WADAU wa lugha ya Kiswahili wanaendelea kulalamika kwamba mchango wa wale walio katika vyombo vya habari kufikia sasa wahitaji kuimarishwa zaidi ili uweze kuikuza lugha kwa njia ifaayo.
Majuzi niliisikia kauli hiyo ikikaririwa tena na magalacha wawili wa Kiswahili Prof. Ken Walibora na mwenzake Wallah bin Wallah. Walilalamikia matumizi ovyo ya lugha katika vyombo hivi muhimu ambavyo vinawafikia Wakenya wengi ambao wanaamini kuwa kila kinachotangazwa ama kuandikwa ni sahihi na ni rasmi.
Mabingwa hao wa lugha walilalamikia ukasuku mwingi unaojitokeza miongoni mwa watumizi wa Kiswahili hasa kwa wale ambao hawataki kufanya utafiti wowote baada ya kuyasikia matumizi fulani ya lugha kisha kuyakariri na matokeo yake ni kuiboronga lugha.
Wanasema, “Makosa mengi yanatokea kutokana na matumizi mabaya ya msamiati, semi na tafsiri potoshi za wanahabari ambao ni wavivu; wasiotaka kuchoka kwa kufanya utafiti ama wanaojiamini mno. Kwa desturi wanapolisikia neno likitumiwa katika mazungumzo ama maandishi nao hulidakia na kulitumia bila kujali kuijua maana yake na muundo wake vizuri.”
Jambo la kwanza linalokera ni kiimbo kinachojitokeza kwa kila mmoja wa wasomaji wa habari katika radio na televisheni zetu wakiamini kuwa hiyo ndiyo fasheni ya kusoma habari.
Usomaji habari
“Aghalabu inakuwa vigumu kuwatofautisha wasomaji hawa wa habari kutokana na kila mmoja wao kuiga usomaji wa mwenzake. Wataimba na utadhani kwamba wamefundishwa kufanya hivyo na ajabu ni kwamba mtindo huo hauongezi thamani yoyote katika utangazaji,” anasema Wallah bin Wallah.
Kulingana na bingwa huyo, msomaji anafaa kusoma akizingatia tu kiimbo kile cha kawaida cha kupanda na kushuka kwa matamshi, kusisitiza ujumbe na pia kuhifadhi uhalisia wa msomaji.
Itakuwa rahisi kujua kwamba mtangazaji Leornard Mambo Mbotela yumo studioni kwani tunaijua sauti yake. Na hata tunapokutana naye nje ya studio tunaihusisha ile sauti yake na yeye mwenyewe. Hatuelewi kwa nini kuwe na sauti nyingine za ajabu ajabu ambazo ni za kuiga tu na wala hazihusiani kwa vyovyote na mtangazaji mwenyewe.
Wataalamu hao pia walilalamikia sana tafsiri mbovu katika vyombo vyetu vya habari. Ni tafsiri ambazo zinafanywa kiholela na kupotosha maana kabisa kwa wasikilizaji na wasomaji. Inafaa kuzingatiwa kwamba tunapotafsiri tunatafsiri wazo kuu linalozungumziwa katika habari wala si neno kwa neno.
Wakati tunapotafsiri food security kuwa usalama wa chakula bila shaka kuna dosari. Wazo kuu hapa ni hali ya nchi kuwa na akiba ya kutosha ya chakula; yaani ule uhakika wa kuwa na chakula cha kutosha. Tumewahi pia kusikia Shahada ya Makapera wa Sayansi kumaanisha Bachelors of Science degree! Hii kwa hakika ni shahada ya kwanza tu, ya pili ndiyo tuiitayo Shahada ya Uzamili na kisha ya tatu inakuwa Shahada ya Uzamifu. Hizi tafsiri sisisi tutaziepuka lini jamani?
Semi
Matumizi ya semi zisizo na maana pia nayo yamevamia sana vyombo hivi vya habari. Makosa ya kimsingi kama kusema, “Timu yetu tuipendayo ya Man U iliweza kufungwa mabao matano bila na Chelsea hapo jana. Mwingine anasikika akisema: “Ajali ya kutisha imetokea na abiria zaidi 10 wameweza kuaga dunia.”
Kauli hizi zinashangaza kwani dhana tuipatayo ni kwamba kumekuwa na jitihada ya kufungwa kwa muda mrefu na jana ndipo timu hiyo ya Man U imefungwa. Imekuwa ikijitahidi! Je, timu inahitaji kujitahidi ili ifungwe? Je, mgonjwa anahitaji kufanya jitihada gani ili afe? Haya ni maajabu!
Hata juzi nimesoma katika gazeti la Tanzania la Mwananchi kwamba tuna methali isemayo: Mbaazi ikikosa maua husingizia jua. Mbaazi (I-ZI) haina maua. Kinachokuwa na maua ni ule mmea Mbaazi (mmea uzaao mbaazi (U-ZI). Kwa hivyo, ni mbaazi ukikosa maua husingizia jua.
Ushauri wa wataalamu hawa ili kuyakabili matatizo haya ni kusoma kwa bidii na kuyafanyia utafiti maneno mapya, methali na semi mpya kabla ya kujitosa tu katika matumizi yake. Ni muhimu kuwa na hakika ya kile kinachotangazwa kwa wananchi na vyombo hivi vya habari ili kuepuka kuwapotosha.
Kwa kauli moja iliafikiwa kuwa suala la kuimarisha lugha na kuisanifisha kutafaulu tu iwapo baraza la Kiswahili la taifa litaundwa na kuisimamia inavyotakikana. Baraza litabuni sera mwafaka za kuiongoza lugha ili kufikia malengo ya taifa na wala si ya kundi moja la kibinafsi.