Kubadili msimbo ni dhana inayomaanisha kuingiza maneno ya lugha tofauti pindi mtumiaji wa lugha atumiapo lugha fulani. Ubadilishaji wa msimbo hufanywa na watumiaji wengi wa lugha katika miktadha mbalimbali ya mtumiaji wa lugha. Malengo ya kubadili msimbo hutofautiana kutoka kwa mtumiaji mmoja wa lugha hadi mwingine.
Ubadilishanaji wa msimbo hutawala katika maeneo mbalimbali kama vile bungeni, kwenye vyombo vya habari katika taasisi za elimu na baadhi ya sehemu za kazi.
Ziko sababu nyingi za kubadili msimbo. Miongoni mwa sababu hizi ni umilisi wa lugha zaidi ya moja dhana ambayo hufanywa na wasomi wanaofikiri kuwa ni kuweka msisitizo katika jambo linaloelezwa .
Dhana hii haiepukiki katika baadhi ya mazingira hasa katika ufundishaji wa lugha za kigeni kwa kuwa kwa namna moja au nyingine lazima ufundishaji wa namna hii uhusishe tafsiri ya lugha inayofundishwa na lugha ya mwanafunzi husika.
Zaidi ya mazingira hayo, na katika utabibu, tafsiri na ukalimani si jambo la kuendelezwa kama wengIne wafanyavyo kwa kuwa lina madhara yake katika lugha.
Kwa baadhi ya watu kubadili msimbo watumiapo Kiswahili limekuwa ni jambo la kawaida mno kwao. Mathalan kwao hao kila baada ya neno moja la Kiswahili linalofuata ni la Kiingereza au kila baada ya sentensi moja inayofuata ni ya Kiingereza.
Sababu kubwa zinazowafanya watu kubadili msimbo ni kudhani kuwa wakitumia lugha mbili tofauti kwa wakati mmoja hasa lugha ya pili ikiwa ni Kiingereza, basi huonekana wasomi mbele ya jamii.
Miongoni mwa madhara ya kubadili msimbo bila sababu za msingi ni pamoja na ujumbe kutowafikia walengwa. Wako baadhi ya watumiaji wa lugha ambao hupenda kubadili msimbo bila ya kuangalia hadhira husika kama inajua lugha ya pili au la. Suala hili huifanya hadhira hiyo isielewe kinachoongelewa na hivyo kushindwa kupata ujumbe unaokusudiwa.
Kubadili msimbo bila sababu za msingi hudunisha lugha. Lugha kuu ya mawasiliano kwa wakati huo ndiyo inayoathirika. Ikiwa lugha kuu ya mawasiliano ni Kiswahili, basi lugha nyingine inayotumika hukifanya Kiswahili kionekane hakijakamilika kimsamiati na kiistilahi jambo ambalo si kweli.
Utumiaji wa lugha kwa mtindo huu ni chanzo cha matumizi mabaya ya lugha na upotoshaji wa ufasaha wa lugha. Pai hupotosha wanaojifunza lugha mathalan wageni na watoto wakadhani kuwa Kiswahili kipo katika hali hiyo ya mseto.
Mara zote mtumiaji wa lugha anapaswa kuwa makini atumiapo lugha ili kuhakikisha kwamba anaitendea haki lugha. Kuchanganya maneno ya lugha zaidi ya moja kwa wakati mmoja bila sababu ya msingi siyo jambo zuri, tena ni fujo zinazosababisha adha masikioni.
Wakati wa vikao vya Bunge, tabia hii imekuwa ni ya kawaida kabisa kwa baadhi ya wabunge wetu. Aghalabu hubadili msimbo bila kujali kuwa Watanzania wengi wanakielewa zaidi Kiswahili kuliko Kiingereza.
Watumiaji wa Kiswahili, tuache mazoea ya kuchanganya lugha bila sababu za msingi. Mazoea hayo mabaya hutufanya tuonekane hatujui Kiswahili wala Kiingereza. Kiswahili kinajitosheleza kimsamiati na kiistilahi hivyo kinaweza kutumika chenyewe bila kuchanganya na lugha nyingine.