Kuhusu
HALMASHAURI
Bwana Rwaka rwa Kagarama, hii ni mara ya pili ambapo wanitaja kwa jina na kunitaka nitoe maoni yangu kuhusu maswali uulizayo hapa ukumbini mwetu. Mara iliyopita sikuweza kuuitikia mwito wako kwa sababu ya kuzongwa na mambo mengine. Na hata hivi leo ni kama namkata jongoo kwa meno! Ili usije ukanifikiria kwamba nakusafihi, nikaona niupatilize huu upenyenye nilioupata leo ili nitoe maoni yangu kuhusu asili na maana ya hili neno "halmashauri" uliloliuliza.
Mwenzetu Bwana Njonjolo Mudhihir, ambaye naye, maashaaAllah, si mchache, ameshalifafanua. Hakulisaza! Na mzee mwenzangu, Bwana Mudhihir Mohamed, ashayathibitisha aliyoyaeleza Bwana Njonjolo. Kwa hivyo, mimi nitajaribu kuliangalia kivyengine tu hili neno.
Tushaelezwa na Bwana Njonjolo kwamba "halmashauri" latokana na Kiarabu; na pia kwamba neno hili ni mkusanyiko wa kiambishi cha lugha ya Kiarabu "al-" na jina (nomino) "mashawr" au "mashawrah". Maneno haya ndiyo ambayo kwa Kiswahili twayaita "mashauri", na umoja wake likawa "shauri". Maana na matumizi mbalimbali ya haya maneno mawili katika Kiswahili yajulikana; hayahitaji kuelezwa zaidi.
Turudi kwenye hicho kiambishi cha Kiarabu, "al-". (Na hapa najitia usuluhivu, na huenda nikawa napiga maji mafamba, kwani maji haya ni makuu nami; yangu ni ya magoti. Kwa hivyo, iwapo nitateleza, nawaomba wenzetu tulionao humu walio na ujuzi wa lugha ya Kiarabu, wanionapo nazama waniokoe na kunirakibisha.) Nifahamuvyo, hichi "al-" ni kiambishi kitumikacho kuainishia kitu maalumu kizungumzwacho, au kilichokusudiwa. Kwa mfano, tusemapo "kitaab" (كتاب) chaweza kuwa ni kitabu chochote kile kiwacho. Lakini tusemapo "al-kitaab" (الكتاب) huwa twakusudia kitabu maalumu, au tulichokuwa tukizijua habari zake kabla. Bwana Njonjolo ametueleza kwamba, "AL-MASHAURI ni pahala pa masikizano ya kushauriana ili kupata malengo, maelekeo, tuo na alama ya kuweka au inayofaa kufatwa." Kwa hivyo, tukiyazingatia hayo matumizi ya "al-" niliyoyaeleza (na kama sikuteleza), basi hapo patakuwa ni pahala maalumu pa kushauriana; si pahala popote tu.
Lakini tuliangaliapo hilo neno "halmashauri" kama litumikavyo katika Kiswahili, tutaona kuwa - mbali na kuwa ni "pahala" - pia lawa na maana ya watu walioteuliwa au waliochaguliwa kushughulikia mambo fulani, aghlabu ya kiutawala. Ndipo tukawa na halmashauri za miji, za makampuni, na za mambo mengineyo. Kutokana na kwamba "halmashauri" laweza pia kuwa na maana ya watu kama hao, ndipo nikaona kuwa neno hilo lawa pia na maana ya "watu wanaoshauri"; na kwamba hii "hal-" iliyoko mwanzo wa neno hili yatokana na mabadiliko ya matamshi yaliyofanywa na Waswahili lilipoingia katika Kiswahili. Na hayo matamshi yenyewe yaliyobadilishwa yatokana na neno jengine la Kiarabu: (اهل) "ahl".
Kwa Kiarabu, "ahl" lina maana ya "watu"; na aghlabu hutumiwa pamoja na kimilikishi - kwa mfano, (اهلي) "ahliy" (= watu wangu). Au huweza kutumiwa pamoja na jina jengine - kwa mfano, (اهل قرية) "ahl qaryat/qaryah" (= watu (wa) kijiji; wanakijiji); (اهل بيت) "ahl bayt" (= watu wa nyumba (fulani); jamaa), na kadhalika. Au hutumiwa kwa kuchanganya jina na kimilikishi: (اهل قريتي) "ahl qaryatiy" (= watu wa kijiji changu); (اهل بيتي) "ahl baytiy" (= watu wa nyumba yangu).
Kwenye hiyo lugha ya Kiarabu, "ahl" laweza pia kuwa na maana ya "mwenye" au "wenye". Kwa mfano, katika Qur'ani neno "ahl" limetumika mara sabiini na moja, na kwa minyambuliko yake tafauti tafauti. Mahali pamojawapo lilipotumika kwa maana ya "mwenye" ni katika Sura ya 74 (Sura Muddaththir), Aya ya 56: وما يذكرون الاّ ان يشآٰء الله هو اهل التقوىٰ واهل المغفرة (Wa maa yadhkuruwna illaa an-yashaaAllahu, huwa ahlu-t-taqwa wa ahlul-maghfirah) (= Na hawatakumbuka isipokuwa apende Mwenyezi Mungu; Yeye ndiye mwenye (anayestahiki) kuchiwa (kuogopwa) na ndiye mwenye kusamehe.)
Neno jengine la asili ya Kiarabu lianzalo kwa "ahl", ambalo nalo Waswahili walilibadilisha matamshi yake na kuwa "hal-" ni "halbadiri". Maana ya neno hili ni kisomo ambacho watu wengine waamini kwamba kikisomwa kwa nia ya kumwapiza aliyedhulumu, basi huyo dhalimu atadhurika. Katika lugha yake ya asili, neno hili ni "ahl Badr", yaani watu wa Badr. Badr ni mji ulioko jimbo la Madina, katika nchi ambayo hivi leo yaitwa Saudi Arabia, na ambayo kabla ya kuanzishwa utawala wa kifalme huko na kubadilishwa jina, ilikuwa ikiitwa Hijaz. Kisomo hicho cha halbadiri kina majina ya Waislamu wapatao 300 walioongozwa na Mtume Muhammad kupigana katika Vita vya Badr (Kita cha Badr), na wakawashinda wapinzani wao wapatao 1,000. Vita hivyo vilipiganwa tatehe 17 Ramadhani, mwaka wa pili wa Hijra (kwa kalenda ya Kiislamu), ambayo ni sawa na tarehe 13 Machi, mwaka 624.
Hili neno "ahl" lilipoingia katika Kiswahili lilitoholewa na kuwa "ahali" na pia "ahli". Na mwanzo likitumika zaidi kwa maana ya "mke" - lakini pamoja na kimilikishi. Watu wengine wakisema (na mpaka leo wako wasemao), "ahali/ahli yangu" badala ya "mke wangu". Baadaye likaongezewa maana ya "jamaa" wa karibu wa familia au ukoo fulani.
Hizi ndizo maana mbili nilizokuwa nikizijua; na ndizo zilizoelezwa katika makamusi mawili ya Frederick Johnson, Kamusi ya Kiswahili (1935) na A Standard Swahili-English Dictionary (1939); makamusi ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili), Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo la 1981 na la 2004); Kamusi la Kiswahili Fasaha (Baraza la Kiswahili la Zanzibar (2010); na Kamusi ya Karne ya 21 (2011). Lakini katika Kamusi Kuu ya Kiswahili (Baraza la Kiswahili la Taifa, Tanzania, (2015), kuna maana ya tatu: "mwanachama wa klabu au chama cha siasa". Na pia katika Kamusi Elezi ya Kiswahili (2016), iliyotayarishwa Kenya, kumeelezwa maana ya tatu kuwa ni: "wanachama au washiriki katika jambo fulani". Makamusi haya mawili hayana sentensi za mifano ya namna ya kulitumia neno "ahali" kwa maana hizi. Kwa vile maana hizi ni ngeni kwangu, niliwauliza wazungumzaji kadhaa wa Kiswahili wa marika mbalimbali ninaowakinai kwamba waijua vyema lugha hii, ili kuhakikisha. Wote hawakuzijua! Basi kama kuna wenzetu walioko hapa wazijuao, na wawezao kututolea mifano ya sentensi za kuonesha matumizi yake kwa mujibu wa maana hizi, naomba msaada wao.
Kwa ufupi, Bwana Rwaka rwa Kagarama, nakubaliana na maelezo ya Bwana Njonjolo kwamba neno "halmashauri" lina asili ya lugha ya Kiarabu; na pia nakubaliana na maana aliyoieleza. Tutafautianapo ni kuhusu lianzavyo neno lenyewe huko kwenye lugha yake ya asili litokako. Bwana Njonjolo aona ni "al-" na mimi naona ni "ahl-". Hali iwavyo, la muhimu ni kwamba twakubaliana kwa maana na kwa matumizi ya neno lenyewe - kama litumikavyo leo katika Kiswahili. Natumai nimetumika!
- Abdilatif Abdalla
Hamburg, Ujerumani
19 Juni, 2021

Mwl Maeda