08-13-2021, 05:54 AM
UTENZI WA FURAHA
Kwakowe Mola Wadudi,
Utenzi naabtadi,
Unipe kujitahidi,
Tenzi iwe kitabuni.
Safusafu beti hizi,
Nisitunge nisihizi,
Nipe yako maongozi,
Uliye wangu Manani.
Nishike palipo nibu,
Unifungue ububu,
Nandike yaso harabu,
Yawafae duniani.
Dunia utenzi huu,
Uwe breviari kuu,
Wazee na vitukuu,
Uwaache furahani.
Utenzi wa manukato,
Kwa wakubwa na watoto,
Na beti zenye mnato,
Viwashike akilini.
Mabeti jozi kwa jozi,
Wazaliwa na wazazi,
Utungo huu kuhozi,
Wakautia thamani.
Ewe Mola wa Mbawazi,
Niongeze shinikizi,
Situnge ya uchokozi,
Nihasiri majirani.
Bali uwe yangu taa,
Nendapo njia kung’aa,
Hata chini nikikaa,
Nibaki mwako nuruni.
Pia nina maombezi,
Kwa mama yangu mzazi,
Mlaze basi mwenyezi,
Palipo pako peponi.
Peponi awe mkazi,
Malaika watetezi,
Ndio wakawe walezi,
Mama awe farajani.
Nikakufuru wakati,
Nikwone Wabarakati,
Wewe nduli kama nyati,
Nakuomba samahani.
Nisamehe Mola wangu,
Kwa hasira za uchungu,
Msiba wa mama yangu,
Mungu nikuone nyani.
Nimetambua najua,
Muumba na muumbua,
Utoaye na kutwaa,
Anayekupinga nani?
Miaka kumi kutimu,
Tangu awe marehemu,
Mama yangu Mariamu,
Namuweka utenzini.
Mola una maajabu,
Mambo unayaratibu,
Pamwe nilipata tabu,
Ukanikuza thamani.
Hivihivi ukiwani,
Ukanitia shuleni,
Nikafika na chuoni,
Chuo hapo Mlimani.
Ukiwani nikasoma,
Ukanipa na uzima,
Pia marafiki wema,
Nikabaki farajani.
Yupo Ntambi wa Stella,
Wa Kagera si Mwela,
Naye huyu sikulala,
Tulikesha darasani.
Ni mapenzi nikahozi,
Yakanifuta machozi,
Nikazimaliza kozi,
Kufundishwa darasani.
Umenituza kipaji,
Kutunga nikawa gwiji,
Ni rahisi kama uji,
Nikorogavyo mekoni.
Kipaji chaninyanyua,
Sasa ninainukia,
Nawe wanongoza njia,
Wengine hunitamani.
Huniuliza maswali,
Naipataje sahali,
Nikatunga bulibuli,
Pasi sumbuo kichwani?
Hata mwenyewe sijui,
Ni kama maruirui,
Hii fani sikatai,
Naiweza kama nini.
Japo sipendi kutuna,
None wengine hawana,
Ukweli wanauona,
Wanafumbia moyoni.
Dibaji naterekeza,
Kueleza nakatiza,
Nisijefanya ajiza,
Wanione majununi.
Naikabili furaha,
Kinyume chake karaha,
Hapa sileti mizaha,
Naiweka upeoni.
Furaha ijapo kwetu,
Sisi hujiona watu,
Huwa sio mali kwetu,
Inapokuja huzuni.
Furaha kama yakuti,
Kuipata ni bahati,
Tasifu Wabarakati,
Kumuweka masifuni.
Pia ni kama feruzi,
Kuwa nayo ni ujuzi,
Shida hazifululizi,
Hiki ni kitu thamani.
Tena ni kama dhahabu,
Inayokimbiza tabu,
Yende mbali jitanibu,
Furaha kwetu jubuni.
Kama maua waridi,
Harufuye maridadi,
Tutamani ikarudi
Iendapo ghaibuni.
Twaona mithili riha,
Harufu iso karaha,
Katu huwezi kuhaha,
Ikufikapo moyoni.
Furaha ya uzeeni,
Tajiona utotoni,
Ukumbuke ujanani,
Ubakie kushaini.
Furaha inahuisha,
Kicho kufa hufufusha,
Maisha kuyarefusha,
Ifananishwe na nini?
Kila mja duniani,
Furaha huitamani,
Hutafuta masokoni,
Ikae mwao fukoni.
Husakwa madarasani,
Kwa kisomo vitabuni,
Maandiko kurasani,
Furaha kuipateni.
Mafyatu majalalani,
Ni watupu maungoni,
Kucha huchakura chini,
Furaha kuishikeni.
Hutafutwa migodini,
Waja huzama shimoni,
Huko huwa hatarini,
Na kujiweka kufani.
Pia huko mashambani,
Mkulima na mpini,
Kusiha na mavunoni,
Furaha maandamoni.
Hata na mama ntilie,
Chakula ajipikie,
Walaji awauzie,
Furaha iwe fukoni.
Machinga barabarani,
Kutwa hushinda juani,
Na bidhaa mikononi,
Furaha kuiauni.
Cherehani yu kitini,
Habanduki mashononi,
Anachowaza moyoni,
Furaha iwe kichwani.
Waashi nao sawia,
Hujenga na kubomoa,
Huku wakitia nia,
Watulie furahani.
Wahunzi vyuma hufua,
Bidhaa kujiundia,
Haja yao hutambua,
Furaha mwao nyumbani.
Mangi naye yu gengeni,
Haondoki mauzoni,
Hung’ang’ana dirishani,
Furaha kuitamani.
Na wagonjwa vitandani,
Ijapo huwa tabani,
Wanamuomba Manani,
Wabakie furahani.
Waumini kanisani,
Na kule misikitini,
Magoti altareni,
Mola raha kuwapeni.
Waandishi kama mimi,
Nasi japo hatuvumi,
Lakini tunajihami,
Tusitoke furahani.
Mapadiri, mashemasi,
Askofu, makasisi,
Furaha wakaihisi,
Haja yao fuadini.
Wafanyakazi nyumbani,
Kutwa apo shughulini,
Halali kibaruani,
Lengo awe furahani.
Walinzi huliwa mbu,
Ila yao kumbukumbu,
Wakiyafanya malumbu,
Furaha iwe nguoni.
Rais naye kitini,
Kutwa huomba Manani,
Furaha iwe nchini,
Pia na mwake moyoni.
Makatibu na wabunge,
Na hao wasijitenge,
Bila raha wasiringe,
Japo washinda bungeni.
Furaha twaitafuta,
Ni tunu hii kupata,
Kiu zetu kuzikata,
Tuondoke matatani.
Pasi furaha sumbuko,
Tusombwe na nung’uniko,
Tubadili miondoko,
Twende kwa mwendo wa nyani.
Pasi furaha kilio,
Hakuna tena pumuo,
Na maisha huwa sio,
Kwetu huwa msibani.
Furaha rafiki shibe,
Tule matumbo tuzibe,
Kingine tukakibebe,
Twende kula majiani.
Tena nduguye sherehe,
Tuimbe tusherekehe,
Zile nyimbo za kihehe,
Kadhalika za wangoni.
Swahiba wake mapenzi,
Waja mapenzi twaenzi,
Kama kidonda na nzi,
Abakivyo furahani.
Tena jiraniye pesa,
Paso pesa anasusa,
Pesa huja kutakasa,
Palipo jaa huzuni.
Amani ni wake mbasi,
Bila amani kuhisi,
Furaha huwa tatasi,
Ikimbiavyo vitani.
Huketi pamwe malazi,
Si kulala kwenye zizi,
Furaha kamwe kuhozi,
Hapati hiyo zizini.
Pia huketi na vazi,
Ikiwa hatupendezi,
na mwili husitirizi,
twaondokewa jubuni.
Na tuwe na marafiki,
Wema sio wazandiki,
Furaha haiondoki,
Daima huwa moyoni.
Pasipo na maonevu,
Na kuitwa mpumbavu,
Hata ukiwa shupavu,
Hufurahi dharauni.
Haitadumu furaha,
Popote penye karaha,
Tajionea udhiha,
Tahamia kwa jirani.
Furaha penye shutumu,
Hapo huwa marehemu,
Ama penye madhulumu,
Na hapo huwa tabani.
Furaha hudhoofika,
Pa vijembe na dhihaka,
Njaa na kuhangaika,
Raha wenda ghaibuni.
Tuondokewapo ndugu,
Hapo huota magugu,
Mioyo huzuka sugu,
Furaha huwa kandoni.
Furaha kwa tegemezi,
Kuwa nayo huiwezi,
Upewe kwa simangizi,
Utapata raha gani?
Furaha na matatizo,
Hawamalizi mizozo,
Hutofauti mawazo,
Hawa kamwe wapatani
Furaha na tafrani,
Mithili moto na kuni,
Furaha huwa kinywani,
Humezwa na tafrani.
Furaha penye mabavu,
Ja samaki nchi kavu,
Kadhalika na pa wivu,
Haiwi pumzikoni.
Fura ni kitu bora,
Kizidicho njema sura,
Hupendwa kila idara,
Kila rika kila dini.
Furaha kila kiumbe,
Mola wake amuombe,
Hawezi huyu atambe,
Sipo kuwa furahani.
Furaha zama na zama,
Ndo kilicho kitu chema,
Ndanimwe ikikuhama,
Bora wende kaburini.
Kukikosa kitu hiki,
Mwenyewe tajidhihaki,
Ujione hujitaki,
Vile hauna thamani.
Penye chuki na madhila,
Furaha hapo pahala,
Kamwe hawezi kulala,
Ijapopita njiani.
Na pale penye izara,
Na maudhi ya kukera,
Hata kwa mja sogora,
Raha huwa hatarini.
Furaha kwa masikini,
Hata atie makini,
Na hapo nikabaini,
Furaha huwa kufani.
Kadhalika penye gubu,
Furaha hupata tabu,
Kuishi haijaribu,
Huishia maozoni.
Penye ghiliba na wizi,
Uchawi na uchochezi,
Pa maudhi na machozi,
Furaha yenda zikoni.
Furaha pasi uzazi,
Uzae Juma na Rozi,
Kuzaa kuwe tatizi,
Furaha hauioni.
Furaha mali ghalani,
Sio kuwa utumwani,
Waja wakuone nyani,
Furaha hapo shakani.
Furaha penye kushindwa,
Na moyowe ukadundwa,
Hofu woga ukapandwa,
Utaambua huzuni.
Furaha mali ya Mungu,
Pasi yeye ni uchungu,
Hata uwe kwa mzungu,
Sifanye ya ushetani.
Shetani yeye balozi,
Anayeunda machozi,
Dhiki na maangamizi,
Kaviweka duniani.
Taifa bila furufu,
Hulega kama mkufu,
Hilo taifa dhaifu,
Hata liwe uzunguni.
Dunia bila jubuni,
Tungekuwa kama mbuni,
au kwale wa nyikani,
tubakie mawindoni.
Koo bila kitu hiki,
Kamwe wasingeshiriki,
Vikao kuvimiliki,
Wabaki matenganoni.
Familia nayo pia,
Bila raha ni mdhia,
Waja wangeomba njia,
Ukimbizi majiani.
Darasa bila furaha,
Wanafunzi tungehaha,
Kufunzwa kwetu fadhaha,
Tenge pata raha gani.
Watoto bila jubuni,
Nini wangekithamini?
Kuishi pao nyumbani,
Kamwe wasingetamani.
Furaha hushika dira,
Tunapotaka kugura,
Tukikosa twazurura,
Hakwendeki mahalani.
Na wapishi majikoni,
Wao huchochea kuni,
Chakula kupakuani,
Chenye furaha yakini.
Lolote lenye mwenendo,
Kadhalika na matendo,
Yaliyo yetu mapendo,
Litufurahi moyoni.
Wengine hutaka ndoa,
Na wengine hukia,
Hao walitambua,
I wapi raha yakini.
Mtunzi Filieda Sanga
Mabibo Dsm
0753738704
Kwakowe Mola Wadudi,
Utenzi naabtadi,
Unipe kujitahidi,
Tenzi iwe kitabuni.
Safusafu beti hizi,
Nisitunge nisihizi,
Nipe yako maongozi,
Uliye wangu Manani.
Nishike palipo nibu,
Unifungue ububu,
Nandike yaso harabu,
Yawafae duniani.
Dunia utenzi huu,
Uwe breviari kuu,
Wazee na vitukuu,
Uwaache furahani.
Utenzi wa manukato,
Kwa wakubwa na watoto,
Na beti zenye mnato,
Viwashike akilini.
Mabeti jozi kwa jozi,
Wazaliwa na wazazi,
Utungo huu kuhozi,
Wakautia thamani.
Ewe Mola wa Mbawazi,
Niongeze shinikizi,
Situnge ya uchokozi,
Nihasiri majirani.
Bali uwe yangu taa,
Nendapo njia kung’aa,
Hata chini nikikaa,
Nibaki mwako nuruni.
Pia nina maombezi,
Kwa mama yangu mzazi,
Mlaze basi mwenyezi,
Palipo pako peponi.
Peponi awe mkazi,
Malaika watetezi,
Ndio wakawe walezi,
Mama awe farajani.
Nikakufuru wakati,
Nikwone Wabarakati,
Wewe nduli kama nyati,
Nakuomba samahani.
Nisamehe Mola wangu,
Kwa hasira za uchungu,
Msiba wa mama yangu,
Mungu nikuone nyani.
Nimetambua najua,
Muumba na muumbua,
Utoaye na kutwaa,
Anayekupinga nani?
Miaka kumi kutimu,
Tangu awe marehemu,
Mama yangu Mariamu,
Namuweka utenzini.
Mola una maajabu,
Mambo unayaratibu,
Pamwe nilipata tabu,
Ukanikuza thamani.
Hivihivi ukiwani,
Ukanitia shuleni,
Nikafika na chuoni,
Chuo hapo Mlimani.
Ukiwani nikasoma,
Ukanipa na uzima,
Pia marafiki wema,
Nikabaki farajani.
Yupo Ntambi wa Stella,
Wa Kagera si Mwela,
Naye huyu sikulala,
Tulikesha darasani.
Ni mapenzi nikahozi,
Yakanifuta machozi,
Nikazimaliza kozi,
Kufundishwa darasani.
Umenituza kipaji,
Kutunga nikawa gwiji,
Ni rahisi kama uji,
Nikorogavyo mekoni.
Kipaji chaninyanyua,
Sasa ninainukia,
Nawe wanongoza njia,
Wengine hunitamani.
Huniuliza maswali,
Naipataje sahali,
Nikatunga bulibuli,
Pasi sumbuo kichwani?
Hata mwenyewe sijui,
Ni kama maruirui,
Hii fani sikatai,
Naiweza kama nini.
Japo sipendi kutuna,
None wengine hawana,
Ukweli wanauona,
Wanafumbia moyoni.
Dibaji naterekeza,
Kueleza nakatiza,
Nisijefanya ajiza,
Wanione majununi.
Naikabili furaha,
Kinyume chake karaha,
Hapa sileti mizaha,
Naiweka upeoni.
Furaha ijapo kwetu,
Sisi hujiona watu,
Huwa sio mali kwetu,
Inapokuja huzuni.
Furaha kama yakuti,
Kuipata ni bahati,
Tasifu Wabarakati,
Kumuweka masifuni.
Pia ni kama feruzi,
Kuwa nayo ni ujuzi,
Shida hazifululizi,
Hiki ni kitu thamani.
Tena ni kama dhahabu,
Inayokimbiza tabu,
Yende mbali jitanibu,
Furaha kwetu jubuni.
Kama maua waridi,
Harufuye maridadi,
Tutamani ikarudi
Iendapo ghaibuni.
Twaona mithili riha,
Harufu iso karaha,
Katu huwezi kuhaha,
Ikufikapo moyoni.
Furaha ya uzeeni,
Tajiona utotoni,
Ukumbuke ujanani,
Ubakie kushaini.
Furaha inahuisha,
Kicho kufa hufufusha,
Maisha kuyarefusha,
Ifananishwe na nini?
Kila mja duniani,
Furaha huitamani,
Hutafuta masokoni,
Ikae mwao fukoni.
Husakwa madarasani,
Kwa kisomo vitabuni,
Maandiko kurasani,
Furaha kuipateni.
Mafyatu majalalani,
Ni watupu maungoni,
Kucha huchakura chini,
Furaha kuishikeni.
Hutafutwa migodini,
Waja huzama shimoni,
Huko huwa hatarini,
Na kujiweka kufani.
Pia huko mashambani,
Mkulima na mpini,
Kusiha na mavunoni,
Furaha maandamoni.
Hata na mama ntilie,
Chakula ajipikie,
Walaji awauzie,
Furaha iwe fukoni.
Machinga barabarani,
Kutwa hushinda juani,
Na bidhaa mikononi,
Furaha kuiauni.
Cherehani yu kitini,
Habanduki mashononi,
Anachowaza moyoni,
Furaha iwe kichwani.
Waashi nao sawia,
Hujenga na kubomoa,
Huku wakitia nia,
Watulie furahani.
Wahunzi vyuma hufua,
Bidhaa kujiundia,
Haja yao hutambua,
Furaha mwao nyumbani.
Mangi naye yu gengeni,
Haondoki mauzoni,
Hung’ang’ana dirishani,
Furaha kuitamani.
Na wagonjwa vitandani,
Ijapo huwa tabani,
Wanamuomba Manani,
Wabakie furahani.
Waumini kanisani,
Na kule misikitini,
Magoti altareni,
Mola raha kuwapeni.
Waandishi kama mimi,
Nasi japo hatuvumi,
Lakini tunajihami,
Tusitoke furahani.
Mapadiri, mashemasi,
Askofu, makasisi,
Furaha wakaihisi,
Haja yao fuadini.
Wafanyakazi nyumbani,
Kutwa apo shughulini,
Halali kibaruani,
Lengo awe furahani.
Walinzi huliwa mbu,
Ila yao kumbukumbu,
Wakiyafanya malumbu,
Furaha iwe nguoni.
Rais naye kitini,
Kutwa huomba Manani,
Furaha iwe nchini,
Pia na mwake moyoni.
Makatibu na wabunge,
Na hao wasijitenge,
Bila raha wasiringe,
Japo washinda bungeni.
Furaha twaitafuta,
Ni tunu hii kupata,
Kiu zetu kuzikata,
Tuondoke matatani.
Pasi furaha sumbuko,
Tusombwe na nung’uniko,
Tubadili miondoko,
Twende kwa mwendo wa nyani.
Pasi furaha kilio,
Hakuna tena pumuo,
Na maisha huwa sio,
Kwetu huwa msibani.
Furaha rafiki shibe,
Tule matumbo tuzibe,
Kingine tukakibebe,
Twende kula majiani.
Tena nduguye sherehe,
Tuimbe tusherekehe,
Zile nyimbo za kihehe,
Kadhalika za wangoni.
Swahiba wake mapenzi,
Waja mapenzi twaenzi,
Kama kidonda na nzi,
Abakivyo furahani.
Tena jiraniye pesa,
Paso pesa anasusa,
Pesa huja kutakasa,
Palipo jaa huzuni.
Amani ni wake mbasi,
Bila amani kuhisi,
Furaha huwa tatasi,
Ikimbiavyo vitani.
Huketi pamwe malazi,
Si kulala kwenye zizi,
Furaha kamwe kuhozi,
Hapati hiyo zizini.
Pia huketi na vazi,
Ikiwa hatupendezi,
na mwili husitirizi,
twaondokewa jubuni.
Na tuwe na marafiki,
Wema sio wazandiki,
Furaha haiondoki,
Daima huwa moyoni.
Pasipo na maonevu,
Na kuitwa mpumbavu,
Hata ukiwa shupavu,
Hufurahi dharauni.
Haitadumu furaha,
Popote penye karaha,
Tajionea udhiha,
Tahamia kwa jirani.
Furaha penye shutumu,
Hapo huwa marehemu,
Ama penye madhulumu,
Na hapo huwa tabani.
Furaha hudhoofika,
Pa vijembe na dhihaka,
Njaa na kuhangaika,
Raha wenda ghaibuni.
Tuondokewapo ndugu,
Hapo huota magugu,
Mioyo huzuka sugu,
Furaha huwa kandoni.
Furaha kwa tegemezi,
Kuwa nayo huiwezi,
Upewe kwa simangizi,
Utapata raha gani?
Furaha na matatizo,
Hawamalizi mizozo,
Hutofauti mawazo,
Hawa kamwe wapatani
Furaha na tafrani,
Mithili moto na kuni,
Furaha huwa kinywani,
Humezwa na tafrani.
Furaha penye mabavu,
Ja samaki nchi kavu,
Kadhalika na pa wivu,
Haiwi pumzikoni.
Fura ni kitu bora,
Kizidicho njema sura,
Hupendwa kila idara,
Kila rika kila dini.
Furaha kila kiumbe,
Mola wake amuombe,
Hawezi huyu atambe,
Sipo kuwa furahani.
Furaha zama na zama,
Ndo kilicho kitu chema,
Ndanimwe ikikuhama,
Bora wende kaburini.
Kukikosa kitu hiki,
Mwenyewe tajidhihaki,
Ujione hujitaki,
Vile hauna thamani.
Penye chuki na madhila,
Furaha hapo pahala,
Kamwe hawezi kulala,
Ijapopita njiani.
Na pale penye izara,
Na maudhi ya kukera,
Hata kwa mja sogora,
Raha huwa hatarini.
Furaha kwa masikini,
Hata atie makini,
Na hapo nikabaini,
Furaha huwa kufani.
Kadhalika penye gubu,
Furaha hupata tabu,
Kuishi haijaribu,
Huishia maozoni.
Penye ghiliba na wizi,
Uchawi na uchochezi,
Pa maudhi na machozi,
Furaha yenda zikoni.
Furaha pasi uzazi,
Uzae Juma na Rozi,
Kuzaa kuwe tatizi,
Furaha hauioni.
Furaha mali ghalani,
Sio kuwa utumwani,
Waja wakuone nyani,
Furaha hapo shakani.
Furaha penye kushindwa,
Na moyowe ukadundwa,
Hofu woga ukapandwa,
Utaambua huzuni.
Furaha mali ya Mungu,
Pasi yeye ni uchungu,
Hata uwe kwa mzungu,
Sifanye ya ushetani.
Shetani yeye balozi,
Anayeunda machozi,
Dhiki na maangamizi,
Kaviweka duniani.
Taifa bila furufu,
Hulega kama mkufu,
Hilo taifa dhaifu,
Hata liwe uzunguni.
Dunia bila jubuni,
Tungekuwa kama mbuni,
au kwale wa nyikani,
tubakie mawindoni.
Koo bila kitu hiki,
Kamwe wasingeshiriki,
Vikao kuvimiliki,
Wabaki matenganoni.
Familia nayo pia,
Bila raha ni mdhia,
Waja wangeomba njia,
Ukimbizi majiani.
Darasa bila furaha,
Wanafunzi tungehaha,
Kufunzwa kwetu fadhaha,
Tenge pata raha gani.
Watoto bila jubuni,
Nini wangekithamini?
Kuishi pao nyumbani,
Kamwe wasingetamani.
Furaha hushika dira,
Tunapotaka kugura,
Tukikosa twazurura,
Hakwendeki mahalani.
Na wapishi majikoni,
Wao huchochea kuni,
Chakula kupakuani,
Chenye furaha yakini.
Lolote lenye mwenendo,
Kadhalika na matendo,
Yaliyo yetu mapendo,
Litufurahi moyoni.
Wengine hutaka ndoa,
Na wengine hukia,
Hao walitambua,
I wapi raha yakini.
Mtunzi Filieda Sanga
Mabibo Dsm
0753738704
Mwl Maeda