08-26-2021, 05:22 PM
Utengano
Mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano ya Said Ahmed Mohamed
Muhtasari
Kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia ni mojawapo ya mada kuu za majadiliano ya kimataifa juu ya maendeleo ya nchi za bara la Afrika. Kuna msimamo maarufu kwamba maendeleo ya wanawake ni maendeleo ya jamii nzima. Kwa hiyo, insha hii inalenga kujadili moja kati ya matokeo ya kutokuwepo kwa usawa huo, yaani mgogoro wa kijinsia katika nchi nyingi za kiafrika unaosawiriwa kwa kina na mtunzi Said Ahmed Mohamed katika riwaya yake ya Utengano. Insha hii inazungumzia kwa kina sababu, maendeleo na suluhisho za mgogoro huo katika riwaya ya Utengano. Inahitimishwa kwamba sababu kuu za mgogoro wa kijinsia uliomo katika jamii husika ya riwaya ya Said Ahmed Mohamed ni siasa za ubaguzi, mwelekeo wa wanaume wa kuwadharau wanawake na kutokuwepo kwa wanawake wengi wanao ari ya kuyaleta mabadiliko. Aidha, kuondolewa kwa sababu hizo kunaweza kueleweka kama suluhisho kuu ya mgogoro wa kijinsia.
Utangulizi
Katika matumizi ya kawaida neno mgogoro hutumiwa katika maana ya ‘hali ya watu kutoelewana ambayo huweza kusababisha ugomvi’ na kila siku tunakabiliana na migogoro ya aina fulani. Katika matumizi ya kifasihi mgogoro ni kipengele kikuu cha uhahiki wa dhamira kuu ya mwandishi katika kazi yake ya fasihi na unaweza kuwa wa (1) mtu na nafsi yake, (2) mtu na mtu mwengine, (3) kikundi cha watu na kikundi kingine na pia, (4) kikundi cha watu na mtu mmoja. Dhamira ya mwandishi, ambayo ni kipengele muhimu cha maudhui, ‘inachukuana na azma, lengo au kusudi la mtunzi katika kuitunga kazi yake’ na hakuna mwandishi anayetunga bila dhamira. Kwa hiyo, katika kazi nyingi za fasihi wandishi wanasawiri mgogoro fulani ambao, aghalabu, unadhihirisha maoni yao juu ya jambo maalum na, vilevile, uhalisi wa kimaisha wa jamii yao. Katika riwaya ya Utengano (1980) mtunzi Said Ahmed Mohamed anaisawiri migogoro kadhaa mathalan migogoro ya kitabaka, kisiasa au kiutamaduni lakini mgogoro wa kijinsia ndio mgogoro unaojitokea mwanzoni mwa sura ya kwanza na kuendelezwa mpaka mwisho wa ploti. Mgogoro wa kijinsia umejikita sana katika fasihi ya Kiswahili na mifano miwili ya wandishi wengine wanaohusisha kazi zao na dhamira hiyo ni Eurphrase Kezilahabi katika riwaya yake ya Rosa Mistika au Mohamed Said Mohamed katika riwaya yake ya Kiu. Lengo la insha hii ni kuueleza mgogoro huo katika riwaya ya Utengano kwa kuvifuata vipengele vikuu vitano, yaani: (1) sababu za mgogoro wa kijinsia, (2) jinsi mgogoro huo unavyotokea, (3) jinsi unavyoendelezwa na mwandishi, (4) nani anashiriki katika maendeleo ya mgogoro huo na mwishowe – (5) jinsi mgogoro wa kijinsia unavyosuluhishwa na mwandishi. Mwishoni, insha hiyo inafikia hitimisho (a) kwamba mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano (unaoweza kugawika kwenye mgogoro mkuu na migogoro midogo inayochangia katika maendeleo ya mgogoro mkuu) hauwezi kusuluhishwa kamili mpaka jitihada za wanawake, wanaume na pia, serikali, ziunganishwe pamoja, na (b) kuwa kuwepo kwake ni hatua ya kwanza ya kuuleta usawa kati ya wananchi wote katika jamii husika bila kujali jinsia.
Migogoro midogo ya kijinsia katika riwaya ya Utengano
Insha hii inapendekeza kwamba katika riwaya ya Utengano kuna mgogoro wa kijinsia mkuu unaozungushwa na kukuzwa na migogoro midogo ya kijinsia iliyomo, vilevile, ndani ya ploti. Said Ahmed Mohamed anautambulisha mgogoro wa kijinsia mkuu katika sura ya kwanza ya riwaya na anauendeleza mpaka mwisho wa ploti, yaani anayazungumzia matokeo yake na anayapendekeza maarifa ya kuusuluhisha. Mwanzoni, migogoro midogo inazungumziwa.
Kwanza, insha hii inajadili kwamba katika riwaya ya Said Ahmed Mohamed, kuna mgogoro wa kijinsia ndani ya fikra na hisi za mhusika wa kike unaotokea wazi mhusika huyo anapomkabili kiumbe wa kiume. Kazija ni mhusika wa kwanza msomaji anayekutana naye katika riwaya ya Utengano na jambo la kwanza tunalopata kujua kuhusu yeye ni chuki anayohisi dhidi ya wanaume wote. Mwandishi anatuelezea kwamba sababu ya msimamo wake huo wenye chuki ni kutokuwepo kwa usawa kati ya wanaume na wanawake (‘Anamchukia mwanamme kwa sababu dhahiri, nayo ni kuwa amewekwa mbele, ingawa Kazija hajui na nani.. Pamoja na hayo, Kazija anajichukia kwa kiasi anavyomchukia mwanaume kwa sababu ya nafsi yake ‘iliyolemaa na kuridhi siku zote kumpembejea mwanamme ambaye ni kiumbe kama yeye’. Upevu wa mgogoro wa kijinsia unaokuzwa ndani ya fikra za Kazija unatokea katika sehemu chache za riwaya ya Utengano. Katika sura ya kwanza Kazjia anapokutana na mvulana anayeitwa Mussa tunashahidi jinsi mwanamke huyo alivyopevuka katika kuyatetea maslahi yake na yale ya wanawake wengine. Ingawa Mussa ni mvulana wa umri mdogo, tayari ameingia katika mambo ya ulevi na anamwandamana Kazija ambaye ni mtu mzima. Kazija anapomkabili anajizungumzia akilini mwake kuhusu unyonyaji unaopokewa na wanawake wengi kutoka kwa wanaume (‘Mwanamke, mtumwa […] Viumbe vya kupika na kupakua, kufua na kupiga pasi, kushika mimba na kuzaa…’). Zaidi ya hayo, Kazija hasiti kuzungumza kwa sauti ya ushujaa anapomwonyeshea Mussa ufahamu wake mzuri juu ya sababu ya kutokuwepo kwa elimu miongoni mwa wanawake, Mussa anapojaribu kuzungumza katika lugha ya Kiingereza (‘Usiniseme Kizungu miye. Si ndivyo mlivyotuweka? Tusisome. Tuwe wajinga. Mtutawale na kutuparamia maisha, au sivyo?’). Hali kadhalika, Kazija anapomkabili Makusudi (mwanasiasa na baba yake Mussa), anajawa na hisia zile zile za chuki na ghadhabu (‘Alimtazama Makusudi kama vile alikuwa kakabiliana na chatu’). Anamwambia kwa maneno ya ujasiri kwamba anawadhulumu wanawake na, vilevile, kuwa ni mwanasiasa anayetawala kwa njia ya vitendo vilivyopotoka. Kwa sababu ya msimamo wake wenye chuki dhidi ya wanaume na ari ya kuanza vita vya ukombozi wa wanawake, Kazija anakubali kumsaidia rafiki yake wa kike, Farashuu, kwenye kumlipiza kisasi Makusudi aliyesababisha kifo cha mwanawe, Mwanasururu – hatua ya kwanza ya maendeleo ya mgogoro mkuu wa kijinsia katika riwaya ya Utengano. Yaani, Kazija anaamua kuwa mwanamke wa kando wa Makusudi na, sawia, kuzikubali posa za kimapenzi za Mussa ili kuusababisha ugomvi wa kifamilia hadi nyumba ya Makusudi itenganishwe na ishindwe na kisirani. Mwishoni, Kazija ndiye mshindi katika mgogoro baina yake na mwanaume – alitekeleza lengo lake na alipata jina la ‘mwanamke aliyekuwa na ujasiri kuliko wanaume’. Biti Kocho (mtumishi katika nyumba ya Bwana Makusudi) ni mhusika anayefanana kimsimamo na Kazija. Kama Kazija, Biti Kocho anasumbuliwa na mgogoro wa kijinsia uliomo akilini mwake na unaotokeza anapokabiliwa na mwanaume au matokeo ya dhuluma zake. Anapotambua jinsi Makusudi anawatendea Tamima (mkewe) na Maimuna (mwanawe) na, vilevile, anavyowalaghai wananchi, Biti Kocho anajaribu kuwatetea na kumkabili Makusudi kwa kupaza sauti yake ya ujasiri (‘Kumbe bwana wewe mjinga een. Yupo mtu asiyejua siasa dunia hii? Wadanganye hao wasiokujua, mimi nakujua vilivyo’). Anakata shauri kuwashawishi Maimuna apate uhuru wake kwa kutoka nyumbani (‘Wewe ni wa kufungwa ndani kama kuku? Huyo kuku ana afadhali’) na Tamima amwite mkunga wa kienyeji akamzalishe pasi na idhini ya Makusudi. Biti Kocho anamwita mkunga wa kienyeji anayeitwa Farashuu, yanni mwanamke anayepanga kumlipiza kisasi Bwana Makusudi. Ingawa katika mgogoro baina Biti Kocho na Makusudi hakuna mshindi wala mshindwa wazi, kwa minajili ya mwamko wake, Biti Kocho anatoa uamuzi wa kuchangia kwenye kuitekeleza mipango ya Farashuu na kwa maneno mengine – kwenye maendeleo ya mgogoro mkuu wa kijinsia katika riwaya ya Utengano.
Pamoja na hayo yote, kabla ya kujadili juu ya mgogoro mkuu wa kijinsia, maelezo mafupi kuhusu mgogoro wa kijinsia katika ndoa yangefaa ambao, katika riwaya ya Utengano, unawahusu hususan wahusika wawili – Selume na mumewe, Shoka. Ingawa mgogoro baina yao hauchangii katika maendeleo ya mgogoro mkuu wa kijinsia, unasisitiza kadiri kubwa ya upevu wa mgogoro wa kijinsia wa kijumla uliojikita katika jamii husika. Selume anayafahamu manyanyaso ya wanaume na anajaribu kupingana na Shoka ambaye ni mlevi asiyejali kuhusu wema wa aila yake. Bali, anapendelea kulała nje kumlaghai mkewe na kumwachia watoto wao ili awatunze pekee yake. Selume anaonekana kuwa mshindwa katika mgogogro baina yao kwa sababu walau anasema ‘tumo taabuni wanawake na huu utumwa kamili’, haelewi namna gani wanawake ni watumwa na anafikiri kuwa kuwafuata wanaume ni sharti zilizo ngumu kubadilika.
Mgogoro mkuu wa kijinsia katika riwaya ya Utengano
Kama ilivyotanguliwa kusemwa hapo awali, wanawake watatu wanahusika katika mgogoro mkuu wa kijinsia (Farashuu, Biti Kocho na Kazija) wanaopingana na mwanaume mmoja – Bwana Makusudi. Chanzo cha mgogoro huo ni matendo mabaya ya Bwana Makusudi ambaye alikisababisha kifo cha mke wake wa kwanza, Mwanasururu (binti yake Farashuu). Makusudi aliponyima mali Mwanasururu aliyorithi, akamwacha na Mwanasururu akawa mlevi, mwendawazimu na mwishoni akafa. Katika sura ya kwanza tayari tunapata kujua kwamba Farashuu aliamua kumlipiza kisasi kwa yote aliyomtendea binti yake na kuyasababisha madhara katika aila yake (‘Mimi nitalipa kisasi […] Bado nalia na kilio changu bado hakijanyamaza’). Pamoja na wenzake wawili, Kazija na Biti Kocho, walitoa uamuzi wa kuziunganisha sababu zote za chuki wote watatu waliyosikia dhidi ya Makusudi ili kuitenganisha familia yake. Kama ilivyoelezewa hapo awali, Kazija alisababisha utengano baina Makusudi na mwanawe wa kiume, Mussa. Farashuu pamoja na Biti Kocho waliwatenganisha Makusudi na Maimuna na mkewe, Tamima, aliyepewa talaka na kufukuzwa kutoka nyumbani. Aidha, Makusudi alipojaribu kuwahutubia wananchi wakati wa kampeni ya kugombea uchaguzi, Kazija aliwadhihirishia wasikilizaji ubaya Makusudi alionia na unyama ambao aliifanyia aila yake (‘Huyu Makusudi ambaye ameshindwa kuiendesha nyumba yake ataweza kuangalia maslahi yetu?’). Kwa hiyo, Makusudi alifungwa gerezani kwa muda wa miezi kadhaa na baada ya kutoka na kujaribu kumwona bintiye, Maimuna, akalazwa hospitalini kwa minajili ya kupigwa. Maimuna akaamua kumsahau baba yake na kubaki kutenganishwa na yeye kwa sababu ya yote mabaya aliyomtendea. Walau Said Ahmed Mohamed hauendelezi mgogoro mkuu wa kijinsia moja kwa moja mpaka mwisho wa ploti, anayazungumzia matukio yanayozuka kwa minajili ya mgogoro huo yaani momonyoko wa maisha ya Maimuna na Makusudi. Aidha, mgogoro wowote hauwezi kuanzishwa bila ya sababu, iwe ya maana kubwa au ndogo. Insha hii inajadili kwamba kuna sababu kadhaa za mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano, zinazoimarishana na kupishana.
Sababu za mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano
Kuna mshabihiano mkuu baina ya migogoro ya kijinsia iliyomo ndani ya ploti ya riwaya ya Utengano – yote inazuka kwa minajili ya matendo mabaya ya wanaume wanaowabagua wanawake na, sawia, kwa sababu ya ufahamu wa wanawake kuhusu ubaguzi unaotendwa dhidi yao na shauku yao ya kuukoma. Hata hivyo, mizizi ya mgogoro huo inafichwa ndani zaidi. Insha hii inajadili kuwa kuna sababu zinazokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mgogoro wa kijinsia (utengano baina wanawake na wanaume) na zile ambazo haziuna (siasa na dini). Aidha, zote tatu zinapishana na zinaimarishana. Utengano baina wanawake na wanaume unatajwa kama sababu ya mgogoro wa kijinsia na mwandishi mwenyewe tayari katika sura ya kwanza anapomsawiri mhusika anayeitwa Kazija. Kazija anatambua kuwa mwanamke ni ‘pambo la mwanaume ambalo alitazame apumbae nalo’ na kwa sababu hiyo anawachukia wanaume na anaamua kuwashinda. Utengano huo unawasababisha wanawake wawe wanyonge wakati wanaume wanafaidika kutoka kwa cheo chao cha juu. Insha hii inajadili kuwa utengano kati ya wanawake na wanaume una mizizi miwili mikuu, yaani siasa za ubaguzi na dini inayowatenganisha wafuasi wake (wanaume na wanawake). Said Ahmed Mohamed anazungumzia mada ya siasa na dini ili kuonyesha jinsi zote mbili zinavyoathiri maisha ya jamii husika. Mwandishi anatuelezea matendo ya wanasiasa wanaojali kuhusu maslahi yao tu kuwabagua wanawake na wanyonge wengine. Vilevile, anatudhihirishia kwamba siasa ni eneo la wanaume pekee yao ambapo mwanamke haruhusiwi kuingia, kwa hivyo – haruhusiwi kujitawala na kuyatawala maisha yake ambayo yanamtegemea mwanaume, kiumbe mwenye kuamua juu ya kila jambo. Hii inaonekana wazi Makusudi anapomwambia Biti Kocho ‘katafute kifuu na mchanga uchezee, usijitie kwenye mambo usiyoyajua’. Aidha, dini ya Kiislamu inachangia sana katika kuwepo kwa mgogoro wa kijinsia katika jamii husika, ingawa jambo hilo halipendekezwi na mwandishi moja kwa moja. Kwanza, dini ya Kiislamu inawaruhusu wafuasi wake kulipiza kisasi na inakubali ulipizaji kisasi uwe njia bora zaidi ya kutia adhabu (kanuni ya ‘jino kwa jino, jicho kwa jicho’). Ulipizaji kisasi ni silahi inayochaguliwa na Farashuu anapotoa uamuzi kwamba atapingana na mwanaume, Makusudi. Pili, Korani yenyewe inakubali wanawake lazima wawe chini ya wanaume na daima wakae watiifu (‘na uvumilie kwa kimya nyumbani kwako…’). Kwa muujibu wa Korani, mwanamke lazima apate idhini ya mwanaume ya kutoka nje au kumkaribisha mgeni nyumbani kwao – jambo linaloonekana wazi nyumbani kwa Makusudi anayemkataza mkewe, Tamima atoke bila ya maarifa yake (‘babako hataki tutoke nje ila kwa ruhusa yake, na humu asiingie mtu ila kwa ruhusa yake’). Bila shaka yoyote kanuni hizo zilizaa ghadhabu ya Biti Kocho aliyekata shauri kutozitii, kinyume cha Tamima aliyetaka kubaki mtumwa wa mumewe. Aidha, wakati wa kujadili kuhusu mgogoro katika kazi ya fasihi ni lazima kujiuliza, je mwandishi anaipendekeza suluhisho yoyote?; na aya inayofuata italichambua swali hilo.
Suluhisho za mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano
Mwanzoni, ni muhimu kukubali nani ni mshindwa na mshindi wa kijumla katika mgogoro huo: mwanamke au mwanaume? Makusudi anaonekana kuwa mshindwa kwa sababu anateseka – anatenganishwa na familia yake, anafungwa gerezani, analazwa hospitalini, mwishoni anakufa na hapati nafasi ya kuwaona wote katika familia yake waliojikusanya kwa ajili ya arusi ya Maimuna. Licha ya hayo yote, mwanamke bado hawezi kuitwa mshindi kwenye mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano kwa sababu kadhaa zilizo, vilevile, suluhisho za mgogoro wa kijinsia. Insha hii inajadili kuwa mgogoro wa kijinsia unaachwa na mwandishi bila kusuluhishwa lakini mtunzi anapendekeza kwamba mgogoro huo unaweza kusuluhishwa mwanamke anapomshinda mwanaume na mwanaume anapokubali ushinde wake na kujibadilisha kitabia. Kwa hivyo, kwanza, Said Ahmed Mohamed analenga kutuambia kwamba wanawake wanaweza kuwa washindi katika siku za mbele ikiwa wote wataziunganisha bidii zao kuwakabili wanaume na unyonyaji unaofanyiwa nao. Katika riwaya ya Utengano, wanawake, badala ya kuziunganisha nguvu zao zote ili kuyapambana na maudhui ya wanaume, wana mwelekeo wa kuwadhuru wanawake wengine jinsi Farashuu and Biti Kocho walivyosababisha unyonge wa Maimuna. Pili, wanawake wengi (kama Selume au Tamima) wanaamini kwamba mila au dini yao inawashurutisha daima wawafuate wanaume na kuwa hawaruhusiwi kupambana na kiumbe wa kiume (‘alijiona anafuata kawaida na kanuni iliyotoka mbali ambayo imekuwa ngumu kugeuka’). Said Ahmed Mohamed anania kuwadhihirishia wasomaji kwamba moja kati ya suluhisho za mgogoro wa kijinsia ni kuwepo kwa wanawake kama Biti Kocho, yaani ufahamu mzuri wa umuhimu wa uhuru miongoni mwa wanawake ambao bado wanaogopa kusimama na kuzitetea haki zao. Tatu, mwandishi anayapendekeza mabadiliko ya mfumo wa kisiasa ambao ni mmoja wenye ubaguzi na ufisadi. Wanasiasa wana nguvu kuliko wananchi wengine na mgogoro wa kijinsia utaendelea kujikita katika jamii husika ikiwa wao hawatazibadilisha sera zao kwenye zile za kidemokrasia (yaani, kama zile za mwanasisasa Siwa). Mwishoni mwa riwaya, Maimuna anasoma katika gazeti kwamba serikali inapanga kufanya kampeni ya maendeleo ya wanawake kwa sababu ‘maendeleo ya wanawake ni maendeleo ya jamii nzima, na ukombozi wa wanawake ni ukombozi wa jamii nzima’. Mwisho lakini si uchache, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa wanaume kama Kabi (mume wake Maimuna) na geuko la mtazamo wa wengi wa wanaume ambao bado wana mwelekeo wa kuyadharau maneno ya wanawake (‘inahitajia wanaume waelimishwe kuhusu maslahi ya wanawake’).
Hitimisho
Mwenda Ntarangwi alivyosema na kinachoonekana wazi katika riwaya ya Utengano ya Said Ahmed Mohamed ni kwamba ‘uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mambo ya kati kabisa katika fasihi’. Hakuna mwandishi anayetunga kutokana na ombwe bali tajriba yake (mambo aliyoshuhudia) iliyomtilia moyo wa kuwawasilishia watu ujumbe fulani, uwe mzito au mwepesi. Said Ahmed Mohamed aliamua kuandika kuhusu mgogoro wa kijinsia kwa sababu dhahiri – mgogoro huo umejikita sana katika jamii nyingi za Waswahili bila kusuluhishwa na hicho ndicho mojawapo ya vizuizi vikuu vya maendeleo yao ya kijumla. Insha hii inajadili kwamba mgogoro wa kijinsia katika riwaya ya Utengano unaweza kugawika kwenye mgogoro mkuu na migogoro midogo inayochangia kwenye maendeleo na kadiri ya mgogoro mkuu unaoendelezwa kutoka mwanzo mpaka mwisho wa ploti ya riwaya. Insha hii inahitimisha kwamba kuwepo kwa mgogoro wa kijinsia ni hatua ya kwanza ya kuyaleta mabadiliko yanayohitajika ili kuboresha hali ya maisha ya jamii husika. Hata hivyo, mtunzi anapendekeza kwamba mgogoro huo uko katika Afrika kwa sababu kadhaa, yaani: siasa za ubaguzi, mwelekeo wa wanaume wa kuwadharau wanawake na kutokuwepo kwa wanawake wengi wanao ari ya kuyaleta mabadiliko, ambazo ni vizuizi vikuu vya kuusuluhisha mgogoro wa kijinsia.
Bibliografia
Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili, Institute of Kiswahili Research, Tanzania (Dar es Salaam), 1996
Kamusi ya Kiswahili ya Karne ya 21, Longhorn Publishers, Kenya (Nairobi), 2011,
Mwenda Ntarangwi, Uhakiki wa kazi za fasihi, Augustana College, Rock Island, 2004
Said Ahmed Mohamed, Utengano, Longhorn Publishers, Tanzania (Dar es Salaam), 1980
//www.thereligionofpeace.com
Kamusi ya Kiswahili ya Karne ya 21, Longhorn Publishers, Kenya (Nairobi), 2011, ukurasa 313
Mwenda Ntarangwi, Uhakiki wa kazi za fasihi, Augustana College, Rock Island, 2004, ukurasa 80
Said Ahmed Mohamed, Utengano, Longhorn Publishers, Tanzania (Dar es Salaam), 1980, ukurasa 1[url=https://mwalimuwakiswahili.co.tz/mgogoro-wa-kijinsia-katika-riwaya-ya-utengano-ya-said-mohamed/#_ftnref4][/url]
Qur’an(33:33), tafsiri yangu (//www.thereligionofpeace.com/Quran)
Said Ahmed Mohamed, Utengano, Longhorn Publishers, Tanzania (Dar es Salaam), 1980, ukurasa 20
Mwenda Ntarangwi, Uhakiki wa kazi za fasihi, Augustana College, Rock Island, 2004, ukurasa 80
Mwl Maeda