NAFASI YA NYIMBO ZA KISWAHILI ZA TAARAB KATIKA JAMII YA KISASA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: NAFASI YA NYIMBO ZA KISWAHILI ZA TAARAB KATIKA JAMII YA KISASA (/showthread.php?tid=1385) |
NAFASI YA NYIMBO ZA KISWAHILI ZA TAARAB KATIKA JAMII YA KISASA - MwlMaeda - 10-25-2021 Nafasi ya Nyimbo za Kiswahili za Taarab Katika Jamii ya Kisasa Kitula King’ei
Utangulizi
Fani iitwayo ‘nyimbo’
ni mojawapo ya tanzu maarufu katika fasihi simulizi katika tamaduni zote. Katika fasihi ya Kiswahili, utanzu wa nyimbo umeingiliana na kuathiriana sana kimuundo na kimtindo na utanzu wa ‘shairi’ hasa tukichukulia shairi kama fani au bahari moja katika uwanja wa sanaa ya ushairi kwa jumla Abdalla (1978:1-6). Katika karatasi hii hatutajishughulisha sana na swala la historia, ulinganifu au tofauti kati ya ‘nyimbo’ za taarab za Kiswahili na bahari nyingine za ushairi. Haya yameshughulikiwa na wataalamu na wachambuzi wengine wa fasihi ya Kiswahili miongoni mwao akiwa Khatib (1981). Dhamira ya makala hii
ni kukadiria mchango uliofanywa na waimbaji wa nyimbo za taarab za Kiswahili katika mawasiliano hasa ya kimasimulizi. Ni imani ya mwandishi kuwa nyimbo za taarab zimetungwa na zinaendelea kutungwa na kusambazwa kama chombo cha mawasiliano kwa malengo kadha. Kwa sababu hii,
tunaweza kusema kuwa nyimbo hizi zina dhima au jukumu la kutimiza katika harakati za maendeleo ya nchi zetu hasa katika Afrika Mashariki. Jambo hili limedokezwa na Asha Malika, mwimbaji maarufu wa nyimbo hizi yapata miaka kumi iliyopita. Kulingana na Dumila (1977: 21), msanii huyu ameeleza: Nyimbo
zangu hutalii hisia za ndani za mwanadamu na mapenzi na matakwa yake. Hukitumia kipaji change cha sauti tamu kwa manufaa ya wanadamu wote. Huitumia sauti yangu kuhimiza uzalendo kati ya wana Somalia wenzangu, Utaifa kati ya wanapwani wote wa Upwa wetu, Uafrika kati ya Waafrika wote na utu kati ya wote wanisikiao. Jambo analosisitiza
hapa Malika ni kwamba msanii wa taarab ana jukumu la kuchangia maendeleo ya taifa lake na wanadamu wote kwa jumla. Kama fani za fasihi ya maandishi, fani ya nyimbo hubuniwa, kuenezwa na kuchambuliwa kijumuiya. Nyimbo hizi ni zao la falsafa, maoni, hisia na amali nyingine za jumuiya. Jukumu la nyimbo za
taarab kwa mtazamo wa kijamii huishurutisha fani hii kujihusisha kadiri ya mapito ya wakati. Kimuundo na kimaudhui, nyimbo za taarab zimebidika kukaa na kubadilika kufungamana na mabadiliko ya jamii zinamoibuka. Hii ndiyo sifa ya pekee inayoifanya fasihi simulizi kwa jumla na nyimbo za taarab hasa, kujitanzua na ile hoja isiyokuwa na mashiko inayoieleza fasihi simulizi kuwa “fasihi kongwe inayopokezwa kizazi hadi kizazi”. Kama asemavyo F.E.M. Senkoro (1981:1) fasihi simulizi na fani zake zote. Ni
sanaa hai ambayo nayo huhusika katika kanuni ya migongano na ya mwendo katika maisha….sehemu zake zingine vikumbo na wakati na mazingira mapya zikabaki kuwa historia… Mjadala
Nyimbo za taarab katika
Kiswahili zina historia ndefu. Ni wazi kuwa utanzu wa ‘nyimbo’ kama ule wa ushairi umekita katika utamaduni asilia wa jamii zote za binadamu. Kwa hiyo nyimbo za taarab zinazoimbwa kwa kutumia vyombo kadha wa kadha vya kimagharibi na kimashariki ni jambo lililotokea tu katika karne ya kumi na tisa hasa kati ya miaka ya 1870 na 1888. Nyimbo nyingi zilizotungwa kabla ya wakati huu, yamkini zimetoweka katika kumbukumbu. Lakini tunapoyachunguza maudhui ya nyimbo za taarab katika karne moja iliyopita tunapata ushahidi wa kutosha kuonesha sanaa hii imehusika kiasi gani katika maswala ya jamii. Kulingana na maoni ya
M.S. Khatib, sanaa ya taarab katika Afrika ya Mashariki imepitia hatua tatu muhimu na kila kipindi cha maendeleo yake kikiwa na athari fulani juu ya sanaa yenyewe kimaudhui. Kipindi cha kwanza ni cha kati ya mwaka 1970 na 1988 ambapo Waswahili walitunga taarab aghalabu katika majumba ya kifalme, hasa sehemu za Unguja ili kuwatumbuiza watawala na tabaka lao la kibwanyenye kwa jumla. Kipindi cha pili kati ya mwaka 1905 na 1920 ndipo makundi kadha huru ya watribu yalipoanza kubuniwa. Wakati huu nyimbo za taarab zilikuwa zimeigubika jamii finyu tu. Ni katika kipindi cha miaka ya 1920 na 1950 ambapo taarab ilianza kuenea kutoka visiwani na kupenya jamii ya pwani ya Afrika Mashariki. Kutokea miaka ya 1960 taarab imekuwa burudani maalumu katika miji mingi ya pwani hata bara. Taarab hivi leo imefika Burundi na Rwanda. Sasa turudi nyuma na
kuyaangalia maudhui ya mjadala huu ambayo ni “jukumu na maendeleo” ya fasihi ya Kiswahili. Utanzu wa nyimbo kama utanzu mzima wa ushairi na muziki hauwezi kutenganishwa na maisha ya jamii nzima. Katika jamii zote ulimwenguni, sanaa huwa ni chombo kitumikizi. Kwa hivyo, nyimbo za taarab, katika utamaduni wa Waswahili kama kipengele kimojawapo cha fasihi ya Kiswahili zina nafasi na jukumu maalumu kama vile kuelimisha, na kutumbuiza nyimbo hizi za taarab zimewanda kimaudhui na kugubika vitabia na Nyanja zote za maisha ya jamii zetu. Katika kiwango cha kiuchumi kwa mfano, taarab zimetungwa kuambatana na shughuli nyingi za kuzalisha mali kama vile uvuvi, uundaji wa majahazi, usagaji nafaka, uvunaji, usombaji mizigo, usasi na uganga. Isitoshe muziki wa aina hii umewahi kutumiwa tangu jadi kwa kuhimili na kueneza amali za kijamii kama vile elimu maadili na taasisi nyinginezo za kitaifa. Matumizi makubwa ya
muziki wa taarab hata hivyo ni katika mawasiliano ya kijamii. Watungaji wa taarab hutunga nyimbo zao aghalabu kutokana na msisimko wa hisia au kariha waipatayo kutokana na tajiriba zao za kimaisha. Nyimbo hizi hueleza hisia, fikira na mawazo ambayo ni mapana na marefu. Katika kiwango cha
kisanaa, nyimbo za taarab huonesha umbuji wa kusarifu lugha, misemo na mafumbo yake ili kufinyanga mawazo mazito. Nyimbo hizi ambazo huwa na mdundo, mahadhi na lahani mbalimbali zenye kuvutia masikini, huwa na lengo la kuburudisha na papo hapo kufafanua, kueleza, kuchambua, kukashifu, kusifu na kuieleza jamii. Katika kutekeleza wajibu huu, watungaji wa taarab ya Kiswahili hawajifungi kimaudhui bali hujaribu kutungia kila aina ya taathira ya maisha ya jamii. Kutokana na hili, tuna nyimbo za taarab zinazoeleza mapenzi, imani ya dini, sanaa ya lugha, siasa na kadhalika. Fungu kubwa la nyimbo hizi zimesarifu maudhui ya kuiadilisha jamii kwa kusifia nyendo zifuatazo na kukashifu upotovu wa nidhamu na uadilifu. Tukiangazia macho maudhui haya ya kuadibu jamii katika nyimbo za taarab, tutagundua kwamba nyimbo hizi zimeshughulikia sana maendeleo yoyote ya umma yanayostahili kuitwa maendeleo hayana budi kuwa na msingi imara na mwelekeo ufaao wa kitabia, uadilifu wa utu. Jamii inayotawaliwa na mazingira yake na pia ujinga wa kukosa elimu ya kibinafsi na kiutu, huwa haiwezi kupata maendeleo yenye maana. Hapa tunaifasiri dhana ya maendeleo kwa upna wake wa kimaana kuwa juhudi za kuinua hali na kiwango cha maisha katika jamii nzima. Maudhui ya nyimbo za
Si hoja uzuritaarab, hata pale ngoma za taarab zilipoonekana kuwa milki ya mabwanyenye, yalikuwa bado ni ya kijamii. Kwa mfano. Siti Binti Saad katika miaka ya 1920 alipokuwa anavuma kwa nyimbo za taarab hapa Afrika Mashariki, alifikiria juu ya tabia ya binadamu na uadilifu wake. Kulingana na S. Robert (1967:29), Siti aliimba: Na sura jamali Kuwa mtukufu Na jadi kubeli Hasara ya mtu Kukosa akili. Tangu miaka ya 1920 hadi leo nyimbo za
taarab za Kiswahili zimekua kimaudhui. Katika nchi za Afrika ya Mashariki, vikundi vingi maarufu vya taarab vimeenea hasa katika miji kama Lamu, Malindi, Mombasa, Tanga, Dar es Salaam na visiwani Unguja na Pemba. Taarab kama vile lugha na fasihi ya Kiswahili imekuwa ni milki ya jamii finyu ya waswahili bali ni chombo cha mawasiliano kwa jamii kubwa za maarifa yetu. Majina kama vile Asha Malika, Bibie Zuhura, Mohamed Kandoro, Zein Labdin, Juma Bhalo, Maulidi Juma, Jitu Mkali, Noor Khalifa, Zena Mahamud, Bibie Shakila na wengineo yamekuwa maarufu si Afrika Mashariki tu bali kote utamaduni wa Kiswahili ulipofikia. Nyimbo zao zimetumiwa kueneza hisia, mawazo na maongozi mbalimbali ya kijamii. Uwezo wa wasanii wa taarab wa kufinyanga
popo la fikra katika lugha tamu ya kishairi yenye ukwasi wa tamathali za usemi, jazanda, taswira na mafumbo yaliyochama maana zenye undani, ni sifa moja kuu ya nyimbo za taarab. Si ajabu wachambuzi wengi wa fasihi simulizi ya Kiswahili ambao hawajachukua uzito wa kuitalii lugha na semi wanazotumia waimbaji wa taarab, wameangukia kufikiri, kama Khatibu (1981), kuwa taarab, huzungumzia mapenzi, uasherati na ugoni. Kwa hakika taarab, kama tanzu nyingine za fasihi simulizi hujadili matatizo ya jamii kwa jumla na hasa yale ya watu wa kawaida kwa kuelezea hisia, imani, hofu na ghamidha zao. Kwa kuwa maudhui ya taarab yamefichika
au kufungamana sana, si rahisi kuyafasiri kwa juu juu bila kuyafanyia makini. Pengine kule kuyapitia tu mara moja maudhui haya kuyahukumu kunatokana na ile dhana ya kikoloni iliyopuuza fasihi zetu simulizi kuwa hazikuwa na mawazo yoyote yenye maana na uzito, kwa mfano, katika wimbo huu, Maulidi Juma, Mwimbaji wa Mombasa anazungumzia mapenzi na pia siasa katika fumbo moja tu. Joka juu ya
mdimu, limefanya ni makao Lipapo halifahamu,
lasema na wapitao Wala halitaki
ndimu, latisha wazitakao Kiitikio:
Kuna joka la
mdimu, mdimuni limetanda Wala halitaki
ndimu, latisha wenye kutunda Joka hili
limezidi, kutesa wana adamu Kwa hivyo hapana
budi, lazima tulilaumu Joka lafanya
kusudi, wala halitaki ndimu Wenzangu nawauliza,
mnijibu kwa makini Joka lingatukataza,
tusifike mdimuni Kisha ndimu
zikioza, joka litapata nini? Baada ya kuangalia wimbo kama huu, ni dhahiri kuwa mtribu hakuwa tu akifikiria juu ya mtu mwovu mwenye wivu, tadi au inda. Tumesikia mengi kuhusu baadhi yetu ambao licha ya kulimbikiza mali, vyeo na utukufu, wamejipanga kuwaangamiza walio chini yao. Ujumbe huu huu ndio uliomo katika lile shairi maarufu la Abdilatif Abdallah liitwalo, (1973:17) “Mnazi Vuta N’kuvute” ALII
Ndugu ulo
mnazini, wanitafuta balaa Nakwambiya shuka
tini, katakata wakataa Wafanya nini
masikini, mustarehe mekaa Utashuka au la?
BADI
Mdugu tini ya
mnazi, nilo juu nakujibu Haya ni ya
upuuzi, unambiyayo swahibu Kushuka tini
siwezi, pasi kujuwa sababu Hiyo ni yangu jawabu
ALII
Sababu ya
kuwambiya, ya kwamba ushuke tini Ni kuwa nataka
kweye, huko juu mnazi Kwa ajili name piya,
nitunde nazi mwendani N’shakweleza kwa nini
BADI
Hayo ni ya
kutekesha, unambiyayo ndu zangu Wataka niteremsha,
juu yua mnazi wangu? Wanistaajabisha,
kuniamuru kwa change Una kishaa mwenzangu
ALII
Sina kasha
sinani, akili yangu kamili Ni wewe
usobaini, pale ulipo ukweli Mnazi ni tangu
lini, ukawa ni yuako mali? Sintendee feeli
BADI
Wabobojekwa maneno,
yasokuwa na maana Ni ya kupumbavu
mno, hayo uliyonena Iwapo mnazi
huno, si wangu; mbwa nani bwana? Sema nijuwe bayana
ALII
Mnazi ni wa
shirika, mimi na wewe mwendani Unshakuwa wataka,
kunitowa shirikani? Hilo halitatendeka,
wala haliwezekani Sikubali abadani
Marejeo Katika kipindi
cha baada ya 1960 na hasa baada ya 1965, swala muhimu katika mifumo ya siasa zetu ni kuhusu ugawaji wa mali na njia za kuzalisha mali pamoja na utajiri wote wa taifa. Utaratibu wa kikoloni tuliourithi wa kitabaka ulikuwa na kasoro nyingi hasa kwa vile haukutilia maanani usawa na haki katika ugawaji wa mali za jamii. Hali hii ilizaa mtafaruku wa migogoro kati ya makundi mbalimbali. Jambo hili lilisababisha dhuluma na maonevu dhidi ya tabaka la wanyonge lililo na wengi miongoni mwa umma. Mgogoro huu wote haujawaepuka wasanii wetu wa taarab hata kidogo. Kwa mfano, bibie Shakila anaikejeli hali
hii ya ugomvi na ushindani kati ya wenye nguvu na uwezo. Anasema: Najua mwanilaumu,
mwenzenu kutojiunga Nawajuza mfahamu,
sababu ya kujitenga Kinyang’anyiro
kitamu, lakini kina mtanga Kiitikio:
Nawajuza mfahamu,
sababu ya kujitenga Kinyang’anyiro
kitamu, lakini kina mtanga Eni mliojitolea,
mwenzenu nawashauri Mimi singeyakimbia,
mwajua yana dosari Mambo yakung’ang’ania,
hayana mwisho mzuri Marejeo
Kwa mtazamo mmoja, huenda tukafikiri kwamba mwimbaji hapa anajiepusha na uhalisi wa maisha katika jamii yake. Hasa hili silo. Anachofanya ni kutoa utetezi wake dhidi ya uovu huo wa kuwadhulumu wanyonge kwa sababu ya hali yao dhaifu. Hasemi, “Dau la mnyonge haliendi joshi au mnyonge hana haki”. Bali anasema, “Dhuluma ina mwisho wake na wanyonge wana siku yao”. Hajitengi na maendeleo ya jamii yake bali anajihusisha nayo. Ni kama Maulidi Juma anapoimba, KANU ndiyo ilo
unda, wanajeshi kukusanya Ili wapate
tulinda, na mengine ya kufanya KANU ilileta
tunda, la uhuru hapa Kenya. Kiitikio:
KANU oh, kanu
yajenga nchi Yatupasa kujipinda,
kulla tuliko mahali Chama chetu
kukilinda, kizindi kuwa adili Ndicho chama
kilounda, hii yetu sirikali Hatusemi kwamba waimbaji hawa hukashifu
ama kusifu tu kikasuku. Kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa nyimbo hizi huichambua jamii kwa jicho la undani. Hawachelei kuwaeleza viongozi katika mapito yafaayo. Hili ndilo jukumu la kila msanii anayestahili kuitwa msanii wa kweli. Wasanii wakiwemo watribu, hufundisha jamii “sheria” zifaazo na kuzieleza katika umbuji wa lugha. Huwaadhibu wazivunjao sheria hizi kwa kuwakashifu na kuwazawadia wanaozizingatia kwa sifa. Wasanii hawa hujitwisha jukumu la kuwa ‘walimu’ wa jamii zao. Jambo lililo wazi kuwa si wasanii wote
wa taarab wala si kila raia katika nchi zetu ambaye ameupata mwamko wa kihisia, kimawazo na kisiasa. Si kila mmoja awezaye kuichanganua jamii yake katika uhalisi wake na kwa njia ya kimantiki kiasi cha kubagua baina ya haki na batili, ukweli na unafiki; maneno matupu ya kidomo ladha nay ale ya dhati. Fasihi isiyotimiza lengo lake la kijamii haidumu na mara huchujwa na kutupiliwa mbali. Fasihi simulizi, hasa taarab, haiwezi kungojea wasanii wake waimarike kisiasa ndipo watekeleze wajibu unaowapasa kwa jamii zao. Wahakiki, waandishi, washairi na waimbaji pamoja na wanasanaa wengine wanawajibika kuihimili fani hii kwa kuipa nafasi katika jamii na vyombo vyote vya mawasiliano. Hili ndilo analohimiza Abdilatif Abdallah (1977), anaposema. Tucheze huku
tapima, vyema tupime, miaka iliyosabiki Tujue tulipo
kwama, tupatilize, na kung’oa visiki Tulipovuka salama,
tutie shime, alo na haja Hachoki.
Mchezo unaohimizwa hapa ni kule kuutoa,
kuubaini na kuutetea ukweli wa mambo kama ulivyo katika jamii zetu. Waimbaji wetu wa taarab wamejaribu kwa kiasi chao kufanya hivyo. Ukweli ndio nguzo ya maendeleo ya jamii yoyote. Kama alivyosema Shaaban Robert (1968), Kweli itashinda
namna tunavyoishi Kweli haihofu
tisho, wala nguvu za majeshi La uwongolina
mwisho, kweli kitu cha uashi Kweli itashinda
kesho, kama leo haitoshi. Lakini taarab na fasihi yote kwa jumla
ina lengo au jukumu zito zaidi ya hili la kuonesha ukweli ulivyo au kuuchora ukweli kisanaa kwa kutumia lugha inayonata. Fasihi lazima iwe na misingi ya kinadharia na itikadi. Ni lazima ichukue msimamo hasa katika jamii zenye mifumo ya kitabaka kama zetu. Fasihi ni lazima ieneze na kupigania maendeleo kwa walio wengi kwa kujaribu kuzisisimua hisia na mawazo ya hadhira yake na hasa kuziathiri fikra na vitendo vya hadhira hii kwa njia maalumu kwa kusudi la kuleta maendeleo ya kweli kwa umma wote. Iwapo wasanii wa taarab wamefikia hatua hii iwapo wameutekeleza wajibu huu ni mambo yanayohitaji utafiti zaidi. Tangu wimbo wa kwanza wa Kiswahili uitwao “Hamziya” ulioandikwa kwa hati za Kiarabu mnamo mwaka wa 1652, hadi leo, nyimbo za Kiswahili na hasa taarab zimepiga hatua kubwa na kuchangia maendeleo ya jamii zetu. Lakini hata hivyo wasanii hawa bado wana nafasi kubwa kuweza kuimarisha hadhi na wajibu wa sanaa yao hii ili iwe chombo madhubuti cha kuwasilisha mawazo ya kimaendeleo katika jamii zetu. Hitimisho
Kama tanzu nyingine za fasihi simulizi,
taarab haijapata kuenezwa vyema kupitia katika vyombo vyetu vya mawasiliano na elimu kama Topan (1984) alivyosema, hli ni tatizo ambalo linaweza kutinga maendeleo ya fani hii na fasihi simulizi kwa jumla. Wakati umefika ambapo hii na fasihi simulizi kwa jumla inapaswa, kuenezwa, kufunzwa na kutafitiwa kwa undani kwa manufaa ya maendeleo ya jamii zetu kwa jumla. Makala hii imejaribu kujadili kwa ujumla
nafasi na michango ya nyimbo za taarab kama chombo cha mawasiliano katika jamii za Afrika ya Mashariki. Ingawaje sanaa hii bado imefunguka kitamaduni katika jamii ya waswahili, lakini bila shaka athari zake zimeivuka mipaka hii na zinazidi kutapakaa. Kama anavyosisitiza Khatib ( 1992), kuhusu uhusiano baina ya sanaa na jamii, tunapaswa kusisitiza jambo moja. Jambo hili ni kuwa, jamii huiwekea sanaa mipaka fulani na hali kadhalika sanaa huitungia jamii ‘sheria’ fulani ili kuathiri nyendo zake. Basi, ni wazi kuwa, ili kuendelea, jamii na sanaa zote hutegemeana. Fasihi andishi ama simulizi kama taarab ni kipengele cha jamii. Kwa hivyo kipengele hiki kinaathiri na kuathiriwa na jamii. Kutoka miaka ya 1870 hadi leo, bila
shaka taarab ya Kiswahili imebadilika na kuku asana kimaudhui na kimtindo. Maendeleo hayo ni uthibitisho wa umuhimu wa utanzu huu katika jamii. Taarab imetumika sana katika kipindi cha kuanzia 1960 kuwasilisha maudhui ya kijamii, kisiasa na pia kukuzia na kueneza fani bunifu za lugha na fasihi ya Kiswahili. Watunzi wa taarab, kama wasanii wote wa fasihi na muziki, sharti watafute kariha zao katika maisha ya kila siku na hasa mitindo ya matumizi ya lugha. (Wa Thong’o 1991:149) makala ya Mlama (1980:44) yameeleza kwa undani jinsi sanaa ya taarab ilivyoweza kusaidia kukuza lugha ya Kiswahili. Taarab itaendelea kukua na kuenea jinsi
lugha na fasihi ya Kiswahili inavyoenea. Utanzu huu utaendelea kutumika katika Nyanja nyingi za maisha yetu katika eneo hili yawe ni ya kitamaduni au kisiasa. Muziki wa densi na santuri za taarab sasa ni chumo kubwa na bila shaka utazidi kuwa maarufu katika uchumi wetu vile vile. Kioo cha Lugha 2, 1996/97:101-110 |