SHAIRI: ASILI YA MWAFRIKA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: ASILI YA MWAFRIKA (/showthread.php?tid=1552) |
SHAIRI: ASILI YA MWAFRIKA - MwlMaeda - 11-24-2021 Kumshukuru manani Kutuleta duniani Kama alivyojaliya. 2. Tunamshukuru Mungu Kwa kutupanga mafungu Kutuweka chungu chungu Duniani kueneya 3. Hakufanya ubaguzi Sababu si yake kazi Kila kitu kiko wazi Na sote twajioneya. 4.Mataifa kayaweka Kama tulivyogawika Kwengine ulikutaka Ni kama kwenda tembeya. 5. Kila mtu ana pao Atembeapo kwa mwao Palipo asili yao Awezapo jivuniya. 6. Waweza kuleta hoja Ni ubora kuyataja Mataifa moja moja Kule yanako tokeya. 7. Hapa petu afrika Ndipo Mungu katuweka Hatuwezi kuondoka ila iwe kutemnbeya. 8. Kuna ndugu wa Asia Wana kwao nao pia. Jingine huwezi tia Utakuwa wa kuoseya. 9. Wengine ni waarabu Hawa kwao ni karibu Ukiwataka si tabu Unapo wahitajiya. 10. Wazungu kwao Ulaya Ndiko hasa asiliya Makabila sitotiya Nashindwa kupangiliya. 11. Kila mtu amepewa Pale alipojaaliwa Akakaa akatuwa Maisha yakamwendeya. 12. Hiyo jadi ya azali Tulikuwa hatujali Hata kikiwa cha mali Twaweza kuzawadiya. 13. Tulikuwa makarimu Bora maneno matamu Twaweza kupewa sumu Na huku twachekeleya. KUJA KWA WAGENI 14. Nazianza simulizi Kuwasema wachokozi Walivyoifanya kazi Hata humu kueneya. 15. Ujuzi nilionao Siwashindi wajuao Ni wale niwapatao Wanaonidokoleya. 16. Sababu ya walowezi Kupanda zao jahazi Wakenea nchi hizi Kidogo taelezeya. 17. Walisafiri wakaja Mtu mmoja mmoja Sababu hawakutaja Hapo walipabaniya. 18. Wakajita wavumbuzi Kuuficha ubazazi Ni kama waota njozi Wanayo jiropokeya. 19. Sababu kubwa ni njaa Ndipo wakatapakaa Afrika kuzagaa Kila pembe kueneya. 20. Walioshindwa kusubiri Wakazianza safari Haidhuru za hatari Lakini hakuna njiya. 21. Waliingiya vyomboni Kusafiri baharini Kwenda wasiko tamani Japokuwa kupoteya. 22. Hawakuwa majasiri Hapo waliposafiri Kwani pepo za bahari Hakika zikitishiya. 23. Dhiki ilipowabana Wakaiona namna Ndipo wakaandamana Kila pembe kuelekeya. 24. Walifika Afrika Wakapokewa haraka Kwa furaha na kucheka Wakila na kuvimwaya. 25. Jumla tulisimama Kuwapokeya kwa wema Hakuna aliyesema Tuwatendee ubaya. 26. Mambo haya kwa hakika Ambayo nayatamka Bara zima afrika Kila walipofikiya. 27. Walipokewa vizuri Wasifanyiwe jeuri Kila walipoabiri Tabu haikutokeya. 28. Yote waliyofanyiwa Kuwekwa na kupokewa Na hadhi kukirimiwa Thamani hawakutiya. 29. Waliona ni lazima Wao kupewa heshima Kwani walizinga nyuma Kutufanyia ubaya. 30. Sababu waligeuka Wakaanza kutushika Utumwa kutupeleka Bila ya kukumbukiya. 31. Wema hawakukumbuka Macho yaliwakauka Ni vile walivyotaka Na walivyofikiriya. 32. Walifanya watakavyo Majambo yao ya ovyo Wakiona hivyo ndivyo Mabaya kutufanyiya. 33. Hakika kwa siku hizo Hatukuwa na uwezo Tuliugeza mzozo Bali walituzidiya. 34. Kwani hatukukubali Kugeuzwa yetu hali Tena na watu wa mbali Wale tulowapokeya. 35. Tuliona ni wageni Tukawamba karibuni Hapa ni penu nyumbani Na kula kuwapatiya. 36. Kabisa hatuna chuki Tunapenda marafiki Twamtendea ya haki Kila anaetujiya. 37. Kumbe yote ni ya bure Wakiitika kwa shere Nyoyoni wapiga hure Huku wanafurahiya. 38. Sababu fikira zao Ni kutawala wenzao Na kupeleka makwao Mapato na watu piya. 39. Hisani walofanyiwa Na walivyochukuliwa Kamwe hawakutambuwa Wala kujifikiriya. 40. Haja yao watawale Tena wakae milele Wanyonye wende wakale Wapate jifaidiya. 41. Tulikuwa tumekaa Kila mtu kwa wasaa Ndipo wakaleta baa Tusiyoitazamiya. 42. Tukayaanza matata Tukasimamisha vita Rungu, mishare na nyuta Ndivyo tulivyotumiya. 43. Tuuhifadhi uhuru Tukaebila uhuru Pasiwe wa kuamuru Amri kututoleya. 44. Tulivijaribu sana Vita hivyo kupigana Njia ikawa hapana Mambo yakatutatuliya. 45. Ndipo kukaa mezani Wakazichora ramani Wakagawana kwa kani Bara letu nakwambiya. 46. Waligawa kama nyama Kila mtu atazama Hatukuweza kusema Ila kuwaangaliya. 47. Yule kiga yule ini Na wengine ni kichwani Walobaki miguuni Kila mtu atapiya. 48. Bara wakaligawanya Ili wapate linyonya Na mali kuyakusanya Vyomboni kuyapakiya. 49. Wakatiya na mipaka Kila walipopataka Wakaanza kumushika Na kuzitiya shariya. 50. Bara zima Afrika Majina wakabandika Kila waliyoyataka Nayetu yakapoteya. 51. Yetu yasiwe na enzi Yakafanywa ya kishenzi Tusiwe nayo mapenzi Tusije kukumbukiya. 52. Hapo tukakosa haki Hatuna pa kushtaki Ndipo hapo tukabaki Kuzifuata shariya. 53. Wakatupora uhuru Tukabaki kushukuru Wakaanza kuamuru Myaka ikateketeya. 54. Makodi wakatutoza Na huku wakatubeza Ni mambo ya kuchukiza Siwezi kuhadithiya. 55. Amri hizi na hizi Kuzikataa huwezi Hata kama upuuzi Ni lazima kutimiya. 56. Na kama mkikataa Mtaiona balaa Mtafute pa kukaa Na roho kutotuliya. 57. Muone mashaka gani Yaloingiya nchini Ayaletayo mgeni Msiemtazamiya. 58. Kukubali ni lazima Amri walizosema Wala hawarudi nyuma Ila kuzishikiliya. UKOMBOZI 59. Watu walikaa chini Kufikiri kwa makini Mambo haya hadi lini Yatakapotokomeya. 60. Hatuwezi kungojeya Aula kuwaachiya Lazima kuyazuwiya Tumekwisha kuchokeya. 61. Zamani tulijaribu Kuziangusha dharubu Wakatushinda kwa tabu Ndipo walipoingiya. 62. Sasa na tuanze tena Kwa njia kila namna Hata kama kubinyana Ili wapate kimbiya. 63. Maana tulifikiri Watu hawa ni jeuri Vipi waje washamiri Na sisi tumetuliya. 64. Fikra ikaeneya Toka walio Ulaya Na huku walobakiya Wote wakafikiriya. 65. Ulaya walikutana Viongozi wa maana Na maneno yakafana Waliyozungumziya. 66. Majina sitoyataja Mtu mmoja mmoja Bali kiasi cha haja Ninayoyakumbukiya. 67. Ni huko Manchesta Ndugu Kwame na Kenyatta Waliyazusha kuita Dunia ikasikiya. 68. Hawakuwa peke yao Walikuwa na wenzao Sijuwi majina yao Ningeweza kuyatiya. 69. Kama mnavyofahamu Ulikuwa ni muhimu Viongozi mahashumu Ndio walohudhuriya. 70. Huku kwetu Afrika Sauti ilisikika Hatukuwa na mashaka Sote tuliipokeya. 71. Muamko ukaanza Kila pembe kujifunza Zile hatuwa za kwanza Ambazo za kuanziya. 72. Jambo la kwanza umoja Wala pasiwe na hoja (6) Siku moja itakuja Sote kuwa ni huriya. 73. Hapana kurudi nyuma (29) Wala mtu kusimama Mababa na kina mama Kusiwe wa kulegeya. 74. Tumng’owe mkoloni Arudi kwao nyumbani (35) Kamwe tusikubalini Bara letu ukaliya. 75. Kakaliya bara letu Anawatawala watu Tusipokaza viatu Hawezi kutuachiya 76. Ukaanza ukombozi Bara zima waziwazi Tena bila ya ajizi Sababu tulipaniya. 77. Tukavianzisha vyama Kwa jumla bara zima Na tena vikasimama Watu wakajitoleya. 78. Wakajitoleya kwa mali Na wengine kwa kitali Tena bila ya kujali Nini kitachotokeya. 79. Ikawa bega kwa bega Mkoloni kumswaga Na damu tukaimwaga Hapana kufikiriya. 80. Ukombozi ukashika Pembe zote afrika Uhuru ukalipuka Hakuna asosikiya. 81. Wakoloni kwa hakika Walikuwa wakicheka Wasema mnayotaka Vigumu kuyafikiya. 82. Bure mwajihangaisha Mnayatupa maisha Sisi hapa kuwapisha Hilo halijatuliya. 83. Tena mwajipa mashaka Msitake mkitaka Kwani sisi kuondoka Hamwezi kutwambiya. 84. Hadi ufike mwishowe Au tutake wenyewe Na hapo ndipo mpewe Siku tutayoridhiya. 85. Na sisi tukatamka Lazima mtaondoka Bara letu twalitaka Wenyewe kuangaliya. 86. Tukendelea vitani Mijini na vijijini Na wengine misituni Hakuna alotuliya. 87. Mijini kuna siasa Vijijini kuna visa Sote twasema ni sasa Wakati umewadiya. 88. Vita vikaendeleya Damu yetu tukamwaya Na wao wakapoteya Mawazo yakawajiya. 89. Na mijini tumekaza Siasa kuzieneza Tukazidi kuikuza Na wengi wakaingiya. 90. Wazungu wakaogopa Ndipo kuanza kutupa Huko na kule na hapa Nchi tukazipokeya. 91. Uhuru wakautowa Na wangine kunyakuwa Bara na wenye visiwa Ukaanza kueneya. 92. Nchi nyingi zimepata Zaendeshwa bila tata Myaka mingi imepita Nazo zinaendeleya. 93. Walisema hatuwezi Kuifanya hiyo kazi Hakika ni upuuzi (55) Maneno yaso na njiya. 94. Huko ni kubabaika Maneno ya kuropoka Mtu hawezi tamka Ambaye ametimiya. 95. Ila alo mpungufu Akilize za mkufu Au harufu ya afu Mara imeshapoteya. 96. Nchi zilizobakiya Ni kidogo nakwambiya Majina nitayatiya Na hivi nawatajiya. 97. Kwanza hapo Rodesia Hao hawajasikia Wenyewe kutuachia Bado wameshikiliya. 98. Na Spanishi Sahara Siku moja watahara Watakuja pigwa ngwara Wapate kutokomeya. 99. Twende huko Namibiya Pamoja na Azaniya Kaburu wamezuwiya Wala hataki sikiya. 100. Ameshika ubaguzi Anaiona ni kazi Duniya haisikizi Kila wanavyomwambiya. 101. Na sehemu ya Somali Faransa hakubali Ameifunga kufuli Ufunguo kufungiya. 102. Na visiwa vya Comoro Kuna wake mgogoro Wamekulaza kiporo Hatuja watambuliya. 103. Ndugu zetu Msumbiji Huko sasa twataraji Tumepata mahitaji Tuliyoyahitajiya. 104. Na Angola nako pia Tumekwisha kusikia Tunachokitarajia Karibu kitatokeya. 105. Na sehemu nyinginezo Ambazo zina mizozo Tutavivunja vikwazo Tusafishe kote piya. MASHUJAA 106. Tukumbuke viongozi Walioifanya kazi Hadithi zao ziwazi Siwezi kuzizuwiya. 107. Mashujaa wenye sifa Ambao waliokufa Ni jumla ya maafa Yalokwisha tupitiya 108. Majina yao kutaja Wote mmoja mmoja Kichwani hayatakuja Labda kutokozeya. 109. Najaribu kutamka Majina kuyaandika Yale nitayokumbuka Ambayo yatanijiya. 110. Kwanza ndugu Nkuruma Ambae alisimama Wala hakurudi nyuma (29) Uhuru kupiganiya. 111. Kuna ndugu Gabral Huyo nae ni wa pili Waloigeuza hali Ikatambuwa duniya. 112. Tuje kwa ndugu Lumumba Shujaa ambae kwamba Alieivunja myamba Ya ukoloni mbaya. 113. Sasa ndugu Mandlane Nae pia tumnene Jumla ni watu wane Na bado naendeleya. 114. Abubakari Tafawa Ambae alijitowa Nchie kuikombowa Wapate kuwahuriya. 115. Na ndugu yetu Karume Alosimama kiume Kutawaliwa kukome Nchi ipate tuliya. 116. Na wangine wako ndani Kuwekwa vizuwizini Hivi wamo adhabuni Nasi tunawaliliya. 117. Wakoloni wawaweka Wapate sahaulika Bure wanahangaika Bado twawategemeya. 118. Majina yao ni haya Najaribu kutatiya Yale yanayonijiya Wala sitoyaachiya. 119. Viongozi walo hai Ambao twawatumai Hatutoacha kudai Hadi nnje kutokeya. 120. Kwanza ni ndugu Mandela Anavyopata madhila Kamwe hutoweza kula Utapomfikiriya. 121. Amewekwa kisiwani Nduguze hatumuoni Na yeye atutamani Kaburu amezuwiya. 122. Pili ni ndugu Nkomo Hageuzi msimamo Ameshika muandamo Zimbabwe iwe huriya. 123. Smith amemuweka Asipate kutamka Lakini hajageuka Siku anaingojeya. 124. Na ndugu wa Nabiya Kaburu kawazuwiya Nyayani amewatiya Ili wapate tuliya. 125. Yote hayo kazi bure Ni mruko wa papare Siku ya kupinga hure Mbona itatufikiya. 126. Bara zima afrika Siku moja itafika Sote tutafurahika Kwa uhuru kutimiya. UTAMADUNI 127. Wala hatukukubali Kuyaacha ya asili Tokeya hapo azali Hadi sasa twatumiya. 128. Wageni walidharau Tukaonwa mabahau Upate kauka kau Na uzidi kupoteya. 129. Mataifa Duniani Yanayo utamaduni La ajabu jambo gani Kuwa nao nasi piya. 130. Utamaduni na mila Kati ya zetu kabila Zikiwa kila mahala Bara zima kueneya. 131. Namna zilivyokuwa Karibu zote ni sawa Ufikapo wapokewa (28) Utakapokufikiya. 132. Na sasa ndivyo zilivyo Zitakwenda vivyo hivyo Aone ni za ovyo Anaweza jipakiya. 133. Akenda anakotaka Arudi alikotoka Na sisi hatuna shaka Bara letu kutwachiya. 134. Mambo kushirikiana Kwa kazi kila namna Pamwe na kutazamana Kwa shida zikitokeya. 135. Hapakuwa ubaguzi Inapotokeya kazi Kwa vijana na wazazi Huwa pamoja sawiya. 136. Tunapokwenda mashamba Aula kujenga nyumba Sote huwa ni sambamba Hako anaebakiya. 137. Labda awe mgonjwa Au jambo lisovunjwa Huyo pia hatopunjwa Japo hakuhudhuriya. 138. Tukizifanya pamoja Kazi zote bila hoja (6) Mazao yanapokuja Twayagawa yote piya. 139. Hatukuwa ni wavivu Tulikuwa washupavu Vigumu kuwa mwerevu Kazi inapowadiya. 140. Hatukujuwa tabaka Za watu kugawanyika Wanyonge na watu kuka Hilo haliutokeya. 141. Tafauti kubwa sana Ambayo ungeiona Ni wazee na vijana Popote ukitembeya. 142. Ama misiba na ndowa Namna ilivyokuwa Kila watu wanajuwa Njia wanazopitiya. 143. Upate wa ngoma zetu Siwezi kusema kitu Kwasababu kila mtu Mwenyewe ajioneya. 144. Tukisemeya elimu Tulikuwa nayo hamu Tukijifunza humu Pamwe na zetu tabiya. 145. Mambo tukijifundisha Ya kupeleka maisha Tena tukikamilisha Zetu mila na tabiya. 146. Vijana na wasichana Pamoja na wavulana Elimu wakifunzana Halafu kuitumiya. 147. Tukijifunza kuwinda Kwa kila anaependa Mchana kutwa hushinda Misituni kuviziya. 148. Na vijana ufugaji Halafu ni uchungaji Pamoja na ulimaji Hatuwezi uachiya. 149. Upande wa wanawake Sio kwamba wakapike Bali mikeka wasuke Na maji kujitekeya. 150. Kwa hakika mambo mengi Ambayo yana misingi Tukiyafanya kwa wingi Bila ya kuwategeya. 151. Kwa jumla mambo yetu Tokeya wazee wetu Hawakuyaacha katu Nasi twayashikiliya. 152. Na sasa ndio Zaidi Twaongeza jitihadi Kuyahifadhi ya jadi Yasipate kupoteya. 153. Lugha kwa upande wake Kila mtu ana yake Wakati akiwa kwake Anayoisumuliya. 154. Na nyingine zafanana Maneno yanaungana Sababu wakionana Wanaweza kuongeya. 155. Na tungo tukizitunga Za maneno ya mwanga Na pia tukiyapanga Sababu tukijuliya. 156. Kwa muwala na urari Mpango ulo mzuri Ukiona utakiri Kazi iliyotimiya. 157. Na pia wakitutibu Kina nyanya na mababu Kwa dawa za mjarabu Maradhi yakikimbiya. 158. Kitumiya miti shamba Walokuwa wakichimba Ya kupaka na kwamba Zote tukizitumiya. 159. Na vitu tuligunduwa Halafu vikatumiwa Kama hori na mashuwa Vingine naongezeya. 160. Juwa kali likiwaka Visiwa vikikauka Shuruti kuteremka Ndipo atayafikiya. 161. Buyu likatobolewa Vilo ndani vikagewa Na Kamba likasukiwa Ili maji kutekeya. 162. Hapo tukapata ndoo Kwa wote si kwa ukoo Watu wasema hoo Tumekwisha tambuliya. 163. Baada ya kuipata Tukawa maji twachota Yeyote anaepita Anaweza kutumiya. 164. Mchanga tukiuchoma Kwa kutengenezeya chuma Kwa majembe ya kulima Na mashoka kuchanjiya. 165. Vyembe pamwe na mikuki Ni silaha hazitoki Kukitokea halaki Hutwaa kupiganiya. 166. Na moto tukipekecha Popote kunapokucha Wala huwezi uficha Mwenzio wamgawiya 167. Kama utafanya choyo Kwa kitu au kandeyo Watakuacha pekeyo Watu hawatakujiya 168. Jambo hilo ni aibu Kama mtu lamswibu Kutengwa na akrabu Wapi atakimbiliya. 169. Na samaki tukivuwa Kwa malema na mabuwa Pia kwenda kuchokowa Chaza pamwe na chapiya. 170. Wanyama tukiwatega Ulimbo tukiumwaga Wanase bila kupiga Kitoweo cha kuliya. 171. Michezo tukiicheza Tena yenye kupendeza Wala hatukupuuza Kuyaacha mambo haya. 172. Mchezo kama wa nage Holi kifura msege Hamkai lege lege Na jungwe kuongezeya. 173. Na watu wakiitana Wakati wa kupambana Kwa wingi hukusanyana Huku wakishangiriya. 174. Hakika michezo hiyo Na Zaidi mingineyo Ni mambo tuliyonayo Toka zama asiliya. 175. Kwevu na kuendeana Pamwe na kueleana Na pia kualikana Majambo yakiwadiya. 176. Haya ni mambo ya kweli Kwenye bara letu hili Wala hatuja badili Mila zetu kupoteya. UCHUMI 177. Uchumi tukiufanya Na mali tukikusanya Wala sio kwa sinya Udhalimu kutumiya. 178. Tukitowa letu jasho Tena sio kwa vitisho Au kwa maamrisho Ya mtu kutuwekeya. 179.Tukibadili mazao Kwa wake watu wajao Wakija na vitu vyao Wakifika vyabakiya. 180. Vitabaki palepale Wala hakuna kelele Kama wanao mchele Kunde watajitwaliya. 181.Kwa upande wa wanyama Mbuzi wawili kwa ndama Maneno watayasema Na mwisho yatafikiya. 182. Tulikuwa na mazizi Ng’ombe, kondoo na mbuzi Yevu ni mali azizi Jingine kutosikiya. 183. Hatusikii maneno Yawaza wala nong’ono Japo ni mbuzi watano Akiba twajiwekeya. 184. Tukifanya biashara Ya faida na hasara Wala huwezi kugura Kwa mali kukupoteya. 185. Pembe tukiuziana Mali kibadilishana Na kile ambacho huna Mwinziyo takipatiya. 186. Watu wingiya nyikani Mizigo yao nyikani Wanalala machakani Hawajali kuumiya. 187. Wauzaji wa urembo Au vyombo vya mapambo Wanashika zao fimbo Wapita wakiteteya. 188. Na mali ya asiliyo Dhahabu uijuwayo Wala siyampashiyo Ni safi ya kutumiya. 189. Tunayo na almasi Na miti ya sandarusi Nyinginezo hazikosi Japo zimejifukiya. 190. Pangine hatujulii Thamani yake ni hii Zimefifiya fifii Twabaki kuangaliya. 191. Kuna wanyama porini Simba, twiga na manyani Ni mali kubwa kamani Watalii huwajiya. 192. Mungu bara kuliumba Na tena akalipamba Ni kututiya kasumba Kwa kutudharauliya. 193. Lina mito na mabonde Kwa kulima zetu konde Maharage au kunde Akiba kujiwekeya. 194. Majabali na milima Yenye kujaa wanyama Na miti iliyomema Mwapendeza kutembeya. 195. Kuna ndege na wadudu Na mauwa ya waridu Mtu aweza husudu Harufu akisikiya. 196. Na vitu vya kupendeza Mungu alivyovijaza Barani kavieneza Kiasi katujaliya. DUA 197. Sasa namuomba Mungu Alo wa tangu na tangu Naanza maneno yangu Kuzidi kuombeleya. 198. Viumbe vyako dhalili Twakuomba ya jalali Utubadilishe hali Maovu kutondoleya. 199. Bara letu litukuke Duniani lisikike Tukae tupumzike Tupate kuendeleya. 200. Tupendane sisi sote Mapenzi yalo na kite Mfitina tuwakate Wasipate pa kungiya. 201. Bara zima afrika Ulishushie baraka Mambo yapate swafika Kila nchi kutuliya. 202. Zimwendee shukrani Ndugu Yakub Gowon Kutukaribu nchini Tutokao Tanzaniya. Utenzi huu uliingiya katika mashindano ya maonesho ya Afrika huko Lagos, Nigeria mwaka 1974. Nilishinda nikawa mtu wa pili katika Tanzania.Niliuanza kuuandika tarehe 6, October, 1974 na kumaliza 29, October, 1974 SALIM ALI KIBAO S.L.P 75339 DAR ES SALAAM |