07-15-2021, 07:48 AM
Simba awapo nyikani – yeye si wakutishika,
Huwataka hayawani – mbuaji kwenye machaka,
Si viumbe vya bandani – vimtie kushutuka,
Simba kumjibu paka – nikujitowa thamani
Akaapo hadharani – kucha zake hufinika,
Mfano kiumbe duni – ela kwa yeye kutaka,
Vimbelembele pembeni – havimpi kusumbuka,
Simba kumjibu paka – nikujitowa thamani
Atembeapo ndiani – si wakupekwa haraka,
Anapishwa hapishani – apandapo na kushuka,
Wakuuliza ni nani – amuwekee mipaka,
Simba kumjibu paka, nikujitowa thamani
Huchaguwa ushindani – si huo wa vijipaka,
Ati pamoya ngondoni – na kuanza patashika,
Hilo litakuwa shani – na nimuhali kutuka,
Simba kumjibu paka – nikujitowa thamani
Kwenye mijusi kutani – ndiko kwa paka hakika,
Na kina panya tobweni – wamjibu akitaka,
Asijitie kundini – ya simba akayataka,
Simba kumjibu paka – nikujitowa thamani
2020.02.26, Yakubu Julius, Nairobi
Mwl Maeda