08-26-2021, 03:31 PM
UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI KATIKA RIWAYA YA “ADILI NA NDUGUZE” ILIYOANDIKWA NA SHAABAN ROBERT
1.0 Utangulizi
1.0 Utangulizi
Kazi hii inahusu uchambuzi wa fani na maudhui katika riwaya ya “Adili na Nduguze” iliyoandikwa na Shaban Robert mwaka 1952. Katika kujadili riwaya hii tutaeleza dhana ya riwaya, usuli wa mwandishi, muhtasari wa kitabu chenyewe, nadharia zitakazotumika kuchambua fani na maudhui ya kitabu hiki, uchambuzi wa fani na maudhui na hitimisho.
1.1 Dhana ya Riwaya
Kwa mujibu wa Madumulla (2009) akimrejelea Msokile (1992) anafafanua kuwa riwaya ni kazi ya sanaa ya kubuni, ni maandishi ya nathari (ujazo) yanayosimulia hadithi ambayo kwa kawaida ina uzito, upana, urefu wa kutosha, ina wahusika wengi wenye tabia mbalimbali, ina migogoro mingi mikubwa na midogo.
Senkoro (1982) anasema riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja, na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii.
Wamitila (2003), Samwel na wenzake (2013), wanasema kuwa riwaya ni kazi andishi ya fasihi ambayo kwa kawaida ni ndefu zaidi kuliko hadithi fupi. Urefu wa riwaya maana yake ni kwamba msuko simulizi umejengeka vizuri, kuna wahusika wengi, inaenea muda mrefu, na mada zake ni nzito na pana kiasi. Mifano mizuri ya riwaya kwa lugha ya Kiswahili ni “Nagona” au “Mzingile” riwaya za mwandishi Euphrase Kezilahabi.
Kwa ujumla riwaya ni hadithi ndefu za kubuni zenye wahusika wengi au wachache zinazoelezea maisha ya mtu au jamii fulani.
1.2 Usuli wa Mwandishi
Sheikh Shaaban Bin Robert alizaliwa tarehe mosi January mwaka wa 1901 katika kijiji cha Vibambani, mahali paitwapo Machui, maili sita kusini ya Tanga. Yakisiwa kuwa jina hili la ‘Robert’ lilitokana na matamshi mabaya ya Jina lake alilopewa akiwa skuli, Msimbazi, kwa kuwa baba yake hakuitwa Robert. Mara nyingi aliandika jina lake kama “Roberts”
Baba yake alifanya kazi kama karani katika Shamba la makonge la Amboni. Mama yake alikuwa Mdigo. Yasemekana kuwa wazazi hawa wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Lakini, Sheikh Shaaban alikataa kuitwa Myao akawa mmoja wa watu wachache waliojiita Waswahili.
Baba yake alifanya kazi kama karani katika Shamba la makonge la Amboni. Mama yake alikuwa Mdigo. Yasemekana kuwa wazazi hawa wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Lakini, Sheikh Shaaban alikataa kuitwa Myao akawa mmoja wa watu wachache waliojiita Waswahili.
Shaaban alitafuta mke wake wa kwanza kwa utulivu na makini kwa miaka kumi. Alitaka mke mzuri, mwaminifu na mwenye tabia ya kuigwa katika nyumba. Alifanikiwa hata akaoa mke wake Amina. Baada ya miaka kumi mke wake alifariki dunia. Shaabani aliomboleza kifo cha mke wake hata akatunga shairi la msiba huo. Yasemekana kuwa mke wake aliacha watoto watano, dada yake mwana Saumu na mama yake. Alivumilia maisha ya ugane kwa miaka mitano. Kisha akaposa mke wake wa pili na kuoa tena. Alioa mara tatu.
Kuanzia mwaka wa 1926 hata1944, Shaaban alifanya kazi na Idara ya Forodha, Pangani. Alikuwa mtu mwenye kufanya kazi yake kwa uangalifu na uvumilivu hata alipandishwa vyeo viwili katika kazi hii: “Grade III Higher Division” na “Grade II Local Service Council”. Alihamishiwa Mpwapwa mwaka wa 1944 akafanya kazi na Idara ya wanyama hadi 1946. Kutoka 1946 hadi 1952, alifanya kazi ofisi ya mkuu wa Jimbo la Tanga. Kabla ya kustaafu mwaka wa 1959 alifanya kazi na ofisi ya kupima nchi Tanga. Alikuwa mtu mwaminifu, mwenye kupenda urafiki, mvumilivu na mwenye bidii sana. Alipostaafu, akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumbukiza kwa upigishaji chapa uandishi wake. Hii ilikuwa ni kazi ngumu na ya kugharimu fedha nyingi sana. Lakini hakufa moyo kwa maana ilikuwa ni kazi ya hiari na mpenda hiari si mtumwa kama alivyopenda kusema.
Kuanzia mwaka wa 1926 hata1944, Shaaban alifanya kazi na Idara ya Forodha, Pangani. Alikuwa mtu mwenye kufanya kazi yake kwa uangalifu na uvumilivu hata alipandishwa vyeo viwili katika kazi hii: “Grade III Higher Division” na “Grade II Local Service Council”. Alihamishiwa Mpwapwa mwaka wa 1944 akafanya kazi na Idara ya wanyama hadi 1946. Kutoka 1946 hadi 1952, alifanya kazi ofisi ya mkuu wa Jimbo la Tanga. Kabla ya kustaafu mwaka wa 1959 alifanya kazi na ofisi ya kupima nchi Tanga. Alikuwa mtu mwaminifu, mwenye kupenda urafiki, mvumilivu na mwenye bidii sana. Alipostaafu, akiba ndogo aliyokuwa nayo aliitumbukiza kwa upigishaji chapa uandishi wake. Hii ilikuwa ni kazi ngumu na ya kugharimu fedha nyingi sana. Lakini hakufa moyo kwa maana ilikuwa ni kazi ya hiari na mpenda hiari si mtumwa kama alivyopenda kusema.
Sheik Shaaban alikuwa hodari kwa kazi yake ya uandishi na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili. Uandishi wake ulikuwa kazi ya hiyari na matokeo ya mazoezi ya ujana wake. Aliandika hadithi za mawazo yake kama Kusadikika na Kufikirika, Historia kama vile utenzi wa vita vya pili vya dunia, Insha, Magazeti, Tawasifu na vitabu vya wasifu kwa mjazo na ushairi. Lugha aliyoitumia ilikuwa bara bara na uandishi wake ulihusu mambo yanayotokana na wahenga. Alitilia maanani desturi iliyoenea na ile inayoelekea kusahauliwa kwa sababu ilitumiwa na washairi waliotangulia. Uandishi wake ulikuwa na maneno ya hekima tupu na mafundisho yanayowafaa wake na waume katika ndoa, wajane, watoto na hata wazee. Hivyo basi, aliweza kutunzwa kwa zawadi ya waandishi inayoitwa “Margaret Wrong Memorial prize”. Alikuwa mwandishi wa kwanza wa Kiwahili kutuzwa nishani ya “Member of British Empire, (M.B.E.)” kutoka kwa Malkia wa Uingereza. Tuzo nyingine aliyopata ilikuwa nafasi ya kwanza kwa kuandika insha juu ya maisha yake katika shindani lililofanywa Afrika Mashariki. Katika Shindano lingine la uandishi wa insha juu ya utaifa na uzalendo, insha ya Shaaban ilipata zawadi ya kwanza. Shindano hili lilitolewa na serekali ya Bara la Hindi.
Katika uendelezaji wa lugha, Shaaban alijiunga na vyama kama vile, “East African Swahili Committee, East African Literature Bureau, Tanganyika Language Board, Tanga Township Authority”. Aliheshimiwa Dar es Salaam akawa mtu wa pili kati ya watu kumi na mmoja kupewa shahada ya kutoka chuoni. Waziri wa Elimu Dar es Salaam mwaka wa 1966, alimsifu Shaaban na kusema kuwa jina lake limeota mwamba usiobomoka mioyoni mwa waafrika wengi wa Afrika Mashariki.
Shaaban alifungua duka lake la vitabu Julai 1960. Alisaidiwa na rafiki yake Mzungu kupigisha chapa katika kiwanda kingine Kenya. Biashara hii ilikuwa ngumu kwa maana watu wengi walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Wachache waliojua kusoma na kuandika, hawakuwa na fahamu kwamba katika vitabu ndimo ghala za utamaduni na elimu hupatikana. Alifurahia kuwapa hawa watu wachache vitabu vyake wasome bure. Hodari huyu wa lugha ya Kiswahili ameandika zaidi ya vitabu ishirini vya Mashairi. Katika vitabu vyake, amewashawishi wasomaji wasome mara kwa mara kuendeleza lugha. Ingawa hayuko sifa zake bado zaenea na vitabu vyake vyatumika kwa ufundishaji wa lugha katika vyuo vya Tanzania, Kenya na kwingineko ulimwenguni wanakofundisha lugha ya Kiswahili.
Alifariki tarehe 22 Juni mwaka 1962. Mpaka anafariki kwa maradhi ya moyo na upungufu wa damu, Shaaban Robert alifanikiwa kuandika vitabu 24 kwa lugha adhimu ya Kiswahili, na mpaka sasa kazi zake zinazidi kukusanywa na taasisi ya uchunguzi na kukuza Kiswahili (TUKI) ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Kipo kitabu cha 25 ambacho kilitolewa miaka ya karibuni ambacho kina barua alizokuwa akiandikiana na jamaa zake.
Katika kitabu hicho kumeonekana uwezo mkubwa aliokuwa nao Shaaban Robert katika kuchagua maneno na ufasaha wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Kwani watu wengi walidhani Shaaban Robert hakuwa mjuzi wa lugha ya Kiingereza lakini katika barua zake zipo ambazo aliziandika kwa lugha hiyo ya kigeni kwa ufasaha wa hali ya juu.
1.3 Muhtasari wa kitabu
Adili na Nduguze ni riwaya iliyotungwa na Shaaban Robert; mwandishi mashuhuri (maarufu) kutoka Tanzania. Riwaya hii ilitungwa mnamo 1952. Katika riwaya yake anashughulika na mambo mengi kuhusu tabia mbalimbali za watu. Mtunzi anatueleza kuwa tushinde uovu kwa kutenda mema yaani “Wema hauozi”. Adili alimwokoa Huria wakati alipokaribia kuuwawa na Hunde. Kutokana na wema huo, Huria naye alimwokoa Adili wakati alipotoswa baharini na ndugu zake. Haya yanazingatiwa na msemo wa Kiswahili “kinifaa huangua, nitakufaa kwa mvua” au methali isemayo “Mwosha huoshwa”. Katika kufikisha ujumbe mwandishi ameijenga kazi yake kwa kuwahusisha wahusika mbalimbali. Amemchora Mfalme Rai kuwa ni kiongozi mzuri na mfuatilizi bora wa kazi ambayo humwezesha kuistawisha nchi yake ya Ughaibu katika mifugo. Mshauri wake Ikibali alikuwa bingwa wa uchunguzi wa kodi za wanyama ila alielemewa na siri ya kiongozi wa Janibu, Adili kuwaadhibu vikali manyani waliokuwa kwake. Alishangaa kuona jinsi ukatili huo ulivyohitilafiana sana na tabia ya wema na huruma ya Adili akaamua siri hiyo ifichuliwe mbele ya Mfalme Rai. Alipoletwa mbele ya Mfalme Rai, Adili alijitetea akieleza kuwa wanyama hao walikuwa zamani nduguze kwani walizaliwa na baba mmoja, Faraja. Alijulisha kuwa alilazimika kuwagawia urithi wake wakati walipofilisika ugenini na kurejea nyumbani kwao Janibu. Alisimulia jinsi ndugu wote watatu walivutwa na faida za biashara na kusafiri mpaka walipoufikia mji wa mawe, Adili alipokutana na mchumba, Mwelekevu. Hapo hapo, Adili alieleza kuwa uovu waliomfanyia nduguze ndio uliwafanya wageuzwe kuwa manyani. Kwanza kutokana na mali aliyoleta jahazini na mwanamke huyo mrembo kutoka mji wa mawe, nduguze walimwonea wivu na kumlia njama za kumtosa baharini. Wakati huo huo, aliokolewa na jini, Huria binti Kisasi, ambaye aliwahi kulisaidia liliposhambuliwa na nyoka, ama jini jingine Hunde. Adili aliporejea katika chombo akiwa na Huria, jini hilo ndipo liliamua kuwafanya manyani ikiwa ni adhabu na kutoa amri ya kuwa watapigwa kila siku kutokana na maovu yao. Adili aliporudi nchini mwake, Ughaibu, ndiye aliadhibiwa wa kwanza kwa kusahau kuwapiga manyani. Tokea hapo ilikuwa mazoea yake kuwapa chakula na kuwapiga vikali hadi siku Ikibali alipogundua siri hiyo. Baada ya kisa hicho, Mfalme Rai almsihi Adili asiwapige tena manyani ila awatunze vizuri na kula nao. Alijitahidi kuwaombea msamaha kwa Mfalme wa majini Kisasi na bibiye Huria. Ombi lake lilisikilizwa na nduguze Adili waligeuzwa kutoka uhawayani na kuwa watu tena. Siku hiyo ilikuwa ya furaha, na nduguze wote watatu walifunga ndoa pamoja.
1.4 Nadharia / mkabala wa Ki-akisiko/kifumano
Nadharia hii inaelezea fasihi kama inayoakisi uhalisia uliopo nje yake. Mawazo ya aina hii yanahusishwa na Lenin. Mtaalamu huyu aliziona kazi za Leo Tolstoy kama zilizoakisi mikinzano ya kijamii iliyoishia kuyasababisha mapinduzi ya Urusi. Kwa njia hiyo ni kazi za kifanisi. Mkabala huu unategemezwa kwenye itikadi ya kiujumi iliyokuzwa na Myunani Aristotle katika dhana yake ya ‘muhakati’ au ‘mimesia’ pamoja na msimamo wa Marx kuwa uhalisia ulio wazi au dhahiri unachukua nafasi ya kwanza kabla ya mawazo akilini. Mhakiki wa Ki-hungary, George Lukacs anayehusishwa na mkabala huu anaichukulia fasihi kama maarifa ya uhalisi. Hii haina maana kuwa lazima pawepo na mfanano wa moja kwa moja na uhalisi. Uhalisi huo lazima ushughulikiwe na ubunifu wa mwandishi, na kazi yake inayoupa muundo maalum. Katika msingi huu panakuwapo na jinsi mbalimbali za kuwasilisha uhalisi fulani. Njia hizi hutofautiana katika mkazo wa masuala fulani yanayoshughulikiwa. Mkabala huu unakuwa msingi mzuri wa kuzitathimini kazi fulani katika msingi wa uhalisia au utohalisia (Wamitila 2002).
Hivyo basi, nadharia ya ki-akisiko/kifumano ni nadharia ambayo hujikita katika mambo yaliyopo yaani uhalisia wenye matukio mahususi na matokeo yanayoweza kuthibitika na mambo yasiyokuwepo yaani utohalisia ambao matukio yake ni vigumu kuyathibitisha kama sehemu ya uhalisia. Tukirejelea katika riwaya ya “Adili na Nduguze”mwandishi amejikita katika uhalisia na utohalisia kwani amezungumzia mambo ambayo yanajitokeza na yapo katika jamii na yale ambayo ni sehemu ya utohalisia kwani yanasikika yakisemwa lakini kuyathibitisha kama sehemu ya uhalisia ni vigumu. Hivyo tutatumia nadharia hii kuhakiki maudhui yaliyojitokeza katika kitabu hiki kwa kuwa kitabu hiki kinasawiri mambo ambayo yapo katika jamii zetu na yale ambayo ni utohalisia.
1.5 Nadharia ya Umuundo
TUKI (2004) wanaeleza nadharia kuwa ni mawazo, maelezo na muongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza kutatua au kutekeleza jambo fulani. Nadharia yoyote ile ya kihakiki ni nyenzo ya kusaidia kufikisha lengo fulani.
Ntarangwi (2004) anasema kuwa umuundo waweza kuelezwa kama mtizamo wa kitathimini ambao huzingatia zaidi miundo inayojenga kazi binafsi. Mwasisi anayetajwa sana katika nadharia hii ni Ferdinard De saussure aliyependekeza mtizamo mpya kuhusu lugha. Kinyume na wataalamu wengine walioshughulikia historia na sura maalum za lugha fulani, Saussure alivutiwa na miundo inayohimili lugha zote, huku akijaribu kuonyesha kwamba lugha zote za ulimwengu zaweza kutathiminiwa kwa kaida maalum za umuundo. Alizua istilahi `parole’ na `langue’ kueleza maoni yake: `Parole’ au uzungumzi ni lugha katika matumizi na hiki ndicho walichokizingatia wanaisimu wa awali, lakini Saussure alivutiwa na mfumo wa kinadharia unaounda lugha zote au `Langue’ – yaani masharti au kaida zinazoiwezesha lugha kuwepo na kuweza kufanya kazi. Hata hivyo, kazi ya Saussure ilikuwa imetengewa wanaisimu peke yao. Katika miaka ya 1950, mtizamo huo wa Saussure ulianza kusambaa katika masomo mengine hasa wakati mawazo yake yalipozingatiwa na Mwanaanthropolojia Claude Levi-strauss. Kwa kuchukua maoni ya isimu ya Saussure na kuyaingiza katika sayansi ya kijamii. Hasa alichotaka kuendeleza kidhana ni kwamba pana viwango viwili katika kuelewa maisha ya jamii, isimu, lugha na chochote kingine kile. Viwango hivi ni cha juu juu (surface) na cha ndani (deep).
Mkondo huu wa mawazo ya umuundo kuhusu sayansi za jamii ulianzia ulaya na kuathiri mtazamo wa elimu mbalimbali (duniani) kama vile: Falsafa, Anthropolojia, Historia, Uhakiki wa kifasihi na Sosiolojia. Kwa hivyo twaweza kuangalia jamii katika muundo wake wa kijuu juu na kuielewa lakini tukitaka kupata maana mwafaka lazima tuchunguze muundo wake wa ndani ambao hupatikana katika kila jamii ya wanadamu. Kwa hiyo hata katika kuielewa fasihi lazima tuifahamu lugha yake. Katika kupata maana lazima kuwe na uhusiano wa kipembetatu yaani kuna dhana, alama na kitajwa.
Kama vile muundo wa lugha ulivyo mfumo, muundo wa fasihi pia una vipengele vinavyotegemeana na vinavyoelezwa katika muktadha wa vipengele vingine. Katika kazi ya fasihi kuna kitengo cha kisanaa kama vile maudhui, ploti, wahusika, muktadha na lugha. Hakuna kipengele cha fasihi kati ya hivi kitakachoelezwa katika upekee wake. Lazima kielezwe kwa kuzingatia kuwepo kwa jukumu la vipengele vingine. Kwa mfano katika kueleza au kuzungumzia ploti, wahusika watashirikishwa na lugha yao kuzingatiwa. Kwa hiyo nadharia ya umuundo husisitiza vipengele vya kazi ya sanaa jinsi vinavyohusiana hadi kuikamilisha kazi hiyo. Huangalia namna sehemu mbalimbali za kazi za sanaa zilivyofungamana. Yaani Neno halihitaji urejelezi ili lipate maana, na kazi yenyewe ilivyoundwa ndivyo hutoa maana. Yaani maana inavyoumbwa ina dhima kubwa kuliko maana yenyewe.
Hivyo nadharia hii tutaitumia katika kuchambua sehemu ya fani katika riwaya ya “Adili na Nduguze” kwani nadharia hii itatusaidia kuibua vipengele vilivyoijenga fani na kuifungamanisha katika kutoa kusudio la Msanii kwa jmii husika.
2.0 Maudhui katika Riwaya ya “Adili na Nduguze”
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) maudhui ni mawazo fikra na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi. Maudhui ina vipengele mbalimbali ambavyo ni pamoja na dhamira, ujumbe, falsafa, migogoro, msimamo na mtazamo wa mwandishi. Katika riwaya ya “Adili na Nduguze” vipengele vya maudhui vinavyojipambanua au kujidhihirisha ni pamoja na:-
2.1 Dhamira
Madumulla (katajwa) anasema dhamira ni wazo kuu katika kazi ya fasihi. Dhamira ni sehemu tu ya maudhui. Dhamira ndiyo hujenga kiini cha kazi ya fasihi, yafuatayo ni mawazo au dhamira zilizojitokeza katika riwaya hii ya“Adili na Nduguze”
2.1.1 Uongozi mzuri.
Uongozi ni dhana, taaluma inayompa muhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaoongozwa naye kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia ili kufikia malengo yao. Kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao (www. Sw.wikipedia. org/wiki/uongozi)
Katika riwaya hii ya Adili na Nduguze suala la uongozi mzuri limejitokeza. Tunamwona jinsi Rai alivyokuwa kiongozi muadilifu na mfalme mwema sana katika jamii yake. Hakuwa na tabia ya kumlazimisha mtu kufanya kazi bali aliwashawishi watu kufanya kazi. Alijituma katika kufanya kazi kwa bidii zake zote, hakusita kufanya kazi iwe kubwa au ndogo. Mwandishi anasema;
“Kwa bidii zake kubwa aliweza kushiriki katika mambo mengi ya maisha, akasaidia maendeleo makubwa ya nchi yake. Hakulazimisha mtu yeyote kutenda tendo Fulani, lakini alishawishi kila moyo wa mtu kuiga alivyotenda kwa hiyari yake mwenyewe, alikuwa na mvuto mkubwa juu ya mioyo ya watu. Alitumia mvuto huu juu ya watu mpaka nchi yake ilikuwa haina mvivu, goigoi wala mwoga” (uk 2).
Tukilejea katika jamii ya sasa suala la uongozi mzuri linasisitizwa ili kufikia malengo ya kimaendeleo. Wapo viongozi ambao ni wazuri na uongozi wao ni bora wakiwa wanawajibika katika kuangalia maendeleo ya jamii zao.
2.1.2 Matabaka
Kwa mujibu wa
Katika riwaya hiii ya Adili na Nduguze suala la matabaka limejitokeza kwani tunaona kuna matabaka kati ya mtawala na mtawaliwa. Kwa mfano kuna Rai ambaye ndiyo mfalme wa Ughaibuni na Watawaliwa ambao ndio raia wa ughaibuni. Mwandishi anasema;
Rai, mfalme wa Ughaibu, alikuwa mfalme wa namna ya peke yake duniani.
“……Kutawala suluhu na mapenzi ya wanadamu, utunzaji wa wanyama, na utii juu ya viumbe wasioonekana kama majini hutaka uwezo mkubwa sana. Kmama hivi, fikiri wewe mwenyewe jinsi Rai alivyojipambanua mwenyewe na wafalme wengine”.
Tukilejea katika jamii zetu pia suala la matabaka halipingiki kutokana na kuwepo kwa mgawanyo wa kazi. Yapo matabaka katika nyanja za uongozi, elimu, siasa na hata nyanja za kiuchumi na kidini.
2.1.3 Mapenzi ya kweli
Katika riwaya hii suala la mapenzi ya kweli limejidhihirisha kwani tunamwona muhusika Adili jinsi alivyokuwa na mapenzi ya kweli na ndugu zake. Kwani hakuwa mbinafsi kwa kuwa alikuwa tayari kugawana na yeyote chochote alichokuwa nacho. Mwandishi anasema;
Adili alikuwa tayari siku zote kugawana na mtu yeyote tonge moja la chakula lililokuwa mikononi mwake” (uk. 12).
2.1.4 Ukaidi na Dharau
Katika riwaya hii ya “Adili na Nduguze” watawala wa mji wa mawe ambao ni mfalme Tukufu na Malkia Enzi na raia wao walikuwa waabudu mizimu. Walionywa kuachana na tabia hiyo na Mrefu ambaye alikuwa ametumwa kuja kuwaonya juu ya kuabudu mizimu ambayo ilikuwa ni miti na matokeo ya kaidi hiyo, mji na watu wote waligeuzwa mawe isipokuwa Mwelekevu ambaye alikuwa Binti mfalme kutokana na utii wake kiimani. Mwandishi anasema
“Tukufu hakujali onyo hili akahamrisha kushikwa kwa Mrefu aliyekuwa hasogeleki wala hashikiki……………, kwa laana iliyotamkwa na Mrefu……………kila kiumbe kilichokuwa na maisha katika
fahari kiligeuka jiwe” (uk 29)
2.1.5. Suala la Imani
Imani lina maana mbalimbali (mfano. “huruma”), na maa kuu inahusiana na kitenzi kuamini, kinachofanana nakusadiki. Hapo ni kukubali ukweli wa jambo lisiloweza kuthibitishwa. Katika dini msingi wake ni mamlaka yaMungu aliyeshirikishwa ukweli huo kwa njia ya ufunuo maalumu ili kumsaidia binadamu amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani na ahera. Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza kushikilia jambo bila ya uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo unatia maanani pia akili katika ujuzi wa ukweli.
Katika riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ suala la Imani limejitokeza kwani tunaona kuwa mfalme Tukufu na malkia Enzi na raia ambao waliishi katika mji wa Mawe walikuwa wanaamini katika mizimu, Mizimu hiyo ilikuwa ni miti ambapo baadae miti hiyo iligeuka na kuwa mawe ukutani. Mwandishi anasema;
“Walakini, juu ya sifa hizo, malkia, mfalme na raia walikuwa waabudu mizimu. Mizimu yao ilikuwa miti. Miti yenyewe ni ile iliyogeuka kuwa mawe ukutani. Kawere, mganga na imamu wa mizimu hiyo alivuta mioyo ya watu wote”(uk. 27).
2.1.6 Suala la ukatili
Suala la ukatili limejidhihirisha wazi katika riwaya hii. Tunaona jinsi Ndugu zake Adili (waliitwa Mwivu na Hasidi) walivyomtosa Adili baharini wakati wakiwa katika jahazi kuelekea Janibu, huku lengo lao likiwa ni kumuuwa ndugu yao ili waweze kumuoa kiushirika Mwelekevu ambaye alikuwa ni mchumba wake Adili, kutokana na uzuri aliokuwa nao yule msichana. Mwandishi anasema;
“Alitoswa baharini kama kitu kilichokuwa hakifai.”
Vilevile katika jamii zetu suala la ukatili lipo. Kuna watu ambao wamejeruhiwa na hata kuuawa na ndugu au rafiki zao kwa sababu ya migogoro inayosababishwa na mapenzi.
2.2 Migogoro
Kwa mujibu wa TUKI (2004) wanasema kuwa migogoro ni hali ya kutofautiana baina ya pande mbili au zaidi, wanasema migogoro inaweza kuwa ya familia, matabaka ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Katika riwaya hii imejitokeza migogoro tofautitofauti kama ifuatavyo:
Mgogoro kati ya Mrefu na Tukufu. Mgogoro huu ulitokea baada ya Mrefu kumshauri Tukufu kuachana na kuabudu mizimu, lakini Tukufu alikaidi. Suluhisho la mgogoro huu ni kuwa mtu akikaidi mambo ya kiimani hudhurika.
Mgogoro kati ya Adili na Ndugu zake. Mgogoro huu unatokea pale ambapo Adili aligawa sawia mali zake kwa nahodha,na ndugu zake alizozipata kutoka katika mji wa mawe, lakini ndugu zake hawakuridhika kwani walitaka wapate zaidi. Vivyo hivyo, mgogoro unajitokeza pale ambapo walimtosa Adili baharini kwa lengo la kutaka kumuoa mchumba wake (Mwelekevu). Suluhisho la mgogoro huu ni kuadhibiwa kisheria, kutokana na kufanya matendo ya kihalifu na unyama kwa binadamu.
Mgogoro kati ya Hunde na Huria. Mgogoro huu unajitokeza pale ambapo Hunde ambaye ni jini, anamwitaji Huria kimapenzi, ambaye ni mtoto wa mfalme wa majini lakini Huria anamkataa Hunde. Suluhisho la mgogoro huu ni kuwa Hunde anaemlazimisa Huria kumkubali kimapenzi ni kushtakiwa kisheria na sheria kuchukuwa mkondo wake.
2.3 Ujumbe
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) ujumbe ni kitu ambacho mwandishi hudhamiria kumtumia msomaji, kila kazi ya fasihi hubeba ujumbe ambao msanii hutaka umfikie msomaji wake. Katika riwaya ya hii kuna ujumbe wa aina tofauti tofauti uliojitokeza kama ifuatavyo:
- Uongozi mzuri na uadilifu ndiyo chanzo cha maendeleo.
- Majuto ni mjukuu
- Ukaidi na dharau ni chanzo cha madhara
- Bidii katika kazi ni chanzo cha maendeleo
- Imani ni ukombozi
2.4 Falsafa
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) akimrejelea Msokile (2009) falsafa ni wazo ambalo mtu anaamini kuna ukweli fulani unaohusu maisha yake pamoja na maisha ya jamii. Katika riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ mwandishi anaamini kuwa uadilifu katika uongozi ni nguzo ya maendeleo katika jamii.
2.5 Msimamo
Kwa mujibu wa Madumulla (katajwa) ni mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii. Hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na ndiyo huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana. Msimamo wa riwaya ya Adili na Nduguze ni wa kiimani kwani amesisitiza kuachana na masuala maovu yasiyompendeza Mungu ikiwa ni pamoja na kuabudu mizimu na badala yake kutenda yale yanayompendeza Mungu na binadamu ikiwa ni pamoja na kumwabudu Mungu.
Fani katika riwaya ya “Adili na Nduguze”
Fani ni jumla ya mbinu, ufundi na mtindo wa vipengele vingine vinavyotumika kuwasilisha maudhui (Mhilu na wenzake 2008). Huu ni ufundi wa kisanaa autumiao msanii katika kutoa ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Fani imegawanyika katika vipengele vikuu viwili ambavyo ni muundo na mtindo
3.1. Mtindo
Kwa mujibu wa Senkoro (1982) anasema mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi hiyo na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa (za kimapokeo ama za pekee). Pia Wamitila (2003) anasema mtindo ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi kuwasilisha ujumbe wake, huelezea mwandishi alivyounda kazi yake.
Hivyo tunaweza kusema mtindo ni ule upekee alionao mtunzi wa kazi ya fasihi katika kuipa kazi yake sura fulani kifani na kimaudhui ambao mtunzi mwingine hawezi kufanya hivyo hata kama kinachozungumziwa ni kilekile. Mtindo ndiyo jinsi msanii alivyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika kutenda au kueleza jambo fulani. Mtindo huu ndio hutofautisha kati ya msanii mmoja na mwingine.
Katika riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’ msanii ametumia mtindo wa masimulizi katika kueleza visa na matukio, kwani tunaona msanii anaeleza kisa kinachomhusu Adili na nduguze, Hasidi na Mwivu. Mwandishi anaeleza jinsi vituko vilivyotiririka tokea mwanzo, ndugu hawa watatu waliokuwa wakitoka familia moja, ndugu wawili, (waovu) Hasidi na Mwivu, waliomfanyia Adili na malipo ya uovu huo (kama upeo wa kugeuzwa manyani na kupata adhabu ya kupigwa kila siku). Mwishoni kabisa anaujadili msamaha waliopewa ndugu hao. Kutokana na majuto na ahadi ya kutorudia tena uovu huo.
Pia msanii ametumia mtindo wa nyimbo ili kufikisha ujumbe. Mfano katika uk. 26, msanii ametumia nyimbo katika kutoa sifa ya msichana mrembo aliyekutana na Adili katika mji wa mawe. Vilevile katika uk. 42, msanii ametumia nyimbo akionyesha jinsi Adili alivyokuwa akijutia kuwaadhibu ndugu wa damu yake. Pia msanii ametumia nyimbo katika uk. 48 ambapo uliwakilisha kusherekea baada ya kupata msamaha kutoka kwa mfalme wa majini.
Aidha, msanii ametumia mtindo wa barua katika uk. 44, ambapo amemchora mfalme Rai akiandika barua kwa mfalme wa majini inayohusu kuomba msamaha kwa ajili ya ndugu zake Adili waliogeuzwa manyani kusamehewa. Na matokeo yake msamaha wanaupata na kurudi katika hali yao ya kawaida.
3.2 Muundo
. Hapa tunachunguza jinsi msanii wa kazi ya fasihi anavyofuma, unda na kuunganisha matukio moja baada ya jingine, wazo na wazo, ubeti na ubeti, hata mstari wa ubeti. Baadhi ya vipengele vya kimuundo vinavyotumika zaidi ni mistari, beti, mizani na vina. Hivyo, katika muundo tunaangalia umbo la kazi ya fasihi mfano, yaweza kugawanywa katika sura mbalimbali, sura hizi ndizo hujenga muundo
Mtindo wa riwaya hii ni mtindo wa rejea. Mwandishi huanza kuisimulia riwaya yake wakati Adili anapofanya ukatili wa kuwaadhibu manyani (ambao walikuwa nduguze). Kugundulika kwa uovu huu ndiko kulifuatiliwa na maelezo ya kisa na sababu ya nduguze kuwa manyani na hatimaye kuwa watu tena baada ya ombi la Mfalme Rai kukubaliwa na majini.
Muktadha
Muktadha ni jumla ya mazingira ambamo kazi ya fasihi inafanyikia. Muktadha wa riwaya hii ni ya nchi ya Ughaibu, yaani nchi ya mbali. Nchi hiyo ni ya kufikirika kwa kuwa haipo katika mazingira ya kawaida. Kuna vituko vichache vilivyotokea katika nchi za kigeni zisizotajwa kwa majina na vingine vilitokea katika nchi ya majini.
3.5. Wahusika
Wahusika katika riwaya ya “Adili na Nduguze”, wana majina yanayowiana na tabia zao. Wale ambao hawakubadilika kitabia kama Adili, Mfalme Rai ni wahusika bapa. Wahusika Huria, Hasidi na Mwivu ambao walibadilika kitabia ni wahusika duara. Wahusika hao na sifa zao ni kama ifuatavyo:
3.5.1 Adili
Huyu ni mhusika mkuu wa riwaya hii. Alikuwa mwema, mwenye huruma, msamehevu, mvumilivu na mwenye mapenzi ya kweli, jasiri na mfanyabiashara hodari. Tabia yake ile haikubadilika toka mwanzo hadi mwisho wa hadithi. Kwa hiyo, tabia yake ni mhusika bapa kielelezo.
3.5.2 Hasidi na Mwivu
Hawa ni ndugu zake Adili. Walikuwa watu wakatili, wenye tamaa, choyo kubwa na wabadhilifu kitabia, kwa hiyo ni wahusika duara.
3.5.3 Mfalme Rai
Huyu alikuwa mtawala wa nchi ya Ughaibu ambaye aliiletea nchi yake ustawi wa kiuchumi kutokana na uongozi mzuri, ufuatilizi bora wa kazi na ushauri wa kuwahimiza raia kuwa wachapakazi.
3.5.4 Ikibali
Huyu ni mshauri wa Mfalme Rai na halmashauri yake. Alikuwa mcheshi na mtu aliyechukuana na watu kutokana na kuwatunzia haki zao.
3.5.5 Mwelekevu
Huyu ni msichana mwenye upendo wa kweli, mrembo na mwaminifu kidini na kindoa.
3.5.6 Huria
Huyu ni jini aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kutenda kila jambo alilotaka na kujigeuza sura kwa utashi wake (mhusika duara)
3.5.7 Mfalme Tukufu na Malkia Enzi
Hawa ni watawala ambao walipuuzi/walidharau ujumbe wa Mola, wakaadhibiwa kugeuzwa mawe, mji wao na raia wao.
3.5.8 Mfalme Kisasi
Huyu ni mfalme wa majini aliyewaelekeza raia wake majini kutii uongozi wa binadamu.
3.3 Matumizi ya lugha
Williady (2015) anaeleza kuwa matumizi ya lugha ni ustadi wa msanii katika kutumia lugha itakayoleta mvuto kwa wasomaji au wasikilizaji wa kazi ya fasihi.
Lugha ya Shaaban Robert katika riwaya ya Adili na nduguze ni rahisi na inayoeleweka. Ni lugha yenye msamiati wa kawaida, misemo ya kawaida, nahau na methali nyingi. Pia ametumia lugha ya ushairi, lugha ya picha na tamathali za usemi za kipekee. Kuna wakati mwandishi huyu alipotumia lugha ya kisheria katika barua, na hayo yote ni kuonyesha jinsi ana ustadi wa kuimudu lugha ya Kiswahili katika nyanja zake zote.
3.3.1 b) Matumizi ya methali, nahau, mashairi na misemo
2.2.1.1 Misemo
Misemo ni maneno yanayotumiwa na makundi maalumu ya watu katika jamaii yaliyo jitenga kwa kufuatana na mambo yanayo pendelea, mazoea, kazi au shughuli yao, nafasi yao katika jamii. Ni semi fupi amabazo hutumiwa mara kwa mara kwa lengo la kuleta maana maalumu. (Mwansoko 1994) Misemo iliyotumika katika riwaya ya Adili na Nduguze ni;
(i) Atakaye makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu (uk. 39.)
(ii) Damu nzito kuliko maji (uk. 40)
(iii) Mwenye saburi hukidhiwa haja zake (uk. 45)
(iv) Busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hamna chembe ya wema (uk. 10).
- i)Methali
Ni usemi mfupi w matokeo unaodokeza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yatokanayo na uzoefu wa maisha ya jamii husika. Kauli fupi zenye pande mbili za fikra(www. Wikipedia.org)
Methali zilizojitokeza katika riwaya ya Adili na Nduguze ni;
(i) Mtu huchuma juani akala kivulini (uk. 14).
(ii) Mali bila daftari hupotea bila habari (uk. 12).
- c) Matumizi ya nyimbo
Katika riwaya ya Adili na Nduguze, mwandishi ametumia nyimbo ili kuwasilisha ujumbe alioukusudia kwa hadhira. Nyimbo zimetumika katika (uk.26, 42, 48)
Mfano katika uk. 26 mwandishi anasema;
“ Miguu ya msichana,
Na mwendo aliokwenda,
Adili alipoona,
Moyowe ulimshinda.
- Alikuwa na miguu,
Mfano wa cherahani,
Wala ulimwengu huu,
Hajatokea kifani.
Msanii alitumia ushairi kueleza kwa usanii uzuri wa Mwelekevu”
Tamthali za usemi
Senkoro (1984) anasema tamathali za semi ni maneno, nahau au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Pia Msokile (1992) anasema tamathali za semi ni fungu la maneno lilogeuzwa maana yake kamili ili kuiwakilisha maana nyingine.
Hivyo basi, tamathali za semi ni matumizi ya maneno kwa namna fulani ili kuifanya lugha iwe ya kuvutia na kuifanya kazi ya sanaa iwe ya kupendeza. Vipengele vya tamathali za semi ambavyo mwandishi amevitumia katika riwaya ya ‘Adili na Nduguze’ ni pamoja na tashibiha, sitiari, taswira, tashihisi na tafsida. Vipengele kama hivyo ni muhimu sana katika kuunda au kutoa msisitizo wa maana pamoja na kuunda maana mpya katika kazi ya fasihi.
– Tashbiha:
Hii ni mojawapo ya tamathali za semi ambayo inafanya kazi ya kulinganisha vitu viwili visivyo na hadhi sawa kwa kutumia viunganishi kama vile mithili ya, kama. Tamathali hii ya semi huweza kufanya kazi endapo kuna vitu vinavyolinganishwa wakati kimoja hutumiwa katika kukirejelea kingine. Katika riwaya hii ya ‘Adili na Nduguze’tashibiha zilizotumika ni pamoja na;
(i) Moyo wake ulifumwa na msiba akalia kama motto mdogo (uk.41).
(ii) Tabia yake ijigawa katika theluthi tatu mbalimbali kama rangi ya ngozi ya pundamiliya (uk. 1)
(iii) Alitoswa baharini kama kitu kilichokuwa hakifai (uk. 3)
Tashihisi
Mhilu na wenzake (2008) anasema tashihisi ni tamathali ambayo vitu visivyo na sifa walizonazo watu hupewa sifa hizo. Hivyo, tashihisi ni vitu kama vile jiwe, mti na hata kichaka hupewa sifa ya kutenda kama binadamu afanyavyo. Katika riwaya hii, Tashihisi zilizotumika ni pamoja na;
(i)Wakati umefika wa mawe kusema, miti kujibu na wanyama kuwa watu (uk. 9).
(ii) Mimea hii ilieneza neema ya vyakula kwa watu na malisho ya wanyama (uk. 3).
(iii)Mazizi yote katika miliki yake amekwishalipa kodi zake, ila mazizi ya Janibu (uk.3).
(iv)Atasema kweli, na manyani yatakuwa mashahidi (uk. 9)
Mjalizo
Hii ni aina ya tamathali za semi ambazo msanii/mwandishi huitumia kutaja vitu au mambo yaliyo katika orodha bila kutumia viunganishi
(i) Zilipatikana pacha katika mbuzi, kondoo, ng’ombe, farasi na wanyama wengine (UK. 1)
(ii) Sebule hiyo ilikuwa imesakifiwa kwa marmar za rangi tatu, yaani, nyeupe, nyekundu na samawati (uk. 5).
MAREJEO
Senkoro, F.E.M.K (1982) Fasihi. Dar es salaam: Press and Publicity Centre.
Wamitila, K.W. (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Naiobi: Focus Publishers.
26
Mhilu, G. G na Masebo, J. A (2008) Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha Tatu. Nyambarinyangwine Publishers: Dar es salaam.
Mulokozi, M. M. (1996). Fasili ya Kiswahili. Chuo kikuu huria cha Tanzania: Dar es Salaam
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Oxford University Press: Dar es saam.
Mwl Maeda