06-25-2021, 07:04 PM (This post was last modified: 06-26-2021, 04:23 AM by MwlMlela.)
YALIYOMO
1.0 Utangulizi…………………………………………………………………………….
1.1. Sababu za Anguko la Mfalme Edipode……………………………………………
1.2. Athari za Anguko la Mfalme Edipode…………………………………………….
1.3. Hitimisho……………………………………………………………………………..
1.4 Marejeleo…………………………………………………………………………………
1.0 UTANGULIZI
Mfalme Edipode ni tamthiliya iliyoandikwa na Sofokile (Sophocles) na kufasiriwa na Samwel S. Mushi mnamo mwaka 1993; tamthiliya hii imeandikwa kwa kufuata lugha ya ushairi ili kumpa hali ya mvuto msomaji.
Tamthiliya imejikita zaidi katika kuzungumzia anguko la Mfalme Edipode juu ya jamii yake ya Thebe, katika tamthiliya hii kuna wahusika wafuatao; Edipode ambaye ni mhusika mkuu na wahusika wengine kama vile Jokaste, Kreoni, Teresia, Kahini, pamoja na mtumishi, Mfalme Laio, Polibo na wengine.
Katika uchambuzi huu tumeongozwa na nadharia ya urasimi (Classicism). Nadharia hii huzingatia wakati maalumu ambapo misingi ya kazi za sanaa huwekwa na kukubalika kuwa vipimo bora kwa kazi nyingine, hivyo kila jamii ina urasimi wake. Lakini urasimi wa fasihi ya Kiswahili ulikuwepo kati ya karne ya kumi na nane na kumi na tisa, na ule wa kimagharibi hasa Kigiriki na wa Kiroma ulikuwepo tangu karne ya nne (4) kabla ya Kristo na baada ya Kristo. Nadharia hii huenda sanjari na tamthiliya ya Mfalme Edipode ambayo imejikita katika urasimi mkongwe kama inavyoelezwa na mwandishi Sofokile: alizaliwa Athens, Ugiriki mwaka 496 kabla ya Kristo na aliishi miaka tisini. Aliishi nyakati ambazo mambo mengi yalikuwa yakitokea ugiriki. Hivyo michezo ya kuigizwa ilipendwa sana na Wagiriki wa nyakati hizo na maigizo hayo yalikuwa ya aina tatu; Maigizo ya huzuni, maigizo ya vichekesho na maigizo ya huzuni na vichekesho. Hivyo basi Mfalme Edipode alipata anguko.
Kulingana na TUKI (1990) Anguko ni hali ya kushindwa kwa kuendelea kwa jambo fulani, sasa basi Mfalme Edipode alipata anguko katika jamii ya Thebe na kuwa mwisho wa utawala wake katika jamii hiyo. Anguko hilo la mhusika mkuu lilitokea kwa kuwepo kwa sababu mbalimbali hususani kuwepo kwa nguvu za kiungu.
1.1 SABABU ZA ANGUKO LA MFALME EDIPODE
i. Kuwepo kwa utabiri wa Mungu jua (Apolo) juu ya Mfalme Edipode, Mungu jua (Apolo) alitabiri kwamba mwana wa Mfalme atakayezaliwa atamuua baba yake na kumuoa mama yake. Hali hii ilitimia kwa Mfalme Edipode katika kipindi cha utawala wake ndani ya jamii ya Thebe. Hali hii ilitokea kwa kuwa Mfalme Edipode hakutambua ukweli. Na nukuu:
Mchunga; Ndiyo bwana walisema kuna utabiri mbaya,
Edipode; utabiri wa Namna gani?
Mchunga; uliosema angelimuua baba yake na kumuoa mama yake (UK. 48)
Ujaala (majaliwa au utabiri) ya Mfalme Edipode; Baada ya utabiri Jaala ilitimia kwa Mfalme Edipode kwa kumuua baba yake na kumuoa mama yake kama mke na mume. Hivyo basi mambo hayo yalisababisha madhara makubwa katika jamii ya Thebe kama vifo na njaa baada ya Miungu kukasirika na hatimaye kuwa sababu ya anguko la Kiutawala kwa Mfalme Edipode katika jamii ya Thebe. Na nukuu:
“…Mauti kwenye rutuba na neema, mauti kwenye malisho ya wanyama, mauti kwenye tumbo la uzazi na maradhi yaliyo maambukizi…” (UK 2)
ii. Kutokujua historia ya jamii ya Thebe: Mfalme Edipode hakuijua historia halisi ya jamii ya Thebe kwani yeye alilelewa katika nchi ya Korintho chini ya Mfalme Polibo na
mkewe Melope. Hivyo Mfalme Edipode aliamini kuwa hao ndio wazazi wake na hivyo alitambua vyema historia ya Korintho kuliko jamii ya Thebe. Na nukuu: “Edipode akakua akawa mtu mzima akapendwa na wazee wake na kumlea na raia wa Korinto. Wakamstahi kama mwana wa Mfalme wa Korinto lakini Edipode hakufahamu kwamba alikuwa mtoto wa kulelewa…” (XVI)
iii. Mfalme Edipode kutaka kujua juu ya madhara ya nchi yake Sanjari na jamii yake ya Thebe kutokana na madhara yaliyoikumba ikiwemo vifo pamoja na njaa. Jamii ya Thebe ilikumbwa na madhara mengi ikiwemo kukumbwa na magonjwa najisi, Njaa, Ukame, maumivu ya uzazi, kwa mimea tasa, Barabara za mji zikawa na uvundo (Uk. 8 -9). Hivyo ilipelekea Mfalme Edipode kutaka kujua madhara hayo yametokana na nini ndipo ukweli ulidhihirika kwamba chanzo cha hayo yote ni yeye mwenyewe juu ya jaala alizopata kutoka kwa Miungu ya Thebe. Hivyo ilipelekea anguko kwa Mfalme Edipode kwa kuacha utawala ili kuepusha matatizo katika jamii ya thebe.
1.2 ATHARI ZILIZOIKUMBA JAMII YA THEBE BAADA YA ANGUKO LA MFALME EDIPODE.
Kutokana na Anguko la mhusika mkuu Mfalme Edipode athari mbalimbali ziliweza kuathiri jamii nzima ya Thebe, waliohai, waliokufa, mizimu, na miungu. Athari hizo ni kama ifuatavyo:
i. Watoto wa kike wa Edipode hawataweza kuolewa kwa sababu ni kizazi cha laana. Hii ina maana kuwa watoto wa Mfalme Edipode yaani Usmene na Antigone hawataweza kuolewa kwani ni kizazi cha laana iliyofanywa na Edipode kumuoa mama yake Jakasta ambapo Usmene na Antigone walipaswa kuwa wadogo zake. Na nukuu:
‘’Mtakapopata kuolewa, mtu gani, nani huyo atakuwa shujaa wa kutoijali najisi ambayo itawaletea mkosi wanangu na hata wajukuu wenu? Hivyo hii ni athari kwa waliohai.” (UK. 50-59)
ii. Kifo cha Jokaste,
Kutokana na utabiri kuwa Mfalme Edipode atatembea na mamaye hivyo baada ya malkia kujua ameolewa na mtoto wake ilisababisha malkia kujinyonga na kusababisha anguko la Mfalme Edipode ambaye alijitoboa macho kwa ajili ya kuficha aibu na kutaka kutoyaona mambo yanayotendeka. Na nukuu:
Mtumishi: kwanza kwa kifupi Malkia.. kafa
Wazee: roho maskini ajali gani hiyo?
Mtumishi: ni tendo la mkono wake mwenyewe… (UK. 50)
iii. Wananchi wa Thebe kufa kwa njaa na magonjwa: Hii yote ni kutokana na laana iliyo- wapata watu wa jamii ya thebe kutokana na Mfalme Laio kuzaa mtoto ambaye alikataliwa na miungu na kusababisha miungu kukasirika.
iv. Miungu yao kuwalaani kwa kuwapa ardhi kame. Miungu kama Apolo na wengineo walilaani jamii ya Thebe na kuiathiri jamii hiyo kwa ardhi kuwa kavu na kame. Hivyo hii ni athari iliyokumba walio hai katika jamii ya thebe.
1.3 HITIMISHO
Anguko la Mfalme Edipode ni funzo tosha kabisa kwa viongozi wengi walio madarakani kutojua historia za nchi zao na hatimaye kusababisha athari kubwa ikiwemo vifo kwa jamii nzima.. Pia inatakiwa kufuatilia mawazo ya viongozi wetu waliopita na maonyo ya wazee juu ya uendeshaji wa nchi,. Mambo haya yaliyojitokeza katika tamthiliya ya Mfalme Edipode ni dhahiri kuwa yamejitokeza katika nchi mbalimbali za kiafrika na kusababisha kuanguka kwa utawala.
1.5 MAREJELO
Bakhressa S.K (1992); Kamusi ya maana na matumizi Oxford University press, Nairobi.
Njogu K. (2007); Nadharia za uhakiki wa fasihi, Industries Ltd, Nairobi
Njogu K. (1999); Ufundishaji wa fasihi, Nadharia na mbinu; Autolitho Ltd; Nairobi
Sokofile (1993), Mfalme Edipode
Wamitila K.W (2003); kamusi ya fasihi Istilahi na Nadharia, Focus publications Ltd; Nairobi