MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MBINU ZA KIFANI ZINAZOJICHOMOZA KATIKA RIWAYA ZA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MBINU ZA KIFANI ZINAZOJICHOMOZA KATIKA RIWAYA ZA KISWAHILI
#1
MBINU ZA KIFANI ZINAZOJICHOMOZA KATIKA RIWAYA ZA KISWAHILI
Kwa kiwango cha kozi yetu, tutavidodosa vipengele vifuatavyo:
o   Naratolojia (usimulizi, mwendo wa riwaya)
o   Msuko wa vitushi na motifu
o   Uhusika na wahusika
o   Lugha
o   Mianzo na miisho ya riwaya
Naratolojia
Ni taaluma inayohusu suala la usimuliaji katika kazi za kiuandishi. Hudokeza masuala muhimu yafuatayo:
o   Usimulizi (aina, sehemu alipo msimuliaji n.k)
o   Kuhusiana kwa vitushi na matukio (kusababisha, kuathiriana na kuendelezana).
o   Suala la wakati/muda katika riwaya.
o   Mwendo wa kazi husika.
Aina za Usimulizi katika Riwaya
Kuna aina kuu mbili za usimulizi. Nazo ni: Usimulizi shahidi (huitwa pia usimulizi wa nafsi ya kwanza) na Usimulizi maizi (huitwa pia usimulizi wa nafsi ya tatu).
Usimulizi Shahidi
Huwa na sifa zifuatazo;  
o   Hutumia nafsi ya kwanza.
o   Huwa na umakinifu zaidi katika usimuliaji.
o   Hudondoa yale yashuhudiwayo na mwandishi/msimuliaji tu.
o   Hufaa zaidi katika kazi za kitawasifu na kazi za fasihi pendwa.
o   Humrahisishia msomaji dhana ya masafa ya kiwakati na kijiografia katika kazi husika.
o   Ni rahisi zaidi kupenyeza matumizi ya nafsi ya pili.
o   Dhana ya wakati huenda taratibu.
o   Hujenga uhusiano wa karibu kati ya msomaji na kazi husika (msomaji huweza kujiona yu ahusika zaidi; hivyo, kuweza kwenda hatua kwa hatua samba na mapigo/mihemko ya kazi, hususan kama maudhui yenyewe ni chanya).
o   Mwandishi hana uwezo wa kuona mambo yote kwa wakati mmoja. Hivyo, husimulia jambo hili kisha lile.
o   Huibua kwa karibu kuwapo kwa dhana ya msimulizi ― mwandishi na/au mhusika msimulizi. Rejea usimulizi wa Willy Gamba katika NJAMA.
o Aina hii ya usimulizi huwa na athari kubwa sana kwa wasomaji (kutokana na ufupi wa masafa ya kijiografia na kiwakati).
Usimulizi Maizi
dhana ya umaizi humaanisha uwezo wa mtu kufahamu mambo mbalimbali, ya wazi na ya siri; tena kwa wakati mmoja. Katika uga wa kifasihi, dhana ya umaizi hutumiwa kumrejelea mtunzi/mhusika mwenye uwezo wa kuona, kufuatilia ma kufafanua mambo mbalimbali kwa wakati mmoja. Hata hivyo, ni vema dhana hii ya umaizi ikatazamwa kwa jicho hili tu la kifasihi. Hii kutokana na ukweli kuwa kwa hakika, dhana yenyewe inafungamana sana na uwezo wa KI―UUNGU (uwezo alionao MUNGU). Kuna ukinzani mkubwa wa kimantiki kuhusu usahihi na uwezekano wa utokeaji wake. Hivyo, umaizi unakubalika tu katika muktadha wa kifasihi kutokana na ukweli kuwa mtunzi hujua yote ayatungayo, hujua kila kitu kuhusu wahusika, mandhari n.k. kikubwa akifanyacho ni kuamua tu ni wakati gani (katika tukio/sura gani) na kwa namna gani ayatongoe matukio yake. Kwa hali hiyo, mtunzi huweza kuonekana kuwa ni mmaizi.
Sifa chomozi za Usimulizi Maizi
o   Hutumia nafsi ya tatu.o   Huwa na uhuru zaidi katika usimuliaji (huweza kuteua la kusimuliwa na lakuachwa).
o   Humruhusu mtunzi kurukaruka katika usimulizi wake (huweza kusimulia hili mara lile).
o   Huruhusu usimulizi wa hata mambo yasiyoshuhudiwa na mwandishi/msimuliaji.
o   Hufaa zaidi katika kazi za kiwasifu.
o  Dhana ya masafa ya kiwakati katika kazi husika huweza kukimbizwa au kurushwa―rushwa, kwa mfano usimulizi katika Kusadikika (rejelea suala la safari na umri wa wajumbe).
o   Ni vigumu kupenyeza matumizi ya nafsi ya pili ikilinganishwa na usimulizi shahidi.
o   Uhusiano kati ya msomaji na kazi husika huwa wa kando 9msomaji hujiweka kando), hivyo hufuatilia mtiririko mtiririko wa vitushi kwa utulivu na mtuo.
o   Msimulizi huweza hata kuchupa hadi ndani ya fikra za watu na kutoa kifikiriwacho.
Vijitawi vya Usimulizi Maizi
Usimulizi maize huweza kufanywa kwa namna tatu ambazo ni: Usimulizi Penyezi, Usimulizi Tinde na Usimulizi Horomo.
(a)      Usimulizi Penyezi: Ni Usimulizi ambao msimuliaji hujitokeza na hata wakati mwingine kuwashirikisha wasomaji. Huweza kusimulia kisha akajiingiza mwenyewe. Kwa mfano, “hata mimi niliona aibu, sijui wewe”.
(b)  Usimulizi Tinde. Huu ni usimulizi ambao hutumia kaida za ki―hisia/ki―dhana. Huweza pia kuitwa kwa jina la usimulizi nusu―nusu au usimulizi shinda. Hii ni kutokana na hiyo hali ya msimulizi kutokuwa na hakika ya akisimuliacho. Aghalabu, hutumika katika vitushi vinavyotakiwa kutafuta jawabu/ufumbuzi wa utata fulani. Kwa mfano, vitushi vya riwaya pendwa 9hususan riwaya za kipelelezi).
©      Usimulizi Horomo. Usimulizi wa kurukia―rukia matukio na miktadha tofauti. Usimulizi huu ndiyo unaoruhusu uchanganyaji wa matukio yanayosimuliwa. Ni kama vile mtunzi/msimulizi huwa juu akimulika matukio yatokeayo kote duniani na ndani ya akili za watu kisha kuyasimulia. Ni vigumu sana kwa mtunzi kutumia aina noja tu katuka kazi yake. Mtunzi huweza kuchanganya aina zote za usimulizi katika kazi yake. Hii itategeneana na msuko wa kazi yenyewe pamoja na malengo ya mtunzi.
Mwendo wa Riwaya
Maana
Dhana hii hurejelea suala zima la kasi, mtiririko na mshindilio wa usimulizi wa vitushi vya riwaya kwa kuzingatia vigezo vya Msuko, Maudhui, Masafa ya Kiwakati na Masafa ya Kijiografia. Suala hili la mwendo huuathiri usomaji na msomaji mwenyewe katika ujenzi wa uelewa. Riwaya huwa na viwango tofauti vya mwendo kutokana na kuwepo kwa tofauti katika usanaji wa vigezo vilivyotajwa hapo juu. Kuna zenye mwendo wa kasi, nyingine zina mwendo wa kati/wastani na nyingine zina mwendo wa polepole.
Riwaya zenye mwendo wa kasi ni zile ambazo mtunzi huzisana kwa namna ya kurusha matukio. Aghalabu, riwaya zenye maudhui ya kusisimua au kufurahisha huwa na mwendo wa kasi. Kwa upande mwingine, riwaya zenye maudhui ya kitanzi (ya kuhuzunisha) huwa na mwendo wa polepole. Riwaya zenye maudhui yenye mseto wa kusisimua au kufurahisha pamoja na kuhuzunisha huwa na mwendo wa wastani.
Kwa mfano, riwaya yaweza kusimulia habari za mtu aliyeko Tunduru; kisha mtu huyo hupanga safari ya kwenda Tanga. Katika riwaya yenye mwendo kasi, twaweza kumuona mtu huyo Tunduru kisha ghafla twaambiwa yuko Tanga. Bali kama mwendo wa riwaya ni wa wastani au polepole, tutaweza kuchanganua jinsi atakavyosafiri safari yake yote pamoja na misukosuko mingine ya safari atakayokumbana nayo.
Mifano ya riwaya zenye mwendo wa polepole ni: riwaya nyingi za Shaaban Robert na Kezilahabi kama vileKusadikika, Adili na Nduguze, Mzingire, Nagona, Uhuru wa Watumwa. Mifano ya riwaya zenye mwendo wa wastani ni: Utata wa 9/12. Mifano ya riwaya zenye mwendo wa kasi ni: riwaya pendwa nyingi, mfano, Njama.
 Hitimisho kuhusu mwendo wa riwaya
Kwa jumla, riwaya za Kiswahili zimekuwa zikibadilisha miendo yake kulingana na maudhui ya nyakati mbalimbali. Mwendo wa riwaya nyingi za wakati wa vuguvugu la kudai uhuru ni wa polepole. Hii ni kwasababu ya maudhui yaliyotamalaki kwa wakati huo yalijaa huzuni na jitimai kwa kiasi kikubwa. Baada ya uhuru, mwendo wa riwaya ulibadilika kidogo, ulikuwa wa wastani kwa kuakisi maudhui na msuko. Mwendo wa kasi katika riwaya ulishamiri katika miaka ya 80 ambapo kulikuwa na riwaya zilizoiga kazi pendwa za magharibi. Hizi zililenga kusisimua na kuburudisha zaidi.
Mtagusano
Ni mwingiliano wa vipengele mbalimbali katika kazi ya fasihi. Kwa namna fulani, huweza kuhusishwa na kaida za mwigo au uathiriano. Twaweza kusoma kazi fulani ya fasihi na kuona kuwa ina mwingiliano mkubwa na kazi nyingine. Mtagusano au mwingiliano huo waweza kuchagizwa na hali ya kuiga au kuathiriwa. Mtagusano huweza kujidhihirisha kupitia maudhui (mwingiliano wa kaida za maisha ya watu au jamii tofauti), lugha, mandhari n.k. dhana hii inajitokeza sana katika riwaya za Kiswahili kutokana na sababu zifuatazo: mosi, ni waswahili kuwa na mwingiliano mkubwa na watu wa jamii nyingine, hali ambayo husababisha pia wanariwaya kusawiri maisha hayo ya kimwangiliano katika kazi zao. Pili, ni utandawazi. Kupitia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, dunia imedogoshwa na hivyo, kukuza mwingiliano wa wanaulimwengu.
Msuko wa vitushi katika riwaya za Kiswahili
Riwaya za Kiswahili zimekuwa zikitumia motifu za namna mbalimbali katika kuvisuka vitushi vyake. Motifu ni msuko au mwegamo mkuu autumiao mtunzi kujenga fani na maudhui alengayo kuyawasilisha. Yaani; kupitia motifu husika, sehemu kubwa ya mambo mengine kama vile maudhui na fani. Aghalabu, motifu katika kazi za fasihi huwa na mrudio wa kiwango kikubwa katika ujitokezaji wake; kiasi cha hata kuweza kuathiri fikra za msomaji au mhakiki kwasababu huweza kumeza kiini cha dhamira halisi.
Baadhi ya motifu maarufu zitumiwazo na waandishi wa riwaya ya Kiswahili ni:
o   Mapenzi
o   Safari
o   U ― jini
o   Mauaji
o   Upelelezi
o   Uhusika wa wanyama
o   Usihiri (umazingaombwe)
o   Ufutuhi (sherehe, raha na vichekesho)
o   Utanzia (mateso, vifungo, mabaa/majanga kama vile njaa na ukame).
o   Starehe (pombe, sigara, disko na kamari).
Riwaya za mwanzo zilitumia motifu ya safari katika kuvisuka vitushi vyake. Aghalabu, safari hizo zilihusisha bahari. Hivyo, motifu hizo ziliakisi pia misukosuko ya kibaharia. Mifano: riwaya za mwanzo za Shaaban Robert kama vile Adili na Nduhuze, Kusadikika. Pia Uhuru wa Watumwa. Riwaya nyingine zilitumia motifu ya u― jini au ki―jini. Hizi pia ziliakisi mazingira ya upwa wa bahari. Kama ilivyo kwa motifu ya safari, hii nayo ni miongoni mwa nduni za fasihi simulizi. Nduni nyingine maarufu ya fasihi simulizi ambayo inajitokeza katika vitushi vya riwaya za Kiswahili ni uhusika wa wanyama. Hali hiyo ya matumizi ya wahusika wanyama katika vitushi vya riwaya ni miongozi mwa ithibati ya kuwako kwa ufungamano wa karibu kati ya riwaya na fasihi simulizi; kwani hiyo ni kaida maarufu katika hekaya, visakale, visasili na ngano. Wanyama maarufu wajitokezao katika riwaya za Kiswahili hususani zile za mwanzo ni kama vile nyani (Adili na Nduguze), Paa (Nagona).
Mabadiliko makubwa ya msuko wa vitushi katika riwaya za Kiswahili yanadhihirika katika usahili na uchangamani wake. Dhana hii ya usahili na uchangamani wa vitushi yarejelea mpangilio wa vitushi vyenyewe katika kazi. Katika riwaya za mwanzo, kulikuwa na usahili. Kwa sasa, wasanii huviweka vitushi katika hali ya uchangamani. Riwaya pendwa, kwa upande wake, zilimezwa na motifu za mauaji, starehe, upelelezi na mapenzi.
Mianzo na miisho ya riwaya za Kiswahili
Mianzo
Namna mbalimbali za mianzo ya riwaya za Kiswahili:
o   Ya kisira
o   Ya kifomyula au kijadi au kihafidhina
o   Ya kifalsafa
o   Ya kifumbo
o   Ya ki ― swali
o   Ya kiufafanuzi
o   Ya kimajazi
Miisho 
Kwa upande wa miisho, riwaya nyingi za Kiswahili huwa na miisho ya:
o   Kifomyula au kijadi
o   Ya kifalsafa
o   Ya kiutatuzi
Maelezo ya jumla kuhusu mianzo na miisho ya riwaya za KiswahiliKuna tofauti kubwa ya riwaya za mwanzo na za sasa. Zile za mwanzo ziliakisi kwa kiasi kikubwa mianzo ya nathari simulizi. Mianzo na miisho hiyo twaweza kusema ilichukua matumizi ya vifungu vya kifomyula. Dhana ya vifungu vya kifomyula hapa yamaanisha utunzi wa neno, tungo au aya kwa namna ya kuirudia katika kazi moja au miongoni mwa waandishi tofauti. Mathalani, kulikuwa na matumizi ya vifungu kama vile:
o   Hapo zamani za kale, palikuwa na….(mianzo)
o   Paukwa pakawa (mianzo)
o   Hadithi hadithi (mianzo
o   Na hadithi yangu yaishia hapo (miisho
o   Waliishi raha mustarehe (miisho)
o   Hatimaye alifanikiwa sana (miisho)Baadaye, mianzo na miisho ya hadithi ilibadilika. Mathalani, kukawa na mianzo ya ki ― taharuki, hususani katika riwaya ramsa. Hizi ni zile zinazotawaliwa na msisimko au burudani. Pia, riwaya za kifalsafa.Kuhusu miisho, ingawa wanariwaya waliowafuatia wale wa awali wamejikwepesha na miisho ya kifomyula; bado miisho yao inalandana kimaudhui. Hii ni kwa sababu, kwa jicho la jumla, riwaya nyingi bado zinaisha kwa namna ya kuonesha msfanikio. Mafanikio haya ni yale yatokanayo na mivutano baina ya ama ubaya na wema, ukale na usasa na kadhalika. Mathalani, katika Haini, twaona tutakosa, alifikiria, na kweli leo ametoka! Na hata hao waliobaki, pia watatoka tu! Alisema Hamza. (uk.267). Mwisho huu unamrejelea yuleyule mhusika mkee aliyedokezwa pia katika mwanzo wa kazi hiyo, Hamza.
MUELEKEO WA JUMLA JUU YA MAUDHUI YANAYOJICHOMOZA KATIKA RIWAYA YA KISWAHILI
Dondoo muhimu kuhusu mielekeo ya maudhui
Maudhui ya riwaya ya Kiswahili yalibeba mitazamo na mielekeo ya sera na mipango ya vipindi mbalimbali vilivyobeba mshindo wa fikra za Waswahili. Vipindi hivyo ni:o   Kabla na wakati wa ukoloni (wakati wa vuguvugu la kudai uhuru)o   Baada ya uhuru/wakati wa Azimio la Arushao   Wakati wa vuguvugu la vijiji na vijiji vya ujamaao   Wakati wa vita ya Kagerao   Wakati wa didimio la uchumi wa duniao   Wakati wa sera za mpango wa kuhuisha mfumo wa uchumi barani Afrika na Duniani.o   Wakati wa vuguvugu la kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingio   Wakati wa vuguvugu la utandawazi (ubinafsishaji)
Maudhui ya riwaya za Kiswahili kabla na wakati wa Ukoloni
Riwaya za Kiswahili kama mojawapo ya kazi za fasihi ya Afrika, zilikuwa na maudhui yaliyojaa manunguniko, jitimai na huzuni kutokana na hali halisi iliyokuwa inawakabili waafrika wengi. Katika wakati huu ndipo hasa yalipokuwa yanajidhihirisha maudhui yaliyolenga kuamsha urazini wa Waafrika kuhusu maovu waliyokwa wanatendewa. Aidha, maudhui yalikuwa yanawakumbusha kuhusu suala la ukombozi. Baadhi ya mifano ya riwaya zilizotungwa kabla ya uhuru ni: Uhuru wa Watumwa, Kusadikika, Kufikirika, Kasri ya Mwinyi Fuad n.k.
Maudhui ya riwaya za Kiswahili Baada ya Uhuru
Hapa, riwaya zilizotungwa zilibadili mkondo wa kimaudhui. Ziliwahimiza watu kuzijenga upya nchi zao na maisha yao kwa jumla. Aidha, kimaudhui zilichanganyika na zile zilizotungwa baada ya muongo mmoja kupita toka uhuru wan chi za Waswahili. Hizi ziliakisi hali halisi ya maendeleo yaliyofikiwa na jamii husika baada ya kupata uhuru. Zilimulika pengo la mafanikio baina ya malengo ya kupigania uhuru na kiwango cha kufanikiwa (matunda yaliyojitokeza). Kutokana na kuwako kwa kiwango kidogo cha maendeleo, maudhui haya yalijaa kejeli, malalamiko na manungu‘uniko. Malalamiko haya yalitoakana na mambo mengi kama vile tofauti ya kimaendeleo kati ya vijiji na mijini na umasikini wa kupitiliza. Mifano ya riwaya hizo ni: Shida, Njozi iliyopotea, Kichwamaji na Dunia Uwanja wa Fujo.
Baada ya hapo, kilifuata kipindi cha anguko kuu la uchumi wa Dunia. Anguko hilo lilifuatiwa na kipindi cha ufufuo wa uchumi wa dunia (sera za mpango wa kuhuisha mfumo wa uchumi wa dunia, hususani barani Afrika). Riwaya ya Kiswahili pia iliakisi hali hii.
Maudhui ya jumla yanayojichomoza
Maudhui yanayojichomoza sana katika riwaya ya Kiswahili ni pamoja na:o   Historia au uhistoriao   Mapambano dhidi ya ukoloni (vita vya uhuru/kujikomboa)o   Ujumi wa kiafrikao   Utabakao   Sera za nchi na za kimataifao   Utu na maadili (riwaya za sira)o   Falsafa na itikadi ya kiafrikao   Nafasi ya asasi za dinio   Usihirio   Epistemolojia ya Waswahili
Ujumi katika riwaya ya Kiswahili
Dhana ya ujumi
Ujumi ni tafsiri ya neno la kiingereza “Aesthetics” lililotokana na neno la Kigiriki “Aisthetikos”. Dhana hii iliasisiwa na Alexander Baumgarten mwaka 1735. Ujumi ni taaluma inayoshughulikia falsafa ya uzuri, ubaya na ladha. Taaluma hii hujibu maswali kama vile:
o   Uzuri/ubaya ni nini?o   uzuri/ubaya hutokana na nini?o   Nini hutuongoza kuamua uzuri/ubaya wa kitu?Maswali haya yakijibiwa, itakuwa rahisi kwetu kutoa maamuzi kuhusu ujumu unaojitokeza katika riwaya za Kiswahili na Fasihi ya Kiswahili kwa ujumla. Dhana ya uzuri au ubaya huweza kufafanuliwa vema kwa kuhusisha mambo makuu matau ambayo ni:
o   Ufahamu/akili/hisio   Idili za jamii husikao   Malengo au matumizi
Idili ni jumla ya nguzo―msingi au vigezo ambavyo jamii hujiegemeza kwavyo kama vipimo vya kuhakikia au kulinganishia uzuri au ubaya wa jambo. Kila jamii na kila kipindi kina idili zake ambazo hutumika kupimia thamani ya vitu mbalimbali. Kigezo kingine (ambacho ni sehemu ya idili) kinachotuongoza kufanya maamuzi ya uzuri/ubaya wa kitu ni malengo au matumizi ya kitu husika. Kitu chochote huweza kuwa kizuri/kibaya kwa watu wa jamii tofauti kutokana na kuwa na malengo au matumizi tofauti.
Kwa mfano: Kalamu yaweza kuwa nzuri kwa mwanafunzi na ikawa mbaya kwa mkulima, mwanamke mnene aweza kuwa mzuri kwa Mwafrika na mbaya kwa mjapani. Katika muktadha wa kozi hii, maarifa haya ya ujumi ni kiunzi muhimu kwetu katika kufanya aamuzi ya kiulinganisho kuhusu falsafa za jamii mbalimbali.Hivyo, uzuri ni matokeo ya kuafikiana au kuwiana kwa uhalisi wa kitu (kadri kinavyoonekana) na idili za jamii husika. Ubaya (ambao ni kinyume cha uzuri), ni kutokuwapo kwa uwiano baina ya uhalisi wa kitu hicho na idili za jamii.Udhihirikaji wa ujumi katika riwaya za KiswahiliKatika kazi mbalimbali za fasihi, ujumi huweza kudhihirika kwa kuchunguza vipengele vifuatavyo:o   Usawiri wa wahusikao   Mtindo wa sanaa yenyewe kwa jumlao   Uumbaji wa maumbile ya vitu (mandhari)o   Ukweli na uthabiti wa maudhuio   Katika riwaya za Kiswahili, ujumi wa kiafrika hujitokeza kupitia vipengele mbalimbali. Baadhi ya vipengele hivyo ni:o   Dhana yenyewe ya U―Afrikao   Utamadunio   Vyakula na mfumo ― mloo   Mgogoro wa mwingiliano wa ujumi wa Kiafrika na ujumi wan chi za kigeni.
Historia au uhistoria
Kwa jicho hili, riwaya huweza kutazamwa kama:o   kama kazi ya historia ya waswahilio   kama nyenzo ya kufundishia historiao   kama sehemu ya historia yenyewe
Riwaya huweza kubeba vionjo vingi vya kihistoria. Kwa namna fulani, riwaya huweza hata kutumika kufundishia historia kwa jamii fulani. Hata hivyo, kwa yeyote aamuaye kuzitumia kwa lengo la kufundishia historia lazima awe na uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya riwaya na historia.
Riwaya, kwa kawaida, zina vipengele vya ubunifu, hivyo uhistoria uweza kuwapo kwa malengo ya kiyakinifu (kuakisi uhalisia wa mambo) au kwa lengo la kisanaa. Hivyo, kupitia riwaya hizo, jamii hupata nafasi nzuri ya kujitambulisha na kujifunza mambo mengi yaliyotokea katika nyakati zilizopita. Baadhi ya mifano ambazo zaweza kutupatia maarifa ya kihistoria ni: Miradi Bubu ya Wazalendo, Gamba la Nyoka, Ndoto ya Ndaria, Uhuru wa Watumwa na Moto wa Mianzi.
Utabaka katika Riwaya za Kiswahili
Maudhui haya yalitokana na kuwako kwa wakoloni katika jamii za waswahili kwa muda mrefu. Hata baada ya uhuru bado jamii ilitawaliwa na matabaka. Riwaya ya Kiswahili haikuwa nyuma katika kuisawiri hali hiyo. Katika riwaya mbalimbali waandishi waliwajenga wahusika katika namna ya kujipambanua na kuyapambanua matabaka mbalimbali yaliyokuwapo katika jamii. Aidha, waandishi wenyewe walipaswa kuwa makini kwani walimulikwa na jamii. Hii ni kutokana na ukweli kuwa jamii ilikuwa inajiuliza:
o   mwandishi au wahusika wa kazi husika ni nani?o   Wako katika tabaka gani?o   Wanamsemea nani?
Suala la mipango na sera za nchi na za kimataifa katika riwaya za KiswahiliSuala hili pia limezungumziwa sana na riwaya za Kiswahili. Suala la sera na mipango kadha huwenda sambamba na vipindi mbalimbali vinavyoshuhudia kuanzishwa kwa sera hizo. Kila kipindi kilikuwa na mipango na sera zake.
Epistemolojia ya waswahili katika riwaya za Kiswahili
Epistemolojia ni tawi la falsafa linalishughulikia maarifa. Kila jamii ina duara lake la maarifa na ujuzi. Riwaya za Kiswahili zinamchango mkubwa wakuwasilisha maarifa mbalimbali kwa wasomaji. Dhana ya maarifa hapa yafaa itazamwe kitofauti na dhamira za kawaida. Hii ni kwasababu, maarifa hayo si lazima yawe wazi kwa wakati mwingine huwa fiche. Jambo hili la kuwasili epistemolojia huweza kufanywa na mtunzi kwakukusudia au bila hata kukusudia. Vilevile, miongoni mwa wasomaji wa riwaya, lazima pawe na utofauti katika kuibua epistemolojia inayopatikana katika riwaya husika. Hii inatokana na ukweli kuwa suala la kubaini mafunzo, maarifa na ujuzi linauhusiana pia na utambuzi na tajiriba ya msomaji.
Falsafa na itikadi ya kiafrika katika riwaya za Kiswahili
Maana ya falsafa na itikadi
Falsafa: kweli ambayo mtu anaiamini, anaisimamia na anaiishi au anaishi nayo.
Itikadi: ni njia mkondo au nyenzo ambayo mtu anaishikilia na kuitumia ili kuifikia kweli anayoiamini (falsafa). Dhana hizi mbili zinakanganya na zinachanganya wanazuoni wengi.
Falsafa na itikadi za kiafrika katika riwaya za Kiswahili
Kuna riwaya kadhaa zenye maudhui ya kifalsafa katika riwaya za Kiswahili. Baadhi ya wanazuoni wa kifalsafa wanadai kuwa hakuna mtu anayeishi bila falsafa. Hivyo, hata waandishi wa riwaya ni ngumu kusema huyu hana falsafa: kwamba, takribani kila riwaya kuna falsafa inayoshadidiwa na kupigiwa mbiu. Baadhi ya falsafa zinazojitokeza sana katika riwaya za Kiswahili ni:
o   Uduara wa maisha
o   Ujuala (kuwapo kwa Mungu na kani za Kiuungu)
o   Usihiri na ushirikina
o   Thamani ya mtu na utu:
o   Udugu na mbari/ukoo (thamani ya uzazi n.k.)Baadhi ya itikadi zinazojitokeza sana katika riwaya za Kiswahili ili kushadidia falsafa hizo ni:
o   Dhima ya dini na asasi zake
o   Ujadio   Sera mbalimbali kama vile ujamaa na kujitegemeao   Dhana ya kijadi kama vile uganga, matambiko n.k.
Suala la nafasi na asasi za dini katika riwaya za Kiswahili
Maudhui yake yanamulika masuala yafuatayo: maana na asili ya dini: dini zinanafasi gani katika jamii? Umuhimu wa watu kumcha Mungu, unafiki wa wacha Mungu, udhaifu wa asasi za dini au viongozi wa asasi za dini n.k. mifano ya kazi au riwaya: Siku ya Watenzi Wote, Pete n.k.
Suala la Usihiri katika riwaya za Kiswahili
Ni miongoni mwa nduni maarufu zinazojitokeza katika baadhi ya riwaya za Kiswahili. Suala hili uhusisha dhana za ushirikina, uchawi, wanga na uganga.
Uchawi: ni ufundi au utaalamu wa kutumia dawa na mbinu nyingine za uganga kwaajili ya kuleta madhara kwa watu na viumbe. Pia uhusisha maudhui yanayoakisi uhalisia ajabu au uhalisia mazingaombwe. Kuna migongano kuhusu kuwa au kutokuwapo kwa dhana ya uchawi hapa duniani. Wapo wanaoafiki kuwapo kwake na wengine wanapinga na kudai kuwa hizo ni imani tu. Hata hivyo, kuwapo kwa jambo hili kunadhihirishwa na hata vitabu vitakatifu vya dini. Mifano ya riwaya zenye imelea vya usihiri ni: Babu alipofufuka, Utata wa 9/12, Dunia Yao, Miradhi ya Hatari, Walenisi, Bina —adamu n.k.
Riwaya ya Kiswahili na kumbo la maendeleo ya kiteknolojia
Sayansi na teknolojia kwapamoja zimesaidia kukuza utanzu huu wa riwaya. Sayansi na teknolojia zimeshadidia katika ukuaji wa mambo kadhaa katika maendeleo ya riwaya, baadhi ya mambo hayo ni pamoja na:
o   Utunzio   Uchapishajio   Usambazajio   Usomajio   Urejeleaji n.k.
UHAKIKI WA RIWAYA TEULE ZA KISWAHILI
Dondoo muhimu katika uhakiki wa riwaya teule
o   Vitabu vinavyopaswa kusomwa
o   Vitabu vinavyopaswa kuzamiwa
o   Mambo ya kuzingatia katika uhakiki
Mambo haya matatu yanaendana sanjari na:
o   Kuijua nadharia ya uhakiki
o   Nadharia za kuhakikia
o   Kufanya uhakiki (wajumla na ule mahususi, uzingatia
o vipengele mahususi).
o   Ushahidi katika suala la uhakiki
o   Kufanya uhakiki linganishi
Nadharia za kuhakikia fasihi
Ni jicho la kurunzi ya kufikia lengo fulani. Uhakiki mzuri ni ule utumiao nadharia. Zipo nyingi sana bali huweza kugawanywa kutokana na lengo la uhakiki. Hakuna nadharia bora wala dhaifu. Kati  ya nadharia hizo nyingi hukamilishana, hutegemeana na kuathiriana. Makundi makuu au maaru ni:o   Zilengazo masuala bia (Ya kiulimwengu)o   Zilengazo masuala ya kijamii (za kisosholojia)o   Zilengazo kazi husika (Umbo au muundo au maana)o   Zilengazo msomaji wa kazi za fasihi.
Baadhi ya nadharia hizo ni:
o   Uhemenitiki
o   Usemezano
o   Uhalisia
o   Uhalisia ajabu
o   Ualisia
o   Umatini au semiotiki
o   Urasimi
o   Urasimi mpya
o   Ulimbwende
o   Undhanaishi
o   Uana au Ufeministi
o   Umaumbo
o   Umuundo
o   Udenguzi au uumbaji
o   Upokezi
o   Udodosinafsi au saikolojia changanuzi
o   Mwingiliano matini
o   Usimulizi au Naratolojia
o   Mwitikio wa Msomaji
o   U — Bakhtini au Ukanivali
o   Ungitamaduni au Ubaada Ukoloni
o   U — Foucault
o   Umaksi
o   Uyakinifu wa kitamaduni
o   Uakisio   Unegritudi
o   Usasao   Usasa leo
o   Uhistoria
o   Uhistoria mpya
o   Uhakiki mpya.
Vitabu vya riwaya vinavyopaswa kusomwa
Angalau riwaya za kila kundi au kijikundi zisomwe na kupata picha ya jumla ya maudhui na fani yake (usomaji huu wa jumla pia uzingatie riwaya zilizotungwa na waandishi kutoka kanda kubwa za waswahili ambazo ni Tanzania bara, Tanzania visiwani na Kenya).
Mwongozo kwa watakaowasilisha uhakiki
Madondoo muhimu yapaswayo kuwemo katika uwasilishaji ni:
o   Ikisiri (taarifa za mtunzi na utunzi, aina ya riwaya)
o   Dhamira chomozi
o   Mbinu chomozi za kibunilizi
o   Hitimisho (kituo au mkolezo, riwaya zinazofanana nazo).
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)