10-18-2021, 04:40 PM (This post was last modified: 10-18-2021, 04:41 PM by MwlMaeda.)
MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2021, unaoruhusu sasa lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya Sheria na Mahakama umepitishwa rasmi na Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba, ndiye aliyewasilisha muswada huo bungeni leo unaopendekeza kufanyiwa marekebisho katika sheria tatu ambazo ni Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1, Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Sura ya 216 na Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11.
Alisema katika Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 84 ili kuondoa matumizi ya lugha ya Kiingereza kama lugha ya sheria na lugha ya Mahakama na badala yake kutumia lugha ya Kiswahili.
Waziri huyo alieleza kuwa lugha hiyo ya Kiswahili ndiyo lugha ya taifa inayoeleweka na inatumika katika shughuli zote za maendeleo nchini.
Alisisitiza kuwa kutumika kwa lugha hiyo kisheria na kimahakama kutasaidia upatikanaji wa haki nchini.
“Marekebisho haya yanakusudia kuimarisha mfumo wa upatikanaji haki kwa wananchi ambao ndio watumiaji wa sheria husika. Mapendekezo haya yamezingatia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya tafsiri za Sheria ambayo imeweka msingi wa lugha ya mahakama, mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili," alieleza.
Alisema kwa mujibu wa marekebisho hayo, pia yanapendekeza vyombo vya utoaji haki kutumia lugha ya Kiingereza pale itakapoonekana ni muhimu kufanya hivyo kwa maslahi ya utoaji haki kwa mashauri husika..
“Hata hivyo, endapo chombo cha utoaji haki kitalazimika kutumia Kiingereza tafsiri ya mwenendo na uamuzi kuhusu shauri husika itatolewa mara moja," alisema.
Waziri huyo alisema kuwa kupitia marekebisho hayo Waziri wa Sheria anapewa mamlaka ya kutunga kanuni ili kubainisha mazingira ambayo lugha nyingine zinaweza kutumika katika kutunga sheria au katika mfumo wa utoaji haki.
Alisema pia Jaji Mkuu anapewa Mamlaka ya kutunga kanuni kwa ajili ya kutoa mwongozo ili kubainisha mazingira ya lugha ya kiingereza inaweza kutumika katika utoaji wa haki.
Waziri huyo alisema muswada huo pia unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Sura ya 216 na Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 kwa kufuta vifungu vinavyoweka sharti kuhusu lugha ya Mahakama na sasa itatumika kiswahili.
Mapendekezo hayo yamezingatia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Tafsiri za Sheria ambayo imeweka msingi wa lugha ya Mahakama, mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili.
Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, kupitia Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohammed Mchengerwa, ailishauri serikali kuweka kifungu kinachompa mamlaka Waziri ya kutangaza tarehe ya kuanza kutumika sheria hiyo.
Pia, kamati hiyo ilishauri kuwepo kwa mwongozo maalumu utakaobainisha namna ya kushughulikia mashauri yanayoendelea kwa sasa mahakamani.