Hizi ni sifa za kimatamshi zinazoambatanishwa kwenye sauti za lugha ya mwanadamu, sifa hizi huitambulisha sauti kimatamshi zaidi na husaidia kubainisha taarifa za msingi kama hali ya msemaji, hisiya za msemaji, umbali, n.k
Matamshi:
Kifonolojia matamshi ni utaratibu maalum utumikao katika utoaji wa sauti za maneno ya lugha ya binadamu. Matamshi huhusu lugha za wanadamu peke yake.
Utaratibu wa matamshi ya sauti za lugha huzingatia mambo mawili: Mahali pa matamshi, yaani sehemu katika mkondo wa utamkaji wa sauti mbalimbali ambapo sauti fulani hutamkwa. Jambo la pili ni jinsi ya matamshi yaani namna ambavyo sauti fulani hutolewa.
Lafudhi
Lafudhi ni matamshi ya msemaji wa lugha fulani ambayo yanatokana na athari za kimazingira.
Mazingira hayo yanaweza kuwa eneo atokalo mtu, mahali alikosomea, au kiwango chake cha elimu
Shadda/mkazo
Ni utaratibu wa utamkaji wa maneno ambapo silabi fulani hutamkwa kwa nguvu nyingi zaidi kuliko ilivyo katika silabi nyingine za neno hilohilo.
Mkazo unaweza kuchukuliwa kama kilele cha kupanda na kushuka kwa sauti katika utamkaji wa neno.
Silabi yenye mkazo inakuwa na msikiko mzito zaidi kuliko silabi nyingine za neno hilohilo.
Lugha nyingi hasa za kibantu hazitumii mkazo, Lugha nyingi hutumia toni. Kiswahili sanifu hakitumii toni na zaidi hutumia mkazo.
Kidatu:
Kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.:
Kiimbo
Ni utaratibu maalum wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti unaojitokeza katika utamkaji wa lugha fulani.
Katika utaratibu wa utamkaji dhanna ya Kiimbo huandamana pia na dhanna ya kidatu (yaani, kiwango cha juu, cha kati au cha chini cha sauti katika usemaji), Kwa hivyo ni muhimu hapa kueleza tofauti zilizopo baina ya kiimbo na kidatu. Wakati kiimbo kina maana ya kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti ya lugha, kidatu kina maana ya kiwango cha sauti isikikayo, wakati wa utamkaji ama kuwa juu, kuwa katikati au kuwa chini.
Aina za kiimbo
Kiimbo cha maelezo: Kiimbo cha maelezo ni kile ambacho kwa kawaida msemaji wa lugha akiwa kwenye kidatu chochote kile mawimbi sauti ya usemaji wake yanakuwa takriban katika mstari ulionyooka.
Kiimbo cha kuuliza: Kiimbo cha kuuliza hujitokeza kwa kutumia viwango tofauti vya kidatu kutegemeana na aina ya swali linaloulizwa .
Kiimbo cha amri: kiimbo cha amri hakitofautiani sana na kiimbo cha maulizo.Uchunguzi wa kifonetiki, unaonesha kuwa katika kutoa amri, mzungumzaji hutumia kidatu cha juu zaidi kuliko ilivyo katika kiimbo cha maelezo.
Otografia :- Neno otografia lina asili ya kigiriki na maana yake ni utaratibu wa kutumia alama au michoro ya maandishi kuwakilisha sauti zisikikazo katika lugha.
Kila lugha ina mfumo tofauti wa usemaji na hutumia mfumo tofauti wa sauti.
Kila lugha haina budi kubuni mfumo wake wa kuziwakilisha sauti zake katika maandishi.
Mfumo huo wa maandishi ndio ujulikanao kama othografia.
Mfumo huu huwa unawasilisha herufi maalumu zinazobuniwa ili kuwakilisha sauti za lugha inayohusika kimaandishi.
Silabi:
Silabi ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho kwacho sauti za Lugha hutamkwa mara moja kwa pamoja kama fungu moja la sauti. Kuna aina mbili za silabi, yaani silabi funge na silabi huru. Silabi huru ni zile ambazo huishia na irabu na silabi funge ni zile zinazoishia na konsonanti. Silabi za Kiswahili sanifu mara nyingi huangukia katika kundi la silabi huru.
Miundo asilia ya silabi za Kiswahili
Miundo ya silabi ya irabu peke yake (I).
Mf. A katika Anasoma
Miundo ya silabi ya konsonanti na irabu (KI).
Mf. Ka, ba, ma
Miundo ya silabi ya nazali pekee (N)
Mf. N katika Nta,
M katika Mtoto
Muundo wa silabi wa konsonanti, konsonanti na irabu (KKI)
Mf. Cha, sha,
Muundo wenye konsonanti,konsonanti,kiyeyusho,irabu (KKkI)
Mf. Shwa,
Muundo wa konsonanti,kiyeyusho,irabu (KkI)
Mf. Kwa, mwa
Muundo wa silabi za Kiswahili sanifu zenye asili ya lugha za kigeni
Muundo wa silabi wa Konsonanti, konsonanti na irabu (KKI)
Mf. Labda, leksika, teknolojia
Muundo wa silabi wa kosonanti, consonanti, konsonanti na Irabu (KKKI)