MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
(MTAGUSANO) NA MBINU ZA KIFANI KATIKA RIWAYA YA MZINGILE YA E.KEZILAHABI (1991)

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
(MTAGUSANO) NA MBINU ZA KIFANI KATIKA RIWAYA YA MZINGILE YA E.KEZILAHABI (1991)
#1
Riwaya ya Mzingile ni riwaya ya kifalsafa iliyojikita katika swali “nini maana ya maisha Katika kujibu swali hili mwandishi amemtumia Kakulu aliyezaliwa katika mazingira ya ajabu kwa kumchora kama neema kwa maana ya kuona kama mkombozi kwa kutatua matatizo ya njaa na magonjwa.

Hata hivyo Kakuru anapoteza maana baada ya watu kuanza kumpinga hivyo anakimbilia mlimani. Pia kwa kutumia swali nini maana ya maisha mwandishi anamlika taasisi za dini ambazo kimsingi ndio mhimili wa maadili zinaposhindwa kudhibitisha hilo kwa viongozi wa dini (mashekhe na mapadri) wanavyokiuka maadili. Kwa kutumia swali hilohilo pia mwandishi anaainisha matatizo yanayotokana na uongozi mbaya unaofanywa na viongozi wabadhilifu na wasiojali  maslahi ya wengi, japo wananchi waliwaamini kwa kuwapa fursa  hiyo kuongoza.Mwandishi amemaliza kwa kueleza kuwa jamii mpya iliyokuwa na unyanyasaji, utabaka na vitu vingine visivyofaa inawezekana pale watu wanapoamua kuungana na kufanya mambo kwa kuelewana na ndio mwanzo hasa wa amani katika jamii.

Tunayaona haya pale kichaa na mwanmke walipoungana pamoja na kujenga jamii mpya isiyokuwa na ubaguzi, unyanyasaji na utabaka. Kwa kifupi riwaya hii inadodosa maana ya maisha ambapo mwandishi anasema maisha ni kama mkufu unaochukua kipande hiki na kile unaviunganisha, kipande kimoja kikikatika unakiacha unachukua kingine kinachokufaa wewe hicho kitamfaa mwingine, siku ya kufa kila mtu atavikwa mkufu wake.
 Mwendo wa riwaya;
Hurejelea suala zima la kasi, mtiririko na mshindilio wa vitushi vya riwaya kwa kuzingatia vigezo vya msuko, maudhui, masafa ya kiwakati na kijografia. Mwendo wa riwaya hii ya “Mzingile” ni mwendo wa taratibu kutokana na kuwa na maudhui yaliyojaa utanzia mwingi,  masafa ya kijiografia  na yale ya kiwakati, yamebainishwa wazi pia kunamshindilio mkubwa wa vitushi. Maudhui ya riwaya hii ni ya kitanzia.

Kwa mfano, msimulizi amekumbwa na matatizo na migogoro mbalimbali katika harakati za safari zake za kumtafuta mzee. Msimuliaji anasema “Giza lilipoingia sikuweza kuziona nyayo tena. Kwa kuogopa kupotea njia nilikata shauri kutafuta mahali pazuri pa kulala. Nilivua shati nikafunikia uso wangu ili mchanga usiingie machoni mwangu. Niliota. Niliota mtu akinisemesha. Mtu aliyekuwa akizungumza nami alikuwa amefunikwa na hali ya mawingumawingu au labda ukungu. Sura yake sikuweza kuitambua.Alinitazama bila kusema neno kwa muda. Nilijaribu
kuinua kichwa lakini kilikuwa kizito. Nilitaka kupiga kelele lakini kinywa kilikataa kufunguka na ulimi ulikuwa mkavu” (uk 9-10) Masafa ya kijiografia yamebainishwa wazi kama vile kijijini kwa mfano “Siku ambayo mama yake aliumwa uchungu, aliitwa mkunga mashuhuri kijijini kuja kumhudumia” (uk1), msituni, kwa mfano “Yasemekana Kakulu alipojiona mzee aliwateua wazee watano, mmoja kila kijiji akaenda nao msituni” mlimani (uk
11).

Masafa ya kiwakati nayo pia yamebainishwa wazi ili kumpa msomaji nafasi ya kujua kile msimuliaji amekikusudia kwa mfano mwandishi anasema “Ilikuwa jioni kama saa kumi nilipoamka. Macho yalikuwa mazito. Katika jitihada ya kutaka kuona niliona mwanamke amesimama karibu name akinitazama” (UK 9). Masafa ya kiwakati yameonekana pia katika (uk 4, 13, 44).
Naratolojia;
Ni taaluma inayohusu suala la usimulizi katika kazi za kiuandishi. Katika taaluma hii ya usimuliaji, kuna masuala mbalimbali yanayojitokeza kama matumizi ya nafsi, suala la wakati na mwendo wa kazi husika. Katika riwaya hii ya “Mzingile” mwandishi ametumia usimulizi shahidi na usimulizi maizi. Usimulizi shahidi umejitokeza ambapo pana matumizi ya nafsi ya kwanza. Mfano, “Safari yangu ilianza asubuhi na mapema wakati ambapo fikra zilikuwa bado kuchoka. Sikujua nielekee upande gani maana hakuna aliyejua kwa hakika mahali alipoishi. Nilifuata silka zangu” (UK 7) pia usimulizi huu umeruhusu kupenyeza matumizi ya nafsi ya pili, katika ukurasa wa pili kunamatumizi ya nafsi ya pili kwa mfano,“Na ninyi mnatafuta umbea! Ondokeni hapa! ” (uk 2).
Usimulizi maizi pia umetumika pale mwandishi alipotumia nafsi ya tatu kwa mfano “Wazee walikumbuka kuwa alipenda sana ubuyu, walianza kutoa sadaka chini ya mibuyu….” (uk 4)
Mtagusano
Ni athari au mwingiliano wa vipengele mbalimbali katika kazi za fasihi, kwa kawaida hii inahusishwa na mwigo au uathiriano wa kazi moja na nyingine. Vipengele hivyo vyaweza kuwa usawiri wa wahusika, lugha, mandhari, na maudhui. Vifuatavyo ni vipengele vya mtagusano kama vilivyojitokeza katika Riwaya ya “Mzingilie”
Usawiri wa wahusika. Usawiri wa wahusika, ni kitendo cha kuwachora, kuwafafanua, kuwatambulisha na kuwajenga wahusika huku wakipewa maneno, matendo, hadhi na uwezo unaolandana na unaowiana. Mwandishi amesawiri wahusika kwa namna ifuatayo;
Mbinu ya mtunzi kumwelezea mhusika, hii ni mbinu ambayo mtunzi huitumia kumwelezea mhusika juu ya matendo yake, mienendo na tabia za mhusika. Kwa mfano, katika riwaya ya “Mzingile” mtunzi amemwelezea Kakulu kama ifuatavyo; “Kakulu alitunza vizuri migomba iliyoachwa na mama yake, alilima viazi na mahindi, akaishi kwa kujitegemea. Alizoea kuwatembelea majirani zake asubuhi na mapema akimung’unya ubuyu…..”(UK 2). Mbinu ya uzungumzaji nafsi, hii ni mbinu ambayo mhusika huzungumza na nafsi yake mwenyewe. Katika riwaya hii ya “Mzingile” mbinu hii imetumika pale Mhusika Kichaa anazungumza na nafsi yake “Ninataka kuwa kichaa!”. Kwa sauti yenye kutisha nilipiga kelele, “Ninaweza kuuwa mtu nikamla mzimamzima!” (UK
20).
Mbinu ya kuzungumza na hadhira, mbinu hii inatumika ambapo mwandishi humchora mhusika akizungumza na hadhira, hadhira huweza kumfahamu mhusika kupitia mazungumzo yake mwandishi ametumia mbinu hii ambapo mhusika Kakulu amezungumza na hadhira kwa mfano mwandishi anasema “…akawakaripia wanaume waliokuwa karibu, ondokeni hapa! Mnachuguliachungulia nini? Hampashwi kuona mwanzo wangu na njia niliyoijia!” (uk 1) pia Kakulu anazungumza na wanawake waliokuwa karibu naye “Na ninyi mnatafuta umbea! Ondokeni hapa! ” (UK 2) Mbinu ya mhusika kuwafafanua wahusika wengine, kwa mfano sehemu ya sita mwandishi amewachora baadhi ya wahusika wakiwazungumzia wahusika wenzao na matendo yao kwa mfano maongezi ya msimulizi na kijana, mfuga mijusi
“Ulimwona?”
“Nani?”
“Mzee”
“Unamjua!”
“Alipita hapa na blanketi lake akiwa amejiharishia. Amezeeka sana
sasa.Alitembea kwa kuyumbayumba kama aliye ndotoni”. (Uk 56)
Mbinu ya majazi, hii ni mbinu ya kuwapa wahusika majina kulingana na sifa zao, tabia au dhima anazotakiwa kupewa. Katika riwaya ya “Mzigile” jina la mhusika Kakulu alipewa kulingna na sifa yake ya kuzaliwa akiwa na uwezo wa kufanya matendo yanayopashwa kufanywa na watu wenye umri mkubwa. Kwa mfano
mwandishi anasimulia “Wanakijiji walimpa jina la Kakulu kwa sababu alizaliwa akiwa na ndevu tayari-Kakulu, kakubwa, kazee” (UK 1)
Mandhari Mandhari iliyotumika ni kama vile; kijijini kwa mfano, “Siku ambayo mama yake aliumwa uchungu, aliitwa mkunga mashuhuri kijijini kuja kumhudumia” (UK 1), mandhari ya msituni uk 4 “Yasemekana Kakulu alipojiona mzee aliwateua wazee watano, mmoja kila kijiji akaenda nao msituni” mlimani uk 11, majini uk, baharini uk… Matumizi ya lugha Ametumia lugha ngumu iliyojaa picha Kwa mfano, ametumia mizinga, nyuki na asali. Mzinga ni nchi, asali ni rasilimali na nyuki ni wananchi (UK 77), kundi la mijsi kubadilika kuwa ng’ombe (UK 55) ni sawa na viongozi wasiowaadilifu kujigeuza na kuonekana kama wanatenda wema kwa wananchi wao, pia ametumia mbinu ya safari ndefu yenye mahangaiko kuwakilisha hali halisi ya maisha ya binadamu na misukosuko waipatayo binadamu Ametumia semi mbalimbali kama vile methali na misemo kwa mfano ametumia methali kama vile “Asiyesikia la mkuu huvujika guu! Ulimwengu huu haukusikia la mkuu” (uk 2), ametumia pia misemo kama vile “mkubwa haibi, anachukua” msanii anasema “Wazee wakaanza kugawana kile kidogo kilichokuwepo. Msemo ukawa mkubwa haibi, anachukua” (uk2), Ametumia tamathali za semi mbalimbali kama vile sitiari, tashibiha, nk kwa mfano, ametumia tashibiha pale aliposema “Maisha ni kama mkufu” (UK 7),”Hata hivyo watu walikufa kama panya” (UK 54), Ametumia pia tashihisi pale mwandishi anasema “Nitakupeleka,”pundamilia alisema (UK 83) Maumizi ya mbinu nyingine za kisanaa kama vile; nidaa (UK 23) Matumizi ya Mbaalaga, kwa mfano mwandishi anasema “Ikafikia hatua ya binadamu kumla binadamu mwenzake” (UK 54) Matumizi ya kejeli, kwa mfano “Kawaimbieni nyimbo hizo wake zenu” (UK 53) Matumizi ya lugha changamani kwa mfano, ametumia maneno ya lugha ya kiingereza kama vile, “Beyond reasonable doubt” (UK 41), well done (UK 47), once more (UK 56)

Mianzo na miisho ya riwaya
Hii ni namna riwaya zinavyofunguliwa au kusanwa na kumalizia. Riwaya inaweza kuanza na taharuki, maswali/kiu au wakati mwingine simulizi. Riwaya ya “Mzingile” sehemu ya kwanza imeanza na simulizi juu ya maisha ya Kakulu na kuzaliwa kwake kimaajabu. Kwa mfano msanii anasema “WALIMWITA Kakulu. Sasa bado tunamwita Kakulu na wajao watamwita hivyohivyo. Ukweli wake ulizingirwa na ukungu wa kisasili. Hakuna mtu aliyewajua barabara wazazi wake. Kuwako kwake kulianza kama mzaha.yasemekana kuzaliwa kwake kulikuwa kwa ajabu”(UK 1) Riwaya hii pia imeishia na hali ya taharuki.

Mtindo katika riwaya ya Mzingile
Ameigawa kazi yake katika sehemu mbalimbali kama vile sehemu ya kwanza (UK1-UK 5), sehemu ya pili(UK6-) sehemu ya tatu sehemu ya nne sehemu ya tano sehemu ya sita  sehemu ya saba Matumizi ya nyimbo kwa mfano katika ukurasa wa 33,na 78. Ambapo kuna matumizi ya wimbo.
“Ninaimba juu ya giza liligubika ulimwengu.
Tumetembea katika msitu wa kurasa potovu
Na kutafuna kila neon na kila aina ya wino.
Tumemeza yapashwayo  kunywewa
Na kucheua yatakiwayo kumezwa.” (UK 33)
Pia ametumia muziki ili kuihaisha kazi yake kwa mfano uk 46 mwandishi anasema “Saa mbili kamili mambo yalianza. Pazia tu lilipoinuliwa tu vifijo vilianza kusikika sehemu ya nyuma. Muziki wa kuingilia uliwekwa. Msichana wa kwanza aliinigia akicheza kwa mwendo wa haraka haraka uliodhihirisha uhai wake…” UK 46 Matumizi ya dayolojia kwa mfano sehemu ya sita (uk 51) kuna mazungumzo ya msimulizi na watoto waliokuwa wanawinda
“Mnakaa peke yenu?”
“Hapana. Yupo kaka”
Kijiji chenu kikubwa? Walitazamana na sikupata jibu
“Kuna kanisa? Niliendelea”
“Kaka ametukataza tusiseme mengi kwa wageni” (UK 51) Matumizi ya barua kwa mfano (uk 64 na 65) mwandishi anasema , juu ya sehemu hii nyeusi maandishi hafifu yaliweza kuonekana. Niliposogea karibu niliweza kuyasoma: “Kwa mtakaosalia. Msifanye makosa tuliyofanya sisi. Tulifunzwa hatukufunzika. Hatukuweza kuongoza mkondo wa sayansi na uchumi, siasa iliposhika hatamu…….”(UK 64) Matumizi ya nafsi zote tatu kwa mfano Pia mwandishi amechanganya lugha ya kiswahili sanifu na maneno ya  lugha za kikabila kama vile neno Kakulu pia maneno ya lugha za kigeni kama vile kiingereza na kilatini kwa mfano, “ Beyond reasonable doubt” (UK 41),  well done (UK 47), once more (UK 56)

UBUNILIZI KATIKA RIWAYA YA MZINGILE 
Ubunilizi ni neno linalotokana na neno buni lenye maana ya kutengeneza kitu kwa mara ya kwanza, gundua, zua au tunga jambo (Kamusi ya Kiswahil Sanifu:34).Hivyo basi fasihi si kazi inayohusu mambo ya kipekee bali ni uwasilishaji wa maisha ya jamii kwa njia bunifu isiyo ya moja kwa moja. Mbinu za kibunilizi zilizotumika katika Riwaya ya “Mzingile” ni kama zifuatazo;

Ufumbaji ni utumiaji wa kauli zenye maana fiche katika kazi ya fasihi. Kauli hizo huwa na maana kinyume na kazi zinazohusika. Katika kazi za fasihi ufumbaji hutumiwa kwa malengo tofautitofauti kama vile; kukwepa mkono wa dola, kuepuka kugusa hisia za wahusika moja kwa moja na pia kuwapa wasomaji nafasi ya kuwafikirisha. Katika riwaya hii ufumbaji umejitokeza katika sehemu mbalimbali. Kwa mfano, ametumia mizinga nyuki na asali (UK 77). Mzinga ni nchi, asali ni rasilimali na nyuki ni wananchi, kundi la mijsi kubadilika kuwa ng’ombe (UK55) ni sawa na viongozi wasiowaadilifu kujigeuza na kuonekana kama wanatenda wema kwa wananchi wao, pia ametumia mbinu ya safari ndefu yenye mahangaiko kuwakilisha hali halisi ya maisha ya binadamu na misukosuko waipatayo binadamu.

Usawiri wa wahusika, ni kitendo cha kuwachora, kuwafafanua,
kuwatambulisha na kuwajenga wahusika huku wakipewa maneno, matendo, hadhi na uwezo unaolandana na unaowiana. Mwandishi amesawiri wahusika kwa namna ifuatayo; Mbinu ya mtunzi kumwelezea mhusika, hii ni mbinu ambayo mtunzi huitumia kumwelezea mhusika juu ya matendo yake, mienendo na tabia za mhusika. Kwa mfano, katika riwaya ya “Mzingile” mtunzi amemwelezea Kakulu kama ifuatavyo; “…Kakulu alitunza vizuri migomba iliyoachwa na mama yake, alilima viazi na mahindi, akaishi kwa kujitegemea. Alizoea kuwatembelea majirani zake asubuhi na mapema akimung’unya ubuyu…..”(UK 2).

Mbinu ya uzungumzaji nafsi, hii ni mbinu ambayo mhusika huzungumza na nafsi yake mwenyewe. Katika riwaya hii ya “Mzingile” mbinu hii imetumika pale Mhusika Kichaa anazungumza na nafsi yake “Ninataka kuwa kichaa!”. Kwa sauti yenye kutisha nilipiga kelele, “Ninaweza kuuwa mtu nikamla mzimamzima!” (UK
20).

Mbinu ya kuzungumza na hadhira, mbinu hii inatumika ambapo mwandishi humchora mhusika akizungumza na hadhira, hadhira huweza kumfahamu mhusika kupitia mazungumzo yake mwandishi ametumia mbinu hii ambapo mhusika Kakulu amezungumza na hadhira kwa mfano mwandishi anasema “…akawakaripia wanaume waliokuwa karibu, ondokeni hapa! Mnachuguliachungulia nini? Hampashwi kuona mwanzo wangu na njia niliyoijia!” (uk 1) pia Kakulu anazungumza na wanawake waliokuwa karibu naye “Na ninyi mnatafuta umbea! Ondokeni hapa! ” (UK 2)

Mbinu ya mhusika kuwafafanua wahusika wengine, kwa mfano sehemu ya sita mwandishi amewachora baadhi ya wahusika wakiwazungumzia wahusika wenzao na matendo yao kwa mfano maongezi ya msimulizi na kijana, mfuga mijusi
“Ulimwona?”
“Nani?”
“Mzee”
“Unanjua!”
“Alipita hapa na blanketi lake akiwa amejiharishia. Amezeeka sana
sasa.Alitembea kwa kuyumbayumba kama aliye ndotoni”. (Uk 56)
Mbinu ya majazi, hii ni mbinu ya kuwapa wahusika majina kulingana na sifa zao, tabia au dhima anazotakiwa kupewa. Katika riwaya ya “Mzigile” jina la mhusika Kakulu alipewa kulingna na sifa yake ya kuzaliwa akiwa na uwezo wa kufanya matendo yanayopashwa kufanywa na watu wenye umri mkubwa. Kwa mfano
mwandishi anasimulia “Wanakijiji walimpa jina la Kakulu kwa sababu alizaliwa akiwa na ndevu tayari-Kakulu, kakubwa, kazee” (UK 1)

Mbinu ya utanzia, ni mbinu ambayo mtunzi hutumia vipengele
mbalimbali vizuavyo huzuni, jitimai, masononeko, masikitiko na mateso kwa hadhira yake. Kipengele hiki ni kinyume na ufutuhi, katika riwaya hii ya Mzingile mwandishi ametumia utanzia kama ifuatavyo; mateso, kifungo, vifo, ugumu wa maisha, magonjwa njaa, ukame na mahangaiko kwa ujumla. Kwa mfano, mwandishi anasimulia jinsi mwanamke wa kiafrika alivyokamatwa, akafungwa jela, akauwawa na pia kunajisiwa. Msanii anasema “Walimfunga, wakampeleka chumbani kwa meneja. Baada ya kumpiga viboko walimfungua. Alianza tena kupigana nao. Walimuua akipigana. Walimnajisi huku akiwa amekufa” (Uk 50), ameongelea pia suala la ukame uliosababisha watu, mimea wanyama na wadudu kufa na kupotea kwa sababu ya ukame uliokikumba kijiji baada ya msimulizi kwenda safari ya kumtafuta mzee msanii anasema “Ukame ukaanza tena, ukaweka chachu ya dhuluma. Wao wakiuana, wanyonge wakifa njaa. Ukame ukaongeza ukakasi. Vifo vikazidi kuongezeka” (uk 51-55).
Mbinu ya ufutuhi, ni mbinu ambayo msanii hutumia ucheshi au furaha kwa hadhira yake.Hii ni kinyume na tanzia. Katika riwaya ya “Mzingile” mwandishi anaonesha ufutuhi pale anaposimulia vituko vya Kakulu aliyekuwa na tabia ya kuwaingilia mapadri, masisita, mashehe kwenye baibui na kanzu zao. Kwa mfano, msanii anasema “Alikuwa mtani wa kila mtu. Mapadri wa siku hizo, masista, wavaa baibui na mashehe walikaogopa, maana kalizoea kufunua makanzu
yao na kuingia miguuni mwao. Ilikuwa vigumu kukaondoa humo. Utawasikia wakipigapiga makanzu yao kama kwamba wanatoa vumbi, We Kakulu acha kufanya hivyo!”. Kalichowafanyia wao wenyewe walijua (UK 3) Pia wenye mabinti walimtania Kakulu awapelekee maji na kuni ili wampatie binti wa kuoa, kwa mfano masnii anasema “Kwa hiyo wenye mabinti wakawa wanakatania. Ukinitafutia kuni nitakupa binti uoe. Jioni hiyo utamwona Kakulu anapeleka mzigo wa kuni uliomzidi kimo” (uk 3) pia Kakulu kumtia mimba mwari kimzaha (uk 3)

Mbinu ya taharuki, taharuki ni matarajio ambapo tunahamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye Wamitila (2003), hivyo basi, ni hali ya kuwa na dukuduku la kutaka kujua juu ya nini kitafuatia katika usimulizi wa kazi za fasihi, mtunzi huijengea hamu hadhira yake ya kutaka kujua zaidi.Mbinu hii imeoneshwa katika’’ Riwaya ya “Mzingile” pale  mwandishi amekatakata matukio kwa kurukia tukio jingine kwa mfano tukio ……….., kaanza na tukio tokeo (uk 1) na baadae tukio chanzi uk……, msanii ameanza kwa kusema “WALIMWITA Kakulu. Sasa bado tunamwita Kakulu na wajao watamwita hivyohivyo.” Pia anwani yenyewe Mzingile imejengwa kitaharuki kwani pale msomaji aonapo anwani hii atakuwa na shauku ya kuisoma ili apate kujua maana halisi ya anwani hii.

Utomeleaji, ni kuingiza baadhi ya kaida za kazi fulani
kwenye kazi nyingine. Tunatomelea ili kuipa uhai kazi ya fasihi na kuifanya hadhira ijione kuwa ni sehemu ya kazi hiyo au kazi husika. Katika riwaya hii ya Mzingile utomeleaji umejitokeza katika ukurasa wa 33,na 78. Ambapo kuna matumizi ya wimbo.
“Ninaimba juu ya giza liligubika ulimwengu.
Tumetembea katika msitu wa kurasa potovu
Na kutafuna kila neon na kila aina ya wino.
Tumemeza yapashwayo kunywewa
Na kucheua yatakiwayo kumezwa.” (UK 33)
Pia ametumia muziki ili kuihaisha kazi yake kwa mfano uk 46 mwandishi anasema “Saa mbili kamili mambo yalianza. Pazia tu lilipoinuliwa tu vifijo vilianza kusikika sehemu ya nyuma. Muziki wa kuingilia uliwekwa. Msichana wa kwanza aliinigia akicheza kwa mwendo wa haraka haraka uliodhihirisha uhai wake…”
UK 46

Mbinu ya ritifaa, ni mbinu ambayo mtunzi huwasilisha mambo kwa kuwaonesha wahusika wake wakiwasiliana na mtu aliyembali (umbali wa kijiografia au aliyefariki).mfano katika riwaya ya Mzingile
mwandishi amemuonesha.

Dayolojia, hii ni mbinu ya kutumia kauli za kiusemezano kwa lengo la kufikisha ujumbe uliokusudiwa. Mtunzi hutumia vinywa vya wahusika ili kufikisha ujumbe. Katika riwaya ya Mzingile mbinu hii imetumika kama njia ya kuonyesha ufundi wa mtunzi kuweza kusawiri wahusika na hadhi zao pia imesaidia kuwasilisha mawazo kwa hali ya uasilia kwa sababu wahusika wenyewe wamwtamka maneno kwa vinywa vyao wenyewe. Katika riwaya ya Mzingile kuna mazungumzo ya wahusika mbalimbali kwa mfano kuna mazungumzo kati ya msimulizi ma mzee (uk  14)
       “Nimetumwa kuja kukuona”
      “Mimi”
       “Ndio. Wewe”
       “Kuhusu”
  “Kifo cha mwanao. Nimekuja kukujulisha kuwa mwanao ameuawa”
Mbinu ya ujadi, ni utumiaji wa kauli za asili, kauli zinazofungamana sana na jamii inayoandikiwa.Hutumika zaidi ili mwandishi aweze kujipambanua kuwa naye ni sehemu ya jamii ile. Kauli hii hujumuisha methali, nahau, misemo na vipengele vinginevyo vya kimazungumzo, mfano katika Riwaya ya Mzingile ametumia methali kama vile “Asiyesikia la mkuu huvujika guu! Ulimwengu huu haukusikia la mkuu” (uk 2), ametumia pia misemo kama vile “mkubwa haibi, anachukua” msanii anasema “Wazee wakaanza kugawana kile kidogo kilichokuwepo. Msemo ukawa mkubwa haibi, anachukua” (uk2), pia ametumia maneno ya kijadi
kama  vile jina la Kakulu ni la kijadi likiwa na maana ya kakubwa, kazee kalikokomaa. Matumizi ya usihiri pia yandhihirisha  ujadi katika jamii, kwa mfano tukio la mijusi kugeuka kuwa ng’ombe (uk 55). Hivyo basi kupitia mbinu hii ya ujadi hadhira hujiona iko karibu sana na kazi husika waonapo baadhi ya vipengele vya usimulizi wa kijadi wavitumiavyo katika jamii zao vimetumika katika kazi husika

Mbinu ya kisengerenyuma, ni namna ya usimuliaji ambao huanza na tukio- tokeo kisha hufuatia tukiochanzi, mbinu hii mtunzi huelezea kitu na baadae asili au mwanzo wa kitu kile.Mbinu hii imeneshwa pia katika Riwaya ya “Mzingile’’ kuanzia (uk1) anazungumzia habari ya Kakulu kuitwa Kakulu na watu wa kale, waliopo wanamwita kakulu na wajao pia watamwita Kakulu. Kwa mfano mwandishi anasema “WALIMWITA Kakulu. Sasa bado tunamwita Kakulu na wajao watamwita hivyihivyo.” Halafu baadae akasimulia kisa cha Kakulu kuitwa Kakulu

Msuko wa vitushi katika riwaya ya Mzingile
hiki ni kipengele kingine kilichotumiwa na waandishi katika kuwapa wasomaji hamasa ya kuendelea kusoma kazi ya fasihi unajumuisha mambo kama vile muwala na motifu mbalimbali. Mfano, katika Riwaya ya Mzingile
Muwala
Katika riwaya ya mzingile kuna mwendelezano wa vitushi katika kila sehemu, vitushi hivyo vinajengana kiasi cha kuleta mwendelezo wa matukio katika usimulizi. Kwa mfano katika sehemu ya pili kuna vitushi viwili, kitushi cha kwanza kinahusu kifo kilichompelekea msimulizi kuanzisha safari ndefu ya kumtafuta mzee aliyeishi sehemu za mbali, msimulizi anasema “Safari yangu ilianza asubuhi na mapema wakati ambapo fikra zilikuwa bado kuchoka. Sikujua nielekee upande gani mana hakuna aliyejua kwa hakika mahali alipoishi” (uk7) pia kisa cha mzee kuishi mafichoni kimejitokeza katika sehemu hii ya pili (uk 16) kwa mfano mwandishi anasimulia “Kwa kuwa nilikuwa na tuhuma ya kusalitiwa nilijenga nyumba hii ili kujikinga na ghadhabu ya wale ambao wangependa kujilipiza kisasi wakati nimeishiwa nguvu……..Ndiyo maana niko hapa mafichoni” (uk 16) Sehemu ya saba inakamilisha safari yamsimulizi aliyekuwa anapeleka taarifa ya kifo kwa Mzee. Mtirirko wa matukio au vitishi umeleta ujumbe unaoeleweka kwa wasomaji.

Motifu
Motifu ya safari, mwandishi ametumia motifu ya safari kuanziz
sehemu ya pili mpaka sehemu ya saba. Kwa mfano uk 7 msimulizi alianza safari ndefu ya kumtafutaKakulu msanii anasema “Safari yangu ilianza asubuhi na mapema wakati ambapo fikra zilikuwa bado kuchoka. Sikujua nielekee upande gani mana hakuna aliyejua kwa hakika mahali alipoishi” (uk7)

Motifu ya ndoto, mwandishi ametumia motifu hii ya ndoto katika
(uk 9-10) ambapo mwandishi anasema “Giza lilipoingia sikuweza kuziona nyayo tena. Kwa kuogopa kupotea njia nilikata shauri kutafuta mahali pazuri pa kulala. Nilivua shati nikafunikia uso wangu ili mchanga usiingie machoni mwangu. Niliota. Niliota mtu akinisemesha. Mtu aliyekuwa akizungumza name alikuwa amefunikwa na hali ya mawingumawingu au labda ukungu. Sura yake sikuweza kuitambua.Alinitazama bila kusema neon kwa muda. Nilijaribu kuinua kichwa lakini kilikuwa kizito. Nilitaka kupiga kelele lakini kinywa kilikataa kufunguka na ulimi ulikuwa mkavu” (uk 9-10)

Motifu ya majini, msanii ametumia motifu hii katika (uk 8-11) kwa mfano msanii anasema “Nilipotoka majini nilijisugua mwili mzima hadi mapafu yalipohitaji hewa tena. Nilijitumbukiza tena majini, nikaondoa uchafu uliokuwa umekokomolewa na mchanga” (uk 8)
MAREJELEO
Kezilahabi, E (2011), Mzingile, Toleo la tatu: Dar es Salaam University Press: Dar es salaam Tuki (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.

Wamitila, K. (2003); Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd, Nairobi
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)