UTAMADUNI wa wanajamii fulani huelekeza kwa kiasi kikubwa jinsi lugha inavyotumiwa na jamii husika.
Waama, lugha na utamaduni wa watu ni vitu viwili changamano mno ambavyo haviwezi kutenganishwa kwa urahisi. Uvurugaji wa utamaduni wa watu utamaanisha uvurugaji wa lugha yao vilevile. Utamaduni hutuwezesha kufahamuni kwa kiasi gani kaida, maadili na kanuni zinavyoelekeza namna lugha inavyopaswa kutumiwa na kusarifiwa katika jamii ili kudhihirisha umilisi wkimawasiliano.
Tasfida
Utamaduni huo unaweza kuwaasa wanajamii wasiyatumie maneno au msamiati ambao unachukuliwa kuwa mwiko katika jamii. Mathalani, katika takriban jamii zote za Kiafrika, kunao msemo wa adabu unaopaswa kutumiwa kuonyesha kitendo cha mama mjamzito kujikopoa mwana. Kitendo hicho hutofautiana na kile cha mnyama kuzaa. Waswahili husema kwamba fulani amejifungua wala si kuwa fulani amezaa ilhali jamii ya Wakamba husema, ‘Nimusyai’ wakiwa na maana kuwa mwafulani amekuwa mzazi. Jamii ya Wakikuyu hutumia msemo, ‘Nu1FD9arateithu1FD9kire’ ambao una tafsiri ya ‘amesaidika’. Katika jamii ya Abagusii, msemo unaoafiki maana ya ‘amejifungua’ ni ‘Ogonkirie’ nayo fasiri ya kitenzi, ‘gonkia’ ni kunyonyesha. Jamii ya Waluo hutumia msemo, ‘Okonyore’ ukiwa na maana ileile ya ‘amejifungua’.
Kuisarifu lugha kwa namna hii kutoka jamii moja hadi nyingine ndiko kunakojulikana katika lugha ya Kiswahili kama matumizi ya tasfida. Lugha inapotumia tasfida husemekana kuonyesha hadhi na heshima kwa anayerejelewa au kinachorejelewa katika mazingira mahususi. Vinginevyo, tasfida inapopuuzwa, husemekana kwamba lugha imekiuka kaida na kanuni muhimu zinazotakikana kuwepo ili kufikia umilisi wa kimawasiliano (communicative competence).
Hivyo basi, katika muktadha huo, lugha husemekana kuchukiza au ‘kuchafua roho’. Matumizi ya msamiati mwingine huenda yasilenge kuondoa udhia au chukizo kwa kinachorejelewa lakini hudhamiriwa tu kuonyesha huruma au ugeuzi-nafsi (empathy) kwa warejelewa. Hebu tuchukue mfano wa msamiati ‘marehemu’. Katika lugha ya Kiswahili, msamiati huu hutangulizwa katika usemi pale ambapo mzungumzaji anamwomba Mungu amwonee huruma yeyote aliyeaga dunia kabla ya kulitaja jina lake. Vivyo hivyo, jamii tofauti huwa na msamiati tofauti wa kuwarejelea wote wanaohitaji kuhurumiwa au kuonewa huruma na jamii husika. Kwa mfano, jamii ya Abagusii hutumia maneno, ‘Chintakana’ na ‘Ababoraka’ kuwarejelea mayatima na wajane katika mtawalia huo. Maneno hayo yanapotumika katika hali hiyo, huvutia hisia za huruma na hata wakati mwingine huwanasihi watu kuwa radhi kuwafaa.
Utamaduni huelekeza matumizi ya lugha
Utamaduni huelekeza namna jinsia au rika fulani linavyotarajiwa kuitumia lugha na kwa kiasi fulani ishara ambazo rika hilo au jinsia hiyo inapaswa kuziambatanisha na ujumbe unaowasilishwa. Kwa mfano, katika jamii fulani, inatarajiwa kuwa msichana anapoongea na mwanamume, anapaswa kuonyesha haya usoni, kutazamatazama chini na kuchora ardhini kwa vidole vya miguu au kuyapura majani ya mmea ama kuumauma kucha za vyanda vyake vya mikono. Kwa upande mwingine, watoto hawapaswi kuwakata kalima watu wazima wanapoongea au hata kuwajibiza moja kwa moja. Mwanamke naye hana uhuru wa kusema mbele ya mume wake hadi pale atakapopewa idhini na mumewe kufanya hivyo. Vivyo hivyo, katika jamii nyingi za Kiafrika, anayetarajiwa kumshawishi mwanamke au msichana, ni mwanamume au mvulana na wala si kinyume chake.
Udhaifu
Katika jamii hizo, huchukuliwa kama kitendo cha udhaifu mwanamke au msichana anapokuwa wa kwanza kumshawishi mvulana au mwanamume.
Utamaduni huonyesha jinsi mahusiano baina ya watu yanavyoweza kuelekeza lugha wanayopaswa kuitumia katika miktadha maalum. Mathalani, wakazawana wanatarajiwa kujichukulia kwa namna fulani wanapozungumza na wakwe zao. Kwa upande mwingine, watani huwa na uhuru mwingi wa kuitumia lugha kwa namna wapendavyo. Baadhi ya msamiati na misemo ambayo haitumiki aghalabu au imepigwa marufuku kwa sababu ya kuchukuliwa kama mwiko, huja wakati ikatokomea kabisa kutoka katika jamii husika. Lugha na utamaduni wa watu ni kama kinu na mchi.