Kilio, kilio, kilio kwa kijana wa leo, Afrika! Wakati vijana wengine wanapoombwa kujiunga na jeshi ili kujenga na kulinda nchi yao, siyo kwangu. Kwangu naburutwa msituni, kujiunga na jeshi kuendeleza vita ya wenyewe kwa wenyewe. Napigana na ndugu zangu ndani ya taifa moja ili matumbo machache yafaidi almasi, dhahabu, mafuta na maliasili nyingine. Naingizwa katika vita isiyo na maana yoyote kwangu.
Nikitaka kutafuta elimu, hakuna madarasa. Upepo umeezua paa la nyasi la shule yetu! Nikibahatika kupata kaelimu kadogo; chini ya mti, nazuiwa kufikiri zaidi. Naambiwa kuwa, Afrika hakuna kufikiri! Mtu mweusi hana fikra ila mtu mweupe ndiye mwenye fikra. Natakiwa nifuate fikra zake!
Nikitaka ajira, naambiwa uzoefu miaka mitano au kumi na zaidi. Uzoefu nitaupata wapi? Nikitamani kujiajiri mazingira hayaniruhusu: Umasikini, umasikini tena umasikini umenikumbatia! Nikijiunga na siasa, wimbo maarufu kote ulimwenguni ni demokrasia.
Demokrasia ina mizengwe, umajimbo, ukabila, udini, ubabe, rushwa, ubabaishaji, yutapeli na kushindana bila kukubali kushindwa. Siasa barani kwetu ni kiini macho na matokeo yake ni ‘demoghasia’ isababishayo vifo. Ubinafsi umejaa! Kujipitishia marupurupu kibao! Ubaguzi! Majigambo! Dharau…..!
Nikitaka kusema, naambiwa mjinga, Nikidai haki, naambiwa madai yangu ni ya kijinga. Nalazimishwa kuandika barua ya kuomba msamaha na kuahidi kuwa sitadai haki tena! Nalazimishwa kuwa bubu. Kijana msomi nanyimwa uhuru wa kutoa mawazo yangu mbele ya jumuiya yangu. Kijana msomi nafungwa mdomo. Kijana msomi kukaa na kunyamaza kimya ni usaliti. Usaliti kwa jamii ya walipa kodi ambao pesa zao zimenisomesha hadi kuitwa msomi. Kijana msomi, kutofikiri ni dhambi nyekundu pyuuu!- isiyosameheka. Msomi kutofikiri ni kifo cha kifikra kwangu mimi kijana wa
Kiafrika. Chochote ninachotaka kufanya kinanikatisha tamaa. Nikiwa ‘deiwaka’ mpiga debe, kila siku nitaamkia korokoroni! Nikitaka kujiburudisha na gongo au viroba – ni kifo cha ajabu. Nikibugia unga – kwangu ni kifo cha mende wekundu! Nikijiingiza kwenye ukahaba, natozwa kodi ya maendeleo!
Nikitaka kuwa “changudoa”, UKIMWI unaniwinda kama mamba awindavyo viumbe baharini! Sasa nifanye nini? Balaa kubwa kwangu! Nikiamua kuokoka, wokovu hauonekani. Nimebaki njia panda. Mchungaji amekuwa mwongo, katu hasemi ukweli. Ananilaghai kuwa wokovu upo karibu kuingia badala ya kuniambia kweli wokovu umekwishatoweka. Naambiwa kuwa nijiwekee hazina mbinguni ambako kutu na wadudu hawataharibu mali yangu…Huu ni utapeli.
Ingekuwa vizuri kama ningeelezwa wazi jiwekee akiba tumboni mwa sheikh au tumboni mwa mchungaji au tumboni mwa padre! Naambiwa kuwa toeni ulichonacho utabarikiwa badala ya kuambiwa kuwa kitayabariki matumbo ya wachache! Nakumbuka wakati mama yangu alipokuwa mwalimu katika shule ya msingi ya Mabonde Kuinama, aliniambia kwamba, urithi wa utamaduniwetu ni mila na desturi za Afrika. Lakini siku hizi sivyo. Siku hizi naambiwa kuwa urithi wa kizazi kipya ni bia aina ya “Safari Larger”.
Kijana wa sasa naangalia wizi wanaofanyiwa watu maskini lakini sisemi chochote. Najinyamazia kimya. Wizi umo makanisani, misikitini, Ikulu, mahakamani na hata bungeni. Lengo ni kuwanyanyasa, kuwadhulumu, kuwaonea, kuwanyonya na kuwadhalilisha wanyonge. Hakika kunyamaza kwangu ni usaliti. Nimeitambua nafsi yangu. Naahidi kupambana hadi kufa na kupona.