MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
Dhima ya Lugha ya Mawasiliano katika Jamii: Kiswahili na Mkakati wa Usomaji kuelekea

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
Dhima ya Lugha ya Mawasiliano katika Jamii: Kiswahili na Mkakati wa Usomaji kuelekea
#1
Dhima ya Lugha ya Mawasiliano katika Jamii: Kiswahili na Mkakati wa Usomaji kuelekea Umajumui wa Kiafrika
Aldin K. Mutembei
 Ikisiri
Dhima ya lugha ya mawasiliano imejadiliwa na wanazuoni kadhaa. Wengi wameiangalia kama yenye kuongelea masuala ya jamii inamochipuka wakiihusisha na fasihi, au ile yenye kutumia lugha za picha au kitaswira katika kuumba maana iliyokusudiwa. Makala hii inalenga mambo mawili ya msingi. Mosi, ni kuangalia dhima ya lugha ya mawasiliano katika baadhi ya kazi za kifasihi zinazovuka mipaka ya jamii zinamochipuka na pili, ni kuiangalia ikiwa lugha hii inao uwezo wa kutabiri yale yatakayokuja. Katika lengo la pili, makala inakwenda hatua moja zaidi na kuangalia ikiwa suala la Umajumui wa Kiafrika linaweza kujengwa na namna ya usomaji chanya wa kazi za kifasihi. Kwa hiyo, makala inajadili dhana ya “usomaji” kwa maana pana zaidi ya kuangalia maandishi na kupata maana. Katika mjadala wa vipengele hivyo, makala hii itatumia nadharia ya Thieta ya Walalahoi (Theatre of the Oppressed) kwa mujibu wa mawazo ya Boal (2008). Mawazo ya Boal, ndiyo yatakayotuongoza kufafanua maana ya “usomaji” kwa mujibu wa makala hii. Makala inaonesha kuwa Umajumui wa Kiafrika unaweza kujengwa na kuimarishwa kupitia katika usomaji wa kazi za kifasihi wenye kulenga ukombozi. Mawasiliano katika lugha ya Kiswahili na baadhi ya kazi za Kifasihi za Kiswahili yanatolewa kama mfano wenye kuweza kutumika katika kujenga Umajumui wa Kiafrika.
1.0Utangulizi
Makala hii inajadili suala la uwezekano wa Umajumui wa Kiafrika kupitia katika usomaji hasa wa kazi za Kifasihi ya Kiswahili. Ziko sehemu tano zinazokamilisha mjadala huu kwa mawanda tofauti. Sehemu hizi tano zinaanza na utangulizi unaoangalia suala la usomaji wa miaka ya 1970 kwa kulinganisha na usomaji wa miaka ya 2007. Jambo linalosisitizwa hapa ni ile ari ya usomaji na mwamko uliokuwamo katika vichwa vya waasisi wa hatua hizo. Sehemu ya Utangulizi inaendelezwa chini ya kipengele cha ‘usomaji baada ya mwamko wa uhuru’. Makala inaongozwa na Nadharia ya Thieta ya Walalahoi ya Augusto Boal inayojadili suala la dhima ya mawasiliano ndani ya kazi za kifasihi katika sehemu ya pili. Sehemu ya tatu inafafanua maana ya dhana ya “usomaji” kwa mujibu wa makala hii. Katika sehemu hii, dhana za ‘elimu’ na ‘usomaji’ zinajadiliwa kwa mifano. Sehemu ya nne ina vipengele vingine vidogo ndani yake. Kwa ujumla inajadili dhana ya Umajumui wa Kiafrika kupitia katika lugha. Kipengele chini ya sehemu hii kinajadili kwa undani lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo inayolengwa katika mjadala wa Umajumui wa Kiafrika. Katika mjadala huu pia, swali linaloibuka ni usomaji katika Kiswahili uwe wa namna gani. Hiki ni kipengele kimojawapo katika sehemu ya nne. Kwa kuwa kuna dhana potofu kuhusu usomaji, kipengele kingine kinachogusiwa ni dhana ya “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara”. Huu ni mfano mmojawapo katika mingi ambao unafafanua wazi kuhusu namna ya usomaji unaopotosha. Mifano mingine inayolenga kuonesha usomaji wa kudharaulisha Waafrika inachukuliwa kutoka katika baadhi ya kazi za kifasihi hasa zilizotafsiriwa kutoka jamii za nje ya Afrika na kuingizwa katika Kiswahili. Mjadala huu ndio unaojenga kipengele kingine chini ya sehemu hii ya nne. Sehemu ya mwisho ni hitimisho. Hii ni sehemu ya tano inayozungumzia usomaji wa sasa ikilenga si kutoa muhtasari wa yaliyojadiliwa, bali kuacha mapendekezo ambayo yanaweza kuwa mwanzo wa ujenzi wa Umajumui wa Kiafrika kupitia katika lugha ya Kiswahili.
1.1 Usomaji baada ya Mwamko wa Uhuru Kipindi cha kuanzia mwanzoni mwa mwaka 1971 hadi mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1980 kiliifanya Tanzania ijulikane katika dunia ya wasomaji kupitia mpango wa usomaji kwa wote wa “Elimu ya Watu Wazima”.1 Zaidi ya watu milioni tatu walitathminiwa, wakati kampeni ya kupigana na adui ujinga ilipoanzishwa rasmi mwaka 1971. Matokeo ya tathmini ya hali ya usomaji iliyofanyika mwaka 1981 yalithibitisha kuwa ahadi na mpango wa Serikali ya Tanzania ya wakati huo, kuhusiana na usomaji kwa faida ya wananchi wake wote, ulikuwa umetekelezwa kwa mafanikio. Kwa mujibu wa Boal (2008:97), wananchi hao waliojua kusoma walithibitisha kuwa, kutokujua kusoma, sio kutokujua kujieleza, bali hawakufahamu kujieleza katika lugha fulani. Elimu ya Watu Wazima ni mpango uliopitia katika lugha ya Kiswahili na kuwa na mafanikio makubwa hata kuifanya Tanzania kupewa Tuzo ya juu kabisa ya UNESCO ya Nadezhda K. Krupskaya (Bhola na Gomez, 2008). Ni mpango uliowezekana chini ya mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea ambapo watu wa umri mbalimbali, hususani wale ambao wakati wa ukoloni na mfumo kandamizi hawakuwa na bahati ya kusoma, walianza kusoma na kujua kuandika, wakifurahia elimu iliyopatikana vitabuni.
Moto na ari ya usomaji pamoja na kutaka kujua kuandika vilivishinda vizingiti vya ujinsia, umri, na hata usehemu – maana wazee wa vijijini na wa mijini walipata fursa sawa ya kujifunza kusoma kupitia katika programu ya Kisomo chenye Manufaa. Asilimia ya wale ambao hawakujua kusoma na kuandika katika sehemu kulikofanyika utafiti ilikuwa 27 mwaka 1977 na ikashuka hadi 21 mwaka 1981 (Bhola na Gomez, 2008:32). Kwa kiasi fulani, tunaweza kuyalinganisha mafanikio hayo ya miaka ya sabini na mafanikio yaliyopatikana katika Mradi wa Vitabu vya Watoto (miaka thelathini baadaye). Kwa mujibu wa Nadharia ya Thieta ya Walalahoi, madhumuni ya elimu hii yalikuwa ni kuwabadili watu, kutoka kuwa watazamaji tu wa usomaji, na kuwa watendaji. Mipango yote miwili, ule wa Elimu ya Watu Wazima, na ule wa Mradi wa Vitabu vya Watoto ililenga kuleta mabadiliko miongoni mwa watu.
Mwaka 2007 Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (CBP2 ) ulipata Tuzo ya UNESCO ya Usomaji, ijulikanayo kama “King Sejong Literacy Award” kutokana na mafanikio yake ya usomaji kwa watoto (taz. www.cbp.or.tz). Pamoja na mafanikio haya hata hivyo, leo hii Tanzania kwa ujumla wake, imerudi nyuma na kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika ikilinganishwa na kipindi hicho cha miaka ya sabini (UNESCO, 2015). Je, ni kitu gani kilichotokea hadi mpango huu na programu ya Kisomo chenye Manufaa ukafa? Je, tunawezaje kuunganisha mafanikio ya Elimu ya Watu Wazima ya miaka ya 70 (wazee) ambayo akina Bhola na Gomezi (wameshatajwa) wameieleza Tanzania kama mama wa uanzilishi wa shughuli zote za kusoma na kuandika katika Afrika (2008: 31); na mafanikio ya CBP ya mwaka 2007 (watoto); ili kuwa na maendeleo ya usomaji unaovuka kizingiti cha umri, jinsia na usehemu? Ikiwa maendeleo ya miaka ya 70 na yale ya 2007 yalipitia katika Kiswahili, tunawezaje kutumia maendeleo ya sasa ya teknolojia na vipengele mbalimbali vya utandawazi kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kimajumui itakayoleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi si kwa Tanzania tu, bali barani Afrika? Sasa Kiswahili si cha nchi moja tu, bali ni lugha pekee inayosimama na kuwa kielelezo cha Mwafrika kwa ujumla, ndani ya Afrika na hata nje ya Afrika. Tunawezaje kuufanya usomaji3 kupitia katika lugha ya Kiswahili uwe ni wenye kumkomboa Mwafrika kifikra na kiuchumi? Au kwa mujibu wa Boal, uwe usomaji wenye kuwaletea wasomaji mabadiliko, kutoka kuwa wapokeaji, hadi kuwa watendaji? Boal alitumia thieta ili kuwaonesha watu, jinsi ya kuamka na kujiletea mabadiliko. Mawazo yake aliyapitisha katika thieta ya umma ili kuleta maendeleo ya watu. Katika makala hii, tunachukua mawazo yake katika kuiangalia fasihi ya Kiswahili inavyoweza kuleta mabadiliko kwa Afrika nzima kwa kuzingatia mawasiliano yaliyomo ndani ya kazi za kifasihi.
2.0 Dhima ya Mawasiliano katika Kazi za Kifasihi Njia mojawapo ya usomaji wenye kulenga mabadiliko ni ile ya kusoma kupitia katika kazi bunifu za kifasihi. Kazi hizi zinaangaliwa kama miongoni mwa njia za mawasiliano katika jamii. Ni kupitia katika kazi kama hizi ambapo wanajamii “husomeshwa” ili wawe na mawazo fulani ama kuwahusu wao wenyewe, jamii zao au taifa lao na mataifa mengine. Kama tutakavyoona, “kusomeshwa” kunaangaliwa kama njia ya kumtazamisha mtu jambo au dhana fulani, kwa makusudi fulani yaliyo chanya.
Nadharia ya Thieta ya Walalahoi ya Boal (2008) inaonesha hatua nne zinazoelezeka kupitia katika thieta. Hatua ya kwanza ni ya kuujua mwili na uwezo wake, hatua ya pili ni kuufanya mwili ujieleze kwa kutenda matendo mbalimbali, hatua ya tatu ni kuifanya thieta iwe ni lugha yenye uhai au kitu kilicho hai wakati huo, na mwisho ni hatua ya thieta kama sehemu ya maongezi ambapo wahusika huongea ili kukamilisha wayatendayo (2008:102). Kiasi kikubwa cha mawasiliano ya kifasihi yatakayotumiwa katika makala hii ni yale yenye dhamira za ukombozi. Ni mawasiliano yaliyo katika kazi zilizolenga wasomaji wakomboke kifikra ili wao wenyewe waamue kwa hiari yao kupiga hatua na kujiletea maendeleo. Mawasiliano hayo yana hatua tatu: kujitambua, kufanya uamuzi na kujikomboa. Kwa mujibu wa Boal (2008) kazi kama hizi za fasihi ni silaha ya ukombozi; silaha inayowalenga walalahoi ili wajikomboe kifikra.
Nguvu ya ushindi katika harakati za miaka ya 70 kuhusu usomaji kwa watu wazima, iliungwa mkono na mawasiliano ya kifasihi yaliyowasilishwa yakiwa na dhamira ya kuwakomboa wasomaji. Katika mawasiliano hayo wajinga wasiojua kusoma walichekwa. Kuchekwa huko kulikuwa ni hatua muhimu ya kuwafanya wajitambue. Jamii ikajitahidi kuanza kusoma na “kufuta ujinga” ili jamii hiyo isiendelee kuchekwa. Hiyo ilikuwa ni hatua ya kufanya uamuzi. Kwa kuwa wanajamii walichukua uamuzi, hatua ya tatu ilifanya mawasiliano ya kifasihi yaliyojenga dhana ya kujikomboa kifikra. Akizindua suala la ukombozi wa kifikra kupitia usomaji, Mwalimu Nyerere alisema hivi kuhusiana na Elimu ya watu wazima:
Kwanza, ni lazima tuwaelimishe watu wazima. Watoto wetu hawatakuwa na athari katika maendeleo yetu kiuchumi kwa miaka mitano, kumi au hata ishirini ijayo. Fikra ya watu wazima kwa upande mwingine inazo athari sasa (Bhola, 1984:138).
Athari hiyo katika uchumi, ilimaanisha kuwa ni matokeo chanya ya watu waliojikomboa namna walivyotarajiwa kutenda katika kujiletea maendeleo. Dhamira nyingine ambayo ilichangia katika mafanikio hayo, ukiachilia mbali itikadi ya Ujamaa, ni ile ya kuukuza uzalendo – jambo ambalo liliwafanya waliokuwa wanajua kusoma na kuandika, kujitolea kusaidia wenzao ambao hawakubahatika kujua kusoma na kuandika. Licha ya uzalendo, wako waandishi kadhaa wa fasihi ya Kiswahili walioandika kazi za ukombozi kwa Mwafrika. Mawasiliano yenye dhamira hizo yanaweza kuonekana kwa mfano, katika kazi za tamthilia kama vile Tambueni Haki zetu (P. Muhando, 1973), Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi (E. Hussein, 1976), na Ngoma ya Ng’wanamalundi (E. Mbogo, 1988) yakilenga kumkomboa Mwafrika kutoka katika makucha ya kiukandamizaji, yakisisitiza kuwa ukombozi wa kweli huanzia katika fikra. Fikra inayosababisha mtu kujitambua na kisha kufanya uamuzi wenye urazini. Mawazo ya kujisaka na kujikomboa yamo pia katika kazi ya Pambo (P. Muhando,1975) na ile ya Amezidi (S.A. Mohammed,1995). Wahusika katika kazi hizo wanajenga maongezi na matendo ambayo yanamfanya msomaji afikirie mara kadhaa maana ya kuwa huru, kujitawala, vizingiti vinavyoletwa na ukoloni mamboleo, na vizingiti vinavyoletwa na watu binafsi au jamii katika nchi huru. Ukombozi mwingine ulioongelewa, ni ule wa kujikomboa kutoka kwenye minyororo ya mila na tamaduni kandamizi. Ukombozi dhidi ya manyanyaso na makandamizo ya kijinsia. Tamthilia za Wakati Ukuta (E. Hussein, 1970) na ile ya Kwenye Ukingo wa Thim (E. Hussein, 1988) ni miongoni mwa vielelezo vizuri dhidi ya mila potofu na kandamizi.
Sawa na tamthilia, kazi mbalimbali za riwaya ziliandikwa ili kumkomboa msomaji. Tukiziangalia riwaya za miaka iliyokaribia kupata uhuru, kwa mfano zile za Shabaan Robert zilizoukemea uovu katika jamii na kuutetea wema dhidi ya ubaya kama katika Kusadikika, Adili na Nduguze na hata riwaya za miaka ya tisini kama ile ya Ken Walibora ya Siku Njema, tunaona kuwa mawasiliano katika riwaya hizi yanalenga kumkomboa mtu kutoka katika mawazo ya uovu na kujenga jamii yenye wema na utengamano. Mawazo kama haya yamo pia katika kazi ya Mhina ya Mtu ni Utu. Kwa upande mwingine, riwaya za Kezilahabi kama vile Dunia Uwanja wa Fujo na Kichwamaji zilijenga dhana ya ukombozi katika ncha zake mbalimbali zikiendeleza pale alipoachia Shabaan Robert. Hizi ziliangalia kwa kina hali ya Tanzania na Mwafrika kwa ujumla baada ya kujitawala. Usomaji wa kazi kama hizi unamjengea msomaji na jamii kwa ujumla, fikra za kujielewa na kutaka kujikomboa. Katika riwaya pia, kulikuwa na harakati za kuhimiza ukombozi dhidi ya mila, desturi na tamaduni kandamizi na manyanyaso ya kijinsia. Riwaya ya Rosa Mistika (E. Kezilahabi, 1971) na ile ya Haki Haizami (A. H. Njama, 1995) zinasimamia vema mkabala huu.
Kazi za mashairi, sawa na tanzu za tamthilia na riwaya, zilijenga usomaji wenye kuhimiza ukombozi kwa Mwafrika. Ni kwa jinsi gani kwa mfano, tunaweza kuzitumia kazi za washairi kama za Kahigi na Mulokozi katika Malenga wa Bara (1995), na ile ya Kezilahabi ya Kichomi (1974) ili kuwafanya wasomaji wa leo wa Kiswahili kuwa na usomaji unaolenga kuwakomboa? Nchini Kenya mawazo ya Abdilatif Abdalla katika ushairi wake wa Sauti ya Dhiki (1973), ni kielelezo cha dhana ya ukombozi dhidi ya ubeberu na matawi yake katika nchi huru za Kiafrika.
Kwa hakika kujitokeza kwa fasihi ya Kiswahili barani Afrika kunaonekana pia katika baadhi ya kazi za tafsiri. Kwa mfano, kazi za fasihi za mwandishi maarufu wa Nigeria Wole Soyinka zimetafsiriwa kwa Kiswahili. Soyinka ni mmoja wa Wanafasihi maarufu aliyewahi kupendekeza kuwa lugha ya Kiswahili iwe lugha ya Umajumui ili iweze kuwaunganisha Waafrika, na itumike barani Afrika (Waliaula, 2013). Tamthilia yake ya Trials of Brother Jero iliyotafsiriwa kwa Kiswahili ikaitwa Masahibu ya Ndugu Jero (A.S. Yahya, 1981) ni ushahidi wa kutosha kuwa kupitia katika Kiswahili Waafrika wanaweza kujieleza kifasihi. Yale yanayozungumzwa katika masahibu yaliyomkuta Jero, ni mojawapo ya mambo yaliyozikumba nchi nyingi za Kiafrika baada ya kupata uhuru wa bendera. Masuala ya kukumbatia dini za kigeni, utapeli unaotolewa na baadhi ya viongozi wa kidini, uaminifu dhidi ya uwongo ni masuala jumuishi yanayojitokeza katika nchi nyingi za Kiafrika.
Mwandishi mwingine maarufu ambaye kazi zake za kifasihi zimetafsiriwa kwa Kiswahili ni Chinua Achebe. Baadhi ya kazi hizo ni kama vile No Longer at ease, iliyotafsiriwa na Adam, M.M. kuwa Hamkani si Shwari tena; Things fall Apart, iliyotafsiriwa na Clement Ndulute kuwa Shujaa Okonkwo; na A Man of the People, iliyotafsiriwa na Douglas F. Kavugha kuwa Mwakilishi wa Watu, kutaja tu kwa uchache. Katika kazi hizo, dhamira mbalimbali zinazozungumziwa zinaakisi yale yaliyotokea na yanayotokea katika nchi za Kiafrika kwa ujumla wake na wala si katika Nigeria pekee. Umajumui huu wa lugha ya Kiswahili haupo katika tafsiri za fasihi kutoka Nigeria tu, bali pia kutoka nchini Ghana kazi ya fasihi ya Ayi Kwei Armah ya The Beautful Ones Are Not Yet Born, ilitafsiriwa na Abdilatif Abdalla kuwa Wema Hawajazaliwa ikiongezea kuonesha ukuaji wa Kiswahili katika kuzieleza fasihi za Kiafrika, na yale yanayowasibu Waafrika.
Kutoka Afrika ya Kusini, mwangwi wa fasihi ya Alan Paton aliyeandika Cry the Beloved Country mwaka 1948 unajitokeza katika Ushairi wa Kezilahabi kupitia shairi lake la Namagondo II anapojiuliza maana ya uhuru:
“Watoto sasa wazee, mabinti mama wazima, Vichochoro nilivyovijua, vimekwishazibwa. Nimekuwa mgeni kijiji nilikozaliwa. Miaka yote ya uhuru imeleta nini Namagondo!” ( Karibu Ndani, 1988:39).

Kwa Kezilahabi, kuikumbuka Namagondo kijiji alichozaliwa na kupitia kwacho kutunga ushairi unaoeleza maana pana ya uhuru, kwa mtu, kijiji hata nchi, anaweza kulinganishwa na Nyerere alipoandika Tanzania, Tanzania! (1993) akiikumbuka nchi aliyoijenga na umoja wake alioupigania. Usomaji wa aina hii unakumbusha dhima pana ya fasihi kuwa, sio tu suala la kisanaa, lakini zaidi ukombozi wa binadamu katika mawanda yake yote.
Kwa ujumla, usomaji kupitia lugha na fasihi ya Kiswahili unaweza kuwaunganisha Waafrika, kuwafanya wajitambue, wachukue hatua na kujikomboa. Baada ya kuangalia dhima ya mawasiliano katika kazi za kifasihi, makala inajadili dhana ya elimu na usomaji. Kwa kufuata mawazo ya Boal, thieta haikuwa tu ni suala la elimu, bali elimu iliyomlenga mlalahoi na kumzindua aweze yeye mwenyewe kujiletea mabadiliko. Ndani ya kazi za kifasihi, kinachozingatiwa kwa nadharia hii, sio tu yale yaliyoandikwa au yanayosimuliwa, bali matokeo yake. Ni muhimu kusisitiza kuwa katika fasihi simulizi au andishi, wasikilizaji au wasomaji hawazingatii tu maneno na mapambo ya lugha, bali elimu iliyomo ndani yake na ambayo inalenga ukombozi. Kwa hiyo, katika kusoma kazi za kifasihi, lililo la muhimu ni kuunganisha elimu na usomaji ili kujiletea ukombozi. Sehemu inayofuata inajadili mawazo hayo.
3.0 Elimu na Usomaji Nchi au taifa lolote lile halijawahi kuendelea bila kuwa na maendeleo katika elimu. Hata hivyo, elimu sio lazima ipatikane vitabuni tu kama ambavyo wakoloni walipenda waliotawaliwa waamini. Ukweli huu ni mojawapo ya dhana muhimu zinazoangaliwa na makala hii wakati wa kujadili kuhusu ni kitu gani kinachosomwa. Kwa kusisitiza kuwa elimu hupatikana vitabuni tu, na humo ndimo muna maendeleo, wakoloni na mabeberu kutoka nje ya utamaduni wa lugha-simulizi waliliangalia bara la Afrika kama bara lisilokuwa na maendeleo yoyote kabla ya majilio na uvamizi wao. Kutokana na kudharau kwa makusudi na kuyabeza maendeleo yote yaliyokuwa yamefikiwa na Waafrika katika sekta mbalimbali, na labda kutokana na woga dhidi ya uwezo wa Waafrika, watawala wa kibeberu walifanya kila njia kuyafifisha maendeleo ya Afrika kabla ya usomaji kupitia vitabuni. Bila shaka, wakoloni na mabeberu hawa, hawakuweza kuufuta ukweli wa “wasomaji bingwa” kama mwanafalsafa Ogotommeli wa Mali ambaye hakujua maandishi, lakini kupitia katika masimulizi yake majuzuu kadhaa yaliandikwa kuhusu falsafa ya Kiafrika.4 Kwa mujibu wa makala hii, Ogotommeli alikuwa msomi na mwenye elimu. Hawakuweza mabeberu kuufuta ukweli wa elimu ya mzee Ogotommeli na ya Wadogoni wa Mali ambao bila ya kutumia vyombo vya kimagharibi kuhusu utafiti wa anga, walikwishakujua tangu zamani za kale, kuhusu mfumo wa sayari na nyota. Waliweza kujua hata mizunguko ya sayari na hata uzito wa baadhi ya sayari hizo miaka elfu nyingi kabla ya Masihi.5 Usomaji wa Wadogoni hao, ulikuwa usomaji uliowakomboa wao, kijamii na kielimu – nje ya ukuta wa maandishi; na kuyafanya maisha yao kuwa ni maisha yaliyojitosheleza kwa wakati wao na kwa kiwango chao. Ingawa, bado mabeberu hawakupenda kukubaliana na ukweli wa ujuzi huu.
Mabeberu hawakuweza kuufuta ukweli wa maendeleo katika teknolojia na sayansi ya ufuaji chuma hapa Watanzania katika miaka kabla ya Masihi (Chami, 1994; Schmidt, 1997). Au, ukweli kuwa hata leo wanasayansi mbalimbali bado wanastaajabia ujenzi wa piramidi za Misri. Haya yote yaliletwa na elimu ambayo sio lazima kwamba ilipatikana katika maandishi; na usomaji ulioletwa na wakoloni na wavamizi waliokuja kututawala kutokea nje ya Afrika. Kwa maneno haya ya utangulizi chini ya sehemu hii, makala inalenga kusisitiza kuwa elimu na usomaji ni zaidi ya yale yapatikanayo katika maandishi. Hata hivyo, makala hii itazungumzia elimu inayopatikana kupitia katika kusoma maandishi – maandishi ya kifasihi. Iwe katika vichwa na usimulizi, au katika maandishi, maendeleo ya kweli huja ikiwa nchi au taifa litawekeza katika elimu.
Ukipita katika shule za msingi mijini, na hata vijijini nchini Tanzania, utakuta vibao vinavyoitambulisha shule fulani vikiwa vimeandikwa kauli mbiu ya shule hiyo: kwa mfano “Elimu ni uhai”, “Elimu ni ngao”, “Elimu ni Maendeleo” n.k. Katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nembo yake inasema: Hekima ni Uhuru. Hekima inayozungumzwa hapa inatokana na elimu inayopatikana Chuoni hapo. Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kauli mbiu yao ni Elimu ni Nguvu (uwezo). Mifano hii michache inatueleza kuwa ili elimu ilete maendeleo, taifa husika halina budi kuwekeza sio katika kusoma kunakojali maandishi tu, bali usomaji wenye elimu itakayompa msomaji hekima, uwezo na nguvu ya kupiga hatua kifikra na kimwili; elimu itakayokuwa ni ngao ya jamii, elimu ambayo hatimaye italinda uhai na kuwapo kwa jamii; elimu ya ukombozi wa kifikra, kimwili na kimazingira. Usomaji huu wenye elimu hauna budi kuanza kabla ya shule ya awali – nyumbani katika familia, hadi ngazi ya Chuo Kikuu na kuvuka mipaka hiyo ukawa na maana katika maisha ya kila siku ya wanajamii. Kwa hiyo, swali hapa sio tu usomaji bali zaidi msomaji anasoma nini, na matokeo ya kusoma kwake ni nini.
Hebu tujiulize kwa pamoja maswali haya: masomo yanayotolewa katika ngazi mbalimbali yanasisitiza elimu ipi? Ndani ya usomaji unaoutarajiwa mna elimu gani? Ndani ya lugha itumiwayo kila siku katika maisha ya kawaida na katika kisomo mashuleni, mna elimu gani? Na je, elimu hiyo inamlenga nani na kwa nini? Maswali haya ni ya msingi ikiwa mtu anahitaji usomaji wenye kulenga ukombozi; na ukombozi ulio mkuu kwanza ni ukombozi wa kifikra. Fikra inayojadiliwa katika makala hii ni ile inayosisitiza kuhusu Umajumui wa Kiafrika.
Ikiwa mtu atajiuliza maswali haya leo, majibu yake yatatarajiwa kujenga wananchi wenye nguvu watakaojitegemea kesho. Mtu asipojiuliza maswali haya na kuyapatia majibu, itakuwa ni kama kuandaa mataifa yatakayokuwa na “utapiamlo wa kielimu” kesho. Leo haijapita. Bado upo muda wa kujenga, na mjengo huo kwa mujibu wa makala hii ni ule utakaoelekeza kupitia katika lugha ya Kiswahili kuelekea katika Umajumui wa Kiafrika.
4.0 Umajumui wa Kiafrika na Suala la Lugha Dhana ya Umajumui wa Kiafrika imefafanuliwa na watu wengi, ikiangaliwa kwa namna mbalimbali. Dhana hii inahusishwa na watu kama vile Kwame Nkrumah, Leopold Sedar Senghor, Julius Nyerere na Ahmed Sekou Toure. Hawa ni baadhi tu na huu ni mkondo mmoja tu wa mawazo kuhusu Umajumui wa Kiafrika. Mkondo huu uliangalia uwezo wa kipekee wa Waafrika na kupitia humo kuwa na azma ya kutaka kujitegemea. Ipo mikondo mingine inayouona Umajumui wa Kiafrika kama harakati za kupinga utumwa na kujitangazia utu wa Kiafrika; kwamba ni kupinga kutawaliwa na kubaguliwa kama Mwafrika; kwamba Umajumui hulenga kumaanisha umoja wa Kiafrika, n.k. (Adogamhe, 2008). Si lengo la makala hii kuingia kwa undani katika uwanja huu wa mjadala. Itoshe tu kusema kuwa Mazrui (1995) anauangalia Umajumui wa Kiafrika kama harakati zinazochochewa na sababu mbili. Kwa upande mmoja, anasema kuna Umajumui wa Kiafrika uliochochewa kwa kupinga ubeberu na kutaka kujikomboa, na kwa upande wa pili ni Umajumui uliolenga kuwa na muungano. Anasema kuwa, kwa Afrika, ule Umajumui uliolenga ukombozi ulifanikiwa ilihali ule wa muungano umeshindwa. Mazrui anaangalia kiini cha Umajumui duniani kuwa ni muunganiko wa hali ya ujinamizi na ndoto, raghba na idhilali. Kwa upande wa Ulaya, mafanikio ya Umajumui wake yaliletwa na vita kwa upande mmoja na ushairi kwa upande wa pili (Mazrui, 1995).
Kama Ulaya, Afrika pia kulikuwa na ushairi kama kichocheo kimoja cha Umajumui, na cha pili kikawa kupinga ubeberu. Hata hivyo, Mazrui anasema, Umajumui wa kweli kwa Afrika hauna budi kuachana na ulimbwende wa ushairi na wa kupinga ubeberu ili upige hatua kuelekea Umajumui wa kiuchumi utakaoongozwa na nchi za kusini mwa Afrika (ambapo anaelekeza mawazo yake katika SADC6 na nguvu inayoingizwa humo na Taifa la Afrika ya Kusini). Aidha anaona Umajumui wa kiutamaduni utakaoongozwa na nchi za Afrika ya Mashariki (ambapo anaiangalia lugha ya Kiswahili kama kiunganishi cha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Rwanda, Burundi, DRC, Msumbiji na Malawi). Anaangalia pia Umajumui wa kisiasa kupitia katika nchi za Afrika kaskazini na Umajumui wa kijeshi kupitia katika muungano wa ECOMOG7 wa nchi za Afrika magharibi. Ingawa hatukubaliani na mawazo ya Mazrui katika kuacha vita dhidi ya ubeberu, lakini tunayapanua mawazo yake katika kuangalia Umajumui wa Kiafrika kupitia katika lugha ya Kiswahili tukishadidia kipengele cha usomaji.
4.1 Lugha ya Kiswahili Wapo wataalamu kadhaa walioandika kuhusu umuhimu wa umoja wa lugha katika kujenga utaifa, au kinyume chake kuwa, kuyumbayumba kwa umoja wa lugha kunaweza kutoa mwanya wa kujipenyeza kwa watawala wa nje kupitia katika lugha zao. Mazrui (1998) anasema kuwa, kwa kuwa lugha za Kiafrika zilikuwa hazijaandikwa wakati wa uvamizi wa ukoloni, hazikutiliwa mkazo wa kuzihifadhi wakati ukoloni ulipoingia. Suala hili pia linagusa isimu ya lugha kwa ujumla likihusianishwa na utaifa. Simala (2003) anaona kuwa maingiliano ya wakoloni yalilenga kuvuruga mustakabali wa Afrika. Kwamba, walitaka Waafrika wajione kuwa masuala yao yalikuwa ni ya kishenzi, yasiyo na mbele wala nyuma, na kwamba walikuwa wanajichelewesha kwa kutokumbatia kwao haraka maendeleo yaliyokuja na ujuzi wa kusoma kupitia lugha za KiUlaya.

Simala (2003) anaangalia utaifa wa kiisimu kama itikadi muhimu ya Umajumui wa Kiafrika. Yeye anaangalia dhima ya wasomi na mchango wao katika kuufikia Umajumui wa Kiafrika. Anaona kuwa lugha ndiyo njia pekee ya kuwaunganisha wanajamii. Anamnukuu Cheikh Anta Diop8 , akisema kuwa ilikuwa ni muhimu kuwa na umoja wa kisarufi kupitia katika lugha tuliyoichagua ambayo itateuliwa kuwakilisha utamaduni, mila na jadi za Waafrika na ambayo itaweza kupambana na mila za kiulimwengu. Bila ya lugha kama hii, umoja na Umajumui wa Kiafrika utakuwa ni ndoto tu. Kwamba, lugha za Ulaya hazipaswi kuonwa kama almasi ambazo zinatuvutia kama nondo motoni. Ni lazima tuyaelekeze mawazo na mustakabali wetu katika maendeleo ya historia yetu. Simala anaendelea kusema kuwa lugha ya Kiswahili ndiyo inayobeba sifa za kuwa lugha wakilishi na ambayo inabeba dhana ya Umajumui wa Kiafrika. Ikiambaa kutoka katika pwani ya kusini mashariki mwa Somalia, inazungumzwa hadi kaskazini mashariki mwa pwani ya Msumbiji ikishabikiwa na watu wa Malawi, Zambia, kusini mwa Sudani, na Ethiopia (Simala, 2003). Lakini swali kuu hapa ni je, hawa wote wasomapo, husoma kuhusu nini? Ni maneno gani au lugha gani ambayo wananchi kutoka katika nchi zinazozungumza Kiswahili na hasa vijana ambao wana wajibu wa kuendeleza umuhimu wa Umajumui wa Kiafrika husikia kupitia katika lugha hii? Kipengele hiki cha lugha na jinsi inavyozungumzwa na yale inayoyawakilisha ndicho mjadala unaofuata.
4.1.1 Usomaji upi kupitia katika Lugha? Ili mtoto akue akipenda na kufurahia kusoma, hana budi kuanzia nyumbani. Yale mazingira ya hadithi simulizi yaliyokuwa yanamkuza tangu kale sasa yanachukuliwa na maandishi na vifaa vya kielektroniki. Ila je, ni maandishi au simulizi zinazomjenga kwa fikra gani? Kwa vyovyote vile usomaji wa miaka ya sitini na sabini haitakuwa sawa na usomaji wa miaka ya hivi karibuni ambapo teknolojia imeingiza katika jamii mapinduzi makubwa ya vifaa vya mawasiliano. Maendeleo ya teknolojia kwa sasa yanawafanya watoto na vijana kupenda kusikiliza zaidi elimu na usomaji kupitia katika vyombo vya teknolojia ya kisasa. Leo hii wanafunzi wengi wanavutiwa zaidi na vifaa vya usomaji kama vile Kindle, iPod, iTeacher, YouTube, n.k. Humo ndimo munamopatikana maarifa yanayowavutia watoto na vijana wa kizazi hiki. Je, ni jinsi gani Waswahili – wanaweza kutumia teknolojia hii ili kuhimiza usomaji unaoelekeza Umajumui wa Kiafrika? Labda suala la teknolojia lingekuja katika hatua ya pili. Katika hatua ya kwanza ni vema kujiuliza maswali haya: Ni mambo gani yawemo katika usomaji wa watoto ili kuwafanya waweze kuutetea na kuukamilisha Umajumui wa Kiafrika? Kwa ngazi ya taifa, ni jinsi gani wananchi wanaweza kuurudisha utaifa na uzalendo uliokuwapo miaka ya 1970? Maana ni ndani ya uwelewa huo, wananchi wa nyakati hizo walifanikiwa hata kuendesha Kisomo Chenye Manufaa. Uzalendo huo kwa sasa umo mashakani. Ikiwa watu si wazalendo, – wakalipenda taifa lao – hawawezi kutarajiwa kuwa watetezi wa Umajumui, wakalipenda bara la Afrika.
Kulipenda bara la Afrika na kuutetea Umajumui wa Kiafrika, kunaanzia nyumbani au taifani katika vitu vya kawaida katika usomaji. Kwa mfano, leo hii kupitia katika simu za viganjani, wananchi wengi wanapokea ujumbe kuhusu “namna ya kupata na kufuatilia ligi ya Uingereza au Ujerumani au Italia.” Tena ujumbe hausemi ligi ya Uingereza. Unasema ligi ya United Kingdom. Ni hali ile ile ya kasumba, na kujidharau, sasa inapitishwa katika usomaji wa ujumbe mfupi mfupi. Mpokeaji wa ujumbe kama huu, hatarajiwi apende na kufuatilia ligi za Kiafrika, achilia mbali ligi za hapa nyumbani Tanzania. Anahamasishwa kumwabudu, kumpenda na kumtukuza mkoloni: Mwingereza, Mjerumani, Mfaransa n.k. Ni kama alivyoandika Ebrahim Hussein katika tamthilia ya Mashetani. Shetani anamwuliza, – au katika muktadha huu, anamsomesha binadamu: “Je, unanicha? Unaniogopa? Unanisujudia? Unaniabudu? Mbona sioni kunicha kwako, kuniogopa, … kunisujudia, kuniabudu? Nionyeshe jinsi unavyoniabudu…” (Mashetani, 1971:4-5). Hayo ndiyo tunayowasomesha wananchi wetu. Labda haitakuwa haki tusipojihakiki sisi wenyewe. Wasomi katika maeneo mbalimbali nao pia wamejikuta wanaingia katika kumwabudu beberu kupitia katika usomaji. Maneno tunayotumia, majina na misemo ni ya kujidhalilisha, kujifanya tu wadogo mbele ya “wakubwa wazungu”, “Wakubwa” hawa walikuja na majina na dhana mbalimbali za kishenzi kuhusu bara la Afrika.
Zamani, Afrika liliitwa “bara la giza”, “bara la washenzi”. Vitabu vilivyoandikwa Ulaya na Amerika viwe vya kifasihi, kihistoria au kianthropolojia– vikiandaa ujio wa wakoloni, vilisomwa vikiwa na lugha hiyo. Hii ilikuwa katika karne za kumi na nane na kumi na tisa. Ni kwa jinsi gani huu “ugiza” umepungua au kwisha kabisa? Na kuitwa “bara la giza” ilimaanisha nini kwa msomaji kutoka ndani ya Afrika? Ni giza lipi? Katika mikutano ya dini, wahubiri waliokuja kwa minajili ya kuandaa ukoloni, walitafsiri walivyotaka wao na kusisitiza yale yaliyoandikwa katika Biblia wakisema: “Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu; nao waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia (Mathayo 4:16). Tafsiri potofu ya wahubiri hawa, iliwaingia na kuwapumbaza baadhi ya Waafrika, wakajiona wamo gizani na wanahitaji kupewa au kusomeshwa ili wapate nuru kuu. Pamoja na usomaji wa aina hiyo uliopumbaza, maneno yaliyotumika kwa kuliita bara la Afrika, miongoni mwake kama tulivyoonesha, yalikuwa: Afrika ni “Bara la washenzi”. Ushenzi ni nini, na kwa nini kuitwa washenzi? Ni kwa jinsi gani huo “ushenzi” uliopachikwa umeondoshwa? Baadaye kidogo, yale yaliyoandikwa na kusomwa kuhusu bara hili, yalisema kuhusu “bara la magonjwa”; Bara la vifo visivyo vya lazima – vifo vya kishenzi; Bara la uchafu, n.k. Kutokana na kuandikwa na kusomwa hivi, Waafrika waliokuwa wakisoma walifanywa kujiona “wachafu”, wajinga, wenye magonjwa na walio katika giza kuu. Giza lenye kuleta ushenzi. Na hapo wakajitahidi kujitoa katika alama hizo bila kujua kuwa waliingizwa humo kwa makusudi na kwa nia maalumu. Katika Ensaiklopedia ya Mtandaoni iitwayo: Wikipedia, inaandikwa kwamba, liliitwa ‘bara la giza’ kwa vile kwanza yale yaliyokuwa yakitendeka ndani ya bara hilo, hayakujulikana nje ya bara lenyewe, na hasa kujulikana kwa watu wa Magharibi, lakini pia wengi wa wenyeji wa eneo lililosemwa kuhusu ugiza huo, walikuwa na ngozi nyeusi. Anaongeza kusema, kwa sasa, jina hilo (au usomaji wa aina hiyo) limeachwa na kwa hakika linaposemwa huchukuliwa kuwa ni kashfa au tusi. Aidha, inaendelea kuandika kuwa jina hilo lilikuwa halisemi ukweli wote, maana Waafrika wenye ngozi nyeusi ni wenyeji pia wa Afrika kaskazini, sehemu ambayo haihusiki linapozungumziwa eneo hili la bara la giza. Hata leo inawezekana kuna Waafrika ambao bado wanajiona kama waliomo katika ugiza huo, au ushenzi huo. Mojawapo ya jambo linaloshadidiwa hapa na ambalo linashikiliwa hata na wasomi leo hii, ama kwa kujua, lakini nadhani zaidi, kwa kutojua, ni dhana ya, au jina la “Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.” Haikutosha kuiona Afrika, kuisoma kupitia katika magonjwa, leo hii tunashawishika tuione kupitia katika jangwa.
4.1.2 Dhana Potofu ya Usomaji wa “Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara” Lililoandikwa hudumu. Yako mataifa na jamii nyingi ambazo huwa na mapungufu kadhaa na udhaifu wenye kuleta changamoto kwa maendeleo ya mwanadamu. Hata hivyo, udhaifu wao, hausomwi na kusemwa hadharani kuwakilisha utambulisho na utaifa wao, au Umajumui wao. Nchi ambazo huongoza kwa vifo na magonjwa ya moyo, haziitwi nchi za “magonjwa ya moyo.” Nchi ambazo zinaongoza kwa magonjwa na taabu ya unene au kansa, haziitwi nchi zilizogubikwa na magonjwa ya unene au kansa. Binadamu wa kawaida, hamwoni binadamu mwenzake kupitia katika udhaifu au tabu yake, achilia mbali tabu au udhaifu wa kulazimisha. Kwanini iwe kwa Afrika? Leo hii watu wengi wanaitumia dhana ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, bila ya kujali na kujua maana yake, kashfa na dharau yake. Iliposemwa “Afrika ni bara la giza” ilichukua muda mrefu Waafrika kulikataa jina hilo. Ilipokubalika kuwa yalikuwa makosa kuwasomesha watu kwa kuwaonesha dharau, kashfa na kuwatukana, jina lilibadilika. Utambulisho huo wa ugiza ukafutika. Ubatizo mpya ukafanywa, na kukuzwa sana hasa katika kazi za kifasihi kuanzia miaka ya sabini. Si zamani sana ambapo jina la “Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara” lilianza kutumika kumaanisha eneo lile lile lililoitwa wakati wa majilio ya wakoloni: “Bara la giza.” Kabla ya wakati huo, eneo hili lilikuwa na majina mengine mojawapo likiwa ni “Afrika isiyo ya Waarabu” au “Afrika kusini mwa Arabia” (Allen, 1959:5). Je, jina la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara linaleta dhana gani katika usomaji?
Mwandishi wa masuala ya utamaduni na mtengenezaji wa filamu, Owen Alik Shahadah anasema kuwa jina hili la “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara” lina mizizi yake ndani ya ubaguzi wa rangi. Hakuna mipaka ya kijiografia au ya kisiasa au hata ya kihistoria inayoweza kuoneshwa kumaanisha eneo hili. Anasema: “Istilahi: ‘Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara’ ni zao la ubeberu wa Ulaya, ni neno linalomaanisha Waafrika wasioendelea, eneo ambalo hakuna maendeleo na ndio maana tunasikia wakisema: hakuna lugha iliyoandikwa iliyochipuka Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, Misri sio sehemu ya Ustaarabu wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara….” (Shahadah, 2005:Sura 5). Maneno kama hayo anayasema pia mwanazuoni Chika Onyeani (2009). Lakini ni nini hasa kiini cha haya? Ilioneshwa pale mwanzoni kuwa, usomaji unahusisha usimulizi na maandishi katika kuleta elimu. Ilijadiliwa kuwa, usomaji wa usimulizi wenye elimu ulikuwapo Afrika hata kabla ya usomaji wa maandishi uliokuzwa hasa baada ya mapinduzi ya viwanda na kuvumbuliwa kwa mashine za maandishi kama sehemu ya kutanuka kwa ubeberu. Mashine – kwa muktadha huu, ziliyaboresha tu maandishi na kuyafanya kuenea kwa kasi. Kwa kuwa eneo la Mesopotamia na Misri kulikuwa na maandishi ya kale, basi eneo la Misri linasemwa kuwa sio la Afrika. Maana “ustaarabu wa maendeleo haya ya mashine haukuwapo sawa na ule wa mapinduzi ya viwanda. Au hata ikionekana kuwa suala la muhimu ni kuwapo kwa maandishi, ukweli ambao unafafanuliwa na tafiti za kisayansi kuwa Misri kulikuwa na maandishi, basi inasemwa, Misri si Afrika; walau sio “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.” Na jambo hili linasomeshwa kwa mkabala huo. Hatimaye, ndani ya kusomeshwa huku leo, hata nchi ya Afrika ya Kusini inasemwa kuwa haiko ndani ya “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.” Basi, eneo hili linalolengwa, sasa linabakia kuitwa “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara lakini kaskazini mwa Limpopo” ili kuiondoa Afrika ya kusini katika eneo linalozungumzwa.
Lakini, kwa ‘bahati mbaya’ nchi za Lesotho na Swaziland “zinaharibu” maana ya majina kama haya kwa mtazamo huo wa kibeberu. Kwa kifupi, majina ya kijiografia yaliyokuwa yakitumika kama vile Afrika ya Kitropiki, au Afrika ya Kiikweta, yaliachwa kwa makusudi ili Waafrika waendelee kusomwa na kujulikana kupitia katika dhana hasi: dhana za magonjwa, vita, njaa; na ikishindikana kabisa, basi dhana za jangwa na ukame zitumike: kusini mwa jangwa. Na baadhi ya wasomi wa leo wanajikuta wakitumia dhana hii katika maandishi yao na kudidimiza kabisa ukombozi wa kifikra. Baadhi wanaisomesha dhana hii na kuzidisha ufukara wa fikra. Wanasaliti hatua za kishujaa za usomaji wa usimulizi uliofanywa na bibi na babu zetu wakilenga kuinua maendeleo katika jamii mbalimbali za Kiafrika. Usomeshwaji huu na upotofu mwingine unaolenga kumdidimiza Mwafrika unapatikana pia kupitia katika fasihi na maandishi bunifu mengine.

4.1.3 Dhana Potofu kupitia katika Usomaji wa Fasihi Mara baada ya wakoloni (Waingereza) kuona kuwa hawana budi kuondoka katika makoloni yao, juhudi kubwa ilifanywa ya kusambaza kasumba ya kuendelea kumwabudu Mwingereza kupitia katika lugha ya Kiingereza. Juhudi hizi zilikwenda sambamba na kupiga vita kwa njia mbalimbali lugha za Kiafrika. Lugha ya Kiswahili ilikumbana na dhoruba ya kipigo hiki katika Afrika Mashariki. Mtafiti wa lugha na utamaduni wa Kiswahili bwana Allen (1959:5) anaandika hivi kuhusu hali ilivyokuwa: “Kwa muda wa miongo miwili iliyopita, mwelekeo rasmi na fikra kuhusu Kiswahili imeendelea kuwa ni ya kuidharau na kuipuuza lugha hii, na kuishusha hadhi ionekane kama mojawapo ya vilugha vya kienyeji ambavyo matumizi yake ilifikiriwa kuwa yatapotea kutokana na kuenea kwa ufahamu wa lugha ya Kiingereza” (Tafsiri ya Mwandishi). Fikra kama hizi zilionekana pia katika maandishi ya kifasihi:

Mojawapo ya vitabu vya zamani kuwa na lugha na usomaji wenye kujenga fikra hasi ni kile cha Henry Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman (Mtafsiri Frederick Johnson, 1948). Tafsiri ya kitabu hiki inatokana na kitabu cha mwanzo kilichoandikwa kwa Kiingereza kikiitwa” King Solomon’s Mines (1885). Mwaka huo ni muhimu kwa Waafrika maana ndipo bara la Afrika lilipogawanywa vipande vipande na wakoloni wakajitwalia kila mtu eneo apendalo katika Mkutano wa Berlin wa Novemba 1884 hadi Februari 1885. Maelezo yaliyomo yanaendana sana na kitabu cha pili kilichofuatia kilichojulikana kama Allan Quatermain (1887), vyote vya mwandishi yule yule. Tunasomeshwa kupitia katika utanzu huu wa fasihi kuwa Mwafrika ni kiumbe mshenzi, asiyestaarabika ilihali mtu wa Magharibi, Mzungu, ni mtu mstaarabu. Kwamba; Mwafrika ni mtu wa uchawi na Mzungu mtu wa sayansi. Kwamba; Mwafrika ni mtu wa kushindwa na Mzungu ni mtu wa kufaulu kila wakati. Katika safari za Quatermain katika maeneo ya Afrika ya kusini kupitia nchi za Swaziland na Lesotho hadi Zimbabwe ya leo, tunasomeshwa kwa njia ya fasihi hizi “ushenzi” na “uchawi” huo na udhaifu unaoambatana nao kwa upande mmoja, na “ustaarabu”, sayansi na “utu” wa wazungu na nguvu zao kwa upande mwingine. Katika mwangwi wa dhamira kama ya Mashimo ya Mfalme Sulemani, tunaoneshwa miaka ya karibu na uhuru hadi kupata uhuru, jinsi Waafrika walioanza kuandika vitabu walivyofuata mkondo huo bila kujijua. Katika nchi za Afrika Mashariki zilizotawaliwa na Mwingereza, kazi za miaka ya mwishoni mwa 1950 tunasomeshwa kuhusu Waafrika wasiojua Kiingereza na wanaoonekana kuwa “washamba” wakichekwa. Tamthilia za mwanzo ziliwacheka watu wa aina hiyo, na baadhi ya riwaya zikawajenga kwa kuonesha udhaifu na kushindwa kwao, kwa vile hawakufanana na Wazungu. Uzungu ukawa unatukuzwa ilihali Uafrika, ukionekana ni ushenzi, ukidhalilishwa. Likapatikana kundi la Wazungu weusi kama Martin Kayamba ambaye alijibadili jina na kujiita Kayambason ili lifanane angalau kama la Waingereza. Katika tamthiliya ya Martin Kayamba (Uhinga, G. 1968) mhusika anajipambanua na uzungu, lakini kutokana na mwamko wa miaka ya mwishoni mwa sitini, anachekwa kwa kuukana Uafrika wake.

Majina ya kuongeza “son” mwishoni mwa majina ya Kiafrika ni kasumba ile ile iliyoletwa na wakoloni kupitia katika maandishi yao. Ni kasumba ile ile inayojitokeza leo katika maandishi ya “Afrika kusini mwa jangwa la Sahara”, Afrika ya bara la giza, na Afrika ya magonjwa. Taratibu umma wa Waafrika unasomeshwa bila kujua kujitambua kupitia katika majanga, magonjwa na mambo yaliyo hasi; na baadhi yao, kama Martin Kayamba, wanaongeza “son” ili kuonekana wazungu, waliostaarabika. Jambo hili halina budi kukataliwa kabisa. Usomeshwaji wa aina hii na maandishi ya aina hii yanayofukarisha fikra za Waafrika hayana budi kupingwa kwa nguvu zote. Lakini je, sasa kifanyike nini ili usomaji uwe wenye kuleta manufaa na kujenga Umajumui wa Kiafrika? Ifanyike nini leo, ili kuyaweka pamoja mafanikio ya miaka ya 70 ya mpango wa Kisomo Chenye Manufaa yaliyopitia katika Kiswahili; na yale ya majuzi ya Mradi wa Vitabu vya Watoto (kwa ajili ya kuinua usomaji) ambayo nayo yaliwezeshwa na Kiswahili, ili wasomaji wa leo waweze kufaidika na kuwa na usomaji wenye kuleta maendeleo?
5.0 Hitimisho: Usomaji wa Sasa Makala hii, haikutoa majibu kwa maswali yote yaliyoibuliwa. Maswali hayo yanabaki kuwa kichocheo cha fikra na mijadala ya baadaye. Hata hivyo, kizazi cha sasa hakina budi kuamka, kujitambua na kubadilika ili kuwezesha Umajumui wa Kiafrika kufanikiwa na Waafrika kujiletea maendeleo yao wenyewe. Ikumbukwe kuwa, mojawapo ya dhima za mawasiliano kupitia katika tanzu za fasihi miaka ya 70, hapa Tanzania ilikuwa ni kuhamasisha Kisomo cha Watu Wazima. Kupitia katika Kiswahili, tanzu za fasihi kama vile nyimbo zilitungwa, mashairi yakaimbwa, tamthilia zikaandikwa na sanaa za uigizaji zikaigizwa majukwaani – miongoni mwa mambo mengine, ilikuwa ni kwa ajili ya kuhamasisha watu kusoma na kuandika. Leo hii, na kwa mujibu wa nadharia ya Boal ya thieta ya walalahoi, kunaweza kufanyika mashindano ya tanzu kama hizi na watunzi wakapewa suala moja tu kuliandikia: usomaji kwa maendeleo ya Afrika. Tanzu mbalimbali zikashindana kwa kutunga na kuonesha ubunifu wa wasanii, zikilenga dhamira moja tu-Usomaji.
Kisha, kazi hizo zikatumika kuhamasisha watu wengi katika jamii mbalimbali kupenda kusoma kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Lakini, ili jambo hilo lionekane lenye kuwa na tija, halina budi kutumia yale yaliyomo katika jamii husika na hasa kwa kutumia lugha yenye uasili wa kijamii au inayokaribiana nayo.
Katika jamii nyingi zenye asili ya Kibantu, Kiswahili kiko karibu nazo zaidi kuliko Kijerumani, Kifaransa au Kiingereza. Katika jamii za Kiafrika, Kiswahili na mizizi yake katika asili, kiko karibu nazo zaidi kuliko lugha za Magharibi. Haina maana hata kidogo leo, kuandika hadithi kuhusu utamaduni wa Uingereza au Ujerumani au Marekani na kumsomesha mtoto wa Kiafrika. Haiyumkiniki kuwa na usomaji wenye kulenga maendeleo na hasa ukombozi kwa mtoto wa Kitanzania kumjengea fikra za hadithi za Kiingereza ilihali yeye analala na kuamka akiwa Afrika, Tanzania. Hili linafanana na mfano kuhusu lugha na ujumbe katika simu za kiganjani. Linalofanyika kwa taratibu ni kuing’oa mizizi ya utu wa mtu. Kumtoa mtu kwao, na kumpeleka pasipo na makao. Hatimaye hatajua au kuona atokako, wala hataona aendako. Kitakachobaki hapo, ni kushikwa mkono ili apelekwe mahali asikojua, maana yeye haoni tena. Yako mambo mengi katika jamii zetu yenye maana kubwa kwa wanajamii na ambayo ikiwa kupitia katika Kiswahili, yataandikwa kisanii yatavuta macho, usikivu na hamu ya kusoma kwa wanajamii. Usomaji wa fasihi kama huo ni usomaji wenye maana na wenye kulenga maendeleo.

Kutoka katika hadithi za kale na masimulizi ya wahenga zinaweza kutungwa hadithi za Kiswahili zikitumia mbinu za kisasa. Zinaweza kutungwa nyimbo, mashairi, tamthilia n.k zenye kuwa na maana na zinazohusiana na jamii zetu. Kutoka katika usimulizi, mashairi na nyimbo za Wafulani, Wayoruba au Wahausa wa Afrika Magharibi, hadi tanzu kama hizo za fasihi kutoka Wahabeshi wa Ethiopia, Wasomali au Wasudani hadi tanzu za kifasihi za Afrika ya kati na kusini katika nchi za Malawi, Zimbabwe, Namibia, Swazilandi, Botswana tukitaja kwa uchache tu. Afrika imejaa utajiri wa kifasihi ambao unaweza kulikomboa bara hili. Utajiri wa kifasihi ambao ukisomeshwa na wasomeshaji wazalendo, watoto wa bara hili wataunganishwa kwa pamoja na kuwa na nguvu na sauti moja kupitia katika lugha ya Kiswahili.
Tamthilia na hadithi kama hizi zinaweza kuwekwa katika redio na runinga na zikasimuliwa katika mashule katika nchi mbalimbali. Zinaweza kuwekwa katika maandishi ili zisomwe miaka na miaka kwa vizazi vingi vijavyo. Katika Tanzania, miaka ya 70 kulikuwa na redio moja tu iliyosikika mahali pote (Radio Tanzania Dar es Salaam – RTD), iliyokuwa na vipindi vya mashuleni, ikihamasisha wanajamii. Leo hii kuna redio nyingi zinazoweza kuchukua jukumu hili, na kwa wale ambao wanaweza kupata televisheni, wanaweza kusikia na kuona hadithi, masimulizi na tamthilia zinazobeba yale wanayoyajua na kuyafahamu, kwa lugha wanayoijua na inayokaribiana na wanayoijua kwa uasili. Yanayosimuliwa, watayaona kwa njia ya kisanii, wakiyafurahia na yakiwajenga kifikra na kuwaletea maendeleo au yakitoa changamoto kifikra. Kwa wale wakaao mijini na wanaokwenda na usasa-magharibi, nyimbo na tanzu nyingine za kifasihi zinaweza kuwekwa katika vifaa vya kisasamagharibi vinavyopendwa siku hizi kama vile iPod, iPad, Kindle na aina zote za MP. Hii itawafanya vijana kuzipenda maana wanakwenda na muktadha wa wakati wao. Elimu kupitia katika lugha ya Kiswahili itakuwamo ndani ya vifaa vya kisasa ambavyo wanavipenda na kuvitumia. Kanda za kunasia picha zikisambazwa mashuleni na vyuoni zikiwa na dhamira na ujumbe maalumu, wanafunzi wataangalia na kuhamasishwa. Kupitia katika mtandao: kuna YouTube, na iTeacher ili walio na uwezo kuingia katika mkondo huo wafaidike na kuhamasishwa kwa njia hiyo.
Uhamasishaji utandae na kuelekea vyuoni na mashuleni ambapo mashindano ya usomaji wenye mwelekeo huu yanaweza kufanyika. Kwa mfano, leo hii kuna vipindi vya mashindano baina ya vyuo ambapo wanafunzi hushindanishwa kupima ujuzi wao wa mambo mbalimbali. Kipindi hiki kinaweza kupanua wigo na kulenga katika kukuza usomaji, msisitizo ukiwa uzalendo na Umajumui wa Kiafrika utakaopitia katika lugha ya Kiswahili. Maswali yanaweza kulenga waandishi na kazi zao, kuhusu maisha ya waandishi hao, na yale waliyoyatetea katika jamii; kuhusu namna mbalimbali za kujenga na kukuza Umajumui. Hapo jamii zitakuwa zinapiga hatua kuelekea katika kurudisha na kujenga uzalendo, ambayo ni hatua moja kubwa kabla ya kufikia Umajumui wa Kiafrika. Haya yanaweza kufanyika katika mpango wa majimbo ya lugha za Kiswahili.

Majimbo ya lugha za Kiswahili ni dhana inayolenga kuhamasisha ukuzwaji wa Kiswahili katika nchi mbalimbali. Kuna Kiswahili sanifu ambacho kinaweza kukutwa katika maandishi rasmi. Lakini pia tutambue kuwa kuna Kiswahili tofauti tofauti katika nchi zetu. Massamba anasema: “…kabla ya kuanzishwa kwa Kiswahili sanifu na wakoloni, jina la lugha ya Kiswahili lilikuwa likitumika tu kama jina jumuishi likiwa na maana ya lugha mbalimbali za pwani zilizokuwa na uhusiano wa karibu sana…” (2002: 257). Hapa ndipo dhana ya umajimbo inapoibuka. Kwa mfano wale wanaokaa katika DRC wana Kiswahili ambacho kinachimbuka kutoka lahaja mojawapo ya Kiswahili. Inawezekana hawa na wale ambao wanazunguka eneo hili kama vile Zambia na magharibi mwa Burundi na Rwanda wakashadidia Kiswahili hicho na kukikuza kimsamiati na kimatumizi, na hivyo kukafanyika kuwa hilo ni jimbo moja la lugha ya Kiswahili. Kiswahili kama hicho kwao, kitakuwa na maana na kitakuwa karibu zaidi na lugha za Kilingala, Kinyanja, Kibemba Tshiluba, Kirundi, Kinyarwanda, n.k. Katika maeneo ya kusini mwa Afrika kutokana na sababu za vita vya ukombozi kuna wasemaji wa Kiswahili ambao wametawanyika katika nchi za Namibia, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Afrika ya Kusini yenyewe. Hawa wakiungana na wale wa Botswana na Malawi wanaweza kuwa na jimbo jingine la lugha ya Kiswahili. Kiswahili chao kitakuwa na ukaribu na lugha zao kama Kitswana, Kimbundu, Kikongo, Cichewa, Kishona, Sizulu, n.k. Kutokea kusini mwa Somalia na Ethiopia litaibuka jimbo la lugha ya Kiswahili litakaloungana kukiimarisha Kiswahili cha eneo hilo, hicho kikawa na maana, kwa kuwa ki karibu na Kijareer au Kigosha. Hatimaye eneo lote la Afrika ya kati kuanzia kusini mwa Sudani, Afrika ya Kati yenyewe, hadi kusini mwa Afrika kukawa na majimbo ya lugha ya Kiswahili ambayo yatajipambanua kwa tofauti chache za misamiati. Kazi ya kutafuta usanifu wa lugha hizi inaweza kufanyika baadaye ikiwa ni lazima.
Viko vyuo na shule zinazofundisha Kiswahili kule Afrika Magharibi na Afrika Kaskazini. Watumiaji wa lugha hii huko, wanaweza kufanya umoja wa kijimbo na kuendeleza lugha hii wakitumia mbinu zilezile hamasishi ili kukikuza Kiswahili kama lugha ya Umoja wa Kiafrika. Jambo hili likishadidiwa na hasa kuwa na utashi wa kisiasa wa viongozi mbalimbali wa Kiafrika, linaweza kuwa ni mwanzo wa safari inayowezekana ya usomaji wenye manufaa, na unaolenga maendeleo kwa bara la Afrika kupitia katika lugha moja- Kiswahili. Jambo la muhimu na la kusisitiza ni yale yanayokuwamo katika lugha hii jumuishi; yale yanayosomeshwa ni lazima yawe ya kuleta ukombozi kifikra.
Marejeleo
Adogamhe, P.G. (2008). Pan-Africanism Revisited: Vision and Reality of African Unity and Development. African Review of Integration, Juz. 2 na. 2, July 2008: 1-34.
Allen, J.W.T. (1959). Editorial in Swahili Bulletin No. 30.
Bhola, H.S na Gomez, S.V. (2008). Signposts to Literacy for Sustainable Develoment:
Complementary Studies. Hamburg: UNESCO Institute for Lifelong Learning.
Bhola, H.S. (1984). “The Tanzania Mass Literacy Campaign 1971 – 1981”. Katika
Campaining for Literacy: Eight National Experiences of the Twentieth Century,
with a Memorandum to Decision Makers. Paris: UNESCO.
Boal, A. (2008). Theatre of the Oppressed. London: Pluto Press.
Chami, F. A. (1994). The Tanzanian coast in the first millennium AD. Archaeology of the
Iron Working, farming communities. Katika Studies in African Archaeology Na. 7.
Uppsala: Societas Archaeological Upsaliensis.
Gérard, A.S na Vajda, G.M. (wahr) (1986). European-language Writing in subSaharan
Africa. Budapest: Akademia Kiado.
Haggard, R. (1948). Mashimo ya Mfalme Suleiman. Nairobi: Longaman Kenya Ltd.
Kezilahabi, E. (1988). Karibu Ndani. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi: The Jomo
Kenyatta Foundation.
Mazrui, A. A. (1995). “Pan-Africanism: From Poetry to Power” Issue: A Journal of Opinion,
Vol. 23, No. 1, African Studies (Winter – Spring), pp. 35-38. African Studies
Association. http://www.jstor.org/stable/1166980: Imesomwa Julai 29. 2016.
Mazrui, A.A na Mazrui, A.M. (1998). The Power of Babel: Language and Governance in
the African Experience. Chicago: University of Chicago Press.
Nyerere, J.K. (1993). Tanzania Tanzania, Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Onyeani, C. (2009). “Contemptuousness of Sub-Saharan Africa.” Makala ya Mkondoni.
Schmidt, P. R. (1997). Iron Technology in East Africa: Symbolism, Science and
Archaeology. Indiana: Indiana University Press.
Scranton, L. (2006). The Science of the Dogon: Decoding the African Mystery Tradition
Inner Traditions. Vermont: Rochester.
Shahadah, A. O. (2005). “Linguistics For a New African Reality.” Makala ya Mkondoni
mwa Januari 23. 2016.
Simala, K. I. (2003). “Pan-Africanism and the Language Question: Re-Reading African
Cultural and Intellectual History” CODESRIA 30th. Anniversary Conference.
Dakar, Senegal: Swala Publications.
Udobata, R. na Onunwa, U. R. (2010). A Handbook of Methodologies of African Studies.
Pittsburgh: Red Lead Press.
Uhinga, G. (1968). Martin Kayamba. Darlite. Juz 2. na. 2. kur. 133-152.
Waliaula, K W. (2013). The State of Swahili Studies: Remembering the Past, Present and
Future. Katika Studies in Literature and Language. Juz. 6 Na. 2. Kur. 8 – 17.
Kutoka Mitandaoni
Kutoka Mitandaoni
UNESCO(1973).
https://pediaview.com/openpedia/UNESCO_N...teracy_pri
ze Imesomwa Septemba 17. 2016.
UNESCO (2007). UNESCO International Literacy Prize Winners 2007.
http://www.unesco.org/new/en/education/t...7/Imesomwa
Septemba 20. 2016.
UNESCO (2015). http://www.indexmundi.com/facts/tanzania/literacy-rate).
Imesomwa Septemba 17. 2016.
Kazi za Kifasihi ya Kiswahili zilizorejelewa
Abdalla, A. Sauti ya Dhiki, OUP, 1973.
Achebe, C. Hamkani si Shwari Tena, EAPH, 1972 ; Shujaa Okonkwo,
EAPH, 1973; Mshale wa Mungu, EAPH 1974; Mwakilishi
wa Watu, HEB, 1977.
Armah K, A. Wema Hawajazaliwa, HEB,1976.
Hussein, E. Wakati Ukuta,EAPH, 1970; Mashetani, OUP, 1971;
Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi, OUP,1976; Kwenye
Ukingo wa Thim ,OUP, 1988.
Kahigi, K.K na
Mulokozi, M.M.
Malenga wa Bara, EALB, 1976.
Kezilahabi, E. Rosa Mistika, EALB, 1971; Kichomi, HEB,1974;
Kichwamaji, EAPH, 1974; Dunia Uwanja wa Fujo, EAPH
1981; Karibu Ndani, DUP, 1988.
Mbogo, E. Ngoma ya Ng’wanamalundi, TPH, 1988.
Mhina, G.A Mtu ni Utu, TPH, 1980.
Mohammed, S, A. Amezidi, EAEP,1995.
Muhando, P. Tambueni haki zetu, TPH, 1973; Pambo, NFB, 1975.
Njama, A. Haki Haizami, JKF, 1975.
Nyerere, J.K. Tanzania, Tanzania DUP,1993.
Paton, A Cry the Beloved Country, Macmillan, 1948.
Robert, S Kusadikika Nelson, 1970; Adili na Nduguze, Nelson 1967
Walibora, K. Siku Njema Longhorn, 1996.
Yahya, A.S. Masahibu ya Ndugu Jero, OUP, 1981.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)