MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
UHAKIKI WA RIWAYA YA MFADHILI - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
UHAKIKI WA RIWAYA YA MFADHILI - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Uhakiki wa kazi za fasihi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=78)
+--- Thread: UHAKIKI WA RIWAYA YA MFADHILI (/showthread.php?tid=1840)



UHAKIKI WA RIWAYA YA MFADHILI - MwlMaeda - 12-27-2021

UHAKIKI WA RIWA YA MFADHILI
KIDATO CHA 5 NA 6
KITABU – MFADHILI
MWANDISHI – HUSSEIN TUWA
WACHAPAJI – MACMILAN
MWAKA – 2007

FUNGUA HAPA PDF >>>>>> [attachment=810]

UTANGULIZI
Mfadhili ni riwaya inayoongelea suala la mapenzi na ndoa, ikonesha matatizo mbalimbali yanayotokana na mapenzi na ndoa na athari zake kwa wanaohusika. Ni riwaya inayoongelea juu ya penzi zito baina ya Gaddi Bullah na Dania Theobald, na jinsi penzi hilo lilivyoingiliwa na mitihani na majaribu makubwa. Ni riwaya ambayo kwa mapana yake inajadili kwa kiasi kikubwa suala la mapenzi na ndoa na athari zake kwa jamii.
MAUDHUI
Dhamira
Mwandishi katika riwaya hii licha ya kujadili dhamira ya mapenzi na ndoa, vilevile amejadili dhamira mbalimbali kama vile usaliti, umuhimu wa uongozi bora, wizi wa mali ya umma, chuki, uzembe kazini, dharau, uongo na ulaghai, n.k
Dhamira kuu: Fadhila
Katika kujadili suala hili mwandishi anaonesha jinsi suala la kufadhiliana lilivyomuhimu katika jamii bila ya kujali unayemfadhili alikutendea mema au mabaya huko nyuma. Mfano mzuri katika suala hili ni fadhila za Gaddi kwa Dania, ambapo mwandishi anaonesha jinsi Gaddi alivyogeuka mfadhili wa ini kwa Dania na kuokoa maisha ya Dania licha ya kutendwa unyama usiosemeka katika mahusiano yao. Ukweli huu unadhihirishwa na Dkt. Viran alipokuwa akimshawishi Dania juu ya kwenda kumuona Gaddi na hatimaye akamtobolea siri kuwa Gaddi ndiye mfadhili wa ini lake.
Dhamira ndogondogo
  1. Mapenzi na ndoa
Katika kujadili dhamira hii msanii ameainisha aina kuu mbili za mapenzi na ndoa; mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo, ndoa ya kweli na ya uongo.
Tukianza na mapenzi ya kweli, haya yanaoneshwa kati ya Gaddi Bullah na dada yake Bi. Hanuna. Hawa walipendana kwelikweli na ndio maana mmoja akiwa na tatizo linakuwa ni tatizo la wote wawili. Mtu akimwudhi Gaddi amemwudhi na dada yake Bi. Hanuna, na walisaidiana katika shida zao zote.
Mapenzi mengine ya kweli ni kati ya Gaddi na Dania. Mwanzoni walipendana hasa; mchana walikuwa wakienda kula chakula pamoja na hata walifikia hatua ya kutembeleana. Gaddi katika kuonesha mapenzi kwa Dania, alimsaidia kwa kila hali hata wakati war aha na shida (uk. 101-106). Hata baada ya Dania, kumsaliti Gaddi, bado alimpenda na hata akamfadhili baada ya kusalitiwa na Jerry kwa mara ya pili (uk. 137-139).
Pia kuna mapenzi ya kweli kati ya Gaddi na Junior, mtoto wa Dania. Pamoja na kwamba Junior hakuwa mtoto wake, Gaddi alimpenda sana na ndio maana baada ya Junior kuumia mkono aliyempeleka hospitalini ni Gaddi na wala si Baba yake Jerry (uk. 118). Vilevile, Junior aliposikia taarifa za ugonjwa wa Gaddi alilia na wakati wa kifo cha Gaddi wosia pekee alioutoa kwa Dania ni kumtunza vizuri Junior, anasema (uk. 146);
“Gaddi akimgeukia Dania. “Junior Dania……..Junior mtunze vizuri Junior! Umepata bahati ya kue…ndelea kuishi ili umtunze mwan…na….o!” Gaddi aliyasema yote hayo kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa Junior.
Mapenzi mengine ya kweli ni ya Mama Mlole (Bi. Fausta) kwa wafanyakazi wa chini yake kama Gaddi na Dania. Pamoja na Gaddi kuharibu kazi, mama Mlole alimtetea sana asifukuzwe kazi bali aangaliwe upya (uk. 69-71). Vilevile alimtetea sana Dania asifutwe kazi kipindi anaumwa. Mama Mlole ni mfano wa viongozi wenye mapenzi ya kweli kwa wale anaowaongoza.
Vilevile kuna mapenzi ya kweli kati ya Nunu na Dania. Nunu alikuwa bega kwa bega na Dania wakati wa maandalizi ya harusi ya Dania na Jerry. Nunu alimsaidia sana Dania. Vilevile alimshauri sana Dania asirudiane na Jerry kwa vile alimsaliti mara ya kwanza (uk. 113-115). Pia alimsaidia sana kumlea mtoto wake Junior wakati Dania yuko kituo cha kuponya walevi (uk. 115). Kama hiyo haitoshi, Nunu alikuwa bega kwa bega na wazazi wa Dania wakati wa ugonjwa wake na hata akamsaidia kumtafuta Gaddi na Bi. Hanuna ili awaombe msamaha kwa yote aliyowatendea.
Kuna mapenzi ya kweli kati ya Nunu na Boaz. Hawa walipendana kwa dhati na ndiyo maana shida ya Nunu ilikuwa shida ya Boaz pia. Ni kutokana na mapenzi ya dhati waliyokuwa nayo ndiyo maana walisaidiana kwa hali na mali, kwa heri na shari katika kumtafuta Gaddi aliyekuwa anatakiwa na rafiki yake Dania. Hata wakafikia hatua ya kuhatarisha maisha yao kwa kumteka nyara Bi. Hanuna kwa lengo la kumsaidia Dania (uk. 36-56).
Mapenzi mengine ya kweli ni kati ya Dakta Viran na Gaddi. Hawa walipendana hasa, na ndiyo maana Viran alimsaidia Gaddi katika matatizo mbalimbali. Kwa mfano, kumtibu mpenzi wake Dania, kumtibu yeye mwenyewe alipopata shinikizo la moyo, baada ya kuachwa na Dania na mwisho Viran anakuwa mpatanishi kati ya Gaddi na Dania na Nunu kutokana na ugomvi wa kuachwa kwa Gaddi na mpenzi wake Dania. Vilevile tunamwona Dakta Viran anavyohangaika kuokoa maisha ya Gaddi kutokana na ugonjwa aliokuwa anaumwa ingawa hakufanikiwa. Haya yote aliyafanya kwa sababu alimpenda Gaddi kwa dhati na Gaddi vilevile alimpenda Viran.
Vilevile kuna mapenzi ya dhati kati ya wazazi wa Dania kwa mtoto wao Dania. Wazazi wake Dania walimpenda sana mtoto wao, ndiyo maana wakati wa shida za Dania walimsaidia kwa hali na mali hadi wakampeleka Afrika  Kusini kutibiwa ugonjwa wake wa ulevi. Wakati wa ugonjwa wake wa ini, wazazi wake  walimsaidia sana mpaka hatua ya kuweka matangazo redioni ili kumsaidia mtoto wao kwa mtu ambaye angejitolea ini. Gharama zote walikuwa tayari kumlipa mtu yeyote ambaye angejitokeza kufanya hivyo. Hayo ni mapenzi ya dhati ya wazazi kwa binti yao.
Mapenzi mengine ya dhati ni kati ya Nunu na Gaddi. Nunu alimpenda Gaddi kwa dhati, ndiyo maana alimshauri sana Dania asimwache Gaddi na kurudiana na Jerry. Nunu alimkatalia Dania asirudiane na Jerry si kwa sababu alimsaliti, bali awe na Gaddi aliyemsaidia wakati wa shida (uk. 114-115). Vilevile Gaddi alimpenda Nunu kama rafiki mzuri anasema (uk. 146);
“………Nunu”… “A…Abee! Nunu aliitikia kwa upole huku akitiririkwa na machozi “wewe…..ni rafiki…mzuri….. “Gaddi alimwambia……”
Baada ya kifo cha Gaddi, Nunu pamoja na wengine wote walilia sana kuonesha mapenzi yao kwa Gaddi.
Mapenzi ya uongo
 Mapenzi ya uongo ni kati ya Jerry kwa Dania. Jerry inaonesha hakumpenda kwa dhati Dania na ndiyo maana alimsaliti wakati wa harusi yao. Jerry alipenda zaidi masomo kuliko kufunga ndoa na Dania. Aliona maandalizi ya harusi lakini akaondoka kwenda Marekani kusoma kwa ahadi ya kurudi siku ya harusi. Lakini siku ilipofika Jerry hakuonekana na hivyo ndoa ikashindikana kufungwa.
Vilevile kitendo cha Jerry kumtoroka Dania akiwa hospitalini pindi ambapo msaada wake ulitakiwa ni usaliti unaothibitisha kuwa hakuwa na mapenzi ya dhati kwa Dania. Jerry alitakiwa kumfadhili Dania ini ili kuokoa maisha yake, lakini siku ilipofika hakufika hospitalini na hawakumwona tena (uk. 133-135)
Mapenzi mengine ya uongo ni kati ya rafiki yake Gaddi kwa Gaddi. Huyu hakuwa rafiki wa kweli kwani alimshauri vibaya Gaddi (uk. 64). Kana kwamba hiyo haikutosha, alimtorosha mke wa Gaddi na kumuweka kinyumba (uk. 64-67). Kuhusu suala la ndoa, nazo zipo za aina mbili ambazo ni ndoa za kweli na ndoa za uongo. Ndoa ya kweli ni kati ya Gaddi kwa Nyambuja. Gaddi alimpenda sana mkewe na alimjali kwa kila kitu. Lakini mke wake hakuwa na mapenzi ya dhati katika ndoa yao. Baada ya mwaka mmoja tu wa ndoa yao, Nyambuja alianza kumsaliti mumewe kwa kuchelewa kurudi nyumbani, kusafiri bila taarifa kwa mume wake na mwisho akamwacha na kwenda kuolewa na rafiki wa mumewe (uk. 60-67).
  1. Usaliti
Usaliti ni dhamira ingine ambayo imejadiliwa sana katika riwaya hii ya Mfadhili. Katika kujadili dhamira hii, msanii anaonesha jinsi watu mbalimbali wanavyosaliti wenzao na athari za usaliti huo kwa wahusika.
Kwanza tunaoneshwa jinsi Nyambuja alivyomsaliti mume wake na kwenda kuolewa na rafiki wa mumewe. Kwa upande mwingine rafiki wa Gaddi alimsaliti Gaddi na kumchukua mke wa rafiki yake. Usaliti huu ulisababisha Gaddi kupoteza umakini kazini kutokana na msongo wa mawazo na kuishia kupewa barua ya onyo kwa kuidhinisha malipo hewa ya matengenezo ya magari ya kampuni (uk. 62-63).
Usaliti mwingine ni ule wa Afisa usafirishaji kwa kumsaliti Gaddi kazini. Huyu aliandaa vocha ya malipo hewa na kuipeleka kwa Gaddi ikasainiwe. Matokeo ya usaliti huo ni Gaddi kushushwa cheo na kuhamishwa chake cha kazi (uk. 71-72)
Usaliti mwingine ni wa Dania kwa Gaddi. Kwanza Dania alimsaliti Gaddi kwa kutoandaa ripoti aliyotakiwa kuiandaa kwa ajili ya kusomwa kwenye kikao cha wakuu wa vitengo. Dania hakuandaa ripoti hiyo, na siku ya kikao hakuonekana kazini hadi muda wa kikao ulipoanza saa mbili na nusu Asubuhi (uk. 77-79). Matokeo yake Gaddi alimlima barua ya onyo na kumtaka ajieleze. Lakini kwa busara za Mama Mlole alisuluhisha mgogoro huu.
Pili, Dania alimsaliti Gaddi kwa kumwacha wakiwa katika mapenzi mazito na wakati huohuo wanajiandaa kufunga ndoa. Dania alimwacha Gaddi na kurudiana na Jerry ambaye alimsaliti siku ya harusi yake. Matokeo ya usaliti huo ni Gaddi kupata ugonjwa wa shinikizo la moyo, kupigana na Jerry, na dada yake Bi. Hanuna kuwekwa ndani (polisi).
Usaliti wa Jerry kwa Dania. Kwanza alimsaliti Dania wakati wa harusi yao. Jerry hakuhudhuria harusi hiyo, alikuwa Marekani na wakati huohuo aliahidi kuwa angehudhuria (uk. 83-85). Ni kutokana na usaliti huo, harusi ilishindikana na kumfanya Dania aingie kwenye matatizo makubwa ya ulevi wa pombe kali (uk. 87). Kutokana na ulevi huo Dania alipata ugonjwa wa ini.
Pia Jerry alimsaliti Dania akiwa mgonjwa mahututi hospitalini kwa kuahidi kutoa ini baada ya vipimo kuonesha inawezekana, lakini hakufanya hivyo. Kwanza, hakumsaidia kwa kumpa ini. Pili akamtoroka akiwa kitandani hospitalini (uk. 133-134). Katika kuokoa maisha ya Dania, pamoja na kwamba alimsaliti, Gaddi alijitokeza kuwa mfadhili wa ini kwa Dania.
Katika riwaya hii mtunzi anaonesha kuwa wasaliti katika jamii wapo, anaweza kuwa mkeo (Nyambuja), mpenzi wako (Dania), mfanyakazi mwenzako (Afisa usafirishaji), mumeo (Jerry) au rafiki yako wa karibu (rafiki wa Gaddi), hivyo tuwe macho na wasaliti, kwani wanaharibu mapenzi ya watu na kazi zao.
  1. Umuhimu wa uongozi mzuri
Mwandishi amejadili dhamira hii katika riwaya yake ya Mfadhili. Katika kujadili dhamira hii, msanii anamtumia mhusika Mama Mlole. Mama Mlole alikuwa kiongozi mzuri ambaye aliwajali wale aliowasimamia, jambo ambalo linasaidia kuongeza ufanisi katika kazi yake.
Gaddi Bullah alipopata matatizo kazini yaliyotokana na athari za kuachwa na mke wake, Mama Mlole alimtetea sana asifukuzwe kazi baada ya kumweleza matatizo yake (uk. 70). Na ni Mama Mlole huyohuyo aliyependekeza Gaddi ahamishiwe Dar es Salaam ili aangaliwe zaidi badala ya kufukuzwa kazi. Mama Mlole alifanya hivyo kutokana na utendaji mzuri wa kazi aliokuwa nao Gaddi mwanzoni kabla ya kukumbwa na matatizo yaliyomsibu.
Vilevile ni Mama Mlole aliyemtetea Dania asifukuzwe kazi baada ya kuachwa na Jerry. Baada ya kuvunjika kwa ndoa yake na Jerry, utendaji wake wa kazi uliathirika sana. Alifikia hatua ya kuja ofisini akiwa amelewa (uk. 88) na hatua aliyofikia ilikuwa aachishwe kazi. Lakini Mama Mlole kama Afisa utumishi wa kampuni alimtetea sana na akapendekeza apewe likizo bila malipo kwa muda wote atakaokuwa kwenye matibabu ya ulevi wake (uk. 88)
Kiongozi mzuri daima hupendwa na watu anaowaongoza na mara nyingi ufanisi wake kazini vilevile huwa mzuri. Hapa msanii anachotaka kuifundisha jamii ni kuwa cheo ni dhamana lazima kukitumia kwa faida ya watu wote na sio kunyanyasa wengine.
  1. Bidii katika kazi
Bidii katika kazi ni dhamira ingine inayojitokeza katika riwaya hii ya Mfadhili. Katika kujadili dhamira hii, mwandishi anaonesha kuwa ili kuleta maendeleo katika jamii lazima kuwa na bidii katika kazi.
Katika kujadili hili mtunzi anamtumia Gaddi Bullah ambaye alionesha kuwa kijana mdogo lakini mchapakazi mzuri. Alipendwa sana na wafanyakazi wote waliokuwa chini yake na hata wakuu wake wa kazi huko makao makuu (uk. 59).
Pili tuna Dania, mwanzoni alikuwa mmoja kati ya wafanyakazi wenye nidhamu, bidii na ushirikiano mkubwa hapo makao makuu. Dania akiwa anatoka kwenye familia ya kitajiri. Aliwaheshimu wafanyakazi wote na wala hakuruhusu utajiri wa wazazi wake umpe kichwa. Kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi, ndiyo maana alipewa wadhifa wa kuongoza kitengo muhimu cha kukusanya madeni cha kampuni na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Katika kujadili zaidi dhamira hii, msanii anaonesha kuwa matatizo ya mtu binafsi au hata ya kifamilia yanaweza kupunguza bidii na ufanisi wa mtu katika kazi anayoifanya. Kama ilivyokuwa kwa Gaddi na Dania. Gaddi alipoachwa na mke wake alichanganyikiwa na kupoteza umakini katika kazi hata akasaini na kuidhinisha cheki hewa (uk. 63) ambayo ilimletea matatizo makubwa kazini kwake.
Vilevile Dania baada ya kuachwa na Jerry, ufanisi wake wa kazi ulipingua na kufanya kazi hovyo. Kwanza, utendaji wake uliathirika vibaya sana. Alifika ofisini akiwa amelewa. Kutokana na kitendo hicho, wazazi wake ilibidi wampeleke kwenye kituo maalumu cha kutibu watu wenye tatizo la ulevi wa kupindukia huko Afrika Kusini (uk. 88).
Kwa ufupi msanii anaonesha kuwa bidii katika kazi ni kichocheo cha maendeleo ya jamii. Pindi mtu anapokumbwa na matatizo, mara nyingi ufanisi wake wa kazi hupungua na hupata matatizo. Matatizo hayo yanaweza kuwa ya kufukuzwa kazi au kushushwa cheo kama ilivyokuwa kwa Gaddi. Vilevile matatizo yanaweza kumfanya mtu achanganyikiwe, aache kazi na kuuza kila kitu kama alivyofanya Gaddi baada ya kuachwa na Dania. Kwa hiyo, mwandishi anaitahadharisha jamii kuepukana na matatizo.
  1. Chuki
Chuki ni dhamira ingine inayojadiliwa katika riwaya ya Mfadhili. Katika kujadili dhamira hii, msanii anaonesha wahusika mbalimbali na chuki zao binafsi zinazosababishwa na mambo mbalimbali.
Kwanza, Bi. Hanuna alikuwa na chuki na Nunu kwa sababu ya Dania. Kitendo cha Dania kumuacha kaka yake, Gaddi wakati wako katika mapenzi ya raha na furaha. Kitendo hiki kilimuudhi sana Bi. Hanuna. Hata Nunu alipokwenda kwake kuomba msaada wa kumpata Gaddi alikataa katakata. Pia shida yao alikataa hata kuisikiliza kutokana na chuki aliyokuwa nayo, Bi. Hanuna anasema (uk. 25);
“Shida?” Aliguna kwa kebehi”. Eti shida! Mnaijua shida ninyi? Hebu niondokee hapa sasa hivi mwana asiye haya we! Shida niulize mimi mliyenisweka gerezani….”
Hata Nunu anapojitetea kuwa ya zamani wayaache wagange yaliyopo, Bi. Hanuna anamkatalia Nunu (uk. 24);
Bi. Hanuna vilevile alikuwa na chuki na Dania. Hii ilikuwa baada ya kumwacha kaka yake, Gaddi na kumweka ndani (gerezani) Bi. Hanuna. Hapo ndipo chuki ya Bi. Hanuna ilipoanza kwa Dania kama anavyosema (uk. 125);
“Na ni hapo ndipo chuki ya Bi. Hanuna dhidi ya Dania Theobald ilipodhihiri moyoni mwake. Wakati akimtazama ndugu yake akisema maneno yake na jinsi sura yake ilivyokuwa na uchungu na kukata tama, Bi. Hanuna alijua kuwa Dania Theobald atakuwa adui yake milele!!”
Msanii anaendelea kuonesha kuwa, jinsi Bi. Hanuna alivyokuwa anamwona mdogo wake akiteseka ndivyo alivyozidi kumchukia Dania, msanii anasema (uk. 126):
Bi. Hanuna alimueleza. Na kadiri alivyokuwa anamweleza kisa kile ndivyo ghadhabu dhidi ya Dania ilivyozidi kumpanda”
Ni kutokana na chuki hiyo ndiyo maana Bi. Hanuna alikwenda kwa Dania na kumtukana matusi mengi ambayo yalisababisha vurugu kubwa. Msanii anaonesha chuki ya Bi. Hanuna kwa Dania hivi (uk. 126-127)
Wewe ni Malaya usiye na haya baradhuli na hayawani! Hukumstahili mdogo wangu hata kidogo! Bi. Hanuna alimwambia kwa hamasa na muda huo Jerry alitoka ndani na kuanza kumfukuza huku akimtukana”
Kutokana na tukio hilo, Bi. Hanuna alikamatwa na polisi na kuwekwa rumande kwa kosa la shambulizi. Bi. Hanuna akalala rumande siku ile. Wakati mdogo wake amelala hospitalini yeye alikuwa amelala rumande na aliumia sana na akazidisha chuki yake kwa Dania kama anavyosema msanii (uk. 127);
“Kwa hakika chuki yake kwa Dania iliongezeka maradufu, na aliapa kumchukia kwa uhai wake wote uliobakia.”
Ni kutokana na chuki hiyo kwa Dania ndiyo maana alikataa kuwaeleza Nunu na Boaz, Gaddi alipo. Vilevile alikataa hata  kupeleka barua kwa Gaddi iliyotoka kwa Dania ya kuomba msamaha (uk. 24) mpaka alipomuona kweli Dania akiwa katika hali ya kukatisha tama ya kuishi (uk. 56).
Mhusika mwingine aliyeonesha chuki waziwazi kwa wahusika wengine ni Dania. Dania alikuwa na chuki na Gaddi Bullah kwa kumwona kama mtu aliyemnyang’anya cheo chake, msanii anasema (uk. 75);
“Chuki kubwa ilijengeka moyoni mwa Dania dhidi ya Gaddi Bullah. Kwake, Gaddi alikuwa ni mtu aliyemchukulia wadhifa wake na kumdhalilisha kama mwanamke, na alimwona ni mmoja tu kati ya wanaume wengi ambao kwake walikuwa wanyama na wahalifu.”
Dania anamwona Gaddi kama mnyama au mhalifu kutokana na chuki. Matokeo yake alijikuta akizidi kumchukia zaidi na zaidi. Chuki haikuishia ofisini tu bali hata kwenye sehemu za starehe hakutaka hata kukaa naye, mpaka alifikia hatua ya kumfukuza kwenye meza aliyokuwa amekaa na mtoto wake Junior  kwenye baa, msanii anasema (uk. 76);
“Naomba utupishe….hapa ni mahali petu! Dania alimjibu kifedhuli”
Kutokana na chuki aliyokuwa nayo Dania kwa Gaddi, anafikia hatua ya kumharibia kazi ili aonekane hafai (uk. 77-79). Matokeo yake Dania akaandikiwa barua kali na Gaddi ya onyo na kumtaka ajieleze ni kwanini asifukuzwe kazi (uk. 79).
Dania vilevile alikuwa na chuki na Jerry hasa baada ya kumwacha wakati maandalizi yote ya harusi yao yamekamilika. Kitendo cha Jerry kushindwa kuja kwenye harusi kama alivyoahidi kilimwudhi sana Dania. Dania alilia sana. Hata Jerry aliporudi kutoka Marekani alimfukuza kama mmbwa nyumbani kwake, msanii anasema (uk. 107);
“Toka! Dania alimfokea kwa ukali huku akimwonyesha sehemu ulipo mlango wa kutokea kwa kidole chake….Nasema ondoka Jerry na sitaki uje tena kunifuata hapa, wala popote pale niwapo! Ondoka!”
Nunu naye alikuwa na chuki na Jerry kwa sababu ya kumwacha rafiki yake Dania. Hata Jerry alipokwenda kwake kuomba msaada wa kumshawishi Dania alimfukuza na kumtaka asirudi tena nyumbani kwake (uk. 109);
Wazazi wa Dania nao walikuwa na chuki na Jerry kwa sababu ya kumsaliti mtoto wao. Jerry alipokwenda kwao kuwaomba msamaha walikuwa wakali zaidi ya mbogo na walimfukuza nyumbani kwao (uk. 109-110).
Msanii katika kujadili dhamira hii ya chuki, anaonesha kuwa wenye chuki kuna wakati watasameheana. Bi. Hanuna anamsamehe Dania, Gaddi vilevile anamsamehe Dania, Bi. Hanuna anamsamehe Nunu, halafu Dania anamsamehe Jerry ingawa msamaha huo ulileta matatizo mengine kwa Gaddi na Bi. Hanuna. Hivyo, msanii anaonesha kuwa umsamehe mtu aliyekufanyia makosa ili uishi kwa amani na utulivu.
  1. Dharau
Dharau ni dhamira inayojitokeza katika riwaya hii ya Mfadhili. Katika kujadili dhamira hii, msanii anamtumia Nyambuja kama mtu mwenye dharau kwa mumewe. Nyambuja hakuwa na upendo wowote kwa mume wake na ndio maana alikuwa anamdharau. Hata akiulizwa swali na mumewe majibu aliyokuwa anayatoa yalikuwa yamejaa dharau tupu (uk. 60). Vilevile kitendo cha Nyambuja kusafiri safari za ghafla na kumtaarifu mumewe kwa simu ni sehemu ya dharau. Gaddi kama mume wake alistahili kuagwa kwa kufuata taratibu za mume na mke zilivyo, lakini Nyambuja hakujua hilo ila dharau ilitawala (uk. 61).
Kitendo cha Nyambuja kufanya mapenzi na rafiki yake Gaddi na kumwacha nayo ni dharau ya hali ya juu. Hata barua aliyomwandikia Gaddi (uk. 65) ni barua iliyojaa dharau ya Nyambuja kwa Gaddi. Mara nyingi mwanamke mwenye dharau ndani ya nyumba kwa mume wake husababisha kuvunjika kwa ndoa na ndivyo ilivyotokea kwa Gaddi na Nyambuja.
Mhusika mwingine anayeonesha kuwa na dharau ni Dania. Kwanza alimdharau  Gaddi siku ya kwanza tu alipomkuta ofisini kwake. Kitendo cha Dania kumwita Gaddi kwamba wewe ni “Gaidi Bullah” (uk. 73) ni sehemu ya dharau aliyoionesha kwa Gaddi. Vilevile kitendo cha Dania kumfukuza Gaddi kwenye meza aliyokuwa amekaa na mtoto wake Junior kwenye baa ni sehemu ya dharau. Dania alimfukuza Gaddi kwenye meza kama mbwa mwizi; ambapo katika hali ya kawaida asingefanya hivyo, au angemwomba kwa upole awapishe na sio kwa kumkaripia kama mtoto mdogo, hii yote ni dharau.
Vilevile Dania alionesha dharau ya hali ya juu baada ya kumwacha na kurudi kwa Jerry. Majibu aliyokuwa anamjibu Gaddi yalikuwa majibu ya kijeuri na dharau tupu (120-123). Lakini msanii anaitahadharisha jamii kuwa makini juu ya suala la dharau kwani unayemdharau leo huwezi kujua baadaye anaweza kukufaa. Dania alimwacha Gaddi, alimdharau, lakini baadaye akawa mfadhili wa ini lake baada ya kutelekezwa na Jerry kwa mara ya pili akiwa mgonjwa mahututi hospitalini. Hivyo, tuepuke dharau kwani hazina maana yoyote.
  1. Nafasi ya mwanamke katika jamii
Katika riwaya hii, mwanamke amechorwa katika nafasi mbbalimbali. Kwanza amechorwa kama kiumbe asiye na msimamo katika kufanya maamuzi. Hapa tunamuona Dania akiwa na maamuzi yasiyofaa, kwa kutokuwa na msimamo na kuamua tena kumrudia Jerry ambaye alimuumiza mwanzoni.
Pili, mwanamke amechorwa kama mtu mwenye huruma na mshauri mzuri. Mfano mzuri ni Nunu alivyomhurumia rafiki yake, Dania na kumhangaikia kwa hali na mali. Vilevile tunaoneshwa jinsi alivyokuwa mshauri mzuri wa Dania.
Tatu, mwanamke amechorwa kama mtu katili na msaliti. Hapa tunamuona Nyambuja na Dania walivyomtenda vibaya Gaddi na hatimaye kumsaliti na kwenda kwa wanaume wengine.
Nne, mwanamke amechorwa kama mtu jasiri. Hapa tunamuona Nunu ambaye alifanya kazi kubwa sana ya kumpatanisha Dania na Gaddi hata akafikia hatua ya kumteka kwa nguvu dada yke Gaddi, Bi. Hanuna, ili aweze kuwasaidia kumpata Gaddi.
Tano, mwanamke amechorwa kama mtu mwenye upendo, moyo wa huruma na wa kusaidia. Hapa tunamuona Bi. Hanuna alivyokuwa na upendo kwa kaka yake Gaddi, halafu pia tunamuona Mama Mlole alivyokuwa na upendo kwa wafanyakazi wa chini yake.
Ujumbe
  1. Rafiki wa kweli ni yule anayekusaidia au kukujali wakati wa shida.
  2. Si kila king’aacho ni dhahabu
  3. Mtu anapotenda kosa, lazima akubali kutubu kosa
  4. Ni vigumu kumpata mtu mwenye mapenzi ya kweli au atakayekupenda kama unavyompenda wewe
  5. Bidii na ufanisi katika kazi ni chanzo cha maendeleo katika jamii
  6. Matatizo, majaribu, chuki na dharau ni vitu vya kutegemewa kwenye mapenzi na ndoa.
  7. Kipenda roho hula nyama mbichi
Falsafa
Msanii anaamini kuwa katika suala la mapenzi kuna kupenda na kutopendwa, kuna kuoa na kuachwa. Hivyo, ni vigumu kupata mtu mwenye mapenzi ya dhati.
Msimamo
Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi, kwani anaonesha wazi kuwa katika suala la mapenzi na ndoa kuna changamoto zake. Watu lazima tukubali kusameheana kwani hujui ni yupi atakayekusaidia wakati wa shida.
Mtazamo
Mwandishi anaonekana kuwa na mtazamo wa kiyakinifu, kwani ameyaweka mambo wazi kwa kuonesha kuwa mapenzi ya dhati yapo kwa akupendaye asiyekupenda usimtegemee anaweza kukuumiza.
Migogoro
  1. Mgogoro kati ya Gaddi na Nyambuja
  2. Mgogoro kati ya Gaddi na Dania
  3. Mgogoro kati ya Gaddi na Jerry
  4. Mgogoro kati ya Nunu, Boaz na Bi. Hanuna
  5. Mgogoro kati ya Dania na Jerry
  6. Mgogoro kati ya Jerry na wazazi wa Dania
  7. Mgogoro kati ya Nunu na Jerry
  8. Mgogoro kati ya Gaddi na rafiki yake
FANI
Muundo
Msanii ametumia muundo changamano, amechanganya muundo rejea na moja kwa moja. Sura ya kwanza ametumia muundo wa rejea na kuanzia sura ya pili na kuendelea ametumia muundo wa moja kwa moja mpaka mwisho wa riwaya.
Mtindo
Msanii ametumia kwa kiasi kikubwa mtindo wa masimulizi na kiasi kidogo mtindo wa dayalojia, nafsi zote tatu zimetumika. Vilevile kuna matumizi ya barua (uk. 65).
Matumizi ya lugha
Lugha aliyotumia ni lugha rahisi iliyojaa misemo, methali, tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.
Misemo/Nahau
Jibu lile lilimkata maini (uk. 36)
Methali
a       Ukiyastaajabu ya Musa utayaona ya Firauni (uk. 27)
b       Hakuna marefu yasiyo nan cha (uk. 117)
c        Ni bora nusu shari kuliko shari kamili (uk. 127)
d       Mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi (uk. 135)
Tamathali za semi
Tashibiha
a        Paa lake lililokuwa limejengwa kwa mithili yam domo wa lile              dege aina ya Concord (uk. 11)
b       Gari iliruka mbele kama jiwe na kutimua vumbi (uk. 41)
c  Kamfukuza kama mbwa kutoka kwenye nyumba ya marehemu           mumewe (uk. 60)
Mbinu nyingine za kisanaa
Tanakali sauti (Onomatopea)
a        Vilitilia mkazo uharaka wa binti yule kwa kutoa sauti za Ko! Ko! Ko! (uk. 1)
b       Aaakh! Ni – niache! Uuuuuwwiiiii !! Yallaaaah (uk. 37)
Takriri
a        Toka hapa ! Ondoka! Na usirudi tena! (uk. 32)
b       Nimesema sitaki! Sitaki! Sitaki! (uk. 35)
c        Sikubali! Sikubali! Nawaambia nitawashitaki kwa hili ! (uk. 43)
Mdokezo
a        Oh! Mungu wangu, sasa itakuwaje jamani….(uk. 13)
b       Ah! Ni kweli Anti….lakini…..(uk. 12)
Wahusika
Gaddi Bullah
  1. Huyu ndiye mhusika mkuu wa riwaya hii. Huyu alikuwa meneja wa kampuni
  2. Kijana mchangamfu na mwenye huruma
  3. Mkarimu na mchapakazi
  4. Alikuwa na upendo wa dhati
  5. Ni msamehefu na mwenye kuzitawala hasira zake
  6. Mume wa kwanza wa Nyambuja na mpenzi wa Dania
  7. Gaddi anafaa kuigwa na jamii kutokana na tabia na matendo yake mazuri
Dania
  1. Huyu ni mwanamke ambaye alizaliwa katika familia ya kitajiri
  2. Ni mwenye hasira anapokuwa amechukizwa na mwenye chuki
  3. Hana msimamo na hudanganyika kirahisi
  4. Ni mfanyakazi mwenye nidhamu, bidii na ushirikiano
  5. Alikuwa mlevi wa kutupwa baada ya kuachwa na Jerry
  6. Dania ni mwanamke ambaye anafaa kuigwa kwa baadhi ya mambo na hafai kuigwa kwa baadhi ya mambo
Bi. Hanuna
  1. Huyu alikuwa dada wa Gaddi Bullah, alimpenda sana mdogo wake kiasi cha kukataa kumsaliti
  2. Alikuwa na chuki na mtu yeyote aliyemuudhi mdogo wake
  3. Bi. Hanuna anafaa kuigwa na jamii kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa mdogo wake
Jerry
  1. Huyu alikuwa mpenzi wa Dania na alikuwa mtaalamu wa kompyuta
  2. Jerry alikuwa mcheshi, mtanashati na mwenye mvuto mkubwa kwa akina dada
  3. Jerry alikuwa katili na msaliti mkubwa kwani alimsaliti Dania mara mbili
  4. Jerry hakuwa na mapenzi ya kweli ndio maana alikuwa muongo na laghai wa mapenzi
  5. Jerry kutokana na tabia zake hafai kuigwa na jamii
Nunu
  1. Huyu alikuwa rafiki wa Dania
  2. Alikuwa na mapenzi ya kweli kwa watu na aliwasaidia sana watu, maana aliwasaidia sana wakati wa shida. Hivyo, anafaa kuigwa na jamii
Wahusika wengine wanaojitokeza katika riwaya hii ni Boaz, Mama Mlole, Mary, Aisha, Agnes, Junior na wengineo.
Mandhari
Mandhari ya riwaya hii ni halisi, inatalii maeneo kama vile Arusha, Dar es Salaam na Pemba. Katika sehemu hizo zote kuna mandhari ya ofisini, nyumbani, baa, barabarani, hospitalini, n.k
Jina la kitabu
Kwa kiasi kikubwa jina la kitabu linasadifu yale yaliyomo katika kitabu. Mfadhili ni mtu anayemdhamini mtu katika kugharimia kitu fulani. Hivyo katika riwaya hii msanii anaonesha ufadhili wa aina mbalimbali kama ifuatavyo:
Kwanza tunaona ufadhili wa Mama Mlole kwa Gaddi baada ya kukumbwa na kashfa ofisini kwake asifukuzwe kazi. Mama Mlole ndiye aliyemtetea Gaddi hata kumhamishia Dar es Salaam kwa uangalizi zaidi.
Pili, Mama Mlole alimfadhili Dania asifukuzwe kazi kutokana na kuwa mlevi sugu baada ya kuachwa na mpenzi wake Jerry.
Tatu, Mama Mlole alimfadhili Gaddi na Dania kwa kuwapatanisha kutokana na uhasama baina yao ambao ungeathiri utendaji kazi.
Gaddi vilevile alimfadhili Dania baada ya kuachwa na Jerry hata kuwa mlevi wa kupindukia. Pili, Gaddi alimfadhili Dania kwa kumpa ini lake moja wakati anaumwa baada ya kusalitiwa mara ya pili na Jerry. Tatu, Gaddi alimfadhili Junior kwa kumpeleka hospitali baada ya kuumia mkono. Isingekuwa Gaddi pengine Junior angepata matatizo makubwa zaidi.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
  1. Kimaudhui, msanii amefaulu kuonesha matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii yetu hasa katika suala la mapenzi na ndoa na kuonesha suluhisho la matatizo hayo.
  2. Kifani, amefaulu kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na ujenzi mzuri wa wahusika wake.
KUTOFAULU
  1. Kutumia viswahili badala ya Kiswahili sanifu (uk. 15-16)
  2. Matumizi ya Kiingereza, kwa mtu asiyejua Kiingereza atashindwa kupata ujumbe.