MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
AINA MBALIMBALI ZA LUGHA YA MAZUNGUMZO

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
AINA MBALIMBALI ZA LUGHA YA MAZUNGUMZO
#1
AINA MBALIMBALI ZA LUGHA YA MAZUNGUMZO
UTANGULIZI:
Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.
Lengo la kuandaa makala haya ni kuonesha aina mbalimbali za lugha ya mazungumzo kwa kuzingatia mazingira rasmi na yale yasiyo rasmi, utambulisho wa kijamii kama vile: matabaka, hadhi yake, mshikamano na mwachano. Pia tutatalii jinsi gani utambulisho wa kimuktadha unavyoweza kuzalisha aina tofauti tofauti za lugha ya mazungumzo kwa mfano; lugha ya siri na yenye mipaka, michezo ya vitendo, kucheza na maneno, uganga kama miviga na utani kama miviga.
Hebu sasa tujipe wasaa kwa kutalii kipengele kimoja baada ya kimoja kama vilivyoorodheshwa katika utangulizi wetu.
Aina ya lugha ya mazungumzo kwa kuzingatia mazingira rasmi na yasiyo rasmi:
Mazingira rasmi: kwa mujibu Kihore (2004) haya ni yale mazingira yanayoendana na kaida za kijamii, kisheria na kiutamaduni ambazo huhusisha matumizi ya lugha iliyosanifu. Huu ni muktadha unaohusisha ushirika wa upande mmoja, kama vile msamiati wa kiufundi na adabu maalum. Mfano wa mazingira rasmi ni kama vile ofisini, mahakamani, bungeni, kanisani, msikitini na katika elimu. Katika mazingira rasmi tunapata aina mbili za lugha ya mazungumzo ambazo ni jagoni na rejesta.
Jagoni: ni aina mojawapo ya lugha inayotumika katika taaluma fulani mahususi kama vile fasihi, isimu, sheria, sayansi, uhandisi, biashara nakadhalika. Hii ina maana kwamba, lugha hii itafahamika na wale tu walioko katika taaluma husika au wenye maarifa ya taaluma hiyo. Kwa mfano wanaisimu hutumia maneno kama vimadende, vitambaza, vipasuo kwamizi nk. wakirejelea jinsi ya utamkaji wa aina fulani za sauti katika lugha.
Rejesta: Halliday (1989), anafasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi au shughuli. Vilevile fasili hii inaendana na fasili ya Habwe na Karanja (2007).
Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani nakadhalika.
Mazingira yasiyo rasmi: haya ni mazingira ambayo hayafungwi na kaida, sheria na tamaduni za kijamii. Mazingira haya hutumia msamiati ambao si rasmi yaani lugha isiyokuwa sanifu. Katika mazingira haya tunapata aina zifuatazo za lugha ya mazungumzo: misimu, agoti, rejesta na lahaja.
Misimu: Msanjila na wenzake (2009:19) wanafasili dhana ya misimu kuwa ni aina ya misemo katika lugha ambayo huzuka na kutoweka. Sifa kuu ya misimu ni kwamba haidumu muda mrefu na sio lugha sanifu, na watumiaji wa misimu huwa ni kikundi cha wazungumzaji wa lugha katika jamii ambao kimsingi huishi katika eneo moja.
Ngure (2003:147) anaonekana kukubaliana na Msanjila kwa kiasi kikubwa isipokuwa yeye anaweka mkazo zaidi hasa pale anapodai kwamba, uzukaji wa misimu ni wa ghafla na wakati fulani hufuatana na mambo au matukio maalum ya wakati au msimu huo. Anaendelea kufafanua kuwa misimu huzuka/huibuka na kutokeweka kufuatana na hali mbalimbali za kimazingira. Hata hivyo baadhi ya misimu hudumu na kuwa sehemu ya lugha. Kwa mfano neno matatu (Kenya) au daladala (Tanzania) ni neno lililotumika kurejelea nauli iliyolipwa miaka ya sitini. Hivi leo limekuwa neno linalomaanisha aina fulani ya magari ya usafiri. Katika muktadha wa mazungumzo misimu inachukuliwa kama ni aina mojawapo ya lugha ya mazungumzo itumiayo maneno yanayozuka kutokana na matukio mbalimbali ya kijamii, ambayo hiibuliwa na makundi mbalimbali katika jamii, hivyo misimu hutofautiana baina ya kundi moja na jinguine. Kwa mfano, misimu wanayotumia vijana ni tofauti na wanayotumia wazee au yanayotumia wanaume ni tofauti na wanayotumia wanawake.
Vilevile hata mazingira inamotumika misimu si mazingira rasmi kutokana na maneno yake kuzuka na kutoweka na hayatumiwi katika mazingira rasmi.
Agoti: ni lugha itumiwayo na kundi fulani la wahalifu au watu ambao wanaficha uovu wao usifahamike katika jamii wanamoishi. Mara nyingi lugha hii hutumiwa katika mazingira yasorasmi na kikundi kidogo cha watu kama vile, madereva wa magari, watumiaji wa madawa ya kulevya (mateja), majambazi, vibaka na wahuni wa mtaani. Mfano wa agoti inayotumiwa na watumiaji wa madawa ya kulevya ni kama vile, ndumu – bangi, sherehe ilikuwa na waalikwa wengi – soko la madawa ya kulevya lilikuwa na wateja wengi. Rejesta: Katika mazingira yasiyo rasmi, rejesta hutumia msamiati usio rasmi, matumizi ya misimu na ukatizaji wa maneno pamoja na udondoshaji wa baadhi ya vipashio katika maneno. Mfano, rejesta inayotumika katika mazingira yasiyorasmi kama vile mgahawani au hotelini ni kama vile nani wali ng’ombe? Ikiwa na maana kwamba nani aliyeagiza wali na nyama ya ng’ombe.
Utambulisho wa kijamii, Katika kipengele cha utambulisho wa kijamii tunaangalia namna aina ya lugha ya mazungumzo inavyoweza kujidhihirisha miongoni mwa watumiaji wake au kuwatambulisha na kuwatofautisha wanajamii husika. Lugha ya mazungumzo huweza kutambulika kutokana na aina zake, kwani katika jamii kila mtindo wa lugha ya mazungumzo una utambulisho wake katika jamii, kwa mfano agoti katika utambulisho wa kijamii unajulikana kama ni lugha ya wahalifu, jagoni ni lugha ya wanataaluma nakadhalika. Pia katika utambaulisho wa kijamii tunaangalia vile ambavyo mtu hutambulika katika jamii kulingana na namna anavyoongea kulingana na hadhi, tabaka, na jinsi ambavyo mtu huyo anavyoweza kusababisha mshikamano au mwachano katika mazungumzo. Kwa mfano jamii itamtambua mwanajamii kuwa ni msomi kulingana na mtindo wa lugha ya mazungumzo anaoutumia.
Nafasi yake: Katika kipengele hiki tunaangalia nafasi ya aina mbalimbali za lugha ya mazungumzo katika jamii husika. Je aina hizi za lugha ya mazungumzo kama vile agoti, rejesta, jagoni, lahaja na misimu zina nafasi gani katika nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu? Kwa mfano, kiuchumi, kisiasa, kielimu na kiutamaduni. Tukianza na kiuchumi, kwa mfano rejesta, ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Hii ni kutokana na kwamba, kwa mujibu wa King’ei (2010:94) madhumuni makuu ya mawasiliano katika biashara ni kuwavutia wateja na kuwafanya kuamini kuwa bidhaa ama huduma wanazouziwa ni za kiwango cha juu na ni thamani bora kwa pesa zao. Hivyo lugha ya biashara (rejesta), kwa kawaida ni lugha ya kutangaza uzuri wa bidhaa au huduma, huwa na sentensi au vifungu vifupi, mfano “Okoa mapesa chungu mbovu” pia huwa na lugha ya kupumbaza na kuaminisha, mfano “Kunywa XYZ kufumba na kufumbua afya yako itakurudia”.
Pia inasaidia sana kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji katika masuala mbalimbali ya kibiashara na hata katika huduma mbalimbali za kijamii. Mfano hospitalini “mbili mara tatu”, hotelini “kuku wali tafadhali”, sokoni “kata nusu” na maeneo mengine. Baadhi ya rejesta na misimu hutumika kupunguza idadi ya maneno hivyo kufanya mazungumzo yawe mafupi na yanayoeleweka kwa urahisi mfano msimu “Daladala” kwa Dar es salaam linaweza kueleweka kwa urahisi zaidi kuliko kusema magari madogo yanayotumika kuchukua abiria chini ya 50 kutokea eneo moja hadi jingine kwa nauli ya shilingi 300.
Pia rejesta za hotelini kama vile:- Muuzaji: wapi ng’ombe? Mteja: hapa Muuzaji: wapi chai chapati? Mteja: hapa. Si katika uchumi tu bali hata katika elimu rejesta ina nafasi muhimu sana, kwani zipo rejesta ambazo zinatumika katika maeneo rasmi kama vile shuleni katika kutolea elimudunia. Hapa rejesta inayotumika huwa rasmi na yenye kudhihirisha nidhamu. Mfano hutumika katika kuwanukuu watu wanaohusika katika maandishi ya kitaaluma, kama vile “kwa mujibu wa Pamphily, A. J. (2012) anafafanua kwamba…”
Pia katika kutolea elimu ya dini kanisani na msikitini rejesta ina nafasi kubwa katika kujenga maadili. Vilevile rejesta na misimu ina nafasi ya kupamba mazungumzo, wazungumzaji wengi wanapozungumza hapa na pale hupenda kutumia maneno tofautitofauti kama vile misimu ili kufanya mazungumzo yawe ya kuvutia. Pia baadhi ya watu wanaona kuwa matumizi ya mitindo ya lugha ndio ujuzi wa lugha, hivyo hupenda sana kutumia mitindo hii ya lugha ili kuweza kurahisisha mawasiliano. Hivyo ina pendezesha lugha wakati wa mazungumzo. Mfano mazungumzo miongoni mwa vijana:
Kijana 1: Jo? vipi tena mbona zii? Kijana 2: Poa Jo. Kama kawa… mambo mwaaa! Si rejesta na misimu tu, hata jagoni ina nafasi kubwa sana katika maendeleo ya kitaaluma, kwani wanataaluma mbalimbali hufanikisha malengo ya taaluma zao kupitia aina hii ya lugha ya mazungumzo. Mfano wahadisi, wahasibu, wanasayansi na washeria kila mmoja ana jagoni yake ambayo humsaidia kurahisisha mawasiliano miongoni mwao. Nafasi ya rejesta haiishii katika elimu au taaluma tu, bali hupea hata kuvuka mipaka ya kielimu na kutamalaki katika uwanja wa kisiasa. Hapa wanasiasa kama vile wanasayansi na wanasheria nao wana namna yao ya kutumia lugha. Mfano hupenda kuteua msamiati wenye kuleta mvuto na ushawishi katika jamii. Mfano maneno ya nasaha, kauli za kifalsafa mfano; “tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” na uradidi wa vifungu mbalimbali vya maneno, hii yote inalenga katika kumfikirisha au kumpumbaza mtu kisiasa. Mbali na nafasi yake katika siasa, lugha ya mazungumzo kama ilivyo misimu, jagoni na rejesta agoti nayo ina nafasi yake miongoni mwa watumiaji katika jamii. Mfano wa nafasi ya agoti katika jamii ni kama vile: hutumika katika kujihami, kuficha na kuhifadhi siri za kikundi. Pia tusisahau kwamba mitindo mbalimbali ya lugha kama vile misimu inayo nafasi kubwa sana katika kukuza lugha hasa kwa kuongeza msamiati wa lugha husika, hasa misimu. Kwa mfano misimu iliyosanifishwa na kuingizwa katika lugha sanifu ni kama ifuatayo:- Daladala Basi la mtu binafsi linalotumika kusafirisha abiria mjini, linatumika zaidi Tanzania, jina lililotokana na nauli yake hapo mwanzo kuwa sawa na thamani ya shilingi tano ambayo ilikuwa ikijulikana kama dala kama msimu ilioibuka kipindi hicho. Kasheshe Hali ya kutoelewana inayotokana na watu kutokubaliana na jambo fulani.
Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba aina zote hizo za lugha ya mazungumzo zilizojadiliwa hapo juu zina nafasi kubwa sana katika kikundi husika kinachotumia mtindo huo na katika jamii nzima kwa ujumla. Mfano wa nafasi yake katika matumizi ni kama vile kujihami, kujitetea, kukosoa, kurekebisha mienendo isiyokubalika, kukejeli, kutoelea maarifa, kurahisisha mawasiliano, kuficha au kuhifadhi siri za kikundi fulani, kupamba lugha na kutambulisha jamii husika au kikundi husika. Mfano wa rejesta zenye uficho ni kama vile:- Maneno ya mitaani maana katika lugha sanifu Demu msichana Kanyoosha goti kafariki. Kula kona ondoka. Mfano wa agoti zenye uficho:
Maneno ya madereva wa daladala maana katika lugha sanifu. Maiti Askari au mwanajeshi. (abiria asiyelipa nauli) Mchawi Gari linalokuja nyuma. Bibi Titi Askari mwanamke.
Matabaka, kwa mujibu wa kamusi ya Oxford (2004) ni kundi la watu wenye hali moja linalotokana na jamii yenye mfumo wa kiuchumi ambao hugawa watu.
Katika kipengele hiki cha matabaka, tutaangalia lugha kama kitambulisho cha jamii huwa na mitindo mbalimbali ya uzungumzaji ambayo huweza kuitwa aina mbalimbali za lugha ya mazungumzo. Aina hizi yaani rejesta, lahaja, jagoni, misimu na agoti ndizo zitakazo tudhihirishia uwepo wa matabaka mbalimbali miongoni mwa wanajamii. Njia mojawapo ambayo huweza kutumika katika kuonesha matabaka au tofauti za kijamii ni lugha azungumzayo mtu. Hii huweza kumtambaulisha kwamba yeye ni wa tabaka la juu au la chini, tabaka la wasomi au la wasiosoma, tabaka tawala au tawaliwa, tabaka la wenye nacho au la makabwela (wasio na kitu/masikini). Hivyo basi tujipe fursa ya kutalii matabaka haya huku tukihusianisha na aina ya lugha ya mazungumzo.
Tabaka la juu, yaani hili ni tabaka la watu ambao wana hadhi fulani katika jamii kama vile mamlaka au cheo. Tabaka hili katika uzungumzaji wao hutumia lugha rasmi, fasaha na yenye staha, uteuzi mzuri wa msamiati na miundo sahihi ya tungo, kwa lengo la kulinda hadhi na mamlaka yao na kujitofautisha na tabaka la chini. Mfano wa lugha inayotumiwa na kundi hili ni rejesta rasmi. Tabaka la chini, yaani watu wasio na hadhi au mamlaka yoyote katika jamii. Matumizi ya lugha katika tabaka hili si fasaha kutokana na muktadha waliomo. Kwani shughuli zao kwa kiasi kikubwa huzifanya baina ya wao kwa wao pasipo kuchangamana na tabaka la juu.
Hivyo aina ya lugha ya mazungumzo itakayopatikana katika tabaka hili ni rejesta isiyo rasmi pamoja na lahaja. Tabaka la wasomi, hili ni tabaka la watu wenye taaluma fulani, mfano wadaktari, waalimu, wahasibu, wahandisi na wengineo. Aina ya lugha itayotumiwa na tabaka hili kulingana na taaluma zao ni lugha rasmi kama vile jagoni na rejesta rasmi. Tabaka la wasiosoma, hili ni tabaka pana sana ambamo ndani mwake mna makundi mbalimbali ya wazungumzaji kama vile makuli, wamachinga, wapiga debe, vijana wa vijiweni, mfano mateja, vibaka na majambazi. Kundi hili ni kundi ambalo lipo katika mazingira yasiyo rasmi kutokana na shughuli wazifanyazo. Hivyo ni wazi kwamba hata lugha wazungumzayo si rasmi. Mfano wa lugha ipatikanayo katika tabaka hili ni agoti pamoja na misimu.
Ieleweke kwamba, mgawanyo wa matabaka haya haimaanishi kuwa mzungumzaji wa tabaka fulani hataweza kuzungumza aina ya lugha au mtindo wa lugha wa tabaka jingine lahasha! Mzungumzaji wa tabaka lolote anaouwezo wa kuzungumza mtindo wowote wa lugha isipokuwa jagoni, kwani hapa mzungumzaji asiye wa taaluma hiyo hataweza kuzungumza mpaka awe na ujuzi wa taaluma husika. Hivyo mzungumzaji mmoja ataweza kuzungumza aina mbalimbali za lugha ya mazungumzo kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo; umri, mada ya mazungumzo, mahusiano baina ya wazungumzaji, muktadha na hadhira. Pia katika mazingira mengine mzungumzaji anaweza kujinasibisha na aina fulani ya lugha ya mazungumzo inayopewa hadhi ya juu kama vile rejesta rasmi, misimu au jagoni kwa lengo la kutaka aonekane kana kwamba naye ni watabaka la juu au la wasomi.
Hadhi; Msanjila na wenzake (wameshatajwa) wanaeleza kuwa lugha yenye hadhi ni lugha iliyosanifishwa na kutumika katika mawasiliano yote rasmi, kwa mfano shuleni, kanisani au shughuli za kiserikali, katika kipengele cha hadhi hapa lugha ya mazungumzo inazingatia nafasi aliyonayo mtu katika jamii yake. Kwa hiyo hadhi ya lugha huendana na hadhi ya wazungumzaji wa lugha husika, kwa mfano mwalimu, askofu, ustadhi au kiongozi wa serikali katika mazungumzo yake hutumia lugha yenye hadhi ambayo ni lugha rasmi ambayo imesanifiwa na kukubalika kutumika katika mawasiliano yaliyo rasmi. Hadhi ya lugha huweza kuibua mitindo mbalimbali ya lugha ambayo ni kama vile rejesta na jagoni. Kwa mfano rejesta za shuleni hutumia msamiati wa lugha yenye hadhi ambayo ina msamiati ulio rasmi, kwa mfano msamiati utakaozungumzwa na mwalimu ni msamiti rasmi kulingana na hadhi yake na hadhi ya lugha inayotumika katika mazingira yote ya shuleni. Vile vile msamiati utakaozungumzwa na Askofu, padre au mchungaji atazingatia hadhi yake na hadhi ya lugha anayoitumia katika mazingira ya kanisani. Msamiati utakaotumika ni msamiati wa lugha yenye hadhi. Vilevile katika mtindo wa jagoni tunaweza kupata msamiati ulio rasmi na unaotumika na watu wenye hadhi fulani katika jamii. Kwa mfano:-
Jagoni za kikemia. Msamiati wa kawaida wa kiswahili. H2O Maji O2 Oksijeni Co Hewa ya ukaa. Jagoni hizo huzungumzwa na watu wenye ujuzi wa kemia.
Jagoni za wanaisimu msamiati wa kawaida wa Kiswahili. Uwandani Mafunzo kwa vitendo Ndaki Vyuo vikuu. Ndiva Bwawa kubwa la kuhifadhi maji. Jagoni hizi huzungumzwa na wasomi. Kwa hiyo hadhi ya wazungumzaji wa lugha hufungamana sana na hadhi ya lugha waitumiayo katika mazungumzo. Kulingana na utofauti wa kihadhi walionao wazungumzaji katika jamii ni wazi kuwa utofauti huu utapelekea kutokea kwa mambo kadhaa, kama vile: • Upekee katika mtindo wa mawasiliano, mfano hotuba, mahubiri, mawaidha nakadhalika. • Adabu katika mazungumzo. • Upekee katika uteuzi wa msamiati kulingana na hadhi. Hivyo aina ya lugha itakayopatikana kulingana na hadhi ya mzungumzaji itakuwa ni rejesta rasmi. Hii ni kutokana na kwamba mazingira ya mchungaji, ustadhi, ofisa na viongozi wa serikali ni mazingira rasmi na ndio maana hata rejesta inayotumika ni rasmi.
Msikamano na mwachano: katika utambaulisho wa kijamii dhana ya mshikamano katika aina mbalimbali za lugha ya mazungumzo, Crastal anfafanua dhana ya mshikamano kuwa inamaanisha mfanano wa uzungumzaji uliopo katika watu, familia, jinsi, tabaka moja, watu wenye hadhi sawa au shughuli sawa au makabila sawa. Kwa hiyo watu hawa watakuwa na mshikamano (mfanano) katika namna ya utamkaji wa vipashio mbalimbali katika maneno na pia watakuwa na mshikamano katika msamiati. Mfano, walimu, madaktari, machinga, wahandisi na kadhalika.
Dhana ya mwachano: katika lugha ya mazungumzo dhana ya mwachano inamaana kwamba ni ile hali ambapo wazungumzaji wa lugha moja hutofautiana katika baadhi ya vitamkwa katika maneno na pia hutofautiana katika baadhi ya msamiati. Mfano, Mhandisi na Daktari huweza kuwa na mwachano katika baadhi ya msamiati, kwa mfano, daktari anaweza kutumia msamiati kama vile “bomba” akimaanisha kifaa kinachotumika kwa ajili ya kudungia sindano wakati huohuo mhandisi atatumia neno hilohilo akimaanisha kifaa kinachotumika kusafirishia maji kutoka chanzo chake hadi kwa watumiaji, hivyo hali kama hii huweza kusababisha mwachano. Mwachano huu uliopo baina ya wazungumzaji huweza kusababishwa na mambo yafuatayo:
  • Elimu; Yule (1985) anasema kwamba hata wazungumzaji wasomi walio na usuli sawa wa elimu, mfano waliomaliza shule miaka ya hivi karibuni watakuwa na mwachano na wale wanaoendelea kusoma.
  • Shughuli/kazi; Yule (ameshatajwa) anasema kwamba shughuli au kazi wanazozifanya watu katika jamii watakuwa na kiasi fulani cha athari kwa kila mzungumzaji, hii ni kwa sababu kila kazi ina kiasi fulani cha jagoni ambacho hakihusiani na shughuli nyingine, hivyo itapelekea kutokea kwa mwachano.
  • Matabaka ya kijamii; Labov (1972) katika utafiti wake alioufanya katika jiji la New York aligundua kwamba kunamwachano mkubwa kati ya tabaka la chini na la juu, anasema kwamba sauti /˄/ kama katika neno sun /s˄n/ inatumiwa na tabaka la juu wakati tabaka la chini wanatumia sauti /ʊ/ katika neno hilo hilo, vilevile kiambishi tamati –ing katika neno kama vile coming kinatamkwa na tabaka la juu wakati tabaka la chini wanatamka kwa kuishia na kiambishi –in katika neno hilo hilo.
  • Umri;Yule anasema mwachano au mshikamano unaweza kusababishwa na umri wa wazungumzaji. Anasema kuwa hata katika tabaka fulani katika jamii, mwachano huweza kudhihirika kutokana na kigezo cha umri wa wazungumzaji, kwa mfano vijana waishio katika eneo fulani watatofautiana na wazazi wao katika namna yao ya kuzungumza.
  • Jinsi; hii pia hupelekea mwachano katika uzungumzaji, Yule anasema wasichana wanapenda kutumia miundo ya lugha ambayo inahadhi ya juu katika jamii, tofauti na wanaume ambao wote wana usuli sawa wa kijamii. Miundo kama I done it na he ain’t hutumiwa sana na jinsi ya kiume katika mazungumzo yao na miundo kama I did it na he isn’t hupatikana sana katika mazungumzo ya jinsi ya kike. Pia tofauti hujitokeza katika namna ya kutamka neno, matamshi hutofautiana namna wanavyotamka jinsi ya kike na jinsi ya kiume.
  • Tukio; mwachano mwingine hutokea katika hali ya mzungumzaji kulingana na tukio lililoko mbele yake. Mfano, mzungumzaji anayekwenda kufanya usaili wa kazi atazungumza na katibu mhutasi: “samahani, meneja yumo ofisini? Nina miadi naye”. Mzungumzaji huyo huyo anapomuuliza rafiki yake juu ya rafiki yake mwingine atasema: oya, huyo mjinga bado amelala? Nataka kuonana naye juu ya jambo fulani. Kwa hiyo kutokana na tofauti hizi wazungumzaji wengi wana uamuzi wa kuchagua mwachano upi au mshikamano upi wafuate, mfano anapokuwa na mchumba wake, mpenzi wake, watoto, bosi, daktari, mchungaji, padri, au sheikh.
 Kwa ufupi David Crystal anasema kwamba, mwachano na mshikamano huonekana kwa urahisi pale ambapo meneja wa biashara fulani anapotumia lugha rasmi anapokuwa ofisini na kuhamia lugha isiyo rasmi anapokuwa nyumbani. Pia mhadhiri anapotoa mhadhara atatumia lugha rasmi na fasaha lakini anapokuwa na wahadhiri wenzake atajadili hoja hizo hizo katika lugha isiyo rasmi. Kimsingi dhana hizi mbili yaani mwachano na mshikamano ndizo hupelekea kutokea kwa aina za lugha kama lahaja, jagoni, rejesta, agoti na misimu.
Utambulisho wa kimuktadha. Katika kujadili kipengele hiki tutaangalia aina za lugha zinazojitokeza katika lugha ya siri na yenye mipaka, michezo ya matendo, kucheza na maneno, uganga kama miviga na utani kama miviga.
Lugha ya siri na yenye mipaka, ni lugha inayotumiwa na watu wawili au zaidi kwa kuzungumza lugha ambayo hubagua baadhi ya hadhira iliyopo. Lugha itumikayo haitoweza kueleweka kwa wale wasiolewa msamiti unaotumika, madhumuni ya kutumia lugha ya uficho ni kutaka mazungumzo hayo yawe siri baina ya wazungumzaji peke yao. Mara nyingi watu wanapotumia lugha ya uficho aghalabu misimu huzuka.
Mfano katika jamii ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuna baadhi ya maneno yanatumika chuoni peke yake, iwapo maneno hayo yatatumika nje ya mazingira hayo ya chuo hayataeleweka kwa wanajamii wa nje ya chuo.
Hivyo basi suala la mipaka ya kijiografia huingia katika suala hili. Mipaka ya kijiografia hutumika kuangalia jinsi msamiati kadhaa unavyotumika katika jamii bila kuvuka mipaka, kwa maana hiyo tunaweza kusema kuwa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuna msamiati ambayo huwa na mipaka, haiwezi kutumika nje ya chuo.Mfano wa masamiati kama vile madesa, neno hili lina maana ya kitini, kitini hiki huweza kuwa na ukubwa wowote. Kwa mwanafunzi yeyote wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam msamiati huo wa madesa ni msamiati ulio vichwani mwao na kueleweka. Lakini iwapo msamiati huu utatumika nje ya chuo (nje ya mipaka ya chuo) utakuwa ni msamiati mgumu kueleweka kwa walio nje ya chuo mfano msamiati huu ukizungumzwa maeneo ya Tabata, Mbagala au Tanga wananchi wa maeneo hayo hawataelewa.
Pia katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuna msamiati mwingine unaotumika ambao ni “darasa la saba” wanachuo waonapo askari huwaita darasa la saba neno hili linaweza kuwa na maana sawa na msimu. Katika mipaka ya ndani ya chuo neno hili lina maana ya askari. Iwapo wanafunzi wawili kutoka chuoni wakiwa katika mazungumzo katika mazingira ya nje ya mipaka ya chuo huku wakiwa katika mazungumzo yao wakiwaona askari basi watasema, “…unawaona darasa la saba?....” wakimaanisha askari. Hivyo kama kuna wanajamii walioko pembeni yao hawatoweza kuelewa chochote kwani hii ni lugha yenye uficho na yenye uwezo wa kuwa na dhima ya misimu. Ruti, neno hili linamaanisha maandamano katika chuo cha Dar es salaam. Neno hili linaweza kuwa sawa na hadhi ya misimu iwapo litatumika nje ya mipaka ya chuo halitaweza kufahamika kwa hadhira hiyo. Wanafunzi wakitoka nje ya mipaka ya chuo na kusema “ ...kesho tunapiga ruti…” Watu hawataelewa neno hilo litakuwa gumu kuelewa kwa wanajamii na litakuwa na uficho kwa wanaomzunguka yule anayeongea. Vilevile kikundi cha wahalifu kama vile wavuta bangi, hawa pia wana lugha siri na mipaka ijulikanayo kama agoti. Kundi hili huitumia lugha ya siri na yenye mipaka pale wanapokuwa katika vitendo vyao vya kihalifu.
Lengo la kutumia lugha hii ni kuficha uhalifu wao kwa watu walionje ya kundi hilo. Kwa mfano wanapomuona askari utasikia wakisema “…soo mwana…” yaani wakimaanisha hali ya hatari. Hivyo basi kwa ujumla tunaweza kuona jinsi gani lugha ya siri na yenye mipaka inavyoweza kuzalisha lugha ya mazungumzo.
Michezo ya matendo: ni michezo ambayo aghalabu huendana na vitendo kutendeka kuendana na mazungumzo yanayozungumziwa. Mtu azungumzapo maneno fulani, basi hufanya vitendo vinavyolandana na maneno anayotamka. Katika jamii yoyote ile hapakosekani michezo, michezo hiyo inaweza kuchezwa na watu wa rika fulani, mfano watoto wadogo hawa wana michezo yao, pia katika umri wa vijana wanaobalehe au kuvunja ungo. Kwa mfano, katika mchezo wa watoto wa kujificha unaoitwa kombolela, katika mchezo huo watoto wengi hutakiwa kujificha sehemu mbalimbali na kumuacha mototo mmoja kulinda kopo moja lisigongwe na watoto wengine waliojificha na kuwakomboa wenzake. Neno “kombolela” limetokana na neno komboa, pindi mtoto mmoja anapojitokeza na kupiga kopo lile husema “kombolela” yaani nimewakomboa wenzangu.
Hivyo katika mchezo huu tutaweza kupata rejesta kama vile kombolela na pia katika mchezo huu mtoto mmoja akionekana na mlinda kopo basi mlinzi huyo hutamka neno moja (jina) la mtoto aliyemuona mfano Juma, Aziza, Salome au Ndege hapa akimaanisha nimemuona Juma, Aziza, Salome au Ndege. Hivyo atamkapo jina moja inamaanisha kuonwa kwa mtoto. Hii ni mojawapo ya lugha ya mazungumzo katika mchezo huu.
Pia katika mchezo mwingine wa vitendo ni mchezo wa karata, mchezo huu huchezwa na watu wenye umri tofauti tofauti, hutumia kadi ndogo ndogo zipatazo 54. Katika mchezo huu aghalabu tunapata lugha ya mazungumzo ambayo ni tofauti na lugha itumikayo katika michezo mingine kama mchezo wa mpira wa miguu, pete au ule wa watoto wa kombolela, hapa tunaweza kupata maneno tofauti tofauti kama vile:- “Lamba” neno hili linamaanisha ongeza karata au muda mwingine wachezaji husema “inama” wakimaanisha chukua karata au kadi ya ziada. “Lasti kadi” mchezaji iwapo amebakiwa na karata ya mwisho basi husema lasti kadi kumaanisha amebakiwa na kadi ya mwisho inayoweza kumaliza mchezo na kuibuka mshindi.
Pia kuna maneno kama vile cheza mavi, kopa au kisu mchezaji mwingine, ataelewa lugha hiyo wakati wa kucheza mchezo. Neno jingine ni “geuza mchezo” mchezaji mmoja akitamka neno hilo basi humaanisha mwelekeo wa mchezo kama ulikuwa uelekee kushoto basi mchezo sasa utaelekea kulia, pia kuna neno stop, mchezaji akimaanisha mtu fulani aliye karibu yake katika mchezo anapaswa kusubiri, yaani asicheze kwanza.
Kwa ujumla mchezo wa vitendo kama huu huwa na lugha yake ya mazungumzo ambayo kwayo tunapata dhana ya misimu na rejesta. Kucheza na maneno, ni mbinu ya kifasihi ambayo kwayo, maneno yanayotumiwa yanakuwa na hoja kuu ya kazi. Kimsingi hutumiwa kwa ajili ya kuleta athari iliyokusudiwa au kuburudisha. Mara nyingi mchezo wa maneno huusisha sifa zifuatazo, kutoa tabia za majina, maneno na maana zake zisizoeleweka kwa urahisi, usemaji wenye ujanja wa kuficha maana ya moja kwa moja na sentensi ambazo zinakiuka miundo ya kawaida ya sentensi. Mifano ya michezo ya maneno inayotoa tabia za majina ni kama ifuatayo:- Dar es Salaam = Lala salama Afrika nzima = Wazimana Tanga = Wanatanga tanga Wakenya = Wanakenyana Tanzania = Wanazamia Naiorobi = Wanaibiana Arusha =Wanarushana rushana Wasukuma = Wanasukumana Uganda = Wanagandana Mfano miundo ya sentensi zisizo na mpangilio maalumu kwa lengo la kuficha maana ya moja kwa moja. Kuzungumza kwa kupindua maneno na kuwa kinyume:- “naku zimwi ndapamea nyekwe riga”. Maana yake ni, kuna mwizi amepanda kwenye gari. Mfano mwingine wa kucheza na maneno, “katibu kata wa kata ya makata alikataza katakata kukata miti iliyo katikati ya kata ya makata”.
Vilevile katika lugha ya kiingereza mchezo wa maneno huweza kujidhihirisha kama ifuatavyo: “Katai is a maasai, Katai can tie and utie a tie, if Katai can tie and untie a tie why can’t I tie and untie a tie like Katai?”
Utani kama miviga, utani kama miviga ni kipengele cha lugha ya mazungumzo kinachoweza kuibua mitindo mbalimbali ya lugha. Oxford, (2004) wanaeleza kuwa utani ni taratibu za kimila ambazo zinawafanya watu kuambiana au kutendeana jambo lolote bila ya chuki, maneno ya kutania, dhihaka na masihara.
Ipara, na Waituru, (2006) Utani ni kufanyiana mzaha au masihara baina ya watu na makundi mbalimbali katika. jamii. Maana ya miviga. Ngure, A. (kashatajwa) nafafanua kwamba miviga, ni sherehe za kijadi ambazo zinajihusisha na kumpa mtoto jina, harusi, mazishi, matambiko, kutawazwa kwa viongozi, unyago, jando na kadhalika. Utani kama miviga una umuhimu wake katika jamii, umuhimu huo ni kama vile kukumbusha mambo muhimu katika jamii, hapa mambo muhimu ni yale ya kihistoria ya jamii husika, pia hufundisha na kuadilisha, mila na desturi, maadili na tamaduni mbalimali katika jamii. Pia utani kama miviga huwa na dhima ya kuburudisha jamii.
Vilevile utani kama miviga husaidia kuonyesha uhusiano iliopo baina ya wanajamii, kujenga na kudumisha mahusiano bora katika jamii, pia hutumika kutoa onyo, kutahadharisha jamii kwa njia ya ucheshi. Utani pia hujumusiha vitendo maalumu kama vile kuimba, kurukaruka na kucheza ngoma. Hivyo basi, kipengele hiki cha lugha ya mazungumzo huweza kuibua mitindo mbalimbali ya lugha isiyo rasmi ambayo ni kama vile rejesta na misimu.
Uganga kama miviga: Oxford wanafasili uganga kuwa ni kazi ya kuponya wagonjwa, utabibu, dawa. Mkwera, (hakuna mwaka) anadadafua dhana ya uganga kwa kuhusianisha na waganga. Anaeleza kwamba kuna waganga wa aina sita, katika makundi mawili. kundi la kwanza ni la matabibu wa kweli, waganga waponyao magonjwa. Hawa ndio waganga wa mitishamba wa dawa ndogo ndogo (waganga wa kienyeji), madaktari na wauguzi (hawa ni watu waliosomea elimu ya magonjwa mbalimbali, aidha teknolojia na njia mbalimbali zilizo safi na halali za uponyaji), waombezi (hawa ni waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu karama (uwezo) ya kuponya. Kundi hili halina ushiriki na kusalia miungu. Kundi la pili ni wale naofanya uganga kwa kujishughulisha na kujihusisha sana na majini mizimu, kama vile waganga wa kitamaduni wa maradhi, wajuzi wa mazingira, wataalamu wa kienyeji na kadhalika. Katika kundi hili la pili wamo: wapiga ramli, walozi na wachawi.
Hivyo basi katika kipengele hiki tutaangali kwa jicho pevu uganga kama miviga unaofanywa na waganga walio katika kundi la pili. Uganga kama miviga ni sherehe maalum zinazofanywa kwa lengo la kuponya maradhi, kuagua, kutuliza miungu na mizimu, kuondoa mikosi na kutakasa wanajamii. Mara nyingi uganga kama miviga huambatana na matendo mbalimbali yafanywayo na mganga pamoja na washiriki wake. Matendo hayo ni kama vile kurukaruka, kuimba na kucheza na kububujika vifungu vya maneno visivyo na mantiki wala kueleweka. Kwa mfano, Mganga anamwita mhemba wake, “Msondo”
“Labekha Bwana”, aliitika Msondo.
“Lete lile pembe langu la tunguli, ubani, na kisu cha kuchinjia”
“Ewala Bwana”.
Anaendelea kububujika maneno yeye peke yake;
“Ndiyo, ndiyo, Nieleze Ruhani, yalikuwaje?”… “Kwa nini hunipi mfupa wa taarifa yote; ni wapi yalitokea yote haya?”… “Nani alimtuma? Kwa kisa gani? Ni nini akitakacho?”… “Ahaa! bibi yake alikwenda Bubuye kwa mganga na kuliomba hilo kombe?”… Mfano wa wimbo wakati wa shughuli za uganga, “Ee changu, changu njoo! Ee changu, changu njoo! Ee changu, change njoo!
Mlete babu mwamba, mlete yeye ajue’ Mlete yeye aone, mlete yeye tumchinje, Mlete yeye tumkamate; mlete, mlete, mlete!
Mlete, mlete, mlete! Mlete, mlete, mlete! Eee ee hoo; ee ee hoo; ee ee hoo!
Cheza, soma, toroka, itika, imba! Eee ee hoo; ee ee hoo; ee eehoo!”
Haya ni baadhi ya maneno ambayo pindi yatumikapo mara moja mtu hugundua ni mazingira ya nama gani yanazungumziwa hapa. Katika hali ya kawaida mtu asikiapo maneno kama hayo hawezi kuhusisha na mazingira ya kanisani, bali atahusisha na mazingira ya maeneo ya kiganga na nguvu za giza.
Kwa ujumla kipengele hiki cha uganga kama miviga, tunaona jinsi kinavyoibua mitindo ya lugha ya mazungumzo kama vile rejesta isiyo rasmi, lahaja, misimu ambayo huibuliwa na kutumika na makundi haya ya waganga. Pia agoti hujitokeza kwa lengo la kuficha siri ili mteja (mgonjwa) wake asigundue ujanja wake. Ifahamike kwamba mazingira haya si rasmi kama ilivyo kwa waganga wa kundi la kwanza, hivyo hata aina ya lugha ya mazungumzo itumikayo haitakuwa rasmi.
HITMISHO:
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa katika kukamilisha dhana nzima ya matumizi ya lugha, tumeweza kuona uhusiano mkubwa uliopo kati ya mitindo mbali mbali ya lugha ya mazungumzo na utambulisho wa kijamii na kimuktadha na jinsi mitindo hiyo inavyoweza kutambulisha na kutofautisha makundi mbalimbali ya wazungumzaji katika jamii.
 
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)