“Kwa hakika hakuna tofauti kati ya vivumishi na vikumushi.” Vikumushi na vivumishi ni dhana mbili ambazo zimekuwa zikileta mkanganyiko mkubwa sana katika taaluma ya isimu. Maneno haya huweza kufanana na kufanya kazi sawa, lakini kwa upande mwingine huweza kutofautiana. Kama inavyojadiliwa hapa chini.
Chuo kikuu cha Oxford (2005) wamefasili kikumushi kuwa ni neno ambalo linaweza kuwa kivumishi au kielezi ambacho kinaelezea neno au kundi la maneno mengine (tafsiri). Katika fasili hii maana ya kikumishi imetolewa kiupana kwa kiasi fulani, lakini bado kikumushi kinaweza kuwa zaidi ya kivumishi au kielezi, na kuwa kitenzi na aina
nyingine za maneno. Khamisi na Kiango (2002:58) wameeleza maana ya kikumishi kuwa ni maneno ambayo siyo
vivumishi asilia, lakini hufanya kazi kama vivumishi, yaani kazi ya kukumusha (kuongeza sifa au taarifa muhimu) nomino.
Wanaendelea kusema kuwa vikumishi siyo vipashio vilivyo katika kiwango cha neno tu, bali ni pamoja na makundi ya maneno ambayo yamo katika kiwango cha kirai au kishazi. Mfano; Kikumushi nomino: baba watoto ; Kikumushi Kirai: baba wa taifa (KH) Kikumushi Kishazi: mtoto aliyeshinda . Hivyo basi kutokana na fasili hizo mbili zilizotolewa tunaweza kusema kuwa kikumushi huweza kufasiliwa katika mawanda finyu na mawanda mapana. Katika mawanda finyu; kikumushi ni maneno yanayotoa taarifa ya ziada kuhusu nomino. Mfano; watoto wangu , mtoto wa juma . Maneno wangu na wa Juma ni vikumushi vya nomino watoto na mtoto. Katika mawanda mapana: kikumushi ni maneno yanayotoa taarifa ya ziada kuhusu aina nyingi ne yoyote ya maneno yaani
nomino, kitenzi, kielezi.
Mfano; aliyeimba kwa madaha, Mfano wa pili; Anacheza vizuri sana. Neno kwa madaha na vizuri sana yanakumumusha vitenzi aliyeimba na anacheza vizuri. Kwa upande mwingine kivumishi kama aina mojawapo ya aina za maneno imefasiliwa na wataalamu kama ifuatavyo; Matei (2009:43) anasema kuwa “kivumishi ni neno ambalo hutoa maelezo zaidi kuhusu nomino au kiwakilishi cha nonimo. Ni neno ambalo huonesha sifa
mojawapo ya nomino/kiwakilishi cha nonimo.” Fasili hii inajitosheleza kwani mara nyingi kazi kubwa ya kivumishi ni kutoa sifa juu ya nonimo au kiwakilishi.
Mfano, Mtoto mzuri. Neno mzuri ni kivumishi kinachovumisha nomino mtoto. Baada ya kuelezea fasili mbalimbali za maneno makuu, maelezo yafuatayo huelezea kwa kina ni jinsi gani kivumishi ni kikumushi. Katika fasili ya kivumishi na kikumushi, huweza kuleta ufanano fulani kwani kivumishi hutoa maelezo zaidi kuhusu nomino. Pia
kwa maana finyu ya kikumushi ni kwamba kinatoa taarifa ya ziada kuhusu nomino. Hivyo basi kivumishi na kikumushi huelezea juu ya nomino.
Mfano, Kijana mtanashati, mchezaji mashuhuri . Kwa muktadha huu neno mtanashati na mashuhuri huelezea
juu ya nomino, hivyo maneno hayo yote ni vikumushi au vivumishi kwani vivumishi na vikumushi vyote hufanya kazi ya kutoa maelezo ya ziada juu ya nomino. Kutokana na kufanya kazi sawa katika sentensi, tofauti inaweza
isiwepo. Mfano, mwanafunzi msafi . Mwanafunzi aliyeugua amepona. Hivyo neno msafi katika sentensi ya kwanza ambayo ni kivumishi na aliyeugua katika sentensi ya pili ambayo ni kikumushi hufanya kazi sawa ya kutoa taarifa juu ya nomino.
Hata hivyo ufanano unaoonekana kati ya kivumishi na kikumushi ni pale tu kikumushi kitakapofasiliwa kiufinyu, lakini kikumushi kwa maana pana hudhihirisha tofauti kubwa sana kati ya kivumishi na kikumushi kama inavyooneshwa hapa chini. Kivumishi huwa ni neno moja lakini kikumushi huwa ni neno moja au zaidi. Mfano; ng’ombe mweusi anakunywa maji. Neno mweusi ni kivumishi ambapo ni neno moja. Mwalimu aliyenipa kalamu ameondoka. Katika sentensi hii neno aliyenipa kalamu ni kikumushi chenye zaidi ya neno moja. Hivyo kivumishi ni neno moja tu lakini kikumushi huweza kuwa neno moja au zaidi, kirai au kishazi.
Kivumishi hutoa taarifa kuhusu nomino au kiwakilishi tu lakini kikumushi hutoa taarifa zaidi juu ya nomino, viwakilishi na aina zingine za maneno. Mfano; kiongozi muadilifu huongoza kwa busara, wewe ni msafi kuliko wote.
Maneno muadilifu na msafi hutoa taarifa juu ya nomino na kiwakilishi. Mfano; anayetembea kwa maringo . Neno kwa maringo ni kikumishi kirai kihusishi ambacho hutoa taarifa juu ya kitenzi anayetembea. Mara nyingi neno kivumishi hutumika kuelezea aina ya maneno hayo katika muktadha wa kimuundo na kileksika lakini kikumushi hutumika kuelezea maneno hayo hayo (ambayo ni kivumishi) na maneno mengine katika muktadha wa kidhima,
huangalia kazi ya neno hilo. Mfano; mtoto mpole hulelewa vizuri. Neno mpole katika muktadha wa kimuundo ni
kivumishi lakini katika muktadha wa kidhima ni kikumushi kwani hufanya kazi ya kutoa taarifa juu ya nomino mtoto. Mfano mwingine, mwanafunzi mtukutu hafaulu vizuri. Neno mtukutu ni kivumishi kimuundo na kikumushi
kidhima. Kivumishi huweza kuwa katika ngazi ya neno na kirai katika tungo. Mfano; mchezaji mashuhuri . Neno mashuhuri ni aina ya tungo neno ambalo ni kivumishi na ni aina ya tungo kirai ambalo ni kirai kivumishi. Hivyo kivumishi hakiwezi kuvuka ngazi hizo mbili za tungo, lakini kikumushi huweza kuwa katika ngazi ya tungo neno,
kirai, kishazi na hata sentensi. Mfano; mwanafunzi anayesoma kwa bidii atafaulu mtihani . Neno mtihani limesimama kama kikumushi cha kitenzi atafaulu kama tungo neno. Kwa bidii ni kikumushi kirai, anayesoma ni kikumushi kishazi.
Utofauti mwingine hujitokeza katika dhana kwamba kila kivumishi ni kikumushi, lakini si kila kikumushi ni kivumishi. Hivyo basi kwa muktadha huu siyo dhahiri kuwa kivumishi ni kikumushi. Mfano; kijana mtukutu anaadhibiwa na mwalimu . Neno mtukutu ni kivumishi na ni kikumushi, lakini neno na mwalimu ni kikumushi na siyo kivumishi, hivyo ni kwa kiasi kidogo sana juu ya ufanano wa kivumishi na kikumushi.
Kwa kuhitimisha, kauli kuwa kivumishi ni kikumishi huthibitika tu endapo fasili ya kivumishi itakuwa katika muktadha wa maana finyu ambapo vyote huelezea juu ya nomino na hufanya kazi ya kutoa taarifa ya ziada juu ya nomino. Lakini kwa upande mwingine wa fasili ya kikumushi katika muktadha wa maana pana, kuna utofauti mkubwa kimuundo na kazi kati ya vikumishi na vivumishi. Hivyo basi kwa kiasi fulani vivumishi ni vikumushi na
kwa kiasi fulani vikumushi si vivumishi.
MAREJEO:
Khamisi, A.M na John, G.K. (2002). Uchanganuzi wa Sarufi ya Kiswahili . TUKI. Dar es salaam.
Chou Kikuu cha Oxford (2005). Advanced Learners Dictionary . Oxford University Press. U.S.A.
Matei, A.K. (2008). Darubini ya Sarufi. Phoenix Publishers. Nairobi.
Mitaala ni jumla ya mipango na uzoefu ulioratibiwa kwa ajili ya mafunzo ya aina fulani yenye malengo maalumu kwa wanafunzi. Mipango hiyo inaweza kuwa ni mambo, matendo na uzoefu wa aina yoyote ile ambayo wanafunzi wanapata chini ya uongozi na usimamizi wa shule. Hutegemea falsafa ya nchi na siasa inayoiongoza.
Mfano: nchini Tanzania falsafa ya nchi ni: Ujamaa na Kujitegemea (kutokana na siasa iliyokuwa ikiongoza chini ya Mwalimu Julius K. Nyerere. Falsafa ya elimu ni: Elimu ya Kujitegemea (inatokana na falsafa ya nchi). Madhumuni/Malengo Makuu ya Elimu nchini yameainishwa katika Sera ya Elimu ya Taifa na katika mihtasari ya masomo kwa kila ngazi (Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Juu)
Bila mwongozo wa falsafa ya nchi na madhumuni ya elimu kitaifa wakuza mitaala watakosa mwelekeo maalumu wa ukuzaji mitaala. Hivyo ina hatari ya kufanya mtaala uwe mkusanyiko wa mambo yasiyokuwa na mwelekeo maalumu kitaifa. Madhara yake ni watumiaji kukosa mwelekeo na msimamo maalumu unaolingana na mwelekeo wa kitaifa.
Sifa za mtaala
Kwa kawaida mtaala huzingatia taaluma (maarifa) ufundishaji (matendo) na kujifunza (uzoefu) katika kiwango au ngazi fulani ya elimu.
Pia mtaala lazima uoneshe walengwa wa mtaala (aina ya wanafunzi watakaotumia mtaala huo), kwa mfano chekechea, watoto wa shule za msingi na sekondari na walemavu
Muda utakaotumika kufundisha mtaala huo, kwa mfano miaka miwili saba na minne mitatu mitano n.k)
Sifa za walimu watakaofundisha mtaala huo mfano walimu wenye daraja A stashahada na shahada.
Vifaa vitakavyotumika kufundishia walengwa na njia na mbinu zitakazotumika kupima maendeleo ya wanafunzi na ubora wa mtaala.
Kwa hiyo mtaala ni jumla ya mpango uliondaliwa kwa ajili ya kufundishia na kujifunza kwa lengo la kuwapatia walegwa maarifa ,stadi na mielekeo mbalimbali. Nguzo kuu ya mtaala ni muhtasari ambayo hutumika katika kutekeleza mtaala huo.
Muhtasari: Ni mkusanyiko wa mada zinazokusudiwa ili kukamilisha kiwango fulani cha elimu , kazi au mafunzo maalumu.Katika shughuri za wakuza ukuzaji mitaala, wakuza mitaala wanapaswa kuongozwa na malengo makuu ya elimu yanayowekwa kitaifa.
Umuhimu wa kuwa na mtaala
Kudhibiti mfumo wa elimu
Kuongoza walimu katika ufundishaji ili wasitoke nje ya malengo makuu ya elimu na falsafa ya nchi
Kuwezesha kurekebisha na kuendeleza elimu
Kuweka malengo muhimu yaliyo kusudiwakufikia katika ufundishaji
Kuwa dira na mwongozo muhimu kwa walimu katika ufundishaji
Kutaja na kuelekeza nyenzo na vifaa vya kufundishia
Kuelekeza malengo makuu ya elimu katika jamii husika
Kuchukua taswira yote ya falsafa ya elimu ya nchi inayohusika.
Matumizi ya mtaala
Kusaidia walimu na wanafunzi kutambua malengo makuu yanayo kusudiwa kufikiwa katika utoaji wa elimu
Kufahamisha mwalimu na mwanafunzi kuhusu masomo au mada atakazo fundishwa ili kufikia malengo aliyojiwekea
Kumsaidia mwalimu kutambua na kuchagua njia za kufundishia zinazofaa ili aweze kufikia malengo aliyojiwekea
Kumsaidia mwalimu na mwanafunzi kuchagua na kufaragua vifaa vya kufundishia na kujifunzia mada mbalimbali
Kumwelekeza mwalimu kuhusu njia atakazopima maendeleo ya wanafunzi na ubora wa mtaala wenyewe.
Aina za mitaala
Mtaala rasmi
Mtaala usiyo rasmi
Mtaala ficho
Mtaala rasmi
Ni mkusanyo wa mambo yote anayopaswa kuyafanya na kuyafahamu mwanafunzi anapokuwa darasani. Au ni mtaala uliopangwa kwa madhumuni ya kumfundisha mwanafunzi katika mfumo rasmi wa elimu.
Sifa za mtaala rasmi
Huainisha na kuweka wazi mambo, matendo na uzoefu wa aina yoyote ile ambayo mwanafunzi ataupata chini ya uongozi na usimamizi wa shule yaani taaluma ufundishaji na kujifunza katika kiwango fulani cha elimu
Huweka wazi aina ya walengwa
Huweka wazi malengo ya kufundisha mtaala
Huweka wazi mambo, matendo na uzoefu ambao mwanafunzi ataupata chini ya uongozi wa shule au chuo
Huweka bayana njia ambazo mwalimu atatumia kufundishia
Huweka bayana njia za kupima maendeleo ya mwanafunzi
Kupunguza tofauti zinazoweza kutokea iwapo kila shule au jamii itajitungia mtaala wake
Kurahisisha kuandaa vifaa vya kujifunzia
Kurahisisha ufuatiliaji na upimaji wa maendeleo ya wanafunzi
Huweka bayana utaratibu wa kutahini na sifa za wale watakaofuzu baada ya kufundishwa na kutahiniwa kwa kuutumia mtaala husika.
Mapungufu ya mtaala rasmi
Humfanya mwanafunzi ashindwe kufanya mambo yote yaliyo nje ya darasa kama vile ufugaji uvuvi, mila na desturi ya jamii yake.
Mitaala isiyo rasmi
Ni mtaala unaofundisha mambo yote anayopaswa kujifunza mtoto nje ya mtaala ulio rasmi katika maisha ya kawaida ya kujifunzia. Mara nyingine mtaala huu huitwa mtaala uliofichika.
Mara nyingi mitaala hiyo huandaliwa kulingana na mahitaji ya jamii ya mwanafunzi na jamii husika kwa wakati ule.
Sifa za mtaala usio rasmi
Hutokana na jamii au mazingira anayoishi mwanafunzi
Mada au mambo anayofundishwa zinalenga kumpatia mwanafunzi maarifa na stadi za kutatua matatizo aliyo nayo kwa wakari ule
Hukazia maarifa na stadi zinazo lenga kutatua matatizo yanayokabili jamii husika
Unaweza ukakoma mara matatizo yanapomalizika
Kwa kawaida haupangwi na kuratibiwa na njia kwa njia zilizo rasmi
Mwanafunzi anaweza kupata maarifa na stadi bila kuwa chini ya usimamizi wa shule au chuo.
Mapungufu
Mwanafunzi hukosa ujuzi wa maarifa yaani mambo yote yanayofundishwa darasani katika mtaaala rasmi.
Mtaala ficho
Mtaala huu unajumuisha matendo yote yanayosaidia ujifunzaji usiokusudiwa au usioratibiwa. Kwa mfano ujifunzaji wa utii kwa mamlaka, kuwahi/kujali muda, usafiri nakadhalika. Yaani unajumuisha mambo yote ambayo hayaonekani kwenye muhtasari wa shule kama sehemu ya mtaala.
Vipengele vya mtaala
Katika mtaala vipengele vilivyo muhimu ni vitano ambavyo hufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kutegemeana:
Malengo ya mtaala
Maudhui
Njia za kufundishia
Zana
Tathmini
Vipengele hivi vitano hufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kutegemeana kama viungo vya mwili wa binadamu. Ni vigumu kuvitenganisha ila kwa faida ya kujifunza na kuelewa kwa undani, tutavitazama kimoja kimoja katika maelezo.
Malengo ya mtaala
Malengo ni matokeo au matarajio yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mpango/programu fulani. Mtaala wowote ule lazima uwe na malengo. Katika uwanja wa elimu, malengo ya mtaala ni mabadiliko ya tabia na mwenendo wyanayotarajiwa kupatikana kwa wanafunzi baada ya kupata programu fulani ya mafunzo.
Umuhimu wa malengo ya mtaala
Malengo kama kipengele cha msingi cha mtaala yana umuhimu mkubwa kwani:
Huwa ni msingi wa vipengele vingine vyote viine vya maudhui ya mtaala
Huwa ni msingi wa malengo katika ngazi/kiwango vyote vya elimu-elimu ya msingi, sekondari na vyuo
Huwa ni msingi wa shughuri za kazi za wakuza mitaala. Wakaguzi na walimu, wanafunzi na watawala wa elimu.
Malengo ya jumla na malengo mahususi
Malengo ya jumla ni matarajio au mabadiliko kitabia ambayo tunatarajia kuyaona kwa mtu ambae amepata elimu.Malengo ya jumla ni malengo na madhumuni ya elimu kitaifa yaliyokusudiwakutimizwa na program mbalimbaliza mafunzokatika viwango mbalimbali vya elimu. Kimsingi malengo haya yanatokana na sera ya elimu katika nchi husika.
Baadhi ya malengo ya kitaifa ni
kuongoza kuendeleza na kukuza vitu na uwezo wa watanzania ili waweze kutumia rasilimali zilizopo kuleta maendeleo yao binafsi na kwa Taifa zima
Kukuza ari ya Watanzania ili wapende kuthamini utamaduni, mila na desturi za nchi
Kuendelezana kukuza ndani ya Watanzania moyo wa kujiamini na tabia ya kisayansi, uelewa wao na kuuheshimu.
Sifa za malengo ya jumla
Huchukua muda mrefukukamilika. Mfano hadi mwisho wa programu
Siyorahisi kuyapima kwa sababu hayako wazi
Huchukua vitendo kama kujua, kufahamu n.k.
Malengo mahususi
Malengo mahususi ya mtaala hutokana na malengo ya jumla. Haya ni malengo yaliyokusudiwa kutimizwa na programu mbalimbali za mafunzo katika viwango mbalimbali vya elimu.
Ni kutokana na malengo mahususi kila kiwango cha ngazi fulani ya elimu ndiyo yanapatikana mahususi yanayowaongoza walimu katika kuandaa maazimio yao wanayofundishia darasani.
Maudhui haya ndio yawezayo kumuongoza mwalimu kutoa maarifa na stadi ambazo zinaweza kubadili tabia ya mwanafunzi ambayo inaweza kupimika.
Kwa mfano tunapofundisha somo la Hisabati,tunatarajia kuona mabadiliko fulani katika tabia ya mtoto kutokana na kujifunza somo zima au mada fulani. Mabadiliko hayo yanaweza yakawa maarifa,stadi au mwelekeo mwanafunzi anaouonyesha kutokana na kujifunza somo la Hisabati ambao hakuwa nao kabla ya kujifunza somo hilo.
Tunaweza kugawa malengo mahususi katika Nyanja tatu ambazo ni
Utambuzi
Stadi
Mwelekeo
Sifa za malengo mahususi
Ni malengo yaliowazi
Ni rahisi kupima kufanikiwa au kutofanikiwa kwake
Hutumia muda mfupi wa ukamilishaji wake
Huumia vitendo kama fafanua,taja,eleza n.k.
Maudhui
Katika kuunda maudhui ya mtaala ni vizuri kuzingatia maswali kama vile:
Ni maarifa na stadi zipi zinafaa kwa kiwango kipi cha elimu
Ni tabia na mwenendo upi unaofaa kurithiwa.
Misingi/vigezo vya kuchagua maudhui ya mtaala
Uthabiti: Uwezo wa maudhui katika kutimiza malengo ya masomo katika kiwango husika.
Umuhimu: Maudhui yanayopewa kipaumbele ni yale yanayolingana hali halisi ya mausha ya jamii, uchumi wan chi inayohusika. (Ni yale yenye umuhimu katika maisha ya walengwa).
Mvuto: Maudhui yafaayo ni yaleyenye kuvutia na yenye kuamsha ari ya mwanafunzi ya kupenda kufahamu maudhui hayo.
Kufundishika: Maudhui yawe na uwezo wa kufunzika/kufundishika yaani yaendane na uwezo wa walengwa.
Njia na mbinu: Maudhui yazingatie mbinu na njia za kujifunzia na kufundishia
Muda na idadi ya maada: Maudhui yazingatie muda wa program husika. Maudhui yanapoandaliwa huwakatika mfumo wamada kubwa na mada ndogo, kulingana na mfululizo huu unatakiwa uwe unaanzia na mada rahisina kuendelea hadi zile ngumu. Mpangilio wa aina hiyo ni muhimu kwani huhusishaujifunzaji na ufundishaji kulingana na umri wa wanafunzi.
Njia na mbinu
Ili kuweza kufanikisha tando zima la ufundishaji katika kufanikisha maudhui na malengo ya somo mwalimu hutumia vitendo mbalimbali vijulikanavyo kama njia. Na njia peke yake haiwezikufanikisha somo lazima isaidiwe na mbinu. Mbinu ni stadi maalumu inayobainisha ni jinsi gani ya kufundishia/kujifunzia itakvyowezeshwa katika tendo la kufundisha na kujifunza. Njia ni namna mwalimu anavyowasilisha mada katika mchakato mzima wa kufundisha.
Kuna njia mbili zinazoweza kutumika katika swala zima la kujifunzia na kujifunza:
Njia shirikishi
Njia isiyo shirikishi
Misingi ya kuchagua njia/mbinu
Maudhui: Hali ya somo lenyewe na maarifa ambayo mwanafunzi wanafunzi wanatakiwa wayapate hivyo maudhui yanatakiwa yafundishike.
Hali ya mwanafunzi: Umri wa mwanafunzi, kukomaa na kutokomaa kiakili, mazingira yao hivyo njia/mbinu ziendane na hali za walengwa.
Malengo: Nini malengo ya wanafunzi wanatakiwa kufanikisha nini katika maisha yao? Njia/mbiu lazima zifanikishe malengo yaliokusudiwa.
Mwalimu: Uwezo mwalimu katika kutumia nji/mbinu ujuzi na utaalamu wake.
Vifaa vya mtaala
Mtaala una vifaa vyake maalumu ambavyo vinatakiwa vitumike kwa usahihi ili kutekeleza mtaala kwa ufanisi. Vifaa hivyo ni:
Muhtasari
Vitabu vya kiada
Vitabu vya ziada
Kiongozi cha mwalimu
Kitabu cha mwalimu na rejea
Muhtasari
Muhtasari ni mwongozo unaotaja kwa kifupi tu mambo yote yanayotakiwa yafundishwe katika mwaka mzima katika darasa fukani au kwa miaka kadhaa kwa kila darasa kwa mmpangilio maalumu.
Muundo wa muhtasari
Muhtasari una sehemu kuu mbili:
Utangulizi: Hii ni sehemu ambayohuelekeza sababu za kuwepo kwa muhtasari huo, muundo wake , malengo ya elimu katika kiwango husika na malengo ya kufundisha somo hilo katika kiwango hicho.
Majedwali ya kutumia kufundishia: Hii ni sehemu ambayo huwa na maudhui ya somo husika yanayotakiwa kufundishwa kila mwaka. Majedwali ya kufundishia yana vipengele vikuu vilivyopangwa katika safukama ifuatavyo.
Vipengele vya muhtasari
Mada kuu na mada ndogo
Lengo la kufundishia mada hiyo
Mapendekezo ya njia za kufundishia na kujifunzia
Vifaa /zana za kujifunzia na kufundishia
Matumizi ya muhtasari
Kumwongoza mwalimu kuandaa maazimio ya kazi na maandalio ya masomo
Kuongoza waandishi wa kitabu cha kiada ,kiongozi cha mwalimu na vitabu vya rejea
Kuelekeza njia zifaazo katika kufundisha na kujifunzia
Kuandalia mwongozo wa upimaji wa maendeleo ya wanafunzi kwa mwaka au kwa kipindi cha miaka kadhaa
Kutathmini mtaala baada ya kipindi maalumu cha matumizi ya muhtasari huo.
Kitabu cha kiada
Ni kitabu ambacho kinafafanua mada zote za muhtasari kwa ukamilifu. Kitabu hiki ndicho kinachobeba maudhui ya somo kwa ukamilifu.Mfano vitabu malimbali vya masomo vilivyomo mashuleni.
Sifa za kitabu cha kiada
Kiwe chenye lugha rahisi inayo eleweka kulingana na kiwango cha mwanafunzi
Kiwe na mada zinazopangwa kwa mtiririko wenye mantiki kuanzia mada kuanzia mada rahisi hadi zile ngumu
Kiwe na maandishi yanayosomeka kwa urahisi ya kuvutia
Kiwe na maelekezo na mazoezi yanayomshirikisha mwanafunzi katika kujifunza
Kiwe kinaendana na muhtasari pamoja na kiongozi cha mwalimu.
Matumizi ya kitabu cha kiada
Mwalimu hukitumia kwa kuelekeza maarifa. Hutumiwa na mwanafunzi pia kwa kujikumbushia na kufanya marudio.
Uchambuzi wa kitabu cha kiada
Vitabu vingi vya kiada vimeandaliwa katika mitindo tofautitofauti, hivyo ni jukumu la mwalimu w somo pengine akishirikiana na wanafunzi kuchagua kitabu kinachofaa. Ili kuweza kufanya uamuzi wa kitabu kinachofaa huna budi kuchambua kwa kuzingatia mambo yafuatayo: Kwa kiasi gani mada zote za muhtasari zimefafanuliwa kwa ufanisi pamoja na kuzingatia sifa za kitabu cha kiada.
Kiongozi cha mwalimu
Hiki ni kitabu kinachompa mwalimu maelekezo ya mada ya kufundisha, jinsi ya kuifundisha, maudhui gani yafundishwe na kutumia vifaa au zana gani. Pia kinaitwa kitabu cha mwongozo kwa mwalimu.
Sifa za kiongozi cha mwalimu
Kiwe na utangulizi ambao unaelekeza mambo makuu na muhimu yatakayo zingatiwa katika ufundishaji. Mfano mgawanyo wa muda katika kufundisha mada mbalimbali. Mada kuu zitakazofundishwa.
Malengo mahsusi ya kufundisha kila mada
Mapendekezo ya njia na mbinu za kufundishia
Mazoezi ya kulingana na mada zilizoko katika kitabu cha kiada
Jinsi ya kupima ujifunzaji wa wanafunzi
Majibu ya mazoezi na na maswali yaliyomo katika kitabu cha kiada
Mapendekezo ya vitabu vya rejea vitakavyosaidia kutoa maarifa ya ziada kuhusu mada husika.
Umuhimu wa kitabu cha mwalimu
Humweleza mwalimu jambo la kufanya la kufanya humpa dira au mwelekeo wa ufundishaji
Humsaidia mwalimu kujijengea moyo wa kujiamini na hasa kama si mzoefu wa ufundishaji wa somo hilo
Humsaidia mwalimu katika kuandaa somo
Humpa mwalimu maudhui na mifano ya ziada kuzidi kuzidi kumpanua mawazo na upeo.
Dhana ya kitabu cha mwalimu
Ni kitabu kinachotoa maelezo ya kina kuhusu ufundishaji wa somo fulani
Kinaelezaa jinsi ya kutenda katika hatua zote tangua uandaaji wa somo, ufundishaji hadi upimaji
Ni mwongozo ambao unammpa mwalimu ujuzi wa ufundishaji.
Sifa za kitabu cha mwalimu
Kina vitendo vyote ambavyo mwalimu hupaswa kutenda katika hatua za ufundishaji
Kinaeleza jinsi ya kutekeleza kazi ya ufundishaji hatua kwa hatua
Huweza kutumiwa na mwanafunzi pia
Hutoa ufafanuzi wa mada kwa kiwango cha juu zaidi ili kupanua mawazo ya mwalimu na kumuimarisha zaidi kitaaluma.
Tofauti kati ya kitabu cha mwalimu na kiongozi cha mwalimu
Kitabu cha mwalimu humwelekeza hatua za kufuata katika kufundisha somo au kufanya jaribio fulani. Kiongozi cha mwalimu hupendekeza njia na mbinu mbalimbali za kufundisha somo.
Kitabu cha mwalimu huweza kutumiwa na mwanafunzi na mwalimu. Kiongozi cha mwalimu hutumiwa na mwalimu tu.
Kitabu cha mwalimu huhusika zaidi na mchakato au hatua za utendaji, kam vile utafitijaribio. Kiongozi cha mwalimu huhusika na jinsi ya kufundisha mada za masomo.kwa kawaida hutumika pamoja na kitabu cha kiada.
Vyanzo vya mitaala
Ni muhimu kujua vyanzo vya mtaala ili kuhakikisha vinahusishwa na kuzingatiwa wakati wa kuandaa mtaala. Vyanzo hivyo ni pamoja na
Jamii
Siasa ya nchi
Wanafunzi
Wazazi
Walimu
Waajiri
Wataalamu mbalimbali.
Marejeo
TET (1994), Ukuzaji mitaala na Kunasihi.KIUTA (DSM)
Wizara ya elimu na Utamaduni(2005).mpango wa mafunzo ya walimu kazini Daraja la IIIC/B-A: Moduli ya soma la Mitaala. Wizara ya elimu na Utamaduni.
TET (2013), Moduli ya kujifunzia somo la ualimu. Taasisi ya Elimu Tanzania (DSM). Retrieved on February 05,2014 from Http:www.luwingu.wordpress.com/Mitaala.