Ueneaji: hii ni dhana inayotumiwa kueleza mojawapo ya nadharia za Fasihi simulizi. Hutumiwa kuelezea uhusiano unaokuwepo kati ya hadithi za jamii mbalimbali. Dhamira ya kimsingi ya nadharia hii ni kuonesha kuwa inawezekana kuwa jamii zinazohusika ziliingiliana kihistoria au kutokana na ukaribu wao wa kijiografia kuingiliana huku kunaweza kuwa msingi wa kuwepo kwa hadithi zinazosimuliwa ambazo zinafanana.
Hii ni nadharia ambayo inaelekea kupinga uwezekano wa hadithi hizo kuwa na vyanzo tofauti kwa mujibu wa wafuasi wa mtazamo huu. Inawezekana tu kuwa jamii moja iliathiri nyingine ambayo inaichukua hadithi ya jamii hiyo na kuingiza kwenye utamaduni wake. Kwa njia hiyo ikaishia kuwa na sifa za utamaduni wa jamii mpya. Kuna visakale viwili tunavyoweza kuvitaja kueleza uhalisi huu.
Mfano wa kwanza ni mugani wa Fumo Liyongo. Mugani huu unapatikana katika jamii kadhaa za pwani ya Kenya kama Waswahili, Wapokomo, Wabajuni, n.k. inawezekana kuwa kupatikana huku ni matokeo ya ueneaji, hasa kwa kuwa hizi ni jamii zinazokaribiana kijiografia na zilizohusiana kihistoria. Mfano wa pili unahusu shujaa wa jamii ya Wahaya anayeitwa Magasha. Kisakale chake kinapatikana katika jamii kadhaa zilizoko karibu na ziwa Victoria.
Sababu za kuenea kwa Fasihi simulizi
Kuanzishwa kwa vikundi vya sanaa na muziki
Vikundi mbalimbali vya sanaa na muziki vilianzishwa, kazi yake ikiwa ni kuendeleza tanzu mbalimbali za Fasihi simulizi hapa nchini. Vikundi vya sanaa za maonesho, vikundi vya taarabu na muziki vinafanya kazi kubwa ya kueneza Fasihi simulizi hapa nchini.
Mwingiliano na Fasihi andishi
Kuenea kwa kazi ya Fasihi simulizi kwa asili ni kwa mdomo na masikio, yaani usimulizi. Hata hivyo, maendeleo ya watu yamefanya baadhi ya kazi za Fasihi simulizi zienee kwa maandishi. Maandishi ni jitihada ya kuhifadhi kazi ya Fasihi simulizi na kuifikisha mahali ili ikatambwe, iimbwe au isimuliwe. Hadithi mbalimbali kama vile Hekaya za Abunuwas na Hadithi Nyingine (1915), Hadithi za Essopo (1890), Fasihi ya Mtanzania: Hadithi (1977) (TUKI)n.k. zimehifadhiwa na kuenezwa kwa maandishi. Vilevile Fasihi andishi inatumia vipengele mbalimbali vya Fasihi simulizi katika uandishi wao na hivyo kuviendeleza. Vipengele hivyo ni matumizi ya semi mbalimbali, matumizi ya nyimbo, matumizi ya hadithi ndani ya hadithi, matumizi ya mianzo na miishilizo ya hadithi za Fasihi simulizi, matumizi matumizi ya majigambo, utani, n.k. Kwa sasa, methali, vitendawili, nahau vimewekwa katika maandishi kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye, na vipengele hivi vinaenezwa kwa njia ya maandishi.
Ufundishaji shuleni na vyuoni
Mfumo wa elimu nchini nao kwa kiasi kikubwa unasaidia kueneza Fasihi simulizi hapa nchini. Kwa sasa, Fasihi simulizi ni somo linalofundishwa kuanzia darasa la kwanza hadi ngazi ya chuo kikuu. Vilevile kuna shule na vyo mbalimbali hapa nchini vinavyofundisha baadhi ya tanzu mbalimbali za Fasihi simulizi kama vile sanaa za maonesho na muziki (chuo cha sanaa Bagamoyo, Butimba, Nyegezi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
Mabadiliko ya kiteknolojia
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwa sasa Fasihi simulizi inaenezwa na vyombo vya habari kama vile redio, televisheni na mitandao. Kwa mfano TBC kupitia vipindi vya “mama na mwana”, “watoto wetu” na “cheichei shangazi” vinasaidia sana kueneza Fasihi simulizi hapa nchini. Katika vipindi hivi, watoto husimuliana hadithi mbalimbali walizopata kusimuliwa, hutegeana vitendawili, humalizia methali na kuimba nyimbo. Televisheni nazo zinasaidia sana kueneza Fasihi simulizi hapa nchini, huonesha michezo mbalimbali ya kuigiza.
Kwa hiyo, mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia hayawezi kuiua Fasihi simulizi, bali Fasihi hii inaendelea kuzihudumia jamii zetu kulingana na mahitaji ya maendeleo ya wakati uliopo na ujao. Maendeleo ya kiteknolojia yanasaidia Fasihi simulizi kuenea na kufika mbali katika muda mfupi zaidi. Kanda za kunasia sauti, redio, televisheni, video na filamu ni vyombo vya kisasa ambavyo vinasaidia kuieneza Fasihi simulizi haraka zaidi kuliko njia ya masimulizi yam domo.
Mwingiliano na mataifa mengine
Hali hii imesaidia kuenea na kupanuka kwa fani za Fasihi simulizi, hasa kipengele cha muziki. Kutokana na mwingiliano huu tumepata muziki wa kizazi kipya (muziki wa kemo) pamoja na Rege. Vijana wa kizazi kipya wamechota miundo na mitindo ya muziki kutoka nje na kuendeleza muziki wao, ingawa maudhui bado wanajadili yaleyale yaliyojadiliwa na wanamuziki wa zamani.
Kwa ufupi, matumizi ya Fasihi simulizi katika sayansi na teknolojia yamesaidia sana kuenea kwa Fasihi simulizi; kwani Fasihi simulizi inapata hadhira kubwa kwa wakati mmoja, lakini hadhira hiyo haionani ana kwa ana na fanani wao kwa kutumia vyombo hivyo vya sayansi na teknolojia.