08-27-2021, 03:03 PM
Taswira ya Mwanamke katika Riwaya ya Kezilahabi (1971) Rosa Mistika
Mwandishi Kezilahabi katika riwaya yake ya Rosa Mistika anamtumia Rosa kama mhusika mkuu wa riwaya yake. Ukuu wake umezawadiwa kwa kubeba jina la riwaya husika. Rosa katika riwaya hiyo anaoneshwa kuwa alizaliwa na kukulia kwenye mazingira ya kunyanyaswa na baba yake, mzee Zakaria. Aidha, mwandishi anasawiri maisha ya Rosa alipokuwa anasomo shule ya sekondari na pia alipokuwa katika Chuo cha Ualimu. Mwandishi ametuonesha katika kazi yake hii, jinsi Rosa alivyobahatika kwa mafanikio makubwa kuhitimu mafunzo yake ya ualimu na kuajiriwa kama mwalimu. Mwisho mwandishi anamsawiri Rosa katika picha ya kusikitisha. Kwa ujumla, kwa kumpitia Kezilahabi, tunamwona mwanamke akisawiriwa katika taswira zifuatazo:
Taswira ya Unyanyaswaji wa Wanawake
Tunaposema taswira ya unyanyaswaji, tunamaanisha kwamba, mwanamke anafanyiwa vitendo au mambo ya dharau na dhuluma kwa kunyimwa haki zake za msingi. Taswira hii inajitokeza kwa kiasi kikubwa kwenye riwaya hii, ambapo tumemwona Rosa akinyanyaswa na baba yake mzazi mzee Zakaria. Mzee huyu alimnyanyasa binti huyu kwa kumpiga kila mara. Manyanyaso haya ya binti kuitwa na kupigwa yanaoneshwa na mwandishi:
…..Zakaria alichafuka, Rosa aliitwa mara moja, Rosa alikuja hali shuka ikiteremka chini. Kabla hajasema lolote alipigwa na kuanguka chini makofi yalikwenda mfululizo hata damu ikamtoka puani na mdomoni (uk. 6).
Nukuu hii inaonesha na kuthibitisha ukatili wa wazazi wa kiume kwa mabinti zao. Wazazi mithili ya mzee Zakaria huhofia kuwa mabinti zao wataharibika endapo watapewa uhuru usiokuwa na mipaka. Kisa kilichomfanya Zakaria aonekane akimpiga Rosa ni kile kitendo cha kupewa na kupokea fedha na barua toka kwa kijana wa
kiume aitwaye Charles.
kiume aitwaye Charles.
Mwandishi anatuonyesha jinsi unyanyasaji huu unavyoweza kuleta athari kubwa katika malezi na makuzi ya vijana hususan wale wa jinsia ya kike. Hii inampelekea Rosa kujijengea tabia ya kumwogopa baba yake tangu alipokuwa mdogo. Woga huo umeonekana kudumu hadi kuleta mfarakano katika familia ya mzee Zakaria. Ikafikia hatua kwamba, Rosa anaamua kumuasi kabisa baba yake, kama mwandishi anavyothibitisha kwa kuandika:
Kila wakati Unatuchunga. Unafikiri utatuoa wewe. Rosa mwishowe aliyasema haya maneno. Maneno aliyopaswa kusema siku ile aliyopigwa angali msichana. Zakaria aliyapata yote. Zakaria kutunza heshima yake, alifunua mdomo. Maneno fulani yalitoka mdomoni mwake “Rosa, tangu leo wewe si mtoto wangu Tangu leo wewe si baba yangu”Rosa alidakia…. (uk. 58).
Kwa hakika katika nukuu yake hiyo, Rosa anachorwa katika taswira hii ili kuakisi hali halisi ya maisha ya jamii nyingi za Kiafrika, ambapo wazazi wanaamini kwamba, wasichana wanastahili kuchungwa ili kuwaepusha na mitego ya wavulana.
Wazazi wengi kama Zakaria, huwaadhibu kwa kuwapiga na hata kuwanyima uhuru mabinti zao kwa kisingizio kuwa eti wataharibika au kuwa na tabia mbaya. Wazazi hawa wamesahau kuwa malezi haya ni uasi na mfarakano mkubwa miongoni mwao na watoto wao. Wamesahau pia kuwa, malezi yao hayo yatarithiwa na watoto wao wa kiume kutokana na ukweli wa usemi usemao kwamba, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Wazazi wengi kama Zakaria, huwaadhibu kwa kuwapiga na hata kuwanyima uhuru mabinti zao kwa kisingizio kuwa eti wataharibika au kuwa na tabia mbaya. Wazazi hawa wamesahau kuwa malezi haya ni uasi na mfarakano mkubwa miongoni mwao na watoto wao. Wamesahau pia kuwa, malezi yao hayo yatarithiwa na watoto wao wa kiume kutokana na ukweli wa usemi usemao kwamba, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Mwanamke kama Chombo cha Starehe na Biashara
Katika riwaya ya Rosa Mistika, taswira hii inatufungamanisha na ile hali ya umalaya kwa wanawake. Mwandishi amemsawiri mwanamke kuwa ni mpenda starehe na umalaya. Hata hivyo tukiangalia kwa undani suala hili la starehe na umalaya halitendwi na mwanamke peke yake, bali linawashirikisha wanawake na wanaume. Tendo hili linaloshirikisha jinsia zote mbili, zinazopata starehe ya pamoja ingawa linaonekana kwa makusudi kabisa kusukumiwa kwa jinsia ya kike. Kwa hakika hapa panazuka suala la unyanyaswaji wa kijinsia, ya kuwa mwanamke ndiye anayeonwa kumwingia mwanamume. Pia lipo swali la kujiuliza kuwa, ni kwa nini Rosa aliitwa malaya na kupachikwa jina la Laboratory na wanachuo wenzake huko Morogoro ilhali walishiriki tendo hilo na wanaume? Jibu na ufafanuzi wa swali hili ni yale tunayoyaita katika utafiti huu unyanyaswaji wa kijinsia, ambapo mwanamume ndiye anaonekana kuwa mtakatifu siku zote.
Katika riwaya ya Rosa Mistika, Rosa amesawiriwa na mwandishi akiendesha umalaya kuanzia alipokuwa kwenye shule ya sekondari ya Rosary. Rosa alibadilika tabia alipofika kidato cha tatu baada ya
kushawishiwa na rafiki yake Thereza. Hapa mwandishi anatueleza kuwa, mwanzoni Rosa alikataa ushawishi huo wa picha za wavulana toka kwa Thereza. Hata alidiriki kukataa kuongea na wavulana kwa kudhihirisha kuwa alikuwa akiziogopa tabia za wanaume.
kushawishiwa na rafiki yake Thereza. Hapa mwandishi anatueleza kuwa, mwanzoni Rosa alikataa ushawishi huo wa picha za wavulana toka kwa Thereza. Hata alidiriki kukataa kuongea na wavulana kwa kudhihirisha kuwa alikuwa akiziogopa tabia za wanaume.
Hata hivyo alipokuwa kidato cha tatu, ndipo tabia ya Rosa ilipobadilika ghafla, akawa ni wa kwenda kwenye madansi, hata akakutana na mwanamume Deogratias, ambaye alileta mabadiliko makubwa katika tabia ya Rosa. Baada ya hapo, Rosa aliyavamia mapenzi kwa nguvu zote na kwa kipindi kifupi alijipatia wapenzi watano. Rosa anamweleza rafiki yake Theresa kuwa:
Unafahamu, Thereza, siku hizi ninawachezea wavulana kama mtu aendeshaye punda…
(uk. 33).
Taswira hii ya umalaya haikuishia katika ngazi ya sekondari, bali iliendelea hadi Rosa alipojiunga na Chuo cha Ualimu. Rosa anaoneshwa akibadilisha wavulana apendavyo ili mradi anapata fedha. Ndipo vijana walipoamua kumpachika jina la Laboratory kwa maana ya majaribio, kwani kijana yeyote aliweza kufanya jaribio lake la kukutana naye kimwili. Haya yalithibitishwa na mwandishi anapowachora vijana wakiangalia gazetini na Rosa akawasikia wakihojiana kuwa:
……staili hii bado sijaitumiaKwa nini bwana usiende Lab Lab kwenyewe ni wapi? (uk.5). Aidha mwandishi anabainisha kuwa Rosa aligundua kuwa alibandikwa jina la Laboratory yaani nyumba ya kufanyia majaribio. Katika kuthibitisha umalaya wa Rosa, mwandishi anamchora Rosa akivuruga ndoa ya mkuu wa Chuo cha Ualimu, Bwana Thomas. Haya yanaonekana wakati Rosa apoalikwa na mwalimu Thomas amtembelee nyumbani ilihali akijua yule ni mkuu wake wa Chuo. Matokeo ya mwaliko huo ni majuto na kupotea kwa kiungo cha mwili wa Rosa. Mwandishi anatuonyesha jinsi ukahaba huu unavyoleta madhara Rosa asemapo:
…..Rosa alipofika shuleni aliingia upesi chumbani mwake. Alipojiangalia ndani ya kioo hakuweza kuamini! Alilia kwa sauti. Alililia sikio lake. Yule mwanamke alimuuma sikio na kutoa sikio lote la nje (uk 55). Hapa taswira ya umalaya wa Rosa inahusishwa tabia za baadhi wa wanawake, wenye kuvuruga asasi ya ndoa, kwa kuwa kumekuwepo na mifarakano mingi katika ndoa nyingi. Lakini, umalaya huu umesawiriwa upande mmoja tu wa Rosa kuvuruga ndoa ya mwalimu. Upande wa mwalimu kuuvuruga ujana, kumvurugia Rosa elimu na kuuharibu mwili wa Rosa haukuongelewa, kisa ni mwanamke kutumika kama chombo cha kumstarehesha mwanamume. Hii inatuonesha taswira ya uonewaji wa jinsia ya kike na utukuzwaji wa jinsia ya kiume. Mtazamo huu unaenda kinyume na nadharia ya ufeministi inayozingatia usawa baina ya jinsia ya kike na kiume.
Mwanamke katika Taswira ya Ulaghai
Taswira nyingine tunayoipata katika riwaya ya Rosa Mistika ni ile ya Rosa kuonekana mlaghai. Mhusika huyu anachorwa akiwalaghai vijana wengi akiwemo Charles na kujipatia fedha nyingi. Vilevile Rosa ameoneshwa akiwadanganya wazazi wake juu ya matukio kama yale ya kupoteza sikio lake.
Kama vile haitoshi, Rosa anaendelea kumlaghai Charles kuwa yeye ni bikira (hajafanya ngono na mwanamume yeyote) ili waweze kuoana. Ulaghai huu unathibitishwa katika majibizano kati ya Rosa na Charles wakati wakiwa chumbani kama ifuatavyo:
Charles siyo leo, Mpaka siku tutakayooana. Afadhali tungoje siku yenyeweHaiwezekani…. Vumilia kidogo muda umekaribia. Ninakuomba usiniharibu kabla ya muda. Charles — mimi ni bikira (uk. 78).
Ulaghai huu unaofanywa na Rosa una athari kubwa mara inapogundulika kuwa msichana si bikira kama alivyotegemewa na mchumba wake. Kwa tabia kama hii ya ulaghai unaweza kutuletea maswali ambayo yanahitaji maelezo ya kina, Je ni kwa nini mwanamume haonekani mlaghai anapomdanganya mwanamke kuwa atamuoa na asimuoe? Je, ubikira wa mwanamke ndicho kipimo cha yeye kuolewa? Je, kuna uhalali gani kwa mwanamume kukutana kimwili na mwanamke kabla ya kufunga ndoa? Je, ni kwa
nini mwanamume asipimwe na mwanamke kwa kutumia kigezo cha ubikra? Maswali haya na mengine mengi yatapatiwa ufumbuzi katika sura ya tano.
Mwl Maeda