VITENDAWILI NA MAANA ZAKE
A
1. Adui lakini po pote uendako yuko nawe. Inzi
2. Afahamu kuchora lakini hajui achoracho. Konokono
3. Afuma hana mshale. Nungunungu
4. Ajenga ingawa hana mikono. Ndege
5. Ajifungua na kujifunika. Mwavuli
6. Akitokea watu wote humwona. Jua
7. Akitokea watu wote hunungunika na kuwa na huzuni. Ugonjwa
8. Akivaa nguo hapendezi, akiwa uchi apendeza. Mgomba
9. Alipita mtu ana bunda la mshale. Mkindu
10. Alipita mtu mwenye kibandiko cha nguo. Inzi
11. Aliwa, yuala; ala, aliwa. Papa
12. Amchukuapo hamrudishi. Kaburi
13. Amefunika kote kwa blanketi lake jeusi. Giza
14. Amefunua jicho jekundu. Jua
15. Ameingia shimoni akiwa uchi, akatoka amevaa nguo nzuri. Mbegu
16. Amejitwika mzigo mkubwa kuliko yeye mwenyewe. Konokono/Koa
17. Amekaa kimya na watoto wamemzunguka pande zote. Mgomba
18. Amekula ncha mbili. Wali
19. Amevaa joho kubwa kuliko yeye mwenyewe. Kaburi
20. Anakuangalia tu wala halali au kutembea. Picha
21. Anakula kila siku lakini hashibi na hatashiba. Mchanga
22. Anakula lakini hajashiba na hatashiba milele. Ardhi
23. Anakula lakini hashibi. Mauti
24. Anapendwa sana ingawaje ni mkali sana. Moto
25. Anatoka kutembea, anakuja nyumbani anamwambia mama, ‘Nieleke’. Kitanda
26. Ashona mikeka wala hailali. Maboga
27. Askari wangu wote wamevaa kofia upande. Majani
28. Askari wangu wote wamevaa mavazi meusi. Chunguchungu
29. Asubuhi atembea kwa miguu mine, adhuhuri kwa miwili. Fedha
30. Atapanya mbegu nyingi sana lakini hazioti. Mvua
31. Atolewapo nje hufa. Samaki
B
32. Baba alinipa mfupa, nikautunza ukawa fahali. Muwa
33. Baba ameweka mkuki nje nikashindwa kuukwea, mdogo wangu akaukwea. Sisimizi
34. Babako akojoapo hunung’unika. Mawingu
35. Babu amefunga ushanga shingoni. Mtama/Nazi
36. Babu anakula ng’ombe, analea fupa linakuwa ng’ombe. Muwa
37. Babu hupiga kelele akojoapo. Mvua
38. Babu mkubwa ameangushwa na babu mdogo. Mti na shoka
39. Babu, nyanya, mjomba, mama, baba na watoto, mna safari ya wapi? Siafu
40. Bak bandika, bak bandua. Nyayo
41. Bawabu mmoja tu asiyeogopa chochote duniani. Mlango
42. Bibi kikongwe apepesa ufuta. Kope za macho
43. Bibi yake hutandikwa kila siku, lakini hatoroMoyoKinu cha kutwangia
C
44. Chakula kikuu cha mtoto. Usingizi
45. Cha ndani hakitoki nje, cha nje hakiingii ndani. Nyama na mfupa
46. Chang’aa chapendeza, lakini hakifikiwi. Jua
47. Chatembea na hakijapata kupumzika hata nukta moja. Mwezi/Jua
48. Cheupe chavunjika manjano yatokea. Yai
49. Chumba change kina ukuta niondoa na kuusimika nitakapo. Pazia
50. Chungu change cha udongo hakipasuki kikianguka. Mjusi/Panya
51. Chungu kikubwa sana chenye kifuniko kikubwa sana. Dunia na mbingu
D
52. Dada yangu akitoka kwao harudi kamwe. Jani likwanyukapo
53. Dada yangu kaoga nusu. Jiwe mtoni
54. Drrrrrh1 Ng’ambo. Daraja la buibui
55. Dume wangu amelilia machungani. Radi
F
56. Fahali wa ng’ombe na mbuzi wadogo machungani. Mwezi na nyota angani
57. Fika umwone umpendaye. Kioo
58. Fuko kajifukia, mkia kaacha nje. Kata mtungini
59. Funga mizigo twende Kongo. Mikia ya mbwa
H
60. Hachelewi wala hakosei safari zake. Jua
61. Haina miguu wala mikono, lakini, yabeba magogo. Maji
62. Hakihitaji maji, wala udongo, wala chakula; lakini chamea. Nywele
63. Hakionekani wala hakishikiki. Hewa
64. Hakisimami, na kikisimama msiba. Moyo
65. Hakuchi wala hakuchwi. Kula
66. Halemewi wala hachoki kubeba. Ardhi
67. Hamwogopi mtu yeyote. Njaa
68. Hana mizizi, nimemkata mara nyingi lakini haachi kukua. Ukucha
69. Haoni kinyaa. Mvua
70. Hapo nje panapita mtu mwenye miguu mirefu. Mvua
71. Hasemi, na akisema hatasahaulika. Kalamu
72. Hasimamishwi akiwa na ghadhabu. Upepo
73. Hata inyeshe namna gani haifiki humu. Kwapani
74. Hata jua likiwaka namna gani hakauki wala kupata joto. Pua ya mbwa
75. Hata Mzungu ameshindwa. Mauti
76. Hauchagui chifu wala jumbe. Utelezi
77. Hausimiki hausimami. Mkufu
78. Hawa wanaingia hawa wanatoka. Nyuki mzingani
79. Hesabu haihesabiki. Nyota
80. Huitumia kila siku lakini haiishi. Miguu
81. Huku kutamu, huku kutamu, katikati uchungu. Jua
82. Huku unasikia ‘pa’ Huku unasikia ‘pa! Mkia wa kondoo
83. Hula lakini hashibi. Sindano
84. Hulala tulalapo, huamka tuamkapo. Jua
85. Humu mwetu tuko wanne tu, ukimwona wa tano mwue. Matendegu ya kitanda
86. Huna macho lakini wakamata wanyama. Ndoana
87. Hupanda mtini na mwenye kichaa wake. Kivuli
88. Hutembea watatu. Mafiga
89. Hutoka upesi sana lakini hasalimu. Kuku
90. Huwafanya watu wote walie. Moshi
91. Huwezi kukalia alipokalia msichana wangu mweusi. Chungu jikoni
92. Huzikwa mmoja, hufufuka mmoja, huzeeka wengi. Mbegu na matunda
I
93. Inaonekana mara mbili katika dakika moja na mara moja tu katika mwaka. Herufi "K"
94. Ini la ng’ombe huliwa hata na walioko mbali. Kifo
K
98. Kaburi la mfalme lina milango miwili. Kata ya kuchukulia Maji kichwani
99. Kaka yangu anapanda darini na fimbo nyuma. Paka na mkia wake
100. Kama kingekuwa mkuki, ungekuta kimekwisha kuua wote. Kizingiti cha mlango
101. Kama unapenda, mbona usile? Ulimi
102. Kanipa ngozi nikapikia, kanipa nyama nikala, kanipa mchuzi nikanywa, kanipa mfupa nikautumia. Nazi
103. Kapanda mti pamoja na uchawi wake. Tumbaku inaponuswa puani
104. Kidimbwi kimezungukwa na majani. Macho
105. Kikioza hutumiwa, kikiwa kichungu hakitumiwa. Maziwa
106. Kila linapofika kwetu hutanguliza makelele. Mvua
107. Kila mtu atapitia malango huo. Kifo
108. Kila mtu hata mfalme huheshimu akipita. Mlango
109. Kila siku hupita njia hiyo hiyo bali arudipo hatumwoni. Jua
110. Kileee! Hiki hapa. Kivuli
111. Kilimsimamisha chifu njiani. Chawa
112. Kina mikono na uso lakini hakina uhai. Saa
113. Kinaniita lakini sikioni. Mwangwi
114. Kisima cha Bimpai kina nyoka muwai, ndiye fisadi wa maji. Taa ya utambi
115. Kisima kidogo kimejaa changarawe. Kinywa na meno
116. Kitendawili change ukikitambua nitakupa hirizi. Mimba
117. Kiti cha dhahabu hakikaliwi na watu. Moto
118. Kiti cha Sulatni hukaliwa na mwenyewe. Kuku aatamiapo mayai
119. Kiti nyikani. Uyoga
120. Kitu changu asubuhi chatembea kwa miguu mine, saa sita kwa miguu miwili, jioni kwa miguu mitatu. Maisha ya binadamu
121. Kiwanja kizuri lakini hakifai kuweka mguu. Kipara
122. Kombe ya Sultani Ii wazi. Kisima
123. Kondoo wangu amezaa kwa paja. Mhindi
124. Kondoo wangu mnene kachafua njia nzima. Konokono
125. Kondoo za mtoto zamaliza mavuno. Jiwe la kusagia
126. Kufanya kwa ridhaa mojamoja. Kusuka mkeka
127. Kuku wangu aliangua mayai jana, lakini si kuku wala ndege. Nyoka au samaki
128. Kuku wangu amezalia miibani. Nanasi au chungwa
129. Kuku wetu hutagia mayai mikiani. Matunda
130. Kuna mlima mmoja usio pandika. Nafasi kati mdomo na pua
131. Kuna mtu mwenye tumbo kubwa aliyesimama nje. Ghala
132. Kuna ziwa kubwa ambalo limekauka na limebakiza mizizi. Chongo
133. Kunguru akilia hulilia mirambo. Mtoto akililia maziwa
134. Kwenye msitu mkubwa Napata mti mmoja tu, lakini kwenye msitu mdogo naweza kupata miwili. Watoto wa ng'ombe na mbuzi
135. Kwetu mishale na kwenu mishale. Mikia ya panya
136. Kwetu twalala tumesimama. Nguzo za nyumba
L
137. La mgambo limelia wakatoka weusi tu. Chunguchungu
138. Likienda hulia, likirudi halilii. Debe aka buyu
139. Likitoka halirudi. Neno
140. Liwali amekonda lakini hana mgaga. Sindano
M
141. Mama ametengeneza chakula lakini hakula. Chungu cha kupikia
142. Mbona kinakumeza lakini hakikuli? Nyumba
143. Mbona mwakunjiana ngumi bila kupigana? Mafiga
144. Mbona mwasimama na mikuki, mwapigana na nani? Katani
145. Mchana ‘ti’ usiku ‘ti’. Mlango
146. Mdogo lakini humaliza gogo. Mchwa
147. Mfalme amesimika mkuki wake hapa name nikausimika wangu kando yake, baadaye
hatukuitambulisha tena. Kohozi
148. Mfalme hushuka kwa kelele. Mvua
149. Mfalme katikati lakini watumishi pembeni. Moto na mafiga
150. Mfalme wetu hupendwa sana, lakini wakati wa kumwona lazima umtoe nguo zote kwanza. Hindi
151. Mhuni wa ulimwengu. Inzi
152. Mkanda mrefu wafka mpaka pwani. Njia
153. Mke wangu mfupi, lakini huvaa nguo nyingi. Hindi
154. Mlango wa nyumba yangu uko juu. Shimo la mchwa
155. Mlima mkubwa wapandwa kuanzia juu. Sima/Ugali
156. Mlimani sipandi. Maji
157. Mlima umezuia kutazama kwa mjomba. Kisogo
158. Mlima wa kupanda kwa mikono. Mlima
159. Mlima wa kwetu hupandwa na mfalme. Nafasi kati ya mdomo na pua ya ngombe
160. Mlima wa mwenyewe hupandwa na mwenyewe. Buibui na utando wake
161. Mpini mmoja tu lakini majembe hayahesabiki. Mkungu wa ndizi
162. Msitu ambao haulii hondohondo. Mimba
163. Mti mkubwa, lakini una matawi mawili tu. Kichwa na masikio
164. Mti mnyanya mti kerekeche mti ah mti ah!. Ngoma na upatu
165. Mti wangu una matawi kumi na mawili na kila tawi lina majani kadiri ya thelathini. Mwaka
166. Mtoto asemea pangoni. Ulimi mdomoni
167. Mtu mdogo mwenye miguu mirefu ambaye aweza kutembea dunia nzima kwa dakika tano. Mawazo
168. Mvua hema na jua hema. Kobe
169. Mvua kidogo ng’ombe kaoga kichwa. Jiwe
170. Mwadhani naenda lakini siendi. Jua
171. Mwalimu analala na mwanafunzi wanamsomea. Kinyesi na inzi
172. Mwanamke mfupi hupiga kelele njiani. Kunguru
173. Mwanamke mfupi hutengeneza pombe nzuri. Nyuki
174. Mwanang’ang’a hulia mwituni. Shoka
175. Mwepesi, lakini aweza kuvunja nyumba za mji wote. Tufani
176. Mwezi wangu umepasuka. Kweme
177. Mzee Kombe akitoa machozi wote hufurahi. Mvua
178. Mzee Kombe akilia watu hufurahi. Mvua
179. Mzizi wa miti hutokea mbali. Siafu
180. Mzungu yuko ndani na ndevu ziko nje. Hindi
N
181. Naitumia ngazi hiyo kwa kupandia na kushukia. Mwiba
182. Nakikimbilia lakini sikikuti. Njia
183. Nakupa lakini mbona huachi kudai. Tumbo
184. Nakwenda msituni na mdogo wangu, lakini yeye namwacha huko.
185. Nameza lakini sishibi. Mate
186. Namkimbiza lakini simkuti. Kivuli
187. Namlalia lakini halii. Kitanda
188. Namwomba atangulie lakini hukataa kabisa. Kigino
189. Nanywa supu na nyama naitupa. Muwa
190. Napigwa na mvua na nyumba ipo. Matunda ya pua/Kwapa
191. Natembea juu ya miiba lakini hainichomi. Miiba
192. Natembea juu ya miiba lakini sichomwi. Ulimi
193. Natembea na wenzangu lakini tukifika kwenye nyumba mimi hukaa mlangoni. Mbwa
194. Natengeneza mafuta lakini nimepauka sana. Mzinga was nyuki kwa nje
195. Natengeneza mbono lakini alama hazionekani. Mzinga wa nyuki
196. Ndege wengi baharini. Nyota
197. Ndugu wawili wafanana sana, lakini hawatembeleani. Macho
198. Ngoja nikumbuke. Boga changa
199. Ng’ombe wa baba watelemka mtoni. Mawe mtoni
200. Ng’ombe wa babu huchezea miambani. Mijusi
201. Ng’ombe za babu zikienda machungani hulia, zikirudi hazilii. Vbuyu
202. Ng’ombe za babu zinalala na mkia nje.Viazi vitamu udongoni
203. Ng’ombe wamechanganyika nikakosa wa kwangu. Pesa/Nyayo
204. Ng’ombe wangu ni weupe kwatoni. Katani
205. Ng’ombe wangu wote hunywa maji isipokuwa mmoja. Fimbo ya kuchunga
206. Ngozi ndani nyama juu. Firigisi
207. Nguo ivaliwayo kila siku isiyoingiwa na chawa. Nyusi
208. Nikicheka kinacheka, nikinuna kinanuna. Kioo
209. Nikienda arudi, nikirudi aenda. Kivuli majini
210. Niiita ‘baba’ huitika ‘baba’. Mwangwi
211. Nikija kwenye ndege wananifukuza, na nikienda kwenye wanyama hawanitaki. Popo
212. Nikimpiga huyu huyu alia. Utomvu wa papai
213. Nikimpiga mambusu. Puliza kidole wakati unapojikwaa
214. Nikimwita hunijibu nani. Mwangwi
215. Nikipewa chakula nala bali natema. Shoka
216. Nikitembea walio wafu huniamkia na walio hai hukaa kimya. Majani makavu na mabichi
217. Nikitembea yuko, nikikimbia yuko, nikiingia ndani hayupo. Kivuli
218. Ni kitu gani ambacho kutoa ni kuongeza? Shimo
219. Nikitupa mshale wangu mchana huenda mbali sana, lakini niutupapo usiku hauendi mbali. Jicho
220. Nikiwaambia ondokeni hukataa, lakini mjomba akitokea wote hukimbia. Umande na jua
221. Nilijenga nyumba yangu nikaiacha bila kuiezeka majani; lakini niliporudi nilikuta imekwisha ezekwa majani. Mahindi machanga
222. Nilijenga nyumba yangu yenye mlango mmoja. Jani la mgomba la nchani
223. Nilimkata alafu nikamridhia. Kupanda mbegu
224. Nilimtuma askari vitani akaniletea kondoo mweusi. Fuko
225. Nilipandia majanini nikashukia majanini. Mwiba
226. Nilipigwa na tonge la ugali la moto nilipopita msituni. Manyigu
227. Nilipitisha mkono wangu chini la ardhi, nikamshika beberu mkubwa sana. Kiazi kikuu
228. Nilipoangalia kwenye magereza ya Wazungu, nikaona wameketi juu ya mabati. Pelele
229. Nilipofika msituni nilikuta chungu cha pure kinachemka. Mzinga wa nyuki
230. Nilipoingia Rumi, alitoka mtu na wake kumi; kila mke na tundu kumi, kila tundu na kuku
kumi; kila kuku na mayai kumi. Mayai, kuku, tundu, wake, kumi kumi kumi. Wangapi
walikwenda Rumi? Hakuna
231. Nilipo, juu kuna miiba na chini vivyo hivyo; lakini sichomwi. Ulimi kinywani
232. Nilipokuwa mchanga nilikuwa na kijikia lakini sasa sinacho. Chura
233. Nilitembea na mwezangu naye hupita vichakani. Kivuli
234. Nimechoma fimbo yangu pakabaki pa kushikia tu. Njia
235. Nimefyeka mitende yote kiungani isipokuwa minazi miwili tu. Masikio
236. Nimejenga nyumba babu akaihamia kabla mimi sijahamia. Mjusi
237. Nimekata mti, akaja samba mwekundu akaukalia. Utomvu
238. Nimekata mti bara ukaangusha matawi pwani. Nzige
239. Nimekwenda na rafiki yangu kwa jirani, yeye akafika kabla yangu. Sauti ya nziga
240. Nimemtahiri binti wangu akatoa damu mchana kutwa. Kivuli
241. Nimempeleka kondoo wangu akatoa damu mchana kutwa. Mgomba
242. Nimemtuma mtu kumwamkua mtu, yeye amekuja, Yule aliyetumwa hajaja. Kuangua tunda Ana nazi
243. Nimemwacha mzee kikongwe mtoni anangojea mgeni kulaki. Mtego
244. Nimempandikiza mti wangu ukapeleka matawi ng’ambo ya mto. Kivuli
245. Nimesimama mbali nyikani lakini naonekani. Moto
246. Nimetembea kitambo, kukumbuka sikufunga nyumba. Dirisha Ana ufa
247. Nimetoka kutembea kutembea, nikashika ng’ombe mkia. Kata
248. Nimetupa mshale angani wala sitambui utateremsha ndege wa namna gani. Mimba
249. Nimeweka ndizi yangu, asubuhi siioni. Nyota
250. Nimezaliwa na mguu mmoja. Uyoga
251. Nimezungukwa na adui wengi, lakini siumizwi. Ulimi na meno
252. Nina kijiti change, nizidivyo kukikata ndivyo kizidivyo kuwa kirefu. Maisha
253. Nina kitu changu kitumiwacho na wengine kuliko mimi. Jina
254. Nina kitu kizuri sana nyumbani, lakini siwezi kukichukua. Dada
255. Nina kitu nipendacho ambacho hata baba, mama, dada, kaka hata na mgeni nimpendaye sana siwezi kumwazima. Mke
256. Nina mwezi ndani ya bakuli. Maziwa
257. Nina ng’ombe wangu nisipomshika mkia hali majani. Jembe
258. Nina nyumba yangu imezungukwa na mifupa. Mdomo
259. Nina pango langu lilojaa mawe. Kinywa
260. Nina watoto wangu hamsini na wote nimewavisha visibau vyeupe. Kunguru
261. Nina watoto watatu, mmoja akitoka kazi haifanyiki. Mafiga
262. Nina badilika umbo langu baada ya kila muda mfupi. Kivuli
263. Ninachimba mizizi ya mti usio na mizizi. Jiwe
264. Ninacho, nakitumia, lakini kila nikitumiapo, sikiharibu ila nakipa rangi. Maji na mkojo
265. Ninakula vitu vyote vinono lakini sikui wala sinenepi. Chungu cha kupikia
266. Ninakwenda naye na kurudi naye. Kivuli
267. Ninao mlima ambao una msitu kileleleni tu. Kichwa
268. Nitokeapo kila mmoja asema namtazama yeye tu. Jua au mwezi
269. Njia yapitwa siku zote lakini haina alama. Njia ya jua au mwezi
270. Njoo hapa nije hapo. Kiraka
271. Nne nne mpaka pwani. Matendegu
272. Nusu mfu nusu hai. Sungura alalapo
273. Nyama ndogo imewashibisha wengi wala isiishe. Kinoo
274. Nyama ya Reale haijai kikombe. Mkufu
275. Nyanya yako ana huruma kukubeba ulalapo. Kitanda
276. Nyumba yangu ina makuti tele, lakini mvua ikinyesha huvuja. Mwembe
277. Nyumba yangu ina milango mingi. Kichuguu
278. Nyumba yangu ina nguzo moja. Uyoga
279. Nyumba yangu kubwa, haina mlango. Yai
280. Nyumba yangu kubwa, haina taa. Kaburi
281. Nyumba yangu kubwa hutembelewa mgongoni. Konokono
O
282. Oh! Mwanamke aliyevunja chungu mshangao wake
283. Ondoka nikae. Maji ya mfereji
P
284. Paa alipenga hata pua ikapasuka. Mbarika
285. Palikuwepo watu watatu wakivuka mto. Mmoja alivuka pasipo kukanyaga maji wala kuyaona; wa pili aliyaona maji lakini alivuka bila kuyakanyaga; wa tatu aliyaona na kuyakanyaga alipovuka.
Ni nani hawa? Was kwanza in Mtoto tumboni mwa mamake, was pili ni Mtoto aliyebebwa mgongoni, was tatu ni mama mwenyewe
286. Panda ngazi polepole. Sima ya ugali
287. Para hata Maka. Utelezi
288. Pete ya mfalme ina tundu katikati. Kata ya kuchukulia mizigo
289. Poopoo mbili zavuka mto. Macho
290. Po pote niendako anifuata. Kivuli
R
291. Rafiki yangu ana mguu mmoja. Uyoga
292. Reli yangu hutandika ardhini. Siafu
293. Ruka Riba. Maiti
S
294. Shamba langu kubwa lakini mavuno hayajazi kiganja. Nywele kichwani
295. Shamba langu miti mitano tu. Mkono wa vidole
296. Shangazi yangu ni mrefu sana lakini hafikii tumbo la kondoo. Njia
297. Sijui aendako wala atokako. Upepo
298. Sijui afanyavyo. Nyoka apandavyo mtini
299. Sina dada wala kaka, lakini baba wa huyu jamaa ni mtoto wa babangu. Ni nani huyo? Mtoto wangu
300. Subiri kidogo! Miiba
301. Sultani alipiga mbiu watu waje kufanya kazi yake lakini wakashindwa. Maji
T
302. Taa ya bure. Jua au mwezi
303. Taa ya Mwarabu inapepea. Kilemba
304. Tajiri aniweka mfukoni na maskini anitupa. Makamasi
305. Tandika kitanga tule kunazi. Nyota
306. Tangu kuzaliwa kwake sijamwona asimame wala kukimbia. Mkufu
307. Tatarata mpaka ng’ambo ya mto. Utando wa baibui
308. Tatu tatu mpaka pwani. Mafiga
309. Tega nikutegue. Mwiba
310. Teke teke huzaa gumugumu, na gumugumu huzaa teke teke. Mahindi ama yai
311. Tengeneza kiwanja kikubwa kabila Fulani lije kupigania. Mbono
312. Tonge la ugali lanifikisha pwani. Jicho
313. Tukate kwa visu ambacho hakitakatika. Maji
314. Tulikaribishwa mahali na mdogo wangu, yeye akaanza kushiba kabla yangu. Kucha
315. Tuliua ng’ombe na babu, kila ajaye hukata. Kinoo
316. Tuliua ng’ombe wawili ngozi ni sawasawa. Mbingu na nchi
317. Tumvike mwanamke huyu nguo. Kuezeka nyumba
318. Tunajengajenga matiti juu. Mapapai
319. Twamsikia lakini hatumwoni. Sauti
U
320. Ukimcheka atakucheka, ukimwomba atakuomba. Mwangwi
321. Ukimwita kwa nguvu hasikii, lakini ukimwita polepole husikia. Fisi
322. Ukimwona anakuona. Jua
323. Ukitaka kufahamu ana mbio, mwonyeshe moto. Kinyonga
324. Ukitembea ulimwengu wote utakosa nyayo. Mwamba
325. Ukiukata haukatiki, ukiushika haushikiki. Moshi
326. Ukiwa mbali waweza kumwona Fulani umatini. Tundu LA sindano
327. Ukoo wa liwali hauna haya. Wanyama
328. Ule usile mamoja. Kifo
329. Umempiga sungura akatoa unga. Funds LA mbuyu
330. Unatembea naye wote umjiao atakuona. Bakora
331. Upande wote umjiao atakuona. Kinyonga
332. Ushuru wa njia wKujikwaa Kujikwaa
333. Utahesabu mchana na usiku na hutamaliza kuhesabu. Nywele
V
334. Viti kumi nyumbani, tisa vyakalika lakini kimoja hakikaliki. Moto
W
335. Wake wa mjomba kimo kimoja. Vipande vya kweme
336. Wako karibu lakini hawasalimiani. Nyumba ama kuta zinazoelekeana
337. Wanakuja mmoja mmoja na kujiunga kuwa kitu kimoja. Matone ya mvua
338. Wanameza watu jua linapokuchwa. Nyumba
339. Wanamwua nyoka. Watu wanaotwanga
340. Wanangu wawili hugombana mchana, usiku hupatana. Mlango
341. Wanao wakati wao wa kuringa, nao ni weupe kama barafu. Nyota
342. Wanapanda mlima kwa makoti mazuri meusi na meupe. Vipepeo
343. Wanastarehe darini. Panya
344. Wanatembea lakini hawatembelewi. Macho
345. Watoto wa mtu mmoja hulala chini kila mwaka. Maboga
346. Watoto wangu wana vilemba, asio kilemba si mwanangu. Fuu
347. Watoto wangu wote nimewavika kofia nyekundu. Jogoo
348. Watoto wangu wote wamebeba vifurushi. Vitovu
349. Watu ishirini walipanda juu ya mti, wawili wakaona chungwa, watano wakalichuma, kumi wakalimenya, wote wakaridhirika mtu mmoja alile. Je, ni watu gani hao? Waliopanda ni vidole vya miguu na mikono, walioona ni macho mawili, waliochuma ni vidole vitano vya mikono, waliomenya ni vidole vya mikono yote miwili, na aliyelila ni mdomo
350. Watu waliokaa na kuvaa kofia nyekundu. Kuku, katani au mahindi
351. Watu wamehama askari wekundu wakazidi nyikani. Viroboto
352. Watu wawili hupendana sana; kati ya mchana hufuatana ingawa mmoja ni dhaifu. Usiku mdhaifu
haonekani tena. Kivuli
353. Watu wote ketini tumfinye mchawi. Kula ugali
354. Wewe kipofu unaenda wapi huko juu? Mkweme
Y
355. Yaenda mbali lakini haiondoki ilipo. Njia
Z
356. Zilitazamana na mpaka sasa hazijakutana. Kingo za mto
357. Ziwa dogo linarusha mchanga. Chungu jikoni
358. Ziwa kubwa, lakini naogelea ukingoni tu. Moto
Katika makundi ya wanafunzi wawili wawili, watunge kifungu cha habari ambacho kinadhihirisha matumizi ya nahau zisizopungua tano.
Mfano wa kifungu chenye kutumia nahau zisizopungua tano
Kulikuwa familia moja ya Baba , bibi na watoto. Wanaishi kijiji Maendeleo. Familia hii ina matatizo ya makao, kupata chakula si kitu rahisi kwao, watoto hupekua….. Kila wakati baba akipata pesa kazi yake ni kuponda raha na kuvaa miwani. Haleti chochote nyumbani.
Kwa ushirikiano wa watoto na mama wao walijijengea nyumba ya mbavu za mbwa na mahali pa kwenda kujisaidia. Baadaye, baba naye alitoa mchango wake na kuepukana na tabia zote mbaya alizokuwa nazo. Walianza kuwa na maendeleo na kuishi kwa amani.
Watoto wao walikomaa na kufika kwa umri wa kujipatia jiko. Msichana wake alipata kijana ambaye alikuwa na nia ya kumuoa. Walikuwa pete na kidole.
Watoto wote walibahatika katika familia zao na baba na mama nao wanashukuru Mungu aliyewasidia. Hivi sasa ni famalia tajiri. 106
MAJIBU KUHUSU TATHMINI YA MADA YA PILI
Sanaa ni ufundi unaowakilisha mawazo na hisia alizo nazo binadamu kwa njia ya ubunifu.
Kuna aina mbalimbali za sanaa kama vile uchoraji, uchongaji, ususi, uhunzi, usonara, fasihi, uashi, sinema, uimbaji, ufinyanzi, ufumaji, upishi, ushonaji, udarizi n.k.
Sanaa ina nafasi kubwa kwa ujenzi wa taifa, kwani hupunguza ukosefu wa ajira na huwezesha jamii kutosheleza baadhi ya mahitaji yao ya kila siku kupita kazi mbalimbali zinazofanywa na wasanii. Wasanii nao hujiendeleza kiuchumi kutokana na pato linalotoka kwenye kazi zao .
Tanzu za fasihi simulizi ni:
Hadithi
Methali
Nahau
Vitendawili
Nyimbo na mashairi
Fasihi ina umuhimu mkubwa katika jamii. Katika jamii fasihi inaweza:
Kuelimisha jamii
Kuburudisha jamii,
Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii,
Kudumisha na kuendeleza lugha
Kuunganisha jamii,
Kukuza uwezo wa kufikiri,
Kumtajirisha msanii
Fasihi inaweza kuwa chanzo cha madhara katika jamii inapotumiwa vibaya kupitia nyimbo na methali zinazochochea ubaguzi na uadui baina ya wanajamii. Mfano ni jinsi nyimbo zilivyochochea uhasama baina ya wananchi na kuishia kwenye mauwaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mnamo mwaka wa 1994.
Soga
Huu ndio mwisho wa hadithi au Hadithi inakomea hapa.
“Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” Methali hii inamaanisha kwamba jinsi unavyomlea mtoto wako ndivyo atakavyokua. Yaani ukimpa malezi mazuri naye atakuwa mzuri, yakiwa mabaya naye atakuwa mbaya vile vile.
Fasihi simulizi imeelezwa kwa namna tofauti na wataalamu mbalimbali wa fasihi.
Finnegan (1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalumu. Katika fasili hii Finnegan hajagusia mambo muhimu katika fasihi simulizi kama vile muktadha, namna ya uwasilishaji, uhifadhi na badala yake amejikita zaidi katika ubunifu alionao msanii anayeiumba fasihi husika.
Kirumbi (1975:15) ameona kwamba, fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu awali, kwa ajili hii basi, tutaona katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kusema).
Kutokana na Riro S. Matinde katika kitabu chake cha Dafina ya Lugha na Nadharia, (2012). Anasema; “Kiambishi hutokana na neno ambika ambapo kuambika ni kuweka kitu mahali kwa kukiegemeza kwa kingine”. Hivyo basi anaendelea kusema kuwa; “Viambishi ni vineno vilivyoshikishwa katika mzizi wa kitenzi, kabla na hata baada ya mzizi wa kitenzi hicho”.
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa viambishi ni maneno yanayowekwa mwanzoni au mwishoni mwa kitenzi na kuleta maana fulani. Pia tunaweza kusema kuwa kiambishi ni silahi inayofungamanishwa na mzizi wa neno, kwa hiyo kiambishi ni Mofimu Tegemezi.
Riro S. Matinde anaendelea kusema kuwa kuna aina mbili za viambishi ambavyo ni:-
(1)Viambishi Awali – hivi ni viambishi ambavyo hutokea mwanzoni mwa Kitenzi (kabla ya mzizi) na huwa vya aina mbalimbali.
(2)Viambishi Tamati – Hivi ni viambishi ambavyo hutokea mwishoni mwa Kitenzi (baada ya mzizi).
Viambishi vya Mnyambuliko:
Vitenzi hunyumbuliwa au kurefushwa kwa kuongezwa viambishi ambavyo hudokeza kauli mbalimbali kati ya Kitenzi na Kiishio. Viambishi hivi vya mnyambuliko ni viambishi ambavyo hutokea baada ya mzizi wa kitenzi. Huwa upande wa kulia wa mzizi. Matinde anaeleza kuwa Viambishi hivi huwa na uamilifu ufuatao:
(a)Kiishio hicho ni kiambishi ambacho hutokea mwishoni mwa Kitenzi, aghalabu {a} hutokea katika vitenzi vinavyotokana na lugha za kibantu ilihali {e}au {i} au {u} hutokea katika vitenzi vyenye asili ya lugha za kigeni, mathalani ingia, ongoza, vua, starehe, ahidi, sahau na vinginevyo vingi.
(b)Virejeshi – virejeshi hutumika kulingana na ngeli za nomino, viambishi hivi hutuelekeza kwa mtenda au mtendwa katika baadhi ya vitenzi.
Kwa mfano:
(i) Vibaka wasumbuao mjini wmeongezeka mara dufu.
(ii) Akufukuzaye hakwambii toka.
(iii)Kimsumbuacho ni urembo wake.
(iv)Amwambiaye uongo ni bibi yake.
Kwa maana hiyo tunaweza kusema kuwa viambishi vya mnyambuliko wa vitenzi hubadilika Kisintaksia kulingana na mnyambuliko wa vitenzi. Kwani kama inavyojulikana kuwa Sintaksia ni tawi la Isimu linalojishughulisha na maumbo mbalimbali ya maneno.
Kutokana na maelezo hayo hapo juu tunaweza kusema kwamba athari za viambishi vinyambulishi katika kitenzi zinaweza kuonekana katika kauli mbalimbali kama ifuatavyo:
(i) Kuali ya kutendea.
(ii)Kauli ya kutendewa .
(iii)Kauli ya kutendana .
(iv)Kauli ya kutendesha.
(i)Kauli ya kutendea – Kauli hii huonyesha hali ya kumfanyia mtu/kitu jambo fulani, na hapa atahari ya kiambishi huonekana pale ambapo Kitenzi hunyambuliwa au hurefushwa. Kwa mfano:
Soma – som-e-a.
Imba – imb-i-a.
Cheza – chez-e-a.
Osha – osh-e-a
(ii) Kauli ya kutendewa – Kauli hii huonyesha mtu / kitu kufanyiwa jambo fulani na mtu/kitu mwininge na athari ya kiambishi huonekana kama ifuatavyo:-
Weka – wek-ew-a.
Lima – Lim-iw-a.
Lipa – Lip-iw-a.
Beba – beb-ew-a.
(iii) Kauli ya kutendana – Hii ni ile hali ya kumfanya mtu kitendo naye anakufanya hivyo hivyo:
Mfano:
Piga – pig-an-a.
Pika – piki-a-na.
Omba – omb-a-n-a.
Fanya – fany-a-n-a.
(iv) Kauli ya kutendesha – Hii ni ile hali ya kumfanya mtu atende jambo Fulani. Mfano wa athari za vitenzi vinyambulishi katika kauli hii ya kutendesha ni kama ifuatavyo:
Andika – andik-ish-a.
Lima – lim-ish-a.
Cheza – chez-esh-a.
Soma – som-esh-a.
Hivyo basi kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa viambishi vinyambulishi vina athari katika vitenzi kwani huonyesha kauli mbalimbali. Pia ambapo vitenzi huyambuliwa au kurefusha
Eleza maana ya ‘kiimbo’
Kiimbo ni sauti maalum inayojitokeza unapotamka maneno fulani. (kupanda na kushuka kwa sauti)
Tunga sentensi mbili zinazodhihirisha uamilifu wa aina mbalimbali wa kiimbo.
Mama ameenda sokoni? -swali
Mama ameenda sokoni. -kauli
Tunga sentensi ya hali timilifu ukitumia kiunganishi cha kibantu
Mwalimu na mwanafunzi wameenda nyumbani.
na- kiunganishi cha kibantu
wameenda – hali timilifu
Kazi hii imekuwa ngumu kwangu. (maliza kwa ….ngumu)
Kwangu, kazi hii imekuwa ngumu.
Andika sentensi hii kwa hali ya ukubwa, wakati uliopita
Ningepelekewa huyu ndama nyumbani ningefurahi.
Nilipelekewa hilo dama jumbani nikafurahi.
Tunga sentensi kutumia kirejeshi cha tamati.
Kiti wakitumiacho kimevunjika.
Kirejeshi tamati ni ‘cho’
Taja yambwa za sentensi ifuatayo :
Mjomba hakupikiwa mlo wa leo kwa bidii.
Mjomba – Yambwa tendewa:
Mlo- Yambwa tendwa
Tunga sentensi kanushi kutumia kiambishi ‘a’
Mtoto asipolishwa vizuri, hawezi kulala.
Andika miundo yoyote miwili ya nomino katika ngeli ya U-ZI huku ukitoa mifano
U-ny uzi-nyuzi
u-nd ulimi-ndimi
w-ny wembe-nyembe
u- ukuta -kuta
Bainisha vitate vifuatavyo kwa kutunga sentensi moja. (alama 2)
kaza, kasa.
Mvuvi alikaza kamba alipomuona kasa akiwa ndani ya wavu.
Taja ala za kutamkia vitamkwa vifuatavyo.
/v/g/j/t/
v- Midomo + Meno
g – Kaakaa Laini
j- kaa kaa ngumu
t- Ufizi
Bainisha shamirisho katika sentensi: (alama 3)
Mwalimu atawasimulia wanafunzi hadithi kwa kipaza sauti
Mwalimu-shamrisho kitondo,
Hadithi- shamrisho kipozi,
kwa kipaza sauti- shamrisho ala
Toa mifano miwili ya matumizi ya ritifaa(’)
Kuonesha king’ong’o kwa mfano ng’ombe
Kuonyesha nambari iliyoachwa kwa mfano ’99
Walipokuwa wanasoma mgeni wa heshima alifika (andika kwa wakati ujao)
Watakapokuwa wakisoma mgeni wa heshima atafika.
Tunga sentensi yenye ni uundo ufuatao:
S KN(N+U+N+V)+KT(T+E+E)
Mama na mtoto wake wanatembea haraka sana.
Tunga sentensi mbili kutofautisha vitate hivi kimaana. (alama 2)
(i) Hawara
(ii) Hawala
Hawara alifukuzwa nyumbani kwa kuwa mzembe.
Alipomaliza kazi, alilipwa kwa hawala.
Kanusha bila kutumia ‘amba’
Nitavaa nguo ambayo ni safi.
Sitafaa nguo iliyo safi.
SWALI: Kwa kutumia mifano ya virai nomino vinavyoundwa na nomino zaidi ya moja na kiunganishi “na”, bainisha na kufafanua kinagaubaga mikakati inayotumiwa na wazungumzaji wa Kiswahili kupatanisha kisarufi virai vya namna hiyo na maneno mengine yanayoambatana navyo. Mifano yako ijumuishe nomino za kutoka ngeli moja na ngeli tofautitofauti. Kwa mfano, ‘baba na mama’, ‘heshima na wema’, ‘nguo na farasi’, ‘chapati na maziwa’, ‘kitumbua na sahani’ na kadhalika.
SWALI – Visa katika tamthiliya hupangiliwa kimgogoro na kuchukua umbo la pembe tatu. Thibitisha dai hili ukionesha hatua tano za ujenzi wa mgogoro katika tamthiliya mbili ulizosoma.
Kirai ni neno au kifungu cha maneno chenye neno kuu moja. Kirai huweza kuwa neno moja (neno kuu peke yake) au neno zaidi ya moja (neno kuu na kijalizo). Neno kuu la kirai ndilo hutambulisha aina ya kirai. Neno kuu ni lile linalotawala na kumiliki maneno mengine katika tungo. Katika sintaksia ya Kiswahili maneno makuu ni matano tu ambayo ni:
Nomino
Kivumishi
Kitenzi
Kielezi
Kihusishi
Viwakilishi na vihisishi sio kategoria za virai kwa sababu zifuatazo:
Moja, maneno hayo si maneno makuu kwa sababu hayamiliki na kutawala maneno ya kategoria nyingine hivyo hayana sifa ya kuwa virai.
Pili, maneno karibu yote katika lugha ya Kiswahili huweza kufanya kazi ya vihisishi yanapowekewa alama ya kushangaa.
Mfano:
Kitenzi: amepita………………..amepita!
Nomino : Juma………………..Juma!
Kiwakilishi: wewe……………wewe!
Tatu, viwakilishi hubadili kategoria na kuwa vivumishi vinapotanguliwa na nomino katika tungo, hivyo dhana ya uwakilishi hutokea tu vinapokaa mwanzoni mwa tungo.
Mfano:
Huyu ni mkorofi
Zile zimeondolewa
Mtoto huyu ni mkorofi
Ndizi zile zimeondolewa
Nne, maneno kama viwakilishi hubeba uamilifu wa namna mbili yani kuwa viwakilishi na vivumishi, maneno yanayosimama kama viwakilishi husimama pia kama vivumishi.
Mfano:
Huyu analima shamba
Mzee huyu analima shamba
Tano, uanishaji wa kategoria za virai huzingatia uhusiano baina ya neno kuu na maneno mengine, viwakilishi na vihisishi si mojawapo ya maneno makuu katika kundi la maneno makuu, hivyo maneno hayo hayawezi kutambulisha kirai chochote.
Sita, uainishaji wa kategoria za virai tangu kipindi cha Sarufi ya mwanzo haukuzingatia uamilifu wa maneno bali uwezo wa neno kumiliki na kutawala maneno mengine hivyo maneno yaliyoshindwa kumiliki na kutawala maneno mengine kama vile viwakilishi, vihisishi na viunganishi hayakuwekwa kwenye kategoria za virai.
Saba, vihisishi kwa kawaida vihisishi ni maneno ambayo huwa hayana uhusiano wa kisarufi na aina nyingine za maneno katika tungo. Hivyo vihisishi hujitegemea na kujitosheleza.
Nane, vihisishi huweza kuondolewa katika sentensi bila ya kuathiri muundo wa sentensi husika. Hata hivyo, viingizi huipa sentensi dhamira/hali fulani.
Kwa ujumla dhana ya kirai ni ya kisintaksia na inadhihirika zaidi neno linapotawala na kumiliki neno lingine ndiyo maana tunazungumzia kuwepo kwa neno kuu kama kitambulisho cha kirai husika.
Posted by: MwlMaeda - 08-28-2021, 08:06 AM - Forum: Riwaya
- No Replies
Riwaya ya ‘Babu Alipofufuka’ imeandikwa na mwandishi maarufu wa kazi za fasihi na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed Mohammed, na kuchapishwa na Jomo Kenyatta Foundation mwaka 2001. Katika gamba lake la mbele, pameandikwa: “pengine ni riwaya ya ujasiri mno kupita zote Said A. Mohammed alizowaji kuandika.” Na hivyo hasa ndivyo ilivyo – hii ni riwaya ya kijasiri, ya kimapinduzi.
Hii ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kejeli, lakini yenye mchomo mkali kwa wale wanaoelekezewa kejeli hiyo – yaani watawala waovu – na pia inayoibua hisia nzito kwa wale wanaoathirika na uovu wa watawala – yaani raia wa kawaida.
Uovu wenyewe unadhihirishwa katika riwaya hii kwa namna ya tashnina na inda, lakini katika hali inayowiana sana na ukweli halisi uliomo katika maisha ya kila siku kwenye mataifa yetu ya dunia inayoambiwa inaendelea. Hadithi nzima inasimuliwa kupitia mazingira yasiyo ya kawaida. Huyo Babu mwenyewe Aliyefufuka anatujia kwa umbo la ajabuajabu kupitia kichwani mwa mjukuu wake, K, ambaye ndiye muhusika mkuu. K mwenyewe ni sehemu ya hao watawala ambao kwao kijembe cha riwaya nzima kinaelekezwa. Kwa ustadi wa hali ya juu, mwandishi anampa Babu nguvu za kuziunganisha dunia zetu mbili – baina ya ile tuionayo kwa macho ya nje na ile ionekanayo kwa jicho la ndani tu.
Baina ya dunia hizi mbili, ndipo msomaji anapopewa taswira halisi ya tafauti za waziwazi na za kificho walizonazo wanaoishi ndani yao. Upande mmoja ni maisha ya starehe na anasa za watawala, kule kujilabu na kujitapa kwao, ule uroho na tamaa zao zisizokwisha. Upande wa pili ni maisha magumu ya watawaliwa, kule kutumai na kutamauka kwako, kule kuinuka na kuanguka kwao, na kule kupambana na kujipapatuwa kwao kutoka makucha ya “wenye dunia yao”.
Katika ukurasa wa 14 hadi 15, kwa mfano, tunakutaka na maelezo kuhusu K ambayo yanawasilisha hisia zake za kuutaka na kuupenda ufakhari kama ilivyo kawaida ya watawala wa aina yake:
“Mbali na gari, kulikuwa pia na kasri la kuonewa fahari. Na fahari ndiyo madhumuni yenyewe. Na kasri lake K linamstahiki kwa kila hali, kwa kile cheo cha kiungo. Kama chumvi na chakula alikuwa. Bila ya yeye, mengi ya wakubwa na wadogo hayachapuki… Mjengo wa kasri lake ni wa aina ya zile husuni za tasnifa tunazoziona kwenye snema za filamu za sayansi ya kubuni.”
Wakati akina K wakiishi maisha hayo ya ukwasi na kujitanua, akina Kali ndio muhanga wa anasa hizo za watawala. Kwao maisha ni msegemnege na hali zao ni ngumu kupindukia. Huko ndiko kwenye ‘maitikwenenda’ kama wanavyoitwa na mwandishi na walivyowahi kuitwa na Sembene Ousmane kwenye God’s Bits of Wood au Ayi Kwei Armah kwenye The Beautiful Ones Are Not Yet Born.
Katika ukurasa wa 115 hadi 116, kwa mfano, tunasimuliwa maisha ya watu kula togonya na mboga ya kikwayakwaya sio kwa kupenda, bali kwa kuwa hawana namna nyengine. Huku ndiko ambako mtu anakwenda hospitalini kusaka matibabu, lakini anaondoka akiwa ameongezwa maradhi mengine zaidi kwa kuwa serikali imezitelekeza zahanati zake:
“Walipofika zahanati, mlango ulikuwa wazi, lakini mwuguzi aliyekuwa zamuni hayupo. Ilichukuwa saa nzima mpaka alipopatikana. Alikuwa kenda kumpiga mtu sindano kwa pesa. Alipofika alimkagua Kali, alisema anahitajia wembe wa kumnyoa nywele. Kisha uzi wa kushonea anao lakini anahitajia sindano au shazia ambayo hanayo. Alisema japo ya kushonea nguo inafaa. Zaidi ya hayo hana vidonge vya kuondolea maumivu. Plasta pia hakuna… Kali akanyolewa bila maji, akashonwa bila ya sindano ya ganzi, akatiwa plasta na kupewa vidonge viwili vya asprini kubwia…. alipoondoka, juso na jichwa lake zima lilikuwa limemvimba.” (Uk. 121-22)
Huko kunaitwa Kataa na K anaamini kisa cha kuitwa hivyo ni kwa kuwa watu wa huko ni wakaidi na hawakubaliani hata kidogo na watawala wao. Ndiko hasa alikotokea K, lakini ambako mwenyewe amekutupa na kukusahau kwa miaka yote hiyo. Kwa ujumla, hali ya maisha ya watu wa huko ni duni sana, nyumba zao ni dhaifu na hawana pesa za kununulia hata mahitaji ya lazima:
“Mbele zaidi waliposonga wakipasua kiini cha miti na mimea iliyokuwa mali kubwa hapo zamani, maisha na uhali yalianza kujiliza. Vibanda viwili vilivyolalia yombo. Kitambo,,, vibanda vyengine vitano vikirukuu. Hatua… vibanda vyengine vikisujudu…. ghafla walitokeza mahala ambapo ungeweza kupapagaza jina la sokoni. Watu walionekana… wamesogelea chanja zilizowekwa biashara… wote wametumbua macho, bila ya kuweza kununua chochote. Wengine wanavitumbulia macho vidaka vya nazi. Wengine vichungwa, vilimau, viembe na vipapai… kwenye soko la samaki, mafungu ya dangaauronga na dagaaupapa yakishindana kutumbuliana macho na watu…” (Uk. 95)
Kwa hivyo, riwaya ya Babu Alipofufuka ni kielelezo cha usimulizi unaoakisi uhalisia wa dunia mbili zinazoishi ndani ya jamii moja kwenye mataifa yetu. Mwandishi anampa Babu nguvu za kumfanya mjukuu wake, muhusika mkuu K, azidurusu dunia hizo ambazo kwa kila hali zimekuwa sehemu yake – moja aliyotokea na akaikimbia na kuitelekeza na nyengine aliyokimbilia, kuipenda na kuitukuza. Babu yake alipofufuka na kumjia kwenye maisha yake ya ndani, ndipo anatoa wasaa kwa msomaji kuyaona yaliyomo kwenye nafsi za madhalimu na madhulumu na zinavyosawirika dunia zao.
Baada ya kuziona dunia hizo, mwandishi anamfanya msomaji wake ahitimishe kwa mambo matatu haya:
Kwanza, watu wa aina ya K, ambao wameendeleza dhuluma kubwa kwa kutumia vyeo na majina yao, huwa wanaishi na khofu ya milele ya kuporomoka. Matokeo yake, kila siku hutamani na kupigania kwenda juu na juu zaidi kusudi wasifikwe na walio chini, ambao wanadhani kuwa endapo mikono yao itawafikia tu, basi watawashika miguu na shingo zao na kuwaporomosha chini kwa kishindo kikubwa. Kwa hivyo, ishara yoyote ya kuporomoshwa huwatia jaka moyo kubwa na kuwatetemesha hadi machango. Katika ukurasa wa 92, mathalan, mwandishi anatuonesha namna K anavyogwaya akiliogopa anguko lake:
“Ghafla alijihisi anachukuliwa na lepe jengine lililomdidimiza katka singizi zito la ajabu. Alitumbukia kwenye singizi huku akienda. Lilikuja tu kwa hakika hilo singizi ama upepo wa ghafla. Lilikuja kumvaa na kumdidimiza kwenye maweko ya chini ya kiini cha dunia. Alihisi anazama kwenye dimbwi refu lisilo ukomo… di, di, di… alididimia mpaka akajihisi ameibuka pahala penye mwangaza wa maisha. Akajihisi kama katupwa hapo. Katupwa kama gunia. Moyo ukaanza kupiga beni alipogundua hivyo. Aa, kubwagwa kila siku yeye alikuwa akikuogopa. Kuanguka alikuchelea. Akihofu kutupwa, hasa namna hiyo.”
Pili, msomaji anahitimisha kuwa watawala wa aina ya K wanakuwa wanajijuwa hasa kwamba wamewakosea raia. Kwa hivyo, kila wanapokaa huwa wanajitia wasiwasi kuwa wanaandamwa au wanafuatwafuatwa na watu hao wenye hasira na wakati wowote wanaweza kulipiziwa kisasi kwa maovu yao. Hayo ndiyo matokeo ya kuishi kwa dhuluma. Siku zote huwa unakhofu kuwa madhulumu wako watakurudi kwa yale uliyowatenda. Huwa huko huru. Angalia vile wanavyopita barabarani kwenye magari yaliyofungwa vioo vyote, tena vyeusi visivyopenya risasi na bado mbele yao ving’ora mita kadhaa ili wapishwe njia peke yao na bado maaskari kibao na bunduki. Hawa hawafanyi yale kwa kupenda, bali kutokana na khofu waliyonayo kwa umma walioukosea (Uk.24-7). Wakati Babu anamzukia K kwa mara ya kwanza kwenye ndoto-macho zake, alijitambulisha kwa namna hii:
“Nikwambie tena, mimi ni babu yako; kisha niongeze kuwa mimi ni dhahiri kwa kisia kikubwa kuliko hata wewe, kwa sababu sina farakano na watu. Wala sina makiwa na utawa kama ulionao wewe. Sina hofu wala siogopi kama uogopavyo wewe. Nakwenda nipendapo. Nakutana na nimpendaye. Ufunguo wa kasi yangu ninao mwenyewe. Hakuna niliyemdhulumu.” (Uk. 21-2)
Tatu, msomaji anahitimisha kuwa khofu hizi za watawala zina uhalali wake na ni za kweli. Ni kweli kuwa wananchi walioonewa na kudhulumiwa kwa miaka mingi hufika pahala pa kusema “hapana” kwa watawala wao. Miongoni mwao huwa wanasema hivyo kwa maneno, wengine kwa vitendo, wengine wakiwa na akili zao na wengine tayari wameshachanganyikiwa kwa mateso ya muda mrefu. La muhimu ni kuwa wananchi hufika mahala wakasema “liwalo na liwe” lakini hawatakubali tena dhuluma nyengine dhidi yao. Katika ukurasa wa 92, K alimkuta Mussa katika eneo la Kataa akijisemea peke yake njiani:
“La, hatutaki, hata ikiwaje hatutali tena…. La, hatutaki, hata iwaje hatutali tena…. La, hatutaki, hata ikawaje, hatutali tena..”
Lakini madhulumu wengine huamua kwenda mbali zaidi ya kupita mitaani wakijisemea peke yao tu. Wao huamua kuwarudi madhalimu wao kwa namna yoyote ile wanayoiona inawafalia na wanaimudu. Mno yachosha eti! Na ni hiki ndicho ambacho kinadhihirika mwishoni, pale umma uliokwishachoshwa na udhalimu wa watawala wao, unapoingia barabarani na kuukabili mkono wa utawala.
“Nje aliwakuta wale mahasimu zake wamejipanga upande huu na huu wa njia. Sasa walikuwa mamia kwa mamia… Kuna waliochukuwa marungu na wengine mabango yaliyoandikwa maneno mengi…M’MEZIFISIDI NAFSI ZETU…. MMEVUNJA HESHIMA ZETU…. VIJANA WETU WANAPOTEA… VIFO NA NJAA NA MARADHI SABABU SI SISI… HATUNA NAFASI PANAPOSTAHIKI NAFASI ZETU… ARDHI INACHUKULIWA HIVI HIVI TUNAONA…. KESHO YETU IMO KATIKA GIZA…TUNAANGAMIA…TUMESHAKWENDA KAPA…na zaidi na zaidi…Mlio ule wa bunduki K aliusikia ndani apokuwa tayari ameshakua kitini ofisini mwake. Alitetemeka kwa muda. Lakini alipojishika, aligunduwa kwamba hata ofisini mambo yalikuwa yamegeuka pia.” (Uk. 154-56)
Riwaya inamalizika kwa kumuonesha K akipoteza kila kitu – ulwa, nyumba, gari na, zaidi kuliko yote, hata ile heshima aliyojidhani alikuwa nayo. Na mwisho anakufa kifo cha kidhalilifu kama alivyosababisha maelfu ya wengine kufa katika udhalilifu kwenye zama za madaraka yake.
“Alfajiri ya siku ya pili, watu wa kijiji kile waliamshwa na sauti ya jibwa kubwa, Biye aliloliita Doggy. Ilikuwa si kawaida jibwa kubwa kama lile kubweka kwa muda mrefu namna ile hapo kijijini. Walipoufuata mbweko wa jibwa, walimkuta K ananing’inia kwenye kigogo cha mti uliokuwa umeota katikati ya kaburi la Babu. Alikuwa mkavu keshang’ang’anaa.”(Uk.165)
Naam, hapa ndipo hasira ya umma ilipomfikisha K. Hapa, kwa hakika, ndipo kiuhalisia wafikishwapo watawala madhalimu wa aina yake. Hivyo ndivyo umma unavyomuhukumu mkosaji wake. Umma ukikosewa kiasi kikubwa kama hiki, ni wenyewe ndio ambao hushitaki, na wenyewe ukahukumu. Na hivi ndivyo Babu Alipofufuka na kumtahadharisha mjukuu wake, K:
“…Pia unashitakiwa na wakati ulioutumia vibaya…Unashitakiwa vile vile na matendo yako mwenyewe…matendo ya upotofu…Maovu yako mwenyewe….Hakuna uchaguzi. Huna njia. Wakati ukifika, utakwenda tu; utakwenda tu…” (Uk. 137) Chanzo >>>>>>>