UTANGULIZI
Almasi za Afrika ni
diwani iliyoandikwa na Shabani Robert mwaka 1959 katika lugha ya Kiswahili na
kuitafsiri katika lugha ya Kingereza kama African Diamonds. Kila shairi
limetafsiriwa katika Lugha ya Kingereza kwa lengo la kudhihirisha
umahiri wake katika lugha hizi mbili, kuwasaidia wa geni wa utamaduni wa
Kiswahili kuzifaidi almasi hizi adimu pamoja na kuonesha namna lugha ya
Kiswahili isivyo maskini kama baadhi ya watu wanavyodhani na jinsi iwezavyo
kuchukuana vyema na lugha nyingine za Kigeni hususani Kingereza. Tafsiri hizo
siyo namna ya uandishi wa mashairi ya Kingereza. Hasha! Ushairi wa Kingereza
una namna yake ya utunzi tofauti na namna ya utunzi wa ushairi wa Kiswahili.
Kwa ufupi diwani hii inazungumzia maadili, utu wema, matendo mema, lugha ya
Kiswahili, ujasiri na kujitoa mhanga. Kwa ujumla hizi ndizo Almasi
zinazozungumziwa katika diwani hii yenye mkusanyiko wa mashairi kumi na moja
ambayo ni Mtukufu Margaret, Wajibu wetu, Sahau,Rangi Zetu, Uzuri, Mali tulizo nazo,
Kiswahili, Kiunzi chetu, Matendo, Tabia na Lugha. Shairi la Mtukufu Margaret
limeandikwa na Mwidau Ulenge ndugu yake Shaban Robert kwa ajili ya kumkaribisha
malkia wa Uingereza aliyezuru nchi ya Tanganyika mwaka 1959 wakati wa vuguvugu
la ukombozi.
UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI
A. MAUDHUI
Kwa mujibu wa Njogu na
Chimera(1999) Maudhui ni ujumbe wa jumla kuhusu matukio kitu, wahusika au hali
ya maisha kama yanavyojitokeza katika kazi ya fasihi, iwe riwaya, tamthiliya,
shairi au wimbo.
1. DHAMIRA
Wamitila(2004) anasema
kuwa dhamira ni lengo la mtunzi katika utungo wake. Lengo hili hutokeza kwa
wazo kuu ambalo hukuzwa katika utungo unaohusika kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
Dhamira Kuu
Maadili mema na Maonyo
katika Jamii
Dhamira Nyingine
i. Tabia
Njema
Suala la tabia njema
limekuwa likigusiwa na wandishi wengi. Katika Almasi za Afrika mwandishi
anaeleza kuwa uzuri wa mtu hujenwa na tabia njema na siyo sura yake. Tabia
ndiyo umfanya mtu akaheshimika au kudharaulika. Shairi la Tabia katika ubeti wa
3 linaelezea mawazo haya.
Tabia hupambanua,
Watu huwa mbalimbali,
Baadhi huchukuliwa,
Katika hadhi kamili,
We ni wa kivuli, hupita
kama ruia.
Vilevile mwandishi
anaeleza kuwa uzuri wa mtu siyo sura walas umbo lake bali ni tabia
njema.Anaeleza haya katika shairi la uzuri.Ubeti wa 2.
Uzuri kupita huu,
Katika hii dunia,
Nawapa msisahau,
Ni uzuri wa tabia,
Ni johari ya heshima
duniani kila mara.
ii. Matendo
Mema
Mtu akiwa na matendo
mema huheshimika katika jamii, hata akifa jamii yake huendelea kumbukwa na
kumuenzi. Katika shairi lamatendo ubeti wa 1 mwandishi anasema:
ROHO ivukapo ng’ambo
yasaliayo matendo,
Mema yasiyo na Kombo
hukumbukwa kwa matendo,
Mabaya yasiyo umbo
huacha nyuma uvundo,
Matendo ni kumbukumbu
ya mtu kukumbukwa.
iii. Umuhimu
wa Lugha
Shaban Robert anasema
kuwa kila lugha kote duniani ni bora na ina manufaa kwa waitumiao kwa hiyo
anasisitiza kutodharau lugha ya mtu mwingine. Anaendelea kusema kuwa mtu asiye
na lugha ni sawa na mtumwa maana hata wanyama wa porini wana lugha zao
wanazozitumia kuwasiliana.Katika sairi la Lugha Ubeti 2
anasema:
Kila lugha ni dhahabu,
hazina bora upeo,
Ni mali ya kuhesabu,
kila siku uishiyo,
Lugha haina aibu, ni
maumbile unayo,
Tena kitu maabuu,
Katika mali za leo,
Hasa wastaarabu,
kutumia wajuao,
Kwao lugha ni kitabu,
elimu na ufunuo.
Vilevile lugha ni mali
ya asili, ni tamu kwa waitumiao na ni cheo kwa mtu aitumiaye lugha husika.Ubeti
wa 6 mwandishi anasema:
Kila lugha huwa mali,
usijali wabezao,
Mali yenyewe halali,
kila mtu kuwa nayo,
Lugha mali ya asili,
mtu huzaliwa nayo,
Wala haina badili, kwa
mtu kama anayo,
Lugha isipokubali, na
akili kwenda nayo,
Maneno yako batili,
awafaamu wenzio.
iv. Umuhimu
wa Lugha ya Kiswahili
Shaban Robert ni mmoja
wa watetezi wa lugha ya Kiswahili. Katika hii anawaasa wanajamii kukipa kukipa
hadhi Kiswahili kwani ndiyo lugha mama, nyingine hazitatufaaa kwani ni za
kuazima. Katika shairi la Kiswahili ubeti wa 8 mwandishi
anasema:
Kila
mtu lugha yake, ndiyo mtumishi mwema,
Lugha
nyingine makeke, kwa nahau kuzisema,
Kila
mkuu na pake, hana hadhi akihama,
Na
Kiswahili nivike, joho lako la heshima,
Titile mama li tamu,
njingine haliishi hamu.
Hata hivyo Shaban
Robert anatambua umuhimu wa blugha za kigeni hasa kujipatia maarifa.
Anabainisha hayo katika shairi la Kiswahiliubeti wa 14.
Lugha ngeni ni elimu, hili sana
naelewa,
Sitishiwi na ngumu, kwa kujifunza
najua,
Lakini ilivyo tamu, lugha ya kulelewa,
Kusema
yanilazimu, kwa hali yoyote kuwa,
Titile
mama li tamu, jingine haliishi hamu.
v. Suala
la Elimu
Mwandishi anasisitiza
elimu kama njia ya kumkomboa mwanadamu katika hali zote za maisha ukiwemo
unyonyaji wa kikoloni. Mwandishi katika shairi la mali tulizo nazo ubeti
wa 7 anasema:
Tuna
vyuo vya elimu, huenda tukakariri,
Maji ya kunywa matamu
huburudisha sudari,
Akili zetu timamu afya
haina dosari,
Bali wachache wa ahmu
wa tendo la ujasiri.
Vilevile mwandishi
anaona kuwa kujifunza lugha ngeni pia ni njia ya kujipatia elimu. Shairi la
Kiswahili ubeti wa 14 linadokeza:
Lugha
ngeni ni elimu, hili sana naelewa,
Sitishiwi
na ngumu, kwa kujifunza najua,
Lakini
ilivyo tamu, lugha ya kulelewa,
Kusema
yanilazimu, kwa hali yoyote kuwa,
Titile
mama li tamu, jingine haliishi hamu.
vi. Ujasiri
na Kujitoa Mhanga
Mwandishi anawahimiza
watu kuwa na roho ya ujasiri na kujitoa mhanga ili kujikomboa dhidi
ya madhila ya kijamii kama vile unyonyaji wa kikoloni. Anahimiza hayo katika
shairi la Mali tulizo nazo ubeti wa 10 na 12.
10. Bila
matendo aushi, haja zetu hazijiri,
Dunia
tunayoishi, hata kitu cha hiari,
Hupata
kwa ushawishi, na bidii na dhamiri,
Hatupati kwa utashi,
usio na ujasiri.
12. Haipatikani
kitu, kama sisi si tayari,
Kutenda
wajibu wetu, kwa bidii na kwa ari,
Kushawishi
haja zetu, mpaka zikatukiri,
Na
hupata kila kitu, kama tuna ujasiri.
vii. Ubaguzi
wa Rangi
Mwandishi anawakemea
watu wenye tabia ya kubaguana wenyewe kwa wenyewe na kuhukumiana kwa kigezo cha
rangi. Anasema kuwa rangi si uchafu, si dalili ya machungu, dhambi, mapungufu
wala kashfa bali nip ambo la Mungu. Shairi la Rangi Zetu Ubeti
wa 2 na 3.
2. Hupamba
nyota na mbingu, na mawaridi nma afu,
Rangi adhama ya Mungu,
na mwilini si uchafu,
Si dalili ya machungu,
dhambi wala upungufu,
Rangi heba yake Mungu,
Mwenyezi mkamilifu.
3. Ni
urembo wake Mungu, Mwenye miliki ya sifa,
Napambo lamalimwengu,
shahada ya taarifa,
Wajinga wa ulimwengu,
rangi hudhani kashfa,
Rangi pambo lake Mungu,
si alama ya maafa.
viii. Dini
Mwandishi anawakumbusha
watu kumtumainia Mungu kwani yeye ndiye muumbaji wa vitu vyote na alitakali
liwe huwa. Maisha ya mwanadamu yapo kutokana na matakwa ya Mungu kwani yeye
huweza kulifanya fupi kuwa refu. Shairi la Rangi Zetu ubeti wa 4 na 6.
Ubeti wa 4. Twajua
mwenyezi Mungu, kwa mambo mabadilifu,
Shani zake na mizungu,
ni Bwana wa masanifu,
La ardhi na la mbingu,
neno lake husadifu,
Rangi heba yake Mungu,
mwenyezi mkamilifu.
Ubeti wa 6. Hashindwi
mwenyezi Mungu, fupi kulipa refu,
Hashindwi na
malimwengu, watawaliwa na utu,
Hashindwi katika
mbingu, kwa rain a utukufu
Rangi heba yake Mungu,
mwenyezi mkamilifu
4. UJUMBE
Wamitila (2004)
anaeleza kuwa ujumbe ni dhana ituwayo kuelezea taarifa ambazo msanii au mtunzi
hukusudia kuzifikisha kwa wasomaji wake au hadhira yake kama njia mojawapo ya
kuhakikiha kwamba dhamira yake imetimia. Ni mafunzo yanayopatikana ndani ya
kazi ya fasihi. Katika diwani hii ujumbe mbalimbali umejitokeza.
1) Uzuri wa mtu siyo umbo wala sura
yake bali ni tabia. Shairi la Uzuri
2)
Elimu ni msingi wa maendeleo katika
jamii yoyote. Shairi la Mali tulizo nazo.
3)
Ubaguzi wa Rangi haufai. Shairi la Rangi
zetu.
4)
Tuthamini lugha yetu ya Kiswahili.
Shairi la Kiswahili.
5)
Ujasiri na kujitoa mhanga ni chachu ya
maendeleo. Shairi la Mali Tulizo Nazo.
6) Tuzithamini lugha ngeni, tujifunze ili
kuongeza maarifa lakini tusizitupe lugha zetu. Shairi la Kiswahili.
7) Kusamehe na kusahau mabaya tuliyotendewa
ni muhimu. Shairi laSahau.
5. MIGOGORO
Kwa kiasi kikubwa
migogoro iliyojitokeza katika diwani hii ni ile inayomhusu mshairi mwenyewe
dhidi ya hadhira anayoiandikia. Ni baada ya kuchukizwa na mwenendo
wa jamii ukajengeka mgogoro katika nafsi yake na kuamua kuandika akiihasa jamii
kuachana na matendo maovu, tabia mbaya, chuki na woga.
6. MTAZAMO
Kwa mujibu wa Wamitila (2004)
mtazamo ni namna au jinsi mtu anavyoyachukulia mambo au anavyofikiri juu ya
jambo Fulani. Kuna mtazamo wa kimapokeo na wa kimapinduzi. Katika diwani hii
mtazamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani ameeleza mambo anuai kama ujasiri,
elimu na kujitoa mhanga ambayo ni mambo muhimu kwa jamii ili kujikomboa na adha
za maisha.
7. MSIMAMO
Ni hali ya mtunzi
kushikilia jambo Fulani kuwa ni sahihi hata kama jamii nzima ahikubaliani nalo.
Upo msimamo wa kidhanifu na wa kiyakinifu. Katika diwani hii mwandishi
anaonekana kuwa na msimamo wa kiyakinifu. Msimamo huu umejibainisha katika
mashairi ya Rangi, Kiswahili na Mali tulizo nazo.
8. FALSAFA
Wamitila (2004) anaeleza
kuwa falsafa ni mawazo aliyo nayo mwandishi juu ya maisha ambayo hujitokeza
katika maandishi yake. Mawazo hayo anayaamini na kuyashikilia kama ukweli
unaoongoza maisha yake na ya jamii kwa ujumla. Katika diwani hii mwandishi
amejenga falsafa yake juu ya wema katika maisha kama ndio msingi wa maisha bora
miongoni mwa wanadamu. Falsafa hii inajidhihirisha katika mashairi ya Wajibu
wetu, saahu, Rangi zetu, Tabia na Matendo.
B. FANI
Kwa mujibu wa Senkoro (1982)
fani ni ufundi wa kisanaa anaoutumia msanii katika kazi yake.
1. WAUSIKA
Baadhi ya wahusika
aliowatumia msanii katika kazi hii ni hawa wafuatao:
i. Malkia
Margaret. Shairi la Mtukufu Margaret
ii. Wamasai,
Wambulu, Waha na Wamakonde. Shairi la Lugha.
iii. Mama.
Shairi la Kiswahili.
iv. Gavana.
Shairi la Mtukufu Margaret.
2. MUKTADHA
Mandhari ya diwani hii
ni nchini Tanganyika kipindi cha utawala wa Waingereza. Harakati za kupigania
uhuru zilikuwa zimeshtadi.
3. MUUNDO
Senkoro (1982) anaeleza
kuwa muundo ni mpangilio na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na
matukio. Katika ushairi muundo unahusisha idadi ya mistari, vipande au
mishororo, beti, urari wa vina na mizani pamoja na kibwagizo.
i. Idadi
ya Mishororo
a) Tarbia(Mishororo
4): Mashairi la Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi Zetu, Mali
tulizo
nazo na Matendo.
b) Takhmisa
(Mishororo 5): Mashairi ya Uzuri, Kiswahili na Tabia.
c) Usita
(Mishororo 6): Shairi la Wajibu Wetu.
ii. Idadi
ya Beti
a) Beti
32: Shairi la Mtukufu Margaret. Uk. 4-18
b) Beti
31: Shairi la Kiswahili. Uk. 42
c) Beti
14: Shairi la Mali Tulizo Nazo. Uk. 36 na Rangi
Zetu. Uk. 30
d) Beti
12: Shairi la Lugha. Uk. 70
e) Beti
8: Shairi la Matendo. Uk. 64
f) Beti
5: Shairi la Tabia. Uk. 68 na Uzuri Uk.
28
g) Beti
4: Shairi la Kiunzi Chetu. Uk. 62
h) Beti
2: Shairi la Wajibu Wetu. Uk. 20
iii. Urari
wa Vina na Mizani
Katika mashairi
ya Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi Zetu, Mali Tulizo Nazo na Matendo vina
vya kati na vya mwisho vinafanana kwa kila shairi. Idadi ya mizani ni 16 kwa kila
mshororo.
iv. Kibwagizo
Mshairi ametumia vina
vya aina mbili. Kibwagizo cha kawaida na Kinabahari.
a) Kibwagizo
cha Kawaida
Kibwagizo cha namna hii
hubadilika badilika kila ubeti. Katika diwani hii kina cha namna hii kimetumiwa
katika mashairi ya Mali Tulizo Nazo Uk. 36, Wajibu
Wetu Uk. 20, Uzuri Uk. 28, Tabia naLugha.
b) Kinabahari
Hiki hakibadiliki, ni
kilekile tangu ubeti wa Kwanza mpaka wa Mwisho. Kibwagizo cha namna hii
kimejitokeza katika mashairi yaMatendo Uk. 64, Kiswahili Uk.
42 na Mtukufu Margaret (Uk. 4)
4. MTINDO
Kwa mujibu wa Njogu na
Chimera(1999) mtindo ni tabia ya utungaji inayompambanua mtunzi mmoja na
mwingine. Mitindo iliyotumika katika diwani hii ni hii ifuatayo:
i) Mtindo
wa Kimapokeo
Hii ni aina ya utunzi
wa mashairi yenye kutii sheria za utunzi wa mashairi kama vile urari wa vina na
mizani, mishororo mine katika ubeti na kibwagizo aghalabu kinabahari. Kwa
kiwango kikubwa mwandishi wa diwani hii ametumia mtindo wa kimapokeo. Mashairi
kama Mtukufu Margaret, Sahau, Rangi zetu, Mali tulizo nazo naMatendo yote
yametii kanuni hii ya uandishi.
ii) Mtindo
wa Kisasa
Mtindo wa aina hii
hautii sheria za utunzi kama zilizoelezwa hapo juu. Mashairi yaliyofuata mtindo
huu katika diwani ya Almasi za Afrika ni Wajibu wetu na Uzuri.
iii) Mtindo
wa Kutumia Herufi Kubwa
Mbinu Hii imetumika kwa
neno la kwanza la mshororo wa kwanza kwa kila ubeti wa kwanza katika mashairi
yote kumi na moja.
iv) Mbinu
ya Mchezo wa Maneno
Mbinu hii imetumika kwa
madhumuni ya kufafanua kile kinachosemwa kwa kuongeza vionmjo. Mbinu hii
imetumika katuka shairi la Kiswahili.
Mfano
wa neno jambo, mkato wa una jambo,
Jawabu
lake sijambo, tafsiri sina jambo,
Tazameni
hili pambo, lizidishavyo urembo,
Wa
kuuliza sana mambo, kwa usemi wenye umbo,
Titile
mama li tamu, jingine haliishi hamu.
5. MATUMIZI
YA LUGHA
Kwa ujumla mshairi
ametumia lugha nyepesi na ya kueleweka kwa wasomaji.
i. Matumizi
ya Methali
a) Mtenda
mema duniani, zawadi yake ni thawabu. Shairi la Kiswahili.
b) Bila
matendo aushi haja zetu hazijiri. Shairi la Mali tulizo nazo.
c) Titi
la mama ni tamu hata kama la mbwa. Shairi la Kiswahili.
ii. Matumizi
ya Tafsiri
Mashairi yote kumi na
moja yametafsiriwa katika lugha ya Kingereza ili kupanua wigo wa hadhira, ili
hata hadhira isiyofahahamu Kiswahili mwisho wa mwisho iweze kunufaika na Almasi
hizi adhimu. Pia mshairi alitaka kudhihirisha mwingiliano uliopo baina ya
Kiswahili na lugha ngeni hususani Kingereza.
iii. Tamathali
za Semi
a) Tashbiha
Wamitila(2004) anaeleza
kuwa tashbiha ni ulinganisgi wa moja kwa moja na gutambulisgwa kwa viunganishi
kama, mithili, mithili ya..,sawa na……nk.
Ktika diwani hii
tashbiha zimejitokeza zaidi katika shairi la Sahau.
Ni
njema kama dhahabu tabia ya kusahau.
Pia katika shairi la Tabia
Humea
kwa kupendeza kama yenye manukato,
Humea
kwa kuchukiza kama madhambi.
b) Sitiari
Msokile(1993) anaeleza
kuwa sitiari ni tamathali ya usemi ambayo kwa kawaida huhusisha matendo, kitu
au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti. Ulinganisho huu unahusisha misingi au
sifa zinazopatikana katika vitu vyote viwili ingawa sifa hizo haziwi wazi kati
ya kitu na kitu.
Katika diwani hii
Sitiari zimetumika katika shairi la Sahau.
Sahau
kwetu dhahabu tena ni kitu kikuu,
Kumbukumbu
ni wajibu, na faraja ni sahau,
Mashaka
yanapoghibu, roho zinakwenda juu,
Faraja
kubwa ajabu, kwa mtu ni kusahau.
c) Tashhisi
Mulokozi(1996) anaeleza
kwamba hii ni tamathali ya kukipa uhai na tabia za kibinadamu kitu ambacho
hakina uhai au tabia hizo.
Mifano ya tashhisi
zilizotumika katika diwani hii ni katika shairi laKiswahili.
Kiswahili
kikikopa, na lugha nyingine pia,
Ambazo
zimenenepa, jambo hili hutumia,
Ama
sivyo zingetupwa, kwa kukosa manufaa,
Kiswahili
kikikopa, si hila ndiyo tabia,
Titile
mama li tamu, jingine haliishi hamu.
d) Takriri
Takriri ni mrudiorudio
wa neno au wazo Fulani kwa lengo la kuweka msisitizo. Katika shairi la Lugha mwandishi
ametumia takriri.
Haihati, haihati…
e) Nidaa
Msokile(1993) anasema
kuwa nidaa ni msemo ambao unaonesha kushangazwa kwa jambo Fulani. Huambatana na
alama ya mshangao kukubali jambo, kuchukia ama kuonesha heshima kuu. Nidaa
zilizotumika katika diwani hii zinapatikana hasa katika shairi la sahau:
Mangapi
ya kuhesabu hapa chini licha juu!
Ya
hatia na thawabu na dhuluma na dharau!
Afadhali
kuwa bubu au ndani ya sahahu!
Faraja
kubwa ajabu kwa mtu ni kusahau!
iv. Ishara
na Taswira
Taswira hurejelea picha
ijengekayo akilini mwa msomaji kutokana na athali za matumizi ya lugha katika
kazi ya fasihi. Hugusa hisia za ndani za msomaji na kumfanya achukie,kupenda,
kukasirika, kucheka, kupata kichefuchefu na ahta kuogopa. Baadhi ya taswira
zilizotumika ni:
a) Almasi
Ni madini ghali na
adimu. Katika diwani hili limetumika kitaswira kumaanisha tabia njema, matendo
mema, Lugha ya Kiswahili, ujasiri na kujitoa mhanga ambavyo kimsingi vinapendwa
katika ustawi wa jamii bora kama yalivyo madini ya almasi.
b) Titi
la mama ni tamu hata kama la mbwa. Shairi la Kiswahili.
Titi la mbwa halipendwi
na binadamu, siyo tamu kwa binadamu ila ni tamu sana kwa watoto wa mbwa. Mwandishi
ametumia taswira hii kuihimiza jamii ya waswahili umuhimu wa kuithamini lugha
ya Kiswahili licha ya kwamba wengine wasiojua utamu wake wanaweza kuwa
wanaibeza.
KUFAULU NA KUTOKUFAULU
KWA MWANDISHI
KIFANI
Mwandishi amefaulu
katika matumizi ya mtindo, muundo na matumizi ya lugha nyepesi yenye kueleweka
vema kwa hadhira pana ikichagizwa na tafsiri ya Kingereza. Vipengele vya fasihi
ya Kijadi vimehusishwa kama methali na misemo ili kudhihirisha uhalisia wa
fasihi ya mwafrika.
KIMAUDHUI
Mwandishi amefaulu kwa
kiasi kikubwa kuifikishia hadhira yake ujumbe ambao ni fawafu katika maisha ya
kila siku kwa njia ya ushairi.
JINA LA KITABU
Almasi ni madini yenye
thamani kubwa yanayopatikana kwa baadhi ya maeneo hapa Afrika. Yanatamanika kwa
watu wengi wenye kutambua thamani yake. Kwa kutumia madini haya historia ya mtu
binafsi hata taifa au mataifa huweza kubadilika haraka sana kutoka hali duni
kwenda hali bora kabisa. Sifa hizo za Almasi ni sawa na zile za lugha yetu ya
Kiswahili inayoongelewa katika maeneo mengi hapa barani Afrika. Vilevile tabia
njema, utu wema, upole, unyenyekevu, kusameheana na kusahau mabaya
tuliyotendewa vyote hivi hujenga utu wa mwafrika na kulinganishwa thamani yake
na madini ya Almasi. Hivyo basi kwa muktadha huu jina Almasi za
Afrikalinasadifu yote yaliyomo ndani ya kitabu.
HITIMISHO
Kwa hakika diwani hii
ni kurunzi fawafu ya kuyamulika mapito ya hadhira ya mwandishi wa diwani hii
ambayo ni Tanzania ya sasa na Afrika kwa ujumla. Ni diwani iliyoshiba kwa wingi
na uzito wa maadili, maonyo na umuhimu wa mambo anuai ambayo mahenga
ameikirimia hadhira yake. Hivyo hii ni diwani bora.
MAREJEO
Msokile, M.(1993) Misingi
ya Uhakiki wa Fasihi. Dar es Salaam, EAEP
Mulokozi,
M.M.(1996) Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam, TUKI
Njogu, K. na R.
Chimera(1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi,
Kiswahili Tertiary Publishing Project.
Robert, S.(1959) Almasi
za Afrika. London, Nelson.
Senkoro,
F.E.M.K.(1982) Fasihi. Dar es Salaam, DUP
Wamitila,K.W.(2004) Kichocheo
cha Fasihi:Simulizi na Andishi.Nairobi, Focus Publications Ltd
|