MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
UHAKIKI WA RIWAYA YA KUSADIKIKA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
UHAKIKI WA RIWAYA YA KUSADIKIKA
#1
Kusadikika ni riwaya yenye sura 9. Kila sura inajadili suala ama jambn muhimu ambalo mwandishi amedhamiria liwafikie wasomaji wake. Pengine tuziangalie sura hizo kifupi.
Sura ya kwanza inahusu mashtaka ya Waziri Mkuu wa Kusadikika yaliyoelekezwa kwa Karama. Aidha, sura hiyo inamwelezea Waziri Mkuu, bwana Majivuno kuwa ni mtu mwenye haiba kubwa na uhodari usiolinganishwa na chochote.
Katika sura hiyo, raia wa Kusadikika aitwaye Karama anadaiwa kuwa:
Quote:
· Anapata haki ya kulindwa lakini hana shukrani
· Karama anadaiwa kuwa ana tamaa na si mtii. Hofu ya majivuno ni kuwa kama Karama angeachwa afanye atakavyo, angeweza kudai udiwani, uwaziri na hatimaye ufalme.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa shtaka lake, baraza lilitakiwa kutoa hukumu kwa mshtakiwa Karama. Aidha, imeelezwa katika sura hiyo kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi ya Kusadikika mshtakiwa aliruhusiwa kujitetea; na utetezi ulichukua muda wa siku sita.
Sura ya pili inaanza na maelezo juu ya taaluma ya uanasheria. Katika maelezo yake, mstakiwa anazumgumza kwa ufasaha mkubwa. Karama anatumia wahusika mbalimbali katika kutoa utetezi wake. Aidha anaelezea kwanza maana ya uanasheria.
Sura ya tatu inaanza utetezi wa Karama. Karama anaelezea madhila yaliyomfika Mwanakusadikika aitwaye Burhani baada ya kuifanyia makubwa nchi ya Kusadikika. Buruhani alifanya safari ya mbali ya Kaskazini kwa ajili ya kuitafutia maarifa nchi ya Kusadikika. Baada ya kurudi nchini Kusadikika na kuelezea mazuri aliyoyaona alikokwenda na ambayo yangewafaa watu wa Kusadikika, Buruhani alitumbukizwa kifungoni – kifungo cha maisha!
Sura ya nne inaelezea madhila yaliyompata mjumbe wa Mashariki aitwaye Fadhili. Inaelezwa katika sura hiyo kuwa Fadhili alileta ujumbe kutoka Mashariki uliohusu kufutiliwa mbali chuki, watu kusikilizana na kushirikiana kwa upendo. Badala ya kufurahiwa na kukubalika, Fadhili aliitwa mwongo, mwoga na mwota ndoto zisizokubalika. Alidharauliwa, hakuthaminika hata kidogo!
Katika sura ya tano, mshtakiwa alisimulia kisa cha Kabuli, mjumbe aliyetumwa Kusini. Karama alielezea safari ya Kabuli aliyesafiri katika nchi tatu: nchi za Juju, Hasira na Kiasi. Kabuli alipata matatizo mbalimbali. Ujumbe aliouleta haukuthaminiwa na alipewa hukumu ya kifungo cha maisha na kazi ngumu.
Sura ya sita inaelezea kuhusu mjumbe aliyetumwa Magharibi ajulikanaye kwajina la Auni. Karama alieleza kuwa Auni alisafiri mbali, akapata matatizo mengi. Auni alielezwa kuwa alikutana na vipofu waliopata madhila kutokana na tabia mbalimbali. Baada ya kupata matatizo makubwa, Auni alirudi Kusadikika, akapata madhila, hakuthaminiwa.
Sura ya saba inahusu mjumbe aliyetumwa Mbinguni. Mjumbe huyu aliitwa Ridhaa. Ridhaa alileta habari mbalimbali zikiwemo kuhusu haki, bidii, thamani ya muda na kadhalika. Taarifa hii ilipofika Kusadikika mjumbe Ridhaa alipatwa na adha zilezile.
Mjumbe wa Ardhi alikuwa wa mwisho, na alielezwa katika sura ya nane. Sikuhiyo Karama alielezakisachamjumbeAmini. Amini alileta habari za watu kuwa waadilifu wakubwa. Kulitolewa rai kuwa watu hawa waigwe, lakini ujumbe huu ulifanya anyang’anywe milki yake na kufungwa maisha.
Baada ya usimulizi wa wajumbe hawa sita, Mfalme aliliamini Baraza litoe hukumu. Upeo wa hadithi hii ni sura ya tisa ambapo inatolewa hukumu. Katika sura hii, inasemekana wale waliohudhuria Baraza waligawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza lilisema mshitakiwa aangamizwe. Kundi la pili lilimwonea huruma kwa sababu alikuwa akitetea haki. Hukumu ilitolewa na mshtakiwa alionekana hakuwa na hatia. Hii ni kwa sababu mshtakiwa alikuwa akitafuta jinsi ya kusaidia Sheria ya Kusadikika kwa njia mpya. Baraza liliamua kwamba Karama pamoja na wale wafungwa sita ambao visa vyao vilisimuliwa wafunguliwe, wapewe fidia na yote waliyoleta Kusadikika yafuatwe.
MAUDHUI
(a) Elimu katika Jamii
Riwaya ya Kusadikika imeleta jambo moja muhimu sana katika mfumo wa maisha ya jamii. Jambo hili linahusu elimu. Elimu inatakiwa ipewe tafsiri inayostahili na ikishatafsiriwa katika misingi na mkabala unaotakiwa, ni muhimu kuhakikisha wanaohusika wanapata elimu inayotakiwa. Katika riwaya ya Kusadikika kuna tafsiri zaidi ya moja ya “elimu ya uanasheria”. Tafsiri ya kwanza inaonyesha chuki na imepotoshwa. Mudir wa Sheria za Kusadikika alipotakiwa kueleza maana ya uanasheria alisema: “Uanasheria ni elimu ya kupingana na sheria” (uk.8).
Lakini Karama mwenyewe (ambaye ni mshtakiwa) alitoa tafsiri ya kuridhisha: Uanasheria ni elimu ya hukumu kwa mujibu wa Sheria zilizokubaliwa. (…) Elimu hii hasa husaidia sheria kwenda katika njia yahaki …” (uk.9).
Katika riwaya ya Kusadikika, tumeonyeshwa kuwa elimu iliyofika nchini Kusadikika ilikuwa ya manufaa makubwa. Manufaa haya yanatokana na matumizi bora ya elimu hiyo. Mwandishi anaeleza kuwa: “Baada ya miaka michache kupita, mafunzo yote yaliyoletwa Kusadikika na wajumbe wake yaliziamsha bidii zilizokuwa zimelala. Mavuno ya mafunzo hayo yaliifanyiza Kusadikika kuwa nchi moja katika nchi zilizostawi kabisa.” (uk.57)
Kauli hii inaonyesha jamii ya Kusadikika ilitumia elimu vyema. Ni muhimu kuelewa hapa kuwajambo hilo la mafanikio halikuja kwa mara moja. Mifano imeonyesha kuwa wengi wa watu waliokuwa madarakani, kama vile Mudir wa Sheria za Kusadikika, ilimchukua muda mrefu kukiri elimu na uwezo aliokuwa nao Karama. Ingawa Mud.ir wa Sheria anaonekana alikuwa na elimu, lakmi elimu yake haikutumiwa vyema kwa muda mrefu. Ndiyo maana pale mwanzoni Kusadikika ilikwama, na elimu ya Uanasheria ilipoanza kutumiwa vyema, mafunzo ya wale wajumbe kutumiwa vyema, Kusadikika ilibadilika!
(b) Haki katika Jamii
Mara nyingi watawala mbalimbali wamekuwa wakikataa kutoa haki kwa baadhi ya watu waliopata kuonyesha uwezo maalumu wa kiuvumbuzi. Kwa mfano, inaonyeshwa katika riwaya ya Kusadikika kuwa lengo la Karama la kuanzisha taaluma ya Uanasheria lilikuwa ni la kutaka haki itumike katika mambo mbalimbali. Nchi ya Kusadikika inaonyeshwa kuwa ilikosa haki kwa watu wake kwa muda mrefu. Imeonyeshwa kuwa watu waliokuwa wamepewajukumu la kulinda na kutetea haki kama vile Mudir wa Sheria hawakuwa wakijua misingi ya haki yenyewe. Katika mazingira kama haya, haki haiwezi ikatendeka.
Utoaji wa haki katika jamii huleta utulivu na maendeleo makubwa. Haki huleta demokrasia ya kweli kabisa. Aidha, imebnyeshwa katika riwaya ya Kusadikika kuwa msimamizi wa haki anatakiwa afuate misingi ya kweli tu, Asijali cheo, dini, kabila na kadhalika. Hali, hii imeonyeshwa na Mfalme wa Kusadikika ambaye alikubali ushauri wa
Madiwani waliomwona kwanza Karama kutokuwa na hatia. Mfalme alikiri akisema: “Taibu, hiyo ni hukumu njema. Naafikiana nanyi kabisa. Hapana hukumu nyingine iliyowezekana juu ya ushahidi uliokuwa mbele yetu. Zaidi ya hayo, natoa amri kuwa watu sita waliotajwa katika kesi hii: Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Ridhaa na Amini, wafunguliwe mara moja”. (uk.57). Aidha, mfalme anamaliza “… Kusadikika inamshukuru sana Karama kwa kuitanabaisha wajibu wake…” (uk.57).
Hapana shaka uamuzi wa aina hii haukumfurahisha waziri Majivuno; ambaye ni mtu anayesemekana alijaa inda na tadi. Lakini angefanyaje kupingana na ukweli? Si rahisi! Majivuno hafai kuwa kiongozi wa watu.
© Kweli na Uongo Haviwezi kuwa pamoja
Hii ni dhamira inayoelezea juu ya kutokuwa au kutokubalika kwa mambo mawili yanayopingana pamoja. Ubaya na uzuri haviwezi vikafikia masikilizano.
Katika riwaya ya Kusadikika mwandishi anaelezea kuwa kuna watu walipendelea kuishi katika “miiba ya mashaka ya dunia… Lila na Fila hawatangamani. Kinywa cha Lila kikasema, sikio la Fila hujidai halisikii. Jicho la Lila likiona, lile la Fila hujifanya halioni; moyo wa Lila ukijilazimisha kwa mapenzi na huruma, ule wa Fila hujifanya mgumu kamajiwe lisilo maisha kwa chuki na uadui…”
Nchi ya Kusadikika ilikuwa na maisha ya namna hii kwa muda mrefu. Wachache (Fila) waliyashika mamlaka ya Kusadikika, lakini wengi (Lila) walikuwa chini ya mamlaka haya. Riwaya ya Kusadikika imeonyesha kuwa “vinywa vingi vikisema kwa umoja … ni lazima mafanikio yatatokea”. Madiwani walisema kwa umoja wakashinda. Aidha, Kusadikika imeonyesha kuwa haki ya mtu haipotei na penye ukweli uongo hujitenga. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
Mwandishi amesisitiza sana dhana ya ukweli katika riwaya hii ya Kusadikika. Katika moja ya kauli zake katika riwaya hii anasema hivi kuhusu msema ukweli. “Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake..” Hapana shaka watu walio wengi ni waongo na wanafiki, jambo ambalo Shaaban Robert analiona kama ajali. Na kwa sababu hii, Shaaban Robert anasema: “Nikipatwa na ajali kama hiyo sitaona wivu juu ya watu wawezao kudumu na marafiki zao siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajinyima ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo…” Katika andiko lakejingine lihusulo ukweli, Shaaban Robert anasema:
Quote:
Kweli itashinda mwisho
Namna tunavyoishi
Lauongo lina mwisho
Kweli kitu cha aushi
Kweli haihofu tisho
Wala nguvu za majeshi
Kweli itashinda kesho
Kama leo haitoshi!
Falsafa ya kweli kuhusu maisha ndiyo inayoelekea kutawala katika riwaya hii ya Kusadikika. Falsata hii ndiyo inayojenga migogoro mbatimbali mingine ambayo inasukwa kwenye mgogoro mkubwa wa mastaka unaokuwa kati ya Waziri Majivuno na Karama anayetaka kuanzisha taaluma ya uanasheria ili kuisaidia Kusadikika.
(d) Hasara ya Wivu na Tamaa isiyo kiasi
Riwaya ya Kusadikika inasimulia piajuu ya tatizo la wivu na tamaa isiyo na mipaka. Katika riwaya hii mwandishi anaelekea kutokubaliana na tabia hii. Mwandishi analielezajambo hili kupitia vipofu wawili, Salihi na Sapa. Salihi alikuwa na bahati ya kuomba chochote akakipata. Sapa alipoona hiyyo naye akatamani awe na uwezo huo; ikiwa na maana kuwa aliomba naye angekuwa na uwezo wa aina hii. Huu ni wivu!
Mwandishi anaendelea kufafanua kuwa Salihi na Sapa waliandikiana mkataba wa kugawana chochote kipatikanacho, na ndipo Salihi akaomba upofu na wote wakawa vipofu. Ni wazi kuwa Sapa hakupenda hilo, lakini hii ndiyo thamani ya chuki na wivu.
Falsafa ya mwandishijuu yamaisha inadai amani, upendo, hurumana mengineyo yanayohusu haki, uvumilivu na ukweli kwa mtu. Wivu au chuki hatimaye huleta hasara kama ilivyotokea kwa Sapa. Mwandishi, kwa kebehi na kejeli anamtumia mjumbe Auni kumshauri Sapa: “Pole, Sapa, lakini huna budi kuvumilia mazao ya wivu wako sasa ili ujifunze kuwa bahati ya mwenzio usiilalie nje! Kila mtu ana bahati yake njema” (uk.33).
Sapa alikuwa na wivu mbaya. Wivu mzuri huambatana na juhudi ya kutaka kujua maarifa na kujitahidi kufanya vizuri zaidi, lakini bila kudhuru maisha ya mtu.
(e) Nafasi ya Ndoa na Malezi
Ingawa suala hili halijitokezi kwa wazi sana, lakini mwandishi anaelekea kuamini kuwa suala la ndoa lina msingi wake imara. Mwandishi analaani tabia ya watu wenye mali lakini huzifuja kwenye tafrija na ngoma za kufurahisha. Vibaya zaidi, wenye fedha hutumia fedha hizo kwa kuoana na kuachana kila siku. Kwa mshangao mkubwa, mwandishi anahoji hivi. “Mume mmoja ana fedha kiasi gani ya kuwaolea na kuwakimu wanawake wote wazuri, au mke mmoja ana uzuri gani wa kuolewa na kila mwanaume?”
Mwandishi anaona tatizo kubwa la kuoa au kuolewa ili kufurahisha nafsi. Thamani ya ndoa hapa haipo na kimsingi jambo hili halikubaliki. Kuhusu malezi ya watoto, mwandishi kwa kumtumia mhusika Auni anaelezea: “Tunazaa watoto wengi lakini hatuwalei kiungwana kwa kuwafunza kuzijuadhima zao katika dunia…” (uk.36).
Ndoa ni mahusiano kati ya mwanamke na mwanamme pamoja na uwajibikaji wa msingi kuhusu masuala yote ya msingi yanayohusu unyumba. Mambu hayo ni pamoja na malezi ya watoto, matunzo na mwenendo mwema na kadhalika.
(f) Uongozi Imara unaozingatia Ushauri mzuri
Riwaya, ya Kusadikika inaonyesha kuwa katika nchi ya Kusadikika Mfalme alikuwa mtu mwenye busara na pia watu wema walimshauri vema Mfalme. Uongozi wa nchi yoyote ile unatakiwa uwe na nguzo za msingi katika mambo mbalimbali. Kiongozi anatakiwaawe mtu mwenye busara na anafuata haki bila kujali dini, kabila au rangi kama ambavyo mwandishi anasema; “Watu wenyewe walihitalafiana kwa rangi, lakini kwa akili zao za namna ya ajabu walipatana sana”. Mfalme wa Kusadikika ameonyesha tabia hii pia, kinyume na Waziri Majivuno au Mudir wa Sheria wa Kusadikika. Nguzo nyingine muhimu ni kuwa na washauri wanaostahili na wanaojua nini wanakifanya. Nao, kama vile ilivyo kwa Kiongozi Mkuu, wanatakiwa kuzingatia haki na ukweli, wasiwe watu wanaopendelea upande mmoja. Madiwani watiomshauri Mfalme kuhusu kesi ya Karama wameonyesha kuwa na tabia hii.
Kinyume na nguzo hizo za uongozi, nchi itaingiwa na malalamiko, dhuluma, fujo na kadhalika. Jambo hili linaweza kuiingiza nchi katika angamizo kubwa! Mshikamano miongoni mwa watu; mshikamano kati ya viongozi na waungozwa utatetereka!
(g) Hatari ya Kuamini bila Kuhoji
Nchi ya Kusadikika, imeelezwa kuwa ilikuwa na watu waliokuwa wanaamini (wanasadiki) kilajambo bila kuhoji umaana wake; wala kuwa na wasiwasi wowote. Lakini kauli hii ni ya kushangaza, na kusema kweli imewekwa kikejeli kabisa. Kwa mfano, imeelezwa kuwa “Wakati mataifa mengine yalipojifaharisha kwa mambo kama vile enzi, uwezo na fahari nyingine, taifa la Kusadikika litijivuna kwa sababu ya kusadiki mambo yaliyotoka vinywani mwa watu wake…” Swali ni kuwa, je, mambo yenyewe yalikuwa kama hayo yanayozungumzwa na Majivuno? Kama ndiyo, tunaonyeshwa “unyonge” wa kuamini au kusadiki kila neno lililokuwa likisemwa na wasadikika. Majivuno ni mroho wa enzi na fahari.
Suala la kuhoji jambo lolote miongoni mwa nchi yoyote ni la kuimarisha demokrasia ya kweli. Kwa kutohoji, au kwa kutopewa nafasi ya kuchangia katika sera na maisha ya nchi ya Sadiki, watu wake walihitaji ukombozi mpya ambao ulikosekana.
Waziri Majivuno anaelekea kuwa kiini cha muhtasari wa tabia za serikali mbalimbali za Kusadikika ambazo kimsingi, zilikuwaza kukera. Salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi hii. Hii ni kwa sababu sheria za wasadiki zilikuwa hazimruhusu mshtakiwa kujitetea dhidi ya ushahidi wa mashtaki. Mashtaka mengi yalikubaliwabilaswali, wala kiapo, jambo ambalo hapana shaka liliongeza kero na mzigo kwa wananchi wa Sadiki wa kawaida. Kwa wenye mamlaka, jambo hili kwao linawapendeza na huwani nguzo ya ukandamizaji.
Riwaya ya Kusadikika kwa kupitia mhusika Karama hatimaye imeonyesha umuhimu au nafasi ya demokrasia ya kujieleza na kujitetea kila pale lizukapo shtaka dhidi ya mtu yeyote. Kujitetea kwa Karama, na kushinda kwake kumetoa mafunzo makubwa kwa wasomaji wa riwaya hii. Demokrasia ya kweli ni ile inayothamini uhuru wa kauli na inayolinda sheria.
(h) Umuhimu wa Kutunza siri
Shaaban Robert anaelekea pia kusisitiza umuhimu wa kutunza siri. Siri kama haitunzwi si rahisi kuwa na mipangu ya kiutawala ambayo ni ya manufaa kwa watu. Kabla jambo halijafanyika ni lazima mipango iwe ya siri kwanza. Penye siri pana thamani kubwa katika mazingira ya kawaida. Lakini ni kweli pia penye siri panaweza pawe na mauaji, fujo, fitina na kunyimwa haki kwa baadhi ya watu. Katika Kusadikika, imeelezwa kuwa Karama alikuwa na siri “kama Kaburi lifunikavyo maiti. Alijizoeza kuvitumia vipawa hivi mpaka vilikuwa tayari kutumika siku yoyote katika maisha yake”. Muda wa matumizi ya siri hiyo ulikuwa umefika!
Baadhi ya Vipengele vya Fani
Baada ya kuangalia vipengele vya kimaudhui, sasa tuangalie vipengele vya kifani. Vipengele hivyo ni vile vinavyohusu muundo na mtindo, mandhari, wahusika na matumizi ya lugha.
(a) Muundo na Mtindo
Riwaya ya Kusadikika inatumia muundo wa moja kwa moja katika sura za kwanza hadi ya nane. Katika sura ya tisa ambapo hukumu inatolewa hadithi marejea nyuma na kuangalia ushahidi wa mashahidi mbalimbali. Aidha, ni katika sura hiyohiyo ambapo hadithi inafikia kilele na mgogoro wake mkubwa ulio kati ya Karama na Majivuno kutatuliwa.
Katika kuijenga hadithi hii, mwandishi ametumia mbinu kadhaa ambazo zinaweza kutajwa kama za kimtindo. Mbinu hizo zinajumuisha matumizi ya lugha na ujenzi wa sentensi ndefu na fupi. Kwa kuhakikisha kuwa Shaaban Robert anaibua hisia kali kwa wasomaji wake, kila sura inayosimuliwa inapomaliziwa kuna mbinu anayotumia ya kuibua hisia za msomaji. Angalia kwa mfano sentensi zifuatazo:
Quote:
1. Nguvu ya sheria zanchi lazima ithibitishwe juu yake ili mtu mwingine yeyote asithubutu kudharau.
2. Hilililiposemwa, baraza liliahirishwa.
3. Moyo wa nani usiohuzunika kwa msiba kama huu!
4. Uko wapi uso usiotahayari kwa aibu kama hii!
5. Macho gani yasiyolenga machozi kwa ubaya kama huu!
6. Kusadikika itashukuru lini fadhili za watu wake bora?
7. Hakimu gani mwema achekaye macho ya mtu mwingine kutazama hukumu aliyoitangaza kuwa ni haki?
8. Kwa kuchechemea, wajumbe wetu wamerudi zizini kutoka safari ndefu lakini hawakusaidiwa.
9. Mavuno ya mafunzo hayo yalifanyiza Kusadikika kuwa nchi moja katika nchi zilizostawi kabisa.
Mtindo huu wa kuibua hisia ni wa kipekee miongoni mwa waandishi wa Kiswahili. Aidha, matumizi yake ya lugha na ujenzi wa mbinu nyingine za kisanaa umemweka Shaaban Robert mahali pa kipekee kabisa kisanaa.
Mtindo na mbinu nyingine katika kuimarisha muundo wake ni ule unaohusu wingi/idadi wa/ya watu kwenye mahakama wakati wa shtaka la Karama. Imeelezwa kuwa katika siku ya kwanza watu waliohudhuria walikuwa sudusi moja ya watu wa Sadiki, mji mkuu wa Kusadikika. Siku ya pili inaelezwa kulikuwa na watu thuluthi moja ya watu wa Sadiki. Siku ya tatu Mfalme mwenyewe alihudhuria pamoja na watu wenye vyeo mbalimbali, pamoja na nusu moja ya umati mkubwa wa Kusadikika. Siku ya nne, watu waliohudhuria ni karibu sudusi tano za umati wa Kusadikika. Katika siku ya sita, mwandishi anasema watu waliohudhuria hawakuhesabika: walijaa… nafasi ya kutemea mate ilikuwa haipatikani kwa sababu ya umati mkubwa kabisa…
Tukichunguza mbinu hii, mwandishi anaonekana kuimarisha sana fani yake. Umaarufu wa Shaaban Robert unajitokeza tena kwa mara nyingine.
(b) Mandhari/Mazingira
Kusadikika ni riwaya ambayo imejengwa kuwa angani katikati ya mipaka sita. La msingi zaidi ni kuwa nchi hiyo hufikirika tu, si kwamba imepata kuweko. Hali hii inafanya kazi hii kuwa ya manufaa kwa kila nchi duniani. Ni waandishi wachache mno wanaweza kuwa na mafanikio ya namna hii.
Kwa upande wa Tanzania, tunaweza kusema kuwa riwaya hii yaweza kuwa na mandhari kubwa, kwani mwandishi wake ni Mtanzania.
Nchi ya Kusadikika ina maajabu mengi: yakiwemo wanawake kuzaa watoto pacha. Nchi hii haijapata kusimuliwa wala kuwekwa katika ramani.
© Wahusika
Kusadikika ina wahusika wa aina mbili. Aina ya kwanza ni ya wahusika wanaojulikana kuwa washiriki. Wahusika wa aina hii ni wale walioshiriki kwa namna fulani katika hadithi. Wahusika hawa ni kama vile Karama, Majivuno, Mfalme, Madiwani, Taadabuni, Komeni, Fujo, Boramimi na kadhalika. Kundi la pili ni la wale wahusika aliowatumia Karama katika kufikia lengo lake. Wahusika hawa hawatokei kimwili, wanatokea kimawazo tu. Kundi hili lina wahusika: Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Ridhaa na Amini.
Katika makundi haya, wako pia wahusika wakuu na wabusika wasaidizi.
Kwa upande mwingine, ujenzi wa wahusika hawa ni wa aina mbili: Kuna wale wahusika ambao wamejengwa na tabia zao. Kwa mfano, Majivuno alikuwa namajivuno, Karama alikuwa mwenye karama kubwa, Fadhili alikuwa na fadhila na kadhalika. Aidha kuna pia kuwajenga wahusikahawawanavyoonekana. Kwa mfano tunaambiwa: “Kwa wasifu wa nje, mshtakiwa (Karama) alikuwa hana umbo la kufanya mvuto kwa watu…” (uk.8). Pengine tungewaangalia wahusika hawa mmoja mmoja.
(i) Karama
Huyu ni mhusika mkuu wa Kusadikika. Karama ni raia aliyeshtakiwa na Majivuno kwa kosa la kupinga Sheria za nchi ya Kusadikika. Kwa upande wa baadhi ya watu wenye mamlaka, Karama alidhaniwa kuwa anagombea cheo au madaraka. Aidha alihesabiwa kuwa ni mkosefu wa utii; na mtovu wa shukrani (hakuwa na shukrahi). Karama alishukiwa pia kuwa na wafuasi wengi waliokuwa wakimuunga mkono; katika taaluma ya elimu ya kupinganana sheria.
Karama alikuwa mshtakiwa wa kwanza katika historia ya Kusadikika kuruhusiwa kujitetea. Ni mtu wa kwanza nchini Kusadikika aliyeweza kubadili sheria za nchi yake, Ni shujaa aliyeweza kupambana na kuwaokOawenzakewaliokuwawamefungwamaisha.
Katika wasifu wake wa ndani na nje, Karama alikuwa na sifa zifuatazo:
Quote:
· Kimaumbile, umbo lake lilikuwa baya. Alikuwa hana umbo la kufanya mvuto kwa watu.
· Kwa wasifu wa ndani Karama alikuwa na ajabu tatu: ubongo wa hekima kichwani, moyo wa ujasiri kifuani na kinywani ulimi wa ufasaha. Ni mkweli na jasiri.
Hivi ni vipawa vilivyoundasiri kubwa katika maisha ya Karama.
Quote:
· Alikuwa na tabia ya kuficha siri kama kaburi lifunikavyo maiti. Karama ni jina linalosadifu kauli na matendo yake. Karama ni mfano wa kuigwa.
(ii) Majivuno
Majivuno ni Waziri Mkuu wa Kusadikika. Mwandishi anamjenga kikejeli kuwa alikuwa mtu mwenye haiba (upendo) na uhodari mwingi, jambo ambalo halikuwa sahihi. Alikuwa mjivuni. Alitawala kwa muda mrefu, akawa waziri katika nyakati mbalimbali za wafalme watatu. AIikuwa mtu mwenye inda na tadi, Majivuno alimshtaki Karama kuwa alikuwa akipingana na sheria za Kusadikika, Alikuwa mtu mwenye chuki na wivu mbaya. Majivuno ndiye aliyekuwamsemaji mkuu katika kesi iliyomhusu Karama. Alikuwa mtu mwenye dharau kubwa, na alijihesabu kuwa kidole chake kidogo kilikuwa na akili nyingi kuliko vichwa na miili ya Wasadikika wote ikiwekwa pamoja. Ni mkatili. Alitumia nafasi au cheo chake kupotosha ukweli, kama vile alipotoa fasiri kuwa, “Uanasheria ni elimu ya kupingana na sheria”. Majivuno si mfano bora wa kuigwa.
(iv) Madiwani
Hawa ni wazee wa Baraza la Kusadikika. Walikuwa na kazi ya kusikiliza mashtaka mbalimbali likiwemo lile la Karama. Ni wapenda haki na hujali ukweli. Walimwona Karama kutokuwa na hatia yoyote.
(v) Taadabuni, Komeni, Fujo na Boramimi
Hawa ni wahusika waliokuwa upande wa serikali na kimsingi hawakushiriki kimwili katika hadithi hii; isipokuwa Boramimi.
Taadabuni ni Katibu waSerikali, wakati Komeni ni Amiri Jeshi mkuu. Fujo alikuwa na kazi ya kulinda hazina wakati Boramimi ni Mudir wa sheria. Wahusika Wa kundi hili walimsaidia Majivuno kukamilisha mashtaka yake ya chuki na wivu dhidi ya Karama.
(vi) Wajumbe
Hili ni kundi la wahusika sita ambalo linatumiwa na Karama katika kujitetea. Kwanza, kuna mjumbe wa Kaskazini aliyejulikana kwa jina la Buruhani. Kazi ya Buruhani ilikuwa kusafiri, kutalii na kuandika habari za mambo ya nchi ngeni aliyoyaona kwamba yangestawisha Kusadikika. Karama anaelezea mkasa wa Buruhani kuwa baada ya kukusanya na kuleta aliyoyaona yanafaa, aliaibishwa na kudaiwa ameleta uzushi usio na faida katikanchi ya Kusadikika. Alitumbukizwa kifungoni: Kifungo cha maisha.
Fadhili ni mjumbe wa pili aliyetumwa Mashariki. Alisafiri kuelekea Mashariki na aliporudi alileta ujumbe kuwa wakazi wa nchi za Mashariki waliuchukia uchokozi, na waliuona kama kitu kikubwa cha aibu: Watu hawa pia waliviapizavita ama laana ipitayo kiasi kwa viumbe waliojaliwa busara ya haki; moyo wa wema; ulimi na ufasaha na nasaha; masikio ya kusikilizana, macho ya uongozi; pua ya kutambua harufu; ushirika wa amani; ajali moja na Mungu mmoja. Badala ya kushangiliwa, aliitwa mwongo, mwoga na mwotaji wa ndoto zisizotabirika. Alidharauliwa na kudhalilishwa.
Mjumbe wa Kusini alikuwa najukumu la kuona mambo yalivyo katika nchi tatu za Juju, Hasira na Kiasi. Mjumbe huyu aliitwa Kabuli. Alipatwa na matatizo mengi, na aliporudi alileta ujumbejuu ya matumizi boraya mamlaka, kutunza heshima za watu, kutotenda maovu, kutotumia nguvu kusuluhusha matatizo, n.k. Lakini roalipo ya Kabuli yalikuwa ni adhabu kali ya kifungo cha maisha.
Auni alikuwa mjumbe aliyekwenda Magharibi. Auni aliona watu walipendana wakaishi bila chuki; bughudha, na kuheshimiana. Aliwaona watu walioheshimu ndoa wakazaa watoto na kuwalea. Alipoleta ushauri huo Kusadikika, alipatilizwa adhabu kali ya kitungo na kazi ngumu.
Ridhaa alitumwa Mbinguni. Aliona hali ya ujenzi bora, mabustani, uchoraji, watu walitunza siri, nafasi ya kubadilishwa viongozi kwa kuzingatia utaratibu maalumu na mengineyo. Lakini kama ilivyokuwa kwa wengine Ridhaa naye aliadhibiwa kwa upanga uleule, kifungo cha maisha.
Mjumbe wa mwisho alikuwa aliyekwenda Ardhi aliitwa Amini. Yeye safari zake zilikuwa kupitia ndege Mangara aliyekuwa akila duniani na kulala nyumbani. Ujumbe wa Amini nchini Kusadikika ni kwamba watu wa Ardhi walikuwa waadilifu na walipaswa kuigwa. Lakini alionekana hakufanya jambo la maana, alihukumiwa kifungo cha maisha.
Kwa kutumia wahusika hawa, Karama amejijengea uhalali wa thamani ya utetezi wake. Falsafa inayojitokeza ni kuwa Karama ni sawa na wajumbe sita waliokwenda sehemu mbalimbali ili kuleta “elimu” kwa Wasadikika, hawakuthaminiwa kama Majivuno asivyomthamini Karama. Huruma iliyojengwajuu ya wajumbe hawa ndiyo iliyomwokoa Karama.
(d) Matumizi ya Lugha
Riwaya ya Kusadikika ni miongoni mwa kazi chache za kisanaa zilizotumia lugha kwa ufasaha mkubwa. Matumizi ya lugha yaKusadikika yamefanya kazi hii ionekane kuwa tofauti na kazi nyingine zisizo za kisanaa. Katika uchambuzi wetu kuhusu matumizi ya lugha, kuna vipengele kama vile matumizi ya semi, nahau, methali, tamathali za usemi na mbinu mbalimbali za kisanaa zitaangaliwa. Aidha, Shaaban Robert ni mpenzi wa sentensi ndefu ndefu.
(i) Misemo, Nahau, Methali na Msamiati
Shaaban Robert amedhihirisha uwezo wake mkubwa katika matumizi ya vipengele hivyo. Tukianza na misemo, mwandishi ameitumia sehemu nyingi kitabuni. Kwa mfano, tunamsikia akisema. “mchwa ukikaribia kuangamizwa hufanywa kumbikumbi na huoteshwa mabawa mawili …; au “msema kweli hukimbiwa na marafiki zake…” Kwa upande wa nahau, hizi nazo ni nyingi. Kwa mfano, mwandishi anapozungumzia madhila ya Buruhani, anasema mjumbe huyu “Hakushukuriwa ili kuvunjiwa kadiri”. Katika sentensi hii nahau ni kuvunjiwa kadiri. Nahau ziko nyingi sana humo kitabuni. Pamoja na misemo au nahau, Kusadikika ni riwaya inayotumia methali nyingi pia, Kwa mfano katika usemi mmoja, mwandishi anasimulia, “Mfalme alishawishika kuwaza kuwa kitanda usichokilalia huwajui kunguni wake”. Wasadikika wana desturiya kutafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka…” (uk.24) na kadhalika. Jambo la mwisho kulizungumza katika kundi hili ni lile la matumizi ya maneno magumu, msamiati na lugha kwa ujumla. Maneno haya mapya na magumu yameandikwa kwa italiki pale yanapotokea mara ya kwanza. Mfano wa maneno haya ni pamoja na haiba, tadi, inda, jalali, bughudha, milizamu, nasaba, tuhuma, taaluma, dhima, madhali, adimu, kuabiri, sudusi, na kadhalika. Maneno mengine ni magumu zaidi, na kwa wasomaji wa kawaida au wanafunzi wanaoanza kubobea katika taaluma ya fasihi huenda wakapata matatizo ya kuielewa riwaya hii kirahisi.
(ii) Mbinu za Kisanaa na Tamathali za Usemi
Mwandishi ametumia mbinu mbalimbali za kisanaa katika riwaya yake.
Mbinu hizo ni:
· Mjalizo: Mbinu hii ni ya kuunga sentensi mbili au zaidi bila kutumia maneno ya viunganisho. Sentensi hizo huungwa kwa mikato kama inavyoonyesha katika mfano ufuatao: “Karibu watu wote huko waliuchukia uchokozi kama aibu kubwa, waliviapiza vita kama taana ipitayo kiasi kwa viumbe waliojaliwa busara ya haki; moyo wa wema; ulimi wa nasaha; masikio ya kusikilizana; macho ya uongozi; pua ya kutambua harufu; ushirika wa amani; ajali moja; na Mungu mmoja”. Kimsingi sentensi hii ina sentensi nyingi, lakini zimeunganishwa kwa mikato mbalimbali.
Licha ya mjalizo, mwandishi ametumia tashtiti na vistari mbalimbali. Mbinu hii imeimarisha kaziya sanaa.
· Lugha ya Kishairi: Mwandishi; ingawa ameandika riwaya, lugha iliyotumika mara nyingi ina tabia ya kishairi. Lugha ya lugha ya kishairi imesaidia sana katika kujenga wizani/ridhimu kitabuni humo. Angalia mifano michache.
Quote:
… Mashtaka ya serikali ya Kusadikika juu ya Karama,
anayelindwa na ulinzi wa Mfalme,
lakini si mwaminifu;
anayefaidi haki na mapendeleo ya utawala huu,
lakini hana shukrani;
na aliye chini ya bendera ya nchi hii,
lakini si mtii. (uk.1)
Quote:
Quote:
II
Quote:
… Hapana kitu kijacho
wala kiendacho (…)
kama itakiwavyo (uk. 16)
Quote:
Quote:
III
Quote:
… Ushujaa (…)
ni ngao
kwa nchi ni tegemeo
na kwa Taifa ni uwezo (uk.21)
… Baada ya kutenda (…) waliyoyaweza
Kabuli alihusudika
Buruhani aliponzeka
(na) Fadhili akateswa mateso makubwa (uk.29)
Quote:
Quote:
V
Quote:
… Maisha (…) yalizungukwa
na sauti za kutumbuiza
harufu ya kuliwaza
na maua ya kupendeza
· Ukinzani: Mwandishi anatumia sana mbinu hii ya ukinzani. Ukinzani ni kinyume cha kauli. Katika riwaya hii tuna mifano michache kama hii ifuatayo:
Quote:
Quote:
I
Quote:
… kuwa chini ya mimea hii walesaji na wateswa (uk.28)
Quote:
Quote:
II
Quote:
… Wafalme huvikwa na kuvuliwa mataji yao. (uk.41)
Quote:
Quote:
III
Quote:
… walikuwa hawajui halali wala haramu (uk.25)
Quote:
Quote:
IV
Quote:
Lakini ushindi uliopatikana mwisho ulibadili misiba (…) kuwa fahari ya milele (uk.18).
· Tamathali za Usemi: ShaabanRobert ametumia tamathali mbalimbali za usemi. Baadhi ya tamathali hizo zimejadiliwa hapa chini.
I
Sitiari: Hii ni tamathali ya usemi inayolinganisha na kuhusisha vitu viwili vilivyo tofauti kimaumbile. Tamathali hii huhamisha hisi kutoka katika kitukimoja na kwenda katika kitukingine.
Mwandishi amezitumia tamathali hizi kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, mwandishi anapomwelezea Auni anasema, “… (mtu) huyu alikuwa na bidii ya mchwa ya kujenga nyumba kwa mate.” (uk.31).
Anapozungumzia suala la ushujaa, mwandishi anasema:
Quote:
“… Ushujaa ni husuni kubwa na hazina bora ya kudumishwa. … Ushujaa (…) ni ngao …” (uk. 21).
Anapozungumzia kuhusu Mjumbe Fadhili na mashtaka aliyokuwa nayo, mwandishi anasema:
Quote:
“… Labda ni kweli kuwa mashaka ni mbegu imara katika mioyo ya wanadamu. (uk. 19).
Kuhusu kilimo, mwandishi anasema:
Quote:
“Kilimo ni uti wa mgongo wa maisha ya mwanadamu.” (uk.16).
II
Tashibiha: Tamathali hii inafanahisha vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno: kama, mfano wa, mithili ya, kana kwamba na kadhalika. Mwandishi wa Kusadikika ametumia aina hii ya tamathali kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano mwandishi anapomweleza Majivuno anasema:
Quote:
“Umri wake mkubwa ulizifanya nywele zake kichwani kuwa nyeupe kama fedha. (uk.1)
Majivuno anapozungumza kuhusu maisha ya Wasadikika anasema:
Quote:
“…. Kusadikika (…) imetukuka ulimwenguni kama nyota ya mwongozo wa haki”. (uk.5).
Akielezea uwezo wa Karama, mwandishi anasema:
Quote:
“… aliyavuta masikio ya baraza nzima kumsikiliza kama imamu aliyekuwa akihutubu …” (uk.9).
Mwandishi anapozungumzia suala linalohusu wakati anasema:
Quote:
“Wakati una mabawa kama ndege… (uk.11)
Hii ni mifano michache ya tashibiha. Kusadikika ina tamathali nyingi za aina hii.
III
Tashihisi: Aina hii ya tamathali hufanya vitu visivyo watu kutenda kama watu. Shaaban Robert ameitumia tamathali hii kwa uchache mno katika Kusodikika. Kwa mfano mwandishi anasema:
“Kwa desturi, maisha huwaficha watu wake bora mpaka tokeo kubwa litokee.
“Maisha” hapa yamepewa uwezo wa kutenda wa “kumficha mtu” hadi kukiwa na matatizo.
Baalagha (chuku): Shaaban Robert ana nyakati anazotia chuku katika riwaya hii. Kwa mfano baadhi ya mambo yanayosimuliwa yanatiwa chumvi mno kiasi cha kutiliwa wasiwasi kuhusu ukweli wake. Maelezo yanayohusu nchi ya Majuju ambayo ilikuwa chini ya Mfalme Jeta inasimuliwa kuwa walafi. Maelezo ya ulafi huo yametiwa chumvi mno. Kwa mfano inasemwa kwa Mfalme Jeta:
Quote:
… Mto mrefu mpana ulikuwa ukimiminika katika kinywa chakekikubwa sana. Tone la maji hata moja halikupata nafasi ya kukiepa kinywa hicho. Tani milioni moja za mwamba, milioni moja za chuma, milioni moja za magogo, na milioni nyingi za samaki zilimiminika pamoja na mkondo wa maji humo kinywani pia kila dakika tano. (uk. 26).
Maelezo haya ni chuku kubwa ambayo inafanya baadhi ya mambo kutoaminika.
V
Kejeli: mwandishi ametumia Kejeli nyingi katika riwaya hii. Kwa mfano katika maelezo yanayotolewa na Waziri Majivuno inaonyesha hali njema na haki kutendeka nchini Kusadikika. Kusema kweli hili si jambo sahihi kabisa, kwani, wananchi wa kawaida walikuwa na hali duni na ya kukandamizwa.
Aidha, hizo ni baadhi tu ya tamathali za usemi. Nyingine zinaweza kutafitiwa na kuongezwa katika orodha hii.
(e) Hitimisho
Tumejaribu kuchambua riwaya ya Kusadikika katika vipengele vya fani na maudhui. Tumejitahidi kuchambua riwaya hii kwa kina lakini ni wazi kuwa hatuwezi kusema tumemaliza kila kitu. Ni juu ya wanafunzi kufanya utafiti zaidi.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)