Kongamano la safari hii liliwakutanisha washiriki kutoka Tanzania, Kenya, Msumbiji, Rwanda, Ghana, Ujerumani, Italia, Marekani, Uingereza, Austria na Ufaransa. Jumla ya mada hamsini ziliwasilishwa na kujadiliwa.
Profesa Ken Walibora, aliyekuwa miongoni mwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili waliohudhuria kongamno la Bayreuth
Kongamano la siku tatu la kimataifa juu ya taaluma za Kiswahili limemalizika mchana wa leo (02.06.2015) katika mji wa Bayreuth, kusini mwa Ujerumani. Wataalamu na washiriki kutoka zaidi ya mataifa na vyuo vikuu 20 ulimwenguni wameazimia haja ya kuunganisha nguvu kukipa Kiswahili uthubutu na nafasi yake kinachostahiki kwenye ulimwengu wa sasa kwani tayari kimejipambanua chenyewe kuwa lugha inayoliwakilisha na kulisemea bara zima la Afrika.
Mohammed Khelef ambaye amekuwa akihuhudhuria kongamano hilo, ametutumia taarifa ifuatayo kutoka Bayreuth.
Kusikiliza ripoti bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.
Kongamano la kumi na tano liliandaliwa chini ya kichwa “Kiswahili, Uwiano, Utangamano na Maendeleo” katika ukumbi wa Chuo cha Kenyatta, mnamo tarehe 23 na 24 Agosti, 2012 mjini Niarobi, Kenya.
Wengine walionekana wametumbua macho wakimtazama mhutubiaji lakini walionyesha hawakuwa wakielewa kile kilichokuwa kikisemwa na wengine walionekana wakiondoka kabisa kwenye mkutano. Nilipowauliza kwa nini walisema wamechoshwa na mhutubiaji kwa sababu haieleweki anazungumzia nini.
Na. ABEID H SAKARA
Siku moja nilikwenda kwenye mkutano fulani uliojaa ukumbi mzima. Niliona mambo ya kushangaza. Kwanza, watu wengi katika ukumbi hawakuwa wakisikiliza hotuba kwa makini. Baadhi ya watu walikuwa wakiongea mambo yao bila kujali aliyokuwa akisema mhutubiaji.
Wengine walionekana wametumbua macho wakimtazama mhutubiaji lakini walionyesha hawakuwa wakielewa kile kilichokuwa kikisemwa na wengine walionekana wakiondoka kabisa kwenye mkutano. Nilipowauliza kwa nini walisema wamechoshwa na mhutubiaji kwa sababu haieleweki anazungumzia nini.
Kila nilipomtazama mhutubiaji nilimuona amekazana kusema hadi mishipa ya shingo ilionekana imetoka na jasho lilikuwa likimtiririka. Wakati mwingine alionekana akishangaa alipowaona baadhi ya wasikilizaji wake wakiongea mambo yao wala hawamsikilizi. Alisikitika alipoona baadhi ya watu wakiondoka mmoja mmoja kwenye mkutano. Kwa hakika alionekana amefadhaika na kukata tamaa.
Jambo kama hili linaweza kumtokea mtu yetote anapoamua kuhutubia watu bila kufanya maandalizi . Hususan, asipozingatia kanuni ambazo huwafanya watu wavutiwe na hotuba yake. Je, wewe katika maisha yako umewahi kuhutubia watu? Kama umewahi, hotuba yako iliwavutia wasikilizaji? Kama haikuwavutia usiwe na shaka. Katika makala haya tutataja baadhi ya kanuni ambazo tunaamini zikizingatiwa husaidia kufanya hotuba iwe na mvuto kwa wasikilizaji.
Maandalizi ya hotuba
Kuna baadhi ya watu huamini kuwa maadhali mtu anajua lugha na ni msemaji hodari hana haja ya kufanya maandalizi kabla ya kwenda kuhutubia. Kuna wengine maandalizi yao huwa kuiandika hotuba yote na kuisoma mbele ya watu kama ambavyo viongozi wengi huwa wakifanya. Wao huandikiwa kwa sababu wanayoyasema mara nyingi huwa ni sera au miongozo ambayo baadaye hutakiwa kutekelezwa. Hivyo, lugha inayotumika katika hotuba zao huwa ndiyo miongozo itakayotumika kwa utekelezaji.
Lakini mtu anapotoa hotuba kwa kuisoma mara nyingi huwafanya wasikilizaji wake wakinai na wahisi kama wanapoteza wakati wao.
Hotuba ya namna hii huwachosha wasikilizaji kwa kuwa anayeitoa huwa hawezi kuibadili au kuirekebisha kufuatana na hali ya mwitiko wa wasikilizaji. Tena huwa hawezi mathalani kurudia sehemu ambayo wasikilizaji wake wanaonekana dhahiri hawakuielewa vyema. Wengine huamua kaikariri hotuba na kuiwasilisha kwa hadhira kama shairi ama wimbo. Mtindo huu ndiyo haufai kabisa.
Hotuba iliyokaririwa inapotolewa mbele ya kadhira muundo wake kuonekana wa kirasimu zaidi kama lugha ya kisheria.
Tunaposoma hotuba tunapoteza au tunapunguza mawasiliano ya uso kwa uso baina ya mtoa ujumbe na mpokea ujumbe hali ambayo ni muhimu katika mawasiliano. Hivyo hotuba nzuri na inayoweza kuwa na taathira kubwa kwa wasikilizaji ni ile ambayo mhutubiaji anaitoa mbele ya hadhira yake huku akiwatazama.
Wakati huohuo akiweza kujirekebisha kwa sauti au maudhui na hata mtindo wa kuitoa hotuba kufuatana na jinsi inavyopokewa na wasikilizaji.
Hata hivyo, tunaposema asiiandike hatuna maana azungumze bila kufanya maandalizi yoyote. Kuna hatua tatu kuu ambazo ni muhimu katika kuandaa hotuba ambazo ni kutafuta na kuainisha maudhui au taarifa atakazozizungumzia.
Hatua ya pili ni kuamua mpangilio mzuri wa maudhui na hatua ya mwisho ni kuandaa hotuba yenyewe tangu mwanzo hadi mwisho.
Vilevile ni muhimu kuandaa muhtasari wa vipengele utakaomwongoza mtu anapotoa hotuba.
Kudumisha mawasiliano ya ana kwa ana
Wasikilizaji wa hotuba hujisikia vizuri wanapomuona mtoa hotuba anaonekana kama anayezungumza na kila mmoja wao binafsi. Kumbuka, hakuna kitu kinachomfanya mtu akusikilize vizuri kama unapozungumza huku akimtazama yeye moja kwa moja. Ingawa unapotoa hotuba mbele ya hadhara huwezi kumtazama kila mmoja, kuna njia inayoweza kukusaidia kuwafanya wasikilizaji wajihisi kama unawatazama wote.
Chagua mtu mmoja katika kila upande wa ukumbi au uwanja na uwe ukiongea huku ukiwatazama watu hao mara kwa mara. Usiendelee kumtazama mtu mmoja kwa muda mrefu.
Kila baada ya sekunde chache hamia kwa mtu mwingine na endelea vivyo hivyo ukielekea kila upande kwa zamu hadi mwisho wa hotuba yako. Kila unapomtazama mtu uliyemchagua katika upande fulani watu wa upande ule watakuona kama unawatazama wote.
Tumia ishara
Mtu anayetoa hotuba huku akitumia ishara ili kusisitiza maneno anayosema huwavutia wasikilizaji. Ishara za makusudi za uso na vitendo vinavyowezwa kufanywa kwa kichwa, mabega na mikono, vinaweza kutumika ili kusisitiza kile ambacho msikilizaji anataka wasikilizaji wake waielewe vyema. Hata hivyo, ni vyema kuepuka kutumia ishara kwa kuwa huweza kumchanganya msikilizaji au kumfanya mtoa hutoba kuonekana kituko.
Sauti
Unapotoa hotuba tumia sauti inayoweza kusikika vyema kwa wasikilizaji isiwe ya kupayuka wala ndogo zaidi.
Utaweza kutambua kama sauti yako inasikika vizuri pande zote kwa kutazama nyuso za wasikilizaji. Kama unaeleza kuhusu jambo la kuchekesha utawaona wanatabasamu ama kucheka na kama unazungumzia jambo la kusikitisha utaona nyuso za huzuni.
Kila mara watazame wale walio mbali kabisa kutoka kwako ili kuhakikisha kama hotuba inasikika.
Licha ya kuhakikisha unasikika, huna budi kuhakikisha unatumia matamshi sahihi ya maneno.
Pia lazima udhibiti kasi yako ya kuongea. Usiongee kwa kasi. Ongea taratibu zaidi unaposisitiza jambo fulani. Vile vile usiongee moja kwa moja bila kutulia kila baada ya muda. Vipindi vya kupumzika kusema katikati ya hotuba humsaidia msikilizaji wako kutafakari na kukifanya ulichosema kingine vyema akilini.
Lugha
Hotuba yenye maneno mengi ambayo wasikilizaji hawayafahamu, siyo tu kuwafanya wasielewe habari inayosemwa bali huweza pia kuwafanya wasiwe na ari ya kuendelea kuisikiliza.
Mtoa hotuba hana budi kuhakikisha anatumia lugha nyepesi na inayoeleka. Ni lazima utumie maneno na miundo ya lugha iliyozoeleka katika kundi la watu analohutubia.
Hitimisho
Tumebaini kuwa kutoa hotuba mbele ya watu na ikaeleweka siyo suala la kuvaa vizuri na kusimama mbele ya watu na kusema kile unachotaka waelewe.
Kuwafanya wasikilizaji waelewe hotuba yako ni suala linalohitaji umakini mkubwa unaoanzia tangu katika kipindi cha kabla ya kusimama mbele ya watu hadi kipindi cha kutoa hotuba yenyewe.
Hili ndilo suali linalotukabili na tuliloulizwa tulijibu, ili ieleweke hasa iwapo katika hizi zama zetu je, ni kweli kwamba malenga tunao au la?
Nami nilichukuwa dhamana ya kwamba nitalijibu ila nimechelewa kwa kuwa na mimi pia ilikuwa pindi ni mpaka nitafutetafute na niulizeulize kutoka kwa wazee wetu huku.
Suala hili limeonekana kuwa na uzito wa kiasi kwani iwapo twatakiwa kueleza hasa huyu malenga ni mtu wa namna gani basi hatupaswi kujibu tu, ila ni mpaka pia tuchimbe na tuingie ndani kwa kina.
Inavyosemekana na kuaminika miongoni mwa wenyeji ni kwamba Malenga ni mtunzi aliye kwasika na stadi wa mashairi na nyimbo.
Utunzi wa mashairi na nyimbo kamwe haujawa ni jambo la rahisi na ndipo ikawa wale waliyopatikana kuwa ni wajuzi wa hayo, mara nyingi walikuwa sio wengi ijapokuwa kwenye kutizama tunaona ya kwamba wapo chungu nzima hao wenye kuandika na kutunga mashairi na nyimbo.
Katika jamii ya Waswahili utunzi wa mashairi unahesabika kuwa ni katika mojawapo ya kunga kuu za lugha, yaani ni siri iliyomuhitaji mpaka mtu apate fundi na mwalimu wa kumfunza na kumwezesha ili naye apate kufaulu hadi akaitwa fundi na malenga.
Tukitizama hivi leo tutaona ya kwamba ushairi kama usanii, fani au kunga basi huwa ni sharti mtunzi awe na kipawa maalum, pamoja na ujuzi na maarifa mengi ambayo bila shaka atakiwa awe ameyapata katika kipindi cha muda mrefu baada ya kufunzwa au kujifunza na kujifanyia mazoezi ya mara kwa mara yeye mwenyewe.
Hii ndiyo ikawa sababu ya kwamba, pindi likiandikwa, basi shairi huhitaji kuchambuliwa maana, mawazo na matumizi ya lugha.
Katika baadhi ya kunga za ushairi zinazoshikiliwa mojawapo ni kwamba mshairi awe na uwezo wa kutumia maneno yasiyokuwa ya kawaida, na hata akiyatumia yale ya kawaida basi aweze pia kuyapa maana yasiyo ya kawaida, huko ndiko tunakokuita kuyapa koo maneno. Tena iwe kwa maneno machache apate kuvyaza hisi, maana na nahau yenye kina kirefu.
Ujuzi kama huu humuhitaji mshairi pia awe ni mwenye kuufahamu vilivyo msamiati wa lugha ya Kiswahili na maana yake ili asipungukiwe na maneno ya kutosheleza katika kutunga kwake.
Mshairi anatakiwa pia awe na uwezo wa kutumia kipawa chake ili aweze kuwakenga na kuwatinga akili wasikilizaji au wasomaji wake, ingawaje iwe haja yake ni kuyafichua mawazo yaliyomsonga katika dhati ya moyo wake. Tena yawe ni yenye kumtoka kwa tabia pasipo kuwa na kujilazimisha, awe ni mtu anayeweza kuzibadilisha na kuzielekeza akili, fikra na nyoyo za watu kule kutakikaniwako wafuate.
Ilivyokuwa ushairi wa Kiswahili ni kunga, basi wengi walikuwa wakienda kwa hao mafundi wa kutunga ili wakafundishwe nao wawe wajuzi nayo pia.
Sijui kwa kule pande nyengine walioko Waswahili wa yale makabila mengine lakini katika hizi sehemu za kwetu huku kama Malindi, Lamu, Pate na Mombasa (Mvita) ulikuwepo mpango maalum wa kuwatambua washairi na watunzi kulingana na daraja zao walizokuwa.
1. Kwa Wa-Pate walianzia pa:
i. Mwanafundi.
ii. Mshairi.
iii. Jimbi.
iv. Shaha.
v. Shaha wa mashaha.
2. Wa –Amu:
i. Mwanafundi.
ii. Mshairi.
iii. Fundizi.
iv. Shaha.
v. Shaha wa mashaha (mke/mume)
3. Wa-Mvita:
i. Mwanafundi.
ii. Mshairi.
iii. Malenga.
iv. Shaha.
Kitakiwacho tukijuwe hapa ni kwamba hivi leo takriban katika wenzi wetu tungali tuko hapo kwenye daraja ile ya U-Mwanafundi na Mshairi. Aghalabu mtu kuitwa Malenga na Shaha au Sha wa mashaha ilikuwa ni mpaka kuwepo na jopo la kumtawazisha yeye cheo hicho, tena si kwa kuwa ni mtunzi tu, ila na pia awe ameweza kukaa katika mashindano na akawapiku washairi wengine kama yeye. Haya yalikuwa ni mambo yaliyofanywa mbele ya hadhira na kukiwekwa malumbano ya magwiji mbali mbali na mara nyingine wakitoka pia sehemu nyengine za Uswahilini ili kuja kupambana.
Ningependa kueleza pia ni kwa nini hasa magwiji kama akina Sheikh Shaaban Bin Robert, Mathias Mnyapala na wengineo ijapo kuwa wao walikuwa wameandika tumbi na chungu za vitabu na diwani pengine hawakuwahi kupawa tuzo hizo za malenga.
Sababu ya kwanza ilikuwa ni kwamba ushairi ni kunga iliyohitaji ufundi na kutawazwa umalenga kulitokana hasa na jamii ya Waswahili wa kule Mshairi alikotoka. Wa – Amu, Wa – Pate, Wa – Mvita walikuwa wakiwatawaza watunzi na washairi umalenga kulingana na mila na dasturi zao, kwa hivyo iliwajibika moja wapo ya sharia zao ni kwamba huyo atakayetawazwa basi awe ni mwenyeji wa jamii hiyo, pili awe na uwezo wa kutunga kwa lahaja safi ya Waswahili wenyeji wa hapo.
Mashairi mengi ya akina Shaaban Bin Robert, Mnyapala na wengineo yalikuwa kweli ni kwa Kiswahili lakini wao hawakuwa na uwezo au pengine hawakutaka kuzitumia zile lahaja zitakikaniwazo.
Ushahidi wa hayo upo kwa kutizama wale waliotuzwa tuzo za umalenga hasa, Malenga wa Mvita, Malenga wa Vumba, Malenga wa Tumbatu, na Malenga wa Mrima. Wote hao walitumia lahaja zao kutoa diwani zao.
Hatimaye suali tuloulizwa lilikuwa na je, hivi leo kunawezekana kupatikana Malenga?
Suala hilo nitawajibu tu kwa kuwaambia malenga kupatikana upo uwezekano lakini ni katika watu wachache, nao ni wale ambao hadi leo wanaandika wakitumia lahaja safi katika tungo zao. Hawa si uwongo, wako washairi wanaopatikana katika sehemu kama vile za Lamu, Malindi na hata Mvita (Mombasa) wanaoandika kwa lahaja za kwao.
Na pengine nitaulizwa basi ni kwanini iwe hivyo na wapo wanaoandika wakitumia lahaja hata humu? Jawabu nitawaambia ni kwa kuwa wengi wetu ni kuwa twajaribu tu.
Hao wanaoandika wakisema wametumia lahaja wengi wetu tunachanganya na pengine hata hatujui wala hatujielewi ipi ni ipi katika lahaja hizo tunazotumia. Tumezisikia, tukazizowea na kuziandika ila tumechanganya tukaweka mkorogo wa lugha na maneno tukidai tumeandika kwa lahaja.
Ni afadhali kuandika kwa Kiswahili cha sawa sawa ukaweza kueleweka na kuthibitika kuliko kuandika na usijifahamu hata wewe mwenyewe kile ulichokiandika.
Marehemu Mwalimu Omar yeye mwenyewe akikataa kuitwa malenga, na sababu zilikuwa ni kama hizi. Kiswahili cha lahaja ni kigumu na chataka mzoefu na mtu mjuzi wa lahaja hizo.
Ushairi una arudhi na namna zake pia, nazo pia nyengine hazifuatwi sawa sawa siku hizi. Hizi inkisari na mazida tusemayo, twajiandikia na kujiamulia pasina kuzingatia iwapo kuna maneno ya kubadilisha au haja ya kupunguza.
Siku hizi ambapo ushairi umegeuzwa kuwa ni taaluma ya kufundishwa shuleni, basi pia kumekosekana mafundi wanaoyajuwa hayo. Walimu watafundisha walivyosomeshwa wao na kwengine jinsi ilivyoandikwa katika vitabu vyao ila pasipo ufahamu mzuri wala mwelekezi. Hakuna mwenye ujuzi na mambo ya ushairi kwa kina pamoja na sharia zake.
Minyambuo watu wanaiweka ya ki-namna namna mpaka maneno yao yakawa hayaeleweki. Watu hunyambuwa pale patakikaniwapo na pale paonekaniwapo labda vina havilingani bali ni lazima kuwe na mbinu, sio vivi hivi tu.
Sio kila neno laweza kunyambulika na sio kila neno laweza pia kupunguzwa, sheria lazima zifuatwe. Akomeapo mwenyeji na mgeni koma papo,
Aliondokea kima akafanya urafiki na papa. Pana mti mkubwa, jina lake mkuyu, umeota katika kilindi, matawi yake nussu yako mjini, na nussu yako baharini. Yule kima kulla siku kwenda akila kuyu, na yule rafiki yake papa huwapo chini ya mti. Humwambia, utupie nami rafiki yangu vyakula; humtupia siku nyingi na miezi mingi.
Hatta siku hiyo papa akamwambia kima, fathili zako nyingi, nataka twende kwetu nikakulipe fathili. Kima akamjibu, ntakwendaje, nasi hatuingii majini, nyama wa barra. Akamwambia, ntakuchukua, tone la maji lisikupate. Akamwambia, twende.
Wakaenda zao hatta nussu ya njia. Papa akamwambia, rafiki yangu weye, ntakwambia kweli. Akamwambia, niambie. Akamwambia, huko kwetu tunakokwenda, Sultani wetu hawezi sana, na dawa tumeambiwa ni moyo wa kima. Kima akamjibu, hukufanya vema usiniambie kulekule. Papa akamwuliza, ginsi gani?
Akafikiri kima akaona, nimekwisha kufa; sasa ntanena uwongo, labuda utanifaa.
Papa akamwuliza, umenyamaza huneni? Akamwambia, sina la kunena, kwani usiniambie kulekule, nikapata kuchukua moyo wangu. Papa akamwuliza, hapa, kunao moyo wako?
Huna khabari yetu? Sisi tukitembea mioyo yetu huacha mitini tukatembea viwiliwili tu, wallakini hutanisadiki, utaniambia nimeogopa, sasa twende zetu hatta huko kwenu, ukanichinje kama utauona moyo wangu.
Papa akasadiki, akamwambia kima, turudi sasa, ukatwae moyo wako. Kima akamwambia, sikubali, ela twende kwenu. Akamwambia, turudi kwanza ukatwae moyo wako, tupate kuenenda.
Kima akawaza ni heri kumfuata hatta mtini, akili nnayo mwenyewe nikiisha fika. Wakaenda wakarudi hatta mtini, akapanda juu yule kima akamwambia, ningoje hapa, papa, naenda twaa moyo wangu, tupate kwenda zetu.
Akapanda mtini akakaa kitako kimya. Papa akamwita. Akanyamaza. Akamwita tena. Akamwambia, twende zetu. Kima akamjibu, twende wapi? Akamwambia, twende kwetu. Akamwambia, una wazimo? Papa akamwuliza, ginsi gani? Kima akamwambia, umenifanya punda wa dobi? Papa akamwuliza kima, ginsi gani punda wa dobi? Akamwambia, Ndiye hana moyo, wala hana mashikio. Papa akamwuliza, ginsi gani kisa cha punda wa dobi? Nambie, rafiki yangu, nipate kujua maana.
Akamwambia, Dobi alikuwa na punda wake, akimpenda sana mwenyewe. Akakimbia punda akaingia mwituni siku nyingi, hatta akamsahao mwenyewe dobi. Akanenepa sana kule mwituni.
Sungura akaondoka, akaenda mwituni, akamwona punda, na yule punda mke. Akamwambia, nimetumwa kuja kukuposa. Na nani? akamwuliza. Akamwambia, na simba. Akakubali, akafurahi sana punda. Akamwambia, Twende zetu, bass.
Wakaenda zao, hatta wakafika kwa simba. Akawakaribisha simba. Wakakaa kitako. Sungura akamkonyeza simba, akamwambia, nyama yako hiyo imekwisha kuja, nami naondoka. Akamwambia punda, nnakwenda chooni mimi, zumgumzeni hapo na mumeo.
Simba akamrukia, wakapigana, akapigwa sana simba kwa mateke, naye akampiga makucha mengi. Akaangusha simba akakimbia punda, akaenda zake mwituni. Akaja sungura, akamwambia, Je! simba, umempata? Akamwambia, sikumpata, amenipiga kwa mateke amekwenda zake, na mimi nimemtia madonda mengi, sababu sina nguvu. Sungura akamwambia simba, tulia we.
Wakakaa siku nyingi, hatta punda akapona madonda yale, na simba akapata nguvu sana. Akaenda sungura kwa simba, akamwambia, waonaje sasa, nikuletee nyama yako? Akamwambia, kaniletea ntaikata vipande viwili.
Akaenda sungura mwituni. Punda akamkaribisha sungura, akamwuliza khabari. Akamwambia, na mchumba wako anakwita. Punda akamwambia, siku ile umenipeleka, amenipiga sana kwa makucha, naogopa sasa. Akamwambia, hapana neno yalio ndio mazumgumzo ya simba. Akamwambia, twende zetu, bass.
Wakaenda hatta wakafika. Simba alipomwona tu, akamrukia akamkata vipande viwili.
Hatta sungura alipokuja, akamwambia, chukua nyama hiyo ukaoke, wallakini sitaki kitu mimi, ela moyo na mashikio ya punda. Sungura akamwambia, marahaba. Akaenda akaoka nyama mahala mbali, simba hamwoni. Akatwaa moyo ule na mashikio akala yeye sungura, hatta akashiba. Na nyama ngine akaziweka.
Akaja simba, akamwambia, niletee moyo na mashikio. Akamwambia, yako wapi? Simba akamwuliza, kwa nini? Akamwambia, huyu punda wa dobi, huna khabari? Akamwambia, ginsi gani kutoa kuwa na moyo na mashikio? Akamwambia, wewe simba mtu mzima hayakuelei? Kama ana moyo huyu na mashikio, angalikuja tena hapa? Kwani marra ya kwanza amekuja akaona atakuuawa, akakimbia, marra ya pili amekuja tena, bassi kama ana moyo angalikuja? Simba akamwambia, kweli maneno yako.
Bassi kima akamwambia papa, nawe wataka unifanye mimi punda wa dobi, shika njia wende zako kwenu, mimi hunipati tena, na urafiki wetu umekwisha.
Kua heri.
—– 1. Umejifunza Nini Kwenye Simulizi Hii! 2. Nini maana ya neno Usiwe kama Punda wa Dobi?
SWALI: Kujadili historia ya tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania tangu kuanza kwake hadi hivi sasa.
Maana ya tamthilia
Tamthilia ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo (TUKI, 2004).
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa tamthilia ni utungo au mchezo wa kuigiza matendo au mawazo fulani yaliyopo katika jamii, ambapo huwa ni majibizano baina ya watu wawili au zaidi.
Historia ya tamthilia nchini Tanzania
Historia ya tamthilia nchini Tanzania inaelezwa kwa kurejelea vipindi vitatu yaani kabla, wakati na baada ya ukoloni.
Kabla ya ukoloni
Kwa mujibu wa Mulokozi (1996:203), katika kitabu chake cha “Fasihi ya Kiswahili”, anaeleza kuwa kabla ya ukoloni tamthiliya zilizoandikwa ili ziigizwe jukwaani hazikuwepo , badala yake, zilikuwepo tamthiliya zisizoandikwa, zilizogezwa au kufaraguzwa kwa ajili ya kuonyeshwa kwenye shughuli maalumu, kwa mfano sherehe za jando na unyago, mazishi, kutawazwa kwa Mtemi, arusi na michezo ya watoto. Tamthilia hizo zilikuwa na sifa kadha za tamthilia yaani hadithi, vitendo, wahusika na waigizaji wao na dayolojia. Hata hivyo tamthilia hizo hazikuwepo na ploti ya K – Aristotle wala matini yaliyoandikwa na kuwa tamthilia simulizi.
Mfano mzuri wa tamthilia hizo awali ni maigizo ya watoto wakati wanapocheza mfano A, B, C na D ambapo A huwa ni baba, B huwa ni mama na C na D huwa ni watoto ambao ni msichana na mvulana ambapo mchezo huanza kwa A kumwambia B aandae chakula, B hufanya hivyo na C anakwenda kuchota maji mtoni na D anapeleka mbuzi malishoni”.
Hivyo basi kabla ya ukoloni hakukuwa na tamthilia zilizoandikwa ili ziigizwe badada yake kulikuwa na sanaa za maonyesho ambazo zilikuwa zikitumika katika shughuli maalumu mfano sherehe, michezo ya watoto wadogo pamoja na jando na unyago.
Kipindi cha ukoloni, (1890 – 1960’s)
Katika kipindi hiki jamiii nyingi za Kiafrika (Tanzania), zilikuwa zikitawaliwa na watawala kutoka nchi za Kimagharibi. Hivyo basi kazi ya tamthilia iliegemea katika utawala wa kikoloni na kupelekea kuibuka aina kuu mbili za tamthilia mpya (zisizokuwa za kijadi) yaani hazikuwa na utamaduni wa Kiswahili ambazo ni tamthilia za Kizungu na tamthilia za vichekesho. Mnamo mwishoni mwa miaka 1950 paliongezeka aina nyingine ya tamthilia ambayo ni tamthilia ya Kiswahili na kupelekea kufikia idadi kuwa tatu (Mulokozi 1996:204).
Tamthilia za Kizungu
Tamthilia hizi ni tamthilia ambazo ziliandikwa kwa lugha ya kizungu (Kiingereza) na zilizojikita katika utamaduni wa kizungu. Lengo kuu za tamthilia hizi zilikuwa ni kuburudisha Maofisa na Masetla wa Kizungu ama kufunza Biblia na imani ya Kikristo.
Katika Tanzania tamthilia za Kiingereza zilianza kuingizwa miaka ya 1920, nyingi zilichezwa mashuleni na zilitungwa na Waingereza, kwa mfano Shakespare na baadhi zilikuwa ni za dini ya Kikristo. Tamthilia hizi zilikuwa zikiunga mkono mfumo wa ubepari na ukoloni. Vilevile katika kipindi hiki kulikuwa na tamthilia chache sana zilizotafsiriwa kwa Kiswahili. Mfano tamthilia ya “Moliere Le Medecin Malge Lui” (Kifaransa “Tabibu Asiyependa Utabibu” (Kiswahili) iliyoandikwa na Morrison 1945 na kuchapwa na E.A.S huko Nairobi.
Baadaye katika kipindi hiki viliibuka vikundi viwili vya kuigiza, ambavyo ni Dar es salaam players mwaka 1947 na Arusha Little Theatre mwaka 1953. Kuanzia wakati huo tamthilia ya Kiswahili ilianza kuhusishwa katika mashindano na hivyo kuchochea utunzi wa tamthilia ya Kiswahili.
Vichekesho
Ni aina ya tamthilia – gezwa zilizotungwa papo kwa papo bila ya kuandikwa zilizokuwa na lengo la kuburudisha wenyeji, na ziliwasuta watu waliofikiriwa kuwa “Washamba” wajinga au wasiostarabika. Tamthilia hizo zilimwonyesha mhusika anayetoka shamba na kwenda kuzuzuka mjini.
Tamthilia – andishi ya Kiswahili
Tangu miaka ya 1920 mpaka 1960 mambo yaliyowakabili wanaotawaliwa yalikuwa ardhi na kujipatia uhuru. Hata hivyo tamthilia zilizoandikwa wakati huo na Watanzania hazikujishughulisha na mambo haya matatu. Katika kipindi hiki kabla ya kuchapishwa vitabu vyote, ilibidi vipitiwe kwenye Kamati ya lugha ya makoloni ya Afrika Mashariki. Hiki kilikuwa chombo cha mtawala cha kusimamia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Kutokana na hali hii maandishi yoyote yale ambayo ni kinyume na ukoloni hayangeweza kuchapishwa.
Tamthilia za wakati huo zilihusu mambo ambayo kwa kiasi fulani yalisababishwa na tabaka tawala lakini hayakuchambuliwa kwa kina kuweza kutoa mwanga wa kuyatatua. Tamthilia hizi zililenga kwenye masuala yanayohusu rushwa, mapenzi, ukabila na migongano ya utamaduni. Iwapo tamthilia hizi zingegusia uondoaji wa ukabila, bali zingeweza kuchangia kuleta Umoja ambao ungetumika kunyakua ardhi ambayo ilikuwa imechukuliwa na mkoloni na hatimaye kuleta vuguvugu la kumtoa kabisa mkoloni.
Tamthilia andishi zilizoandikwa kwanza kabla ya kuingizwa jukwaani zimeanza kutokea miaka ya 1950. Tamthilia za mwanzo zilikuwa za kidini mfano tamthilia ya “Imekwisha” iliyoandikwa na C. Frank mwaka 1951 (Mulokozi 1996).
Kipindi cha Uhuru
Tanzania kuwa jamhuri mwaka 1962 kuliashiria mambo mapya kwenye tamthilia. Kwanza usomi ulipiga hatua kutokana na siasa mpya ya wananchi kujitawala wenyewe. Chuo Kikuu cha kwanza nchini kilianzishwa mwaka 1961. Serikali pia ilianzisha Wizara ya Utamaduni wa Taifa mwaka 1962. Katika kipindi hiki cha uhuru palikuwepo tamthilia za kizungu, vichekesho na tamthilia ya Kiswahili.
Katika kipindi hiki cha Uhuru Tanzania ilikuwa huru katika uendeshaji wa mambo yake hata hivyo aina kuu tatu za tamthilia ambazo zilitumika kipindi cha ukoloni ziliendelea kuwepo.
Tamthilia za kizungu
Kutokana na uhuru waliokuwa nao waandishi, tamthilia muhimu za kizungu zilianza kutafsiriwa na kuigizwa kwa lugha ya Kiswahili ili zilieleweka zaidi kwa wananchi. Mfano wa tamthilia hizo ni Juliasi Kaisari ya Shakespare na Mabepari wa Venisi iliyotafsiriwa na J. K. Nyerere kutoka lugha ya Kiingereza yaani “Julias Caesar” na “Merchants of Venis”.
Hata hivyo tamthilia zilizotafsiriwa hazikuwa za kizungu tu bali hata zile za Kiafrika zilizoandikwa kwa lugha za kigeni na lugha zingine za Kiafrika zilitafsiriwa kwa Kiswahili. Mfano; Mtawa mweusi kilichoandikwa na Ngugi wa Thiong’o, Masaibu ya ndugu Jero kilichoandikwa na Soyinka (Mulokozi, 1996, uk. 205-207).
Vichekesho navyo vilichukua sura tofauti kidogo, ambapo badala ya kuwasuta washamba zilianza kuwasuta wazungu weusi, waafrika wanaoringia elimu, vyeo na kudharau utamaduni wao. Vichekesho hivyo vilibeba ujumbe uliohusu matatizo katika jamii na matukio ya wakati huo. Baadhi ya vichekesho hivyo ni Mahoka, (1974), Pwagu na Pwaguzi (1978) vilivyokuwa vikirushwa katika Radio Tanzania kwa dhumuni la kukemea tabia mbovu za baadhi ya watu. Hata sasa vipo baadhi ya vipindi ambavyo husuta tabia hizo kama vile Futuhi (Star TV), Komedi (East Africa TV), Fataki (TBC).
Tamthilia Andishi Ya Kiswahili
Baada ya Uhuru waandishi wengi chipukizi wa tamthilia ya Kiswahili walipata hamasa ya kuandika kuhusu jamii zao. Mfano E. Hussein, Penina Muhando (Mlama), na Ngahyoma na G. Uhinga waliandika kwa kutumia foni za sanaa za maonyesho. Hivyo basi hii ilipelekea waandishi wengi kuandika juu ya hali halisi iliyopo katika jamii husika (Mulokozi, 1996).
Hitimisho
Kwa ujumla historia ya tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania imekuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii ambapo waandishi wengi wamekuwa wakiandika kazi zao kutokana na mambo yanayoikumba jamii kwa ujumla kama vile rushwa, migongano ya kiutamaduni, matabaka, ugonjwa na dini ambapo imepelekea kukua kwa utanzu wa tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania.
MAREJELEO
Mulokozi, M. (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es salaam. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahil Sanifu. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.