Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
HISTORIA YA USHAIRI WA KISWAHILI
#1
Imeandikwa na Kornelio G. Maanga 22/1/2015
A.G. GIBBE (1980) akimnukuu Shaaban Robert anasema kuwa; Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa nyimbo mashairi na tenzi zaidi ya kuwa ni sanaa ya vina ushairi unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Mulokozi na Kahigi (1982) wanasema ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu na fasaha na wenye muala, kwa lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maandishi au maundui ya wimbo ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kuelekeza tukio au hisia fuani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.
Hivyo basi tunaweza kusema kuwa ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi ikiwa na maana kuwa ushauri waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na ujumbe.
Ushairi wa Kiswahili ni ule ushairi unaotumia lugha ya Kiwahili, utamaduni wa waswahili, lugha ya picha na lugha ya sitiari na wenye mtiririko mzuri na mpangilio wa maneno fasaha ili kufikisha ujumbe kwa hadhira.
Ushairi wa Kiswahili una historia ndefu sana. Ushairi simulizi wa Waswahili unasemekana kwamba ulikuwapo tangu lugha ya Kiswahili ilipoanza kutumika. Samweli na wenzake, (2013) wana wanukuu Mulokozi na Sengo kwa kusema kwamba si rahisi kueleza ni lini hasa ushairi simulizi wa waswahili ulianza. Hali hii inatokana na sababu kuu moja kwamba Wataalamu mbalimbali wamekuwa na mitizamo tofauti juu ya jambo hilo. Kama Swamweli na wenzake (2013) walivyomnukuu Knappert (1979) kuwa anadai ushairi andishi wa mwanzo wa Kiswahili ni Hamziya ulioandikwa mnamo mwaka (1652). Pia wamemnukuu Harries (1995) akidai ushairi wa mwanzo wa Kiswahili ni Tambuka(Tabuka) ulioandikwa mwaka 1728. Hata hivyo utafiti  wa Mulokozi na Sengo unabainisha kwamba huenda wote wawili (Knappert na Harries) wamekosea na kuwa ushiri andishi wa mwanzo  wa Kiswahili umekuwapo tangu wa Fumo Liyongo ambaye anaaminika kuishi  karne ya 13 huko Pate katika pwani ya Kenya. Aidha utafiti huo unabainisha ushairi andishi wa mwanzo wa kiswahiili ni “Swifa kwa mwana wa Manga” unaojulikana pia kama “Tumsifu yanga” ambao unahusishwa moja kwa moja na Fumo Liyongo.
Tangu kuibuka kwa ushairi wa mwanzo wa Kiswahili hadi sasa ushairi huo umepitia historia ndefu sana na vipindi tofauti tofauti vya kihistoria. Tunaweza kuvigawa vipindi hivyo katika makundi makuu mawili; Kipindi cha kabla ya ukoloni na wakati wakati wa ukoloni. Kipindi cha kabla ya ukoloni tunaweza kukigawa katika makundi tofauti madogo madogo, kundi  la kwanza ni kipindi cha ujima, na kundi la pili ni kipindi cha Ustawi wa miji, Utamaduni na tawala za Waswahili.
Kipindi cha kwanza, cha Ujima kilidumu tungu binadamu alipopata Urazini na kutoka kwenye Uhayawani ikikadiriwa hadi mwaka 600. Inadaiwa kwamba binadamu anatokana na Sokwe na alipitia hatua mbalimbali hadi kufikia kuwa mtu kamili (Homo Sapiens). Kipindi cha ujima kilianza pale binadamu alipopata Urazini na kuanza kuishi kama mtu kamili baada ya kutoka katika hali hiyo ya usokwe. Katika hatua za awali za kipindi cha ujima, binadamu waliishi kwa uwindaji na ukusanyaji wa matunda. Taratibu binadamu alipiga hatua na kuanza kuyatawala mazingira yake na kuanza kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kazi ya kilimo katika kile kinachoitwa mapinduzi ya kilimo (Neolithic Revolution). Mpinduzi haya ya kilimo yalisababisha maendeleo makubwa katika maisha ya binadamu na binadamu sasa wakaanza kuishi pamoja.
Katika kipindi chote hiki cha ujima, mwanadamu alishaibua ushairi kama njia mojawapo ya kujiliwaza wakati wa kufanya kazi. Hakuna ushaidi kuwa katika kipindi hiki kulikuwa na kazi nyingine za fasihi bali ushaidi uliopo unaonesha kwamba hiki kilikuwa ni kipindi kilichotawaliwa na nyimbo za kazi. Hivyo ushairi wa kazi unachukuliwa kuwa ndiyo ushairi wa mwanzo kabisa. Mwanadamu aliimba nyimbo mbalimbali wakati wa shughuli mbalimbali alizozifanya.(E. Senkoro, 1988) anasema kuwa ushairi huu wa awali ambao ulijitokeza zaidi katika nyimbo za kazi. Uliathiri hisia za mwimbaji na kumsukuma kufanya kazi kwa dhati zaidi na kumsahaulisha ugumu wa kazi ile. Anaendelea kueleza kwamba jukumu hili la nyimbo la kufanya kazi ngumu na nzito ionekane. Kutokuwa na hatari yoyote ndilo linaloonesha nguvu ya ushairi na hata wataalamu wengine wameipa nguvu hii sifa ya UCHAWI na kusema kuwa ushairi umetokana na uchawi. Nyimbo za kazi ziliendelea kudumu kwa muda mrefu na hadi sasa ingawa kuna mabadiliko makubwa katika utanzu wa ushairi. Nyimbo za kazi (ushairi wa kazi) bado umeendelea kuwa sehemu muhimu ya ushauri wa Kiswahili.
Kipindi cha pili ni kipindi cha Ustawi wa miji, utamaduni na tawala za waswahili kilidumu takrbani miaka 600 hivi (kuanzia mwaka wa 900-1500BK (Baada ya Kristo). Kipindi hiki kilimalizwa na utawala wa Wareno.
Kipindi hiki kipindi cha ustawi wa miji, utamaduni na tawala za waswahili kilidumu kuanzia karne ya kumi na kumi na sita. Kama tulivyoeleza hapo awali, ushairi wa Kiswahili unatokana na ushairi simulizi wa Kibantu. Ushairi huu ulihusisha majigamo, tondozi, pembezaji, mbolezi, nyiso, chapuzo na nyimbo za kazi na kadhalika. Mulokozi na Sengo kama walivyonukuliwa na Swamweli na wenzake (2013) wanabainisha kwamba kipindi hiki kilitawaliwa na tungo zilizodaiwa kuwa za Fumo Liyongo. Kutokana na mapokeo tunaambiwa kwamba mshairi wa kale zaidi anayefahamika ni Fumo Liyongo, ambaye inasemekana kuwa aliishi maeneo ya Shaka Kipini na Pate huko pwani ya Kenya katika karne ya 13.
Ingawa inaaminika kuwa Lyongo aliishi kabla ya karne ya 16 lakini tungo zinazomhusu (zilizotungwa na wengine) ambazo tunazo ziliandikwa mwanzoni mwa karne ya 19. Tungo hizo ni Takhmisa ya Liyongo (Sayyid Abdallah bin Ali inyayokadiriwa iliandikwa 1800) na “Utenzi wa Fumo Liyongo” (Muhamadi Kijumwa 1913) hata hivyo, tungo  hizi za baadaye zilitokana na fasihi simulizi inayomuhusu Liyongo na iliyotungwa zama za Liyongo mwenyewe. Hivyo kwa kiasi fulani kimaudhui na kihisia zinaakisi kipindi 900-1500BK (kabla ya Kristo) tunachokizungumzia. Kwa hivyo, utendi wa Fumo Liyongo ndio utenzi wa kale zaidi katika tenzi tatu za kale (tenzi nyingine mblili ni
 
Utenzi wa Mwanakupona na utenzi wa Ali Inkishafi) ingawa umewekwa katika maandishi karne ya 20 Tazama (Mulokozi, 1999) Katika kitabu cha Tenzi Tatu za Kale.
Tungo za Fumo Liyongo zinahusu ustawi wa miji ya pwani, miji hiyo ni pamoja na Kilwa, Mombasa na Pate. Miji hii ilistawi kutokana na biashara ya bahari ya Hindi (Indian Ocean SlaveTrade) iliyoshamiri sana. Utendi wa Fumo Liyongo kwa mfano, unaelezea kuhusu kustawi kwa mji wa Pate alipoishi Liyongo. Utenzi huu ulitungwa kutokana na hadithi za kimapokeo kuhusu Fumo Liyongo miongoni ya waswahili. Hata hivyo masimulizi ya maisha ya Liyongo kama yanavyotokea katika utendi huo si kamili bali ni simulizi mojawapo tu ya maisha yake. Masimulizi mengine kama yanavyotokea katika nyimbo zake.
Kwa kuhitimisha tunaona kuwa ni kweli kabisa kuwa kabla ya uhuru na hata kabla ya ujio wa wageni ushairi wa Kiswahili ulikuwepo na ulikuwa na maendeleo kadha wa kadha. Pmoja na hoja kadha zilidhotumika katika kujadili historia ya ushairi wa Kiswahili kabla ya uhuru tunaona kuwa ushairi wa Kiswahili ulikuwa na dhima mbalimbali ikiwemo mojawapo ya kuhimiza kazi ambayo ndiyo iliyokuwa dhima kuu katika ushairi wa Kiswahili kabla ya ukoloni. Ushairi w Kiswahili hasa nyimbo za kazi ziliimbwa wakati wa kazi ngumu na kumburudisha mwimbaji na msikilizaji. Pia Ikumbukwe Kuwa nyimbo za kazi ndiyo Ushairi wa awali kabisa wa Kiswahili, ushairi huu pia ulipunguza uchovu wa watu hasa katika kazi kama vile kilimo, ufugaji, uwindaji na kadhalika. (Gibbe, 1980)(Samweli, Kabiero, & Seleman, 2013)(Mulokozi & Kahigi, 1982)
Marejeo
Gibbe, A. (1980). Mitaala ya Lugha na Fasihi. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Mulokozi, M. (1999). Tenzi Tatu za Kale. Dar es Salaam: TUKI.
Mulokozi, M., & Kahigi, K. (1982). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Samweli, M., Kabiero, A., & Seleman, A. (2013). Ushairi wa Kiswahili. Dar es Salaam: Meveli Publishers.
Senkoro, E. (1988). Ushairi Nadharia na Tahakiki. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)