Nyerere wa Tanzania, kiongozi shujaa wa dunia – amepata kutukuka pande zote za dunia. Alizaliwa katika kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara. Alisoma elimu ya msingi katika shule ya Mwisenge – mojawapo ya shule za zamani sana hapa
nchini. Alipata elimu ya sekondari huko Tabora. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kabla ya kwenda huko Uingereza kusomea shahada ya M.A.
Baada ya uhuru toka Uingereza, Mwalimu Nyerere alishughulika sana na suala la ukombozi wa Tanganyika na Afrika kwa ujumla. Alionesha jitihada za wazi kupambana na mabeberu wa Kiingereza hadi uhuru wa Tanganyika ukapatikana tarehe 9/12/1961. Tanganyika ikawa ya kwanza kupata uhuru wake ukilinganisha na cnhi zote za Afrika ya Mashariki na kati – sifa kuu kwa Nyerere wa Tanganyika.
Nyerere alishirikiana na Karume kuziunganisha nchi hizo na kuzaa Tanzania – jina lililotumika na kuheshimiwa kote ulimwenguni. Wakati Nyerere akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar alitamka maneno ya hekima yafuatayo:
“Tumeamua kuziunganisha nchi zetu ili kuimarisha umoja wa Afrika. Naamini kuwa maadui wetu watachukia na kuhuzunika kwa kitendo hiki cha kishujaa tulichokifanya, lakini daima hatutaogopa chochote. Muungano wetu utadumu milele na milele. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika. Amina!”
Sifa ya pekee inayomtofautisha Mwalimu Nyerere unapomlinganisha na wanafalsafa wengine duniani kama vile Karl Marx na Mao ni kwamba yeye aliwapigania wanyonge wote kote ulimwenguni bila kujali ubaguzi wa rangi, kabila, taifa au bara. Aliwatetea wanyonge wa Afrika. Aliwapigania wanyonge wa Ulaya na Mashariki. Aliwapigania wanyonge wa bara la Asia. Halii kadhalika aliwapigania na kuwatetea wanyonge wa bara la Amerika ya Kusini. Hivyo ni sifa ya pekeeinayofaa kumtofautisha na wanafalsafa wengine waliomtangulia.
Nyerere atatukuzwa daima kwa ushujaa wake. Alikuwa si kiongozi wa kujikombakomba kwa matifa mengine ya kibeberu. Alipotishiwa au kuwekewa vikwazo/vitisho, alivunja mara moja uhusiano wa kidiplomasia na taifa linalohusika. Kwa mfano mwaka 1965 alivunja uhusiano wa kidiplomasia nan chi ya Uingereza baada ya nchi hiyo kuitangaza nchi ya Zimbabwe kama koloni lake la kudumu la Walowezi. Kitendo
hiki kilimpatia sifa na heshima kubwa hapa Afrika na duniani kote – kwa wapenda amani. Ingawa ni vigumu kuzitaja sifa zake mpaka mwisho, lakini sifa ya kupiga makelele katika majukwaa ya kimataifa haitaweza kusahaulika. Hakuwa msomi mkimya kama wasomi wa enzi hizi. Alitumia elimu yake ipasavyo kuitetea falsafa yake ya Haki na Usawa kwa Binadamu Wote katika majukwaa ya kimataifa.
Wananchi wa Uganda daima humkumbuka na kumtukuza kwa jinsi alivyotumia nguvu za kijeshi kuung’oa utawala wa kidikteta wa Nduli Idd Amini Dada. Wakikumbuka mateso waliyoyapata enzi za utawala huo, humtukuza na kumuenzi Nyerere usiku na mchana.
Nyerere hataweza kusahaulika kwa jinsi alivyopinga kitendo cha viongozi wachache wenye hila kuendelea kung’ang’ania kwenye madaraka. Alikuwa kiongozi wa kwanza hapa Afrika na pengine duniani kote kung’atuka kwenye kiti cha Urais. Alifanya hivyo kwa hiyari ili kutoa nafasi kwa wananchi wengine washike nyadhifa hii nyeti hapa nchini kwetu.
Mwalimu Nyerere ni mwenzetu, ni rafiki yetu, ni mtu wa watu, ni baba wa taifa letu, ni babu yetu mwenye hekima na busara. Paji lake la uso lilijaa hekima na busara. Kinywa chake daima kilinena maneno ya hekima na busara. Fikra zake zitadumu milele kwenye vichwa vya wakulima, wasomi, wanafalsafa, mapadri, masheikh, wachungaji, watawa na hata kwenye bongo za waovu wa Tanzania daima watamkumbuka.
Kifo cha Mwalimu Nyerere kimeleta pengo kubwa kwa jamii yote ya wapenda amani kote ulimwenguni. Ingekuwa mbegu yam mea tungeipanda sote tuendelee kuhekimika kutokana na hekima na busara zake.
Kifo cha Mwalimu Nyerere ni kama mwindaji asiye na silaha kwenye mwitu wenye wanyama wakali kama fisi, simba, ngiri, tembo, nyoka, nyati, n.k. Je, mwindaji atafanya nini?
Daima sifa na hekima za Mwalimu Nyerere zitukuzwe Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote.
Mbali na Nyumbani ni riwaya iliyoandikwa kwa muundo wa tawasifu ya mwandishi maarufu wa Zanzibar, Adam Shafi anayejulikana zaidi kama Shafi Adam Shafi. Ipo haja kubwa sasa kwa waandishi kujitolea kuandika tawasifu zao au wasifu. Kitabu kimechapishwa na Longhorn (K) Limited mwaka 2012 na uhakiki huu umeandikwa na Prof. Ken Walibora.
Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita yametokea machapisho mengi sana ya bunilizi katika Kiswahili hasa nchini Kenya. Kipindi hiki muhimu kimeshuhudia waandishi wakongwe na chipukizi tumbi nzima kuchapishiwa kazi zao kwa wingi zaidi kuliko kipindi chochote kingine katika historia ya fasihi ya Kiswahili.
Yamkini ongezeko hili la machapisho ya Kiswahili linatokana na ukweli kwamba wachapishaji wamezinduka ghafla kutambua kwamba lina faida pia soko la vitabu vya Kiswahili, lugha ambayo umaarufu wake unakua kwa mapana na marefu kote duniani na hasa nyumbani Afrika Mashariki na Kati. Sababu nyingine ni kuibuka kwa watu wengi wanaokiteua Kiswahili kama nyenzo yao ya kuzibebea kazi zao za kibunifu badala ya Kiingereza au lugha nyingine yoyote.
Lakini hii haimaanishi kwamba kwa ubora na wingi machapisho ya Kiswahili kwa sasa yako sawa na ya Kiingereza. Ni kweli kwamba fasihi ya Kiswahili inajishajiisha kuchuana vilivyo na fasihi ya Kiingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika hasa katika tanzu zake za kibunifu, lakini sivyo ilivyo katika simulizi zinazohusu maisha halisi, tanzu zile ambazo nitaziita uandishi maisha, kama vile tawasifu, shajara, wasifu, n.k.
Tangu gwiji—au tumwite baba wa fasihi ya kisasa ya Kiswahili, Shaaban bin Robert alipotunga wasifu wa mwimbaji wa taarab, Wasifu wa Siti Biti Saad, na tawasifu yake mwenyewe, Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, kumekuwapo na kazi chache sana za Kiswahili katika ulingo wa simulizi za maisha halisi.
Hiyo ndiyo maana tunachangamkia kuchapishwa kwa Mbali na Nyumbani, tawasifu ya mwandishi maarufu wa Zanzibar Adam Shafi, anayejulikana zaidi kama Shafi Adam Shafi. Kwa hakika tawasifu ya Shafi huenda ikawa ndiyo tawasifu yenye ujasiri zaidi na iliyotungwa kwa usanifu na usanii mkubwa zaidi katika kanzi nzima ya fasihi ya Kiswahili.
Tawasifu hii imejikita kwenye maudhui ya maisha ugenini, jasira za ujana, na msako wa elimu pamoja na motifu ya safari. Ni tawasifu yenye kuvutia mno na ambayo ina uwezo wa kuleta mapindukizi makubwa katika uwanja wa uandishi maisha wa Kiswahili.
[url=https://www.blogger.com/null][/url]
Angalao kwa mara ya kwanza tunakumbana na tawasifu iliyosheheni ucheshi lakini ambayo haizingatii majisifu ya mwandishi wala jaribio la makusudi ya kuficha udhaifu wake. Aidha tawasifu hii haikupi maelezo makavu ya tarehe, mambo hakika, na tarakimu huku mwandishi akijisifusifu kama ambavyo twaona kwenye tawasifu chapwa nyingi zilizoko kwenye rafu za vitabu kote kote duniani.
Mbali na Nyumbani inadhihirisha ubora wa kiujumi na hutoa raha kamili kuisoma. Hata hivyo, yamkini ubora mkubwa zaidi wa tawasifu hii kuhusu safari ugenini, humo katika uwezo wake wa kutuonyesha mengi kuhusu hali ya binadamu na kufundisha bila kuhubiri kwa kumshikia msomaji mtutu wa bunduki na kumlazimishia maoni yasiyopindika.
Shafi si mgeni katika ulingo wa fasihi ya Kiswahili. Ingawa si mwandishi wa vitabu vingi kama mathalani Shaaban Robert, K. W. Wamitila na Said A. Mohamed, ameandika riwaya nne za kutajika,yaani; Kuli, Kasri ya Mwinyi Fuad, Haini, na Vuta N’kuvute. Riwaya ya Haini ambayo ni nusu-tawasifu na ile ya Vute N’kuvute ndizo labda kazi zake bora zaidi.
Katika Mbali na Nyumbani, kama ilivyo katika kazi zake nyinginezo, ni msomaji hana budi kumakia umbuji wa lugha ya Shafi, umbuji unaomwezesha kuchonga sanamu yake mwenyewe kwa ajili ya hadhara kutoka kwenye maisha yake ya faragha na kuifanya tawasifu yake kuwa na ubora utakaokiuka vizazi. Kadhalika Shafi anafanikiwa kucheza na kutatiza mpaka mwembamba uliopo kati uhalisia na ubunifu.
Shafi anaelezea jinsi alivyopatwa na maradhi ya kutaka kusafiri kutoka kwao alikozaliwa na kulelewa. Wasomaji wengi ambao wamewahi kutamani kutoka kwao watajitambulisha na hali hiyo iliyomkumba mwandishi. Vyombo ya bahari vilivyotia nanga bandarini Zanzibar ndivyo vilivyochochea roho ya jasira na hamu na ghamu ya Shafi kutaka kuhujuru kwao.
Mafunzo ya ualimu
Alipokuwa mvulana mdogo akikaa ufukweni mwa bahari na kuvitazama vyombo hivyo na mabaharia walioingia na kutoka. Kukaa kwingi ufukweni kulimpatisha adhabu kali kutoka kwa babake ambaye akihofia usalama wa mwanawe. Baadaye maishani, Shafi aliachia katikati mafunzo ya ualimu kwenye chuo cha ualimu Zanzibar na kuanza safari ya kwenda kusoma Misri bila hata kuwaarifu wazazi wake.
Zanzibar ilikuwa katika minyonyoro ya ukoloni wa Uingereza wakati huo, naye akitarajia kupata elimu kwengineko mbali na nyumbani. Pitapita zake za kwenda Misri zinampitisha Kenya, Uganda, na Sudan ambapo mara kadha alikuwa akienda na kurudi au kurudishwa nyuma kutokana na vikwazo safarini.
Shafi anaelezea visa vingi vya kushangaza kukiwemo kufanya kazi ya kondakta kwente basi la Mawingo Bus lililohudumu kati ya Bungoma na Kisumu, uhusiano wake wa mapenzi haramu na wanawake Bungoma na Khartoum na kufungwa jela Uganda Kaskazini n.k. Hadithi ya maisha yake inaishia mpomoko pale ambapo anajikuta kwenye kambi ya siri ya mazoezi ya kijeshi nchini Msiri ili kuipindua serikali ya Mkoloni Zanzibar, badala ya chuo kikuu kusomea elimu aliyodhamiria.
Aidha anaporejea kwao nyumbani anakuta kwamba hana fursa ya kutumia mafunzo ya kijeshi aliyoyapata Misri kwa vile Uhuru unapatikana mara moja bila yeye na wapiganaji wenzake kuhusishwa kwenye mapigano.
Ilmuradi mwandishi anaandika kuhusu makosa yake na taksiri zake kwa ujasiri wa kustaajabisha. Mfano ni masimulizi yake kuhusu wanawake aliofanya nao ngono nje ya ndoa na mara nyingine akiwa mwenyewe kakirimiwa na maimamu msikitini. Lakini tawasifu ya Shafi sio tu masimulizi kuhusu uhusiano wa kimapenzi na wanawake; inazungumzia kwa mapana na marefu awamu ya maisha ya kujasiria kwingi ujanani. Inajumuisha matamanio yake, matumaini yake, mashaka yake, kutamauka kwake, huku akisaka elimu ya chuo kikuu isiyofikiwa katika Afrika iliyokuwa inatawaliwa na Wakoloni.
Elimu kama kiini cha msako wa msimulizi inafanana na tawasifu nyinginezo za Kiafrika kama vile ile ya Leonard Kayira, I Will Try, ambapo mwandishi anaondoka kwao Nyasaland, (siku hizi Malawi) ili kwenda kutafuta elimu ya juu Marekani. Maudhui ya elimu kama kani ya ukombozi yanajirudia tena katika tawasifu ya Shafi nayo ni muhimu katika uelewa wetu wa mkutadha wa Zanzibar kihistoria na mapambano ya kibinafsi ya mwandishi mwenyewe kujinusuru kutokana na madhila yaliyoletwa na ukoloni.
Kwa hiyo tawasifu hii, ni zaidi ya hadithi ya mtu mmoja. Katika safari zake zote, Shafi anaandamana na vijana wenzake wanaotamani kupata nafuu maishani nje ya mawanda yao ya kinyumbani. Kwa maana hiyo basi, tawasifu hii ni ni hadithi ya wengi, kama zilivyo tawasifu nyingi za Kiafrika.
Kichocheo kikubwa
Kama mwaka 2010 ulishuhudia kuchapishwa kwa Dreams in a Time of War, labda kazi bora zaidi ya Ngugi wa Thiong’o, basi 2012 ulioshuhudia kuibuka kwa Mbali na Nyumbani ambayo ni kichocheo kikubwa katika uandishi maisha wa Kiswahili. Kwa maoni yangu kwa kuandika Mbali na Nyumbani, Shafi kutoa changamoto kwa waandishi wenzake pia kugeukia maisha yao halisi kama mada ya uandishi na ubunifu wao.
Wito huu unawaendea wote walio hai kama vile Said A. Mohamed, Mohammed S. Mohammed, John Habwe, Bitugi Matundura, Hezekiel Gikambi, Mwenda Mbatia, Timothy Arege, Omar Babu, Clara Momanyi, na Wamitila nami pia. Ipo haja kubwa sasa kwa waandishi kujitolea kuandika tawasifu zao au wasifu. Vile vile kuandikwa kwa wasifu wa watu wengine unasisitizwa hapa.
Wasifu wa Sheikh Ahmed Nabhanny uliotolewa hivi karibuni ni mfano bora wa aina ya tungo za uandishi maisha ambazo Kiswahili kinazihitaji. Ni matumaini yangu kwamba wasifu wa marehemu Shihabdin Chiraghdin ulioandikwa na kuchapishwa hivi karibuni na bintiye kwenye Kiingereza utatafsiriwa kwa Kiswahili pia. Hiyo ni mojawapo wa njia za kukiwezesha Kiswahili kuchuana barabara na Kiingereza katika ulingo wa fasihi katika eneo la Mashariki na ya Kati Afrika.
Mimi mwenyewe nimetunga tawasifu yangu yenye kichwa, Nasikia Sauti ya Mama: Tawasifu ya Maisha Utotoni, na ambayo nimempa mchapishaji. Nimeitika wito pasi ya kuitwa kwa vile nimeiandika kabla ya kusoma Mbali na Nyumbani. Labda siku moja nayo itachapishwa na kusomwa na wengi. Vyovyote viwavyo, kwa Mbali na Nyumbani, Adam Shafi ametuzindua na kutuonyesha njia ya kuandama. Shime Waswahili, mpo?