|
Matatizo ya Tafsiri katika Matini za Kitalii Nchini Tanzania
Na: Hadija Jilala
Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu sana katika maendeleo ya nchi na ni sekta ambayo huliingizia taifa pato la kiuchumi. Sekta hii huhusisha watu wa jamii mbalimbali duniani, watu wenye tofauti za kiutamaduni, kiuchumi, kiitikadi, kijamii na wanaozungumza lugha tofauti. Pamoja na hayo, utalii ni eneo ambalo bado halijafanyiwa kazi vya kutosha na watafiti wa lugha na tafsiri ili kuona ni jinsi gani lugha na tafsiri vina mchango katika ukuzaji wa sekta ya utalii nchini Tanzania. Makala haya basi yanachunguza matatizo ya tafsiri katika matini za kitalii zilizotafsiriwa kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza. Lengo ni kubainisha matatizo ya tafsiri katika matini za kitalii na kutoa mapendekezo ya namna ya kuyakabili matatizo hayo ili kuleta ufanisi wa mawasiliano.
Utangulizi:
Hali ya Sekta ya Utalii Nchini Tanzania
Kwa mujibu wa TUKI (2004:445) utalii ni hali ya kusafiri mbali au kuvinjari huku na huko ili kufurahia mandhari. Upo utalii wa aina mbalimbali kama vile wa asili, kiutamaduni na mambo ya kale. Makala haya yanaangalia utalii wa kiutamaduni. Utalii wa kiutamaduni unajumuisha mambo mbalimbali kama vile kazi za sanaa, urithi wa fasihi simulizi, majumba ya makumbusho, kazi za mikono, matamasha ya sanaa na majengo ya kihistoria (Bennett, 1995).
Kwa hiyo, makala haya yanashughulikia matini zinazopatikana katika majumba ya makumbusho ambayo yanahusika na kuhifadhi vivutio vya utalii wa kiutamaduni. Kulingana na Benavides (2001) utalii una nafasi kubwa katika uchumi wa Tanzania. Ni moja kati ya vyanzo vikuu vya fedha za kigeni na unatoa nafasi za ajira kwa jamii. Hivyo basi, inaonekana kuwa utalii ni tasnia muhimu sana katika kuongeza upatikanaji wa kazi, kuondoa umaskini na upatikanaji wa fedha za kigeni.
Kufikia mwaka 2015 pato la utalii kwenye uchumi wa taifa la Tanzania linategemewa kufikia dola za Kimarekani milioni 3,699.4. Hata hivyo, serikali inapopanga kuendeleza na kuutangaza utalii wa Tanzania, inatakiwa pia kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili na
za kiutamaduni.
Kutokana na umuhimu wa sekta ya utalii nchini Tanzania, ipo haja ya kuwa na na vyanzo vya taarifa ambavyo vinafikisha mawasiliano sahihi kwa wageni ili kutangaza vivutio vya utalii na utamaduni wa jamii kwa ujumla. Kuwepo kwa vipingamizi vya mawasiliano huweza kuharibu mawasiliano na hata kupoteza idadi ya wageni wanaofurahia utalii wa nchi. Moja ya njia ya kufikisha mawasiliano kwa watalii ni tafsiri.
Tafsiri katika utalii hutumika kama daraja la mawasiliano linalounganisha watu wa jamii na tamaduni tofauti. Si kila tafsiri inaweza kufikisha mawasiliano; kwa sababu zipo tafsiri ambazo zinaweza kupotosha ujumbe na maana iliyokusudiwa na hatimaye kupindisha mawasiliano. Kwa maana hiyo, ipo haja ya kuchunguza
ufanisi wa mawasiliano katika tafsiri za matini za kitalii ili kuona ni kwa jinsi gani matini hizo zinafanikisha mchakato wa mawasiliano. Kwa hiyo, makala haya yamelenga kubainisha na kujadili matatizo ya tafsiri katika matini za kitalii zilizotafsiriwa kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza na kutoa mapendekezo ya jinsi gani tunaweza kuyakabili matatizo hayo ili kuwa na ufanisi wa mawasiliano katika utalii.
Data za makala haya zilikusanywa katika utafiti uliofanyika Mei 2012 hadi Oktoba 2012 katika Makumbusho za Taifa, Nyumba ya Utamaduni, na Kijiji cha Makumbusho zote za jijini Dar es Salaam. Vilevile, Makumbusho ya Majimaji yaliyopo Songea na Makumbusho ya Mwalimu J. K. Nyerere yaliyopo Butiama mkoani Mara. Aidha, data za utafiti huu zilikusanywa kwa kutumia mbinu nne ambazo ni: usomaji wa machapisho, usaili, dodoso na uchunguzi ushiriki. Mbinu ya usomaji wa machapisho, ilitumika kukusanya na kuchambua matini za kitalii zilizotafsiriwa kutoka lugha ya Kiswahili kwenda katika lugha ya Kiingereza. Matini hizo ni lebo zilizobandikwa katika vifaa na maeneo yaliyopo Makumbusho, vitabu vya mwongozo kwa watalii na vipeperushi. Kwa upande mwingine, mbinu za dodoso na usaili zilitumika kwa waongozaji wa watalii (12), wafasiri wa matini za kitalii (12) na wanafunzi (15) wa programu ya uzamili wa kozi ya tafsiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nadharia ya Skopos
Makala haya yanatumia nadharia ya Skopos kama kiunzi cha uchunguzi na uchambuzi wa data za tafsiri ya matini za kitalii. Hii ni nadharia ya tafsiri ambayo ilianzishwa na Hans. J. Vermeer miaka ya 1970 huko Ujerumani. Msingi wa nadharia hii ni kuiona tafsiri kama utekelezaji wa kitendo kwa kuzingatia matini asilia. Wafuasi wa nadharia hii wanaamini kwamba, kila matini hutafsiriwa kwa lengo fulani na kwa hiyo tafsiri lazima itimize lengo hilo. Kwa maana hiyo, tafsiri huzalishwa kwa ajili ya hadhira mahususi, kwa lengo mahususi na muktadha maalumu (Vermeer, 1989a). Nadharia hii hujikita katika kutathmini matini kwa malengo maalumu ambayo yanapelekea kukamilisha dhima sawa katika utamaduni chanzi na utamaduni lengwa. Hivyo, kulingana na mkabala huu, tafsiri nzuri ni ile inayoruhusu hadhira lengwa kupata tafsiri yenye ushikamani na matini chanzi (Lauscher, 2000).
Kulingana na Vermeer (1989a) lengo la nadharia ya Skopos ni kuielezea shughuli ya tafsiri katika mtazamo wa lugha lengwa. Kwa ujumla nadharia hii imejikita katika malengo ya tafsiri ambayo huukilia mbinu na mikakati ya tafsiri inayotumika katika kutoa matokeo stahiki ya kidhima (Nord, 2007). Aidha, nadharia hii inaakisi uhamishaji wa jumla wa kiisimu wa nadharia rasmi ya tafsiri kwenda katika dhana ya tafsiri iliyojikita zaidi kwenye dhima na utamaduni-jamii (Gentzler, 2001).
Nadharia hii ina kanuni mbili: kanuni ya ushikamani na kanuni ya uaminifu. Kanuni ya ushikamani ina maana kuwa matini lengwa lazima iwe na maana kwa hadhira lengwa katika utamaduni wa lugha lengwa na katika muktadha wa kimawasiliano ambao matini lengwa itatumika. Kwa upande mwingine, kanuni ya uaminifu ina maana kuwa lazima kuwapo ushikamani wa kimatini baina ya matini lengwa na matini chanzi ambao ni sawa na usahihi wa matini chanzi.
Sababu ya kutumia nadharia hii ni kwamba, ni nadharia ambayo inaitazama tafsiri kama tendo lenye lengo maalumu kwa hadhira na kwa vile tafsiri ya matini za kitalii hulenga kufanikisha mawasiliano baina ya hadhira ya lugha za tamaduni mbili tofauti, nadharia hii imetumika kuchunguza na kujadili endapo lengo hilo linafikiwa au
la. Aidha, makala haya yametumia kanuni za nadharia ya Skopos, yaani kanuni ya ushikamani na kanuni ya uaminifu, kubainisha na kujadili matatizo ya tafsiri ya matini za kitalii kutoka katika lugha ya Kiswahili kwenda katika lugha ya Kiingereza; na hivyo kuonesha ni jinsi gani ushikamani wa maana ya matini chanzi unafikiwa katika matini lengwa. Nadharia hii pia imetumika katika kupendekeza namna bora ya kukabiliana na matatizo ya tafsiri ili kuwa na ushikamani wa maana na ujumbe baina ya matini chanzi na matini lengwa na hatimaye kufanikisha mawasiliano kwa hadhira lengwa.
Lengo la Kutafsiri Matini za Kitalii
Tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka katika lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana na hayo katika lugha nyingine (lugha lengwa) (Catford, 1965; Newmark, 1988; Mwansoko, 1996; Ordudary, 2007; Venuti, 2008 na House, 2009). Ukichunguza fasili ya tafsiri inayotolewa na wataalamu hao, utaona kuwa kuna mambo ya msingi ambayo yanajitokeza kujenga fasili hiyo. Haya ni pamoja na suala la ulinganifu, maana na ujumbe. Hii ina maana kwamba, tafsiri inapaswa kuwasilisha kwa hadhira lengwa maana na ujumbe
ulio sawa na ule uliowasilishwa na matini chanzi kwa hadhira chanzi. Tafsiri katika jamii ina dhima mbalimbali: kwanza ni daraja la mawasiliano ambalo linaunganisha jamii mbalimbali za watu wanaotumia lugha zinazotofautiana. Vilevile, ni njia ya mawasiliano, nyenzo ya kueneza utamaduni kutoka jamii moja hadi nyingine, mbinu mojawapo ya kujifunza lugha za kigeni na kiliwazo cha nafsi (Newmark, 1988; Mwansoko, 1996).
Tafsiri katika utalii ni taaluma ya msingi na yenye umuhimu mkubwa. Umuhimu huu unatokana na sababu kwamba, katika maeneo ya utalii matini hutafsiriwa ili kukidhi mahitaji ya kimawasiliano kwa watu wanaotoka katika jamiilugha na tamaduni tofauti. Vermeer (1989a) anasisitiza kwamba mchakato wa kutafsiri matini ya aina yoyote ile, hufanyika kwa lengo maalumu na lazima tafsiri itimize lengo hilo (Reiss na Vermeer, 1984). Matini za kitalii kama ilivyo matini zingine hutafsiriwa kwa lengo la kutoa maelekezo na kutoa taarifa muhimu kwa watalii ili waweze kuelewa vivutio vya kitalii vilivyopo katika nchi waliyoitembelea na kufahamu utamaduni wa jamii hiyo. Tafsiri ya matini za kitalii ni aina mojawapo ya tafsiri za matangazo. Matini za aina hii hufanyika kwa lengo la kutoa taarifa na ujumbe kwa hadhira lengwa, kuelimisha juu ya masuala ya jamii chanzi kwa jamii lengwa na kutoa taarifa za matangazo ya biashara na utamaduni. Matini za kitalii zinatoa taarifa zenye dhima tatu, yaani dhima elezi, dhima arifu na dhima amili (Sanning, 2010).
Kwa hiyo, ili tafsiri iweze kufikia malengo hayo, nadharia ya Skopos inasisitiza kwamba, katika tafsiri lazima kuwepo na ushikamani wa maana na ushikamani wa matini. Kwa maana hiyo, mfasiri hujaribu kuzalisha athari sawa kwa hadhira lengwa na ile iliyozalishwa na matini asilia kwa wasomaji wa lugha chanzi. Mathalani, Jin Di na Nida (1984: 102) wanasema, wasomaji wa Kichina huweza kuelewa matini asilia zilizoandikwa kwa lugha ya Kichina kwa sababu wanachangia na mwandishi wa matini hiyo uelewa wa lugha, uzoefu na maarifa ya utamaduni uliozalisha matini hiyo.
Kwa upande mwingine, tofauti za kiutamaduni huwazuia wasomaji wa kigeni kuelewa vema masuala ya kitalii, vitu na vifaa vilivyopo katika maeneo ya utalii. Kwa mfano, majina ya watu, vitu ama vifaa vya kitalii, taarifa za kihistoria na utamaduni. Kwa maana hiyo, mfasiri lazima atumie mbinu bora za kutafsiri ili kupunguza tofauti hizo kwa lengo la kumsaidia msomaji kuelewa ujumbe unaowasilishwa na vivutio vya kitalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali. Maeneo hayo ya kitalii ni kama vile majumba ya makabila ya jamii mbalimbali (aina ya nyumba, vifaa vya ujenzi, mtindo wa ujenzi na dhima ya nyumba), mavazi, vyakula, vinywaji, na vifaa vinavyotumika katika jamii hiyo kama vile: vifaa vya nyumbani, matambiko, uganga, uhunzi, kilimo, ufugaji, silaha za kivita, uwindaji na ulinzi, na fasihi ya jamii hiyo.
Yan na Naikang (2011) wanaeleza kuwa lengo la vifaa vya kitalii ni kuvutia wageni, kuwapa hamu ya kutembelea maeneo ya kitalii na kufurahia matembezi yao. Hivyo basi, dhima arifu ni muhimu sana katika utalii. Hata hivyo, lengo hili linaweza kufikiwa kwa kutoa usuli wa taarifa. Kabla watalii hawajaenda kutembelea vivutio vya kitalii huhitaji kupata taarifa zinazohusiana na makusudio ya utalii. Maelezo toshelevu, angavu na yanayovutia huwapa nguvu watalii ya kutembelea eneo la utalii. Kwa maana hiyo, dhima arifu ni muhimu sana. Kwa upande mwingine, dhima elezi haitakiwi kudharauliwa katika utalii. Kwa kusoma matini za kitalii zilizotafsiriwa, watu wanaweza kuhisi sifa za taifa na makaribisho ya wenyeji wa nchi husika kwenye vitabu vya miongozo ya watalii.
Kutokana na mjadala huu, tunaweza kusema kwamba matini za kitalii hutafsiriwa kwa lengo na dhima maalumu. Ni wajibu wa mfasiri kuhakikisha lengo hilo linatimia kwa walengwa wa matini hizo ambao ni watalii. Kwa hiyo, matini za kitalii zinapaswa kutimiza lengo la kimawasiliano kwa watalii ili waweze kuelewa vivutio vya kitalii vilivyopo nchini.
Tafiti kuhusu Tafsiri katika utalii
Utalii Tafsiri katika utalii ni eneo ambalo limeshughulikiwa na baadhi ya wanazuoni nje ya Tanzania kwa kutumia lugha, muktadha na mitazamo tofauti (Nan, 2005; Su-zhen, 2008; Baolong, 2009; Smecca, 2009 na Mohammad, 2010). Wapo watafiti ambao wamefanya utafiti kuhusu mbinu za kutafsiri matini za kitalii. Kwa mfano, Nan (2005) katika makala yake kuhusu matangazo ya utalii amebainisha mbinu za kutafsiri matangazo ya utalii kuwa ni urudiaji, ukuzaji na unyumbukaji. Mtafiti mwingine, Su-zhen (2008) ameandika makala kuhusu nadharia ya Skopos na mbinu za kutafsiri elementi za kiutamaduni katika matini za kitalii. Katika makala hayo, anapendekeza mbinu za kutafsiri matini za kitalii ikiwa ni pamoja na; mbinu ya tafsiri sisisi, mbinu ya unukuzi, mbinu ya unukuzi na tafsiri sisisi, na mbinu ya unukuzi na muhtasari. Aidha, wapo watafiti ambao wamejadili kuhusu matatizo
ya tafsiri katika matini za kitalii. Kwa mfano, Baolong (2009) alitumia Nadharia ya Skopos kwa lengo la kuchunguza matini za habari kwa kutumia mifano ya matini zinazohusiana na utamaduni wa Shaoxing Mingshi. Kwa kuzingatia Nadharia ya Skopos anajadili kuwa matatizo ya tafsiri yanasababishwa na mfasiri kutokutambua lengo la kutafsiri matini.
Aidha, aligundua kuwa kuna matatizo ya kipragmatiki, kiisimu, kiutamaduni na umahususi wa matini. Kwa kutumia Nadharia ya Skopos anapendekeza kuwa, matatizo hayo yanaweza kukabiliwa kwa kuwa na uelewa wa jumla wa tendo la tafsiri, kusisitiza ushirikiano baina ya mfasiri na mteja, kuhimiza ufahamu wa mfasiri juu ya lengo, uwezo wa lugha zaidi ya moja na viwango vya maadili kwa mfasiri.
Smecca (2009) katika makala yake inayohusu vitabu vya mwongozo kwa watalii na taswira ya ‘Sicily’ katika tafsiri amebainisha matatizo ya kutafsiri matini za kitalii kuwa ni; matatizo ya uhamishaji wa maana, kubadilika kwa mwelekeo na udondoshaji wa maneno ambao unajitokeza katika toleo la Kiitaliano.
Kwa upande wake Mohammad (2010) ameandika makala kuhusu masuala ya kiutamaduni katika tafsiri ya vitabu vya mwongozo kwa watalii nchini Irani, kwa kuangalia matatizo na suluhisho lake kwa kutumia mkabala wa nadharia ya Skopos. Katika makala hayo, amejadili hatua za kutafsiri vitabu vya mwongozo kwa watalii, mbinu, matatizo na jinsi ya kukabiliana na matatizo hayo. Anahitimisha kwamba, kudharau au kutotilia maanani masuala ya kiutamaduni katika kutafsiri vitabu vya mwongozo kwa watalii nchini Irani, ni sababu inayowafanya watalii kushindwa kuelewa utamaduni wa Wairani na pia husababisha tatizo la mawasiliano na upungufu katika kuvutia watalii. Yan na Naikang (2011) katika utafiti wao wamechunguza matatizo ya kutafsiri matini za kitalii kutoka lugha ya Kichina kwenda lugha ya Kiingereza. Katika utafiti huo wamebainisha matatizo yanayozikabili tafsiri za kitalii za Kichina-Kiingereza kuwa ni matatizo ya kiisimu na matatizo ya kiutamaduni. Hivyo basi, makala haya yametumia muktadha wa Kitanzania kuchunguza matatizo ya tafsiri katika matini za kitalii zilizotafsiriwa kutoka lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza na hatimaye kutoa mapendekezo ya namna ya kuyaondoa matatizo hayo.
Matokeo ya Utafiti
Katika kuchunguza na kuchambua matini za kitalii ambazo ni lebo, vipeperushi na vitabu vya mwongozo kwa watalii makala haya yalibaini matatizo ya tafsiri katika matini hizo. Matatizo yaliyodhihirika ni matatizo ya kiisimu, kimaana na kiutamaduni. Sehemu inayofuata inajadili matatizo hayo kwa kutumia mifano iliyobainishwa katika matini za kitalii:
Matatizo ya Kiisimu
Matizo ya kiisimu yanatokana na tofauti za kisarufi na kimuundo katika msamiati, sintaksia na nduni za lugha chanzi na lugha lengwa (Nord, 1993: 66). Mfasiri hukumbana na matatizo na makosa ya kiisimu katika vipengele vya kiwango cha msamiati na kiwango cha kisintaksia. Katika utafiti huu, matatizo ya kiisimu yaliyobainika katika lebo, vipeperushi na vitabu ya mwongozo kwa watalii yamejikita katika viwango vitatu ambavyo ni: kiwango cha msamiati, kiwango cha kisintaksia na kiwango cha maana. Sehemu inayofuata inajadili matatizo ya kiisimu kwa kuzingatia viwango vyake na mifano dhahiri kutoka katika matini za kitalii zilizopo Makumbusho kama ifuatavyo:
Kiwango cha Msamiati
Matatizo ya kiisimu katika kiwango cha msamiati yamejikita katika uteuzi wa visawe vya kiutamaduni katika lugha lengwa. Makosa katika uteuzi wa visawe wakati wa kutafsiri matini za kitalii huweza kusababisha matatizo katika uelewa na ufahamu wa maana iliyokusudiwa na matini chanzi. Hivyo basi, kutokana na makosa au tatizo la uteuzi wa visawe, hadhira lengwa hushindwa kupata maana sahihi endapo kisawe kilichoteuliwa kitakuwa si sahihi. Katika utafiti huu ilibainika kuwa tatizo la uteuzi wa visawe huweza kusababishwa na matatizo binafsi aliyonayo mfasiri wa matini za kitalii ambayo ni uwezo na ujuzi wa lugha, uelewa wa utamaduni chanzi na utamaduni lengwa na pengine mfasiri kutokuelewa maneno ya lugha ya Kiswahili. Mbali na matatizo ya mfasiri, utafiti huu uligundua kuwa matatizo mengine ni: tofauti za kiisimu za lugha chanzi na lugha lengwa ambazo husababisha ukosefu wa visawe vya lugha chanzi katika lugha lengwa na kutokuelewa utamaduni wa lugha lengwa. Mifano ifuatayo inaonesha uteuzi mbaya wa visawe ambao wakati mwingine unasababishwa na tatizo la lugha (uwezo mdogo wa lugha wa mfasiri) la kutokuelewa maneno ya Kiswahili, utamaduni lengwa na pengine ukosefu wa kisawe katika lugha lengwa:
Mifano iliyopo katika jedwali namba 1 hapo juu, inaonesha kuwapo kwa tatizo la uteuzi wa visawe mwafaka vya kiutamaduni. Kuna makosa katika kuteua visawe vya Kiingereza wakati wa kutafsiri maneno ya Kiswahili kwenda katika lugha ya Kiingereza. Uteuzi wa
neno ‘container’ kama kisawe cha‘kibuyu’, ‘fireplace’ kama kisawe cha ‘mafiga’, na ‘spoon’ kama kisawe cha ‘upawa’ inadhihirisha kuwapo kwa tatizo la uteuzi wa visawe vya kiutamaduni kutoka katika utamaduni lengwa kurejelea utamaduni chanzi na mapungufu ya uelewa na ujuzi wa lugha alionao mfasiri. Hivyo basi,
kulingana na nadharia ya Skopos tunaona kuwa kanuni ya ushikamani na uaminifu haijafikiwa na hivyo basi, kutofikiwa kwa kanuni hizo kunasababisha mapungufu ya mawasiliano na kutofikiwa kwa lengo la tafsiri ya matini za kitalii. Utafiti huu unapendekeza kuwa tafsiri sahihi ya maneno hayo ingekuwa kama ifuatavyo: neno mafiga lingefaa kutafsiriwa kama ‘firestones’, neno upawa lingefaa kutafsiriwa kama ‘shallow ladle’ na kibuyu lingefaa kutafsiriwa kama ‘gourd’.
5.1.2 Makosa ya Kisintaksia
Matini za kitalii zinaonesha kuwa zinakabiliwa na makosa ya kisintaksia ambayo pia huathiri ufahamu na uelewa wa maana kwa
hadhira lengwa. Wakati wa kutafsiri matini za kitalii, mfasiri anaweza kuathiriwa na sarufi na ruwaza za miundo na mipangilio ya sarufi ya lugha yake na kuihamishia katika lugha lengwa. Kulingana na nadharia ya Skopos, lengo la tafsiri ni kwa ajili ya hadhira lengwa kusoma na kuelewa taarifa za lugha chanzi. Kwa kuzingatia matini za kitalii, lengo la tafsiri ni kuvutia wageni. Inawezekana wasomaji wakawa wageni kutoka nje na siyo Waswahili. Ilielezwa wakati wa usaili na waongozaji wa watalii na wahifadhi mila katika Makumbusho zilizotembelewa kuwa, watalii kutoka nje ya nchi ndio tegemeo kubwa la utalii kwa sababu watalii wengi wanaotembelea Makumbusho huwa ni wageni kutoka nje ya Tanzania. Kwa hiyo, wakati wa kutafsiri ni vema kuepuka tafsiri sisisi na sentensi changamano ambazo zinaweza kuleta utata wa maana na hatimaye
kusababisha upungufu wa mawasiliano kwa watalii ambao huhitaji kupata taarifa sahihi za kile wanachokiona katika maeneo ya utalii. Tazama mifano katika jedwali lifuatalo:
Ukichunguza mifano katika jedwali namba 2 utaona kuwa, katika mfano wa kwanza kuna udondoshaji wa kiunganishi ‘kama’ katika matini lengwa. Matumizi ya kiunganishi ‘kama’ katika matini chanzi kina dhima ya kuelezea aina ya mtungi unaozungumziwa. Hivyo basi, kuondolewa kwa kiunganishi ‘kama’ katika lugha lengwa kunaathiri maana na uelewa wa maana kwa hadhira lengwa. Taarifa ya matini chanzi ambayo imekusudiwa kutolewa kwa hadhira lengwa hupotea na hivyo hadhira lengwa hupata dhana na maana tofauti na ile iliyopo katika matini chanzi. Katika mfano wa pili, lugha chanzi inasema ‘kwa matumizi ya vinywaji’ na lugha lengwa imetafsiriwa kama ‘used to keep different drinks’. Hadhira chanzi wanapata dhana na picha tofauti kwamba kifaa kinachoelezewa kinatumika kwa ajili ya vinywaji. Kwa upande mwingine, tafsiri ya sentensi hiyo imeparaganyika kisarufi katika uteuzi wa msamiati ambao umetumika kutafsiri na hivyo kutoa dhana na picha tofauti kwa hadhira lengwa ‘used to keep different drinks’ ambapo hadhira lengwa itapata picha kwamba kifaa hiki kinatumika kuhifadhi vinywaji tofauti. Kisarufi matumizi ya neno ‘keep’ kama kisawe cha neno ‘matumizi’ na kuongeza msamiati mpya ‘different’ inaleta athari katika kutafsiri maneno ya kiutamaduni na kusababisha dhana na picha iliyokusudiwa kwa hadhira chanzi kupotea. Vilevile
huwafanya hadhira chanzi na lengwa kujenga dhana na picha tofauti. Ukichunguza mfano wa tatu utaona kuwa kuna udondoshaji wa kirai kihusishi ‘kwa kawaida’ na matumizi ya neno ‘while’ katika lugha lengwa badala ya kiunganishi ‘na’ ambacho kipo katika lugha chanzi. Hivyo basi, tunaona kuwa makosa ya kisintaksia huweza kuharibu ujumbe uliokusudiwa katika matini chanzi.
Makosa ya Kimaana
Maana ni kitu cha msingi katika tafsiri na ndicho kitovu cha tafsiri (Mwansoko, 1996). Tunapofanya tafsiri ya taarifa za lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa huwa tunahamisha maana ya ujumbe uliokusudiwa katika matini chanzi kwenda katika matini lengwa. Katika matini za kitalii ilibainika kuwapo kwa makosa ya maana. Katika makala haya, matatizo ya maana yamewekwa katika viwango vitatu ambavyo ni upotevu na uhamishaji wa maana, upokezi wa maana na utata wa maana.
Upotevu na Uhamishaji wa Maana
Katika baadhi ya tafsiri ya matini za kitalii, imebainika kuwa kuna upotevu na uhamishaji wa maana na ujumbe wa matini chanzi katika matini lengwa. Maana za kiishara za kiutamaduni na maumbo ya maneno hupotea wakati wa kutafsiri. Kihore (1989)
anasema kwamba ingawa lengo kuu la tafsiri ni kuzalisha athari iliyo sawa ya matini chanzi katika lugha nyingine, inatokea kwamba vipengele vya maana na umbo huathiriwa. Kulingana na kanuni ya uaminifu ya nadharia ya Skopos ambayo inasisitiza ushikamani wa matini chanzi na matini lengwa, tunaweza kusema kwamba kukosekana kwa ushikamani katika matini za kitalii ni tatizo la tafsiri. Kwa mfano, wakati wa kufanya uchambuzi wa maudhui ya matini za kitalii ambazo ni lebo, vipeperushi na vitabu vya mwongozo wa watalii, mtafiti aliweza kubainisha upotevu na uhamishaji wa maana na ujumbe katika maneno ya Kiswahili yanapotafsiriwa kwenda lugha ya Kiingereza. Tazama mifano katika jedwali lifuatalo:
Ukichunguza jedwali namba 3 hapo juu, utaona kuwa kuna upotevu na uhamishaji wa maana ya neno la lugha chanzi katika lugha lengwa. Kwa mfano, katika mfano wa kwanza tunaona neno ‘wanaume’ limetafsiriwa kama ‘elders’ hapa kuna upotevu wa maana kwa sababu ‘mwanaume’ na ‘elders’ ni maneno yenye dhana mbili tofauti na urejelezi tofauti kulingana na utamaduni wa jamiilugha ya Waingereza na Waswahili. Neno ‘mwanaume’ hurejelea mtu wa jinsia ya kiume aliyeoa (TUKI: 235) wakati kisawe kilichotumika katika tafsiri kurejelea neno hilo ni ‘elders’ ambalo lina maana ya ‘wazee’. Hivyo basi, tafsiri sahihi inayopendekezwa kwa neno ‘mwanaume’ ni ‘man’ na ‘elders’ ni ‘wazee’. Mfano wa pili unaonesha neno ‘utawala’ limetafsiriwa kama ‘fight experience.’ Tafsiri hii inapotosha maana na historia ya jamii inayozungumziwa katika matini chanzi. Matini chanzi inaelezea kuhusu utawala wakati matini lengwa inaelezea uzoefu wa kivita. Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa matini chanzi na matini lengwa zinatoa taarifa na ujumbe tofauti.
Hii inatokana na kutoa tafsiri ambayo si sadifu. Kwa maana hiyo tunaweza kusema kwamba, tafsiri sahihi ya neno ‘utawala’ ingeweza kuwa ‘administration’. Kwa upande mwingine katika mfano wa tatu, neno ‘wavulana’ limetafsiriwa kama ‘youth’. Matumizi ya neno ‘youth’ kama kisawe cha neno la Kiswahili ‘wavulana’ hupoteza na kuhamisha maana ya msingi ya neno. Upotevu wa maana unatokea kwa sababu neno‘youth’ katika lugha ya Kiingereza (lugha lengwa) hurejelea ‘kijana’ ambaye anaweza kuwa mvulana ama msichana. Kwa maana hiyo, hadhira ya lugha lengwa huweza kupata maana na ujumbe tofauti na hadhira chanzi. Pia kutokana na tafsiri hizo kupoteza na kuhamisha maana humfanya hadhira lengwa kupata ujumbe ambao si sahihi kuhusu utamaduni wa jamii chanzi.
Uhamishaji wa Maana ya Msingi
Uhamishaji wa maana ni tatizo ambalo hujitokeza katika tafsiri ya matini za kitalii. Maana ya msingi ya neno huhusisha maana za kiishara ambazo zinakuwa zimebebwa na Matatizo ya Tafsiri katika Matini za Kitalii Nchini Tanzania 37 neno linalohusika. Katika matini za kitalii, uhamishaji wa maana ulionekana kwa baadhi ya maneno ambapo maana zake za msingi zilionekana kuhama kutoka katika maana moja kwenda katika maana nyingine. Jedwali lifuatalo linaonesha mifano ya maneno ya Kiswahili ambayo yamepoteza maana yake ya asili katika lugha lengwa:
Ukichunguza mfano wa kwanza, ‘jiwe la kusagia’ limetafsiriwa kama ‘grinding machine’ tafsiri hii inapoteza dhana ya msingi ya ‘jiwe la kusagia’ ambalo ni jiwe kubwa mahususi kwa kusagia nafaka, likiwa na jiwe dogo ambavyo vyote hushirikiana. ‘Jiwe la kusagia’ si ‘mashine’, hivyo kwa dhana hiyo ya ‘grinding machine’ kutumika kama kisawe cha ‘jiwe la kusagia’ hakileti ulinganifu sadifu wa maana, umbo na matumizi ya jiwe la kusagia. Hivyo basi, inapendekezwa neno ‘Jiwe la kusagia’ lingefaa kutafsiriwa kama ‘grinding stone’. Tafsiri hii ya ‘grinding stone’ ni sadifu zaidi kuliko ‘grinding machine’ kwa sababu ‘jiwe la kusagia’ linalozungumziwa ni jiwe kubwa na siyo mashine. Hivyo basi, tafsiri hii inaweza kumsaidia hadhira lengwa kuweza kuhusianisha kile anachokiona na tafsiri yake. Mfano wa pili na nne, yaani ‘mwiko’ na ‘chungu’ vimetafsiriwa kwa kutumia kisawe kimoja ‘scoop’. Ukichunguza vifaa hivi katika utamaduni chanzi ni tofauti katika maumbo, ukubwa, utengenezaji na matumizi yake.
Hivyo basi, tafsiri hii inaathiri maana ya dhana iliyokusudiwa katika matini chanzi. Kwa mifano hiyo, utafiti huu unapendekeza kuwa neno ‘mwiko’ lingefaa kutafsiriwa kama ‘wooden spoon’ na ‘chungu’ lingefaa kutafsiriwa kama ‘pot’. Mfano wa tatu na wa sita, yaani ‘makobazi’ na ‘viatu’ vyote vimetafsiriwa kama ‘sandals’. Tafsiri hiyo si sadifu kwa sababu ‘viatu’ ni tofauti na ‘makobazi’, kimuundo na kiuvaaji. Hivyo basi, matumizi ya neno sandals kama kisawe cha ‘viatu’ na ‘makobazi’ yanaathiri dhana ya msingi ya maneno hayo na kuleta utata wa maana. Katika mifano hiyo, utafiti huu unapendekeza kuwa neno la Kiingereza ‘sandals’ linasadifu zaidi kuwa kisawe cha ‘makobazi’ na neno la Kiswahili ‘viatu’ liwe kisawe cha ‘shoes’. Mfano wa tano na wa nane, yaani ‘kibuyu’ imetafsiriwa kama ‘container’, na wakati huohuo mfano wa namba nane ambao ni ‘kibuyu kidogo cha dawa’ umetafsiriwa kama ‘a small calabash’. Mifano hii inaonesha kuwa hakuna ushikamani wa maana baina ya
matini chanzi na matini lengwa. Ukosefu wa ushikamani wa maana unasababisha maana ya dhana ya msingi ya kiutamaduni kupotea katika tafsiri na kuleta utata katika maana ya matini chanzi na matini lengwa. Hadhira lengwa itashindwa kupata dhana na maana halisi ya maneno haya. Katika makala haya inapendekezwa kuwa neno ‘kibuyu’ litafsiriwe kama ‘gourd’ na siyo ‘container’ kwa sababu
‘container’ katika lugha lengwa linabeba dhana tofauti na kibuyu.
Hivyo kutafsiri ‘kibuyu’ kama ‘container’ na wakati huohuo kutafsiri neno ‘kibuyu’ kama ‘calabash’ huleta utata wa maana na uhamishaji wa maana ya msingi.
Utata wa Maana
Utata wa maana ni miongoni mwa matatizo ambayo yamejitokeza katika tafsiri ya matini za kitalii. Mifano ifuatayo inaonesha maneno yenye utata wa maana na ujumbe. Kwa mfano, kibuyu kimetafsiriwa kama ‘container’ na wakati huohuo neno ‘kata’ limetafsiriwa kama ‘water container’. ‘Kijiko’ kinatafsiriwa kama ‘spoon’ na ‘upawa’ umetafsiriwa kama ‘spoon’. Ukichunguza mifano hiyo, utaona pia kunautata wa maana ambapo neno moja linatumika kutafsiri maneno zaidi ya moja. Matumizi ya kisawe ‘container’ yanaleta utata wa maana na kupoteza dhana ya msingi ya maneno hayo.
Upanuzi wa Maana
Upanuzi wa maana ni kitendo cha kulipa neno au maneno maana ya ziada. Maana ya ziada huweza kujitokeza wakati wa kutafsiri matini za kitalii kutoka katika lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa. Maana ya ziada huathiri dhana, ishara na ujumbe unaobebwa na neno hilo. Maneno hubeba dhana, ishara na ujumbe wa neno kulingana na utamaduni unaohusika. Hivyo basi, maana ya ziada inayopewa neno hilo katika lugha ya matini chanzi huathiri asili ya neno na pia hudondosha sifa za kiisimu na kiuamilifu za neno hilo. Uziada huu pia huathiri upokezi na utambuzi wa ujumbe kwa hadhira kwa sababu hadhira haipati mtekenyo ulio sawa wa ujumbe.
Mifano ya maneno na sentensi zifuatazo ambazo zilibainishwa katika lebo zinaonesha na kudhihirisha upanuzi wa maana unavyojitokeza katika tafsiri ya matini za kiutamaduni katika utalii.
Mifano iliyotolewa katika jedwali namba 5a, inaonesha kuwapo kwa uongezaji wa maneno ambayo hayapo katika lugha chanzi lakini yanajitokeza katika lugha lengwa. Uongezaji wa neno ‘aid’ (msaada) ambalo halipo katika matini chanzi linatoa ujumbe wa ziada ambao
haupo katika matini chanzi. Ujumbe wa ziada huweza kuathiri ujumbe wa matini chanzi.
Katika jedwali namba 5b, tunaona kuwa kuna uziada wa maneno ambao unatokea katika matini lengwa. Uziada huu unaathiri taarifa za kiutamaduni za matini chanzi ambazo ni shughuli zinazofanywa na jamii hii. Mfano uongezaji wa shughuli kama vile ‘basketry’ yaani ‘usukaji wa vikapu’. Shughuli hii haijaelezewa katika matini chanzi.
Hivyo uongezaji wa shughuli ambazo hazipo katika matini chanzi ni upanuzi wa taarifa za matini chanzi ambazo huathiri taarifa za kiutamaduni za jamii husika. Mfano mwingine ni huu ufuatao:
Katika mfano huo, tunaona kuwa tafsiri ya neno ‘Agriculture’ kurejelea shughuli za kilimo zilizoainishwa katika matini chanzi ni la jumla sana. Kila jamii hushughulika na kilimo cha mazao tofauti na jamii nyingine kulingana na jiografia ya eneo linalohusika. Hivyo, matumizi ya neno ‘agriculture’ yanapanua maana na ujumbe
wa matini chanzi na kuleta pia utata katika utambuzi wa ujumbe. Je, jamii hii hujishughulisha na kilimo cha mazao ya aina zote? Vilevile, matumizi ya neno ‘livestock keeping’ ni ya jumla sana. Hata hivyo, uziada huu unaotokana na tafsiri jumuishi unaathiri ujumbe wa matini chanzi kwa sababu ukichunguza matini chanzi imebainisha mazao na mifugo mahususi.
Ufinyu wa Maana
Ufinyu wa maana hutokea pale ambapo neno huwa na maana finyu katika lugha lengwa tofauti na maana ya matini chanzi. Aidha, katika maneno, vishazi ama sentensi hutafsiriwa kwa ufinyu wake na hivyo kulifanya neno, kishazi ama sentensi kuwa na maana finyu
katika lugha lengwa tofauti na ilivyo katika lugha chanzi. Ufinyu wa maana huathiri tafsiri kwa sababu matini lengwa huwasilisha ujumbe tofauti na matini ya utamaduni chanzi. Hivyo basi, athari hii huweza kusababisha hadhira lengwa kutokuelewa maana na hivyo kuathiri mawasiliano katika utalii. Mifano ifuatayo inaonesha maneno ambayo yametafsiriwa kwa maana finyu: Mfano namba 1 katika jedwali hapo juu tunaona kuwa matini chanzi imetafsiriwa kwa mstari mmoja na tafsiri hiyo tunaona maana na ujumbe wa matini chanzi umefinywa. Ufinyu wa maana unasababisha athari za kiutamaduni kwa sababu dhana za kiutamaduni na taarifa muhimu za kaida mila na desturi za jamii ya matini chanzi hupotea. Katika mfano namba 2, kuna ufinyu wa maana ambapo taarifa zilizopo katika matini chanzi, zimedondoshwa. Kwa mfano, kifungu cha maneno “mchezo huu uliwasaidia vijana kuwa na shabaha na hivyo kuweza kupiga wanyama kwa ajili ya kitoweo” kimedondoshwa na hivyo dhana nzima ya ujumbe wa utamaduni chanzi imepotea. Katika mfano huu, taarifa muhimu ya namna mchezo huo ulivyowasaidia vijana imedondoshwa katika matini lengwa. Hivyo basi, udondoshaji huu unaifanya hadhira lengwa kukosa taarifa za umuhimu wa mchezo wa kulenga shabaha kwa jamii.
Mfano katika jedwali namba 6b unadhihirisha udondoshaji wa neno ‘zawadi’ ambalo lipo katika lugha chanzi lakini halipo katika lugha lengwa. Udondoshaji wa neno hili unaathiri taarifa ya ujumbe wa matini chanzi.
Matatizo ya Kiutamaduni
Tatizo kubwa linaloweka kipingamizi katika tafsiri ni tafsiri ya dhana mahususi za kiutamaduni. Lugha chanzi inaweza kuelezea dhana ambayo haijulikani kabisa katika lugha lengwa. Utamaduni unaelezwa na Newmark (1988) kuwa ni mkusanyiko wa mila na desturi za jamii inayotumia lugha moja mahususi kama njia yake ya mawasiliano. Wanjara (2011) anasema lugha zinatofautiana sana kiutamaduni na hili ni tatizo kubwa sana kwa mfasiri hata kuliko tofauti za kiisimu. Baker (2000:20) anasema ukosefu wa ulinganifu katika kiwango cha utamaduni husababisha ukosefu wa ulinganifu katika kiwango cha neno, hasa ikiwa lugha lengwa haina ulinganifu wa moja kwa moja wa neno linalojitokeza katika matini chanzi. Matatizo ya utamaduni huweza kujitokeza katika viwango viwili ambavyo ni: tatizo la kutafsiri majina kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa na tatizo la kutafsiri dhana za kiutamaduni kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Tatizo la Kutafsiri
Majina Katika utafiti huu ilibainika kuwa tafsiri ya majina ya vitu ama vifaa vya kiutamaduni vilivyopo Makumbusho vina changamoto kubwa. Hii ni kwa sababu kila jamii huelewa vitu na kuvipa majina kulingana na uelewa na namna wanavyofasili ulimwengu unaowazunguka. Mifano ifuatayo inaonesha maneno ambayo yametafsiriwa kama yalivyo kutoka lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza:
Chanzo: Matini za kitalii Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam, Mei-Oktoba, 2012 Ukichunguza mifano iliyopo katika jedwali namba 7, utaona kuwa maneno ya lugha ya Kiswahili yametafsiriwa kama yalivyo katika lugha lengwa. Hii inadhihirisha kwamba ni vigumu kupata visawe rejelezi vinavyorejelea majina ya lugha chanzi katika lugha lengwa kwa sababu kila jamii huwa na maneno ama majina ya vitu kulingana na utamaduni wa jamii mahususi. Makala haya yanapendekeza kwamba, maneno hayo yatafsiriwe kwa kuhamisha neno kama lilivyo na kulitolea ufafanuzi kulingana na jinsi linavyoeleweka katika utamaduni chanzi. Tazama mifano ya tafsiri inayopendekezwa katika jedwali namba 7b hapa chini:
Jedwali namba 7b hapo juu linaonesha mifano ya kutafsiri matini zilizojikita katika uelewa wa utamaduni mahususi. Mbinu hii ya tafsiri inatambulika kama mbinu ya uasilishaji na ufafanuzi wa visawe. Kwa kutumia mbinu hii hadhira lengwa itaweza kuelewa kwa urahisi zaidi maana, ujumbe, dhima na namna neno hilo linavyotumika katika utamaduni chanzi.
6.0 Mapendekezo Makala haya yanapendekeza kwamba katika kutafsiri matini za kitalii mfasiri anahitaji kuwa na stadi, ujuzi, maarifa ya nadharia na mbinu za tafsiri. Hii itamsaidia kutafsiri matini za kitalii kwa kuzingatia nadharia na mbinu za tafsiri. Kuteua mbinu iliyo bora kutafsiri matini za kitalii kutamsaidia katika uteuzi wa visawe mwafaka kulingana na aina ya maneno aliyonayo katika matini. Aidha, inapendekezwa kwamba ni muhimu kwa mfasiri kuwa na ujuzi na uwezo wa lugha chanzi na lugha lengwa. Ili mfasiri
aweze kutafsiri matini za kitalii ni vema akawa na ujuzi wa lugha zote mbili. Kwa kufanya hivi mtafiti ataweza kuepuka makosa na matatizo ya kiisimu katika tafsiri ya matini za kitalii. Vilevile, mfasiri anatakiwa kuwa na ujuzi na maarifa ya utamaduni chanzi na utamaduni lengwa. Maarifa haya yatamsaidia kuelewa maana za kiishara na za ziada zinazobebwa na neno la utamaduni chanzi na kulihusianisha na neno la utamaduni lengwa.
Hivyo basi, itakuwa rahisi kwa mfasiri kutafsiri matini chanzi kwenda katika matini lengwa. Mfasiri anapokuwa na maarifa hayo, ataweza kuteua mbinu mwafaka za kutafsiri matini ya kiutamaduni kulingana na maarifa na ujuzi alionao kuhusu maana na ujumbe wa
matini hiyo katika utamaduni chanzi na utamaduni lengwa. Makala haya yanapendekeza kwamba, mfasiri anapokumbana na maneno ambayo yamejikita katika utamaduni mahususi na maana zake zinaeleweka kwa jamii mahususi, ni vema kutumia mbinu ya uasilishaji na ufafanuzi wa visawe. Mbinu hii inampa nafasi mfasiri kutafsiri neno kama lilivyo na kulitolea ufafanuzi kuhusu maana, dhima, ujumbe na jinsi linavyotumika katika utamaduni chanzi.
Hitimisho
Makala haya yamejadili juu ya matatizo ya kutafsiri matini za kitalii na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kukabiliana na matatizo hayo ili kuwa na ufanisi wa mawasiliano. Imebainika kuwa, tafsiri ya matini za kitalii huwa na matatizo ya kiisimu, kimaana na kiutamaduni. Kutokana na matatizo hayo baadhi ya matini za kitalii
zinashindwa kufikisha ujumbe sahihi kwa hadhira lengwa na hivyo kusababisha matatizo ya kimawasiliano. Matatizo hayo pia yanasababisha ukosefu wa ushikamani wa maana na ujumbe baina ya matini chanzi na matini lengwa. Kwa maana hiyo, hadhira lengwa hushindwa kupata ujumbe asilia uliokusudiwa na matini chanzi. Aidha, makala haya yanajadili kwamba, kulingana na nadharia ya Skopos tafsiri ya matini za kitalii hutafsiriwa kwa lengo maalumu ambalo ni kufikisha taarifa za kitalii zilizopo katika jamii chanzi. Hivyo basi, ili kufikia lengo hilo makala haya yanapendekeza kwamba, mfasiri wa matini za kitalii lazima awe na ujuzi na maarifa ya kutosha katika tafsiri, nadharia na mbinu, ujuzi wa lugha chanzi na lugha lengwa pamoja na uelewa na ufahamu kuhusu utamaduni chanzi na utamaduni lengwa. Aidha, makala haya yanapendekeza kwamba, matini za kitalii hasa zilizojikita katika utamaduni wa jamii mahususi zitafsiriwe kwa kutumia mbinu ya uasilishaji na ufafanuzi wa visawe. Mbinu hii itasaidia kuweka bayana maana, ujumbe, dhima na matumizi ya neno hilo katika utamaduni wa jamii mahususi. Kwa kufanya hivi, hadhira lengwa wataweza kuelewa neno hilo kwa urahisi na upana zaidi na hatimaye kuwa na tafsiri bora zenye kusababisha ufanisi wa mawasiliano katika maeneo ya utalii.
MAREJELEO
Baker, M. and Malmakjae, K. (2005). Routledge Encyclopedia of Translation Studies. London: Tylor & Francis Group.
Baolong, W. (2009). “Translating Publicity Text in the Light of the Skopos Theory: Problems and Suggestions” katika Translation Journal Volume 13, Na. 1, uk. 29-50.
Benavides, C. and Fletcher C. (2001). Tourism Principles and Practice. New York: Longman.
Bennett, T. (1995). The Birth of The Museums London. London: Routledge.
Catford, J.C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London:
Oxford University Press. Matatizo ya Tafsiri katika Matini za Kitalii Nchini Tanzania
Gentzler, E. (2001). Contemporary Translation Theories. London and New York: Routledge.
House, J. (2009). Translation. Oxford: Oxford University Press.
Kihore, Y. M. (1989). Isimu na Tafsiri Kutoka na Kuingia Katika Lugha za Kiafrika. Makala za Kongamano Kuhusu Matatizo ya Tafsiri Barani Afrika. Dar es Salaam: WAFASIRI, 24-35, “Uzingativu wa Sarufi katika Tafsiri” Swahili Forum, 12, uk. 109-120
Lauscher, S. (2000). Translation Quality Assessment: Where can Theory and Practice meet? The Translator, Juzuu Na. 6, (2), uk.149-168
Mohammad, R.T. (2010). ‘Cultural Issues in the Transalation of Tourist Guidebooks in Iran: Problems and Solutions from a Skopos Theory Pespective’. Translation Journal, Vol. 4 retrieved on July 2011 from http://www.translationdirectory.com/article2183.php
Mwansoko, H.J.M. (1996). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam:TUKI.
Nan, C. (2005). A Talk on Translation of Tourism Advertisement. Unpublished Master Thesis. Foreign Language College, Zhejiang Wan Li University.
Nan, C. (2005). A Talk on Translation of Tourism Advertisement. Tasnifu ya Umahiri (Haijachapishwa). Chuo cha Lugha za Kigeni. Chuo Kikuu cha Zhejiang Wan Li.
Newmark. P. (1988). A Textbook of Transaltaion. London: Prentince Hall.
Ndlovu, V. (2000). ‘Translating Aspect of Culture in “Cry, The Beloved Country in Zulu’ Language Matter, 31: 1, kur. 72-102
Nida, E. A. (2001). Language and Culture: Context in Translating. Shanghai: Shanghai Foreign Language Ed Press
Nida, E. A. and Taber, C. (1969). Theory and Practice of Translating. Leiden: Brill.
Ngozi, I.S. (1992). “The Role of translation in literature in Kiswahili and its problems”. Federation of international des traducteurs (FIT)
Newsletter, vol. X1, No. 1-2: kur 63-67.
Nord, C. (1991a). “Skopos, Loyalty and Translational Conventions” Target, 3 (1): 91- 109
______ (1991b). The Analysis in Translation. Amsterdam: Rodopi.
Matatizo ya Tafsiri katika Matini za Kitalii Nchini Tanzania
______ (1997). Translating as a Purposeful Activity: Functionalist Aproaches explained. Manchester: st. Jerome.
_____ (2001). Translating as a Purposeful Activity-Functionalist Approaches Explained. Shanghai: Foreign Language Education Press.
Ordudary, M. (2007). “Translation Procedures, strategies and methods” Translation Journal. Vol.11,no.3 Availale at www.translationdirectory (retrieved 17th June 2011).
Reiss, K. na Vermeer, H. (1984). Groundwork for a General Theory of Translation. Tubingen: Niemeyer.
Sanning, H. (2010). Lost and Found in Translating Tourist Texts. The Journal of Specialized Translation, Juzuu Na. 13, uk. 124-137.
Smecca, P.D. (2009). ‘Tourist Guidebooks and The Image of Sicily in Translation’ katika Perspective, volume 17, issue 2, uk. 109-119.
Su-zhen, J. (2008). Skopos Theory and Translating Strategies of Cultural Elements in Tourism Texts. Retrieved July 21, 2010 from http://www.linguisti.org.n/doc/su20080906.pdf
TUKI. (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (2nd ed). Nairobi: Oxford University Press.
Venuti, L. (2008). The Translator’s Invisibility: A History of Translation (2nd ed): Routledge 2 Park Square, Milton Park Abingdon, Oxon Ox 14 4RN.
Vermeer, H. (1989a). ‘Skopos and Commission in Translational Action’ katika
Chesterman, A (Ed). Readings in Translation Theory. Pp 99-104.
Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Books.
Wanjala, F. S. (2011) Misingi ya Ukalimani na Tafsiri kwa Shule, Vyuo na Ndaki: Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.
Chanzo>>>>>>>>
|