuhimu wowote katika maisha ya jamii katika zama za kisasa, wanasosholojia waliamini kuwa uamilifu wa FS uko hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na maendeleo ya jamii husika. Dhima hizo ni pamoja na “DHIMA ZA KIJAMII ZA FS…KWA MUJIBU WA WANASOSHOLOJIA”
– FS ni kama Encyclopedia ya hekima za jamii husika
Hii ni kwa mujibu wa Bascom 1959 ambaye alifanya utafiti katika Poetry of Divination katika jamii za Wayoruba wa Nigeria
– FS ni nyenzo muafaka ya kurekodia hatua mbalimbali za maendeleo ya jamii husika. Aylward Shorter 1969…..the tales of origin katika jamii ya Wakimbu Tanzania
– FS inasaidia na imeendelea kusaidia kuimarisha ‘authority of statement or a custom in situation kama vile katika mahakama au contests for Chieftaincy. J.C. Massenger…..Anang of Nigeria 1958, J.B. Christenseu……Fante of Ghana 1958. Hawa walichunguza Methali katika jamii zilizotajwa
· CHANGAMOTO ZAKE…….Pamoja na uzuri uliotajwa bado kuna changamoto kadhaa
Ø Given far less time to illuminating and analyzing the artistic properties of African OL
Ø They have published tale, in flat, unimpressive prose, eliminating features of oral style (repetition and exclamation)
Ø They have done few carefully analyses of techniques of the original language that appealed to the audience of the tale in the first place
Ø The circumstances surrounding the performance of the tale (ushiriki wa hadhira, matumizi ya ala za muziki, nk) not reported
Ø Hata pale ambapo wamejaribu kuuleza vyema muktadha huu, umuhimu na nafasi yake katika kufanikisha au kukwamisha ngano husika haujaelezwa
Ø Ilikuwa vigumu sana kwa kutumia mbinu zao kuona ni kwa vipi ngano kwa mfano inaweza kuwa fasihi
Ø Pia kutokana na mbinu yao ya kusisitiza umuhimu wa FOLKLORE katika utamaduni wa watu, wataalamu kmv BOSCOM NA BEN-AMOS walisisitiza kuwa “Any judgement of a folk text must be based on the views of the society from which the text come”Wazo hili ni zuri sana lkn, ikiwa kazi za fs ya kiafrika zitaeleza mawazo ya wageni na si ya wenyeji, kmv boscom na amos, ni kwa sababu sanaa hizo zina sifa fulani fulani ambazo zinaenda na kueleza mambo fulani yaliyo mbali na dhana ya uzuri kwa waafrika. Mazingira km haya yakitokea, ni jukumu la mwandishi, ikiwa kweli wanaelewa vyema lugha husika, kufafanua sanaa husika na sifa za sanaa hiyo ilimuradi wageni waikubali sanaa husika na waipokee. Kwa hiyo mkabala wa MUKTADHA WA KIJAMII waliokuwa nao wanasosholijia ulikuwa FINYU SANA….. changamoto ya kiuhakiki ktk kazi za kifasihi
· HITIMISHO………..Hata kabla ya wataalamu hawa kufanya uchunguzi wa kisosholojia, walishakuwepo wataalamu wa mwanzo kama vile…………………….. ambao walifanya uchunguzi wa kisosholojia.
Ø Tofauti kubwa ni kuwa wale wa mwanzo waliongozwa na mawazo ya kiuibukaji
Ø Waliongozwa na kuhamasishwa na ….kizazi cha Franzer.
Ø Hawa wa baadaye walijihusisha na kuhamasika zaidi na “ HISTORIES OF THE CULTURES THEY STUDIED
Ø PIA waliongozwa na kuhamasishwa na mawazo ya Malinowski
Ø Pia hawa wa baadaye walitilia mkazo matumizi na uamilifu wa sanaa jadi za kiafrika katika jamii “SOCIETAL FUNCTIONS OF OL
Ø Hata hivyo, bado wataalamu hawa hawakufanikiwa au hitimisho lao halikuendana na tathimini ya karibu na kina kuhusu material walizozikusanya. Hii ni kwa sababu hawakuwa na ujuzi wa kutosha katika lugha za jamii za kiafrika
Tungo Fupi ni kipera cha Fasihi Simulizi kinachojumulisha sanaa simulizi zinazoundwa kwa maneno machache; sentensi moja au mbili hivi. Tungo Fupi nyingi huwa na sehemu mbili na aghalabu huhitaji kujibizana ambapo mtu mmoja hutoa pendekezo au swali; halafu mtu mwengine hutoa jawabu – k.m vitendawili na mafumbo. Baadhi ya tungo fupi husemwa na mtu mmoja tu kama vile methali.
Aghalabu vipera vyote vya tungo fupi hutumiwa katika kazi nyingine za fasihi ( na lugha kwa ujumla ) kama mapambo ya lugha.
Vipera vya Tungo Fupi
Methali
Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya mafumbo. Methali huwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza hutoa hoja nayo sehemu ya pili hutoa suluhisho. Methali hutumika kwa minajili ya kutoa funzo kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Methali nyingine huhitaji hekima ili kujua maana yake.
Vitendawili
Vitendawili ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi na jibu kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huulizia swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti, harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitajika kufikiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa la neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalum kulingana na jamii yake.
Mafumbo
Mafumbo hutumika kuupima uwezo wa mtu kufikira na kufumbua swali ambalo huwa na maelezo marefu. Majibu ya mafumbo huhitaji maelezo na aghalabu hukusudia kujua jinsi mtu anavyoweza kutatua tatizo fulani ambalo linahitaji kufikiria sana.
Vitanza Ndimi
Vitanza ndimi huwa ni sentensi zinazotumia maneno yanayomkanganya msomaji katika matamshi. Vitanza ndimi huhitaji kutamkwa haraka haraka na kurudiwa rudiwa mara kadhaa kwa kusudi la kukuza uwezo wa kutamka.
Vichezea Maneno
Ni maneno yanayokaribiana kimatamshi au kimaana hutumika katika sentensi moja kama njia ya kuonyesha ukwasi wa lugha au kuburudisha. Pia hutumika kama vitanza ndimi.
Misimu
Misimu ni maneno ambayo huzuka miongoni mwa kundi fulani katika jamii na hueleweka tu miongoni mwa watu katika kundi hilo. Misimu hukua na kutoweka baada ya muda.
Lakabu
Lakabu ni majina yanayobandikwa watu kutokana na sifa zao, maumbile, hulka au mambo yanayowahusu. Lakabu pia ni mbinu ya sanaa.
Semi (Nahau na Misemo)
Semi ni mafungu ya maneno ambayo hutumika kuleta maana tofauti na maana halisi ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha maneno makali kwa kutumia maneno mengine. Aidha semi zinaweza kutumika tu kwa minajili ya kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi: Nahau na misemo