MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 1 - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 1 (/showthread.php?tid=1398) |
MAISHA YA SHAABAN ROBERT NA MAWAZO YAKE (M.A. Maganga) – 1 - MwlMaeda - 10-27-2021 Makala haya yamegawika sehemu
mbili. Sehemu ya kwanza inachungua mawazo ya Shaaban Robert aliyoyatoa katika vitabu vyake viwili: Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Sehemu ya pili yatumia mawazo hayo kupimia vitendo na maisha ya Shaaban kama alivyotueleza yeye mwenyewe katika vitabu viwili vingine vilivyokusanywa pamoja: Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Nionavyo mimi, Shaaban Robert
amechukua nafasi ya kuandika vitabu vyake hivi viwili vya mwanzo ili aweze kutoa mawazo na maoni yake kuhusu mambo mabaya na mazuri, yapi ya kufuata na yapi ya kuepuka katika dunia yenye maisha mbalimbali. Baada ya kuvisoma vitabu hivyo kwa makini, nimekatikiwa kuwa Shaaban alikuwa na mawazo yasiyo tafauti na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Amefikiria kuishi kwa ujamaa katika kitabu chake cha Adili na Nduguze na katika Wasifu wa Siti Binti Saad ametoa mawazo yake kuhusu maisha ya kujitegemea; na bila shaka ana lengo halisi katika kutoa mawazo hayo. Pengine alipenda kueleza na kufafanua, au kupanua zaidi, yasemwayo katika Injili Takatifu, yaani ‘umpende jirani yako kama nafsi yako’, na mapenzi hayo ndiyo msingi wa wema, matendo safi, na juhudi ya kazi ziletazo faida kwa watu wote. Kwa kuwa vitabu viwili hivi
vimetumiwa kama vyombo vya kuelezea aina mbili za mawazo na maoni ya mtungaji, naona ni vema nisivichanganye katika uchambuzi huu bali nivichukue kimoja kimoja. Ebu nianze na kile kilichotangulia kutoka. Kimoja kilitoka mara ya kwanza katika jarida la 1958 (Nambari 28/1) la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, na kingine kilitoka mara ya kwanza kama kitabu kamili mnamo 1952, nacho ni Adili na Ndiguze ambacho ndicho tutakachoanzia. Nimesema kwamba mawazo ya Shaaban
‘Kwa marafiki zanguRobert yana lengo au kiini fulani. Katika Adili na Nduguze lengo lake ni upendo, yaani watu wapendane na kuishi kiujamaa-na upendo huo ndio alioufungulia kitabu chenyewe alipoandika mwanzoni: Wazawa wa Afrika Pamoja na Wazungu Wapendao afrika’. Shaaban Robert amekianza kitabu
chake kwa maelezo juu ya Mfalme Rai. Mawazo yenyewe, nionavyo mimi, ni sawa nay ale yasemwayo na Azimio la Arusha kwamba, ili kuleta mafanikio na maendeleo ya nchi, vihitajiwavyo ni ardhi, watu, uongozi bora na siasa safi. Kiini cha kumuanzia Rain i kutaka
kueleza kwamba, hata kama ardhi na watu wapo, jambo la kwanza linalotakiwa ni uongozi bora wenye msingi ufananao na tabia ya Rai. Pengine ardhi na watu wa Ughaibuni walifanikiwa na kuendelea kwa sababu ya uongozi mzuri wa Rai. Mawazo ya Shaaban ni kuwa uongozi mzuri wa nchi ni kama ule wa Rai ambao kiini chake kilikuwa upendo. Alikuwa na mapenzi na wanaadamu, nao wakampenda;alifuata msingi wa kidini wa zamani ambapo Daudi aliwapenda wanyama na Sulemani akatiiwa na majini. Mawazo ya Shaaban juu ya kiongozi
bora wa nchi yoyote yameelezwa katika wasifu wa Rai, ukurasa wa pili. Hapo uongozi bora unaonekana unahitajia uadilifu, wema, kufanya kazi ndogo na kubwa au kutoa amri zifanywe, kusaidia na kushiriki katika maendeleo ya nchi, kutolazimisha watu mambo bali kuwashawishi tu (kama uhitajivyo ujamaa wa kweli), kuvuta mioyo ya watu ili kusiwe na wavivu, magoigoi wala waoga. Kwa namna hii Shaaban Robert atoa
mawazo kwamba viumbe wote wangefurahia sifa ya kiongozi wa namna hiyo-tangu malaika mbinguni hadi ndege angani, watu duniani, samaki majini, na hata majini na mashetani popote pale wafikiriwapo wapo. Upendo na ujamaa wa kweli ni kufanya urafiki na viumbe mbalimbali pamoja na kuwajali watu wote. Baada ya upendo ni matendo. Na hapa ndipo Shaaban aliposema: ‘Tendo hukidhi haja maridhawa kuliko neno.’ Yaani, tendo huleta haja upesi lakini neno huichelesha; na neno tu si njia ya kuleta mapinduzi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Katika kuhukumu mwandishi
aonekane ana machache ya kueleza. Itolewapo hukumu inatakikana kiongozi awe imara, asipendelee bali watu wote wawe sawa mbele ya sheria. Hiyo ndiyo demokrasi halisi-demokrasia ya kiujamaa. Uongozi bora ni ule ufuatao haki ya watu na wanyama pia, na ule ufanyao uchunguzi wa matukio yote-mazuri na mabaya-kwa raia. Na, katika uchunguzi wa Rai kuhusu kasoro iliyotokea Janibu, ndimo Shaaban Robert anamoeleza mawazo yake kuhusu tabaka kwa tabaka za maisha ya kiujamaa nay ale yasiyo ya kiujamaa. Na juu ya huo uchunguzi Shaaban anasema, ‘Mambo katika maisha yambo katika mwnedo huu siku zote. Hayajulikani mpaka yamechunguzwa na kuthibitishwa kwanza.’ Kiongozi bora kama Rai huwa mtu arifu wa mwendo huu! Tunaambiwa vile vile kuwa si
kiongozi tu atakikanaye kuwa mtu wa kufaa bali watu wote walio na wajibu na mamlaka chini yake, kama vile Rai alivyokuwa na Maarifa (Waziri Mkuu) na Ikibali (Mshauri). Na kazi lazima ipokezanwe kwani kiongozi hawezi kufanya kazi zote peke yake. Juu ya Ikibali, ambaye alikuwa na wajibu wa kwenda Janibu kuchungua mambo ya kodi, tunayaona mawazo mengi ya mwandishi kuhusu njia nzuri ya mtu kuiweza kazi yake kwa urahisi. Zaidi ya kuwa na maarifa mengi, kuchuana na watu kwahitaji tabia njema ambayo ndiyo inayomkamilisha mtu. Tabia njema kwa viongozi wa nchi ndiyo alama ya ‘jembe’ au ‘nyumba’ ambayo Shaaban anataka watu waiangalie wanapoteua viongozi wao, na ndiyo sifa inayowapa watu kuwaamini na kuwapenda. Sura ya kwanza ni fupi; lakini
mwandishi ameitumia kutolea mawazo mengi kuhusu uongozi bora wa watu na utumiaji bora wa ardhi, kuhusu raia, serikali, mawaziri, siasa safi na mifano bora ya viongozi. Sehemu yote iliyosalia-na ni kubwa-anaitumia kutolea mawazo yake kuhusu umma na jinsi ya kuishi kwa mapenzi na ujamaa. Na sura zote kumi na nne zifuatazo, hadi kufikia mwisho, ni maoni juu ya ‘machimbo na hazina zake’, ‘biashara na faida yake’, ‘safari na manufaa yake’, ‘utajiri na Baraka yake’, ‘hali na heshima yake’ na juu ya ndugu, watu, jamaa na matendo yao-mambo yahsuyo dunia nzima. Kwanza kabisa amekwisha kutoa maoni yake kuhusu ardhi na mimea yake na mifugo na mazao yake, kwamba ni hazina za urithi wa watu wote. Hebu basi tuangalie ni nini awazacho mtungaji huyu juu ya ujamaa na upendo kati ya watu. Katika sura ya pili, mwandishi
anatoa maoni yake kuhusu mgeni Ikibali aliyekuwa na hulka ya kuwapendeza watu waliokutana naye na ambaye usoni aling’aa kwa kicheko; na aliyekuwa na fadhila na shukrani. Katika kwenda kwake Janibu, Ikibali anakutana na Adili, Liwali wa mji huo ambaye mtungaji anamtumia kuelezea mawazo yake kuhusu namna nzuri na mbaya ya kuishi na ndugu na watu mbalimbali. Ikibali alipotaka kurudi Ughaibuni, Adili alimwomba akae Janibu kwa muda wa siku tatu zaidi ili wazidi kutafaraji pamoja. Ikibali akakubali, kwani ‘waungwana hawanyimani neno’. Kwa hiyo tunaona vile vile kuwa penye upendo pana kujitolea na subira pia. Twafahamu kwamba subira mara
nyingi huvuta heri, basi Ikibali naye katika kusubiri kwake alivuna heri-na heri yenyewe ilikuwa ni kule kuona kuwa kuna kitu fulani kibaya ambacho ilimlazimu Adili kukitenda bila furaha. Juu ya habari hii ya Adili, Shaaban anatutanabahisha tusimchukulie mtu kwa hali yake ya nje tu, tukafikiri yakuwa mtu kama Adili-Liwali mzima-ati hana jambo linalomuondolea furaha. Mtu kama huyo, tunapogundua ana tatizo, inafaa tumsaidie-si katika mambo ya kikazi tu bali hata mambo yake mwenyewe binafsi. Hii ndiyo sababu Ikibali akaazimia kumsaidia mwenziwe ingawa hilo jambo la kusaidiwa lilikuwa ni la siri: siri ambayo ilibidi ifichuliwe ili msaada upatikane. Ndipo Ikibali akaitoboa siri hiyo, ya Adili na manyani wake, na baadaye akenda naye mbele ya Rai, si kwa ajili ya kumuaibisha bali kumfanya Rai ayasikilize maelezo ambayo huenda yakawa ndio ufunguo wa furaha. ‘Aonae kosa akitoa hana lawama’, ndivyo asemavyo mwandishi. Na kusaidiana ni dalili ya upendo nan i ujamaa. Katika sura ya tatu, mawazo ya
mwandishi ni kuwa vitendo ni mapinduzi. Tunaambiwa kwamba busara nyingi humjia mtu baada ya jambo kufanyika. Hivyo, Adili hakumkasirikia Ikibali kwa kumtolea siri yake kwa Rai. Inaonekana kwamba wazo la mtungaji ni kusema kuwa itukiapo ajabu, au jambo la kushangaza, huenda kukawa na sababu maalumu na kwamba, jambo lenyewe likichunguzwa, huenda sababu yenyewe ikaonekana. Ajabu ya wale manyani waliopanda farasi na kumfanyia mfalme ishara inapochunguliwa ndipo sababu yake inapofahamika. Katika kusikiliza shauri la Adili na manyani kuna wazo kwamba ‘waungwana hawasemi uongo’. Kwa hivyo ingawa Adili ameshtakiwa kwamba anawatesa manyani, tunaona anawageukia manyani wale wale na kuwataka wayathibitishe ayasemayo. Kuhusu malezi ya Hasidi, Mwivu na
Adili, mtungaji atoa wazo kwamba kumlea mtoto ni kumtunza mwili, kumfundisha mawaidha na kuzipanua fikra zake, na zaidi ya yote ni kumfundisha ‘wema’ wa moyoni. Moyo ndio makao ya upendo ambao ndio msingi wa ujamaa. Kuhusu madeni inaonekana kwamba,
ili kutengeneza maisha ya upendo na kujitegemea, kukopa si jambo zuri na kwamba, kama imekuwa lazima kulipa kabla ya kudaiwa. Na yule anayekukopesha naye asiwe na lazima ya kudai kwa kero au inda. Shaaban anamtumia Adili kueleza
kuwa, ingawa yeye alikuwa kitinda mimba, aliweza kuwa na busara na subira zaidi ya wakubwaze. Busara yake ilimfanya afaulu katika biashara kwani aliweka daftari ya mapato, kwa hivyo mali yake haikupotea bila ya kuelewa vile ilivyopotea. Wazo la mtungaji ni kuwa biashara au shamba lahitaji mpango ambao usipokuwepo patapatikana hasara. Kwa kuwa ndugu zake Adili hawakuwa na mpango walifilisika baada ya mwaka mmoja tu. Na hivi ndivyo watu wengi duniani wafanyavyo: hupata mali wakafanyia pupa kwa kutaka kuchuma zaidi bila mpango, mara wakapata hasara. Lakini mtu kuvumilia na kusamehe ndugu zake ndilo jambo linalohitajia, na hapa mtungaji anazidisha sana wazo lake la ukarimu. Kwa ajili ya upendo, Adili aliwagawia tena mali nduguze ili wafanye tena biashara na wajitegemee, wasimnyonye. Katika safari waliyoifanya wote watatu, Shaaban anachukua nafasi ya kueleza faida za safari kwa kusema kuwa safari huleta ‘kufarijika kkatika hamu, kujua namna ya kuendesha maisha, kupata elimu mpya, kuelewa tabia za watu mbalimbali, kukutana na marafiki wa kweli kushinda ndugu, na mtu mwenye bahati mbaya kwao huweza kupata bahati njema ugenini.’ Katika sura ya sita mwandishi
aeleza tena kwamba upendo ndiyo jambo muhimu duniani, kwani Adili ‘aliwapenda ndugu zake kama pumzi ya maisha yake mwenyewe’. Pendo huleta huruma, na huruma hii ndiyo iliyomwezesha Adili kumwokoa yule tandu aliyetaka kuangamizwa na nyoka. Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba jema hulipwa na jema. Yule tandu, ambaye alijigeuza msichana, aliahidi kumlipa wema Adili na akamwombea dua njema. Sura hii inaonesha kwamba ujasiri unatakiwa sana katika kufanya mambo yaonekanayo kuwa magumu. Kwa ujasiri wake, Adili alipata maji, na safari ya pili akajitolea peke yake kwenda mji wa Mawe kutafuta tena maji ya kunywa. Sura ya saba haina mawazo mengi
ya mtungaji ila kusema kwamba duniani kuna mali nyingi lakini ni vigumu mtu kuipata ikiwa amejificha. Watakaoipata ni wale wajasiri tu wenye nia ya kuipata. Sura ifuatayo yasema hivyo hivyo: bahati ya turufu humwendea mchezaji, na ndivyo ilivyokuwa bahati ya Adili, hata sasa akawa na bahati ya kukaribishwa humo mjini na msichana mrembo. Mawazo ya uongozi bora yarudiwa
tena katika sura ya tisa. Katika ukurasa wa 35, tunaelezwa jinsi kiongozi ahitajiwavyo kuwa katika maingiliano yake na watu na vile vile na dini ya kweli ya Mungu. Mrefu alimwangamiza Mfalme Tukufu na enzi yake yote (ila bintiye, Mwelekevu) kwa sababu kiongozi huyo alimdharau Mungu akawa anaamini mizimu na uimamu wa Kabwere. Rehema za Mungu huwafikia wanaomtii, na hivi ndivyo Mwelekevu alivyojaaliwa kukipata kile kitabu kitakatifu pamoja na ule mkomamanga. Mizimu na kutomjali Mungu ni kinyume cha ustawi wa moyo. Maelezo yafuatayo yanahusu wivu. Mtungaji
anatwambia kwa njia hii hii ya hadithi kuwa wivu haufai. Mwenye kupata kitu kwa jasho lake aachwe kufurahia mapato yake. Katika ukurasa wa 40, mtungaji anahubiri juu ya mambo machafu na hila mbovu kama za wale ndugu zake Adili ambao kila mmoja wao aling’ang’ania kutaka kumwoa Mwelekevu na baadaye wakaonelea kuwa yule binti awe mke wa wote-jambo ambalo ni chafu sana. Na hapo ndipo atoapo mawazo yake kuhusu ndoa yenye msingi kamili, kuwa ndoa si jambo la watu wote; ni la watu wawili tu-mume na mke. ‘Mwanamume hakukusudiwa kuwa fahali wa kila mtamba, wala mwanamke kuwatembe wa kila jogoo’. Mafanikio ya Adili yaliwakata maini nduguze, kwa hivyo maoni ya Shaaban hapa ni kwamba watu wafanikiwao ni lazima wawe macho, watahadhari na kijicho wanachoonewa, kwani si watu wote wapendao au wanaofurahia mafanikio yao. Tena nduguze Adili, waliokuwa hawapendi Adili, wakamtosa majini kwa wivu. Tunaoneshwa kuwa, kwa upande mwingine, pendo likitoka upande mmoja tu katika maisha ya ujamaa basi huwa halina msingi imara, na maisha yake huwa si marefu. Pendo lazima litoke pande zote mbili sawa kwa sawa. Adili alitoswa majini lakini ile
dua ya msichana-tandu ikamuokoa. Mtenda mema mara ntingi hulipwa mema, na mtenda mabaya naye pia hupata kadiri ya ule ubaya wake. Basi Adili akapata mali zaidi, na nduguze walio na wivu wakaadhibiwa wakageuzwa manyani na kupigwa mijeledi kila siku. Sura ya kumi na nne na ya mwisho
zaonesha mambo mawili hasa: wajibu wa kiongozi kuwaangalia wafuasi wake kwa shida zao-kama vile Rai alivyojishughulisha kumpatia Adili ushahidi kutoka kwa babake Huria, Kisasi-na mafundisho kuhusu hali ya binadamu na vitendo vyake. Mawazo haya ya Shaaban yasemwa na Rai kuwaambia nduguze Adili: ‘Weavivu walijitahidi kuwa hodari, ilikuwa kinyume hodari kuwa wavivu; kama waovu walitaka kuwa wema, ilichukiza wema kuwa waovu; kama maskini walitafuta utajiri, ilikuwa ujinga matajiri kufuja walichokuwa nacho; kama mbegu kidogo iliongezwa mchanga, ilikuwa uharabu mtu kuua ndugu yake; pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri kutenda maovu.’ Kwa hiyo, ni dhahiri yakuwa
katika Adili na Nduguze Shaaban afundisha watu waishi kwa kupendana chini ya uongozi bora, na wajisaidie kiujamaa badala ya kujiangamiza na kuoneana wivu ambao hauna faida-si kwa hao wenye wivu tu, bali kwa nchi nzima. Vile vile anawaambia wale wenye busara na werevu kwamba dunia ni kubwa na imejaa mali na vitu vizuri ambavyo vitakuwa ni vya kila avitoleaye jasho na mwenye wema moyoni na akili kichwani. Wasifu wa Siti Binti Saad zaidi unaonesha pendo kuliko ujamaa,
lakini kiini chake ni ‘kujitegemea’. Kama Bwana Waziri Juma asemavyo katika dibaji ya kitabu hicho (uk. vii), ni sawa kama mwandishi awatia moyo wasichana na wanawake wengi wa Kiafrika wanaojibidiisha kwa shughuli mbalimbali kwa ajili ya maisha yao. Shaaban Robert ana nia ya kueleza
kwamba ni lazima mtu ajitegemee kwanza ndipo atakapofanikiwa kupata yale ayatakayo. kule kuwa mwanamke, au kutosoma, au kutokuwa na fedha, au kutozaliwa na kukaa mjini, au kutokuwa na sura nzuri, hayo yote si kitu kwani kujiamini, kuwa na nia, na kuwa na subira na juhudi kunaweza kuleta mafanikio mengine makubwa yasiyoweza kufikiriwa hata kidogo hapo mwanzoni. karibu kitabu chote kinazungumza habari za mtu mmoja tu, na hakisemi mengi juu ya watu wengine ila kuonesha tu yakuwa wapo wengine waliomuonea wivu Siti wakastahili kupewa jibu la kuwatia vidaka vya midomo. kwa hivyo inaonekana kwamba maelezo yaliyomo humu ni kama safari ya barabara moja yenye vipingamizi, na mtungaji anaonesha vile msafiri mmoja anavyoendelea na safari yenyewe. na hata huyu msafiri mwenyewe, Siti, ametumiwa na mtungaji ili awe mfano kwa wanawake wengine wanaojidharau na kuona kwamba hakuna lolote hapa duniani wawezalo kulifanya. Lakini hivyo sivyo; ulimwenguni ni mpana. Shaaban Robert anataka kuonesha
kuwa katikati ya vizuizi mtu anaweza kusimama na kufanya kazi kwa bidii hata akajipatia sifa. Siti hakuwa na bahati njema ya kuviepuka ‘vipingamizi’ vile vilivyotajwa hapo juu (kutokuwa na sura nzuri na kadhalika), lakini vivyo alianza safari yake katika maisha. alijua kuwa wazazi wake ni maskini, kwa hivyo aliendelea na biashara yao ya kuuza vyungu. hakuna mtu aliyepata vyote au aliyekosa vyote. Mtumwa-jina la Siti la hapo mwanzo-alikosa sura nzuri, lakini alifadhiliwa sauti ya kuvutia kweli kweli. Fimbo iliyo mkononi ndiyo iuayo nyoka; kwa hivyo Siti aliifanya sauti yake ndiyo fimbo yake, na akaitumia vilivyo. Hapa Shaaban anachukua nafasi ya kutueleza kuwa sura nzuri si kitu cha kukiangalia sana maishani mara kwa mara, wala si kizima kiu cha mapenzi. Mawazo yake ni kuwa inambidi mtu aikubali hali yake kwanza, kisha ndipo atakapoweza kuona ni wapi anapofaa ili aweze kufanya jambo atakalo kwa kadiri ya uwezo wake. na haya yote yawezekana, si ya ajabu. Lakini, katika kukata shauri juu
ya jambo la kutekeleza, mtu mara nyingi humbidi kuyatoa mhanga mambo yake fulani aliyokuwa nayo kama vile Siti ilivyombidi kukiacha kijiji chao Fumba, mumewe, mtoto wake na maisha ya utulivu yasiyo na ghasia, akakata shauri kukidhihirisha kipawa chake kwa kuimba katika taarab mjini Unguja. Alihitajia sana subira, juhudi, kujiamini na kujitegemea katika maisha mapya ya mjini yaliyokuwa na vipingamizi vingi. kimojawapo cha vipingamizi hivyo kilikuwa ni kushindwa kuimba siku ya kwanza alipotokea hadharani. Alikuwa hajazoea. Lakini baadaye alifaulu kwani ‘alishikilia kazi yake kwa bidii’, akawa na dhamira na nia ya kufaulu. Kipawa bila ya ujasiri, dhamira
na nia ni bure tu. Maisha ya mjini ni magumu na hasa kwa mwanamke ambaye ni mgeni tena ni mtu mzima ambaye hapo alipokuwapo hakuwa na mume. Lakini Siti hakuwa muhuni. Aliweza kukaa imara kwani alikwenda mjini kwa kusudi maalumu; na palimfaa kwalo. Hakwenda mjini kutafuta fedha, kwani tunaambiwa yakuwa Siti hakupenda fedha, lakini kazi yake ilikusudiwa kumletea sifa na umaarufu. Hakuwa mnyang’anya watu fedha kwa sababu ‘alikuwa mcha Mungu wa sala na saumu. Alisali vipindi vitano kila siku, akafunga faradhi na suna katika maisha yake yote’. Maoni ya mwandishi hapa ni kuwa mtu awe wa ibada saa za ibada, na mlimwengu wakati wa mambo ya kilimwengu. Pia inaonekana mwandishi
anafikiri kwamba Siti alifanikiwa kwa sababu ya ukarimu wake na Baraka kuliko kuwa ni kwa sababu ya masharti ya mikataba na mapatano katika kazi yake. Mafanikio, kwa wale wajuao wayafanyayo ni kama moto wa mbugani. Mara watu wakawa wanamfuatafuata Siti, watribu wakamzunguka kwa vinanda ili awaimbie, wapiga picha na wapiga chapa nao wakamwendea, watu wa santuri pia wakawa wanamfuata, na kwa njia hii sifa za mwanamke huyu zikatapakaa hata nje ya Afrika Mashariki. Mafanikio mengi ya Siti, asema Shaaban, ni kwa sababu alikuwa mtanashati, hana majivuno, mwenye adabu na mlahaka kwa watu wote. Ni kweli kabisa kwamba ‘jina
kubwa lolote halipatikani duniani bila vizuizi kadha wa kadha’ kwa maana kuna mfano wa Siti ambaye, mara tu alipoanza kupata sifa kwa kuimba, watu walianza kumwonea wivu na kumdharau na hata kumtukana. Kuhusu mambo haya yote, maoni ya mwandishi ni haya: mtu lazima awe na subira, bidii na uvumilivu katika kazi yake; aende mbele bila ya kuangalia nyuma. Safari ya Siti katika maisha
Si hoja uzuri, na sura jamaliilifanikiwa kwa ramani ya maneno. Mwenye busara hujiwekea maneno ya kumwongoza. Katika kuwajibu waliokuwa wakimtia ila na kumtukana, Siti alisema: Kuwa mtukufu, na jadi kubeli Hasara ya mtu, kukosa akili Huu ndio wimbo uliowakomesha
wapinzani wake. Na yaonesha kwamba mtu yambidi kujitetea anaposhambuliwa na binadamu wenziwe, lakini si kujitetea kishenzi kama mnyama wa porini. Kama kawaida, mwandishi
anajiuliza kwa nini Siti alifanikiwa hivyo? Maoni yake ni kwamba, kwanza, Siti alifahamu sana tabia za watu, alikuwa na adabu na alijua kuchukuana nao (wazo lililomo katika kitabu cha Adili na Nduguze pia); na pili aliwapenda sana wasikilizaji wake. Hapa upendo waonekana kuwa ndio msingi wa mafanikio. Hata hivyo, Siti hakujisifu mwenyewe. Baada ya kueleza kwamba Siti
alizidi kusonga mbele, na kuviruka vipingamizi vingi, mwandishi anatoa mawazo yake kwamba hayo hayakuwa mambo ya ajabu; matendo yake yanaweza kuigwa. Siti alikuwa ni mtu kama watu wengine. Katika ukurasa wa 49 yapo mawazo mazuri ya Shaaban yanayosema: ‘Fikiri kama na wewe umepata
kutenda neno lolote la fadhili kwa watu au nchi yako. Kama hujalifanya bado, lifanye sasa. Yamkini una marafiki. Wafurahishe kwa fadhili yoyote uwezayo kutenda. Haikosi una washindani. Wape sababu ya kukuajabia kwa unyofu ulio nao….Maisha yalikuwa matendo, sio usingizi’. Tangu mwanzo mpaka mwisho wa sura
ya nane Shaaban ameacha kutuzungumzia mtu wake. Hapa anasimama na kutoa mawazo yake juu ya jambo moja muhimu sana kwa wanaadamu. Nalo ni tabia njema. Anasema tabia njema imo katika ukweli na mapenzi ya moyoni. Tabia njema haifuati elimu, wala utajiri, wala kuwa na cheo. ‘Tabia ilikuwa kama njia panda kuu katika maisha yaliyogawa watu kwenda pande mbalimbali za dunia.’ Watu hutengana kadiri ya tabia. Hata Mungu anawagawa watu kwa kufuata tabia zao. Ni vizuri kuwa na tabia nzuri ambayo Shaaban Robert anafikiri ina amani na upole, saburi na unyenyekevu, uungwana na uaminifu kwa watu wote-hiyo ni johari. Mwandishi anahubiri juu ya tabia njema itakiwayo, akitoa mfano wa Siti, na anamalizia kitabu chake vizuri sana kwa kutaja waziwazi kiini hasa cha mawazo na maoni yake juu ya maisha. Kama nilivyosema hapo awali,
Shaaban Robert katika Wasifu wa Siti Binti Saad anaonesha jinsi mtu, hata akiwa katika hali ya chini, awezavyo kujitahidi hadi akaweza kustawi na kujitegemea. Sura ya mwisho inatilia mkazo neno kuu la kitabu hiki, ‘kujitegemea’. ‘Kujikimu ni kujiruzuku. Kujiruzuku ni kujitegemea kwa chakula, nguo na masurufu mengine katika maisha.’ Na hapa ndipo tutakapokomea kutoa mawazo ya mtungaji wa kitabu hiki. Baada ya kuhakiki Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, na pia nikiyapima mawazo ya marehemu
Shaaban Robert katika fasihi zake nyingine kama mashairi yake Masomo Yenye Adili, Kusadikika, na Kufikirika, naona vigumu sana kuuepa ukweli kwamba marehemu aliandika vitabu vyake kwa nia ya kufundisha watu; alitoa fasihi yake iwe kioo cha watu kujiangalia ili waone jinsi wanavyoishi na wanavyotaka kusihi, na vile vile waone jinsi ambavyo yeye mwenyewe Shaaban Robert angependelea watu waishi. Kwa sababu hii, maandishi yake yote yanang’aa kwa ilani isemayo, ‘Maisha ya mtu ni msingi wa maendeleo ya nchi.’ Maneno haya ndiyo ufunguo uliomo mwanzoni kabisa mwa Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini-kitabu ambacho kwacho Shaaban ametueleza na kutuonesha sehemu ya maisha yake. |