12-25-2021, 06:31 PM
KITABU : USIKU UTAKAPOKWISHA
MWANDISHI-MBUNDA MSOKILE
MWAKA-1990 WACHAPISHAJI-DUP
UTANGULIZI
Riwaya ya Usiku Utakapokwisha imejadili kwa kina masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika jamii ya Tanzania baada ya miaka ishirini na mitatu ya Azimio la Arusha.Mwandishi ameyaangalia baadhi ya kwa jicho pevu matatizo yanayoikumbaTanzania katika juhudi zake za kujenga jamii mpya ya kijamaa. Riwaya hii imekitwa kwa wahusika watatu: Chioko, Gonza na Nelli.
Nelli ni mchumba wake Chioko na wanaishi kwa Gonza ambaye ana chumba kimoja tu,Gonza anaishi kwa kutegemea kuuza karanga na kufanya shughuli nyingine ambazo Chioko hazifahamu. Katika msako unaofanyika mjini ili kutafuta wazururaji, Nelli anakamatwa na kupelekwa kijii cha mapinduzi. Chioko hafanikiwi katika juhudi zake za kutafuta kazi: Gonza anamshauri Chioko waende Zambia amabako watapata kazi. Chioko anatilia mashaka mpango huo; lakini anapopata barua kwa Nelli kumweleza kwamba,anakuja kumtembelea na hali yeye hana pesa anashawishika na mpango huo.
Mwandishi Kupitia wahusika hawa watatu anaichambua jamii ya Tanzania na hali nzima ya mfumo wa kiuchumi na kijamii, na kuonesha uozo uliomo katika jamii hii ambayo inatarajia kujenga mfumo wa Ujamaa. Suala la rushwa, na utumiaji mbaya wa madaraka kwa viongozi, matabaka, dhiki za Walalahoi/makabwela na masuala mengine mengi yanayohusiana na hali halisi ya kiuchumi,kisiasa na kijamii Mwandishi ameyapa nafasi kubwa na kuyajadili kwa kina katika riwaya hii.
MAUDHUI
DHAMIRA KUU;UMASKINI AU HALI NGUMU YA MAISHA
Hali ngumu ya maisha au umaskini kwa makabwela umemshughulisha sana Mwandishi katika riwaya hii ya Usiku Utakapokwisha. Katika riwaya hii, mwandishi anaonesha kuwa umasikini umewatawala sana watu wa tabaka la chini kiasi kwamba, hata mahitaji muhimu hukosa na kusababisha vifo vyao, kama asemavyo msanii (uk.7);
“Kifo kilichotokea kati ya mama na watoto wake wawili uko Buguruni kinasikitisha. Ukweli ni kwamba haya ni madhara ya ufukara na umasikini, watu hawa hawakua na kazi kwa muda mrefu na maisha yao yamekuwa yakitegemea mno chakula kilichotokana na kuuzwa kwa vifaa na vyombo vyao vya nyumbani. Lakini vifaa na vyombo hivyo vimeuzwa hadi vikaisha. Mwishoni wakafa kutokana na kukosa chakula”.
Ugonjwa wa ufukara ulikuwa umewasonga sana watu wa tabaka la chini. Kila wakijaribu kuutibu kwa kufanya kazi walishindwa (uk.11). Matatizo ya maisha yaliwakumba wengi.Walijitahidi kupambana na shida usiku kucha, mchana kutwa lakini mafanikio yao yakazidi kuwa duni. Mtatizo haya hayakuwakumba watu wa tabaka la chini tu, yaliwakumba hata vijana wa shule.Katika uk. 16 mwandishi anasema;
“Kwa watoto wa shule, hasa wasichana walipita mitaani huku wakiwa wamebeba vyeti vya maisha yao. Kwa upande wao, mtu aliyempa chai ni ‘mpendwa’. Aliyetoa pilau ni mfadhili na yule aliyetoa lifti wakati wa jua kali lililokausha midomo yao na kuwatoa jasho alikuwamungu mtu”.
Kutokana na umasikini vijana wengine walipoona hawana fedha, walivuta bangi ili kutoa woga. Kisha wakawa wanauza bangi kwa siri, walifanikiwa na walioshindwa walijiingiza kwenye vitendo vya wizi (uk.17).
Mwandishi ameonyesha namna makazi ya makabwela yanavyokatisha tamaa. Waliishi sehemu duni ambazo hazina miundo mbinu kama Manzese. Manzese ni sehemu muhimu ya mji wa Dar-es-salaam na ina mambo mengi. Huko ndiko wanakoishi makabwela na makapera wa jiji hili, sehemu ambayo ni chafu na haitamaniki.Katika uk.1 mwandishi anasema;
“Sehemu ya jiji ambayo inafukuta harufu ya uozo wa aina aina; sehemu ambayo ina mashimo na makaro yanayobwabwaja maji machafu ya mji, sehemu ambayo ina mabanda mbavu za mbwa yenye kushika tama kwa unyonge! Manzese inahuzunisha!”.
Mwandishi ameonyesha namna makabwela/maskini wanavyoishi maisha ya taabu sana, nyumba zao si salama, chakula chao cha taabu daima wanaishi na wadudu kama vile nzi, mbu, panya, kama rafiki zao. Maisha ya mtu masikini hayakudhaminiwa ndio maana hata wakipeleka malalamiko yao serikalini hawashughulikiwi (uk.7).
Hali ngumu ya maisha au Umaskini imesababisha makabwela kutegemea majaa ya takataka kupata chakula chao.Hawa waliokota vile vyakula vilivyotupwa na wenye pesa ili kuokoa maisha yao ya kila siku. Katika uk.25 mwandishi anasema;
“Wengine walikua wamejaa kwenye jaa moja la takataka, karibu na barabara wakiokota punje ndogo ndogo za mchele zilizokuwa zimetupwa huko.Pengine ilibidi wapepete makapi ya mchele zilizokuwa zimetupwa huko.Pengine ilibidi wapepete makapi ya mchele kwa saa nyingi huku jua kali likiwachoma.Hakika lilikuwa tatizo”.
Hali ya umasikini ina madhara yake kwa jamii.Kutokana na umasikini makabwela wanapoteza utu wao. Mfano mtu yuko tayari kufungwa kwa niaba ya mwenye pesa ya kununulia chakula kama asemavyomsanii (uk. 40);
“Mtu mmoja, mheshimiwa, mwenye pesa alikuwa amepatikana katika kosa, akahukumiwa kifungo. Lakini yeye liamua kulinda hadhi yake kwa kumtafuta mtu wa hali ya chini akafungwe ili alipwe pesa”.
Maisha ya masikini yalitegmea kuzunguka mitaani na kuuza karanga, na njugu huku wakifukuzwa na mgambo kila sehemu. Maisha yao niya kukimbizana na mgambo kila sehemu; masikini akipata matako hulia mbwata. Kwa ujumla, msanii anaonesha kuwa watu masikini kula kwao ni kwa taabu, kulala kwa kwa taabu, kunywa kwao kwa taabu, kila kitu ni taabu kwao, hawana nafuu yoyote.
Mwandishi anaonyesha kuwa kwenye hoteli za makabwela vyakula vinavyouzwa navyo ni vya hali ya chini sana ukilinganisha na mahoteli makubwa wanaokula viongozi na watu wengine wenye pesa.Katika uk.37 mwandishi anasema;
“Akapita mbele ya jingo moja, akaona kibao kimeandikwa bei mbalimbali za vyakula. Maandishi yake yalikuwa yakisomeka wazi.
NKom Ba hoTeLI
BEI:MAkonGolo…………………………………………………Shs 25.00
BatA La kUchoMA………………………………………….Shs 20.00
PUA ya nguluwe……………………………………………Shs 15.00
MBavu YamBuZI…………………………………………Shs 20.00
SuPu Ya kicHwa CHA kuku…………………….…….Shs 3.00
UtumBo wa KUKU………………………………………Shs 4.00
KichWA chA KuKu…………………………………………Shs 6.00
UGAli……………………………………………………………Shs 5.00
fIrIGIsi la BAtA ……………………………………………Shs 10.00
Fika JioNEE mWENYEWE: nDunGu:
ChAKula Ni uZIMA: NKomBa end GampaNi
Sehemu hii ilikuwa maarufu kwa watu wa tabaka la chini, lakini wa hali ya juu haikuwa sehemu maarufu kwao, kwani hoteli yenyewe haikuwa ya hadhi yao. Pua ya nguruwe, supu ya kichwa cha kuku, utumbo wa kuku, na filigisi za bata ni vyakula vya makabwela.
Katika kuondokana na tatizo hili la umasikini. Gonza anasema lazima itafutiwe sababu ili tuweze kuondokana na umasikini. Gonza anasema (uk.8);
“Panapowezekana pawezekane! Panaposhindikana pashindikane;na sababu itafutwe na kutolewa hadharani”.
Mwandishi anaona kuwa ili tuondoe umasikini, lazima tutafute kwanza chanzo cha umasikini huo.Chanzo kikipatikana, hata hatua zakuchukua dhidi ya umasikini itakuwa rahisi kupatikana.Mwandishi anapendekeza kuwa, kufanya kazi kwa bidii ni njia mojawapo ya kuondoa umasikini.(uk. 11);
Mwandishi anaonesha kuwa kufanya kazi kwa bidii kutaondoa ugonjwa huu wa ufukara kwa makabwela. Bila kufanya kazi kwa bidii;itakuwa ndoto kuondokana na huu umaskini.
Mwandishi anaona kuwa kurudi shamba si suluhisho la umasikini kwani hata huko shamba kuna matatizo yake kama ilivyo mjini. Mwandishi anasisitiza kuwa sio makabwela tu walazimishwe kwenda shamba mabadiliko ya nchi lazima yawe ya watu wote na sio makabwela tu (uk. 19). Mwandishi anaonesha kuwa lazima huduma zote muhimu zipelekwe huko kijijini ili ziwavutie watu kwenda huko (uk. 19).
Mwandishi anaona kuwa ili kuondokana na umasikini ni muhimu kuanzisha miradi mjini. Lakini kwanza lazima tuwe na nia, kama hatutakuwa na nia miradi hiyo itakufa. Miradi anayopendekeza mwandishi ni kama vile maduka ya ushirika. Kwa upande wa Gonza na Nyundo wanaona njia pekee ya kuondokana na umasikini ni kupambana na wenye pesa kwa nguvu na kugawana kile wanachomiliki: Gonza na Nyundo wanaona wenye vyeo ndio wamesababisha umasikini, kwahiyo tunapotaka kuondoa umasikini lazima tupambane nao (uk. 74);
“Leo jioni kuna kazi………leo usiku tutakwenda nyumbani kwa yule meneja wa kampuni ya mabomba…… Tanzania frendi; hatuwezi kulala njaa wakati watu wengine wanachezea mifwedha…… wanasaza mifedha……”
Mapambano ya Gonza dhidi ya wenye navyo yanaangamiza maisha yake kabla usiku haujaisha. Mwandishi anatuonesha kuwa mapambano dhidi ya umaskini si lelemama bali yanahitaji umoja na mshikamano wa makabwela, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu (uk. 39).
Mwandishi wa riwaya hii ameonesha matatizo mbalimbali yanayoikumba Tanzania ya leo kama vile umaskini,uongozi mbaya na rushwa,matabaka,wizi na ujambazi,umalaya na matatizo mengine mengi na hizo ndizo dhamira ndogo ndogo.
- SUALA LA UONGOZI NA RUSHWA
Azimio la Arusha lilianzishwa mwaka 1967 hapa Tanzania lilikusudia kujenga mfumo wa Ujamaa.Katika Azimio hilo suala la uongozi bora lilijadiliwa kwa kina hasa misingi yake.Mwandishi anaonyesha kuwa licha ya kulipa kipaumbele suala la kujenga ujamaa lakini bado kuna viongozi ambao wanakiuka misingi ya kujenga jamii yenye haki na usawa.Mwandishi ameonesha kuwa viongozi wetu wako mstari wa mbele kupokea rushwa ili watoe huduma .Katika uk 13 mwandishi anasema;
“Natafuta kazi”
“Kazi?”
“Ndiyo kazi”
“Je una chochote?”
“Kama nini?”
“Ma-dalla kadhaa!”
“Ya kazi gani?”
“Ili tumlainisha meneja. Unajua meneja ni mzee wa nyumbani, lakini habari hii ya dalla anaipenda sana. Hii ni silaha kubwa tukitaka kufanikiwa mambo ya siku hizi magumu”
Akameza mate na kuendelea kusema
“Isitoshe, kila mtu tutakamopita kabla ya kufika kwa mzee itabidi kutoa dalla kadhaa. Iko kazi”
Pia Suala hilo linajitokeza tena katika uk.21 pale Gonza anapomtaka Chioko amshawishi mpenzi wake Nelli ahonge mwili wake ili apate kazi, mwandishi anasema;
“Mwambie shemeji ahonge bwana.Kama hana pesa kama sisi anaweza kutumia njia nyingine. Kama ujuavyo yeye ni msichana bwana. Anao uwezo mkubwa sana wa kuwaweka sawa maofisa wa aina yoyote ile. Usiwaone wasichana wengine wamevalia wakipita mitaan ukadhani ni hivihivi tuu”
Watu walioshika nafasi za uongozi kwenye taasisi mblimbali wanaajiri watu baada ya kupata hongo au rushwa na Iwapo mwombaji kazi ni mwanamke basi wanatarajia kulala nae kwanza kabla ya kumpatia kazi. Lakini wakati mwingine msichana anayehusika anakuwa kama mcheza kamari kwani anaweza kutoa penzi na kazi hapati kama anavyosema mwandishi (uk. 21);
Kuna vijana ambao pengine wanahonga lakini kazi yenyewe wasipate, na kuna wasichana ambao pamoja na kuyakubali matakwa ya wakubwa, lakini hawafanikiwi katika matumaini yao ya kupata kazi; wakubwa waliowaahidi kuwapa kazi wanawapa mimba na kuwatelekeza. Hivyo basi, mwandishi anaona kuwa wanasichana hawanabudi kuepuka rushwa kwani katika hali kama hii msichana anaweza kuwa Malaya.
Mwandishi anaitaka jamii kuwainga viongozi wanaotumia vibaya madaraka waliokabidhiwa. Badala ya kuwaajiri watu kufuatana na kanuni zinazofahamika katika masuala ya ajira, wao wanafuata kanuni zao wenyewe ambazo zinawaletea maslahi binafsi.Mwandishi anaonyesha kuwa Matokeo ya msichana kutafuta kazi yanakuwa kupata mimba (uk. 42-43). Msichana wa namna hii, ambaye anapata mtoto na hana uwezo wa kumhudumia,kuna uwezekano mkubwa wa, kama hakufikiria kutoa mimba kabla ya kujifungua au kumtupa mtoto baada ya kuzaa.
Suala la uongozi mbaya, wizi na njia mbaya ambao watu wenye nyadhifa wanazitumia ili kupata pesa za kutumia kwa ajili ya starehe zao ni kinyume na misingi ya Azimio la Arusha. Gonza anasema kwamba, watu wengi ambao wana fedha nyingi wamepata fedha hizo kutokana na njia ya dhuluma au za wizi. (uk 43);
“Wewe sikiliza, Chioko uawaona wale wenye mifedha hapa mjini”? Wengi wao wamedhulumu walishikwa? Hawakushikwa. Walioshikwa n bahati mbaya na hawana raha”.
Katika hali kama hii maskini au walalahoi au makabwela hawafurahii matunda ya uhuru yaani kana kwamba uhuru umetekwa nyara na watu wachache ambao wananufaika kutokana na uhuru huo.
Wakulima na wafanyakazi sio wanaonufaika na jasho lao, bali vibepari uchwara ambavyo vimepata bahati ya kujipachika katika sehemu za uongozi. Wao ni wanyonyaji wa jasho la wakulima na wafanyakazi. Wakati wakulima na wafanyakazi wanatoa jasho lao kufanya kazi, viongozi hao ndio wanaolifaidi jasho hilo. Matokeo yake ni kuwa, matunda ambayo mkulima na mfanyakazi wanayahangaikia usiku na mchana hawayaoni. Hawaoni jinsi ambavyo serikali inajitahidi kuondoa matatizo yao yanayowakabili. Wameshindwa kujikimu walau kwa mahitaji yao ya lazima.
- UJENZI WA VIJIJI VYA UJAMAA (Operesheni sogeza)
Miaka ya 1974 Tanzania ilifanya ikifanya jitihada ya kujenga vijiji.Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kujenga vijiji .Katika kujenga vijiji vya ujamaa hapa Tanzania njia mbili zilitumika ambazo ni:
Ø Kuwaweka pamoja watu ambao nyumba zao zilikua mbalimbali
Ø Kuwasaka watu wasio na kazi mjini na kuwapeleka vijijini.
Dar-es-salaam,kama miji mingine ya Tanzania umewahi kukumbwa na msako wa watu wasio na kazi ambao wamekamatwa na kupelekwa kijiji cha mapinduzi.Riwaya ya Usiku Utakapokwisha inalishughulikia tatizo hili.Watu wasiokua na kazi wanakamatwa na kupelekwa kwenye kijiji cha ujamaa cha mapinduzi, miongoni mwa wanaokamatwa ni wauza karanga,maji ya barafu,korosho kama asemavyo msanii(uk. 48);
“Walishikwa wa aina aina.Wauza kashata,Njugu na karanga,walikuweko wauza pombemwenye mabaa,walikuweko walevi pia,walikuweko wale waliofikiriwa pia kuwa ni wezi walikuwepo.Tulipofika huko tulikua watu wengi, huko tulikuta pia wachawi waliokuwa wamekamatwa na kupelekwa huko kama adhabu. Tulikutana wengi……………………”
Watu hawa wote walishukiwa kwamba,wao ndio wezi ambao usiku wanabomoa majumba. Iwapo ni hivyo, basi kitu ambacho kinafanyika ni kama kuusafisha mji, watu ambao hawatakiwi kuwepo mjini na kuwapeleka vijijini.
Je,ndiyo kusema kwamba vijiji ndio vimekuwa ngao ya kuhimili mishale inayorushwa?Je, pengine kusingeweza kupatikana na uwezekano mwingine wa kuwashirikisha watu hawa katika shughuli za kijamii wakiwa hukohuko mijini badala ya kuwasukumizia vijijini ambako hawakai bali wanatafuta mbinu za kutoroka na kurejea tena mjini? Aidha, kuwapeleka watu kama wezi na wanyang’anyi vijijini kunatoa picha ya kwamba vijijini ni mahali pa kuishi watu wa aina iyo. Hivyo basi, kitendo hiki kinaweza kufisha juhudi zote za kujarbu kuviimarisha vijiji na kuvifanya mahali pazuri pa kuishi.
Katika maongezi yake, Nelli anakisifu mno kijiji cha Helela.Anatoa picha ya kwamba hapo ni mahali ambapo hakuna matatizo (uk. 49);
“Kijiji hiki kina wakazi wapata elfu saba. Kina umeme, kina maji, kina chakula kingi na cha kutosha kuwalisha majirani wa vijiji vikubwa visivyopungua kumi. Helela imesonga mbele, kijiji cha Helela kina mashamba mengi ya mahindi na ngano, mashamba ya maharage, ndizi na smatunda mengineyo. Naikumbuka Helela, naipenda Helela. Helela imesonga mbele”.
Picha anayoitoa Nelli kuhusu Helela ni ishara ya maendeleo ya kuridhisha kwa vijiji vya ujamaa vilivyoanzishwa na serikali, na vijiji lazima viige maendeleo ya kijiji cha Helela.
Baada ya kukamatwa Nelli na kupelekwa kijiji cha mapinduzi, kulitokea matatizo mbalimbali. Kwanza kulitokea fujo, mkusanyiko wa waovu mbalimbali hauwezi kujenga jambo la maana. Kutokana na kuwepo kwa wachawi, wezi, wahuni ikatokea vita vya kugombea wasichana (uk. 48).
Baada ya zile vurugu za kijiji cha mapinduzi, watu wengi sana walifanikiwa kutoroka na kurudi tena mjini. Kurudi kwao mjini kunaonesha kwamba, katika mfumo kuna jambo Fulani ambalo linakosekana. Je, jambo hilo ni lipi? Nelli (uk.50) anasema; “Utaratibu wake si mzuri”.
Katika mfumo wetu wa kijamii kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa mji na kijiji, mfumo wa kiuchumi na kijamii umeipendelea zaidi niji kuliko vijiji. Katika masualaya mawasaliano na huduma nyingine za kijamii hakuna uwiano kati ya miji na vijiji. Vitu hivi vimeshughulikiwa mjini lakini vijiji vimeachwa nyuma. Huu upendeleo wa miji dhidi ya vijiji ndio unaowafanya watu wakapendelea zaidi kuishi mijini kuliko vijijini. Na ndio maana watu waliosakwa na kupelekwa kijiji cha Mapinduzi wanaamua kutoroka kutoka huko na kurudi mjini ambako kuna starehe ambazo huko vijijini hazipatikani.
Kwa upande wa Gonza, yeye hana sababu ya kwenda kijiji cha mapinduzi. Gonza amezaliwa mjini, amekulia mjini na ataendelea kuishi mjini kama alivyosema(uk. 50);
“Mimi binafsi sipendelei “Alijibu Gonza haraka haraka”.
“Kwa nini?
“Nimezaliwa mjini, nimekulia mjini; na sasa makazi yangu ni mjini; shamba nimfuate nani na nikafanye nini?”
Kwa upande wa Nelli, amejifunza maisha ya kijijini na baada ya kurudi mjini anatamani kurudi tena kijijinimradi tuu ahakikishwe usalama wake, anasema (uk. 51);
“Niko tayari kurudi tena huko nikihakikishiwa usalama wangu”.
Gonza anashangaa kusikia tamko la Nelli la kutaka kurudi kijijini. Kwa ujumla, msanii anaonesha kuwa kuwasaka watu na kuwapeleka vijijini si suluhisho la msingi. La muhimu ni kutafuta suluhisho la matatizo hayo mjini hukohuko.
- SUALA LA MAPENZI
Ni hali ya kupenda na kuvutiwa sana inayojengeka baina ya mtu mzima mmoja na mwingine.Mwandihi ameainisha aina mbili ambazo;
Ø mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo (pesa).
Ø Mapenzi ya kweli
Kwa upande mwandisi ameainisha kama ifuatvyo;
Mosi,mapenzi ya kweli kati ya Chioko na Nelli; hawa walipendana hasa katika shida na raha,katika uk.2-3 Chioko anasema;
“Barua hiyo ilikuwa imetoka kwa mpenzi wake Nelli. Nelli alikuwa tumaini la maisha yake ……Nelli……Nelli alikuwa waridi la moyo wake.Nelli alikuwa kioo cha maisha yake…..Nelli alijazwa katka kilakona ya maisha yake”.
Pia katika uk.6 Chioko anaendelea kusisitiza kuwa ;
“Nelli ndiye ua langu…Nelli ndiye waridi la moyo wangu mchanga ……….Nelli wangu “
Maneno ya Chioko dhidi ya Nelli ni ishara tosha kuwa ,hawa watu walipendana kwa dhati na mapenzi yao hakuna wa kuyatenganisha labda kifo tu.
Pili,mapenzi ya kweli kati ya Chioko na Gonza, Chioko na Gonza walikuwa marafiki hasa na wasiri wakubwa. Walikuwa wamesoma wote huko Iringa,ingawa kiini chao kilikuwa tofauti.Wazazi wao walikuwa wakifanya kazi huko Iringa. Na huko ndiko walikokutana vijana hawa wakashibana.Walielewana sana.Walikuwa wameelewana hata wakawa wanazungumza kwa kutumia viungo vya miili yao na sasa walikuwa wamekutana tena hapa jijini na waliishi pamoja kwa kusaidiana hadi kifo cha Gonza.
Kwa upande wa mapenzi ya uongo ambayo msingi wake ni pesa mwandishi anaonyesha kuwa Wanawake wengi waliwapenda wanaume tofauti kwa sababu ya pesa. Wanafunzi nao walikua kwenye mkumbo huohuo,wa kupenda wanaume kwa sababu ya pesa,kama asemavyo msanii (uk 17);
“Utanipa nini nawe katika kipindi hiki cha dhiki”? Alidharau msichana mmoja alipokuwa ametupiwa kombora la penzi na kivulana kitanashati kilichokua kinasoma hapa jijini”.
Mwandishi wa riwaya hii anaonesha kuwa mapenzi ya pesa kwa kiasi kikubwa yanatokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili watu wa tabaka la chini. Nakutokana na hali hiyo ndiyo maana linajitokeza tatizo la umalaya jijini.
- TATIZO LA USAFIRI
Mwandishi anaonesha kuwa katika jiji la Dar-es-salaam kuna tatizo kubwa la usafiri kwa watu wa tabaka la chini.Usafiri pekee unaotumiwa na watu wa tabaka la chini ni UDA ambapo mtu unakaa kituoni kwa muda mrefu Kutokana na uchache wa mabasi ya UDA.Katika uk. 27 mwandishi anasema;
“Walifika kituoni, hapa walikuta umma wa watu, utadhani kulikuwa na sherehe ya kumtoa mwali na ambaye leo hii amefunga ndoa”
Mwandishi anaoneshak kuwa Licha ya watu kukaa sana vituoni kusubiri usafiri pia kuna tatizo la msongamano wa watu kwenye vyombo hivyo vya usafiri. Watu wanasukumana, kila mmoja akigombea nafasi.Hasara za kusukumana huko ni kuibiana na kupata vilema ambavyo havikutegemewa (uk. 29).
Mwandishi naonesha kuwa kwenye vyombo hivyo vya usafiri, kuna matusi ya kila aina.Mtoto anamtukana mtu mkubwa, konda anamtukana abiria,abiria wanamtukana konda na dereva, matokeo yake ni matusi mtindo mmoja. Kutukana matusi kwenye vyombo vya usafiri ni kinyume na utaratibu wa jamii, kwani kwenye vyombo hivyo kuna watoto.Hivyo matusi hayo yanawakomaza watoto kabla ya umri wao (uk. 29-34).
Kutokana na tatizo hili la usafiri kwa watu wa tabaka la chini; wengi wao wanachelewa makazini na kwenye shughuli nyingine za kujenga taifa. Mwandishi ameongelea tatizo hilo miaka ya 1990, na bado tatizo hili linaendelea, leo hii watu wanapitia madirishani kutokana na tatizo la usafiri.
- UTOAJI MIMBA NA UTUPAJI WA WATOTO
Suala la utoaji mimba linaonekana kuota mizizi katika jamii ya sasa.Mwandishi amejadili suala hili kwa mapana.Kwa kuangalia suala hili kwa mapana zaidi inaonekana kwamba, ukiacha wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi wengine wote wanafukuzwa shule wanapopata mimba. Tatizo hili pia linapelekea utoaji mimba au utupaji wa watoto (uk. 56).
Mwandishi wa riwaya hii anaonesha kuwa suala la utoaji mimba na utupaji wa watoto ni tatizo sugu, na hili kwa kiasi kikubwa linasababishwa na umasikini .Katika uk. 42-43 mwandishi anasema;
“…… Mara ngapi watu huimba jijini juu y wasichana wanaoitwa Malaya ‘ na wale wanaotupa watoto mapipani……… wanawalaumu…… eti Malaya! Ati wahuni! Ni kweli wanauza miili; sawa lakini tumekaa na kufikiri kwa nini? Nani anapenda mwili wake? Ni mwanake gani angependa kumridhisha kila mwanaume? Hakuna!Nani anapenda kutupa watoto? Hakuna lakini kuna maana gani kutunza mtoto wakati huna chakula cha kumlisha? Uhai wa mtoto huyu ni nini kama si chakula? Kwa msichana anayetafuta fedha akipata mimba ni suala la bahati mbaya yeye anataka chakula …… matokeo ya mtoto hayakutarajiwa wala hayaheshimu”
Suala hili linafungamana na suala zima la mfumo wa kiuchumi na kijamii. Wasichana wanatoa mimba au kutupa watoto kwasababu hawawezi kuwakimu kimaisha. Mkabala wa jamii dhidi yao ni wa kikatili. Kupata kwao mimba kunaangaliwa kama mtu ambaye amefanya dhambi isiyosameheka.Kuogopa hali ngumu ya jamii kunawasukuma wasichana hawa ama kutoa mimba au kutupa watoto.
Katika kutatua tatizo hili mwandishi anapendekeza kwamba, lazima tuchunguze kwanza mfumo wa uchumi na kijamii. Mfumo mzima wa kiuchumi na kijamii hauna budi kuchunguzwa. Na katika mambo hayo ndimo ambamo jawabu la tatizo hili linaweza kupatikana.
- NAFASI YA MWANAMKE
Katika riwaya hii mwanamke amechorwa katika nafasi mbalimbali.
Kwanza mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe kwa wanaume.Viongozi na mameneja wengi wanawatumia wanawake kukidhi haja zao za kimwili pindi wanawake hao wanapokwenda kutafuta kazi ili apate kazi lazima amstareheshe kwanza mwajiri wake (uk. 23).
Pili,mwanamke amechorwa kama kitega uchumi na ndiyo maana Gonza alimshawishi rafiki yake Chioko amshawishi mchumba wake Nelli akahonge penzi apate kazi ili wapate hela ya kwaajili kukidhi mahitaji yao muhimu ya nyumbani.
Tatu, mwanamke amechorwa kama kiumbe duni asiye na maamuzi yoyote katika jamii zaidi ya kumtegemea mwanaume, katika uk 56 mwandishi anasema;
“Mwanamke …kwani mwanamke nani? Kila cha maana hubebwa na mwanaume.Haki zote anazo mwanaume. Ndio mwamuzi na hakimu nyumbani.Kazi ya mwanamke? Kuzaa, kupika na kumtumikia mume. Mwanamke!”
Nne, mwanamke amechorwa kama mshauri mzuri wa mwanaume,mwandishi anaonesha kuwa Nelli kama mshauri mzuri.Kwanza aliwashauri Gonza na Chioko kurudi kijijini na pia aliwashauri kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali za kibiashara zinazoweza kuwafanya waishi na ndugu na wote wanaowahusu hapa mjini (uk. 51).
kwa ujumla Mwandishi anawalakini juu ya nafasi ya mwanamke katika jamii.Mwandishi anaona mwanamke hana mchango wowote katika jamii zaidi ya kumtegemea mwanaume tu.Mwanamke pia ananafasi yake katika kuleta maendeleo ya jamii kama alivyo mwanaume.
DHAMIRA NYINGINE
8.UGUMU WA AJIRA
UJUMBE
Ø Ili tuweze kujenga jamii mpya lazima tupige vita uongozi mbaya na rushwa.
Ø Mfumo wa elimu unaotolewa haumjengi mwanafunzi kujitegemea, bali kutafuta kazi za ofisini.
Ø Umoja na mshikamano kwa watu wa tabaka la chini ni njia mojawapo ya kupambana na umasikini.
Ø Kufanya kazi kwa bidii ni njia mojawapo ya kuondokana na umasikini.
Ø Kutoa mimba au kutupa watoto chanzo kikubwa sni hali ngumu ya maisha kwa wale wanaohusika.
Ø Tatizo la usafiri litatatuliwa iwapo tu serikali itajenga miundo mbinu zaidi ili kuwezesha kununuliwa kwa magari mengi.
MGOGORO
v Kuna mgogoro kati ya wenye navyo (matajiri) na wasio navyo (masikini).
v Mgogoro kati ya tabaka tawala na tabaka tawaliwa.
v Mgogoro kati ya mgambo na walalahoi (masikini).
MSIMAMO
Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii na baadhi ya suluhisho la hayo matatizo.
FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa umasikini utaisha iwapo masikini watafanya kazi kwa bidii na kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara ambayo itawaingizia kipato cha kuweza kujikimu. Vilevile anaona kuwa mfumo wa kiuchumi na kijamii lazima ubadilishwe.
FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa rejea katika riwaya yake. Ameigawanya riwaya yake katika sura tisa na matukio kutoka sura moja kwenda sura nyingine ni changamano.
Mtindo
Msanii ametumia mtindo wa masimulizi na Nafasi zote tatu amezitumia. Vilevile ametumia mbinu mbalimbali za kifasihi simulizi.
Kwanza kuna matumizi ya nyimbo,mfano katika ukurasa wa 23;
KILINDWACHO
Ajabu ya kilindwacho,
kwa upeo wa kulinda,
kilindwacho hutokea.
Na kwa mwizi kikanenda
Jizi likatoa macho
na kikanena kilindwa,
mwizi ni’ be hima hima,
ili nende nikalindwe.
Pili mwandishi ametumia hadithi ndani ya hadithi. Hii inapatikana katika kurasa za 19, 24 na 42.
Tatu,matumizi ya barua,Barua mojawapo ni ile anayoandakiwa Gonza na Chuchu kutoka Zambia inayomtaka Gonza aende Zambia, huko kuna maisha mazuri.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha rahisi iliyojaa misemo, methali, tamathali za semi, mbinu nyingine za kisanaa na taswira mbalimbali.
v Misemo/ Nahau
- Mtu anayelala mbavu za mbwa – (uk.1).
- Mtu anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio yake (uk. 7).
- Hatukupata kiamsha kinywa (uk.10).
- Jitu hili la miraba mitano (uk. 29).
- Hawamziki mama yao akafika chini (uk. 39).
v Methali
- Ukishindwa kupata kwale mawindoni rudi na bundi (uk. 43).
- Nguo ya kuazima haisetiri matako (uk. 36).
- Jino la pembe si dawa ya pengo (uk. 36).
- Alipo kilema usikunje kidole (uk. 3).
- Usipochomwa mwiba hujui kiatu (uk.5).
TAMATHALI ZA SEMI
v Tashibiha
- Hata majengo yaliyokuwa yamesimama kama askari jela wa kikoloni yalikuwa shwari (uk.4).
- Lakini iliyobeta kdogo mithili ya mdomo wa bata (uk. 5).
- Yalikuwa katika siri ya moyo wake mithili ya kaburi lifichayo maiti (uk. 5).
- Jogoo kama mfalme wa nyumba alifunza vifaranga kunya tunduni (uk. 33).
v Tashihisi
- Alichukuliwa na usingizi haraka haraka, guu moja kalipinda na kuligandisha ukutani bila yeye mwenyewe kujijua (uk. 1).
v Sitiari
- Sehemu ambayo ina mabanda mbavu za mbwa yenye kushika tama kwa wanyonge (uk. 1).
- Nelli alikuwa waridi la moyo wake; Nelli alikuwa kioo cha maisha yake (uk. 3).
- Nelli ndiye waridi la moyo wangu mchanga (uk. 6).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
v Tanakali sauti (Onomatopea)
- “Myaau! myaau!myaau!Sauti kali ya paka ilisikika juu ya paa (uk. 1).
- Haa! Haa! Mwanaume mzima unaogopa (uk. 9).
- Baada ya muda kidogo nasikia sauti kali pyaaaaa.
v Takriri
Ø Kila kitu kilikuwa kimya! Kimya kushoto, kimya kulia …… Hata mbele kulikuwa kimya (uk.3).
Ø Alikuwa na kiu, Kiu kubwa! ….. Alijua miugulio ya kiu (uk. 7).
Ø Nimeporwa a-a-a, nimeporwa jamani? Watu hawakujali (uk. 29).
TASWIRA
Katika riwaya hii mwandishi ametumia taswira mbalimbali kama ifuatavo;
Kwanza ametumia taswira zionekanazo za wadudu/wanyama kama vile nzi, kunguni, mende, viroboto, panya, paka, n.k kuashiria makazi duni ya watu wa hali ya chini huko Manzese.
Pili, sehemu nyingine katika riwaya hii giza limetumika kuashiria matumaini finyu ya makabwela kuweza kupata nafuu katika maisha yao ya kila siku.
WAHUSIKA
Mwandishi ametumia wahusika watatu ambao ndio washiriki katika riwaya hii. Wahusika hao ni Chioko, Gonza na Nelli: kuna wahusika wengine kama vile Chuchu, Nyundo, Matiko, Kazimoto, Priscilla, Titos, n.k.
- CHIOKO
– Amemaliza darasa la saba na anatafuta kazi ya ofisini. Yeye ni kiwakilishi cha vijana ambao baada ya kumaliza masomo yao wanakimbilia mjini ambako wana mategemeo ya kupata kazi ya kuajiriwa.
-Chioko anakaa kwa rafiki yake Gonza, Manzese.
-Alikuwa rafiki yake Gonza na msiri wake na kabila lake ni Mngoni.
-Chioko hakubahatika kwenda sekondari kutokana na kifo cha babake aliyetakiwa ampe vifaa vya shule.
– Alikuwa mpenzi wake Nelli na alikuwa tegemezi kwa kila kitu.
- GONZA
– Huyu ni rafiki yake Chioko na kabila lake ni Mgogo na alisoma mpaka kidato cha nne.
– Anaishi Manzese ambako anaendesha maisha yake kwa kuuza karanga. Ni kutokana na hizo karanga ndio anaweza kutosheleza kwa kiasi fulani maisha yake naya Chioko pamoja na Nelli.
-Anaishi maisha ya kikabwela katika chumba kimoja.
– Anayaelewa maisha na mbinu za namna ya kuyaishi. Gonza ndiye anayemfafanulia Chioko ambavyo wanawake kwa wanaume wanavyotumia mbinu mbalimbali kupata kazi.
– Anawakilisha mawazo na malalamiko ya tabaka linalokandamizwa. Anaona jinsi mfumo wa uchumi unavyowapendelea baadhi ya watu ambao wanafanikiwa kimaisha kutokana na wizi au udanganyifu, pamoja na kutofuata maadili ambayo jamii imekubaliana.
-Malalamiko aliyonayo ni ya kimsingi, ndiyo yanayomsukuma kuwa mwizi.
– Anataka kuyakimbia maisha kwa kwenda Zambia KWANI akifika huko atapata kazi.
- NELLI
– Huyu ni mpenzi wake Chioko na katika harakati zake za kutafuta maisha anakamatwa na kupelekwa kijiji cha Mapinduzi; ambako katika muda mfupi tu wa kuishi huko kunakuwa na athari katika maisha yake.
-Anataka kurudi katika kijiji cha Helela au Mapinduzi kama watamhakikishia usalama wake.
– Ni muhusika ambaye amechaguliwa kuwakilisha mawazo ya kijiji. Kutokana na kuishi kwake kijiji cha Mapinduzi amebadilika kabisa kimaendeleo, na hana analoongelea kuhusu kijiji cha Helela isipokuwa sifa tu. Hivyo anafaa kuigwa na jamii.
MANDHARI
Mandhari ya riwaya hii ni ya jijini Dar-es-salaam,hasa sehemu za Manzese, Kariakoo,Posta,Tandika na Buguruni.Vilevile kuna mandhari ya nyumbani, barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, kwenye mabaa,mitaani, n.k.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu Usiku Utakapokwisha linasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki kwa kuwa Neno Usiku linamaanisha Giza.Giza linaloongelewa na mwandishi ni matatizo wanayokabiliana nayo watu wa tabaka la chini kama vile; Umaskini,Hali ngumu ya maisha,Ukosefu wa ajira,Tatizo la usafiri n.k Je lini matatizo haya yatakapokwisha? Matatizo haya yamefananishwa na Giza kulingana na utatuzi wa matatizo hayo.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Mwandishi amefaulu kwa kiasi kikubwa;
-Kuonesha matatizo mbalimbali yanayowakabili mafukara na makabwela hapa nchini.
-Kuonesha chanzo cha matatizo hayo.
-Kutumia lugha rahisi inayoeleweka na amewachora vizuri wahusika kuwakilisha hali halisi ya jamii.
KUTOFAULU
Suluhisho la matatizo ya makabwela halijapatikana mpaka mwisho wa riwaya, tunachoona ni wahusika kuandika kwenye mikokoteni yao “Iko siku” (uk.36). Hili ni suluhisho la kukatisha tamaa, hiyo siku ni lini na kwa nini isiwe sasa. Kwa hapa mwandishi hajatuonesha wazi suluhisho la matatizo aliyoyajadili.
Mwl Maeda