06-16-2021, 07:27 AM (This post was last modified: 06-16-2021, 07:30 AM by MwlMaeda.)
TAFSIRI ni taaluma ya lugha ambayo imefuata ukalimani baada ya ugunduzi wa maandishi. Tafsiri ni uhawilishaji wa maana iliyo katika matini ya lugha chanzi kwa njia ya kuweka maana inayolingana katika matini ya lugha lengwa.
Kwa hivyo ni shughuli au jaribio la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
Kwa ujumla, fasili hizi zote zinaonyesha kuwa tafsiri hufanyika katika maandishi. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa tafsiri ni shughuli ya uhawilishaji wa maana, mawazo, dhana au ujumbe ulio katika maandishi kutoka lugha chanzi na kuweka badala yake maana, ujumbe, mawazo au dhana inayolingana na ile ya lugha chanzi katika lugha lengwa.
Ikiwa taaluma ya lugha, tafsiri ina majukumu kadhaa ya kushughulikia. Pamoja na majukumu hayo ni kutolea matangazo, mfano katika utalii, brosha n.k. Ni njia ya mawasiliano baina ya watu wanaozungumza lugha tofauti na ni wenzo wa kueneza utamaduni hasa ikizingatiwa jinsi dini za kigeni kama vile ukristo na uislamu zilivyoingizwa nchini kwa njia ya tafsiri na ukalimani.
Tafsiri ni wenzo wa kukuza fasihi, mfano hadithi ya Alfu Lela Ulela (siku elfu moja), Treasure Island (Kisiwa Chenye Hazina), Robinson Krusoe na Kisiwa Chake, Mabepari wa Venisi n.k. waandishi waliweza kuiga mbinu za uandishi na hivyo kuwa na fasihi bora.
Aidha, tafsiri ni wenzo muhimu wa kujifunza lugha ya kigeni na kujifunza miundo na maumbo ya lugha fulani. Kwa mfano watu wanaofanya utafiti kuhusu lugha fulani hutumia tafsiri kama njia ya kuelezea lugha hizo. Tafsiri humwezesha mtu kujiajiri (kama chanzo cha ajira).
Mfasiri anapofanya kazi ya kufasiri anapata pesa na hivyo hizo pesa humsaidia katika maisha yake ya kila siku. Pia ni kama njia ya kukuza lugha kwa kuwa msamiati mwingi huingia katika lugha lengwa na hivyo kuitajirisha.
Sifa za mfasiri
Ili mtu kuitwa mtafsiri anatikwa awe anamudu vizuri sarufi za lugha zote mbili anazofanyia kazi. Anastahili awe na ufahamu wa kutosha kuhusu utamaduni wa lugha chanzi, awe ni mtumiaji mzuri wa kamusi na marejeo mengine muhimu.
Aidha, anastahili kuwa na uwezo mkubwa wa kuandika katika lugha chanzi na angalau awe na ujuzi wa kutumia kompyuta.
Kuna mambo muhimu ambayo mtafsiri anatakiwa kuyazingatia katika kutafsiri matini. Mtafsiri atalazimika kusoma matini yote kabla hajaanza kutafsiri. Anapaswa kufanya hivyo ili aweze kuelewa kinachozungumzwa – ujumbe uliomo. Aweze kuandaa marejeleo muhimu anayohitaji kama vile kamusi, vitabu n.k. ili vimfae katika jitihada za kubaini aina ya matini pamoja na matatizo yanayojitokeza katika matini husika na kuweza kuyatatua matatizo hayo.
Kuna uwezekano wa kuwapo kwa matatizo ya kitahajia katika tungo ambazo hazijakamilika.
Mtafsiri anastahili kuigawa kazi katika vipande kama ni ndefu au inashughulikiwa na watu wengi.
Ingawa hivyo, kuna mwingiliano mkubwa kati ya tafsiri na taaluma nyinginezo kama hizi zifuatazo:
Semantiki
Hii ni taaluma inayohusiana na maana. Katika tafsiri tunazingatia maana ya lugha chanzi ili isitofautiane na maana ya lugha lengwa. Muktadha pia sharti uzingatiwe katika kupata maana.
Isimujamii
Huangalia jamii inavyoathiri lugha na lugha inavyoathiri jamii. Katika taaluma ya tafsiri, tamaduni, mila, itikadi na desturi za jamii husika huzingatiwa.
Mfano unapokutana na maneno ya kitamaduni katika tafsiri kama vile salamu, vyakula n.k hapa inabidi utamaduni wa lugha husika uzingatiwe.
Isimu Linganishi
Katika tafsiri, tunalinganisha lugha moja na nyingine ili kuelewa miundo na maumbo kati ya lugha chanzi na lugha lengwa. Kwa hivyo isimu linganishi huchukua nafasi yake hapa.
Elimu mitindo
Kuna uainishaji wa mitindo ya lugha na muktadha wa matumizi yake katika tafsiri, kitu ambacho kipo pia katika taaluma ya elimu mitindo.
Uhakiki wa matini
Kabla mtafsiri hajaanza kutafsiri matini, ni lazima ahakiki matini chanzi kwa lengo la kubaini upungufu unaojitokeza ili kujua namna ya kuweza kukabiliana nao.
Mantiki
Hii ni taaluma inayohusu ukweli na usahihi katika kauli au matini fulani. Taaluma hii humsaidia mtafsiri kubaini usahihi na mantiki iliyopo katika lugha chanzi.
Falsafa
Ni taaluma inayosisitiza kutafuta maana za maneno kutokana na matumizi halisi katika matini. Hii humsaidia mtafsiri kujua falsafa ya matini husika na hatimaye kuelewa maana yake.