Wimbo wa “Kwangwaru” ni wimbo ulioimbwa na Harmonize akishirikiana na Diamond Platnumz wote ni wasanii kutoka lebo ya WCB Tanzania. Tahakiki hii imejikita zaidi katika vipengele vya maudhui na siyo vipengele vya fani.
DHAMIRA KUU
Dhamira kuu katika wimbo wa Kwangwaru ni MAPENZI.
Msanii anajielekeza kumpamba na kumwelezea mpenzi wake maneno matamu kuhusu mapenzi. Msanii anamweleza na kumuasa mpenzi wake mambo kadha wa kadha ambayo msanii anaamini akifanyiwa na mpenzi wake ataridhika na kutulia zaidi ya yote kudumu katika mapenzi. Msanii anaeleza ujuzi ambao mwanamke wake akimpatia faragha atadumu na kuyafanya mahusiano yao yawe yenye amani.
Msanii anaanza kwa kumpatia mpenzi wake maneno matamu na ahadi kedekede. Msanii anasema kama angekuwa na pesa angeweza kumhonga mpenziwe vitu vya thamani sana. Anamuasa mpenzi wake asilaghaike na wenye pesa kwani wanamlaghai tu, msanii anasema “…usiwaamini, ukishawapa wanakwenda…”
Msanii anajiapiza kwa mpenziwe kwamba anampenda na hakuna atakaye mpenda zaidi yake.
Msanii anasema “…wakija wapoteze jifanye kama huwaoni…”. Msanii anamuasa mpenzi wake asijaribu kumsaliti wala kumuudhi kwani msanii anakiri wazi kuwa hana moyo wa msamaha endapo atasalitiwa hili linajidhihilisha pale ambapo msanii anasema “… moyo wangu mwarobaini u mchungu ukiudhiwa…samehe mara sabini huo uzungu sijaumbiwa…”
Msanii anajaribu kuishirikisha jamii ujuzi wake katika mapenzi ya faragha kwa kutumia lugha ya mnato na ya mficho mno. Msanii anatumia tafsida kuelezea mapenzi ya faragha na zaidi tendo la “ngono”.
Msanii anatumia sentensi kama
“… nikumbate baridini…”
“…nipatie vya kitandani nipe mpaka kwenye kiti…”
“…kitandani nikoleze kwa miuno ya kingoni…”
“…kisha uniongeze ulivyofunzwa unyagoni…”
“…weka mate niteleze kama nyoka pangoni…”.
Msanii anaeleza yote hayo ambayo anaamini kama atafanyiwa na mpenzi wake basi atatulia na hataweza kumsaliti.
MAPENZI YA DHATI
Dhamira ya mapenzi ya dhati imejitokeza kwa msanii kumuasa mpenzi wake asimsaliti kama yeye ambavyo hata msaliti. Msanii anahitaji kuthaminiwa na kuhudumiwa ipasavyo na mpenzi wake na kwamba yupo tayari kutoa chochote kile ili tu kudumisha mahusiano hayo.
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Msanii amemchora mwanamke kama chombo cha starehe cha kumfurahisha mume. Mambo mengi ambayo anayahitaji msanii kutoka kwa mpenzi wake ni mambo ambayo yanalenga zaidi kumstarehesha mwanaume na kumridhisha kimapenzi. Mwandishi anamtaka mpenzi wake aoneshe ujuzi wa hali ya juu aliofunzwa unyagoni tena ” ujuzi wa kingoni”.
Msanii anamchora mwanamke kama mtu mwenye tamaa ya pesa na mali na ambaye anashawishika kirahisi kwa umaarufu wa mwanaume. Hili linajidhihirisha pale msanii anaposema kama angekuwa na pesa angemhonga vya thamani pia anasema “…ama niwe fundi wa kuigiza kama kanumba, masanja, joti usiwe mbali nami…”.
IMANI NA FALSAFA YA MSANII
Msanii anaamini kama mwanamke na mwanaume watatimiza wajibu wao ipasavyo katika mapenzi basi mapenzi yatadumu na hakutakuwepo na kusalitiana.
KUFAULU KWA MSANII
Msanii amefaulu kuelezea hisia zake kwa namna ya pekee mno. Ujumbe wake rahisi kueleweka kwa jamii ya sasa ambayo wengi wa wapenzi wa kazi zake ni vijana hivyo dhamira ya mapenzi ni muafaka japo angeweza kuzungumzia dhamira zingine kama uchapakazi na kujituma.
KUTOFAULU KWA MSANII
Msanii amejenga imani yake katika dhana ya kusadikika kwamba mwanaume anatulia katika mapenzi kwa kuridhishwa na mpenzi wake jambo ambalo halina ushahidi wa kutosha kuwa wanaume wanaosaliti mahusiano yao hawaridhishwi.
Msanii anasema kwamba hawezi kusamehe saba mara sabini na kwake anaona kufanya hivyo ni ” uzungu”. Hii inaweza kuleta picha ya kwamba msanii anahamasisha watu kukosa uvumilivu na ustahimilivu katika mapenzi.
Wanaisimu wengi wamejaribu kufasili dhana ya isimu .kwa mfano , Richards et al (1985) anasema kuwa :
Isimu ni mtalaa ambao huchunguza lugha kama mfumo wa mawasiliano ya mwanaadam (TY)
Hartman (1972) naye anasema:
Isimu ni eneo maalum la mtalaa ambalo lengo lake huwa ni kuchunguza lugha .Wanaisimu huzichunguza lugha zikiwa ni nyenzo muhimu za mawasiliano ya mwanaadamu. (TY).
Verma et al (1989)wanasema kuwa isimu ni sayansi kwa sababu hufuata mbinu za kimsingi za utafiti wa kisayansi.Mbinu hizi huhusisha sifa zifuatazo.
1. Uchunguzi uliodhibitiwa
2. Uundaji wa haipothesia
3. Uchanganuzi
4. Ujumlishi
5.Utabiri
6.Majaribio na uthibitishaji
7. urekebishaji au ukataaji wa haipothesia
Hii ni kusema kuwa isimu haichunguzi lugha kiholela bali kwa uratibu na mwelekeo maalumu.katika kuchunguza lugha ,wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama zifanyavyo sayansi zingine.
TUKI (1990) wanasema kwa ufupi kabisa sana
Isimu ni sayansi ya lugha.
MATAWI YA SAYANSI
Isimu historia
Isimu fafanuzi
Isimu linganishi
isimu jamii
isimu tumizi
isimu nafsia.
USAYANSI WA ISIMU
Utoshelevu wa kiuteuzi
Utoshelevu wa kiuchunguzi
utoshelevu wa kiufafanuzi
Uchechevu
Uwazi
MISINGI YA USAYANSI WA ISIMU
Uwazi
Utaratibu
Urazini
MAREJEO
Mgullu,R.S. (1999) Mtalaa wa Isimu Fonetiki,Fonolojia na Mofonolojia ya Kiswahili.Longhorn Publishersar es salaam,Tanzania.
Habwe,J. na wenzake (2004) Misingi ya sarufi ya kiswahiliPhoenix Publishers :Nairobi,Kenya.
KWA mujibu wa maelezo ya wataalam kuhusu dhana ya isimu, ni bayana kwamba isimujamii ni taaluma mojawapo ya isimu inayochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii anuwai na uhusiano baina yake.
Tawi la isimujamii huchunguza matumizi ya lugha katika mazingira tofauti, aina mbalimbali za lugha na mazingira yake pamoja na uhusiano wa lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.
Hata hivyo, ni vyema kuelewa kwamba bila kuwepo kwa jamii hakuna lugha na bila kuwepo kwa lugha hakuna jamii.
Hii ni kumaanisha kwamba lugha na jamii hukamilishana ili kukidhi haja za mawasiliano.
Isimu ni taaluma pana na kutokana na hali hii inaoana na kuingiliana na taaluma nyinginezo jinsi ifuatavyo:
Isimu na Sosholojia
Sosholojia ni taaluma inayoshughulikia uchunguzi na uchanganuzi wa matabaka na makundi ya watu katika jamii.
Kuna makundi tofautitofauti katika jamii kwa mfano: matabaka ya wanaojimudu kifedha na tabaka la wachochole, tabaka la watawala na wanaotawaliwa na kadhalika.
Uhusiano unaojitokeza baina ya isimujamii na isimu sosholojia ni kwamba katika jamii kuna tabaka mbalimbali na kila tabaka lina namna tofauti tofauti ya kutumia lugha kulingana na mazingira. Kwa mfano vijana wana lugha wanayotumia ambayo ni tofauti na lugha inayotumiwa na wazee.
Vilevile, tabaka la wasomi lina lugha tofauti inayotumika na kueleweka baina yao.
Hivyo basi, ni muhimu kwa mwanaisimu yeyote yule kuyafahamu vyema matabaka yaliyo katika jamii yake na jinsi lugha inavyotumika katika matabaka hayo.
Isimujamii na Anthropolojia
Anthropolojia ni taalama inayohusisha kuchunguza mila na desturi za jamii fulani na jinsi zinavyotumika katika maisha yao ya kila uchao.
Uhusiano wa isimujamii na isimu anthropolojia ni kuwa matumizi ya lugha katika jamii huambatana na mila na desturi zilizomo katika jamii ili kutumia lugha ambayo hujitokeza katika msamiati wa lugha husika.
Kwa mfano, katika jamii yenye utamaduni wa upashaji tohara na ukeketaji, kuna msamiati wa kurejelea kwa aliyetahiriwa na yule ambaye bado hajapitia hatua hiyo.
Hali hii ni tofauti na jamii ambazo hazina utamaduni.
Hivyo basi baadhi ya maeneo lugha inamotumika katika mazingira fulani huonekana ya kawaida ilhali katika mazingira mengine huonekana kama ukiukaji wa kaida za jamii husika.
Marejeo
Msanjila, Y. P. (1990). “Problems of Teaching Through the Medium of Kiswahili in Teacher Training Colleges in Tanzania”. Journal of Multilingual and Multicultural Development II/4:307 – 318
Mtembezi, I. J. (1997). “Njia Mbili Zilimshinda Fisi: Tanzania na Suala la Lugha ya Kufundishia”. Dar es Salaam: BAKITA.
Mulokozi, M. M. (1991). “English versus Kiswahili ni Tanzania’s Secondary Education”. Swahili Studie Ghent.