MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
NGUVU YA KAMATI YA LUGHA NDANI NA NJE YA AFRIKA

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
NGUVU YA KAMATI YA LUGHA NDANI NA NJE YA AFRIKA
#1
Makampuni ya kuchapisha vitabu hayakusita kuchapisha kitabu baada ya ithibati ya kamati kupatikana, kwa sababu hiyo ilikuwa thibitisho kwamba kitabu hicho kitatumiwa katika shule za serikali na zile zenye kupata ruzuku ya serikali. Ithibati ilionyesha kwamba kitabu kitapata wanunuzi, jambo ambalo lilisaidia kupunguza gharama ya kuchapisha vitabu vya Kiswahili ambavyo havikuwa, na hadi sasa havina, wasomaji wengi nje ya shule. Waandishi walipata moyo wa kuandika walipojua kwamba vitabu vyao vitatumiwa kote katika Afrika Mashariki. Vitabu viliuzwa kwa wingi. Kwa mfano, vitabu vinne vya Ronald Snoxall viliuzwa takriban nakala 1,000,000.
Nguvu za ithibati hazikuishia Afrika Mashariki tu. Uwezo wa ithibati wa Kamati ulikuwa ukiheshimiwa kote ulimwenguni, kama asemavyo Ratcliffe:
“Wachapishaji wa Ulaya, Marekani na sehemu zingine za ulimwengu wamekuwa wakitegemea ithibati iliyotolewa na kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa miswada waliopelekewa na waandishi binafsi, Waafrika na Wazungu ili kuwasomea na kuwasahihishia.” (Ratcliffe, ILC Bulletin Na 21, 1951: 3).
Ili kuwatia moyo Waafrika waweze kuandika kusudi watosheleze mahitaji ya vitabu vya fasihi, Kamati ilianzisha mashindano ya kuandika insha mnamo 1935. Ili kuwapa motisha ya kuendeleza vipawa vilivyo- gunduliwa katika mashindano ya insha, mashindano ya uandishi yalianzi- shwa katika mwaka wa 1939. Kutokana na mashindano hayo miswada mingi ilipelekewa Kamati. Mashindano hayo yalianza kuwashirikisha washindani Wazungu katika mwaka 1942 ili kukuza uandishi wa Kiswahili miongoni mwa watawala wa siku za baadaye. (Ratcliffe 1942: 9). Kwa hivyo, kamati ilikuwa ikitekeleza malengo iliyokusudiwa.
Ilikuwa ikichapisha vitabu vya Kiswahili sanifu ili iwashawishi waandishi wapya, na ilihakikisha kwamba vitabu vilikuwa vikitafsiriwa kwa Kiswahili. Kamusi ya Kiswahili-Kiswahili ilichapishwa mnamo 1935 hali kamusi ya Kiswahili-Kiingereza na ya Kiingereza-Kiswahili zilichapishwa Mwaka 1939.
Kamati iliendelea kujibu maswali ya umma kuhusu maneno mapya, asili ya maneno, maneno yaliyoazimwa n.k., na maneno yaliyo-  kubaliwa yalichapishwa katika jarida la l.L.C. Bulletin.
Hapo awali nakala za l.L.C. Bulletin zilikuwa zikitolewa bure kwa wale waliokuwa wakipenda. Baadhi ya vitabu vya sayansi vilikuwa vimetafsiriwa kwa Kiswahili.
2.2 Othografia
Katika utangulizi wa kitabu kinachoitwa A Handbook of the Swahili Language, Askofu Steere alijadali suala la tahajia au hati za maandishi ya Kiswahili, kwa undani. Karibu maandishi yote ya Kiswahili kabla ya wakati wake yalikuwa yameandikwa kwa hati za Kiarabu. Mengi kati ya maandishi hayo yalikuwa ni tenzi na mashairi ya kidini na mambo ya kawaida yaliyoandikwa kwa lahaja ya kishairi ya Kaskazini ambayo Steere alishuku iwapo ilieleweka na watu wengi. Ingawa Kiswahili cha wakati wake kilikuwa kikitumiwa katika kuandikiana barua, Steere anasema kwamba barua kama hizo zilianzia na salamu kwa Kiarabu na pia maneno na vifungu vya maneno ya Kiarabu vilikuwa vikichanganywa na Kiswahili.
Steere alitambua kwamba hati za Kiarabu hazifai kuandikia Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiswahili inazo irabu tano ikilinganishwa na irabu tatu za Kiarabu. Kuhusu konsonati, hati za Kiarabu zinao upungufu wa konsonanti cha, g, p, na v. Steere aliandika hivi:
“Kwa hivyo, Waswahili wanalazimika kuandika ba, f, au p waki- kusudia kuandika mb au b; wanaandika ghain badala ya g, ng, ng’; fa badala ya v, mv na f; ya badala ya ny na y; shin badala ya ch na sh; pia wanaiwacha n inapozitangulia d, j, y na z.” (Steere 1870: 5)
Kwa hivyo, ni wazi kwamba hati za Kiarabu hazifai na hazitoshelezi maandishi ya Kiswahili kwa sababu ya kutatanisha. Ili kuonyesha matatizo ya hati hizi, Steere anaandika hivi:
“Nilipokuwa Zanzibar, kulikuwa na barua iliyotoka Kilwa kuhusu vita. Barua ilitaja kwamba mtu mmoja kati ya wale waliopigana alikuwa amekufa au amevuka na hakuna aliyeweza kusema kile kilichokuwa kimetendeka. Konsonanti mbili za mwisho zilikuwa fa na gaf zikiwa na vitone vitatu juu yake. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya kwanza, mtu huyo alikuwa amekufa. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya pili alikuwa hai, lakini vitone hivyo vilikuwa katikati hivi kwamba hakuna aliyeweza kuvigawanya.
Iwapo Kiarabu kingekuwa na herufi v ingekuwa wazi.” (Steere 1870: 6). Zikilinganishwa na hati za Kiarabu, hati za Kirumi hazileti matatizo yoyote katika kuandika Kiswahili. Sababu yake ni kwamba wasomi wengi wa Kiswahili waliokuja baada ya Krapf na Steere waliamua kutumia hati za Kirumi walizokuwa wamezizoea badala ya hati za Kiarabu zilizokuwa zikitumika kuandika Kiswahili. Maneno na mizani katika Kiarabu mara nyingi huishia kwa konsonati. Hili pia ni jambo lingine linalozifanya hati za Kiarabu zisifae kukiandika Kiswahili.
Dhehebu la UMCA lilichapisha vitabu kufuatia mtindo uliotumiwa katika kuchapisha vitabu vya Steere. Misheni wa Kizungu walifanana na waanzilishi wa uchunguzi wa Kiswahili kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao kutumia hati za Kirumi badala ya zile za Kiarabu. Mkutano wa Dar es Salaam wa 1925 uliamua kutozitumia hati za Kiarabu pamoja na konsonanti za Kiarabu kama vile kh.
Profesa Carl Meinhof alipohudhuria mkutano wa Mombasa wa 1928, waliohudhuria walikuwa na nafasi ya kushauriana naye kuhusu othografia ya Kiswahili. Meinhof alikubaliana na nyingi kati ya tahajia iliyopendeke- zwa kwa kuwa ilikuwa rahisi bila kutatanisha, isipokuwa katika herufi ch na ng’. Meinhof alipendekeza c itumiwe badala ya ch. Badala ya kutumia alama tatu za maandishi (ng’) kusimamia sauti moja, alipendekeza kutumiwa kwa n yenye mkia itumiwe kama ilivyo katika maandishi ya kifonetiki.
Lakini mashauri haya ya Meinhof hayakukubaliwa. Wasomi wa Kiswahili wakati huo walijiona kuwa sahihi, na kwamba mapendekezo ya Meinhof yalifaa tu katika maandishi ya kifonetiki katika isimu lakini hayakufaa othografia ya kawaida ya Kiswahili. Katika majadiliano yao walitaja kwamba ingekuwa vigumu kupiga taipu n hiyo yenye mkia.
Tatizo hili lingetatuliwa hapo mwanzoni kwa kupiga taipu herufi j juu ya n wakingojea kurekebishwa kwa mashine. Suluhisho hili halikukubaliwa, na kwa hivyo tatizo la kuandika sauti ya kwanza ya neno ng’ombe kwa sauti mbili na alama (ng’) lingali laendelea.
Upungufu mwingine wa othografia ya Kiswahili unaoweza kutajwa hapa ni kule kukosa kutofautisha konsonanti za kipua (nazali) ambazo ni mizani kamili na zile ambazo huambatana na irabu ili ziunde mizani kamili. (Taz. Mkude 1982). Mifano ya konsonanti za kipua (nazali) ambazo ni mizani kamili ni m na n za kwanza katika maneno mmea na nne. Sauti n ya neno nguruwe ni sawa na sauti ya n yenye mkia. Kwa hivyo, kama tungefuata othografia sanifu kikamilifu badala ya nguruwe tungeandika ng’guruwe.
Othografia ya Kiswahili sanifu haikukosa malalamiko. Kulikuwa na upinzani na kutoelewana hata kati ya misheni. Kasisi Roehl katika makala yake “Hali ya lugha katika Afrika Mashariki” (Africa Vol.3, Na.2, 1930), anaeleza masikitiko yake kwamba Idara ya Elimu huko Dar-es-Salaam ilikuwa imeanzisha othografia kinyume cha mapendekezo ya wataalamu wa isimu wa misheni. Roehl analalamika kwamba, kati ya makosa mengine, othografia inazipa nafasi za kipekee sauti za Kiarabu na kulazimisha zitumike babala ya kuwapa wazungumzaji wa Kiswahili uhuru wa kuzitamka kutegemea vile wanavyotamka sauti za lugha yao na kuziandika sauti hizo vile wanavyozitamka.
Kasisi Roehl anaeleza zaidi kwamba katika kuunda othografia ambayo inafaa Kiswahili zaidi, isiwe ni Tanganyika pekee ambayo inatoa uamuzi. Anapendekeza Kenya, Uganda na Congo (Zaire) zihusike ili kuunda othografia sanifu kwa watu wote wanaotumia Kiswahili. Kama tunavyojua sasa upungufu mkubwa uliofanywa na nchi za Afrika Mashariki katika kusanifisha Kiswahili ulikuwa ni kushindwa kushirikisha Zaire katika shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kama alivyo- pendekeza Kasisi Roehl. Upungufu huo, licha ya jitihada za Ronald Snoxall, unaeleza kuwepo kwa tofauti kadha kati ya Kiswahili cha Zaire na Kiswahili sanifu.
Kama inavyofahamika na kuelezwa wazi na wasomi kama vile John Williamson katika uchambuzi wake wa Kingwana cha maandishi (I.L.C. Bulletin Na. 21, 1951: 15-16), lahaja ya Kingwana haifuati upatano maalum kwa sababu ya kukosa kusanifishwa. Williamson alipata kwamba, katika makala moja herufi y na j zilitumiwa moja badala ya nyingine. Kwa hivyo maneno kama vile miji, jina, pamoja na kijana yalitumiwa katika sehemu moja ya makala, na kwingine katika makala hiyo hiyo maneno hayo yangeandikwa kama muyi, yina, pamoya na kiyana. Herufi r na l pia zilitumiwa moja badala ya nyingine. Habari, mara na hubiri yaliweza kupatikana katika makala moja na habali, mala na hubili. Herufi k na g zilichanganywa hivi kwamba maneno miziko na mizigo, ukonjwa na ugonjwa pia yalipatikana katika makala moja.
Kupatikana kwa maneno kama vile muyi, habali, miziko, ukonjwa katika makala moja na mji, habari, mizigo na ugonjwa katika othografia ya Kingwana yaonyesha kwamba ni rahisi kusanifisha. Iligunduliwa kwamba ilikuwa rahisi kusoma na kuelewa maandishi ya Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki kwa kutujia ujuzi wa Kingwana: Snoxall anaeleza kwamba alijaribu mara mbili kukifanya Kingwana kifuate taratibu za Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki. Kwanza alimtuma C. G. Richards aliyekuwa mkurugenzi wa East African Literature Bureau kwenda Belgian Congo (Zaire) kuwahimiza wasanifishe Kingwana. Richards alienda huko lakini hakufanikiwa. Snoxall alitamani kusambaza Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki ambacho chatumiwa na watu wengi zaidi. Maoni yake ni kwamba, Kingwana chatumiwa katika sehemu moja ya nchi moja, na kwa kuwa wanaokizungumza wanafahamu Kiswahili sanifu, ingekuwa rahisi kuwaleta pamoja na wale wanaotumia Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki: “Ingekuwa kazi rahisi ikifanywa kwa bidii”. (Snoxall ibid.)
Jaribio la pili alilofanya Snoxall lilikuwa ni kuwaalika Wabelgiji wawili kutoka Kongo (Zaire) kuhudhuria mkutano wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mjini Nairobi. Wabelgiji hao waliitikia mwaliko lakini walishangaa kuona kwamba kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na wajumbe Waafrika. Wabelgiji hawakufikiria kwamba wajumbe wa Kiafrika kama vile Shaaban Robert wangeweza kuwa wataalam wa lugha yao. Kwa hivyo Wabelgiji hawakutaka kujiunga na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Hawakuona kama ingekuwa vizuri kufanya hivyo.
 Ingawaje, Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, iliweza kuwajulisha watawala wa Kongo ya Ubelgiji kwamba tofauti kati ya Kingwana na Kiswahili sanifu ilikuwa ni matamshi yasiyofuata kanuni za safuri. Maoni hayo ya Kamati yalipelekewa watawala wa Kongo na Bwana Sandrart wa kutoka Rwanda aliyetumwa na Kongo ya Ubelgiji kuhudhuria mkutano wa kumi na tatu (13) wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mnamo 1950. Bwana Sandrart aliweza kuifahamisha Kamati mambo kadha kuhusu Kingwana. Tofauti za kimatamshi hazikutatiza kueleweka kwa Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika Zaire, Rwanda na Burundi.
Iwapo Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ingefaulu kuwashawishi watawala wa Kibelgiji kutumia Kiswahili sanifu, hali hiyo ingewezesha kutumiwa kwa vitabu vya Kiswahili sanifu katika eneo kubwa zaidi.
Kiswahili kingepata matumizi mapya ya kuwaunganisha Wazungu wenye asili za Uingereza na Ubelgiji mbali na kuwaunganisha Waafrika wa makabila na mataifa mbalimbali, kwa kuwa kungekuwa na lugha moja ya mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati. Pia Wakongo wangekuwa na Kiswahili sanifu. Kushirikishwa kwa Kongo na nchi zingine zinazotumia Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika makala yake ya 1930.
Canon G. W. Broomfield alijibu makala ya Kasisi Roehl kwa haraka alipoiandika makala yake “Kukifanya Kiswahili kiwe cha Kibantu” (Africa Vol.4 Na. 1,1931). Broomfield anaanza kwa kumfahamisha Roehl kwamba othografia ambayo Roehl anaizungumzia ilifanywa na kamati mjini Dar es Salaam mwezi Oktoba 1925. Kwa hivyo, anaeleza kwamba othografia hiyo haikubuniwa na Idara ya Elimu kama alivyodai Roehl.
Anasema kwamba Tanganyika pamoja na Zanzibar zilihudhuria na kwamba Kenya haikuhudhuria kutokana na kutoelewana hata ingawa ilikuwa imealikwa.
Anaendelea kueleza kwamba othografia iliyoidhinishwa ni ile ambayo ilikuwa ikitumiwa kwa miaka mingi na UMCA isipokuwa kutokutumiwa kwa kh. Maneno ambayo hapo awali yalikuwa yakiandikwa kwa kutumia konsonanti mbili zikifuatana kama vile hatta, milla na marra ingebidi yatumie konsonanti moja: hata, mila na mara. Kutumiwa kwa kh katika maneno kama vile khabari, khatia na khalisi, ilibidi yatumie h pekee: habari, hatia na halisi.
 Katika makala hiyo Broomfield anataja pia kwamba mmishonari mmoja alipinga othografia hiyo katika mkutano wa Dar es Salaamu wa 1925, lakini wanachama watano waliiunga mkono. Maelezo haya yana- onyesha kwamba ni watu wachache sana waliohusika katika kuamua suala la othografia. Yawezekana kwamba kanisa la Roehl, misheni ya Lutheran, haikualikwa kutoa maoni yao au kuhudhuria mkutano huo wa 1925.
Kuhusu msamiati wa Kiarabu katika Kiswahili ambao unasababisha kuwepo na konsonanti za Kiarabu katika othografia ya Kiswahili, Broomfield anaeleza kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno ya Kiswahili. Anadai kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno ya Kiswahili hivi kwamba Kiswahili hakijawahi kuwepo bila ya maneno ya Kiarabu na kwamba hakiwezi kuyaondoa. Kwa hivyo hakubaliani na maoni ya Roehl, ya ukweli kwamba hapo mwanzo Kiswahili kilikuwa lugha safi ya Kibantu na kwamba maneno ya Kiarabu yaliazimwa. Ukweli kwamba Kiswahili kilikuwepo kabla ya kuja kwa Waarabu hauwezi kubishaniwa. Hii ndiyo sababu mhariri wa jarida la Africa alisahihisha maoni ya kupotosha ya Broomfield katika maoni ya mhariri yaliyotangulia makala hiyo.
Majadiliano ya othografia yaliendelea wakati wa vita vya pili vya dunia. Mjadala huo wa wanakamati ulihusu mageuko ya irabu yaliyosababishwa na mfuatano wa irabu mbili katika neno moja. Mageuko hayo ni kama vile kuenda na tuataka kuwa kwenda na twataka. Kasisi A. R. Pittway kutoka Kenya, aliyefanya uchunguzi wake katika lahaja ya Kimvita, aliuanzisha mjadala katika jarida la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Bulletin Na. 13 la 1939. Pittway anaeleza kwamba kwa kuwa usanifishaji unahusu lahaja tofauti kusiwe na lahaja yoyote muhimu itakayopuuzwa. Anasema kwamba maneno ambayo si ya Kiunguja, semi, na miundo ya kisarufi, yastahili kukubaliwa kutumiwa sambamba na Kiswahili sanifu ili kutajirisha lugha.
Kwa maoni yake, kukubaliwa kwa matumizi hayo ya kilahaja kutasaidia kufanya Kiswahili kipendwe sana na watu.
Pittway anaendelea kupendekeza kwamba mw inayotangulia u igeuzwe kuwa mu. Anaeleza kwamba ni kawaida mu kugeuka kuwa mw inapo- tangulia a,i,e na o, lakini kifonetiki si jambo la kawaida kwa mu kugeuka kuwa mw inapotangulia u. Pittway alitaka mabadiliko hayo kwa sababu dhehebu lake la C.M.S. Iililokuwa limeamua kusanifisha Biblia na Kitabu cha Maombi lilihitaji muongozo. Alisema kwamba mabadiliko hayo yalikuwa muhimu kwa sababu matumizi ya mu na mw katika vitabu vilivyopitishwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaelekea hayakufuata kanuni yoyote.
Kama ilivyotarajiwa, makala ya Pittway iliyoandikwa mara tu baada ya kuchapishwa kwa kamusi za Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza, ilipingwa mara moja. Katika jarida, Bulletin Na. 14 la 1948, Ronald Snoxall anatahadharisha dhidi ya othografia inayokwenda kinyume cha kamusi sanifu iliyoichukua kamati miaka mingi kutayarisha. Kwa hivyo pendekezo la Pittway halipaswi kukubaliwa kuvuruga othografia iliyo- kubaliwa. Snoxall anapendekeza othografia iliyotumika katika kamusi ikubaliwe vile ilivyo.
Maoni mengi kuhusu pendekezo la Pittway yalitolewa na Kasisi Fr. Alfons Loogman wa Bagamoyo aliyetahadharisha dhidi ya kukubali kanuni za lugha zibadilishe othografia iliyokubaliwa. Loogman anaeleza kwamba kusanifishwa kwa Kiswahili kuna maana kwamba lahaja moja ilichaguliwa kuwa msingi wake na kwamba inabidi lahaja zingine ziwe tayari kupoteza baadhi ya miundo na kanuni za sarufi zao licha ya umuhimu wa lahaja hizo. Hata hivyo Loogman anaunga mkono kanuni ya mgeuko wa sauti uliotajwa na kusema kwamba hakuna mtu angependa kusema yaitu, waivi au maino badala ya yetu, wevi na meno.
Katika kukomesha mjadala huu, katibu wa kamati Kasisi B. J. Ratcliffe anakiri kwamba hakuna othografia inayoweza kutosheleza mahitaji yote ya lahaja zote. Anatoa msimamo rasmi kueleza hivi:
“‘M’ ya Kiswahili kwa kawaida husimamia ‘m’, ‘u’ hutoweka kabla ya konsonanti, na mara nyingi huwa ‘w’ inapotangulia irabu ila wakati inapotangulia kiini cha neno linaloanzia kwa ‘u’ au kabla ya ‘w’ au hugeuka kuwa ‘w’ wakati mwingine iwapo maneno yanahitaji kugeuka huko.” (ibid. uk. 6).
Ni jambo zuri kwamba Kamati ilipinga mabadiliko ya othografia. Kama watu wangekuwa huru kurekebisha othografia katika siku hizo, hatungejiepusha na makosa. Tungekumbwa na othografia ya kizamani kama ile ya Kiingereza ambapo maneno yanaandikwa kwa njia tofauti sana na vile yanavyotamkwa. Nikitoa mifano miwili tu, neno Leicester hutamkwa Lesta, na Gloucester hutamkwa Glosta.
2.3 Maoni kuhusu usanifishaji
Kumbukumbu iliyojulikana kwa jina “Kiswahili cha Kisasa”, I.L.C. Bulletin Na. 7 1934, iliandikwa na afisa wa Idara ya Elimu nchini Kenya. Kumbukumbu hiyo ilipelekewa katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na Mkurugenzi wa Elimu ili ijadiliwe katika mkutano wa Kamati. Mwandishi ambaye hakutaja jina lake alitahadharisha Kamati kwamba Kiswahili walichokuwa wakishughulikia kilikuwa kikiendelea kuwa lugha ngeni kwa Waswahili wenyewe kwa kutengenezewa kanuni mpya na wageni. Sehemu moja ya kumbukumbu hiyo ilisema hivi:-
“Tumesanifisha Kiswahili, na katika shughuli za kufanya hivyo yaonekana Kiswahili kimekuwa lugha mpya. Bila shaka sote tunakiri kwamba kama lugha zingine Kiswahili kitaendelea na kitapanuka katika nyanja za muundo, semi na msamiati kwa kuathiriwa na ustaarabu wa walowezi. Lakini maendeleo hayo yafaa yatokane na mawazo ya Waswahili; haifai kuwalazimisha kuyapokea.
Lakini hivyo ndivyo ilivyo; tuko katika harakati za kuwafunza Waswahili Iugha yao kupitia vitabuni, vingi ambavyo si vya Kiswahili kimuundo au kimawazo, na ambavyo lugha yake inafanana kidogo sana na lugha inayozungumzwa.
Labda tuna haraka sana kuhepa ukweli kwamba Waswahili wenyewe wana uwezo wa kurekebisha lugha yao kufaa mahitaji ya siku hizi na kwamba tayari wanafanya hivyo kwa haraka ya kustaajabisha.
Hivi ndivyo hali ilivyo huko Mombasa na inaweza kudhihirishwa na wachunguzi wengi. Jambo muhimu sana ni kwamba jitihada zetu hizi za kupata mwana haramu huyu, Kiswahili cha Kiingereza, zina matokeo ya kututenganisha na jamii tunaojaribu kuelimisha. Au tukieleza kwa maneno mengi, tunafikiria kwa Kiingereza hadi wao wanafikiria kwa Kiswahili na hatuwezi kuziba pengo hili.” (I.L.C. Bulletin Na. 7 1934: 4).
Mwandishi anafikiri kwamba sifa nyingi zisizo na kifani zilitolewa kuwasifu wachunguzi wakuu wa Kiswahili kama vile Krapf, Steere, Sacleux, Taylor, Veltten na Beech bila ya kujali kazi zao ambazo zingetumiwa shuleni. Anafikiri kwamba kamati ilikuwa na haraka sana ya kuandika vitabu na kutafsiri vingine na kwamba katika kufanya hivyo wakaguzi wasiokuwa na ujuzi waliajiriwa. Anaendelea kusema kwamba wale wanaoitetea hii lugha mpya wanasema kwamba ndiyo ya pekee inayoweza kueleweka na makabila yasiyokuwa ya Waswahili. Anakanusha wazo hili kwa kusema kwamba ni rahisi kwa Waafrika kujifunza Kiswahili kuliko Kiswahili hiki kilichochanganywa na muundo wa Kiingereza.
Ili kuthibitisha kwamba Waswahili walipinga mtindo huu mpya wa Kiswahili na othografia yake, mwandishi wa “Kiswahili cha Kisasa” aliambatisha makala kutoka gazeti la ‘Al-lslah’ la Mombasa. Makala hiyo ilikuwa ya Juni 20, 1932 ambayo mwandishi aliishambulia othografia mpya ya Kiswhili. Othografia iliyokubaliwa kama tulivyoeleza haikuwa na baadhi ya herufi kama vile kh inayopatikana tu katika maneno yaliyoazimwa kutoka kwa Kiarabu. Othografia iliyokubaliwa ingekuwa na h badala ya kh na hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya mwandishi wa makala ya Al-lslah alalamike. Makala hiyo inasema hivi:
“Ni madhara makubwa tupatayo kwa Kiswahili hiki kilichoharibiwa ni Wazungu. Kiswahili ni lugha ya watu wa Pwani, nacho hakiwi safi ella kitanganyikapo na Kiarabu. Tangu kufika Wazungu, wame- kigeuza na kukiharibu kwa wapendavyo wao; wamepunguza baadhi ya harufu ambazo ni lazima ziwemo katika baadhi ya maneno, na pengine hubadilika maana kwa kukosekana harufu hizo. Wameitungia vitabu vya nahau, na pengine hao watungao vitabu hivyo ni Wazungu wageni hawajui sana lugha hii, na ambao wavitowa makosa ni Wazungu wa bara, wasiojuwa Kiswahili. Na wakiambiwa ni mtu wa Pwani kuwa ni makosa, hawakubali ella kile kile chao …” (I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 8).
Mwandishi wa “Kiswahili cha Kisasa” anaendelea kutilia nguvu mambo aliyoyataja kwa kusema kwamba baadhi ya vitabu vilivyochapishwa hivi karibuni vilikuwa tafsiri ya neno kwa neno ya vitabu vya Kiingereza. Anasema kwamba matumizi ya kanuni za sarufi yalikuwa yakihimishwa sana jambo ambalo lilifanya vitabu vilivyochapishwa kuwa sahihi kisarufi, lakini vilikuwa mbali sana na Kiswahili halisi kwa kuwa sarufi peke yake haiundi lugha. Anataja upungufu mkubwa wa Kiswahili “kipya”. Upungu- fu huo ni, tafsiri ya neno kwa neno, kuzingatia matumizi ya kanuni za sarufi bila ya kujali methali na semi pamoja na kutojali tabia ya kishairi ya Kiswahili. Mwishowe anatoa mifano ya sentensi ambazo zina upungufu kutokana na vitabu vilivyoandikwa kwa Kiswahili sanifu vilivyokuwa vikitumika shuleni wakati huo.
Katika jarida hilo hilo la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, kufuatia makala hiyo ya “Kiswahili cha Kisasa” kuna jibu lake lililo- andikwa na Kasisi Canon Broomfield mwandishi wa kitabu kijulikanacho kama Sarufi ya Kiswahili, ambaye kwa wakati huo alikuwa mhariri kutoka Zanzibar. Canon Broomfield alikuwa ameombwa na katibu wa Kamati kumjibu mwandishi wa “Kiswahili cha Kisasa” kwa manufaa ya wasomaji wa jarida.
Katika jibu lake Canon Broomfield anaonelea kwamba mwandishi wa “Kiswahili cha Kisasa” ametia chumvi suala la kugeuka kwa Kiswahili kuwa lugha mpya. Anasema kwamba marekebisho yaliyokuwa yakitokea yalikuwa hayana budi kuwepo kwa kuwa lahaja moja ndiyo ilichaguliwa kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili. Kwa hiyo marekebisho yalifanywa ili kusaidia kutumiwa kwa lahaja hiyo kama lugha ya mawasiliano kote.
Usanifishaji ulihitaji kusomesha Kiswahili hicho ambacho chaonekana kuwa kipwa. Anaeleza zaidi kwamba Kiswahili sanifu chaonekana kuwa lugha mpya zaidi katika lahaja zinazotofautiana sana na Kiunguja, ambacho ndicho msingi wa usanifishaji.
Kuhusu athari za Kiingereza katika Kiswahili, Broomfield anaeleza kwamba hilo ni jambo lisiloweza kuepukika kwa sababu lugha mbili zinapotumika katika eneo moja hazina budi kuathiriana na haziwezi kubaki kuwa safi, pia matokeo ya kuazima huenda yakatajirisha lugha inayoazima. Anatoa mifano ya semi za Kiebrania zilizoingia katika Kiingereza kupitia tafsiri ya Biblia. Sasa semi hizo zimekuwa Kiingereza.
Anatetea kile kinachoonekana kama tafsiri za neno kwa neno au tafsiri za semi za Kiingereza kwa kusema kwamba Kiingereza kinaathiri Kiswahili cha mazungumzo cha Waafrika wanaozijua lugha zote mbili. Anasema kwamba mabadiliko kama hayo ni ya kawaida kwa kuwa lugha hubadilika kila mara na kwamba Kiswahili cha wakati huo hakikuwa sawa na Kiswahili cha wakati wa Krapf. Haoni kama Kiswahili kinaweza kujiepu-
sha na kuazima kwa istilahi za ufundi na teknolojia. Broomfield anaandika hivi:
“Maendeleo yoyote ya kielimu huhitaji kuwa na mabadiliko na maendeleo ya lugha itakayotumika kueleza elimu hiyo. Tupende tusipende, Kiswahili kitabadilika na kuendelea kwa haraka, kwa sababu hizi. Katika wakati huu kuna maandishi machache sana na tunaanza kusanifisha lugha hii, pia Waafrika wanaojua kusoma na kaundika ni wachache sana. Tena Afrika inawasiliana na ustaarabu wa Uropa; elimu mpya na utaalamu mpya wa kila aina unawafikia Waafrika. Kiswahili cha miaka ishirini tu iliyopita hakifai siku hizi. Ni lazima lugha ibadilike na itabadilika, tupende tusipende…” (Broomfield I.L.C. Bulletin Na 7, 1934: 4).
Njia za kukuza lugha zitakuwa ni pamoja na kuazima maneno kutoka lugha za kigeni hasa Kiingereza na kuunda maneno mapya. Broomfield anaonya kwamba lazima watu wajifunze maneno hayo na vile yanavyo- tumika. Anatoa mfano wa maneno kumi na tisa (19) yaliyoundwa kutokana na neno vote aliloliazima kutoka kwa Kiingereza, ambayo anasema, kwamba yanaweza kueleweka vizuri baada ya kujifunza maana ya neno vote.
Broomfield anasema kwamba mwandishi wa kumbukumbu hakuzi- shughulikia lahaja tofauti za Kiswahili ambazo zatofautiana kimsamiati, kimatamshi, sarufi na semi ambazo zaifanya kazi ya wahariri wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kuwa ngumu. Anasema kwamba wahariri hawatarajiwi kuandika upya miswada wanayopelekewa. Anaeleza kwamba, Kiunguja kinapotumiwa kama msingi wa usanifishaji jitihada zinafanywa kuzihusisha lahaja zingine kwa kuwa lahaja zote kubwa zitakichangia Kiswahili katika siku za baadaye.
Broomfield anakanusha madai ya mwandishi wa kumbukumbu kwamba kuna chochote katika kazi za Meinhof, Werner, Madan, Torrend, Domet, Stigand na kadhalika ambacho chaweza kufaa shuleni.
“Yako wapi maandishi hayo; je, twapata chochote kinachoweza kutumika kama vitabu vya shule vya jiografia, historia, hesabu, afya, elimu ya viumbe, kilimo au uraia? Mbali na uchunguzi wa kiisimu unaokusudiwa kusomwa na Wazungu, maandishi mengine mengi, zaidi ni mkusanyiko wa mila, ngano na hadithi. Nyingi kati ya hizi ni za lugha isiyo na adabu na nyingi hazina umuhimu wowote wa kielimu.” (Broomfield, I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 19).
Anakiri kwamba uandishi wa vitabu umefanywa kwa haraka na kwamba baadhi ya vitabu hivyo havikosi upungufu lakini kuchaguliwa kwa Kiswahili na kule kupenda kwa nchi zote za Afrika Mashariki kutumia Kiswahili wastani kumesabibisha hali kuwa hivyo. Wale walio- andika vitabu walifanya hivyo kwa sababu hapo awali hakukuwa na vitabu kama hivyo na ni juu ya wale wanaotoa lawama kuandika vitabu bora zaidi.
Mwisho kabisa Broomfield anataja kwamba kusanifisha na kuunganisha lugha ni kazi ngumu sana na kwamba wale wanaoishughulikia hawata- pendwa. Makala iliyoandikwa katika gazeti la Al-Islah imeandikwa kwa Kimvita na wale ambao hawatumii lahaja hiyo hawataisifu kamwe. Pia Broomfield anasema kwamba, katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki alijibu makala ya Al-Islah lakini gazeti hilo halikuichapisha.
Huko kuonekana kwa Kiswahili kuwa ni lugha ngeni kwa sababu ya kutafsiri wakati wa usanifishaji, kwa maoni yangu, hakungeepukika. Hiyo ilikuwa deni ambayo ilibidi Kiswahili kilipe kwa maendeleo yake ya haraka. Kiswahili ambacho hapo awali kilikuwa tu lugha ya biashara, kilianza kutumika kwa haraka kama lugha ya elimu siyo tu Uswahilini bali kote katika Afrika Mashariki. Kwa hivyo Kiswahili hakikuwa tena lugha ya Waswahili tu kama vile mwandishi wa “Kiswahili cha Kisasa” alivyosema bali kilikuwa lugha ya halaiki kubwa ya watu wa Afrika Mashariki nzima. Ili kukiwezesha Kiswahili kiumudu wadhifa huo, ilibidi vitabu vitayarishwe kwa muda mfupi. Siku hizo hakukuwa na Waafrika wa kutosha ambao wangeweza ama kuandika vitabu vilivyohitajika au kutafsiri vya Kiingereza kwa Kiswahili.
Maoni kwamba Kiswahili kilikuwa kikichafuliwa kwa kusanifishwa na kwa kutumiwa kwa kuandikia na kutafsiria vitabu vya shule hayakuwa Kenya pekee. Nchini Zanzibar, kilikotoka Kiunguja, kulikuwa na hofu kwamba lahaja ya Kiunguja itachafuliwa na jitihada za usanifishaji. Akitoa ripoti yake kuhusu vitabu vya shule ya mwaka 1927, Mkaguzi wa Shule wa Zanzibar, Bwana G. B. Johnson alieleza masikitiko yake kwamba ni sharti vitabu vinavyotumiwa Zanzibar vikubalike huko Tanganyika. Alisema kwamba ni sharti vitabu hivyo viwe vya “Kiswahili kilichorekebishwa kuambatana na maagizo ya Kamati ya Uchapishaji ya Tanganyika”. Ilibidi vitabu vya Zanzibar vikubalike Tanganyika kwa sababu Zanzibar ilikuwa ikihitaji vitabu vichache sana na gharama ya kuchapisha vitabu vya shule za Zanzibar pekee ilikuwa kubwa.
Zanzibar ilifurahia uamuzi wa kutumiwa kwa Kiunguja kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili. Lakini kulikuwa na hofu kwamba ingewabidi Wazanzibari kutumia maneno na miundo kutoka Tanganyika. Jambo hili liliwakera sana kama inavyodhihirishwa na maneno ya Johnson.
“Yaonekana wazi kwamba hatimaye Zanzibar italazimika kutumia vitabu vya shule vilivyoandikwa kwa lugha yao iliyochafuliwa. Hili ni jambo la kusikitisha hata ingawa yaonekana haliepukiki. Hii ni gharama kubwa ya kulipa dhidi ya usanifishaji wa Kiswahili. Watu wa Zanzibar wanaojiona kwamba wanakitumia Kiswahili safi wanachukizwa na kutumiwa kwa Kiswahili cha bara ambacho kwao wanakiona kwamba ni lugha iliyoharibiwa. Kuhakikisha kwamba shule zetu zinatumia Kiswahili sanifu kutakuwa kazi ngumu isiyo- pendeza na itachukua muda kabla matumizi ya bara hayajakubalika.” Kutumiwa kwa Kiswahili kama lugha ya vitabu vya shule kulikuwa ni matumizi mapya ya lugha hiyo. Lugha ya vitabu vya shule ni tofauti na lugha ya mazungumzo. Katika Kiswahili, tofauti hiyo ilionekana kuwa kubwa sana kwa sababu ya maendeleo ya haraka yaliyochukua muda mfupi na kwa kuwa Waafrika hawakutumiwa kuyatekeleza maendeleo hayo. Jambo muhimu lililosababisha masikitiko ni kule kutumika shuleni kwa vitabu vilivyotafsiriwa vibaya vikiwa na ithibati ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Matumizi ya semi na miundo ya Kiingereza katika vitabu hivyo vilivyotafsiriwa neno kwa neno hayakukanushwa na Broomfield kama nilivyotaja. Baadhi ya wanakamati pia waliyapigia makelele matumizi hayo.
Alipokuwa akiandika kuhusu siku hizo za mwanzo wa usanifishaji wa Kiswahili, Snoxall anatukumbusha kwamba kulikuwa na vitabu vichache sana na kwamba kamati ilitegemea sana tafsiri za Kiingereza zilizokuwa zikitafsiriwa na wanakamati wenyewe. Vitabu vya waandishi kama vile Rivers-Smith, Mkurugenzi wa Elimu Tanganyika, vilifaa sana. Snoxall anasema kwamba baadhi ya tafsiri hizo zilikuwa za neno kwa neno na anashangaa iwapo wanafunzi walizielewa. (Snoxall 1982: 3) . Sehemu iliyonakiliwa inagusia mkutano wa Mombasa wa 1928. Mfano mmoja ambao Snoxall anaukumbuka sana kutoka kitabu cha Uraia ambacho kilikuwa tafsiri ya A Manual of Citizenship na Rivers-Smith ni: “Watu wa Taifa hilo wamekwisha panda kipawa kingine katika ngazi ya ustaarabu”. Wanafunzi walitaka kujua ni nini “Ngazi ya ustaarabu” na ilikuwa wapi?
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)