FUNGUA HAPA CHINI KUSOMA KITABU >>>>
TUTARUDI-NA-ROHO-ZETU1.pdf (Size: 2.15 MB / Downloads: 1)
1.0 Utangulizi[/url]
Kazi hii inahusu uchambuzi wa maudhui katika riwaya ya mkondo wa kipelelezi na kiarifu ambayo inaitwa“Tutarudi na Roho Zetu?”iliyoandikwa na Ben Mtobwa. Katika kujadili riwaya hii tutaeleza dhana ya riwaya, dhana ya mkondo wa kipelelezi, usuli wa mwandishi, muhtasari wa kitabuchenyewe, nadharia itakayotumika kuchambua maudhui ya kitabu hiki, uchambuzi wa maudhui na hitimisho.
1.1 Dhana ya Riwaya
Kwa mujibu wa Madumulla (2009) akimrejelea Msokile (1992) anafafanua kuwa riwaya ni kazi ya sanaa ya kubuni, ni maandishi ya nathari (ujazo) yanayosimulia hadithi ambayo kwa kawaida ina uzito, upana, urefu wa kutosha, ina wahusika wengi wenye tabia mbalimbali, ina migogoro mingi mikubwa na midogo.
Senkoro (1982) anasema riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii.
Wamitila (2003), Samwel na wenzake (2013), wanasema kuwa riwaya ni kazi andishi ya fasihi ambayo kwa kawaida ni ndefu zaidi kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya maana yake ni kwamba msuko simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi, inaenea muda mrefu, na mada zake ni nzito na pana kiasi. Mifano mizuri ya riwaya kwa lugha ya Kiswahili ni “Nagona” au “Mzingile” riwaya za mwandishi Euphrase Kezilahabi.
Kwa ujumla riwaya ni hadithi ndefu za kubuni zenye wahusika wengi au wachache zinazoelezea maisha ya mtu au jamii fulani.
1.2 Dhana ya mkondo wa kiarifu na kipelelezi
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) mkondo wa kiarifu na kipelelezi ni kategoria ya ubunaji kuhusu uhalifu na upelelezi iliyojitokeza katika fasihi ya Kiswahili karibu mwishoni mwa muongo wa hamsini wa karne ya 20.
Mkondo wa kipelelezi; aina hii ya utunzi inahusishahadithi zinazosimulia kuhusu upeleleziwa uhalifu fulani kama vileujambazi, wizi, rushwa, mauaji. Kwakawaida huanza na tukio fulani la uhalifu ambalo limekwisha tendekanaye msimulizi huwaongoza wasomajikatika safari ya kung'amua kiini chauhalifu husika. Sifa kuu ya hadithihizi ni kwamba husheheni taharukinyingi na huiteka hadhira kwa kuchocheahamu ya kugundua au kuteguakitendawili. Kwa mfano riwaya ya'Masaibu ya Ndugu Jero.' (Taifa leo, 2015).
Hivyo basi mkondo wa kiarifu na kipelelezi ni mkondo ambao unahusu riwaya zenye uhalifu na upelelezi ndani yake kama vile ujambazi, rushwa na mauaji. Kwa mfano katika riwaya hii ya “Tutarudi na roho zetu?” ni mfano mzuri wa mkondo huu kwani umejaa upelelezi na uhalifu ndani yake.
1.3 Usuli wa Mwandishi
Kwa mujibu wa Dr. Mikhail (2008) mwandishi Ben Rashid Mtobwa alizaliwa tarehe 28 mwezi wa nane, mwaka 1958 huko mkoani Kigoma, magharibi ya Tanzania. Maisha yake na kazi yake alijikita katika uandishi kwa lugha ya Kiswahili. Alioa na alikuwa na watoto wanne.
Ben Mtobwa alianza uandishi akiwa shule ya sekondari. Baadaye alianza kuandika habari katika magazeti kama “Nchi yangu,” “Bara Afrika” na “Kiongozi”. Pia, uhariri katika magazeti kama “Uhuru na Mfanyakazi”. Akiwa mwandishi alianza kujulikana miaka ya 1980 akiwa miongoni mwa waandishi walioanza kuandika vitabu vya Kiswahili. Vitabu vyake vilivyojulikana sana miaka hiyo ni “Dimbwi la Damu” (1984),“Tutarudi na Roho zetu?”(1984), “Najisikia Kuua Tena” (1985), “Joram Kiango Mikononi mwa Nunda” (1986),Lazima Ufe Joram” (1986),“Pesa Zako Zinanuka” (1986),“Salamu Kutoka Kuzimu” (1987), “Malaika wa Shetani” (1988),Dar es Salaam Usiku” (1990), “Zawadi ya Ushindi” (1992), “Nyuma ya Mapazia” (1996), “Roho ya Paka” (1996) “Mtambo wa Mauti” (2004). Piaaliandika kitabu cha watoto kilichoitwa “Nitakusubiri” na habari ndogo iliyoitwa“Mwanaharamu”na mwishoni kabla ya kifo aliandika kitabu kilichoitwa “Mikataba ya Kishetani”.
Baada ya kujulikana kama mwandishi miaka ya 1980 Ben Mtobwa alikuwa meneja mwongozaji katika kampuni ya uchapishaji ya Heko iliyopo jijini Dar es Salaam. Baadae kampuni hiyo ilikuwa muhimu sana katika usambazaji wa vitabu vya fasihi, uchapishaji wa magazeti na kuwasaidia waandishi chipukizi.
Ben Mtobwa alifariki tarehe 9/11/2008, akiondoka na mipango mingi mipya na matumaini makubwa katika kuikuza fasihi na maisha ya jamii. Hali hii imezifanya jamii kumkumbuka sana kutokana na mchango wake kiuandishi na kifasihi.
1.4 Muhtasari wa kitabu
“Tutarudi na Roho Zetu?” ni riwaya iliyoandikwa na Ben Mtobwa. Riwaya hii inaelezea shughuli zilizofanywa na nchi za mstari wa mbele katika ukombozi kusini mwa Afrika, zimetendwa mengi maovu na utawala dhalimu….hata hivyo haikupatikana kutokea tishio zito la kutisha kama hili, ambalo linakaribia kutokea. Tukio la kutatanisha ambalo linawatoa machozi wananchi wanchi mbalimbali. Wanajitokeza mashujaa kwenda Afrika kusini, lakini kila aendaye huko harudi na roho yake.
Inspecta Kombora nchiniTanzania jasho linamtoka. Anawathamini mashujaa wengi lakini anamtambua shujaa mmoja Joram Kiango. Jambo la kusikitisha ni kwamba sasa hivi Joram ni mtumiaji mzuri ambaye anatembea kutoka jiji hadi jiji akiwa na yule msichana mzuri Nuru. Juhudi za Kombora kumsihi hazikufua dafu. Badala yake Joram anafanya maajabu mengine ambayo yanalichafua jina lake hapa nchini na kote duniani. Wakati huo siku ambayo utawala huo umeweka ili kuachia pigo lao la mwisho inazidi kukaribia. Sasa yamesalia masaa, lakini baadae Joram anaonekana ndiye mkombozi mkuu wa nchi za mstari wa mbele. Mwandishi wa hadithi hii amezungumzia mambo tofauti tofauti kwa zana mbalimbali ambazo ni pamoja na watu wenye bahati na wenye mikosi, wasichana wenye sura nzuri na wale wenye mbaya. Ni hadithi kuhusu mapenzi na chuki, uhai na kifo.
1.5 Nadharia ya Uhalisia
TUKI (2004) wanaeleza kuwa nadharia ni mawazo, maelezo na muongozo uliopangwa ili kusaidia kuelezea kutatua au kutekeleza jambo fulani. Nadharia yoyote ile ya kihakiki ni nyezo ya kusaidia kufikisha lengo fulani.
Kwa mujibu wa Ntarangwi (2004) anasema nadharia ya uhalisia ni uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi, nadharia hii ilizuka katika karne ya 19 hususani kwa sababu za kupinga mkondo wa ulimbwende.
Hivyo basi, nadharia ya uhalisia ni nadharia ambayo hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahususi na matokeo yanayoweza kuthibitika. Tukirejelea katika riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?”mwandishi amejikita katika uhalisia kwani amezungumzia mambo ambayo yanajitokeza na yapo katika jamii. Hivyo tutatumia nadharia hii kuhakiki maudhui yaliyojitokeza katika kitabu hiki kwa kuwa kitabu hiki kinasawiri mambo ambayo yapo katika jamii zetu.
2.0 Maudhui katika Riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?”
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) maudhui ni mawazo fikra na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi.Maudhui ina vipengele mbalimbali ambavyo ni pamoja na dhamira, ujumbe, falsafa, migogoro, msimamo na mtazamo wa mwandishi. Katika riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?” vipengele vya maudhui vinavyojipambanua au kujidhihirisha ni pamoja na:-
2.1 Dhamira
Madumulla (katajwa) anasema dhamira ni wazo kuu katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui. Dhamira ndiyo hujenga kiini cha kazi ya fasihi,yafuatayo ni mawazo au dhamira zilizojitokeza katika riwaya hii ya“Tutarudi na Roho Zetu?”
2.1.1 Ukombozi
TUKI (katajwa) wanasema kuwa ukombozi ni uokoaji wa watu kutoka kwenye hali mbaya ya udhalimu au hali duni. Katika riwaya hii kuna aina mbili za ukombozi zilizojitokeza ambazo ni ukombozi wa kisiasa na ukombozi wa kifikra.
2.1.1.1Ukombozi wa Kisiasa
Katika riwaya ya “Tutarudi na Roho Zetu?”miongoni mwa ukombozi uliojitokeza ni ukombozi wa kisiasa. Mwandishi anadhihirisha ukombozi wa kisiasa kwa kumtumia mhusika wakemkuu Joram ambaye ni mpelelezi, analisaidia bara lake kupata ukombozi kutoka katika mikono ya makaburu akishirikiana na mwenzake Nuru. Mwandishi anasema;
“Kwa kila hali inaonyesha dhahiri kuwa Joram Kiango akishirikiana na mwenzi wake, yule msichana mzuri Nuru. Wameshiriki kwa njia moja au nyingine katika kufanya hayo yaliyofanyika huko Afrika Kusini.Na endapo wasingefanya walichokifanya dakika hii hii Afrika nzima ingekuwa katika msiba kwani kulikuwa na mipango ya mtambo huo kuzishambulia nchi zote za mstari wa mbele kwa pamoja”(uk 173).
2.1.1.2 Ukombozi wa Kifikra
Mwandishi anaonesha ukombozi wa kifikra katikariwaya hii kwa kumtumia mhusika wake Joram.Pale ambapo Joram aliamua kurudi tena na kupigania ukombozi katika bara lake, baada ya kukaa muda mrefu akiwa anastarehe na Nuru katika miji mbalimbali na baadaetunaona jinsi anavyojitoa kusaidia bara lake kwa kutega vigololi vilivyopatikana kwa Chonde na kuvitega katika majengo muhimu ya Makaburu wa Afrika kusini kwa muda wa masaa machache.Mwandishi anasema;
“Wakiwa wameikariri ramani hiyo kikamilifu kazi waliyoifanya mitaani humo ilikuwa ya kufuata yale majengo waliyokusudia na kutega vile vigololi vilivyopatikana kwa chonde na kuvitegesha katika kipindi cha saa tatu kamili”(uk 132).
Katika jamii yetu suala la ukombozi limejitokeza hasa kipindi kilichopita cha uchaguzi, watu wengi wamekombolewa kifikra katika suala zima la siasa, ambapo imepelekea wanajamii (watanzania) wengi kujiingiza katika siasa na kutafuta haki ndani ya siasa.
2.1.2 Kujitoa mhanga
Kujitoa mhanga ni kufanya jambo fulani kwa ajili ya kitu, mtu au watu fulani na kuwa tayari kwa lolote ([url=http://www.merriam-webster.com/dictionary/sacrifice]www.merriam-webster.com/dictionary/sacrifice).Katika riwaya ya hii tunaona suala la kujitoa mhanga limejitokeza, kwani tumeona jinsi Joram na Nuru wanavyojitoa ili kuikomboa nchi yao, hadi kufikia hatua ya kuhatarisha uhai wao na hata wao wenyewe kuua ili tu waweze kulikomboa bara lao dhidi ya makaburu. Mwandishi anadhihirisha suala la kujitoa mhanga kwa kumtumia mhusika wake Nuru alivyojitoa mhanga na kumuua Chonde kwa bastola ili kuokoa maisha ya Joram. Mwandishi anasema;
“Risasi mbili tatu zaidi zilisikika kama zilizopigwa bila shabaha yeyote. Kisha kimya kikafuata, kimya ambacho kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa akikata roho………….” (Uk 47)
Vile vile mwandishi ameonyesha suala la kujitoa mhanga kwa kumtumia mkaburu aliyetoka Afrika kusini kuja Tanzania kwa lengo la kufanya upelelezi huku akiwa amefanya plastic surgery miaka 10 iliyopita, ambapo tumboni alionekana mweusi, usoni na mikononi alikuwa mweupe ili hali yeye kwa asili ni mtu mweupe,hii inathibitisha jinsi mkaburu huyo alivyojitoa mhanga ili aweze kupata taarifa kutoka katika nchi ya Tanzania. Mwandishi anasema;
“………….Ningependa ieleweke kuwa mimi siyo mzungu…..mimi ni mtu mweusi mzaliwa wa Soweto ….. Ngozi hii nyeupe iliyokaa usoni na mikononi ni matokeo ya plastic surgery ambayo niliifanya miaka kumi iliyopita.” (Uk 95)
Katika jamii tunayoishi suala la kujitoa mhanga limejitokeza kwani tunaona baadhi ya viongozi walivyoamua kujitoa mhanga ili kuleta maendeleo katika jamii.
2.1.3 Ujasiri
Kwa mujibu wa TUKI (katajwa) ujasiri ni hali ya kukabili jambo bila ya hofu, uhodari na ushujaa. Katika riwaya hii mwandishi ameonesha suala la ujasiri kwa kuwatumia wahusika wake wakuu Joram na Nuru. Ujasiri umejitokeza kwa kiwango kikubwa kwani tunaona jinsi Joram na Nuru walivyokuwa jasiri katika harakati za kulikomboa bara lao kutoka katika mikono ya makaburu watu ambao waliwafanyia maovu mengi. Mwandishi anasema;
“Lazima tupambane nao, na huu ni wakati pekee wa kuonyesha moyo wetu. Uoga hauwezi kutufanya tukubali kuwa mateka wa utawala haramu kama huu. Lazima tushinde” (Uk 93).
Vilevile tunaona jinsi Joram alivyokuwa jasiri kujibu swali aliloulizwa na Nuru kuhusu wizi alioufanya katika City drive bank. Joram alimjibu kwa ujasiri kuwa ameiba ila ameiba waziwazi tofauti na wenzake wanaoiba kwa siri na kufanya maendeleo ambayo hayaendani na mishahara yao. Mwandishi anasema;
“Huoni watu wenye mishahara ya shilingi elfu mbili wanavyojenga majumba ya mamilioni? Unadhani wanazipata wapi bila wizi? Tofauti yangu na wao ni kwamba mimi nimeiba machomacho, wao wanaiba kusirisiri. Mwizi ni mwizi tu” (uk 65).
Pia tunaona jinsi Nuru alivyoonesha ujasiri wake kwa kumuua Iron Von baada ya kumteka Nuru kwa nia ya kutimiza haja yake ya mapenzi, na kumwonesha alipo Joram na baada ya hapo amuue. Mwandishi anasema;
“Pokea chako, muuaji mkubwa” Nuru alinong’ona na akiifyatua bastola” (uk 159).
Hivyo, katika jamii yetu suala la ujasiri linajidhihirisha wazi kwani tunaona jinsi baadhi ya wanajamii walivyofanya matendo ya kijasiri katika kufichua ubadhilifu unaofanywa na watu wachache katika jamii ili kuikomboa jamii yao au nchi yao.
2.1.4 Uzalendo
Kwa mujibu wa TUKI (katajwa) uzalendo ni hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake. Katika kuchambua riwaya hii ya “Tutarudi roho zetu?” Suala la uzalendo limejipambanua vyema, mwandishi anathibitisha suala la uzalendo kwa kuwatumia wahusika wake Joram na Nuru ambao wameonesha uzalendo mkubwa kwa kuipenda nchi yao kwa dhati hadi kuchukua jukumu la kupambana na kuwaua makaburu ambao wamewatesa kwa muda mrefu kwa lengo la kuikomboa nchi yao kutoka katika mikono ya makaburu. Mwandishi anasema;
“Nadhani inatosha. Wanakufa wenye hatia na wasio na hatia sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya mwisho kulipua huo mtambo” (Uk 34).
Vilevile, suala la uzalendo linajidhihirisha kwa mhusika inspecta Kombora. Matendo yake yalikuwa ya kizalendo kwa nchi yake kwani alitumia mbinu mbalimbali ya kupambana na kuwaondoa makaburu wa Afrika Kusini. Mwandishi anasema;
“Kombora alikuwa mwenyeji, alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo ambao ulifanywa kwa siri kubwa mkutano ambao ulijumuisha watu wenye sura mbalimbali, umri mbali mbali, viwango mbali mbali vya elimu wote wakiwa na dhamira moja” (uk 94).
Pia, Inspecta Kombora amedhihirisha uzalendo pale ambapo aliamua kubaki ofisini baada ya wenzake kuondoka na kwenda kujumuika na familia zao hadi dakika ya mwisho na kushindwa kwenda kujumuika na familia yake ili aweze kuona nini kitatokea. Aliamua kukubaliana na tendo lolote ambalo lingetokea pale. Kwani kutoka muda mfupi uliopita walikuwa tayari wameshapata taarifa kutoka katika kibarua kilichokutwa ikulu kuwa baada ya masaa 3 kungetokea mlipuko katika maeneo hayo. Mwandishi anasema;
“Alikuwa ameamua lolote ambalo lingetukia, limkute katika ofisi yake” (Uk 171).
Katika jamii zetu suala hili la uzalendo linajidhihirisha wazi kwani tunaona jinsi baadhi ya viongozi wanavyojitoa katika nchi hii kwa namna moja au nyingine. Kwa mfano, tunaona baadhi ya viongozi wa kisiasa walivyoonesha uzalendo katika nchi yao kwa kukataa kulipwa hela za ziada au posho za vikao kwa kuona kuwa siyo haki yao bali ni ubadhilifu na kuwanyonya wananchi.
2.1.5Ubaguzi wa rangi
Ubaguzi wa rangi ni ile hali au kitendo cha kuwaweka watu katika makundi kutokana na rangi zao kwa ajili ya kutoa huduma tofauti tofauti kulingana na rangi zao. (https://en.wikipedia.org/wiki/Racial_discrimination).Suala la ubaguzi wa rangi limejitokeza katika riwaya hii ambapo inaelezwa kuwa watu wa rangi nyeusi wanatazamwa kuwa ni watu wenye fikra ndogo, wasiokuwa na akili ambao hawawezi kuleta maendeleo yoyote zaidi ya mtu mweupe. Na pia wanathubutu kusema kuwa ngozi nyeusi ni dalili ya laana ambapo mtu huyu mweupe ndiye anaonekana mwenye akili. Mwandishi anasema;
“Ngozi nyeusi ni dalili ya laana. Nywele fupi nidalili ya akili ndogo. Bila hekima uongozi wa mtu mweupe Afrika ingekuwa bado gizani, na endapo ataondoka mtu mweupe giza litarudi”(uk 104).
2.2 Migogoro
Kwa mujibu wa TUKI(katajwa)wanasema kuwa migogoro ni hali ya kutofautiana baina ya pande mbili au zaidi, wanasema migogoro inaweza kuwa ya familia, matabaka ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Katika riwaya hii imejitokeza migogoro tofautitofauti kama ifuatavyo:
2.2.1 Mgogoro kati ya makaburu (wazungu) na watu weusi
Mgogoro huu ulitokea wakati watu weupe (makaburu) wakiwadharau watu weusi na kuwaona si chochote, watu duni pamoja na kuwafanyia maovu mengi. Mgogoro umesababishwa na tofauti za rangi na kupelekea uadui mkubwa kati ya watu weupe na weusi. Ubaguzi huu wa rangi ambao ulisababishwa na siasa ya magharibi ndio uliopelekea mapigano kati ya watu weupe na weusi na kupelekea vifo hasa kwa watu weusi. Yote haya yamejidhihirisha kwa mawanda mapana katika riwaya hii (uk 104).
2.2.2 Mgogoro kati ya Inspecta Kombora na Joram Kiango
Mgogoro huu ulitokea pale ambapo Inspecta alipomfuata Joram na kumsihi arudi katika kazi yake ya upelelezi. Na Joram kukataa ombi hilo. Suluhisho ni pale ambapo Inspecta Kombora aliamua kuondoka (uk 19).
2.2.3 Mgogoro kati ya Nuru na Joram
Mgogoro huu ulitokea wakati Nuru akimbembeleza sana Joram arudishe pesa alizoiba kutoka katika Benki ya City Drive. Pamoja na kwenda kuomba msamaha ubalozini na Joram kutokubaliana naye kwa wakati ule. Suluhisho ni pale ambapo baadae alikubali kurudisha pesa zile Benki baada ya kulipua mji wa Soweto uliopo Afrika kusini japokuwa hakupenda kwenda kuomba msamaha ubalozini (uk 66).
2.2.4 Mgogoro wa nafsi
Huu ni mgogoro unaojitokeza baina ya mtu mmoja ndani ya nafsi yake. Katika riwaya hii mgogoro wa nafsi umejitokeza kwa Joram pale ambapo alitoka kuongea na Chonde na baadaye akaanza kujiuliza kuwa huyu ni mtu wa aina gani na amelijua vipi jina langu? (uk 25).
2.3 Ujumbe
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa)ujumbe ni kitu ambacho mwandishi hudhamiria kumtumia msomaji, kila kazi ya fasihi hubeba ujumbe ambao msanii hutaka umfikie msomaji wake.Katika riwaya ya hii kuna ujumbe wa aina tofauti tofauti uliojitokeza kama ifuatavyo:
2.3.1Kujitoa mhanga ni njia mojawapo ya kupata ukombozi katika harakati za kudai uhuru mwanamke hapaswi kuachwa nyuma kwani ana mchango mkubwa ambao unapelekea ukombozi.
2.3.2 Ujasiri ni muhimu katika harakati zote za ukombozi.
2.3.3Uzalendo ni muhimu katika harakati za kutafuta ukombozi, mwananchi lazima awe mzalendo na nchi yake.
2.3.4Ubaguzi wa rangi ni kikwazo ambacho kinapelekea uadui mkubwa baina ya nchi na nchi. Hivyo hatuna budi kufuatilia mbali ubaguzi wa rangi.
2.3.5 Katika harakati za kudai uhuru mwanamke mwanamke hapaswi kuachwa nyuma kwani ana mchango mkubwa ambao unapelekea ukombozi.
2.4Falsafa
Kwa mujibu wa Madumulla(katajwa)akimrejelea Msokile (2009) falsafa ni wazo ambalo mtu anaamini kuna ukweli fulani unaohusu maisha yake pamoja na maisha ya jamii.Katika riwaya ya hii mwandishi anaamini kuwa ili kufanikiwa katika suala zima la ukombozi ni lazima tujitoe mhanga tuwe na ujasiri pamoja na uzalendo kwa kile tunachotaka kukikomboa.
2.5Msimamo
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) ni mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii. Hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na ndiyo huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Katika riwaya hii mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha kuwa mtu kuwa na ujasiri, kujitoa mhanga pamoja na uzalendo ni silaha kuu katika kuleta ukombozi.
3.0 Hitimisho
Kwa ujumla riwaya hii ya “Tutarudi na Roho Zetu?”inaelezea namna nchi za mstari wa mbele zilivyoshikamana ili kupinga na kupambana na makaburu huko Afrika ya Kusini waliowatenda maovu watu weusi na kuwachukulia kama watu wasio na akili na hatimaye watu weusi kufanikiwa kuwashinda makuburu kutokana na juhudi kubwa zilizoongozwa na Joram Kiango.
4.0 Marejeo
Gazeti la Taifa Leo, (15-10-2015),Jumatano.
Kezilahabi, E. (1991), Mzingile,University of Dar es Salaam Press; Dar es Salaam.
Kezirahabi, E. (1990), Nagona, University of Dar es Salaam Press; Dar es Salaam.
Madumulla, S.J (2009), Riwaya ya Kiswahili, Nadharia,Historia na Misingi ya Uchunguzi. Mture Educational Puplishers Limited; Dar-es salaam.
Mikhail, G. (2008), Swahili Forum 15. United States International University; Nairobi.
Msokile, M. (1992) Kunga za Fasihi na lugha.Educational Publishers and Distributors, Limited; Dar es Salaam.
Mtobwa, B. (2008), Tutarudi na Roho Zetu?. East Africa Educational Publishers LTD; Dar es Salaam.
Ntarangwi, M. (2004), Uhakiki wa Kazi za Fasihi.
Samwel, M. na Wenzake (2013) Ushairi wa Kiswahili, Nadharia, Mifano na Muongozo kwa Walimu wa Kiswahili.MEVELI Publishers; Dar es Salaam.
Senkoro, E.(1982), Fasihi. Press and Publicity Centre; Dar-es-Salaam.
TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press; Dar es Salaam.
Wamitila na Kyallo,W. (2003), Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia, Focus Publications; Nairobi.
www.en.wikipedia.org/wiki/Racial_discrimination 16:59 on 22nd Dec. 2015
www.merriam-webster.com/dictionary/sacrifice 17:15 on 22nd Dec. 2015
Mwl Maeda