MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
USHAIRI NI NINI?

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
USHAIRI NI NINI?
#1
USHAIRI NI NINI?
Hadi hapa tumekwishakuona kuwa ushairi wa Kiswahili si sanaa ya vina kama Shaaban Robert alivyotuambia; na wala vina na urari wa mizani siyo roho au uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili kama Abdilatif, Mayoka na wanajadi wengine wanavyohubiri. Kwa hakika, mojawapo ya sababu ya wanajadi kuamini kuwa shairi lazima liwe na umbo maalum, na kuwa umbo hilo lazima litawaliwe na vina na urari wa mizani, ni kuwa dhana yao ya ushairi imetawaliwa na utaratibu wa kimaandishi. Hebu tulidadisi jambo hili zaidi.
Ni rahisi kuthibitisha kuwa umbo la shairi la vina na mizani ni la kimaandishi, kwani karibu watu wote hapa kwetu hulitambua shairi kama linavyoonekana kwenye ukurasa wa karatasi (uwe ukurasa wa Uhuru, au wa Mzalendo au wa diwani yoyote ya mashairi). Kwa mujibu wa mtazamo huu, insha ni insha kwa vile huonekana imeandikwa kwa njia ya mjazo; na shairi ni shairi kwa vile laonekana lina vina na urari wa mizani. Hebu tuangalie andiko hili hapa chini:
Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje?
Mwanamme peke yake sijui angeishije! Maisha yetu ya kwanza yangekosa msaada; ya kati yakawa giza kwa furaha kuwa shida; na ya mwisho yangekuwa ni ghali kwa pesa moja: ingekuwa si dunia kwa uchache wa faraja.
Andiko hili lililoandikwa kwa njia ya mjazo, bila shaka laonekana kuwa nathari. Lakini andiko hilo hilo tukigeuza umbo lake, “dhana” ya watu wengi juu ya hulka yake itageuka pia:
Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje?
Mwanamme peke yake sijui angeishije!
Maisha yetu ya kwanza yangekosa msaada;
Ya kati yakawa giza kwa furaha kuwa shida;
Na ya mwisho yangekuwa ni ghali kwa pesa moja:
Ingekuwa si dunia kwa uchache wa faraja.
Umbo hilo haliwakanganyi watu wengi: waliangaliapo mara moja hurukia kusema kuwa ni shairi, na wakiulizwa kwa  nini hujibu kuwa andiko lina vina, urari wa mizani, n.k.
Tuchukue andiko jingine lifuatalo:
Wakadha namshukuru Mungu
Kwa ajili ya sahibu yangu
Mtunzi na kungwi wa mizungu
Mathias Mnyampala
Mfadhili na mwenye jamala
Mashuhuri kwa mashairi ya muwala
Na uandishi wa makala
Ambaye ameniomba niandike hii dibaji
Asaa iwafariji wasomaji
Ambao sanaa hii wanaitaraji
Niwabainishie yaliyo muhimu
Kuhusu Kiswahili na utungaji
Na kubatilisha riwaya za mafukala.
Katika andiko hili tunaona upatanifu wa aina fulani wa vina vya ‘ngu’, ‘la’, na ‘ji’, ni ‘mu’ tu ambayo haina kina chenziye. Na si ajabu wapo watu ambao wanaweza kuliita andiko hili ubeti wa shairi lenye dosari au guni, kwa sababu wameona upatanifu fulani katika umbo lake. Kumbe andiko lenyewe katika uasili wake lilikuwa katika umbo la mjazo kama ifuatavyo:
Wakadha namshukuru Mungu kwa ajili ya sahibu yangu, mtunzi na kungwi wa mizungu, Mathias Mnyampala, mfadhili na mwenye jamala, mashuhuri kwa mashairi ya muwala na uandishi wa makala, ambaye aliniomba niandike hii dibaji asaa iwafariji wasomaji ambao sanaa hii wanaitaraji, niwabainishie yaliyo muhimu kuhusu Kiswahili na utungaji, na kubatilisha riwaya za mafukala.
Kutokana na hayo yaliyokwishasemwa, tunaona kuwa “ana ya ushairi” ya wanajadi imefinywa kwenye “umbo maalum lenye utaratibu wa vina na urari wa mizani”, ambayo kwa kweli ni dhana ya kimaandishi. Na nathari kwao ni andiko lolote ambalo halina utaratibu huo. Wanayaangalia matumizi ya lugha katika tabaka mbili zisizoingiliana: matumizi ya kishairi na yale ya kinathari. Mtazamo huu kuhusu lugha umepotoka sana, na hapo baadaye tutaonyesha upotofu wake. Kwa sasa inafaa tulikabili suala la ushairi ni nini.
Iwapo “umbo” lionekanalo kwenye karatasi haliwezi kutiwa maanami katika ufafanuzi wowote thabiti wa ushairi, basi ushairi ni nini? J.A. Ramadhani, katika makala yake juu ya ushairi, ameeleza kwa urefu na kwa undani maana na sifa za ushairi. Mambo mengi muhimu ameyataja.
Anatuambia kwamba:
(1) Ushairi huanza na hisi au mchomo unaosababishwa na mazingira;
(2) Hisi hizo huwasilishwa kwa msomaji kwa njia ya lugha teule ya kitamathali;
(3) Hisi hizo lazima ziambatane na mawazo na mtazamo wa fikira;
(4) Hali ya kishairi inahusiana kidogo na hali ya kindoto au tabia ya kuona yasiyoonekana na kuwania yasiyowezekana;
(5) Ushairi umefungamana na ubuni, na kwa hiyo hauwezi kuwekewa sheria zisizobadilika, na kwamba kuogopa kubuni kunadumaza maendeleo ya ushairi wa Kiswahili;
(6) Uwezo wa kubuni wa mshairi umetoka kwa Mungu ambaye ndiye mfalme wa sanaa zote.
(7) Shairi ni muungano wa fani na yaliyomo (maudhui).
Kimsingi, ufafanuzi huo wa ushairi hautofautiani sana na ufafanuzi alioutoa Kezilahabi. Anatuambia kwamba:
Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha.
Fafanuzi hizi mbili zinarekebisha ile fikira ya wanajadi kwamba ushairi lazima uwe na urari wa mizani na vina. Hata hivyo, fafanuzi hizi zina upungufu wake.
Upungufu wa maelezo ya Ramadhan umo hasa katika imani yake kuwa uwezo wa kishairi unatoka kwa Mungu.
Hapa sipo mahali pa kujadili imani ya kidini ya Ramadhan juu ya uwezo wa kishairi; suala hili ni kubwa na pengine linahitaji makala ya pekee. Inatosha tu tukisema kuwa ni kawaida ya falsafa za kidhanifu kumuweka Mungu kuwa chimbuko la mema aliyo nayo mtu; na kumuweka shetani kuwa chimbuko la mabaya yote. Upungufu wa kauli ya Kezilahabi hasa umo katika fungu la maneno “ukweli fulani wa maisha”. Je, ni kweli kuwa ushairi lazima ueleze ukweli fulani wa maisha, na siyo uongo? Hali halisi inatueleza kuwa wapo washairi wasemao ukweli fulani kuhusu maisha, na wapo wengine wasemao uwongo, na pia mshairi mmoja anaweza kusema ukweli katika shairi moja na uwongo katika shairi jingine. Fikra hii ni potofa kama ile isemayo kuwa mshairi ni chemchemu ya hekima.
Jambo ambalo halikutiwa maanani katika fafanuzi hizo linahusu dhima ya fasihi na ushairi kama vyombo vya kuburudisha na kustarehesha watu. Ushairi hauelezi mawazo tu kama kemia au fizikia. Ushairi lazima uguse hisi, lazima umsisimue yule anayeusema, kuusoma au kuuimba na yule ausikilizae. Shairi lisilogusa hisi ni kavu na butu, na hata kama limesarifiwa katika vina na urari wa mizani, shairi hilo litaishia katika kuhibiri tu. Na fasihi ikisha hubiri mahubiri makavumakavu kama kasisi mimbarini, bila mvuto wowote wa kifasihi, itakuwa imeshindwa kugusa pale ambapo inapaswa kugusa – hisi za watu. Kwa hiyo basi ufafanuzi thabiti wa ushairi lazima uzingatie uwezo wake wa kugusa hisi za watu.
Kutokana na hayo tuliyokwisha sema, tunaweza kutoa ufafanuzi wa ushairi ambao unazingatia yale yaliyokwisha semwa na hao hapo jua, pamoja na dhima ya ushairi ya kugusa moso au hisi. Nao ni huu: Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara, katika usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani, kuhusu maisha au mazingira ya binadamu, kwa njia inayogusa moyo. Hapa lazima tuseme kuwa, ingawa ushairi wa aina yoyote unaweza kuimbwa, lakini siyo kila kiimbwacho kitaitwa ushairi.
Ushairi ni sanaa ya lugha, na usanaa wake uko katika “mpangilio maalum wa maneno fasaha yenye muwala, kwa lugha ya mkato… kwa njia ya kugusa moyo”, siyo katika uimbaji, unaweza kuuongezea (au hata kuupunguzia!) mguso.
Kwa mujibu wa maelezo haya, uimbaji wa hesabu au aya kutoka kwenye kitabu cha siasa si ushairi.
Ufafanuzi huo wa ushairi unazingatia halka ya ushairi usiofuata urari wa vina na mizani na ule unaofuata urari huo; ule ulio katika fasihi simulizi na ule ulio katika fasihi andishi.
Jambo moja linalojitokeza ni kuwa ushairi ni lugha katika hali ya matumizi maalum; na matumizi maalum haya ni matumizi ya kisanaa ya vipengele vya lugha. Hapa chini tutajadili kwa ufupi baadhi ya vipengele muhimu vinavyoupambanua ushairi.
VIPENGELE VYA USHAIRI
Washairi wa jadi wanadai kuwa “vina na mizani ndio uti wa mgongo wa ushairi.” Dai hili ni batili kifasihi, kwani linageuza kipengele kimoja kidogo cha kisanaa kuwa ndicho msingi wa sanaa yenyewe.
John Ramadhani amezieleza sifa za ushairi kwa urefu na vizuri zaidi. Yeye ametaja mambo yafuatayo yaliyo mahimu:
1) Katika ushairi vitu hupewa nafsi na utu;
2) Picha ni sifa muhimu ya ushairi;
3) Ushairi huweza kuwa na mpangilio wa maneno usio wa kawaida;
4) Ushairi una ridhimu, mlingano wa sauti na mapigo;
5) Shairi ni lazima lionyeshe sifa ya kiumbaji, lisiwe ni nakala ya shairi jingine.
Yote haya ni sawa, ila sisi tutajaribu kuyafafanua zaidi na kuongezea sifa zingine ambazo hazikutajwa. Suala hili tutalijadili kwa kufuata vichwa hivi:
1) Mpangilio wa maneno
2) Picha
3) Tamathali za usemi
4) Takriri na ridhimu
5) Hisia za kishairi
6) Fani na maudhui
Mpangilio wa maneno
Watu wengi wameichukulia kuwa kweli isiyopingika kuwa mpangilio wa maneno (mfuatano wa vipashio vya sentensi) katika ushairi ni tofauti na ule ulio katika nathari. Mpangilio wa maneno hufuata kanuni za miundo inayowezekana katika lugha fulani. Tukichukua Kiswahili, kwa mfano, sentensi iliyozoewa sana ni ile yenye muundo huu:
Kiima – Kitenzi – changizo…
Nomino – kimilikishi – kitenzi – kielezi…
Katika Kiswahili tunaweza kusema:
Baba hujua kulima
Mama hujua kusaga
Mimi sijui chochote
Baba yangu anajua kulima kwa plau
Hii ni miundo ya kawaida ambayo imezoewa sana na wasemaji wa Kiswahili. Lakini, mzungumzaji anaweza kuipangua miundo hiyo, na kutumia miundo isiyo ya kawaida sana, kwa madhumuni ya kuleta msisitizo wa jambo fulani:
Kulima baba hujua
Kusaga mama hujua
Chochote mimi sijui…
Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mtu yeyote, mradi awe ni mzungumzaji wa lugha fulani, anaweza kutunga muundo wa kawaida au usio wa kawaida sana (pengine bila yeye kujua).
Mzungumza lugha anao uhuru wa kutamba katika uwanja wa lugha yake ili aweze kueleza hisia na mawazo yake. Jinsi atakavyopanga maneno katika sentensi itategemea ujuzi na ustadi na uzoefu wake katika jambo hili. Je, mshairi anautumiaje uhuru huu wa kutunga miundo iliyo ya kawaida sana, na ile isiyo ya kawaida sana?
Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mshairi si mtu wa pekee katika ujuzi wa lugha aitumiayo kutungia mashairi yake.
Jambo tuwezalo kulisema pasipo wasiwasi wowote kuhusu tofauti baina ya mshairi na mtu wa kawaida ni hili: mshairi anao uzoefu katika kutunga mashairi, lakini mtu wa kawaida hana uzoefu huo. Uzoefu huu katika sanaa hii humwezesha mshairi kuitumia miundo ya lugha hiyo kutimilizia malengo yake ya kishairi. Uhuru wa mshairi wa kuchagua muundo fulani na kuacha muundo mwingine, kupanga vipengele fulani kwa njia fulani na kuacha kuvipanga kwa njia nyingine, ni uhuru unaotawaliwa na kanuni za sanaa yake, uwezo wake wa kuvipanga vipengele hivyo ili vilete athari iliyokusudiwa hutegemea uzoefu wake, ubingwa wake, na hali aliyo nayo wakati wa kutunga shairi lake.
Katika ushairi wa Kiswahili, mbinu ya upangaji wa vipengele vya sentensi kwa njia isiyo ya kawaida hutumika sana. Utakuta washairi wanasema: mzuri msichana, wangu mke, n.k. badala ya msichana mzuri, mke wangu. Miundo mingine ni kama ile tuliyoitoa mfano hapo juu (kulima baba ajua n.k.).
Ipo miundo mingine isiyotumika sana katika mazungumzo ya kawaida inayotumiwa na washairi. Mpangilio huu usio wa kawaida huvuta udadisi kuliko ligha ya kawaida, na hutumika katika kusisitiza vipengele fulani vya hisi au wazo la mshairi.
Lakini shairi siyo lazima liwe na mpangilio wa maneno usio wa kawaida ili lipendeze. Shairi linaweza kuwa na mpangilio wa kawaida tu, na athari ya mguso ikaletwa na vipengele vingine kama vile picha, takriri, n.k. Kwa hiyo, ingawa mpangilio tulioujadili unaweza kuwa alama mojawapo ya ushairi, lakini si lazima kila shairi lithibiti mpangilio huo.
Picha
Picha ni matumizi ya lugha yanayopambanuliwa na utenzi mzuri wa maneno, uangalifu na udhahiri wa maelezo wenye kuhusisha na kujumuisha dhana mbali mbali tofauti ndani ya dhana moja ili kuleta taswira na athari maalum katika mawazo ya msomaji (au msikilizaji). Kezilahabi ameeleza kuwa athari hiyo aipatayo msomaji au msikilizaji wa ushairi inaweza kuwa ni ya aina ya vionjo vyenye kuhusiana na milango ya fahamu ya kusikia, kuona, kunusa na kugusa. Kwa hiyo, kwa kutumia picha, mwandishi anaweza kumfanya msomaji wake asisimke, aogope, afurahike, avutike, akirihishwe, alie, anyamae au aghadhabike kwa kuathiriwa na picha zilizoteuliwa na kusanifiwa kwa ufundi. Ugumu wa kutunga mashairi ya mtiririko uko katika utenzi na upangaji wa picha na tamathali za usemi zenye kuoana na maudhui yaliyokusudiwa zisizotengua ridhimu ya shairi na zisizofanya lugha ya shairi ipoteze uasili wake. Wakati huo huo, shairi hili liwe na uwezo wa kindanindani wa kuvutia na kudumisha hamu ya msomaji au msikilizaji hadi mwisho. Katika ushairi wa fasihi-simulizi, hamu ya hadhira hudumishwa na uteuzi wa maneno, muziki (kama ala za muziki zinatumika), mazingira au sherehe inayoambatana na tungo hiyo, ushirikishaji wa hadhira kwa kutumia kibwagizo, makofi na vipengele vingine, na umuhimu wa kijamii au kihistoria wa yale yanayoelezwa.
Katika ushairi-andishi wenye vina na mizani, hamu ya msomaji zaidi hudumishwa na ulinganifu wake wa ridhimu na sauti unaotokana na vina na urari wa mizani. Mapigo ya shairi la aina hiyo hufuata mgawanyo wake katika vipande vyenye mizani sawa na shairi husomeka upesi upesi bila kuitumikisha sana akili ya msomaji. Kifani, vina na urari wa  mizani katika ushairi-andishi hufanyakazi ya ala za muziki katika ushairi-simulizi.
Ushairi wa mtiririko ni wa kiwango cha juu zaidi kwa sababu unakataa kupata uhai wake kutokana na mbwembwe za kijuujuu, mambo ya nje ambayo ni nyongeza muhimu juu ya ushairi, lakini si lazima yawe sehemu ya ushairi: vina na urari wa mizani. Ushairi huo unapata uhai wake na utamu wake kutokana na mfumo wake wa ndani ambao ni fungamano la matumizi mahususi ya lugha nzito, hisia nzito na maudhui ya kishairi. Mashairi haya yanamlazimisha msomaji atumie akili zaidi, ajihusishe zaidi kijaziba katika hisia za mtunzi, na atafakari zaidi, badala ya kumkokota kikuku kwa utamu wa kijuujuu wa muziki wa vina na urari wa mizani. Mtiririko ni mashairi yaliyokusudiwa yasomwe na watu wazima, mengi hayafai kusomwa na watoto wa shule za msingi kwa sababu uwezo wao wa kuichambua fasihi bado ni mdogo. Hivyo hapana shaka kuwa kwa miaka mingi ijayo mashairi yenye vina na mizani yataendelea kupendwa zaidi na watoto wadogo, mradi lugha yake isiwe ngumu sana. Kwa ajili ya adhira hiyo, mashairi ya aina hiyo ni lazima na bora yaendelee kutungwa. Bali kwa ajili ya watu wazima waliofikia kiwango fulani cha ufahamu wa fasihi, mashairi ya aina hiyo si lazima, ingawa si mwiko kuyatunga. Kila mshairi apewe uhuru wa kutumia fani inayofungamana vizuri zaidi na maudhui yake, uwezo wake, na pia hadhira aliyokusudia.
Ingawa matumizi ya lugha huweza kuzindua hisi na maono fulani katika akili ya msomaji juu ya kile kinachozungumziwa, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa uhusiano huo unaozinduliwa kati ya picha ya mawazoni na kitu halisi kinachozungumziwa (kinachochorwa) ni wa kinadharia, si wa kimaumbile au wa moja kwa moja. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya maana au umbile la kitu na uwakilishaji wa kitu hicho katika lugha – katika neno mofimu na fonimu. Kifasihi uhusiano tuupatao tunapotumia picha ni ule unaoumbwa na akili ya msomaji mwenyewe inapozinduliwa na ustadi wa mshairi wa matumizi ya lugha na kunga nyingine za ushairi. Usanifu wa mashairi humfanya msomaji wake awe msanifu vile vile; mshairi hudokeza, msomaji hukamilisha; mshairi huumba, msomaji humalizia na kuhusisha kile kilichoumbwa na hali halisi anayoijua. Kwa hiyo msomaji wa mashairi si mpokeaji tu wa sanaa hiyo bali ni mpokeaji msanii vile vile.
Hebu tuutazame mfano ufuatao unaotoka katika shairi la Shaaban Robert, “Mtu na Malaika”.
Mtu Na Malaika
Neno lenye mzunguko, halipatikani mwisho,
Wa huku hafiki huko, wala halina malisho.
Halishibishi huchosha, njiaye ina uchovu,
Na tabu isiyokwisha, wala hupati utuvu.
Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka,
Na milima akapanda, apendako akafika.
Mabondeni akashuka, mwituni akatumbua,
Na mitoni akavuka, hata alikonuia.
Na mzunguko wa dira, mwisho wake ni dirani,
Hupati kupanda bara, na hushuki baharini.
Tazama mashaka gani, njia ya dira si njia.
Katika dondoo hii tunapewa picha tatu mahsusi. Picha ya kwanza ni neno linalozunguka… Mshairi anatuambia kuwa neno ambalo halifuati njia iliyonyooka ‘neno lenye mzunguko” halifikii mwisho wake na halileti mradi uliokusudiwa “halina malisho”. Hapa neno limefanywa kuwa kitu chenye uwezo wa kutembea, kuzunguka. Athari ya neno hilo kwa anayehusika ni kwamba halileti shibe wala utulivu, linachosha: “Halishibishi huchosha”. Hapa tunapewa picha ya shibe, neno linapewa uwezo wa chakula – kitu yakini kinachoshikika na kinacholiwa. Bali mtu hatosheki na “chakula hicho” hatatui matatizo yake iwapo njia anayotumia ni ya mzunguko, ya kulegalega, ya ugeugeu na woga.
Picha ya pili tunayopewa ni ya mtu aendaye safari ngumu kwa ujasiri na moyo na dhati, akipanda milima na kushuka mabonde, akipenya misitu na kuvuka mito, hadi kufika kule anakokwenda. Huyu ni mtu asiyeogopa matatizo, anayeshikilia njia ngumu lakini nyoofu, alimradi anajua kuwa itamfikisha kwenye lengo lake. Ni mtu anayepambana na matatizo badala ya kuyakimbia. Mtu wa aina hii ndiye hupata mafanikio. “Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka”.
Picha ya tatu tunayopewa ni dira. Dira ni chombo kitumiwacho na mabaharia na wasafiri wengine kusahihisha majira yao ili wasipotee njia. Dira ni chombo cha mviringo na mshale wake aghalabu huzungukia pale pale ulipo, katu hautoki nje ya dira. Picha hii inasisitiza wazo la mwandishi kuwa njia yenye kuzunguka haiwezi kumfikisha mtu kwenye lengo lake. Mshale wa dira huzunguka daima lakini haufiki kokote.
Picha hizi tatu kwa pamoja zinafaulu kutupa ujumbe wa mwandishi kuhusu maisha na namna ya kuyakabili: tuyakabili kwa juhudi na ujasiri na nia. Tuamue jambo na tulifanye bila kutetereka. Tusiogope vikwazo wala matatizo.
Maisha ni mapambano.
Kwa kutumia picha hizi tatu, mwandishi kafaulu kufikisha kwetu ujumbe wake wa kishairi. Maudhui yake ni ya kishairi, yanapatikana kwa kuzichambua na kuzifafanua picha alizozitumia. (Shairi hili lingeweza vile vile kufasiriwa kidini kama alivyofanya J. Ramadhani katika makala yake “Ustadi wa Shaaban Robert Mshairi” Mulika No. 7, uk. 46-48)
Mpangilio wa lugha
Katika dondoo tulilolichunguza picha imejitokeza kwa njia ya sitiari (kitu kimoja kuwa badala ya kitu kingine kilicho tofauti: k.m. “msitu” badala ya “matatizo”, “dira” badala ya “tabia ya kukwepa matatizo” n.k.) na mpangilio wa lugha na mawazo. Dhana tatu zinazotofautiana – neno linalozunguka mtu anayesafiri kupitia msituni na baharini, n.k. na dira inayozungukia mahali pale pale ilipo zinaleta wazo moja mahsusi. Zote zimechangamana ili kujenga dhana moja.
Umoja wa wazo linalozungumziwa unaimarishwa pia na mfungamano wa ubeti mzima – pana mfululizo wa fikra na hisi tangu mstari wa kwanza hadi wa mwisho, kifungu kizima ni ubeti mmoja, hakuna mgawanyo wa beti za mistari miwili miwili au minne minne. Wazo linafululiza bila kusita au kukatishwa hadi mwisho kama vile ambavyo maudhui ya shairi lenyewe yanavyotuhimiza kufululiza katika njia moja bila kutetereka hadi mwisho. Muundo wa shairi umeoana na maudhui yake.
Mpangilio wa lugha – herufi, silabi, mofimu hadi maneno na sentensi ni sharti uoane na maudhui. Washairi hutumia kunga mbali mbali za kisauti na kimpangilio ili kuleta hisia fulani. Baadhi ya kunga hizo ni onomatopea, mizani, vina, asonansi (mlingano wa sauti za irabu), konsonansi (mlingano wa sauti za konsonanti) takriri-konsonanti (marudio ya konsonanti) takriri-vina, n.k. Vipengele vyote hivi, isipokuwa onomatopea, ni aina ya takriri na tutavijadili chini ya mada ya takriri.
Onomatopea
Onomatopea ni mwigo wa sauti. Hii ni kunga inayotumiwa na washairi ili kutoa picha au dhana ya kile kinachowakilishwa au kupambanuliwa na sauti hizo. Kwa mfano tukisema:
“Maji yalimwagika mwa” neno mwa ni onomatopea, linawakilisha sauti au kishindo cha maji yanayomwagika. Baadhi ya onomatopea ambazo zimekwisha kuwa sehemu ya msamiati wa kawaida wa Kiswahili ni: pikipiki, bombom, mbwa, yowe, ngurumo, bunduki, gumia, kata, n.k.
Katika shairi lake la “Cheka kwa Furaha” Shaaban Robert ametumia onomatopea ili kuleta ile dhana ya kucheka:
Dhiki ni kama mzaha, asiyecheka ni nani?
Haya cheka ha! ha! ha! ndiyo ada duniani.
Basi cheka kwa! kwa! kwa! kwa! usafike moyo wako
Pamoja na malaika, wema mbinguni waliko;
Maneno yaliyoandikwa kwa italiki ni onomatopea, yanatoa
picha ya kusikika ya sauti ya mtu anayecheka. Huu ni
mpangilio maalum wa sauti ili kutoa picha ya kusikika ya
dhana inayozungumziwa.
TAMATHALI
Tamathali za usemi ni vifananisho au viwakilisho vya dhana fulani kwa dhana nyingine tofauti au zinazofanana. Ni usemi wenye kupanua, kupuuza au kubadilisha maana za dhahiri au za kawaida za maneno ili kuleta maana maalumu ya kishairi iliyokusudiwa na mtunzi. Tamathali nzuri hupanua, huyakinisha na huipa uhai na uhalisi zaidi dhana inayoelezwa, huburudisha na kuzindua akili ya msomaji au msikilizaji wa shairi, na huacha athari ya kudumu katika hisi na mawazo yake.
Tamathali zinazotumika zaidi katika ushairi ni tashbiha, meonymy, uhaishaji (personification) (Tashihisi) synecdoche, baalagha, kejeli na sitiari.
Tashbiha
Hi ni tamathali ya ufananisho au mlinganisho wa vitu viwili au zaidi. Katika tashbiha, kama ilivyo katika sitiari, huwa kuna vitu vitatu vinavyofananishwa ambavyo wataalamu wameviita kizungumzwa, kifananishi na kiungo. Kifananishi ndiyo usemi wenye kuzingatia maana-dhahnia, ni chombo kinachobeba mlinganisho. Kizungumzwa ndicho kitu halisi ambacho kinazungumziwa na kifananishi kwa mafumbo. Kiungo ni zile sifa ambazo zinapatikana katika kizungumziwa na kifananishi na hivyo kuhusisha vitu hivyo viwili. Katika tash- biha, kizungumzwa na kifananishi huhusishwa bila mafumbo kwa uwazi, moja kwa moja, kwa kutumia maneno fulani ya ulinganisho, km. “kama” “fanana na”, “mithali ya” n.k.
Katika tashbiha hakuna maana dhahnia, bali kuna ulinganishaji wa vitu viwili vilivyo bayana. Angalia mfano ufutao:
Kweli ni sawa na radi inapotoa kauli…
Kweli kinywani ikiwa sawa na Mto wa Nili
Kweli kama msumeno hukereza sawa kweli.
Katika dondoo hilo maneno yaliyochapwa kwa italiki yanaunganisha vitu viwili vinavyotofautiana na kuvifananisha. Mstari wa kwanza “kweli” inalinganishwa na radi, mstari wa pili inalinganishwa na “Mto Nili” na mstari wa tatu inalinganishwa na “msumeno”.
Tashihisi (uhaishaji)
Washairi mara nyingine huweza kukipa kitu kisichokuwa na uhai sifa za kitu chenye uhai, hasa za binadamu. Matumizi ya lugha kwa njia hiyo ndiyo huitwa uhaishaji au tashihisi.
Kisanaa maelezo ya kitashihisi huwa na upekee unaomwingia msomaji akilini haraka, kwani si jambo la kawaida, mathalan, kuona mti “ukimpungia mtu mkono” au nyumba “ikimkodolea macho” mgeni. Tashihisi, basi, ni aina ya sitiari na kisanaa kazi yake ni kama ile ya sitiari, japo kwa kiwango cha kidhahnia zaidi.
Mfano wa matumizi ya tashihisi:
Kimya hakineni jambo, si kimya chawatazama…
Kimya chaja zua mambo, pasiwe mwenye kusema…
Kimya kipimeni sana, msione kutosema
Kimya hakichi kunena, kitakapo kusimama
Kimya chaja watukana kizuwe yaliyozama…
Katika dondoo hili, “kimya” (ambayo ni nomino-dhahnia) kimepewa sifa za binadamu, kinaweza kunena, kutazama, kuzua mambo, kusimama nakutukana.
Katika shairi lake la “Fedha”, Shaaban Robert anaipa fedha sifa za binadamu:
Fedha huita wazuri,
Wakaitika labeka,
Wakenda bila hiari,
Mahali wasikotaka.
Mfano mzuri wa matumizi ya tashihisi kishairi tunauona katika shairi la Bwana Rajabu M. Kianda (Selukindo) liitwalo “Jembe”.
Jembe wangu nifariji, nami nikupe uzima,
Jembe wewe ndiye jaji, twakuenzi zote dhima,
Jembe wewe ni mpaji, wa baba na kina mama,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.
Jembe wewe msifika, utuonee huruma,
Jembe shamba tukifyeka, njoo ufanye kulima,
Jembe njoo pasi shaka, ukija lete mtama,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.
Jembe kwetu ukifika, tunapata usalama,
Jembe kote umeshika, ukweli tunausema,
Jembe yakija masika, nawe fika nyuma nyuma,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.
Jembe jua likitoka, nawe usife mtima,
Jembe usije kuchoka, au kupatwa na homa,
Fanya bila kukongoka, fanya usirudi nyuma,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.
Mola akupe hakika, usende kamwe mrama,
Nenda upate kufika, kama tunavyokutuma,
Sote huko tukifika, tutaishi kwa neema,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.
Katika shairi hili “Jembe” limepewa sifa za binadamu: ni mfariji, jaji, mpaji, mtawala, mkulima; linaweza kusafiri, kubeba mtama, kufa mtima, na kupatwa na homa. Ingawa tunajua wazi kuwa jembe ni kifaa tu kinachotengenezwa na kutumiwa na binadamu, kuwa halina hata mojawapo ya sifa hizo, lakini tunaposoma shairi tunaathirika na kushawishika kuwa yasemwayo ni kweli na sana maana. Tunalikubali kwa sababu tunaelewa kuwa tukisomacho ni kiwakilishi tu, ni ishara ya dhana nyingine nzito na muhimu: Umuhimu wa kilimo katika uchumi na uhai wetu, na katika historia wa binadamu. Mtunzi katumia uwezo wake wa kisanaa kuumba picha hii ya jembe, nasi wasomaji inatubidi tutumie uwezo wetu wa kuumba na kutafsiri ishara ili tulielewe na kulifurahia shairi hili. Matumizi ya tashihisi yanaliongezea shairi hili uzito wa kimaana, na yanatushirikisha sisi wasomaji katika ufumbuzi wa “kitendawili” chake. Hivyo shairi hili linatuathiri sana kwa kuwa linatushirikisha akili zetu katika kutafakari vipengele vyake na maana yake.
Karibu.
Jambo!
Habari yako?
Hujambo?
Sijambo!
Habari za safari?
Nimefurahi kukutana na wewe.
Jambo.
Hamjambo.
Hatujambo.
jambo.
karibu.
habari yako?
hujambo?
sijambo.
habari za safari?
nimefurahi kukutana na wewe.
habari?
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 2 Guest(s)