MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
SHAIRI: ASILI YA MWAFRIKA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
SHAIRI: ASILI YA MWAFRIKA
#1
 
1.  Naanza na shukrani
Kumshukuru manani
Kutuleta duniani
Kama alivyojaliya.

2. Tunamshukuru Mungu
Kwa kutupanga mafungu
Kutuweka chungu chungu
Duniani kueneya

3. Hakufanya ubaguzi
Sababu si yake kazi
Kila kitu kiko wazi
Na sote twajioneya.

4.Mataifa kayaweka
Kama tulivyogawika
Kwengine ulikutaka
Ni kama kwenda tembeya.

5.      Kila mtu ana pao
Atembeapo kwa mwao
Palipo asili yao
Awezapo jivuniya.

6.      Waweza kuleta hoja
Ni ubora kuyataja
Mataifa moja moja
Kule yanako tokeya.

7.      Hapa petu afrika
Ndipo Mungu katuweka
Hatuwezi kuondoka
ila iwe kutemnbeya.

8.      Kuna ndugu wa Asia
Wana kwao nao pia.
Jingine huwezi tia
Utakuwa wa kuoseya.

9.      Wengine ni waarabu
Hawa kwao ni karibu
Ukiwataka si tabu
Unapo wahitajiya.

10.  Wazungu kwao Ulaya
Ndiko hasa asiliya
Makabila sitotiya
Nashindwa kupangiliya.

11.  Kila mtu amepewa
Pale alipojaaliwa
Akakaa akatuwa
Maisha yakamwendeya.

12.  Hiyo jadi ya azali
Tulikuwa hatujali
Hata kikiwa cha mali
Twaweza kuzawadiya.

13.  Tulikuwa makarimu
Bora maneno matamu
Twaweza kupewa sumu
Na huku twachekeleya.

KUJA KWA WAGENI

14.  Nazianza simulizi
Kuwasema wachokozi
Walivyoifanya kazi
Hata humu kueneya.

15.  Ujuzi nilionao
Siwashindi wajuao
Ni wale niwapatao
Wanaonidokoleya.

16.  Sababu ya walowezi
Kupanda zao jahazi
Wakenea nchi hizi
Kidogo taelezeya.
17.  Walisafiri wakaja
Mtu mmoja mmoja
Sababu hawakutaja
Hapo walipabaniya.

18.  Wakajita wavumbuzi
Kuuficha ubazazi
Ni kama waota njozi
Wanayo jiropokeya.

19.  Sababu kubwa ni njaa
Ndipo wakatapakaa
Afrika kuzagaa
Kila pembe kueneya.

20.  Walioshindwa kusubiri
Wakazianza safari
Haidhuru za hatari
Lakini hakuna njiya.

21.  Waliingiya vyomboni
Kusafiri baharini
Kwenda wasiko tamani
Japokuwa kupoteya.

22.  Hawakuwa majasiri
Hapo waliposafiri
Kwani pepo za bahari
Hakika zikitishiya.

23.  Dhiki ilipowabana
Wakaiona namna
Ndipo wakaandamana
Kila pembe kuelekeya.

24.  Walifika Afrika
Wakapokewa haraka
Kwa furaha na kucheka
Wakila na kuvimwaya.

25.  Jumla tulisimama
Kuwapokeya kwa wema
Hakuna aliyesema
Tuwatendee ubaya.

26.  Mambo haya kwa hakika
Ambayo nayatamka
Bara zima afrika
Kila walipofikiya.

27.  Walipokewa vizuri
Wasifanyiwe jeuri
Kila walipoabiri
Tabu haikutokeya.

28.  Yote waliyofanyiwa
Kuwekwa na kupokewa
Na hadhi kukirimiwa
Thamani hawakutiya.

29.  Waliona ni lazima
Wao kupewa heshima
Kwani walizinga nyuma
Kutufanyia ubaya.

30.  Sababu waligeuka
Wakaanza kutushika
Utumwa kutupeleka
Bila ya kukumbukiya.

31.  Wema hawakukumbuka
Macho yaliwakauka
Ni vile walivyotaka
Na walivyofikiriya.

32.  Walifanya watakavyo
Majambo yao ya ovyo
Wakiona hivyo ndivyo
Mabaya kutufanyiya.

33.  Hakika kwa siku hizo
Hatukuwa na uwezo
Tuliugeza mzozo
Bali walituzidiya.

34.  Kwani hatukukubali
Kugeuzwa yetu hali
Tena na watu wa mbali
Wale tulowapokeya.

35.  Tuliona ni wageni
Tukawamba karibuni
Hapa ni penu nyumbani
Na kula kuwapatiya.

36.  Kabisa hatuna chuki
Tunapenda marafiki
Twamtendea ya haki
Kila anaetujiya.

37.  Kumbe yote ni ya bure
Wakiitika kwa shere
Nyoyoni wapiga hure
Huku wanafurahiya.

38.  Sababu fikira zao
Ni kutawala wenzao
Na kupeleka makwao
Mapato na watu piya.

39.  Hisani walofanyiwa
Na walivyochukuliwa
Kamwe hawakutambuwa
Wala kujifikiriya.

40.  Haja yao watawale
Tena wakae milele
Wanyonye wende wakale
Wapate jifaidiya.

41.  Tulikuwa tumekaa
Kila mtu kwa wasaa
Ndipo wakaleta baa
Tusiyoitazamiya.

42.  Tukayaanza matata
Tukasimamisha vita
Rungu, mishare na nyuta
 Ndivyo tulivyotumiya.

43.  Tuuhifadhi uhuru
Tukaebila uhuru
Pasiwe wa kuamuru
Amri kututoleya.

44.  Tulivijaribu sana
Vita hivyo kupigana
Njia ikawa hapana
Mambo yakatutatuliya.

45.  Ndipo kukaa mezani
Wakazichora ramani
Wakagawana kwa kani
Bara letu nakwambiya.

46.  Waligawa kama nyama
Kila mtu atazama
Hatukuweza kusema
Ila kuwaangaliya.

47.  Yule kiga yule ini
Na wengine ni kichwani
Walobaki miguuni
Kila mtu atapiya.

48.  Bara wakaligawanya
Ili wapate linyonya
Na mali kuyakusanya
Vyomboni kuyapakiya.

49.  Wakatiya na mipaka
Kila walipopataka
Wakaanza kumushika
Na kuzitiya shariya.
50.  Bara zima Afrika
Majina wakabandika
Kila waliyoyataka
Nayetu yakapoteya.

51.  Yetu yasiwe na enzi
Yakafanywa ya kishenzi
Tusiwe nayo mapenzi
Tusije kukumbukiya.

52.  Hapo tukakosa haki
Hatuna pa kushtaki
Ndipo hapo tukabaki
Kuzifuata shariya.

53.  Wakatupora uhuru
Tukabaki kushukuru
Wakaanza kuamuru
Myaka ikateketeya.

54.  Makodi wakatutoza
Na huku wakatubeza
Ni mambo ya kuchukiza
Siwezi kuhadithiya.

55.  Amri hizi na hizi
Kuzikataa huwezi
Hata kama upuuzi
Ni lazima kutimiya.

56.  Na kama mkikataa
Mtaiona balaa
Mtafute pa kukaa
Na roho kutotuliya.

57.  Muone mashaka gani
Yaloingiya nchini
Ayaletayo mgeni
Msiemtazamiya.

58.  Kukubali ni lazima
Amri walizosema
Wala hawarudi nyuma
Ila kuzishikiliya.

UKOMBOZI

59.  Watu walikaa chini
Kufikiri kwa makini
Mambo haya hadi lini
Yatakapotokomeya.

60.  Hatuwezi kungojeya
Aula kuwaachiya
Lazima kuyazuwiya
Tumekwisha kuchokeya.

61.  Zamani tulijaribu
Kuziangusha dharubu
Wakatushinda kwa tabu
Ndipo walipoingiya.

62.  Sasa na tuanze tena
Kwa njia kila namna
Hata kama kubinyana
Ili wapate kimbiya.

63.  Maana tulifikiri
Watu hawa ni jeuri
Vipi waje washamiri
Na sisi tumetuliya.

64.  Fikra ikaeneya
Toka walio Ulaya
Na huku walobakiya
Wote wakafikiriya.

65.  Ulaya walikutana
Viongozi wa maana
Na maneno yakafana
Waliyozungumziya.

66.  Majina sitoyataja
Mtu mmoja mmoja
Bali kiasi cha haja
Ninayoyakumbukiya.

67.  Ni huko Manchesta
Ndugu Kwame na Kenyatta
Waliyazusha kuita
Dunia ikasikiya.

68.  Hawakuwa peke yao
Walikuwa na wenzao
Sijuwi majina yao
Ningeweza kuyatiya.

69.  Kama mnavyofahamu
Ulikuwa ni muhimu
Viongozi mahashumu
Ndio walohudhuriya.

70.  Huku kwetu Afrika
Sauti ilisikika
Hatukuwa na mashaka
Sote tuliipokeya.

71.  Muamko ukaanza
Kila pembe kujifunza
Zile hatuwa za kwanza
Ambazo za kuanziya.

72.  Jambo la kwanza umoja
Wala pasiwe na hoja (6)
Siku moja itakuja
Sote kuwa ni huriya.

73.  Hapana kurudi nyuma (29)
Wala mtu kusimama
Mababa na kina mama
Kusiwe wa kulegeya.

74.  Tumng’owe mkoloni
Arudi kwao nyumbani (35)
Kamwe tusikubalini
Bara letu ukaliya.

75.  Kakaliya bara letu
Anawatawala watu
Tusipokaza viatu
Hawezi kutuachiya

76.  Ukaanza ukombozi
Bara zima waziwazi
Tena bila ya ajizi
Sababu tulipaniya.

77.  Tukavianzisha vyama
Kwa jumla bara zima
Na tena vikasimama
Watu wakajitoleya.

78.  Wakajitoleya kwa mali
Na wengine kwa kitali
Tena bila ya kujali
Nini kitachotokeya.

79.  Ikawa bega kwa bega
Mkoloni kumswaga
Na damu tukaimwaga
Hapana kufikiriya.

80.  Ukombozi ukashika
Pembe zote afrika
Uhuru ukalipuka
Hakuna asosikiya.

81.  Wakoloni kwa hakika
Walikuwa wakicheka
Wasema mnayotaka
Vigumu kuyafikiya.

82.  Bure mwajihangaisha
Mnayatupa maisha
Sisi hapa kuwapisha
Hilo halijatuliya.

83.  Tena mwajipa mashaka
Msitake mkitaka
Kwani sisi kuondoka
Hamwezi kutwambiya.

84.  Hadi ufike mwishowe
Au tutake wenyewe
Na hapo ndipo mpewe
Siku tutayoridhiya.

85.  Na sisi tukatamka
Lazima mtaondoka
Bara letu twalitaka
Wenyewe kuangaliya.

86.  Tukendelea vitani
Mijini na vijijini
Na wengine misituni
Hakuna alotuliya.

87.  Mijini kuna siasa
Vijijini kuna visa
Sote twasema ni sasa
Wakati umewadiya.

88.  Vita vikaendeleya
Damu yetu tukamwaya
Na wao wakapoteya
Mawazo yakawajiya.

89.  Na mijini tumekaza
Siasa kuzieneza
Tukazidi kuikuza
Na wengi wakaingiya.

90.  Wazungu wakaogopa
Ndipo kuanza kutupa
Huko na kule na hapa
Nchi tukazipokeya.

91.  Uhuru wakautowa
Na wangine kunyakuwa
Bara na wenye visiwa
Ukaanza kueneya.

92.  Nchi nyingi zimepata
Zaendeshwa bila tata
Myaka mingi imepita
Nazo zinaendeleya.

93.  Walisema hatuwezi
Kuifanya hiyo kazi
Hakika ni upuuzi (55)
Maneno yaso na njiya.

94.  Huko ni kubabaika
Maneno ya kuropoka
Mtu hawezi tamka
Ambaye ametimiya.

95.  Ila alo mpungufu
Akilize za mkufu
Au harufu ya afu
Mara imeshapoteya.

96.  Nchi zilizobakiya
Ni kidogo nakwambiya
Majina nitayatiya
Na hivi nawatajiya.

97.  Kwanza hapo Rodesia
Hao hawajasikia
Wenyewe kutuachia
Bado wameshikiliya.

98.  Na Spanishi Sahara
Siku moja watahara
Watakuja pigwa ngwara
Wapate kutokomeya.

99.  Twende huko Namibiya
Pamoja na Azaniya
Kaburu wamezuwiya
Wala hataki sikiya.

100.                      Ameshika ubaguzi
Anaiona ni kazi
Duniya haisikizi
Kila wanavyomwambiya.

101.                      Na sehemu ya Somali
Faransa hakubali
Ameifunga kufuli
Ufunguo kufungiya.

102.                      Na visiwa vya Comoro
Kuna wake mgogoro
Wamekulaza kiporo
Hatuja watambuliya.

103.                      Ndugu zetu Msumbiji
Huko sasa twataraji
Tumepata mahitaji
Tuliyoyahitajiya.

104.                      Na Angola nako pia
Tumekwisha kusikia
Tunachokitarajia
Karibu kitatokeya.

105.                      Na sehemu nyinginezo
Ambazo zina mizozo
Tutavivunja vikwazo
Tusafishe kote piya.

MASHUJAA

106.                      Tukumbuke viongozi
Walioifanya kazi
Hadithi zao ziwazi
Siwezi kuzizuwiya.

107.                      Mashujaa wenye sifa
Ambao waliokufa
Ni jumla ya maafa
Yalokwisha tupitiya

108.                      Majina yao kutaja
Wote mmoja mmoja
Kichwani hayatakuja
Labda kutokozeya.

109.                      Najaribu kutamka
Majina kuyaandika
Yale nitayokumbuka
Ambayo yatanijiya.

110.                      Kwanza ndugu Nkuruma
Ambae alisimama
Wala hakurudi nyuma (29)
Uhuru kupiganiya.

111.                      Kuna ndugu Gabral
Huyo nae ni wa pili
Waloigeuza hali
Ikatambuwa duniya.

112.                      Tuje kwa ndugu Lumumba
Shujaa ambae kwamba
Alieivunja myamba
Ya ukoloni mbaya.

113.                      Sasa ndugu Mandlane
Nae pia tumnene
Jumla ni watu wane
Na bado naendeleya.

114.                      Abubakari Tafawa
Ambae alijitowa
Nchie kuikombowa
Wapate kuwahuriya.
115.                      Na ndugu yetu Karume
Alosimama kiume
Kutawaliwa kukome
Nchi ipate tuliya.

116.                      Na wangine wako ndani
Kuwekwa vizuwizini
Hivi wamo adhabuni
Nasi tunawaliliya.

117.                      Wakoloni wawaweka
Wapate sahaulika
Bure wanahangaika
Bado twawategemeya.

118.                      Majina yao ni haya
Najaribu kutatiya
Yale yanayonijiya
Wala sitoyaachiya.

119.                      Viongozi walo hai
Ambao twawatumai
Hatutoacha kudai
Hadi nnje kutokeya.

120.                      Kwanza ni ndugu Mandela
Anavyopata madhila
Kamwe hutoweza kula
Utapomfikiriya.

121.                      Amewekwa kisiwani
Nduguze hatumuoni
Na yeye atutamani
Kaburu amezuwiya.

122.                      Pili ni ndugu Nkomo
Hageuzi msimamo
Ameshika muandamo
Zimbabwe iwe huriya.

123.                      Smith amemuweka
Asipate kutamka
Lakini hajageuka
Siku anaingojeya.

124.                      Na ndugu wa Nabiya
Kaburu kawazuwiya
Nyayani amewatiya
Ili wapate tuliya.

125.                      Yote hayo kazi bure
Ni mruko wa papare
Siku ya kupinga hure
Mbona itatufikiya.

126.                      Bara zima afrika
Siku moja itafika
Sote tutafurahika
Kwa uhuru kutimiya.

UTAMADUNI

127.                      Wala hatukukubali
Kuyaacha ya asili
Tokeya hapo azali
Hadi sasa twatumiya.

128.                      Wageni walidharau
Tukaonwa mabahau
Upate kauka kau
Na uzidi kupoteya.

129.                      Mataifa Duniani
Yanayo utamaduni
La ajabu jambo gani
Kuwa nao nasi piya.

130.                      Utamaduni na mila
Kati ya zetu kabila
Zikiwa kila mahala
Bara zima kueneya.

131.                      Namna zilivyokuwa
Karibu zote ni sawa
Ufikapo wapokewa (28)
Utakapokufikiya.

132.                      Na sasa ndivyo zilivyo
Zitakwenda vivyo hivyo
Aone ni za ovyo
Anaweza jipakiya.

133.                      Akenda anakotaka
Arudi alikotoka
Na sisi hatuna shaka
Bara letu kutwachiya.

134.                      Mambo kushirikiana
Kwa kazi kila namna
Pamwe na kutazamana
Kwa shida zikitokeya.

135.                      Hapakuwa ubaguzi
Inapotokeya kazi
Kwa vijana na wazazi
Huwa pamoja sawiya.

136.                      Tunapokwenda mashamba
Aula kujenga nyumba
Sote huwa ni sambamba
Hako anaebakiya.

137.                      Labda awe mgonjwa
Au jambo lisovunjwa
Huyo pia hatopunjwa
Japo hakuhudhuriya.

138.                      Tukizifanya pamoja
Kazi zote bila hoja (6)
Mazao yanapokuja
Twayagawa yote piya.

139.                      Hatukuwa ni wavivu
Tulikuwa washupavu
Vigumu kuwa mwerevu
Kazi inapowadiya.

140.                      Hatukujuwa tabaka
Za watu kugawanyika
Wanyonge na watu kuka
Hilo haliutokeya.

141.                      Tafauti kubwa sana
Ambayo ungeiona
Ni wazee na vijana
Popote ukitembeya.

142.                      Ama misiba na ndowa
Namna ilivyokuwa
Kila watu wanajuwa
Njia wanazopitiya.

143.                      Upate wa ngoma zetu
Siwezi kusema kitu
Kwasababu kila mtu
Mwenyewe ajioneya.

144.                      Tukisemeya elimu
Tulikuwa nayo hamu
Tukijifunza humu
Pamwe na zetu tabiya.

145.                      Mambo tukijifundisha
Ya kupeleka maisha
Tena tukikamilisha
Zetu mila na tabiya.

146.                      Vijana na wasichana
Pamoja na wavulana
Elimu wakifunzana
Halafu kuitumiya.

147.                      Tukijifunza kuwinda
Kwa kila anaependa
Mchana kutwa hushinda
Misituni kuviziya.

148.                      Na vijana ufugaji
Halafu ni uchungaji
Pamoja na ulimaji
Hatuwezi uachiya.

149.                      Upande wa wanawake
Sio kwamba wakapike
Bali mikeka wasuke
Na maji kujitekeya.

150.                      Kwa hakika mambo mengi
Ambayo yana misingi
Tukiyafanya kwa wingi
Bila ya kuwategeya.

151.                      Kwa jumla mambo yetu
Tokeya wazee wetu
Hawakuyaacha katu
Nasi twayashikiliya.

152.                      Na sasa ndio Zaidi
Twaongeza jitihadi
 Kuyahifadhi ya jadi
Yasipate kupoteya.

153.                      Lugha kwa upande wake
Kila mtu ana yake
Wakati akiwa kwake
Anayoisumuliya.

154.                      Na nyingine zafanana
Maneno yanaungana
Sababu wakionana
Wanaweza kuongeya.

155.                      Na tungo tukizitunga
Za maneno ya mwanga
Na pia tukiyapanga
Sababu tukijuliya.

156.                      Kwa muwala na urari
Mpango ulo mzuri
Ukiona utakiri
Kazi iliyotimiya.

157.                      Na pia wakitutibu
Kina nyanya na mababu
Kwa dawa za mjarabu
Maradhi yakikimbiya.

158.                      Kitumiya miti shamba
Walokuwa wakichimba
Ya kupaka na kwamba
Zote tukizitumiya.

159.                      Na vitu tuligunduwa
Halafu vikatumiwa
Kama hori na mashuwa
Vingine naongezeya.

160.                      Juwa kali likiwaka
Visiwa vikikauka
Shuruti kuteremka
Ndipo atayafikiya.

161.                      Buyu likatobolewa
Vilo ndani vikagewa
Na Kamba likasukiwa
Ili maji kutekeya.

162.                      Hapo tukapata ndoo
Kwa wote si kwa ukoo
Watu wasema hoo
Tumekwisha tambuliya.

163.                      Baada ya kuipata
Tukawa maji twachota
Yeyote anaepita
Anaweza kutumiya.
164.                      Mchanga tukiuchoma
Kwa kutengenezeya  chuma
Kwa majembe ya kulima
Na mashoka kuchanjiya.

165.                      Vyembe pamwe na mikuki
Ni silaha hazitoki
Kukitokea halaki
Hutwaa kupiganiya.

166.                      Na moto tukipekecha
Popote kunapokucha
Wala huwezi uficha
Mwenzio wamgawiya

167.                      Kama utafanya choyo
Kwa kitu au kandeyo
Watakuacha pekeyo
Watu hawatakujiya

168.                      Jambo hilo ni aibu
Kama mtu lamswibu
Kutengwa na akrabu
Wapi atakimbiliya.

169.                      Na samaki tukivuwa
Kwa malema na mabuwa
Pia kwenda kuchokowa
Chaza pamwe na chapiya.

170.                      Wanyama tukiwatega
Ulimbo tukiumwaga
Wanase bila kupiga
Kitoweo cha kuliya.

171.                      Michezo tukiicheza
Tena yenye kupendeza
Wala hatukupuuza
Kuyaacha mambo haya.

172.                      Mchezo kama wa nage
Holi kifura msege
Hamkai lege lege
Na jungwe kuongezeya.

173.                      Na watu wakiitana
Wakati wa kupambana
Kwa wingi hukusanyana
Huku wakishangiriya.

174.                      Hakika michezo hiyo
Na Zaidi mingineyo
Ni mambo tuliyonayo
Toka zama asiliya.

175.                      Kwevu na kuendeana
Pamwe na kueleana
Na pia kualikana
Majambo yakiwadiya.

176.                      Haya ni mambo ya kweli
Kwenye bara letu hili
Wala hatuja badili
Mila zetu kupoteya.

UCHUMI

177.  Uchumi tukiufanya
Na mali tukikusanya
Wala sio kwa sinya
Udhalimu kutumiya.

178.  Tukitowa letu jasho
Tena sio kwa vitisho
Au kwa maamrisho
Ya mtu kutuwekeya.

179.Tukibadili mazao
Kwa wake watu wajao
Wakija na vitu vyao
Wakifika vyabakiya.

180. Vitabaki palepale
Wala hakuna kelele
Kama wanao mchele
Kunde watajitwaliya.

181.Kwa upande wa wanyama
Mbuzi wawili kwa ndama
Maneno watayasema
Na mwisho yatafikiya.

182. Tulikuwa na mazizi
Ng’ombe, kondoo na mbuzi
Yevu ni mali azizi
Jingine kutosikiya.

183.  Hatusikii maneno
Yawaza wala nong’ono
Japo ni mbuzi watano
Akiba twajiwekeya.

184.  Tukifanya biashara
Ya faida na hasara
Wala huwezi kugura
Kwa mali kukupoteya.

185. Pembe tukiuziana
Mali kibadilishana
Na kile ambacho huna
Mwinziyo takipatiya.

186. Watu wingiya nyikani
Mizigo yao nyikani
Wanalala machakani
Hawajali kuumiya.

187. Wauzaji wa urembo
Au vyombo vya mapambo
Wanashika zao fimbo
Wapita wakiteteya.

188.  Na mali ya asiliyo
Dhahabu uijuwayo
Wala siyampashiyo
Ni safi ya kutumiya.

189.   Tunayo na almasi
Na miti ya sandarusi
Nyinginezo hazikosi
Japo zimejifukiya.

190. Pangine hatujulii
Thamani yake ni hii
Zimefifiya fifii
Twabaki kuangaliya.

191. Kuna wanyama porini
Simba, twiga na manyani
Ni mali kubwa kamani
Watalii huwajiya.

192.                      Mungu bara kuliumba
Na tena akalipamba
Ni kututiya kasumba
Kwa kutudharauliya.

193.                      Lina mito na mabonde
Kwa kulima zetu konde
Maharage au kunde
Akiba kujiwekeya.

194.                      Majabali na milima
Yenye kujaa wanyama
Na miti iliyomema
Mwapendeza kutembeya.

195.                      Kuna ndege na wadudu
Na mauwa ya waridu
Mtu aweza husudu
Harufu akisikiya.

196.                      Na vitu vya kupendeza
Mungu alivyovijaza
Barani kavieneza
Kiasi katujaliya.

DUA

197.                      Sasa namuomba Mungu
Alo wa tangu na tangu
Naanza maneno yangu
Kuzidi kuombeleya.

198.                      Viumbe vyako dhalili
Twakuomba ya jalali
Utubadilishe hali
Maovu kutondoleya.

199.                      Bara letu litukuke
Duniani lisikike
Tukae tupumzike
Tupate kuendeleya.

200.                      Tupendane sisi sote
Mapenzi yalo na kite
Mfitina tuwakate
Wasipate pa kungiya.

201.                      Bara zima afrika
Ulishushie baraka
Mambo yapate swafika
Kila nchi kutuliya.

202.                      Zimwendee shukrani
Ndugu Yakub Gowon
Kutukaribu nchini
Tutokao Tanzaniya.


Utenzi huu uliingiya katika mashindano ya maonesho ya Afrika huko Lagos, Nigeria mwaka 1974.
Nilishinda nikawa mtu wa pili katika Tanzania.Niliuanza kuuandika tarehe 6, October, 1974 na kumaliza 29, October, 1974

SALIM ALI KIBAO
S.L.P 75339
DAR ES SALAAM
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)