06-29-2021, 09:28 PM (This post was last modified: 06-29-2021, 09:38 PM by MwlMaeda.)
DIBAJI YA TOLEO LA KWANZA LA KAMUSI YA KISWAHILI-KIINGEREZA
Kamusi hii ya Kiswahili-Kiingereza ina historia ndefu. Wazo la kutunga kamusi hii ilianzishwa mwaka 1964 na Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili (ambacho kuanzia mwaka 1972 kilijulikana kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili). Wazo hili lilibuniwa wakati wa enzi ya Profesa Wilfred H.Whitely, ambaye wakati huo alikuwa ndiye Mkurugenzi wa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili, ikiwa ni miaka 25 baada ya kuchapishwa kwa kamusi ya Johnson ijulikanayo kama Standard Swahili-English Dictionary (1939). Kazi ya utunzi wa kamusi mpya ilianza baada ya shirika lijulikanalo kama Calouste Gulbenkian Foundation kutoa msaada wa pesa kwa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 1964 hadi Octoba 1967 ili kukiwezesha chuo kumwajiri mchunguzi atakayeweza kuifanya kazi hiyo.
Katika kutekeleza azma hiyo, Chuo kilimwazima Bwana J.A.Tejani kutoka Wizara ya Elimu Zanzibar na kumwajiri kama Mchunguzi. Bwana Tejani wakati huo alikuwa na shahada ya B.A. katika lugha za Kiarabu na Kiajemi ya Chuo Kikuu cha London, na alikuwa pia na ujuzi katika lugha za Kigujarati, Kiurdu na Kiswahili. Ilipangwa kuwa Mchunguzi Tejani angekuwa anasaidiwa na Mchunguzi Msaidizi na angeshauriwa na Miss M.A. Bryan wa School of Oriental and African Studies (SOAS), London Profesa E. Dammann wa Marbury na Profesa D.A. Olderogge wa Leningrad.
Bwana Tejani alipokuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili kati ya mwaka 1968 na 1969, aliendelea kuifanya kazi hii hadi mwaka 1970 alipoikabidhi kwa Mkurugenzi mpya wa Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili, Bwana George Mhina. Mwaka 1967, kabla ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi mpya, Baraza la Kiswahili la Taifa lilikielekeza Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili kuwa kamusi inayopaswa kuandaliwa mwanzo iwe kamusi ya Kiswahili-Kiswahili na wala sio kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Kwa hiyo mwaka 1970 kazi ya kwanza ya Mkurugenzi mpya, Bwana George Mhina, ilikuwa ni kuhakikisha kuwa vitomeo vyote vilivyomo katika kamusi ya Kiswahili-Kiingereza iliyoanzishwa na Tejani vinatafsiriwa upya katika Kiswahili. Mswada wa kamusi ya Kiswahili-Kiswahili ulikamilika Juni 4, 1978 na kamusi ikatoka mwaka 1981.
Mwaka 1972, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ilimpata mtaalamu wa kamusi kutoka Poland, Profesa Rajmund Ohly. Kwa kuanzia profesa huyu alipewa kazi ya kutunga kamusi ya Kiingereza-Kiswahili. Hata hivyo, mwaka 1975, Taasisi ilipounda jopo la wataalamu wa kamusi ili kukamilisha kazi ya kutunga kamusi ya Kiswahili-Kiswahili, Profesa Ohly alisitisha kazi ya kutunga kamusi ya Kiingereza-Kiswahili na kujiunga na jopo la kamusi ya Kiswahili-Kiswahili.
Baada ya kazi ya kutunga kamusi ya Kiswahili-Kiswahili kukamilika mwaka 1978, wachunguzi katika Sehemu ya Kamusi walirejelea kazi ya kutunga kamusi ya Kiingereza-Kiswahili aliyokuwa ameianza Profesa Ohly. Kamusi hiyo ilikamilika na kuchapishwa Desemba , 1996.
Baada ya utunzi wa kamusi za Kiswahili-Kiswahili na Kiingereza-Kiswahili kukamilika na miswada kuchapishwa, Sehemu ya Kamusi ya TUKI ilipata nafasi ya kuurejelea tena mradi wa Kiswahili-Kiingereza uliokuwa umeahirishwa tangu mwaka 1967. Kazi ya kuandaa mswada wa Kamusi hii ilianza rasmi Januari 1997 na jopo la kwanza lililopitia herufi A na B liliketi Machi 1997. Katika kuandaa kamusi ya Kiswahili-Kiingereza, wataalamu wa Sehemu ya Kamusi hawakutegemea kadi za maneno zilizotayarishwa na Bwana Tejani kama msingi wa kupatia vidahizo, bali walitegemea mswada wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu ambao wakati wa udurusu wake uliongezewa maneno mapya kutoka Kenya na Tanzania.
Utayarishaji wa mswada wa kamusi hii ulipitia hatua mbalimbali na kufanyiwa vikao vya jopo na vya uhariri nje ya kituo cha kazi ili kuharakisha ukamilishaji wake. Vikao hivyo vilifanyika huko Kibaha (1997), Moshi (Agosti, 1999), Morogoro (Juni, 2000), Tanga (Septemba, 2000) na Dar-es-Salaam (Desemba, 2000). Wanajopo walioshiriki katika utayarishaji wa muswada na kushiriki katika vikao vya jopo ni Profesa James S. Mdee, Profesa Hermus J. Mwansoko, Dkt. Albina R. Chuwa, Dkt. Eliezer K.F. Chiduo, Dkt. John G. Kiango na Dkt. Zubeida N. Tumbo-Masabo. Tunapenda pia kumtaja Dkt. George Mrikaria, kwa mchango alioutoa katika kazi ya uhariri wa mwisho wa kazi hii, na Bi Eiko Kimura wa ubalozi wa Japani kwa kutuunganisha na wanataaluma wa Chama cha Japan cha Taaluma za Kiafrika ambao wamechangia katika mradi huu.
Wakati wa harakati za utayarishaji wa kamusi hii, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili iliweza pia kuwashirikisha wazawa wa lugha ya Kiingereza katika hatua mbalimbali za uhariri. Tunapenda kutambua ushirikiano na mchango mzuri katika uhariri
uliofanywa na Mabwana Richard Mabala na Christopher Elkington. Tunapenda kutambua ushirikianao na mchango tulioupata kutoka kwa watu na makundi mbalimbali. Kwa kuwa hatuwezi kuwataja wote kwa majina, tunapenda kutoa
shukrani zetu za dhati kwa wote waliohusika. Hata hivyo, hatuna budi kutoa shukrani za pekee kwa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, hususan kwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, Profesa Matthew L. Luhanga, ambaye pamoja na timu yake ya utawala wa Chuo, alihakikisha kuwa hatukwami katika utekelezaji wa kazi hii. Tunapenda pia kuwashukuru wanafanyakazi wote wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ambao wameshiriki kwa namna mbalimbali katika kukamilisha kazi hii.
Mwisho hatuna budi kumtaja Mkurugenzi Mstaafu wa TUKI, Profesa S.A.K.Mlacha, kwa kufanikisha utungaji wa kamusi hii. Yeye ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa mradi huu tangu mwaka 1997. Taasisi inampongeza kwa jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha kamusi hii inachukua muda mfupi kukamilika. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili inapenda pia kuwashukuru wafadhili wetu waliotusaidia katika kuikamilisha kazi hii. Kwanza tunapenda kushukuru Shirika la Canadian Organization for Development in Education (CODE) East Africa, kwa kutupatia msaada wa karatasi. Pili, The Norwegian Council for Higher Education’s Programme for Development Research and Education (NUFU), kwa kutupatia kompyuta na kufadhili gharama za vikao vya jopo la kamusi. Tatu, Profesa Hino Shungya pamoja na wanataaluma na maprofesa wenzake wa Chama cha Japan cha Taaluma za Kiafrika na Kampuni ya uchapishaji ya Kijapan Kodansha Ltd, kwa michango yao waliyoitoa kwa moyo mkunjufu kwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ili kufanikisha uchapishaji wa kamusi hii. Michango yao imesaidia sana siyo tu katika kuikamilisha kamusi hii, bali pia katika kukienzi na kukiendeleza Kiswahili, na pia kuendeleza urafiki uliopo baina ya Tanzania na Japan. Kuchapishwa kwa kamusi hii kunakamilisha seti ya kamusi za Kiswahili. Kwa sasa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili imechapisha Kamusi ya Kiswahili Sanifu (1981), Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili (1996) na Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza(2001). Ni matumaini yetu kuwa kamusi zote tatu zitawanufaisha wasomaji wetu, na kuwa zitakuwa hazina bora ya lugha ya Kiswahili.