MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
NAFASI YA NYIMBO ZA KISWAHILI ZA TAARAB KATIKA JAMII YA KISASA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NAFASI YA NYIMBO ZA KISWAHILI ZA TAARAB KATIKA JAMII YA KISASA
#1
Nafasi
ya Nyimbo za Kiswahili za Taarab Katika Jamii ya Kisasa

 
Kitula King’ei
 
Utangulizi
Fani iitwayo ‘nyimbo’
ni mojawapo ya tanzu maarufu katika fasihi simulizi katika tamaduni zote. Katika
fasihi ya Kiswahili, utanzu wa nyimbo umeingiliana na kuathiriana sana kimuundo
na kimtindo na utanzu wa ‘shairi’ hasa tukichukulia shairi kama fani au bahari
moja katika uwanja wa sanaa ya ushairi kwa jumla Abdalla (1978:1-6). Katika karatasi
hii hatutajishughulisha sana na swala la historia, ulinganifu au tofauti kati
ya ‘nyimbo’ za taarab za Kiswahili na bahari nyingine za ushairi. Haya yameshughulikiwa
na wataalamu na wachambuzi wengine wa fasihi ya Kiswahili miongoni mwao akiwa
Khatib (1981).
Dhamira ya makala hii
ni kukadiria mchango uliofanywa na waimbaji wa nyimbo za taarab za Kiswahili katika
mawasiliano hasa ya kimasimulizi. Ni imani ya mwandishi kuwa nyimbo za taarab
zimetungwa na zinaendelea kutungwa na kusambazwa kama chombo cha mawasiliano
kwa malengo kadha.
Kwa sababu hii,
tunaweza kusema kuwa nyimbo hizi zina dhima au jukumu la kutimiza katika
harakati za maendeleo ya nchi zetu hasa katika Afrika Mashariki. Jambo hili
limedokezwa na Asha Malika, mwimbaji maarufu wa nyimbo hizi yapata miaka kumi
iliyopita. Kulingana na Dumila (1977: 21), msanii huyu ameeleza:
Nyimbo
zangu hutalii hisia za ndani za mwanadamu na mapenzi na matakwa yake. Hukitumia
kipaji change cha sauti tamu kwa manufaa ya wanadamu wote. Huitumia sauti yangu
kuhimiza uzalendo kati ya wana Somalia wenzangu, Utaifa kati ya wanapwani wote
wa Upwa wetu, Uafrika kati ya Waafrika wote na utu kati ya wote wanisikiao.
Jambo analosisitiza
hapa Malika ni kwamba msanii wa taarab ana jukumu la kuchangia maendeleo ya taifa
lake na wanadamu wote kwa jumla. Kama fani za fasihi ya maandishi, fani ya
nyimbo hubuniwa, kuenezwa na kuchambuliwa kijumuiya. Nyimbo hizi ni zao la
falsafa, maoni, hisia na amali nyingine za jumuiya.
Jukumu la nyimbo za
taarab kwa mtazamo wa kijamii huishurutisha fani hii kujihusisha kadiri ya
mapito ya wakati. Kimuundo na kimaudhui, nyimbo za taarab zimebidika kukaa na
kubadilika kufungamana na mabadiliko ya jamii zinamoibuka. Hii ndiyo sifa ya
pekee inayoifanya fasihi simulizi kwa jumla na nyimbo za taarab hasa,
kujitanzua na ile hoja isiyokuwa na mashiko inayoieleza fasihi simulizi kuwa “fasihi
kongwe inayopokezwa kizazi hadi kizazi”. Kama asemavyo F.E.M. Senkoro (1981:1) fasihi simulizi na fani zake zote.
Ni
sanaa hai ambayo nayo huhusika katika kanuni ya migongano na ya mwendo katika
maisha….sehemu zake zingine vikumbo na wakati na mazingira mapya zikabaki kuwa
historia…
Mjadala
Nyimbo za taarab katika
Kiswahili zina historia ndefu. Ni wazi kuwa utanzu wa ‘nyimbo’ kama ule wa
ushairi umekita katika utamaduni asilia wa jamii zote za binadamu. Kwa hiyo
nyimbo za taarab zinazoimbwa kwa kutumia vyombo kadha wa kadha vya kimagharibi
na kimashariki ni jambo lililotokea tu katika karne ya kumi na tisa hasa kati
ya miaka ya 1870 na 1888. Nyimbo nyingi zilizotungwa kabla ya wakati huu,
yamkini zimetoweka katika kumbukumbu. Lakini tunapoyachunguza maudhui ya nyimbo
za taarab katika karne moja iliyopita tunapata ushahidi wa kutosha kuonesha
sanaa hii imehusika kiasi gani katika maswala ya jamii.
Kulingana na maoni ya
M.S. Khatib, sanaa ya taarab katika Afrika ya Mashariki imepitia hatua tatu
muhimu na kila kipindi cha maendeleo yake kikiwa na athari fulani juu ya sanaa
yenyewe kimaudhui. Kipindi cha kwanza ni cha kati ya mwaka 1970 na 1988 ambapo
Waswahili walitunga taarab aghalabu katika majumba ya kifalme, hasa sehemu za
Unguja ili kuwatumbuiza watawala na tabaka lao la kibwanyenye kwa jumla. Kipindi
cha pili kati ya mwaka 1905 na 1920 ndipo makundi kadha huru ya watribu
yalipoanza kubuniwa. Wakati huu nyimbo za taarab zilikuwa zimeigubika jamii
finyu tu. Ni katika kipindi cha miaka ya 1920 na 1950 ambapo taarab ilianza
kuenea kutoka visiwani na kupenya jamii ya pwani ya Afrika Mashariki. Kutokea miaka
ya 1960 taarab imekuwa burudani maalumu katika miji mingi ya pwani hata bara. Taarab
hivi leo imefika Burundi na Rwanda.
Sasa turudi nyuma na
kuyaangalia maudhui ya mjadala huu ambayo ni “jukumu na maendeleo” ya fasihi ya
Kiswahili. Utanzu wa nyimbo kama utanzu mzima wa ushairi na muziki hauwezi
kutenganishwa na maisha ya jamii nzima. Katika jamii zote ulimwenguni, sanaa
huwa ni chombo kitumikizi. Kwa hivyo, nyimbo za taarab, katika utamaduni wa
Waswahili kama kipengele kimojawapo cha fasihi ya Kiswahili zina nafasi na
jukumu maalumu kama vile kuelimisha, na kutumbuiza nyimbo hizi za taarab
zimewanda kimaudhui na kugubika vitabia na Nyanja zote za maisha ya jamii zetu.
Katika kiwango cha kiuchumi kwa mfano, taarab zimetungwa kuambatana na shughuli
nyingi za kuzalisha mali kama vile uvuvi, uundaji wa majahazi, usagaji nafaka,
uvunaji, usombaji mizigo, usasi na uganga. Isitoshe muziki wa aina hii umewahi
kutumiwa tangu jadi kwa kuhimili na kueneza amali za kijamii kama vile elimu
maadili na taasisi nyinginezo za kitaifa.
Matumizi makubwa ya
muziki wa taarab hata hivyo ni katika mawasiliano ya kijamii. Watungaji wa
taarab hutunga nyimbo zao aghalabu kutokana na msisimko wa hisia au kariha
waipatayo kutokana na tajiriba zao za kimaisha. Nyimbo hizi hueleza hisia,
fikira na mawazo ambayo ni mapana na marefu.
Katika kiwango cha
kisanaa, nyimbo za taarab huonesha umbuji wa kusarifu lugha, misemo na mafumbo
yake ili kufinyanga mawazo mazito. Nyimbo hizi ambazo huwa na mdundo, mahadhi
na lahani mbalimbali zenye kuvutia masikini, huwa na lengo la kuburudisha na
papo hapo kufafanua, kueleza, kuchambua, kukashifu, kusifu na kuieleza jamii. Katika
kutekeleza wajibu huu, watungaji wa taarab ya Kiswahili hawajifungi kimaudhui
bali hujaribu kutungia kila aina ya taathira ya maisha ya jamii. Kutokana na
hili, tuna nyimbo za taarab zinazoeleza mapenzi, imani ya dini, sanaa ya lugha,
siasa na kadhalika. Fungu kubwa la nyimbo hizi zimesarifu maudhui ya
kuiadilisha jamii kwa kusifia nyendo zifuatazo na kukashifu upotovu wa nidhamu
na uadilifu. Tukiangazia macho maudhui haya ya kuadibu jamii katika nyimbo za
taarab, tutagundua kwamba nyimbo hizi zimeshughulikia sana maendeleo yoyote ya
umma yanayostahili kuitwa maendeleo hayana budi kuwa na msingi imara na
mwelekeo ufaao wa kitabia, uadilifu wa utu. Jamii inayotawaliwa na mazingira
yake na pia ujinga wa kukosa elimu ya kibinafsi na kiutu, huwa haiwezi kupata
maendeleo yenye maana. Hapa tunaifasiri dhana ya maendeleo kwa upna wake wa
kimaana kuwa juhudi za kuinua hali na kiwango cha maisha katika jamii nzima.
Maudhui ya nyimbo za
taarab, hata pale ngoma za taarab zilipoonekana kuwa milki ya mabwanyenye,
yalikuwa bado ni ya kijamii. Kwa mfano. Siti Binti Saad katika miaka ya 1920
alipokuwa anavuma kwa nyimbo za taarab hapa Afrika Mashariki, alifikiria juu ya
tabia ya binadamu na uadilifu wake. Kulingana na S. Robert (1967:29), Siti
aliimba:
Si hoja uzuri
Na sura jamali
Kuwa mtukufu
Na jadi kubeli
Hasara ya mtu
Kukosa akili.

Tangu miaka ya 1920 hadi leo nyimbo za
taarab za Kiswahili zimekua kimaudhui. Katika nchi za Afrika ya Mashariki,
vikundi vingi maarufu vya taarab vimeenea hasa katika miji kama Lamu, Malindi,
Mombasa, Tanga, Dar es Salaam na visiwani Unguja na Pemba. Taarab kama vile
lugha na fasihi ya Kiswahili imekuwa ni milki ya jamii finyu ya waswahili bali
ni chombo cha mawasiliano kwa jamii kubwa za maarifa yetu. Majina kama vile
Asha Malika, Bibie Zuhura, Mohamed Kandoro, Zein Labdin, Juma Bhalo, Maulidi
Juma, Jitu Mkali, Noor Khalifa, Zena Mahamud, Bibie Shakila na wengineo
yamekuwa maarufu si Afrika Mashariki tu bali kote utamaduni wa Kiswahili ulipofikia.
Nyimbo zao zimetumiwa kueneza hisia, mawazo na maongozi mbalimbali ya kijamii.
Uwezo wa wasanii wa taarab wa kufinyanga
popo la fikra katika lugha tamu ya kishairi yenye ukwasi wa tamathali za usemi,
jazanda, taswira na mafumbo yaliyochama maana zenye undani, ni sifa moja kuu ya
nyimbo za taarab. Si ajabu wachambuzi wengi wa fasihi simulizi ya Kiswahili ambao
hawajachukua uzito wa kuitalii lugha na semi wanazotumia waimbaji wa taarab,
wameangukia kufikiri, kama Khatibu (1981), kuwa taarab, huzungumzia mapenzi,
uasherati na ugoni. Kwa hakika taarab, kama tanzu nyingine za fasihi simulizi
hujadili matatizo ya jamii kwa jumla na hasa yale ya watu wa kawaida kwa
kuelezea hisia, imani, hofu na ghamidha zao.
Kwa kuwa maudhui ya taarab yamefichika
au kufungamana sana, si rahisi kuyafasiri kwa juu juu bila kuyafanyia makini. Pengine
kule kuyapitia tu mara moja maudhui haya kuyahukumu kunatokana na ile dhana ya
kikoloni iliyopuuza fasihi zetu simulizi kuwa hazikuwa na mawazo yoyote yenye
maana na uzito, kwa mfano, katika wimbo huu, Maulidi Juma, Mwimbaji wa Mombasa
anazungumzia mapenzi na pia siasa katika fumbo moja tu.
Joka juu ya
mdimu, limefanya ni makao
Lipapo halifahamu,
lasema na wapitao
Wala halitaki
ndimu, latisha wazitakao
Kiitikio:
Kuna joka la
mdimu, mdimuni limetanda
Wala halitaki
ndimu, latisha wenye kutunda
Joka hili
limezidi, kutesa wana adamu
Kwa hivyo hapana
budi, lazima tulilaumu
Joka lafanya
kusudi, wala halitaki ndimu
Wenzangu nawauliza,
mnijibu kwa makini
Joka lingatukataza,
tusifike mdimuni
Kisha ndimu
zikioza, joka litapata nini?

Baada
ya kuangalia wimbo kama huu, ni dhahiri kuwa mtribu hakuwa tu akifikiria juu ya
mtu mwovu mwenye wivu, tadi au inda. Tumesikia mengi kuhusu baadhi yetu ambao
licha ya kulimbikiza mali, vyeo na utukufu, wamejipanga kuwaangamiza walio
chini yao. Ujumbe huu huu ndio uliomo katika lile shairi maarufu la Abdilatif
Abdallah liitwalo, (1973:17) “Mnazi Vuta N’kuvute”


ALII
Ndugu ulo
mnazini, wanitafuta balaa
Nakwambiya shuka
tini, katakata wakataa
Wafanya nini
masikini, mustarehe mekaa
           Utashuka au la?
BADI
Mdugu tini ya
mnazi, nilo juu nakujibu
Haya ni ya
upuuzi, unambiyayo swahibu
Kushuka tini
siwezi, pasi kujuwa sababu
          Hiyo ni yangu jawabu
ALII
Sababu ya
kuwambiya, ya kwamba ushuke tini
Ni kuwa nataka
kweye, huko juu mnazi
Kwa ajili name piya,
nitunde nazi mwendani
     N’shakweleza kwa nini
BADI
Hayo ni ya
kutekesha, unambiyayo ndu zangu
Wataka niteremsha,
juu yua mnazi wangu?
Wanistaajabisha,
kuniamuru kwa change
       Una kishaa mwenzangu
ALII
Sina kasha
sinani, akili yangu kamili
Ni wewe
usobaini, pale ulipo ukweli
Mnazi ni tangu
lini, ukawa ni yuako mali?
    Sintendee feeli
BADI
Wabobojekwa maneno,
yasokuwa na maana
Ni ya kupumbavu
mno, hayo uliyonena
Iwapo mnazi
huno, si wangu; mbwa nani bwana?
   Sema nijuwe bayana
ALII
Mnazi ni wa
shirika, mimi na wewe mwendani
Unshakuwa wataka,
kunitowa shirikani?
Hilo halitatendeka,
wala haliwezekani
     Sikubali abadani

Marejeo Katika kipindi
cha baada ya 1960 na hasa baada ya 1965, swala muhimu katika mifumo ya siasa
zetu ni kuhusu ugawaji wa mali na njia za kuzalisha mali pamoja na utajiri wote
wa taifa. Utaratibu wa kikoloni tuliourithi wa kitabaka ulikuwa na kasoro
nyingi hasa kwa vile haukutilia maanani usawa na haki katika ugawaji wa mali za
jamii. Hali hii ilizaa mtafaruku wa migogoro kati ya makundi mbalimbali. Jambo hili
lilisababisha dhuluma na maonevu dhidi ya tabaka la wanyonge lililo na wengi
miongoni mwa umma. Mgogoro huu wote haujawaepuka wasanii wetu wa taarab hata
kidogo.  
Kwa mfano, bibie Shakila anaikejeli hali
hii ya ugomvi na ushindani kati ya wenye nguvu na uwezo. Anasema:
Najua mwanilaumu,
mwenzenu kutojiunga
Nawajuza mfahamu,
sababu ya kujitenga
Kinyang’anyiro
kitamu, lakini kina mtanga
Kiitikio:
Nawajuza mfahamu,
sababu ya kujitenga
Kinyang’anyiro
kitamu, lakini kina mtanga
Eni mliojitolea,
mwenzenu nawashauri
Mimi singeyakimbia,
mwajua yana dosari
Mambo yakung’ang’ania,
hayana mwisho mzuri
Marejeo
Kwa
mtazamo mmoja, huenda tukafikiri kwamba mwimbaji hapa anajiepusha na uhalisi wa
maisha katika jamii yake. Hasa hili silo. Anachofanya ni kutoa utetezi wake
dhidi ya uovu huo wa kuwadhulumu wanyonge kwa sababu ya hali yao dhaifu. Hasemi,
“Dau la mnyonge haliendi joshi au mnyonge hana haki”. Bali anasema, “Dhuluma
ina mwisho wake na wanyonge wana siku yao”. Hajitengi na maendeleo ya jamii
yake bali anajihusisha nayo. Ni kama Maulidi Juma anapoimba,
KANU ndiyo ilo
unda, wanajeshi kukusanya
Ili wapate
tulinda, na mengine ya kufanya
KANU ilileta
tunda, la uhuru hapa Kenya.
Kiitikio:
KANU oh, kanu
yajenga nchi
Yatupasa kujipinda,
kulla tuliko mahali
Chama chetu
kukilinda, kizindi kuwa adili
Ndicho chama
kilounda, hii yetu sirikali
Hatusemi kwamba waimbaji hawa hukashifu
ama kusifu tu kikasuku. Kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa nyimbo hizi
huichambua jamii kwa jicho la undani. Hawachelei kuwaeleza viongozi katika
mapito yafaayo. Hili ndilo jukumu la kila msanii anayestahili kuitwa msanii wa
kweli. Wasanii wakiwemo watribu, hufundisha jamii “sheria” zifaazo na kuzieleza
katika umbuji wa lugha. Huwaadhibu wazivunjao sheria hizi kwa kuwakashifu na
kuwazawadia wanaozizingatia kwa sifa. Wasanii hawa hujitwisha jukumu la kuwa ‘walimu’
wa jamii zao.
Jambo lililo wazi kuwa si wasanii wote
wa taarab wala si kila raia katika nchi zetu ambaye ameupata mwamko wa kihisia,
kimawazo na kisiasa. Si kila mmoja awezaye kuichanganua jamii yake katika
uhalisi wake na kwa njia ya kimantiki kiasi cha kubagua baina ya haki na
batili, ukweli na unafiki; maneno matupu ya kidomo ladha nay ale ya dhati. Fasihi
isiyotimiza lengo lake la kijamii haidumu na mara huchujwa na kutupiliwa mbali.
Fasihi simulizi, hasa taarab, haiwezi kungojea wasanii wake waimarike kisiasa
ndipo watekeleze wajibu unaowapasa kwa jamii zao. Wahakiki, waandishi, washairi
na waimbaji pamoja na wanasanaa wengine wanawajibika kuihimili fani hii kwa
kuipa nafasi katika jamii na vyombo vyote vya mawasiliano. Hili ndilo
analohimiza Abdilatif Abdallah (1977), anaposema.
Tucheze huku
tapima, vyema tupime, miaka iliyosabiki
Tujue tulipo
kwama, tupatilize, na kung’oa visiki
Tulipovuka salama,
tutie shime, alo na haja
Hachoki.
Mchezo unaohimizwa hapa ni kule kuutoa,
kuubaini na kuutetea ukweli wa mambo kama ulivyo katika jamii zetu. Waimbaji wetu
wa taarab wamejaribu kwa kiasi chao kufanya hivyo. Ukweli ndio nguzo ya
maendeleo ya jamii yoyote. Kama alivyosema Shaaban Robert (1968),
Kweli itashinda
namna tunavyoishi
Kweli haihofu
tisho, wala nguvu za majeshi
La uwongolina
mwisho, kweli kitu cha uashi
Kweli itashinda
kesho, kama leo haitoshi.
Lakini taarab na fasihi yote kwa jumla
ina lengo au jukumu zito zaidi ya hili la kuonesha ukweli ulivyo au kuuchora
ukweli kisanaa kwa kutumia lugha inayonata. Fasihi lazima iwe na misingi ya
kinadharia na itikadi. Ni lazima ichukue msimamo hasa katika jamii zenye mifumo
ya kitabaka kama zetu. Fasihi ni lazima ieneze na kupigania maendeleo kwa walio
wengi kwa kujaribu kuzisisimua hisia na mawazo ya hadhira yake na hasa
kuziathiri fikra na vitendo vya hadhira hii kwa njia maalumu kwa kusudi la
kuleta maendeleo ya kweli kwa umma wote. Iwapo wasanii wa taarab wamefikia
hatua hii iwapo wameutekeleza wajibu huu ni mambo yanayohitaji utafiti zaidi. Tangu
wimbo wa kwanza wa Kiswahili uitwao “Hamziya” ulioandikwa kwa hati za Kiarabu
mnamo mwaka wa 1652, hadi leo, nyimbo za Kiswahili na hasa taarab zimepiga
hatua kubwa na kuchangia maendeleo ya jamii zetu. Lakini hata hivyo wasanii
hawa bado wana nafasi kubwa kuweza kuimarisha hadhi na wajibu wa sanaa yao hii
ili iwe chombo madhubuti cha kuwasilisha mawazo ya kimaendeleo katika jamii
zetu.
Hitimisho
Kama tanzu nyingine za fasihi simulizi,
taarab haijapata kuenezwa vyema kupitia katika vyombo vyetu vya mawasiliano na
elimu kama Topan (1984) alivyosema, hli ni tatizo ambalo linaweza kutinga
maendeleo ya fani hii na fasihi simulizi kwa jumla. Wakati umefika ambapo hii
na fasihi simulizi kwa jumla inapaswa, kuenezwa, kufunzwa na kutafitiwa kwa
undani kwa manufaa ya maendeleo ya jamii zetu kwa jumla.
Makala hii imejaribu kujadili kwa ujumla
nafasi na michango ya nyimbo za taarab kama chombo cha mawasiliano katika jamii
za Afrika ya Mashariki. Ingawaje sanaa hii bado imefunguka kitamaduni katika
jamii ya waswahili, lakini bila shaka athari zake zimeivuka mipaka hii na
zinazidi kutapakaa. Kama anavyosisitiza Khatib ( 1992), kuhusu uhusiano baina
ya sanaa na jamii, tunapaswa kusisitiza jambo moja. Jambo hili ni kuwa, jamii
huiwekea sanaa mipaka fulani na hali kadhalika sanaa huitungia jamii ‘sheria’
fulani ili kuathiri nyendo zake. Basi, ni wazi kuwa, ili kuendelea, jamii na
sanaa zote hutegemeana. Fasihi andishi ama simulizi kama taarab ni kipengele
cha jamii. Kwa hivyo kipengele hiki kinaathiri na kuathiriwa na jamii.
Kutoka miaka ya 1870 hadi leo, bila
shaka taarab ya Kiswahili imebadilika na kuku asana kimaudhui na kimtindo. Maendeleo
hayo ni uthibitisho wa umuhimu wa utanzu huu katika jamii. Taarab imetumika
sana katika kipindi cha kuanzia 1960 kuwasilisha maudhui ya kijamii, kisiasa na
pia kukuzia na kueneza fani bunifu za lugha na fasihi ya Kiswahili. Watunzi wa
taarab, kama wasanii wote wa fasihi na muziki, sharti watafute kariha zao
katika maisha ya kila siku na hasa mitindo ya matumizi ya lugha. (Wa Thong’o
1991:149) makala ya Mlama (1980:44) yameeleza kwa undani jinsi sanaa ya taarab
ilivyoweza kusaidia kukuza lugha ya Kiswahili.
Taarab itaendelea kukua na kuenea jinsi
lugha na fasihi ya Kiswahili inavyoenea. Utanzu huu utaendelea kutumika katika Nyanja
nyingi za maisha yetu katika eneo hili yawe ni ya kitamaduni au kisiasa. Muziki
wa densi na santuri za taarab sasa ni chumo kubwa na bila shaka utazidi kuwa
maarufu katika uchumi wetu vile vile.
 
Kioo cha  Lugha 2, 1996/97:101-110

Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)