MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI)

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI)
#1
MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI)
USULI WA LUGHA YA KISWAHILI
Kabla ya kuingia kwa undani kuangalia lugha hii ya Kiswahili baada ya uhuru. Tunaweza kutalii dhana ya lugha na usuli wa lugha ya Kiswahili.
Dhana ya lugha
Wanaisimu wamekuwa wakitazama dhana ya lugha kwa mitazamo mbalimbali. Mitazamo hiyo huweza kutoa taswira ya maana ya lugha inavyo weza kuwa.
Lado (1964) Lugha ni chombo cha mawasilianoa baina ya binadamu katika jumuia Fulani.
Potter (1960) Lugha ni utaratibu wa alama za sauti zilizopangiliwa kutokana na mazoea au matamshi ya watu kwa njia ya sauti ambazo wanadamu wanapelekeana habari na wanasikilizana
TUKI (2004)  Lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili ya kuwasiliana.
Kutokana na mitazamo hiyo lugha ya weza kufasiliwa kuwa  ni sauti za nasibu za binadamu zinazobeba maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku.
LUGHA YA KISWAHILI
Kama zilivyo lugha nyingine za kitaifa na kimataifa, Lugha ya kiswahili ina tabia ya kusemwa, kuzungumzwa na kuandikwa kwa nia ya kukamilisha mawasiliano miongoni mwa wanajamii wa kiswahili. Lugha ya kiswahili ni lugha rasmi na Lugha ya Taifa kwa upande wa Tanzania ingawa kwa Watanzania ni lugha ya Pili. Lugha ya kiswahili ina watumiaji wanaokadiliwa  kuwa ni zaidi ya milioni 37 kwa Tanzania. Kiswahili kinafundishwa katika shule za msingi, sekondari na vyuoni. Hivi sasa kiswahili kimeteuliwa na kupewa baraka zote  kuwa  lugha ya Umoja wa Afrika na Kiswahilli kina hadhi ya nafasi ya sita kimataifa kikitanguliwa na na Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiarabu, na Kireno. Pia inakadiriwa kuwa Kiswahili kina wazungumzaji zaidi ya Milioni 160 Duniani. Kuna vituo mbalimbali vya redio na luninga vinayotangaza kwa kiswahili Ndani na nje ya bara la Afrika kama vile Sauti ya Amerika, BBC London, Sauti ya uajemi, KBC, na vingine vingi.Pia kuna vyuo vingi duniani vinavyofundisha lugha ya kiswahili mfano katika bara la Afrika, Asia, Ulaya, na Marekani. Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Minesota, Vyuo vikuu mbalimbali duniani mfano Ujerumani, Uingereza kwa kutaja baadhi.
HISTORIA YA LUGHA YA KISWAHILI
Kuna nadharia mbalimbali zinazoeleza historia ya lugha ya kiswahili, mfano wa nadharia hizo ni nadharia ya kihistoria, na nadharia ya kiisimu
Katika nadharia ya kihistoria inaeleza historia ya kiswahili kwa ujumla. Mfano historia ya Kilwa, ushahidi wa marco Polo na Ushairi wa Fumoliyongo unaosemekana ni ushairi wa Kiswahili ulioandikwa karne ya kumi na tatu BK. Nadharia ya kiisimu inaeleza taratibu na kanuni za lugha. Mfano upatanisho wa kisarufi, maumbo ya maneno (umoja na wingi), muundo wa tungo (kiima na kiarifu) mnyumbuliko wa maneno (kitenzi) na tabia ya vitenzi vya lugha ya kiswahili.. Hivyo lugha ya kiswahili inaweza kutazamwa kwa mtazamo ya kiisimu na kihistoria katika kupata historia ya lugha ya kiswahili kwa usahihi wake. Pamoja na kuwa wananadharia hawa hutofautiana, huweza kukubaliana kwa kutojua au kwa kujua kuwa kiswahili kimetokana na Kibantu.
            Kutokana na shahidi mbalimbali Mfano Shihabuddin Chiraghdin na Mathias Mnyapala (1988) wanaeleza kuwa asili ya lugha ya kiswahili ni kibantu ambacho kinazungumzwa zaidi katika upwa wa Afrika Mashariki mfano Pate, Unguja, Lamu, Comoro, Pemba, Mombasa, Kilwa, Tanga kwa kutaja baadhi. Wageni walikuja hususani Waarabu walikuta lugha hii ya kiswahili ikiwa inazungumzwa na wenyeji wao wa mwambao wa upwa wa Afrika mashariki kwa Lahaja tofauti tofauti kulingana na maeneo mfano kimakunduchi, kimtang`ata (Pangani na Tanga), Kingozi, (Pate na Kisumayu) Kitumbatu, Kimrima(Dar es salaamu na Tanga) Kimvita (Mombasa) Chimiini (Mogadishu/ Somalia) kwa kutaja baadhi. Lugha hizi zinafanana. kutokana na kufanana huko walipokuja Waarabu wakaziita lugha zote zilizokuwa zikizungumzwa upwa wa mashariki mwa Afrika ni Sahil. Kutoka na sababu kadha wa kadha na athari za matamshi ikatokea swahili na baadaye ikapatikana lugha ya kiswahili
Katika ujio wa waingereza ndipo shughuli za usanifishaji zilipoanza. Katika shughuli za usanifishaji shughuli mbalimbali zilifuatwa ikiwa ni pamoja na uteuzi wa lahaja moja miongoni mwa lahaja nyingi zilizokuwepo. Lahaja ya kiunguja ikateuliwa na kufanyiwa mchakato wa usanifishaji. Ndipo tukapata kiswahili sanifu. mfano wa maneno yaliyosanifiwa ni kama :-
Kiunguja                                 Kiswahili sanifu
Cai                                           Chai
Cumba                                     Chumba
Ceza                                        Cheza.  Kwa kutaja baadhi
KISWAHILI BAADA YA UHURU
Baada ya uhuru kuna harakati mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kukiendeleza na kukikuza kiswahili. Harakati hizo ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi 1962.
1964 kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na kuwa kitatumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa mfano katika elimu hususani elimu ya msingi.
Kundwa kwa Chombo cha usanifishaji ambacho kilikuwa na kazi ya kuhimiza maendeleo ya kiswahili, kutayaricha kamusi na vitabu mbalimbali vya sarufi na fasihi ya lugha ya kiswahili na kuandaa wataalamu watakaoshughulikia usanifishaji wa kiswahili
Pia baada ya uhuru kulianzishwa Taasisi mbalimbali zitakazoshughulikia lugha ya kiswahili. Mfano:- BAKITA, TUKI, TUMI, UKUTA, UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha Dar es salaamu.
Baada ya uhuru nchini Tanzania kiswahili kilienea kwa kasi kubwa sana. Kuna sababu mbalimbali ambazo zilichangia kukua na kuenea kwa kiswahili hapa nchini. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na kuteuliwa kwa kiswahili kuwa lugha ya Taifa, Kiswahili kitumike katika Elimu, mfano kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi. kuundwa kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na kuneza kiswahili, Kiswahili kuwa Lugha rasmi na lugha ya Taifa, shughuli mbalimbali za kidini, shughuli za kisiasa na kiutawala na shughuli za kiutamaduni na uchapishaji wa vitabu na majarida mbalimbali.
KISWAHILI KUWA LUGHA YA TAIFA
Baada ya uhuru mwaka 1962 kamati iliundwa ili kuangalia uwezekano wa kutumia kiswahili katika shughulizote rasmi, mfano bungeni na shughuli zote za kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha ya taifa 1964 ambapo katika shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa kutumia lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano yote hususani katika mawasiliano yote hasa katika shughuli za umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili kiliendelea kupanda hadhi zaidi wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani azimio hilo lilitungwa na kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
KUUNDWA KWA VYOMBO VYA UKUZAJI NA UENEZAJI WA KISWAHILI
Tanzania baada ya uhuru ilifanya jitihada za kuunda vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza kiswahili katika nyanja mbalimbali mfano wa vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA TUMI TUKI Taasisi ya Elimu,TAKILUKI na Chama cha Kiswahili Chuo Kikuu Dar es salaam.
KUTUMIKA KATIKA ELIMU
Kiswahili licha ya kutumika katika shughuli mbalimbali za kiserikali, kilipendekezwa kutumika katika shule za Msingi na kufundishwa katika elimu ya sekondari kama somo na katika vyuo vikuu wanatoa shahada mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia katika Elimu ya watu wazima ambao hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza masomo mbalimbali kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua kusoma, kuandika na kuzungumza lugha ya kiswahili fasaha. Kampeni hii ilikuwa kwa nchi nzima ambapo walijifunza elimu ya Afya, Siasa, Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
VYOMBO VYA HABARI
Tangu uhuru ulipopatikana kuna vyombo mbalimbali vya habari vilivyoanzishwa. Vyombo hivi hutumika kueneza kiswahili kwa kiasi kikubwa na hufikiwa na watu wengi licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi. Vyombo hivyo ni magazeti na majarida mbalimbali ambayo huandikwa kwa lugha ya kiswahili lakini kuna redio na runinga ambazo matangazo yake hutangazwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kukifanya kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.
BIASHARA
Shughuli za kibiashara nchini husaidia kuenea na kukua kwa kiswahili kutokana na kuwepo kwa makabila tofauti tofauti ambapo wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili hudumishwa na kutumika katika biashara hizo.
SHUGHULI ZA SIASA NA UTAWALA
Tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kiswahili kimetumika kama nyenzo muhimu kuwaunganisha wananchi. Shughuli nzima za kisiasa zimetumia lugha hii katika kujiimarisha; mfano wakati wa chama kimoja, Azimio la Arusha  na Mfumo wa vyama vingi Kiswahili kimetumika kama njia kuu ya mawasiliano. Pia katika utawala chama kinachotawala kimekuwa na harakati za kukiendeleza kiswahilli katika nyanja zote. Ambapo kiswahili kimekuwa kikitumika katika shughuli zote za kiutawala. Hivyo shughuli za kisiasa na kiutawala zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza, kukieneza na kukiendeleza kiswahili.
UANDISHI NA UCHAPISHAJI WA VITABU
Kuibuka kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili vya sarufi na fasihi ambavyo vilichambua kwa kina mambo mabalimbali yahusuyo lugha ya kiswahili na utamaduni wake, mfano :- F Nkwera, Shabani Robart, Mathias Mnyapala na  Shaffi Adam Shaffi. Waandishi wengine chipukizi walijitokeza na wanaendelea kujitokeza katika tasnia hii ya uandishi wa vitabu.
SHUGHULI ZA KIUTAMADUNI

Shughuli za kiutamaduni zimechangia kueneza kukuza na kuendeleza lugha ya kiswahili. Shughuli hizo ni pamoja na harusi, misiba, matanga na sherehe mbalimbali za kijamii ambazo zimesaidia kukiendeleza kiswahili kwa kuwa huwakutanisha watu tofautitofauti katika shughuli hizo, ambapo huwalazimu kutumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano na kufanya kiswahili kuendelea. Pia katika Sherehe mbalimbali vikundi vya sanaa na muziki vinavyotumia lugha ya kiswahili kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa nyimbo zao kwa ajili ya kukieneza kiswahili Mfano;-(    ) Pia katika sherehe mbalimbali za kiserikali na kisiasa hususani vyama mbalimbali vya kisiasa mfano bendi ya TOT  inayoongozwa na kepteni Komba.

MAFANIKIO YA KISWAHILI WAKATI WA UHURU MPAKA SASA
Kiswahili kimeweza kujizolea na kinendelea kujizolea sifa kemkem ndani ya  Miaka  50 ya uhuru wa nchi yetu hatuna budi kukitolea mifano ili tuone kwa namna moja au nyingine jinsi kilivyofanikisha kuwaunganisha Watanzania katika mapambano dhidi ya utawala wa kikoloni na kusababisha matokeo hasi kwao ambapo kubwa zaidi ni kujipatia uhuru. Kwa maana nyingine, Kiswahili kiadhimishwe kama lugha ya ukombozi wa nchi yetu wa mwaka  1961.
            Mpaka sasa kiswahili kimefanikiwa kuwaunganisha watanzania wote na kwa maneno yake yaliyojaa faraja na matumaini, kimeweza kudumisha amani ya Tanzania (nchi yetu) kwa miaka hamsini sasa. Bado kinaendelea kuwaweka pamoja watanzania na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Pia kimetoa mchango mkubwa katika kuipa sifa kubwa nchi yetu ya Tanzania na kuwa mfano wa kuigwa duniani kote. Tanzania imepewa sifa ya kisiwa cha amani kutokana na amani ya muda mrefu iliyopo nchini ambayo inasimamiwa vilivyo na lugha yetu ya kiswahili.
Katika nyanja ya fasihi, Kiswahili kimeweza kuelezea utamaduni wa nchi nyingine kama vile Kongo Afrika kusini, Uganda n.k . Kwa kutumia muziki kwani sasa kuna wanamziki wengi wanaotoka katika nchi hizo wanaotambulisha utamaduni wao kwa lugha ya kiswahili. Baadhi yao ni Mbili Abel Kutoka kongo, Ivon Chakachaka kutoka Afrika Kusini, Marehemu Miriam Maakeba Kutoka Afrika Kusini pamoja na Jose Kamilion kutoka nchini Uganda. Pia kuna baadhi ya wanamziki kutoka Korea waliweza kuonesha hisia zao kwa kutumia lugha ya kiswahili katika uimbaji wao.
Lugha ya kiswahili ina utajiri wa maneno (msamiati) ambao katika lugha nyingi za kimataifa hazina msamiati huo kama Kiingereza hakina msamiati wa aina hiyo, Mfano wa misamiati hiyo ni pamoja na Shangazi, Baba mdogo, Baba mkubwa, Ugali nk. Kutokana na tafiti zilizofanywa kiswahil kinaonekana kuwa ndiyo lugha pekee kwa sasa ambayo inakubarika kwa kasi zaidi duniani kote kuliko lugha nyingine zinazokua. Hii ni kutokana na ongezeko la watu wanaohitaji kujifunza na kuzungumza kiswahili duniani kote.
Pia kiswahili kimeweza kufikia kiwango cha juu sana cha kusikika kwani sasa kinasikika dunia nzima. Hii ni kutokana na mashirika makubwa ya habari yanayorusha matangazo kwa kutumia lugha ya kiswahili. Mfano BBC, Sauti ya Ujerumani. (Deutsche Welle ) Sauti ya Amerika, Pamoja na shirika la utangazaji la Tanzania TBC kupitia kituo cha runinga kinachorusha matangazo yake kupitia kituo cha DSTV kilichopo nchini Uingereza, kinachorusha matangazo kwa njia ya setilaiti.
Mafanikio mengine ya kiswahili ni kufanikiwa katika sayansi mbalimbali katika jamii ambapo kiswahili kimetumika kuandika vitabu mbalimbali kwa kutungwa au kufasiriwa na wataalamu mbalimbali. mfano  kitabu kinachohusu afya ya binadamu kilichotafsiriwa ambacho hata sasa hutumika katika kufundishia wataalamu wa afya katika vyuo vikuu. kitabu hiki kimefasiliwa na Daktari(….)
Pia Watanzania wanaoishi katika nchi za dunia ya kwanza  wameonyesha nia ya dhati  ya kuwasaidia vijana wakitanzania  kutambua thamani kubwa   ya lugha yao ya Kiswahili. Kwa mfano, Freddy Macha, Mtanzania aishiye Uingereza  kwa kushirikiana na watanzania wengine waliopo barani Ulaya. Wamedhamiria kwa dhati kulifanikisha hilo kwa vitendo, ambapo hivi karibuni wanatarajia kufanya semina na vijana wa Tanzania hapahapa nyumbani. Kwa kushirikiana na Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania (MMVT) na vijana wengine na kujadili mada mbalimbali ikiwamo mada ya Kiswahili inayohusu umuhimu wa kujua lugha mbalimbali kikiwamo Kiswahili na namna ya kukitumia kama nyenzo ya maendeleo na biashara.
Nao Watanzania waliopo Denmark  wamepongeza juhudi zinazofanywa na wadau wa Kiswahili nyumbani  (Tanzania) kwa namna moja au nyingine katika kukikuza na kukieneza Kiswahili na wanakubaliana na misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume  katika kuitumia lugha ya Kiswahili kama kitambulisho cha taifa, ambapo Kiswahili kinatumika kama lugha ya taifa.
Pia wanawapongeza viongozi waliofuata kwa kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili   katika nyanja ya muhimu za elimu, uchumi na utamaduni wa taifa letu la Tanzania
            Pia, watanzania na wadau wote wa lugha ya Kiswahili wanampongeza  Rais mstaafu wa awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Rais wa awamu ya tatu Mh.Benjamini Willium Mkapa wamekuwa Viongozi hodari wa kukisimamia na kukieneza Kiswahili. Hawakuwa nyuma kumpongeza  Raisi  Kikwete kwa  kuhakikisha Watanzania wanafahamu umuhimu wa lugha ya kiswahili  nchini na duniani kote yeye alitia msisitizo kwa kuhutubia mkutano wa Umoja wa Afrika kwa Kiswahili .
Kituo cha runinga cha TBC 1 nacho kwa nafasi na mchango wake katika lugha, kimekuwa kikirusha kipindi cha Lulu za Kiswahili pamoja na kipindi cha Ulimwengu wa Kiswahili na kujadili masuala ya lugha ya  Kiswahili nchini na nje ya nchi. Pia vituo vingine vya runinga ni kama star TV na ITV Ambayo havipo nyuma katika kukieneza na kutangaza Kiswahili.
            Vilevile, kuingizwa Kiswahili katika mtandao ni hatua kubwa inayoonyesha kwamba, Kiswahili kinaendana na hali ya utandawazi ambapo watu wamekuwa wakipata taarifa ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Na kufanya watu wengi hususani wanaojua Kiswahili kusoma makala mbalimbali katika matandao na kupata habari kwa kina.
            Kuwapo kwa kamusi za lugha katika tovuti ambazo huwezesha watu kujifunza lugha kupitia njia ya mtandao.
Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Skuli ya Sanaa na Lugha  pamoja na kuongezeka kwa vyuo vinavyofundisha shahada ya lugha ya  Kiswahili nchini kama vile vyuo vikuu vya SAUT, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar (Suza), Tumaini na pia Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) hatua hiyo imesababisha kuwa na wasomi wengi wenye taaluma ya Kiswahili, licha ya  changamoto ya wanafunzi hao wa Kiswahili kuwa na upungufu wa maeneo ya kufanya  mafunzo ya vitendo, ni changamoto inayopaswa kuangaliwa na kufanyiwa kazi.
Kuongezeka kwa istilahi za lugha ya Kiswahili ni jambo linaloashiria kupanuka kwa matumizi ya Kiswahili na ndiyo maana kumekuwapo na machapisho ya kamusi mpya mara kwa mara ili kukidhi mahitaji na matumizi ya lugha ya kila siku katika mawasiliano . Istilahi hizo zinaongezeka kutokana na sababu mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi lakini pia maendeleo ya sayansi na teknolojia Mfano wa istilahi hizo ni kamazifuatazo;-
Chakachua, ngangali, ng`atuka, ngamizi.
            Vilevile, kuingia katika mfumo wa mawasiliano kwa njia ya setelaiti (digitali) kumehamasisha zaidi matumizi ya Kiswahili hasa katika tasnia ya utangazaji hususani redio na runinga, mfano TBC na ATN. Hivyo hufanya mawasiliano kuwa rahisi miongoni mwa wasikilizaji wao.
Mafanikio menginie ni kuongezeka kwa watu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ulaya, Amerika, Asia na kwingineko kuja Tanzania kujifunza Kiswahili. Pia kufanya tafiti kuhusiana na lugha ya Kiswahili
Kuongezeka kwa nchi nyingi dunia zinazotumia lugha Kiswahili katika mawasiliano na kuhitaji wataalamu wa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya watu wao kujifunza Kiswahili mfano Botswana, Libya, Malawi na Afrika Kusini.
Kiswahili kimekuwa kama sehemu ya ajira katika taasisi na mashirika mbalimbali ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali. Mfano katika tafsiri na ukalimani, pia katika kutoa Elimu Kiswahili kinatumika. Hii inawafanya watumiaji wa lugha hii kuongezeka kwa kasi kubwa.
Kuwepo kwa machapisho mengi ya Kiswahili na kuwepo kwa waandishi wengi wanaoandika kazi mbalimbali za Kiswahili mfano katika fasihi na sarufi ya Kiswahili.
Mfano wa waandishi maarufu walio kama chachu ya maendeleo ya Kiswahili ni              F. Kezilahabi, F. Nkwera, J. Madumulla, I. Huseni, T.Sengo, Kingo, Chachage, Penina Mlama, S. Shaffi na Asha Kunemah. Ambao wametoa changamoto kubwa katika kukikuza na kukiensza Kiswahili. Pia wameonesha mafanikio makubwa katika kazi zao.
Kiswahili kimekuwa maarufu sana na kukubarika katika nchi za Afrika Mashariki. Mfano nchini Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya, mathalani nchini Kenya Kiswahili kimekuwa lugha ya Taifa. Kuandikwa kwa katiba ya Kenya kwa lugha ya Kiswahili na kuwa lugha ya Taifa katika nchi za Afrika Mashariki. Hivyo kukifanya kiswahili kuwa na hadhi kubwa ndani na nje ya bara la Afrika
KISWAHILI NA UTANDAWAZI
Utandawazi ni dhana pana ambayo imeenea na kugusa nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Kiswahili ikiwa ni sehemu ya utamaduni kimeguswa na kuathiriwa na utandawazi.
Dhana ya utandawazi inaweza kuangaliwa kwa mitazamo mbalimbali. Miongoni mwa dhana hizo ni aina ya tabaka jipya la kibepari lililojitutumua kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi, kisiasa, na kiutamaduni. Kujiinua huku hudhihirika katika taaluma na  vyombo vya habari mfano matangazo  na kufanya kuwa dhana inayoenea kwa kasi na kugusa nyanja mbalimbali duniani. Hivyo utandawazi unaweza kuifanya dunia kuwa kama  kijiji . Utandawazi una muonekano wa mradi wa kiitikadi na ajenda ya kujenga mahusiano ya kibinadamu na ambayo ni ngumu kueleweka kwa wanazuoni mbalimbali na kuonekana kuwa ni dhana mpya.
UTANDAWAZI KATIKA UTAMADUNI
Utandawazi huendana na mambo mbalimbali kama vile Lugha, Sanaa, Mavazi, na namna ya kula na hivyo jamii kuathirika kwa sehemu kubwa. Jamii huweza kuathirika kwa kupoteza amali za jamii kwa kupokea mambo ya jamii nyingine hususani mambo ya kimagharibi. Hivyo kiswahili kama sehemu ya utamaduni wa Taifa letu imeathirwa kwa sehemu kubwa.
KISWAHILI NA UTANDAWAZI.
Utandawazi ulianza kuingia katika lugha ya kiswahili wakati wa utawala wa kikoloni. Ambao ulisababisha mabadiliko mbalimbali katika lugha ya kiswahili. mfano Dini, biashara, utawala na elimu vilisaidia kukuza na kueneza lugha ya kiswahili. Utawala wa kikoloni uliambatana na kuanzishwa kwa vyombo vya habari kama vile magazeti, redio. Runinga, tovuti na simu ambapo kuliimarisha utandawazi na kiswahili kupata matumizi makubwa.
Kutokana na utandawazi kumekuwa na ushindani mkubwa katika mambo mengi ikiwemo Lugha. Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha zilizo kwenye ushindani huo. Lugha hii inakubalika na watu wengi wanaoitumia katika mawasiliano, na kukifanya kiswahili kuingia katika utandawazi kwa lengo la kuiunganisha jamii.
Katika utandawazi ajira inaongezeka, Mathalani mtu anayetumia lugha nyingine nje ya kiswahili anakuja nchini  kwa lengo la uwekezaji hulazimika kujifunza kiswahili ili kudumisha mahusiano na wenyeji wake. Hivyo huongeza walimu wa lugha kwa ajili ya kufundisha lugha ya kiswahili pia huweza kueneza lugha kwa njia ya ukalimani.
Watanzania wengi huchukuliwa na nchi mbalimbali kwa lengo la kufundisha lugha ya kiswahili katika nchi zao.
Utandawazi huweza kusaidia kuongeza msamiati wa lugha. Kiswahili ni miongoni mwa lugha inayopokea maneno kutokana na matumizi yake yanayotokana na utandawazi hususani katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, siasa, utamaduni na uchumi. Mfano katika maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna istilahi nyingi za kimtandao.
Utandawazi umeweza kuongeza idadi ya watumiaji wa lugha ya kiswahili. Ambapo ikadiliwa kuwa katika nchi za maziwa makuu idadi ya watumiaji wa lugha kiswahili ni zaidi ya milioni 60.
MADHARA YA UTANDAWAZI
Kila kitu kina pande mbili, kadharika utandawazi nao una pande mbili faida na hasara. Baada ya kuangalia upande mmoja wa shilingi uzuri wa utandawazi katika kiswahili. Sasa tuangalie madhara ya utandawazi katika lugha ya kiswahili
Mosi kutokana na utandawazi kumekuwa na kudharau lugha ya kiswahili. ambapo lugha hii ya kiswahili inaonekana kuwa ni lugha ya watu wa tabaka la wasionacho. Pia Watu huiona lugha ya kiswahili kuwa ni lugha ya watu wasiojua kitu chochote duniani. Kiswahili kinaonekana kuwa si lugha ya sayansi na teknolojia na kwamba haiwezi kutumika katika shughuli zote za kisayansi  hususani katika taaluma ya ufundi.
CHANGAMOTO  KATIKA LUGHA YA KISWAHILI
Pamoja na hadhi na umaarufu wa kiswahili, bado lugha hii inakumbana na matatizo makubwa ya dhana na matumizi ya lugha ya kiswahili.
Katika dhana ya kiswahili bado kuna baadhi ya watu wanaonasibisha kiswahili na dini ya kiislam hili limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa watumiaji wa lugha hii.
Pia upinzani mkubwa kutoka katika lugha ambazo zimekwisha jitanua katika dunia Mfano:- Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Watumiaji au watu wenye asili na lugha hizo wanakipiga vita kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitazimeza lugha zao.
Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha za kigeni kwamba ndio pekee zinazofaa kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hivyo kiswahili kuonekana kuwa hakifai kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kasumba mbaya na mtazamo hasi wa Watanzania katika lugha ya Kiswahili ambao unawafanya watanzania kukitukuza zaidi kiingereza na kutojua kuwa kiingereza ni sawa na lugha nyingine tu.
Kucheleweshwa kwa maamuzi ya sera ya kukipa hadhi kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika nyanja zote za elimu, na kiingereza kuwa somo tu. Hivyo inarudisha nyuma maendeleo ya kiswahili.
Watanzania kuwa nyuma katika kufanya tafiti mbalimbali juu ya lugha ya kiswahili ili kuona ni jinsi gani tunaweza kufunguka kiakili na kufahamu umuhimu wa kuwa na lugha ya kiswahili
Uchumi mdogo wa nchi yetu unakwamisha kwa sehemu kubwa maendeleo ya haraka ya lugha ya kiswahili duniani. Kwa kuwa nchi inashindwa kuzalisha wataalamu wengi wa lugha hii, pia inashindwa kufasiri maandiko kutoka lugha nyingine kuwa katika lugha ya kiswahili kwa sababu ni ghari mno.
Watanzania wanakosa moyo wa kuthamini na kujali tamaduni zao ambapo kiswahili ni lugha inayotangaza utamaduni wao lakini wao wanathamini sana utamaduni wa kimagharibi. Kwa hakika hii ni changamoto kubwa ambayo inakikumba kiswahili katika harakati zake za kujitanua duniani kote.
Pia kuna dhana kuwa Kiswahil ni lugha ya watu duni kitaaluma mathalani watu walioishia darasa la saba. Hivyo hufanya watu kutaka kujifunza Kiingereza. Hii ni dhana ya watu potofu kabisa ambayo inajitokeza kwa watu ambao ni wasomi kabisa.
Kwa upande wa matumizi ya lugha ya Kiswahili, kumekuwa na matatizo makubwa ya kutumiwa isivyosahihi na matumizi yasiyofasaha katika nyanja zake za kimatamshi, kimaandishi na kimaana.  Matatizo hayo ndiyo yanayopelekea kutokuwa na kiswahili sahihi na fasaha. Jambo la kusikitisha na kushtua zaidi ni kuwa kwa muda mrefu, kumebaini na kuwa na kiswahili sanifu nchini lakini kiswahili hiki kinazungumzwa na kuandikwa kimakosa mno. Makosa haya hutendwa na taasisi mbalimbali zikiongozwa na vyombo vya mawasiliano. Mfano katika magazeti waandishi wanatumia lugha inayokiuka misingi na kanuni za kiswahili sanifu tunachokielewa au wanachofundishwa wanafunzi.
MAKOSA YANAYOFANYWA NA UMMA WA WATANZANIA
Makala hii inadokeza na kubainisha makosa ya matumizi ya kiswahili yanayofanywa na umma wa Watanzania, Vyombo vya mawasiliano na Walimu katika shule na vyuo. Pia inaeleza sababu za msingi na athari na matumizi yasiyosahihi  kwa jamii ya watumiaji wa Kiswahili hususani Watanzania wote. Baadaye kutakuwa na mapendekezo ya nini kifanyike ili kupunguza au kuondoa kabisa matatizo hayo ya makosa ya matumizi yasiyosahihi ya lugha hii kwa vyombo vyote vya umma na watu binafsi watumiaji wa kiswahili.
Kabla ya kuangalia makosa ya matumizi yasiyosahihi ya Kiswahili sanifu ni afadhali kwanza kudokeza maana ya umma wa Watanzania, maana ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya Kiswahili na maana ya mawasiliano sahihi na fasaha.
MAANA YA UMMA WA WATANZANIA
Umma wa Watanzania kwa muktadha wa makala hii ni watu wengi wenye kutumia stadi ya kusema na kuandika kwa lugha ya kiswahili. Kwa upande wa kusema au kuzungumza makosa hayo hutokea katika shughuli zisizo rasmi na zile zisizorasmi katika mazingira tofautitofauti ya mawasiliano ya kila siku, kama vile mitaani, nyumbani, ofisini, shuleni na kazini. Kwa upande wa uandishi makosa hayo hutokea katika vitabu, magazeti, majarida na vipeperushi vya matangazo mbalimbali.
MAANA YA MAKOSA YA MATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU
Maana ya makosa ya matumizi  ya kiswahili sanifu kwa upana wake ni yale matumizi ya kiswahili ama ya kuzungumzwa au kuandikwa ambayo yanakiuka taratibu na makubaliano ya kimawasiliano ya kisarufi ambayo ni sahihi na fasaha na kusababisha karaha au upotofu wa mawasiliano rasmi kwa wazawa na wajuzi wa kiswahili fasaha.
MAAN A YA MAWASILIANO SAHIHI NA FASAHA
Mawasiliano sahihi na fasaha ni yale mawasiliano ya kuitumia lugha ya yenye kufuata taratibu za maneno, miundo ya kisarufi pamoja na maana na kuweza kukubalika na wazawa na wajuzi wa lugha hiyo. Ikiwa inasemwa au kimaandishi, bila kuwa na uvulivuli, ukakasi au chukivu kwa wasikilizaji au wasomaji. Kigezo kikubwa cha lugha sahihi na fasaha ni ile lugha ya mazungumzo au maandishi ambayo ikisemwa au ikiandikwa haitagunwa na wazawa au wajuzi mahiri wa lugha ile. Mfano wa lugha ya Kiswahili isiyosahihi na isiyofasaha ni kama mtu akisema au kuandika hivi
 “Tuende wote pale tulikuwa juzi”
Sentensi hii ina makosa ya taratibu za kisarufi, katika upatanisho wa vipashio na muundo unaokubalika kwa wajuzi wa lugha hii na kuleta ukakasi na uvurivuri na  kusababisha kukosa ufasaha. Sentensi hii ilitakiwa kusemwa au kuandikwa hivi “Twende sote pale tulipokuwapo jana”
Hivyo ni uandishi na usemaji wa lugha ya kiswhili ni dhahiri kuwa huwa na taratibu wa kisarufi, muundo na upatanishi wa vipashio unafuatwa na unapelekea sentensi hiyo kuwa na mawasiliano sahihi na fasaha mbele ya wajuziz wa lugha
MAKOSA YA KISWAHILI YANAYOFANYWA NA UMMA WA WATANZANIA
Makosa hayo ya kimatumizi yanabainika kutawala katika maeneo ya matamshi, maumbo, miundo na maana; ama kimazungumzo au kimaandishi. Makosa makuu ya mawasiliano ya umma yanabainika katika nyanja zifuatazoa;-
1                    Matamshi na maandishi mfano thamani badala ya zamani, arubaini badala ya arobaini, samanini badala ya themanini. sambi badala ya Dhambi na sahabu badala ya dhahabu. Wngine pia hushindwa kutofautisha kati ya kula na kura hii inatokana na watu hawa kuwa wamawameathiliwa na lugha mama. Hivyo hata wakati wa kujifunza au kufunza lugha hufunza kwa makosa hayo.
2                    Maumbo ya maneno  ambayo kwa sehemu kubwa huendana na maana za maneno.
mfano:- Zoezi (kazi), zoezi (jaribio)
3                    Miundo ya sentensi, miundo mingi ya sentensi zinazotolewa huwa si sahihi na huleta ukengeushi mkubwa kwa wajuzi wa lugha mfano:- hadi hapo nawaageni, nachukua nafasi hii, kwa niaba yangu. Pia katoka muundo wa sentensi za Kiswahili huanza na nomino na kufuatwa na aina nyingine za maneno Mfano:- Mtoto mzuri anacheza jikoni
  N        V          T           E
                  Tena katika muundo kuna makosa ya upatanishi wa kisarufi ambapo watu wanapotosha au kuchanganya sarufi ya lugha ya Kiswahili.
Mfano:- sisi wote tunapenda nyama  badala ya kusema  Sisi sote tunapenda nyama.
4                    Machapisho na majarida mbalimbali ambayo kwa sehemu kubwa hutumia  lugha inayopotosha jamii, mfano:- pia vyombo mbalimbali vya habari kama Televisheni, Redio, Runinga. ambayo hutumia lugha hii visivyo na pengine hupotosha kabisa umma au jamii. mfano wa matumizi ya neno Chakachua ambapo mtu akakifanya vibaya wanasema amechakachua.
5                    Pia katika elimu kumekuwa na mkanganyiko mkubwa ambao unatoka na sera zisizo na msingi. Pia matatizo ya kimtaala ambayo huleta changamoto kubwa inayotokana na muhutasari wa elimu na mitihani inayotolewa. Katika muhutasari huonesha wanafunzi kujifunza kwa mlengo wa kimawasiliano unaopigia chapuo wanafunzi kupewa stadi za kuwasiliana zaidi huku ikilenga katika masuala mengine hususani upade wa sarufi.
6                    Pia kuna makosa ya kimsamiati ambapo watu huchanganya sana hususani wakati wa kuzungumza  hutumia msaniati usiolingana na maana iliyokusudiwa, pengine hutokana na kushindwa kutofautisha maneno hayo. Mfano: nenepa na nona, wasilisha na wakilisha, ajali na ajili, na mazingira na mazingara. Mfano:- Siku hizi Rachel amenona, badala ya Siku hizi Rachel amenenepa.
Haya ni baadhi ya makosa ya matumizi yasiyokuwa sahihi yanayofanywa na umma wa watanzania. Uzoefu unaonesha kuwa kati ya umma wa watanzania watu wa vyombo vya mawasiliano na habari vya umma huchukua nafasi kubwa ya kufanya makosa ya Kiswahili sanifu watu hao ni waandishi wa habari, wahariri wa magazeti na watangazaji wa redio runinga. kwa kubainisha vyombo hivi vichache  ni kama vifuatavyo: Magazeti Mtannzania, Mwananchi , uwazi, Nipashe, Uhuru Mzalendo Mwanahalisi na habari leo. Kwa upande wa Redia ni TBC Taifa, Radio one, Sauti ya Zanzibar, Redio uhuru nk Pia runinga ni TBC, ITV, Star TV, TVZ, ATA, EATV na DTV. Kinacho jitokeza hapa ni kuwa makosa yanayofanywa na watu hawa husambaa sana na kuchukua asilimia kubwa takribani pande zote za Tanzania na duniani kote tena kwa haraka zaidi. Matarajio ya wengi ni kuwa umma wa watanzania kuwa na uchungu wa lugha hii adhimu ya Kiswahili na kuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kuthibiti uenezi wa Kiswahili sahihi na fasaha. lakini hali haiku hivyo, bali iko kinyume na matarajio
TAATHIRA ZA UMMA WA WATANZANIA KUTANYA MAKOSA KATIKA KISWAHILI SANIFU
Kuna taathira nyingi ambazo zinasababisha mawasiliano ya umma wa watanzania kuwa na matumizi yasiyosahihi kama yalivyoonekana hapo awali. Taathira za msingi hasa ni kama zifuatazo
TAATHIRAYA KUTOELEWA LUGHA YA KISWAHILI NA UTAMADUNI WAKE
Kiswahili ikiwa ni lugha kamili yaa mawasiliano ina kanuni zake za kisarufi na kiutamaduni. Kwa mfano kanuni za kisarufi katika kitenzi ambacho husimama kuwa sentensi basi lazima kiwe na kiambishi cha utendaji, kiambishi cha wakati na shina la kitendo chenyewe. Yaani kama kitenzi atakuja. Kwa upande wa utamaduni mbele ya wenyewe waswahili mtu hawezi kusema au kuandika kwa mfano:- Kama nilivyosema hapo mbeleni. kwani nene mbeleni ni matusi kwa mswahili mzawa.
Kinachoonekana kwa watanzania ni kutokuwa waledi na mahiri wa sarufi na utamaduni wa lugha ya Kiswahili. Kwa watu waliowageni wa lugha hii ya Kiswahili hususani katika sarufi ya Kiswahili wanafanya makosa makubwa na kuleta matatizo makubwa. Kwakuwa katika mawasiliano, kwao kufanya makosa sio tatizo ikiwa mazungumzo au maandishi yao yanaeleweka. Mhina anasema Kiswahili ni lugha ya watu wa unguja kwa hiyo tunapata Kiswahili safikutoka kwa watu wa jamii ya waunguja.
TAATHIRA YA KUKIDHARAU KISWAHILI KUWA HAKINA MWENYEWE
Taathira nyingine inayopelekea Kiswahili kuzungumzwana kuandikwa kimakosa na vyombo vya habari ambayo inasikitisha zaidi ni kuwa kila mmoja ana uhuru wa kuzungumza kukizungumza na kukiandika anavyoona au atakavyo. Hali hii ndiyo inayofanya wengine kusema kuwa Kiswahili hakina mwenyewe. hii ni dharau kubwa na kejeli ya hali ya juu kwa wazawa na wajuzi wa lugha hususani kwa wanazuoni.
Hii inadhihilisha ule usemi usemao anayekutukana hakuchagulii tusi, umechukua mkondo wake. Kwani haijapata kusikika wa haitarajiwi kusikika kuwa Kingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kihaya, Kisukuma, Kibena na Kihehe kuwa lugha hizi hazina mwenyewe. Kwa hakika lugha kama haina mwenyewe basi haipo. Ikiwa lugha ya mazungumzo au maandishi lazima lugha hiyo iwe na wenyewe ambao ni binadamu tu. Wala si lugha ya wanyama, wala si lugha ya miti wala si lugha ya majabali na wala si lugha ya anga ombwe. Hivyo ni muhimu kuunga mkono mawazo ya  Mnyapala na Shiragddin wanaposema “… kiswahi kama zilivyo lugha nyingine hakina budi kukua na …”  mawazo haya ni ya kweli kwa yameandikwa na na wageni wa lugha nautamaduni wa Kiswahili ndio walioanza na matumizi ya yasiyo sahihi na yasiyofasaha. kinachobainika katika maandishi hayo ni kuwa wao ni wataalamu zaidi kuliko wale waswahili wenyewe katika kuandika vitabu vyao. ukweli usiopingika kuwa mawazo ya mazungumzo au maandishi yenye makosa yaliyotendeka na yanayoendelea kutendeka hayakubalikia na hayatakubalika kamwe na baadhi ya waswahili , kwani Kiswahili kina wenyewe. Amabao hawaoni kuwa lugha kama kifaransa au kiingereza ni bora au ni tajiri kuliko Kiswahili. Pia hawa hawaha wala hawatakuwa na dhana kuwa sarufi au lughawiya ya Kiswahili lazima ifuate lughawiya ya lughaya kiingereza au lugha nyingine. Msimamo huu pia unaoneshwa tena na Mnyapala na Shiraghdin  “kulazimisha lugha ya Kiswahili katika sarufi ya kiingereza ni kama kupika mchanyato wa ndizi mbivu… matokeo yake utakuwa si mchanyato bali ni bokoboko la ndizi. Kwa sababu sarufi ya kizungu ni kitu mbali na sarufi  ambayo isingefaa katika Kiswahili kwa namana nyingine.”
TAATHIRA YA WIGO NA KUTOJIAMINI KWA BAADHI YA WANAHABARI
Baadhi ya wanahabari hususani watangazaji wa redio runinga waandishi na wahariri wana mtindo wa kuiga kwa kutojiamini. hali hii hujitokeza pale wanahabari wanapowaiga ama wanahabari wenzao ambao nao wanafanya makosa katika kazi zao. Wanahabari hao huwaiga wanasiasa au viongozi wa nchi japokuwa kile kilichosemwa au kuandikwa ni makosa kabisa hapo ndipo utakapowasikia wakisema:- Chakachua  kusimikwa kwa watu kumi na watano, katoto kale kanaingia sasa. nk. Wanahabari hutumia maneno hayo kwa kuiga bila kujiani. ikitokea nafasi ya kuuliza mbona unatumia maneno hayo? utasikia jawabu atakalo kupa kuwa “mbona watu wengi wanalitumia neon hilo na limekwishaenea. Hoja ya msingi hapa si suala la neon kutumiwa na watu wengi au kuenea, bali ni kuwa neno hilo matumizi yasiyokuwa sahihi na halikubaki katika jamii ya wanazuoni wa Kiswahili.
TAATHIRA YA LUGHA ZA VIJANA KUKIINGILIA KISWAHILI SANIFU
Kiswahili mara nyingine hupata Taathira ya lugha za vijana na baadhi ya watu kuanza kuhusudu na kuyatumia maneno ambayo hayana asili ya Kiswahili na utamaduni wake. mfano Kama neno mambo? kwa maana ya uhali gain? na jawabu lake ni poa yaani sijambo au haliyangu ni njema. Pia kuna neno jingine linalouliza Vipi? na jawabu lake ni Fresho au hamna noma. lakini kuna maneno mengine kama vile Matingo, kughairisha, magharibi na kujiongeza. Kwa hakika lugha hizi si sahihi wala si fasaha kwa kutumiwa na watu wote katika shughuli zilizo rasmi. Lakini la kushangaza ni kuwa utawasikia baadhi ya viongozi wanahabari, wazee na walimu ambao tunawategemea wawemstari wa mbele kukilinda na kukienzi Kiswahili wanatumia lugha hizi zinazotumiwa na vijana. Lakini ilivyo lugha hizi kwa vijana zina sehemu zake maalumu kwa vijana wenyewe tu si kwa watu wenye kustahiwa kama hao waliotajwa hapo juu.
TAATHIRA YA KUCHANGANYA KISWAHILI NA KIINGEREZA (ATHARI ZA UMAGHARIBI, WINGI LUGHA)
Kuchanganya mazungumzo ya lugha ya Kiswahili na lugha ya kiingereza ni suala lililotawala mno katika mawasiliano ya umma na katika vyombo vya habari. Mara nyingi utawasikia watu wakichanganya Kiswahili na kiingereza. Hii ni kutaka kuhakikisha kuwa wanakifahamu kiingereza na kujitukuza mbele yaw engine. Mfano:-
            Ok ndugu wasikilizaji sasa tunaendelea na mchezo wa drama.
well nimekusikia ndugu mtazamaji kwa mchango wako lakini kwa upande mwingine perhaps watu wana mtazamo mwingine juu ya issue hiyo.
Uchanganyaji wa Kiswahili na kiingereza kama huo umewatawala watu wengi wakati wanapozungumza Kiswahili na kukichanganya na lugha hii ya kigeni. wakiti mwingine baadhi ya watu hufikia hatua ya kusema sijui nitumie neno gain hapa la Kiswahili ili ajihalalishie kuchanganya Kiswahili na kiingereza.
TAATHIRA YA KUTOLINGANA KWA TAALUMA YA FONOLOJIA NA OTHOGRAFIA
Mara nyingi wasomi wa lughawia za kiingereza wanatengua baadhi ya matamshi na maandishi ya Kiswahili kwa kuathiliwa na lugha ya iingereza ambacho nacho kimeathiliwa na taaluma ya kifaransa. hali hii husababisha matamshi ya sikuwa sahihi na yasiyokuwa fasaha katika Kiswahili ambacho kina utaratibu wa lugha za kiafrika kuandikwa kama kinavyotamkwa. mfano maneno kama;- themanini, tofauti, arobaini na dhoruba. Maneno kama haya hutamkwa vingine na kuandikwa vingine. ukihoji utajibiwa kuwa ndivyo yalivyokubalika kuandikwa kisanifu na pia baadhi ya maneno huandikwa kinyume na yanavyotamkwa yaani hapa ni kuiga kiingereza lakini hakuna  hoja kwani tukiyaandika kama yanavyotamkwa kama maneno mengine kuna ukakasi gain? Na wenyewe waswahili ndivyo wanavyotamka? Kwa hoja hizi ni wazi kuwa kuna matumizi yasiyosahihi ya matamshi ya maneno haya. La kusikitisha zaidi katika makosa hayo yamoo katika maandishi yote yaliyomo vitabuni, magazetini na katika majarida. Kwa ujumla sababu hizo kama zilivyofafanuliwa hapo katika matumizi yasiyo sahihi ya Kiswahili sanifu. Sababu hizi ni kama sababu zilizofafanuliwa na Pamela Ligami na wenzake wakisema “ kuna sababu mbalimbali zinazochangia matatizo katika lugha ya Kiswahili. Miongoni mwao na athari za lugha ya kwanza: makosa ya kimatamshi, mazingira, sarufi, matatizo ya kijamii na namna ya ufundishaji”
TAATHIRA YA KUDHARAULIWA KWA LUGHA YA KISWAHILI
Taathira nyingine ya msingi ni iayopelekea lughaya Kiswahili kudharauliwa na ama wageni au hata wale wenyeji hasa vijana ambao hawana uchungu wa asili wa lugha yao na utamaduni wao na vilivyo vyao. Hali hii huwasononesha wataalamu wengi hususani wenye uchungu na lugha hii na wakereketwa wa Kiswahili na ambao wanaithamini lugha yao na kujivunia katika Afrika mashariki. Wakereketwa au watu wenye uchungu na lugha yao wanapoona au kusikia matumizi yasiyokuwa sahihi ya lugha yao tukufu huwa na majonzi na masikitiko na ndipo baadhi yao huchukua hatua ya kukemea ama kwa kusema au kwa kuandika kama inavyokemea kimaandishi makala hii
MAKOSA MBALIMBALI YANAYOJITOKEZA KATIKA LUGHA
Kutokana na taadhira hizi kuna aina mbalibali za makosa yanayojitokeza kwa watumiaji wa lugha. Makosa hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni makosa ya Kisarufi na makosa ya kimantiki. Katika kipengele hiki tutaangalia makosa hayo na namna ya kurekebisha.
MAKOSA YA KISARUFI
Kila lugha ina kanuni na taratibu ambazo hutawala katika matumizi ya lugha ili watu waweze kuelewana kanuni hizo zipo vunjwa au kukiukwa huweza kusababisha makosa kujitokeza na upotovu katika lugha. Makosa ya kisarufi yanaweza kugawanyika katika sehemu zifuatazo:- makosa ya kimsamiati, makosa ya kimuundo, makosa ya matamshi, kuongeza vitamkwa au viambishi, kuacha maneno, makosa ya tafsiri sisi.
MAKOSA YA KIMSAMIATI
Watumiaji wa lugha huchanganya masamiati wakati wa kuzungumza au kuandika. Watu hutumia msamiati usiolingana na msamiati usiolinga na maana iliyokusudia
Mfano:- Nona na nenepa
Wengi husema siku hizi umenona sana.
Badala ya kusema, Siku hizi umenenepa sana.
mazingira na mazingara
Watu husema Mazingara yameharibiwa sana siku hizi.
badala ya kusema Mazingira yameharibiwa sana siku hizi.
Ajali na ajili
Watu husema Amefariki wa ajili ya gari.
badala ya kusema Amefariki kwa ajali ya gari.
Wakilisha na wasilisha
Watu husema, Waziri wa fedha atawakilisha bajeti ya mwaka kesho.
Badala ya kusema Waziri wa fedha atawasilisha bajeti ya mwaka kesho.
MAKOSA YA KIMUUNDO
Kwa kawaida sentensi za kiswahili huanza na nomino ya mtenda au mtendwa.
Mfano:- mtoto mpole anacheza
Mzungumzaji asiye fuata kanuni husema Mpole mtoto anacheza.
Kalamu yangu imeibwa.
badala ya kusema kalamu yangu imeibiwa.
MAKOSA YA KIMATAMSHI
Watu wengi hushindwa kutamka baadhi ya sauti za kiswahili wakati mwingine huchanganya na kubadili sauti hizo Mfano Wakurya hutumia ’r’ badala ya ’l’
Nenda karare
badala ya kusema nenda kalale
Wandali hutumia ’s’ badala ya ’z’ na ’dh’ na ’th’
mfano selasini
badala ya thelathini
Sahabu
badala ya dhahabu
Samani
Badala ya zamani
Makosa haya mara nyingi yanatokana na athari ya lugha mama. Kwa kuwa lugha ya kiswahili ni lugha ya pili kwa wazungumzaji wengi. Hivyo lugha ya kwanza huwa na athari kubwa kwa mzungumzaji wa wa lugha ya pili.
KOSA LA KUONGEZA VITAMKWA
Baadhi ya wazungumzaji huongeza vitamkwa mahari pasipo hitajika na hivyo kuharibu lugha.
Mfano. Nendaga
badala ya nenda
Mashule
badala ya shule
Huwaga anapenda fujo
badala ya huwa anapenda fujo
KOSA LA KUACHA MANENO
Watumia lugha huweza kuacha maneno katika sentensi na bado wakafikiri wanatoa ujumbe uleule uliokusudiwa.
mfano, Watu husema Juma ameondoka kazini akiwa na maana kuwa Juma ameondoka kwenda kazini lakini sahihi ni kuwa Ametoka kazini.
Alfredi amerudi kazini akiwa na maana kuwa Afredi ametoka kazini.
Kwa mzungumzaji anatoa maana ambayo ni kinyume kabisa na ile maana aliyo kusudia kusema. Ambapo anakusudia kuuliza kama Alfredi amekwenda tena kazini.
MAKOSA YA TAFSIRI SISISI
Tafsiri sisisi ni tafsiri ya neno kwa neno. Tafsiri hii inapofanywa huleta matatizo ya kisarufi katika lugha
mfano. Kimbizwa hospitali She runed to hospital
badala ya kusema amepelekwa hospitali
At the end of the day
Mwisho wa siku.
Badala ya kusema hatimaye.
MAKOSA YA KIMANTIKI
Mantiki ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Makosa ya kimantiki ni yale yanayoonesha kukosekana kwa utaratibu wa fikra. Nimakosa yanatokana na upotovu wa mawazo ya mzungumzaji
Mfano watu wengi husikika wakiema hivi: Usimwage kuku kwenye mchele mwingi
Badala ya usimwage mchele kwenye kuku wengi
Nyumba imeingia nyoka  Badala ya kusema Nyoka ameingia ndani ya nyumba
Chai imeingia nzi Badala ya kusema Nzi ameingia kwenye chai.
MSWAHILI
Kutokana na mtazamo hiyo na dhana na maendeleo ya lugha ya kiswahili, inaonekana wazi kuwa ni vigumu kumpata mswahili ambaye ni mmiliki wa lugha hii ya kiswahili. Inaonesha dhahili kuwa mswahili anaweza kutazamwa kwa namna tofauti kama zifuatazo;-
i).  Mswahili anaweza kuwa ni mtu mahuruti yaani ni mtu chotara ambaye ni lazima awe ametokana mwingiliano wa pande mbili ambao ni wabantu na watu wanaonasibishwa na Waarabu
ii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu wa mjini aliyeacha dini, utamaduni, mila na desturi zake za asili na kukimbilia dini, utamaduni, mila na desturi kutoka mataifa mengine kutoka uarabuni na nchi za kimagharibi
iii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya kiswahili
iv). Mswahili anaweza kuwa ni mkazi wa ya Afrika Mashariki hususani paeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
v). Mswahili anaweza kuwa ni mtu anayeishi katika maeneo ya kawaida ya mjini (uswahilini)
vi). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye ni mwafrika asili, anayepatikana katika nchi za Kenya na Tanzania
v). Mswahili ni mtu mwenye maumbile na ya kiafrika, ikimaanisha kuwa ni mtu wa miraba minne.
HITIMISHO
Kabla ya uhuru kulikuwa na juhudi za makusudi za waasisi wa Taifa letu kukuza na kukiendeleza kiswahili. Miaka hamsini baada ya uhuru kiswahili kimekuaa na kuenea kwa sehemu kubwa dunia. Pamoja na hayo kiswahili kimekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zimeweza kupotosha lugha hii. Upotoshwaji huo hufanywa na wazawa au watumiaji wa kiswahili na kukifanya kiswahili kionekane kuwa hakina maana wala thamani kwa watu wengine. Watanzania ambao ni watumiaji wakuu wa lugha yakiswahili wanatakiwa kuchukua juhudi za makusudi katika kukifanya kiswahili kiwe katika hadhi yake. Kimatamshi, kimuundo, na kimsamiati. Pia Serikali ichukue juhudi za makusudi za kukikuza na kukiendeleza kiswahili kwa kuwaelimisha na kuwatunza wataalamu wa lugha hii adhimu ya Tanzania. Wataalamu wawe na msimamo mmoja katika taaluma hii maana wakati mwingine huwachanganya watu wanaojifunza lugha hii. Lugha hii ya kiswahili ibaki katika misingi ya sarufi yake ya lugha za kibantu ambazo kwazo zimeunda kiswahili.
VITABU VYA REJEA
  1. Chiraghdin S. na Mnyapala M. (1977) Historia ya Kiswahili, Oxford University Press Nairobi
  2. Nkwera, F.M.V, (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo, THP, Dar es salaam.
  3. Massamba na wenzake (1999) Sarufi Miundo ya Kiswahili  Sanifu(SAMIKISA), TUKI, Dar es  Salaam
  4. Khamis, A.A, 2003 Uchambuzi Halisi wa Matumizi ya Kiswahili Asilia, Zanzibar. SUZA Press
  5. Msokile M (1992) Historia na Matumizi ya KiswahiliEPD Kibaha
    TUMI ( ) Kiswahili Sekondari,
  1. Broomfield (1930) Sarufi ya Kiswahili, London, The sheldon press
  2. Habwe J. na Karanja P. (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Nairobi phonex Publishers LTD
  3. Mwansoko HJM na Tumbo. (1996) Matumizi ya kiswahili Bungeni, TUKI, Dar es salaam
  4. BAKITA, (2004), Makala ya siku ya Kiswahili Kiswahili na Utandawazi, Dar es salaamu
  5. TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la pili, Oxford university press, Nairobi
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)