11-21-2021, 03:20 PM
SWALI: Kujadili historia ya tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania tangu kuanza kwake hadi hivi sasa.
Maana ya tamthilia
Tamthilia ni utungo wa kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo (TUKI, 2004).
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa tamthilia ni utungo au mchezo wa kuigiza matendo au mawazo fulani yaliyopo katika jamii, ambapo huwa ni majibizano baina ya watu wawili au zaidi.
Historia ya tamthilia nchini Tanzania
Historia ya tamthilia nchini Tanzania inaelezwa kwa kurejelea vipindi vitatu yaani kabla, wakati na baada ya ukoloni.
Kabla ya ukoloni
Kwa mujibu wa Mulokozi (1996:203), katika kitabu chake cha “Fasihi ya Kiswahili”, anaeleza kuwa kabla ya ukoloni tamthiliya zilizoandikwa ili ziigizwe jukwaani hazikuwepo , badala yake, zilikuwepo tamthiliya zisizoandikwa, zilizogezwa au kufaraguzwa kwa ajili ya kuonyeshwa kwenye shughuli maalumu, kwa mfano sherehe za jando na unyago, mazishi, kutawazwa kwa Mtemi, arusi na michezo ya watoto. Tamthilia hizo zilikuwa na sifa kadha za tamthilia yaani hadithi, vitendo, wahusika na waigizaji wao na dayolojia. Hata hivyo tamthilia hizo hazikuwepo na ploti ya K – Aristotle wala matini yaliyoandikwa na kuwa tamthilia simulizi.
Mfano mzuri wa tamthilia hizo awali ni maigizo ya watoto wakati wanapocheza mfano A, B, C na D ambapo A huwa ni baba, B huwa ni mama na C na D huwa ni watoto ambao ni msichana na mvulana ambapo mchezo huanza kwa A kumwambia B aandae chakula, B hufanya hivyo na C anakwenda kuchota maji mtoni na D anapeleka mbuzi malishoni”.
Hivyo basi kabla ya ukoloni hakukuwa na tamthilia zilizoandikwa ili ziigizwe badada yake kulikuwa na sanaa za maonyesho ambazo zilikuwa zikitumika katika shughuli maalumu mfano sherehe, michezo ya watoto wadogo pamoja na jando na unyago.
Kipindi cha ukoloni, (1890 – 1960’s)
Katika kipindi hiki jamiii nyingi za Kiafrika (Tanzania), zilikuwa zikitawaliwa na watawala kutoka nchi za Kimagharibi. Hivyo basi kazi ya tamthilia iliegemea katika utawala wa kikoloni na kupelekea kuibuka aina kuu mbili za tamthilia mpya (zisizokuwa za kijadi) yaani hazikuwa na utamaduni wa Kiswahili ambazo ni tamthilia za Kizungu na tamthilia za vichekesho. Mnamo mwishoni mwa miaka 1950 paliongezeka aina nyingine ya tamthilia ambayo ni tamthilia ya Kiswahili na kupelekea kufikia idadi kuwa tatu (Mulokozi 1996:204).
Tamthilia za Kizungu
Tamthilia hizi ni tamthilia ambazo ziliandikwa kwa lugha ya kizungu (Kiingereza) na zilizojikita katika utamaduni wa kizungu. Lengo kuu za tamthilia hizi zilikuwa ni kuburudisha Maofisa na Masetla wa Kizungu ama kufunza Biblia na imani ya Kikristo.
Katika Tanzania tamthilia za Kiingereza zilianza kuingizwa miaka ya 1920, nyingi zilichezwa mashuleni na zilitungwa na Waingereza, kwa mfano Shakespare na baadhi zilikuwa ni za dini ya Kikristo. Tamthilia hizi zilikuwa zikiunga mkono mfumo wa ubepari na ukoloni. Vilevile katika kipindi hiki kulikuwa na tamthilia chache sana zilizotafsiriwa kwa Kiswahili. Mfano tamthilia ya “Moliere Le Medecin Malge Lui” (Kifaransa “Tabibu Asiyependa Utabibu” (Kiswahili) iliyoandikwa na Morrison 1945 na kuchapwa na E.A.S huko Nairobi.
Baadaye katika kipindi hiki viliibuka vikundi viwili vya kuigiza, ambavyo ni Dar es salaam players mwaka 1947 na Arusha Little Theatre mwaka 1953. Kuanzia wakati huo tamthilia ya Kiswahili ilianza kuhusishwa katika mashindano na hivyo kuchochea utunzi wa tamthilia ya Kiswahili.
Vichekesho
Ni aina ya tamthilia – gezwa zilizotungwa papo kwa papo bila ya kuandikwa zilizokuwa na lengo la kuburudisha wenyeji, na ziliwasuta watu waliofikiriwa kuwa “Washamba” wajinga au wasiostarabika. Tamthilia hizo zilimwonyesha mhusika anayetoka shamba na kwenda kuzuzuka mjini.
Tamthilia – andishi ya Kiswahili
Tangu miaka ya 1920 mpaka 1960 mambo yaliyowakabili wanaotawaliwa yalikuwa ardhi na kujipatia uhuru. Hata hivyo tamthilia zilizoandikwa wakati huo na Watanzania hazikujishughulisha na mambo haya matatu. Katika kipindi hiki kabla ya kuchapishwa vitabu vyote, ilibidi vipitiwe kwenye Kamati ya lugha ya makoloni ya Afrika Mashariki. Hiki kilikuwa chombo cha mtawala cha kusimamia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Kutokana na hali hii maandishi yoyote yale ambayo ni kinyume na ukoloni hayangeweza kuchapishwa.
Tamthilia za wakati huo zilihusu mambo ambayo kwa kiasi fulani yalisababishwa na tabaka tawala lakini hayakuchambuliwa kwa kina kuweza kutoa mwanga wa kuyatatua. Tamthilia hizi zililenga kwenye masuala yanayohusu rushwa, mapenzi, ukabila na migongano ya utamaduni. Iwapo tamthilia hizi zingegusia uondoaji wa ukabila, bali zingeweza kuchangia kuleta Umoja ambao ungetumika kunyakua ardhi ambayo ilikuwa imechukuliwa na mkoloni na hatimaye kuleta vuguvugu la kumtoa kabisa mkoloni.
Tamthilia andishi zilizoandikwa kwanza kabla ya kuingizwa jukwaani zimeanza kutokea miaka ya 1950. Tamthilia za mwanzo zilikuwa za kidini mfano tamthilia ya “Imekwisha” iliyoandikwa na C. Frank mwaka 1951 (Mulokozi 1996).
Kipindi cha Uhuru
Tanzania kuwa jamhuri mwaka 1962 kuliashiria mambo mapya kwenye tamthilia. Kwanza usomi ulipiga hatua kutokana na siasa mpya ya wananchi kujitawala wenyewe. Chuo Kikuu cha kwanza nchini kilianzishwa mwaka 1961. Serikali pia ilianzisha Wizara ya Utamaduni wa Taifa mwaka 1962. Katika kipindi hiki cha uhuru palikuwepo tamthilia za kizungu, vichekesho na tamthilia ya Kiswahili.
Katika kipindi hiki cha Uhuru Tanzania ilikuwa huru katika uendeshaji wa mambo yake hata hivyo aina kuu tatu za tamthilia ambazo zilitumika kipindi cha ukoloni ziliendelea kuwepo.
Tamthilia za kizungu
Kutokana na uhuru waliokuwa nao waandishi, tamthilia muhimu za kizungu zilianza kutafsiriwa na kuigizwa kwa lugha ya Kiswahili ili zilieleweka zaidi kwa wananchi. Mfano wa tamthilia hizo ni Juliasi Kaisari ya Shakespare na Mabepari wa Venisi iliyotafsiriwa na J. K. Nyerere kutoka lugha ya Kiingereza yaani “Julias Caesar” na “Merchants of Venis”.
Hata hivyo tamthilia zilizotafsiriwa hazikuwa za kizungu tu bali hata zile za Kiafrika zilizoandikwa kwa lugha za kigeni na lugha zingine za Kiafrika zilitafsiriwa kwa Kiswahili. Mfano; Mtawa mweusi kilichoandikwa na Ngugi wa Thiong’o, Masaibu ya ndugu Jero kilichoandikwa na Soyinka (Mulokozi, 1996, uk. 205-207).
Vichekesho navyo vilichukua sura tofauti kidogo, ambapo badala ya kuwasuta washamba zilianza kuwasuta wazungu weusi, waafrika wanaoringia elimu, vyeo na kudharau utamaduni wao. Vichekesho hivyo vilibeba ujumbe uliohusu matatizo katika jamii na matukio ya wakati huo. Baadhi ya vichekesho hivyo ni Mahoka, (1974), Pwagu na Pwaguzi (1978) vilivyokuwa vikirushwa katika Radio Tanzania kwa dhumuni la kukemea tabia mbovu za baadhi ya watu. Hata sasa vipo baadhi ya vipindi ambavyo husuta tabia hizo kama vile Futuhi (Star TV), Komedi (East Africa TV), Fataki (TBC).
Tamthilia Andishi Ya Kiswahili
Baada ya Uhuru waandishi wengi chipukizi wa tamthilia ya Kiswahili walipata hamasa ya kuandika kuhusu jamii zao. Mfano E. Hussein, Penina Muhando (Mlama), na Ngahyoma na G. Uhinga waliandika kwa kutumia foni za sanaa za maonyesho. Hivyo basi hii ilipelekea waandishi wengi kuandika juu ya hali halisi iliyopo katika jamii husika (Mulokozi, 1996).
Hitimisho
Kwa ujumla historia ya tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania imekuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii ambapo waandishi wengi wamekuwa wakiandika kazi zao kutokana na mambo yanayoikumba jamii kwa ujumla kama vile rushwa, migongano ya kiutamaduni, matabaka, ugonjwa na dini ambapo imepelekea kukua kwa utanzu wa tamthilia ya Kiswahili nchini Tanzania.
MAREJELEO
Mulokozi, M. (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es salaam. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahil Sanifu. Dar es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Mwl Maeda