09-14-2021, 05:10 PM
Maelezo ya Jumla
Katika sehemu hii tunajumuisha maandishi yenye kuonyesha misimamo mbalimbali juu ya swala la wanawake katika nchi nyingine za Afrika, Dunia ya Tatu, na mashirika ya kimataifa yanayosaidia hasa “nchi zinazoendelea”, Tanzania ikiwa mojawapo. Ilibidi tuchague maandishi machache tu kwa vile bibliografia hii inasisitiza zaidi Tanzania. Maswala makuu yanayojadiliwa katika maandishi haya ni mabadiliko ya mgawanyo wa kazi za uzalishaji na uendelezaji wa jamii kutokana na jinsi; hali na nafasi ya wanawake kama wakulima na wafanyakazi, mgawanyo wa kazi duniani na maswala yanayohusu mbinu za utafiti.
Mgawanyo wa Kazi Kutokana na Jinsi
Kihistoria wanawake wa Afrika wamefanya kazi nyingi za uzalishaji wa kilimo pamoja na kazi za kutunza familia au jamii nzima. Uchunguzi uliofanywa na Jeanne Henn (kitomeo 7) unadhihirisha kwamba sehemu mbalimbali za Afrika kabla ya ukoloni zilitofautiana katika mgawanyo wa kazi za kilimo kutokana na jinsi. Tofauti hizo zilitokana na sababu mbalimbali. Baadhi yake ni, aina ya mahusiano ya uzalishaji mali yaliyokuwepo kabla ya ubepari (kwa mfano: mahusiano ya kiumeni yenye msingi wa ukoo, mahusiano ya kikabaila au ya utumwa); mazingira ya ekolojia na mahusiano ya kisiasa na kiitikadi pamoja na mahusiano ya kiuchumi. Kwa hiyo mtu hawezi kutoa tamko sahihi la jumla linalohusu “wanawake katika Afrika”, hasa anapojadili kame zile za kabla ya ukoloni, wakati ambapo jamii za Afrika zilikuwa zinabadilika sana (tz. kitomeo 9).
Uchambuzi wa mgawanyo wa kazi kutokana najinsi unaonyesha kwamba wanawake wa Afrika ni kikundi cha wafanyakazi wanaoajiriwa au wanaofanya kazi kwa mapato madogo sana. Isitoshe, kazi zinazofanywa na wanawake shambani na nyumbani zinawapatia mshahara mdogo na bei ndogo ya mazao. Mshahara wa mfanyakazi haujumuishi hela zote zinazotumiwa kutunza familia. Hali kadhalika bei za mazao (tz. vitomeo 7, 8, 15, 18 vinavyotoa msimamo mbalimbali juu ya tatizo hili).
Wanawake Katika Kazi za Kuajiriwa na Uzalishaji wa Wakulima
Kwa jumla wanawake wanaofanya kazi viwandani wanapewa kazi zile zenye mshahara mdogo, yaani kazi zisizohitaji ufundi wowote, kazi zile “chafu”. Katika wafanyakari wanaoajiriwa kwa muda tu, wanawake ni wengi, na hawapati marupurupu ya wafanyakazi wengine na sheria za haki ya kufanya kazi’ haziwahusu (tz. vitomeo 5, 8, 9 na vingine katika sura zinazofuata). Katika uzalishaji wa kilimo wa kibepari, wanawake wanapewa kari zenye mshahara mdogo zisizohitaji ufundi. Wanawake wakulima wanafanya kazi za kulima mazao ya biashara bila kulipwa. Kwa kawaida wanatakwimu na wanauchumi “hawahesabu” kari hizi au wanaeleza kwamba ni “kazi zinazofanywa na familia, kazi zisizolipwa” (tz. vitomeo 3, 10, 13).
Mgawanyo wa Kazi Duniani
Kazi na mtaji unazidi kutawaliwa na soko la kimataifa na mahitaji yake. Ukweli huu unatusaidia kueleza kwa nini viwanda vingi vya makampuni ya kimataifa vya kutengeneza bidhaa za kuuza nje vimezuka katika nchi za Dunia ya Tatu. Viwanda vinavyoajiri wafanyakazi wengi badala ya kutumia mashine, kwa mfano viwanda vya nguo, ngozi na vyombo vya umeme, vinahamia pale palipo na wafanyakazi wanaoajiriwa kwa mshahara mdogo. Wafanyakazi hawa mara nyingi ni wanawake waliohamia kutafuta kazi (tz. kitomeo 5). Kwa kiasi fulani, sera ya Benki ya Dunia kuhusu Tanzania inatokana na haja ya mabepari wafanya biashara ya kilimo kupata soko kwa kuuza mbolea, dawa za kuua vidudu waharibifu, mbegu na chakula katika nchi za Dunia ya Tatu (tz. kitomeo 20), kama ilivyoelezwa kwa mfano katika Ripoti ya Maendeleo Duniani 1980 (Benki ya Dunia 1980). Msingi mmoja wa ripoti hii ni dhana ya “nafiiu linganishr (comparative advantage). Nchi zinazoendelea zitakuwa na nafuu zaidi zikijenga viwanda vinavyotengeneza bidhaa au vyakula vya kuuza nje badala ya kujenga viwanda vya msingi na kuuza nje bidhaa/vyakula vilivyotayarishwa viwandani kwa mauzo. Dhana hii ya nafuu linganishi inakubaliana moja kwa moja na muundo wa uchumi wa dunia na mgawanyo wa kazi duniani. Inatumiwa kutetea sera zinazojaribu kurekebisha uchumi wa nchi zinazoendelea ili upatane vizuri na muundo wa uchumi wa dunia.
Lakini ukweli ni kwamba sera inayosisitiza biashara na uzalishaji wa biashara za kuuza nje inazifanya nchi zinazoendelea kutegemea zaidi soko la dunia. Pia uchumi unazidi kutawaliwa na matakwa ya mtaji wa kihodhi. Nchi zinazoendelea haziwezi kushindana na soko la dunia la kibepari. Na haziwezi kujenga uchumi unaojitegemea zikiwa bado chini ya uchumi wa soko la dunia. Sera zinazokuzwa na Benki ya Dunia zinapingana na faida ya nchi zinazoendelea na hasa faida ya wakulima na wafanyakazi. kwa mfano, kutokana na hali ilivyo sasa, sera ya kulima mazao ya kuuza nje ni sawasawa na kujiua. Nchi inayouza vyakula vingi duniani ni Marekani. Serikali ya Marekani inatumia chakula kama silaha. Kwa mfano mwaka 1981 serikali ile ilikataa kutoa chakula kwa serikali ya Msumbiji na El Salvador kwa sababu ya sera ya kimapinduzi ya nchi hizo mbili. Hii ingeweza kutokea hapa Tanzania vilevile. Vilevile serikali ikilegeza sheria zinazohusu kusafirisha na kuingiza bidhaa, na ikaachia huru nchi za kigeni kuleta kitega uchumi hapa, uchumi wa nchi ungetawaliwa kabisa na mtaji ulioko nje. Serikali ikipunguza matumizi yake kwenye shule na huduma za afya, huduma hizo zitakufa kabisa, kwa sababu sasa hivi zinapewa hela kidogo sana za matumizi. Isitoshe, sera kama hizo zingeongeza umaskihi wa wananchi kwa jumla; zingekiuka msingi wa serikali za kimapinduzi kama Tanzania, na zingeleta fujo sana ya kisiasa. Kwa hiyo ingawa Benki ya Dunia ina sura ya kuwa shirika la kifedha, ukweli ni kwamba madhumuni yake ni kuimarisha faida ya mtaji wa kihodhi, na hasa wa Marekani.
“Msimamo nafuu” wa Benki ya Dunia unasisitiza haja ya kupunguza umaskini na kukuza maendeleo ya binadamu, yaani afya, lishe, elimu na uzazi. Vipengele hivi vyote havijaendelea sana. Ripoti ya Benki Kuu ya Dunia haikuzingatia kabisa uhusiano uliopo kati ya uenezaji wa ubepari na kuongezeka kwa umaskini, yaani mambo kama ukosefu mkubwa wa chakula bora, vifo vya watoto wengi na uhafifu wa elimu ya shule. Badala-ya kutambua kwamba msingi wa umaskini huo ni ubepari, Benki “inalaumu” ujinga wa maskini na kupendekeza utatuzi wa kiteknolojia, kwa mfano matumizi zaidi ya dawa za kuua mbu, kupunguza malaria (dawa ambazo ni dhahiri zitanunuliwa kutoka kwenye makampuni ya kimataifa). Ripoti inaonyesha wasiwasi mno juu ya jinsi idadi ya watu inavyoongezeka katika nchi zinazoendelea. Kuongezeka kwa idadi ya watu kunahusiana na umaskini na uwezekano wa kuzuka kwa mapinduzi au fujo ya kisiasa. Kwa hiyo Ripoti inasisitiza sana umuhimu wa kuchukua hatua za kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa. Hapohapo, haizingatii mambo muhimu yanayohusiana na swala la idadi ya watoto wanaozaliwa, yaani tatizo la vifo vya watoto wengi wachanga na jinsi wakulima wengi wadogo wanavyowategemea watoto kuongeza uzalishaji wa mazao. Ripoti inataja wanawake katika uzalishaji wa wakulima wadogo, hasa nafasi yao katika kuzalisha vyakula na katika maswala kama elimu, afya, lishe na uwezo wa kuzaa. Aya moja inataja kwamba wanawake, watoto na wakongwe ni “maskini wasiojitegemea?” Maneno haya hayana ukweli na yanatupotosha katika kuelewa nafasi ya wanawake kama wakulima wazalishaji au wafanyakazi katika nchi zinazoendelea.
Takwimu zinazoorodheshwa katika nyongeza ya ripoti ni pamoja na takwimu muhimu juu ya Tanzania, k.m idadi ya watoto wachanga wanaokufa, elimu ya wasichana na wavulana, kiwango cha lishe, cha uzazi, cha uajiri (wanawake kwa wanaume) n.k. Benki ya Dunia ni kituo kikubwa sana cha uchunguzi duniani. Ina uwezo wa kupata data nyingi za siri na inawaajiri wachunguzi wengi. Ingawa wapinzani wa Benki ya Dunia wanapinga mbinu za uchunguzi na sera ya Benki, wanategemea data yake kwa sababu mara nyingi ni data iliyokusanywa hivi karibuni hata kuliko data inayopatikana kwenye nchi zinazoendelea zenyewe.
Sisi tunajadili sana ripoti hii ya Benki ya Dunia kwa sababu hivi sasa Benki hii ina uwezo mkubwa sana wa kuongoza sera za kiuchumi na kisiasa duniani na hasa katika nchi zinazoendelea. Benki inatilia mkazo kwenye nchi “maskini kabisa”, Tanzania ikiwa mojawapo. Katika nchi hizo, inatilia mkazo tabaka maskini kabisa, yaani wakulima maskini, wafanyakazi na watu wa mijini wasio na kazi. Tanzania imekuwa uwanja wao wa majaribio katika mapambano kati ya mtaji wa kihodhi unaotetewa na Benki ya Dunia, na serikali zilizo mstari wa mbele. Sera ya Benki ya Dunia hazitanufaisha wanawake wakulima na wafanyakazi wa Tanzania. Kwa hiyo ni muhimu sana kwa wanawake kutafuta taarifa zaidi juu ya Benki ya Dunia na hasa miradi na mipango yake hapa Tanzania na sera ambazo inazikuza hapa.
Matatizo yanayokabili wanawake wakulima na wafanyakazi yana uhusiano na mgawanyo wa kazi duniani. Jambo hili ni la kimsingi katika majadiliano ya kukataa au kukubali Mpango Mpya wa Uchumi Duniani yanayofanywa huko kwenye Umoja wa Mataifa na penginepo (tz. vitomeo 8, 15, 18). Mkutano wa Dunia juu ya Miaka Kumi ya Wanawake umefanikiwa kuingiza swala la wanawake katika miradi na mbinu za maendeleo. Mapambano haya yamezusha uchunguzi mwingi juu ya wanawake na kazi. Ilionekana kwamba theluthi moja ya wakuu wa familia duniani pote ni wanawake. Jambo hili linadhihirisha mabadiliko makubwa yanayotokea katika mfumo wa familia na uendelezaji wa jamii. Kutokana na uchambuzi huu, wito umetolewa wa kutafuta teknolojia inayopunguza kazi za kilimo, hifadhi na uchukuzi wa mazao na hata utayarishaji wa vyakula pamoja na kuleta maji safi na kutafuta nishati ya aina nyingine (vitomeo 10, na 19). Ukweli kwamba wanawake ndio wazalishaji wakubwa wa chakula na utendaji yanayohusu uhaba wa chakula duniani (tz. kitomeo 19). Mara nyingi tatizo kubwa ni kuwepo kwa dhana ya kwamba kazi za wanawake katika uzalishaji na uendelezaji wajamii hazionekani wazi (tz. vitomeo 11 na 20). Kama kweli hili ndilo tatizo kubwa, kuna haja ya kufanya uchunguzi na kuwaelimisha viongozi juu ya mchango mkubwa wa wanawake katika uzalishaji.
Lakini msimamo huu wa kusisitiza kazi zinazoonekana au zisizoonekana umepotoka. Unaficha hali halisi ya unyonyaji na uonevu wa wanawake wanaofanya kazi ya aina yoyote. Kwa mfano, katika Tanzania kila mtu anajua kwamba wanawake wanapika, wanatunza watoto, wanalima na kukamua ng’ombe na/au wanafanya kazi za kuajiriwa. Lakini watu hawaelewi jinsi kazi hizo zinavyosaidia kushusha thamani ya kifedha ya kazi, ziwe kazi za kilimo au za kuajiriwa; yaani kazi hizo zinashusha mshahara, bei ya mazao na thamani ya njia nyingine za kujipatia maslahi. Tukitaka kuchunguza swala hilo zaidi, lazima tuchunguze mahusiano ya uzalishaji jinsi yanavyotawaliwa na mahusiano ya kibepari. Tumeshataja kwamba makampuni ya kimataifa yanahamia nchi za Afrika kutafuta wafanyakazi wa mshahara mdogo. Wanawake ndio wanaoajiriwa kwa mshahara mdogo kabisa; si hapa Afrika tu, bali ni duniani pote. Jambo kubwa linalozuia wanawake wasifanye kazi za kuajiriwa na wasilime mazao ya biashara ni mahusiano ya kiumeni na mgawanyo wa kazi kutokana na jinsi. Mabepari wanataka kuondoa vikwazo hivi au angalau mabepari wanataka vipengele vingine vya vikwazo hivi ili wazalishe bidhaa zaidi. Vilevile ubepari utanufaika kama mfumo wa kilimo cha kijungumeko, kilimo kinachotegemea sana kazi ya wanawake wakulima, utabatilishwa. Hii ni kwa sababu kadiri wakulima wanavyozidi kulazimishwa kununua mahitaji yao, ndivyo watakavyolazimishwa kuzalisha bidhaa zaidi ili wapatae hela, au watalazimishwa kutafuta kazi ya kuajiriwa. Kwa hiyo ubadilishaji wa kilimo cha kijungumeko unasaidia kujenga uchumi wa bidhaa katika jamii za wakulima. Vilevile unasaidia kuongeza idadi ya watu wasio na kazi na ambao wanaweza kuajiriwa kwa urahisi katika viwanda vya kibepari.
Ni dhahiri kwamba wanawake watanufaika kama mahusiano ya kiumeni yatabadilishwa. Lakini kuna haja ya kuchunguza kwanza mabadiliko yanayotokea sasa katika jamii za Afrika na kuandaa mbinu nzuri za utatuzi. Kama hatufanyi hivyo, “tutakomboa” wanawake wasionewe na mahusiano ya kiumeni lakini waendelee kuonewa na wale wakubwa wenye mashamba makubwa na viwanda; yaani mabepari au serikali yenyewe. Zaidi ya hapo, mtaji hautaki kubadilisha mambo mengine ya mahusiano ya kiumeni, hasa mbinu za kudhibiti wanawake, vijana na watoto.
Mbinu za Utafiti
Makala haya yanasisitiza mbinu za utafiti juu ya wanawake (vitomeo 3, 5, 7, 9, 12, 13, 14). Maswala ya utafiti hayahusu mbinu tu bali yanahusu jinsi tatizo la wanawake linavyoelezwa, hasa kwa kuzingatia hali ya mabadiliko katika jamii. Kwa mfano Ulrike von Buchwald na Ingrid Palmer (kitomeo 3) wanasisitiza umuhimu wa kuchambua jinsi aina ya uzalishaji na uundaji na ukuaji wa tabaka vinavyowaathiri wanawake. Maandishi mengine yanasisitiza mgawanyo wa kazi duniani kama msingi mmoja wa unyonyaji wa wanawake na wafanyakazi (vitomeo 5, 14 na sura zinazofuata). Swala la mgawanyo wa kazi duniani ni swala ambalo linaleta mapambano kati ya wachunguzi (vitomeo 5 na 14). Kutokea kwa maswala haya kunaonyesha haja ya kutunga nadharia inayoweza kuelezea unyonyaji na uonevu wa wanawake. Utafiti unaotoa maelezo ya jinsi hali ilivyo tu hauwezi kufanya hivyo. Vitomeo vingine vinasisitiza haja ya kufanya uchunguzi katika eneo dogo pamoja na uchambuzi badala ya nchi au mkoa mzima. Imeonekana pia vipo vipengele ambavyo ni muhimu sana kwa utafiti wa wanawake (tazama kitomeo 3). Jeanne Henn anajadili umuhimu wa uchunguzi wa kupima muda unaotumiwa kufanya kazi mbalimbali na kuchunguza ulaji kayani. Kwa kutumia takwimu, uchunguzi kama huo unadhihmsha kwamba unyonyaji wa wanawake wakulima upo (kitomeo 7). Kwa mfano, uchunguzi kama huo uliofanywa huko Cameroon (Henn, 1978). Makala nyingine zinapendekeza mada za uchunguzi (vitomeo 3, 5, 9, na 12). Takwimu zilizokusanywa na serikali ya Kenya juu ya elimu ni mfano mzuri wa aina ya uchambuzi wa takwimu unaojitajika katika ufafanuzi wa nafasi tofauti za wanawake na wanaume za kupata huduma mbalimbali kama elimu, afya na ustawi wa jamii.
Ripoti ya Mkutano juu ya Ukandamizaji wa Wanawake ulioandaliwa na IDS (Sussex) unaulizia swala la usambazaji wa matokeo ya taarifa za uchunguzi. Swala hili vilevile linahusu lugha, mawasiliano na mbinu za kupata maoni ya wanawake (na wanaume) wanaoathiriwa na uchunguzi huu. Pendekezo mojawapo ni kutayarisha vijitabu vidogo na maandishi mengine yaliyoandikwa kwa lugha rahisi ili wakulima na wafanyakazi waweze kuvisoma. Uchunguzi wa kushiriki unakuza ushirikiano kamilifu wa wakulima na wafanyakazi katika kufanya utafiti. Ipo mifano mbalimbali ya uchunguzi wa kushiriki katika sura zinazofuata. Uchunguzi huo umechambuliwa na kuhakikiwa katika mapendekezo ya Warsha ya Kanda juu ya Mbinu za Utafiti iliyoandaliwa na Taasisi ya Mitaala na Maendeleo. Uchunguzi huo unatumia mtazamo wa uyakinifu wa kihistoria. Mtazamo huo unasisitiza hali halisi ya nchi na kuzingatia hali ilivyo duniani. Watafiti wanaanza kuunga mkono umuhimu wa kuzalisha na kusambaza ujuzi. Uchunguzi na maandishi hayana haja ya kulenga soko la kimataifa na kujibu au kujadili mambo ambayo mashirika ya kimataifa yanafikiri kuwa ni muhimu. Uchunguzi uwahusuo wenyeji na kujishughulisha na siasa ya vijiji, hauna lengo la kushindania “viwango vya kimataifa” vya utaalam. Lakini mtafiti akitilia mkazo anaweza kupata matatizo mengine ya binafsi. Swala linalojadiliwa katika vitomeo 13 na 14 la nani anafanya uchunguzi linaleta hoja kuwa je, uchunguzi unamnufaisha nani? Hakika jibu la swali hili litaonekana katika vitendo vya mchunguzi mwenyewe.
Marejeo
Benki ya Dunia 1980 World Development Report (Ripoti ya Maendeleo Duniani), Washington, D.C.
Jeanne Koopmen Henn 1978 Peasants, Workers and Capital: The Political Economy of Labour and incomes in Cameroons, Harvard University, tasnifu ya Ph.D. isiyochapishwa.
Warsha ya Kanda juu ya Mbinu za Utafiti iliyoandaliwa na Taasisi ya Mitaala ya Maendeleo 1981 “Mapendekezo” katika Ripoti ya Warsha iliyotajwa hapo juu na iliyofanyika Usa River, Mkoa wa Arusha, tarehe 30 Machi mpaka tarehe 11 Aprili, 1981. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Mitaala ya Maendeleo.
Bibliografia
1. AAWORD (Association of African Women for Research and Development) (Jumuiya ya Wanawake Waafrika ya Uchunguzi na Maendeleo) bila tarehe, AAWORD, Dakar (B.P. 3186, IDEP, Dakar, Senegal) uk. 28.
Kijitabu hiki kinaeleza sababu za kuanzisha jumuiya ya wanawake Waafrika wachunguzi. Sababu hizo ni pamoja na lengo la maendeleo na ukombozi wa Waafrika na ubatilizaji wa ubaguzi wa jinsi au jamii yoyote. Madhumuni mengine ya AAWORD ni kuimarisha mfumo wa mawasiliano baina ya wanawake wachunguzi wanaojishughulisha oa swala la maendeleo ya Afnka, kukuza uchunguzi unaolenga kuleta mabadiliko kwa vitendo, kuhakiki mbinu za uchunguzi na kukuza uchapidiaji. Mwanamke Mwafrika yeyote anayeunga mkono maleago hayo anaweza kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo. Shughuli za AAWORD zinasimamiwa na Baraza Ja Watu Watatu, Kamati ya Uhariri, na Mkutano Mkuu unaofanyika kila baada ya miaka miwili. AAWORD inakuza uchambuzi wa kihistoria na hali halisi ya Afrika na inapinga mwelekeo wa kusisitiza umuhimu wa kuchunguza swala la wanawake. Pia AAWORD inasisitiza umuhimu wa kuchunguza utamaduni na fikra zinazohusu hali ya wanawake, si nyanja za kiuchumi kama ukoloni mamboleo tu. Kutokana na mwelekeo huo, AAWORD inatilia mkazo maswala ya kisheria yanayohusu familia, ndoa, uashiki, elimu na uajiri.
2. BAUMANN, HERMAN 1972 “The Division of Work According to Sex in African Hoe Culture” Africa 1 (3): 289 – 319. (Mgawanyo wa kazi kutokana na Jinsi katika Jamii za Afrika zinazolima kwa Jembe). Makala inatoa hoja kwamba kilimo cha jembe kimegunduliwa kwanza na wanawake ili wawe na makazi ya kudumu. Polepole mwanaume alianza kutegemea uchumi wa mwanamke na hali yake ilishuka kisheria na kijaoui. Hah hii ilijenga msingi wa jamii za kiukeni. Lakini walipoanza kutumia plau, au kulima mazao ya biashara, wanawake walipoteza uwezo wao wa kusimamia matumizi ya shamba. Badala yake walipewa bustani zilizo karibu na nyumbani tu. Ni dhahiri kwamba mabadiliko hayo yanahusiana na kuzuka kwa jamii za kiumeni.
3. BUSHWALD, ULRIKE VON na INGRID PALMER 1978 Monitoring Changes in the Conditions of Women – A Critical Review of Possible Approaches, Geneva, UNRISD, paper for restricted circulation No. 94. (“Ukaguzi wa Mabadiliko katika Hali ya Wanawake – Uhakiki wa Mitazamo Mbalimbali”).
Makala haya yanaeleza mbinu zinazotumiwa kuanzisha ukaguzi wa kitaifa wa mabadiliko katika hali ya wanawake. Maandishi haya yanayohusu maswala kama athari za mabadiliko ya kilimo yaliyotokana na ukoloni na kutojitegemea kiuchumi; mifumo ya ukuzaji wa viwanda na miji, na nafasi ya wanawake katika jamii na mfumo wa uzalishaji mali. Makala inafafanua hitilafu za data aazotumiwa kuchambua mabadiliko katika hali ya wanawake, na kusisitiza takwimu juu ya shughuli za kiuchumi, elimu na mfunzOy afya iia chakula bora. Inajadili mitazamo na mbinu pamoja na kutaja haja ya kuangalia takwimu za kijumla pamoja na takwimu zmazotokana na uchunguzi wa mada maalum. Hatimaye wanapendckeza mfumo wa ukaguzi unaokusanya data mara kwa mara na kutathmmi data muhimu zinazohusu wanawake. Sasa UNRISD inaandaa mpango wa uchunguzi wa awali kuhusu ukaguzi wa mabadDiko katika hali ya wanawake kama hatua moja ya kutekekza pendekezo hilo. Lazuna tuache kuelezea tu snra ya hali ya wanawake kwa juujuu. Lazima tuchambue sababu halisi za hali hii na athari za mabadiliko. Kwa hiyo kuna haja ya uchunguzi wa kimsingi na uchunguzi unaochungaza eneo au mada ndogo tu. Mifano ya maswah ambayo yangeweza kuwa msingi wa ukaguzi ni kama ifuatayo:
Quote:1. Je, ni katika aina gani za uzalishaji mali ambapo wanawake wanajitokeza baada ya athari za dhamaji na uhaba wa kazi wakati ambapo kuna mapinduzi ya kiteknolojia katika kilimo na huko sehemu za vijiji uzalishaji mali unabadilika kuwa wa kisasa upesi upesi?2. Je, mabadiliko ya kiuchumi na kikazi yanasababisha tofauti kubwa za tabaka? Je, yanapunguza usawa wa wanawake uliokuwepo katika uchumiwajadi?3. Je, mgawanyo wa kazi na mamlaka ya kutoa uamuzi katika familia iliyokuwepo kimila yanabadilikaje kutokana na mabadiliko ya nafasi za wanawake na wanaume katika uchumi?4. Ni mambo gani ya utamaduni wa jadi yanayoshusha hadhi ya wanawake katika sekta za jamii zinazoleta maendeleo?5. Kuna uhusiano wa aina gani kati ya habari zilizopatikana (kwa mfano kuhusu elimu, kazi, uwezo wa kushika mimba) tukiangalia habari hizo kwa kuzingatia tabaka?”
Makala hii ni muhimu sana kwa watekelezaji wanaoanza kutambua hitilafu za takwknu na habari nyingine zinazohusu wanawake. Vilevile inafaa wale wanaofanya utafiti juu va wanawake na jinsi ya kuwasadia wanawake.
4. GODY, J. na JOAN BUCKLEY 1973 “Inheritance and Women’s Labour ni Africa” Africa 43 (2): 108 – 121. (“Urithi na Kazi ya Wanawake katika Afrika”)
Katika Afrika wanawake ndio wanaofanya kazi nyingi za kilimo, hasa katika jamii zmazotumia jembe. Nafasi hii muhimu ya wazi hasa huko Congo na kadka Afrika ya Mashanki, Afrika ya Kati na Afrika Kusini. Lakini ingawa wanawake wanafanya sehemu kubwa ya kazi za kilimo, kwa kawaida mashamba humilikiwa na wanaume. Hali hii inaathiri sana mfumo wa uchumi, urithi na ukoo. Inaonekana kwamba nafasi muhimu ya wanawake katika kilimo ina uhusiano na aina mbili za urithi: Kwanza urithi wa kiukem na pili aina ya urithi ambao kwao mali ya wanaume inagawiwa kwa watoto kufuatana na mama zao. Aina hii ya pili ya urithi ni aina ya “urithi kutoka juu” ambayo Gluckman anaiita “mfumo wa nyumba-mali”. Mfumo huo unaonekana kwenye jamii za kiumeni na mara nyingine kwenye jamii zinazotoa urithi kutokana na pande zote mbili, upande wa mama na wa baba.
5. IDS BULLETIN 1979 Special Issue on the Continuing Subordination of Women in the Development Process Vol. 10 (3), Brighton, Institute of Development Studies, University of Sussex, uk. 67. (“Toleo Maalum Kuhusu Ukandamizaji Unaoendelea wa Wanawake katika Jitihada za Maendeleo”).
Ripoti inatoa pendekezo la Mkutano kuhusu mwanamke mmoja ambaye ni mfungwa wa kisiasa. Yeye ni Mzalendo wa Puerto Riko aliyefungwa jela na serikali ya Marekani. Vilevile ripoti inatoa mapendekezo na mwongozo wa uchunguzi. Inapendekeza kwamba msingi wa uchunguzi uwe uchambuzi wa kinadharia kuhusu maendeleo na mifumo inayojenga na kuendeleza utawala wa kitabaka na hitilafu katika hali za wanawake na wanaume. Inasisitiza haja ya kuwa na mawasiliano mazuri ya kupashana habari kwa wale wanaochunguza ukandamizajtwa wanawake, na vilevile kwa wachunguzi na vyama vya wanawake, vikundi vya uchunguzi wa wanawake na jumuiya ya wafanyakazi. Pia kuna haja ya uchunguzi wa pamoja, yaani uchunguzi unaofanywa na wataalam wa fani mbalimbali na uchunguzi unaolinganisha vipengele mbalimbali vya jamii. Makadirio ya miradi yote yawe na kitengo cha fedha kwa ajili ya kutafsiri ripoti ya mwisho ya uchunguzi kwa lugha ya wale waliochunguzwa. Ripoti hn iliandikwa kwa lugha ambayo inaeleweka kwa urahisi na ripoti ipatikane kwa urahisi na wale wanaohusika. Matokeo ya uchunguzi yawasilishwe mapema kwa wanaohusika kwa kutumia vifaa vya elimu kama sinema, picha, na kada za kunasia sauti. Matokeo yajadiliwe mara kwa mara na wale waliotoa habari.
6. KENYA, Central Bureau of Statistics, Ministry of Economic Planning and Community Affairs 1977 “Educational Trends 1973 – 1977” uk. 85 na Jedwali 65 (“Mielekeo ya Elimu 1973 – 1977”).
Kijitabu hiki kinachambua elimu ya msingi na ya sekondari kwa kipindi cha mwaka 1973 hadi 1977. Kina jedwali za takwimu za idadi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kila wilaya, kama ni wasichana au wavulana, aina ya shule, na matokeo ya mitihani ya darasa la saba na ya sekondari. Serikali ilipofuta ada za shule ya msingi mwaka 1973, idadi ya wanafunzi iliongezeka, lakini bado uwiano wa wasichana na wavulana haujawa sawasawa. Inaonekana kwamba kwa wastani wavulana wote wa mijini na vijijini wanafaulu vizuri zaidi katika mitihani ya darasa la saba, yaani mitihani ya Kiingereza, Hesabu, na Maarifa, isipokuwa sehemu za mijini hakuna tofauti kati ya wasichana na wavulana katika mtihani wa Kiingereza. Takwimu za elimu vijijini zinaonyesha kwamba wanafunzi wa kike wanalingana zaidi na wenzao wa kike katika maksi zao na wavulana wanalingana zaidi na wavulana wenzao, hata kama ni wasichana/wavulana wa kikundi kimoja.
Vilevile zipo tofauti kati ya wanafunzi wasichana na wavulana katika shule za sekondari. Asilimia kubwa zaidi ya wasichana.wanahudhuria shule zile ambazo hazipewi ruzuku. Wanafunzi wa shule hizo hawafaulu vizuri. Idadi kubwa ya wasichana wanahudhuria shule hizo. Hii inaonyesha kwamba wazazi wana moyo wa kuwasomesha wasichana wao na kukabili tatizo la nafasi haba za wasichana katika shule zinazopewa ruzuku. Shule zinazopewa ruzuku zina nafasi chache za wasichana, na hasa katika sayansi nafasi chache mno. (Sisi tunafikiri kwamba tunahitaji kuangalia kwa makini hali hii ambapo 2/3 ya wasichana wote wanaosoma sekondari wanasoma kwenye shule hafifu ambazo hazipewi ruzuku – yaani asilimia 67 ya wanafunzi katika shule hizo hafifu ni wasichana. Idadi ya wanafunzi wasichana katika shule hizo inazidi kuongezeka, na hali hii inaonyesha kwamba shule hizo ni kama mahali pa kutupa wanafunzi wa kike ili kupunguza haja ya kutenga nafasi nyingi za wasichana katika shule zinazopewa ruzuku. Kwa hiyo wasichana wengi wanapata elimu ya daraja la chini).
Kwa kuangalia idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza na la pili katika mitihani ya Kidato cha 4 mwaka 1976, wasichana walifaulu vizuri kuliko wavulana. Zaidi ya hapo, wasichana wachache kuliko wavulana walishindwa (asilimia 28 wasichana na asilimia 41 wavulana). Ingawa sababu moja ya kufaulu kwao ni kwamba wasichana wanachujwa zaidi kabla ya kuingia shule ya sekondari, lazima tukumbuke vilevile kwamba wasichana wengi waaasoma kwenye shule zisizopata ruzuku na ambapo kwa wastani wanafunzi hawafaulu vizuri.
7. HENN, JEANNE 1981 “Who Benefits from Peasant Women’s Work? Insights from a Mode of Production Analysis” Economic Reflections 1 (1): 34 – 48. (Nani Anafaidi Kutokana na Kazi ya Wanawake Wakulima? Mawazo Yanayotokana na Uchunguzi wa Mfumo wa Uzalishaji Mali).
Makala haya yanachambua mahusiano ya uzalishaji mali wa kiumeni katika kiwango cha kaya, uzalishaji wa bidhaa ndogondogo ulioenea kwa wakulima wadogo, na uzalishaji wa kibepari. Mahusiano hayo yanathibitishwa katika uchunguzi uliofanyika kuhusu muda unaotumiwa kufanya kazi mbalimbali za uzalishaji mali na uendelezaji wa uzalishaji mali huko kayani na kutofautisha uzalishaji kwa ajili ya kaya na kwa ajili ya kuuza. Uchunguzi wa muda wa aina ya kazi unafafanua ni nani anayepata faida kutokana na kazi zinazofanywa nyumbani. Unaonyesha ni nani anayefaidi kwenye kaya, kijiji, taifa na hata kimataifa. Uchunguzi wa aina ya kazi pamoja na tofauti katika ulaji au matumizi unabainisha wazi mchango mkubwa wa wanawake wakulima katika kilimo na katika kutunza na kuendeleza familia za wakulima.
8. LUCILLE M. MAIR 1981 “New International Economic Order: What Does Development Really Mean to Women” IFDA Dossier 21 (Jan. – Feb.), uk. 56 – 68. (“Mpango Mpya wa Uchumi wa Dunia: Maendeleo yana maana gani kwa Wanawake”).
Makala haya yanatoa hoja ya kwamba wanawake wanafanya theluthi moja ya kazi zile zinazohesabiwa, pamoja na kazi za nyumbani zisizohesabiwa wala kulipiwa. Zaidi ya hapo theluthi moja ya wakuu wa familia duniani ni wanawake. Ukweli huo unapingana na fikra inayotolewa katika vitabu vya shule kwamba katika Afrika na kwingineko, wakuu wa kaya ni wanaume tu. Ingawa wanawake wanafanya theluthi moja ya kazi duniani, wanapata chini ya 1/10 ya mapato ya duniani na wanamiliki chini ya 1/100 ya mali ya dunia.
Hali ya wanawake inahusishwa na hali ya tabaka la chini, ambaioni tabaka la wanawake walio wengi. Asilimia 70 ya dunia inapata asilimia 30 ya mapato ya dunia. Mgogoro uliopo duniani unazidi kuwa mkali kwa sababu ya hali ya uchumi, matatizo ya nishati na madeni makubwa ya nchi zinazoendelea. Ingawa huu ndio ukweli unaoathinmaisha ya kazi ya wanawake wa “kusini”, (nchi-zinazoendelea), wanawake wa “kaskazini” (nchi zilizoendelea za kibepari) wanajitenga na harakati za kusini kwa jumla. Akijadili Mkutano wa Copenhagen wa Kimataifa wa Kipindi cha Miaka 5 ya Miaka kumi ya Wanawake, Mair anataja ubaguzi wa vyombo vya habari ambavyo vinasisitiza tofauti za siasa badala ya kujadili maswala ya wanawake. Anataja kwamba aya 284 kati ya aya 287 za mapendekezo ya utekelezaji zilipitishwa bila kupingwa. Wanawake wa dunia ya tatu, wanajua kwamba haitoshi kuanzisha taasisi zinazoshughulikia wanawake. Tukitaka kuleta ukombozi wa wanawake, kuna haja ya kukabili maswala ya uchumi na historia ya harakati za jamii. Wanawake hawakubali kulazimishwa kujadili aina yoyote ya maswala haya.
9. MBILINYI, MARJORIE J. 1971 “The Participation of Women in African Economies” Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Makala ya ERB Na. 71.12, uk. 34. (“Ushirikiano wa Wanawake katika Uchumi wa Kiafrika”). Pia Addis Ababa, UNECA.
Kwajumla makala haya yanachambua wanawake katika uchumi wa Afrika, lakini kwa kiasi fulani, msingi wa uchambuzi huo unahusu hali iliyopo Tanzania. Makala yanasisitiza kwamba haiwezekani kutoa matamko kuhusu “nafasi ya wanawake wa Kiafrika”, kwa jumla kwa sababu ya hali mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Imeandikwa kwa lugha inayoeleweka kwa urahisi na inachambua jinsi na kwa kiasi gani wanawake walishiriki katika sekta mbalimbali za uchumi kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni. Kwa kila kipindi makala inachambuamaswala ya umilikaji na udhibiti wa njia kuu za uchumi, uthibiti wa wafanyakazi na kazi zao, na ugawaji wa faida zinazotokana na kazi. Mambo yanayozuia uajiri wa wanawake ni ukosefu wa elimu – pamoja na elimu ya ufundi – na fikra na maadili ya kiumeni. Kuanzisha mbinu za kisasa za kilimo kunaleta kazi zaidi kwa wanawake. Pamoja na hayo, wanapoteza uwezo wa kufanya uamuzi kuhusu kazi zao. Uchambuzi uliofanyika juu ya elimu na elimu ya ufundi unadhihirisha ubaguzi wa wanawake katika uchaguzi wa masomo na nafasi za elimu ya juu. Makala inaeleza hatua na mazingira yanayotakiwa kuwapatia wanawake nafasi ya kufanya kazi, kulea familia na kutoa mchango wao kwa jamii. Hatua hizo ni pamoja na vituo vya watoto wadogo vijijini na mijini ambavyo vitatunza watoto siku nzima, chakula rahisi kilichotengenezwa tayari; huduma za afya na marupurupu mengine kwa ajili ya wanawake walioolewa na wasioolewa huko wanapofanya kazi; mshahara sawasawa kwa wanawake na wanaume wanaofanya kazi ya aina moja; uwezo wa kuamua kuhusu matumizi ya hela za mshahara au mapato mengine, na kusaidia wanawake wanaojitegemea oa wasioolewa kujiunga na vijiji vya ujamaa kama wanavijyi wengine. Makala yanachambua vilevile nafasi ya serikali, mashirika ya kimataifa na mashirika mengine. Mwongozo wa maswala ya uchunguzi unaambatanishwa.
10. MCDOWELL, JIM 1976 Village Technology in Eastern Africa. Ripoti ya Semina ya UNICEF kuhusu “Simple Technology for theRural Family” iliyoifanyika Nairobi, Juni, 1976, Nairobi, UNICEF Eastern Africa Regional Office, uk. 63 pamoja na vielelezo. (Teknolojia Vijijini Katika Afrika Mashariki).
Makala haya yanajadili faida ya kuleta teknolojia inayowafaa akina mama na watoto vijijini. Inasisitiza umuhimu wa kuleta vitu vmavyotengenezwa kwa urahisi na ambavyo vitapunguza kazi za wanawake. Vilevile inaonyesha umuhimu wa kuzalisha chakula bora na kingi zaidi kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo na uhifadhi na utayarishaji wa chakula. Inasisitiza vilevile umuhimu wa kuleta maji safi vijijini. Kwa jumla, makala yanatoa maelezo na kutoa mwongozo kuhusu aina nyingi za teknolojia ambazo zingefaa vijijini na jinsi ya kuwapasha habari na kuwaelimisha wanavijiji kuhusu teknolojia hii.
11. O’BARR, JEAN 1975 “Making the Invisible Visible: African Women in Politics” African Studies Review, 18 (3) uk. 19 – 27.(Kufanya Yule Asiyeonekana Aonekane: Wanawake wa Kiafrika katika Siasa).
Makala haya yanaangalia mawazo na fikra juu ya nafasi ya wanawake wa Kiafrika katika siasa na kupinga maoni yasiyo na msingi yanayotolewa na wataalam wa siasa na viongozi. Kwa sababu ya maoni potofu, uchambuzi mwingi uliofanyika kuhusu shughuli za siasa haukutaja wanawake. Makala yanatoa hoja kwamba “shughuli za kisiasa za wanawake ni muhimu sana katika kuelewa siasa ya jamii zinazoendelea”. Katika jamii za Kiafrika ambapo shughuli za nyumbani na shughuli za umma hazikutenganishwa sana, “wanawake wanashiriki kikamilifu katika siasa kwa kutoa hoja, kuendeleza hoja hizo na hatimaye kukubali au kukataa matokeo yake. Inataja makala mengine kuonyesha jinsi uwezo wa kiuchumi unavyojenga uwezo wa kisiasa na umuhimu wa nafasi ya pili ya wanawake. Mifano kutoka Tanzania inatolewa kutoka makala ya M.J. Mbilinyi (“Mwanamke ‘Mpya’ na Maadili ya Jadi Tanzania”) na utafiti uliofanywa na mwandishi mwenyewe huko Upare.
12. PALA, ACHOLA 1974 The Role of African Women in Rural Development, Research Priorities (Nafasi ya Wanawake wa Kiafrika Katika Maendeleo Vijijini Mada au la Uchunguzi) Nairobi, Institute of Development Studies Discussion Paper No. 203 uk. 31.
Makala haya yanachambua makala mengine kuonyesha kwamba katika uchumi wa Afrika kabla ya ukoloni, wanawake walikuwa na nafasi kubwa katika uchumi wa jamii wa wakulima na wafugaji. Hata hivyo, jambo hili halijazingatiwa katika kutunga mbinu za maendeleo vijijini, ingawa wanawake wanatarajiwa a kutoa mchango katika kujenga taifa. Hitilafu hii, kati ya nadharia na hali halisi inasababishwa na mambo mawili. Watawala walioandaa mipango ya kikoloni ya kilimo cha biashara waliwapendelea wanaume kuliko wanawake. Kwa hiyo “walikuza zaidi uzalishaji mali wa mfanyakazi mwanaume” na kumpunja mwanamke. Mtindo huu uliendelea hata baada ya Uhuru. Uchunguzi uliofanyika Tanzania na Kenya, unaonyesha kwamba huduma za kilimo na taarifa za matokeo ya uchunguzi zinapatikana kwa urahisi zaidi kwa wale wakulima “walioendelea”. Hawa kwa kawaida ni wakulima wa kiume wenye mashamba makubwa. Sekta ya kilimo ya kilimo cha kijungumeko wanaachia wanawake na kwa kawaida sekta hiyo haishughulikiwi. Sababu ya pili ni kwamba uchunguzi mwingi kuhusu wanawake wa Kiafrika umefanywa na wageni ambao hawaelewi vizuri mazingira ya uzalishaji mali wa Afrika na maendeleo yake au umefanywa na Waafrika ambao hawataki kutazama matatizo ya maendeleo vijijini kwa kuzingatia mawazo ya wakulima.
Makala yanasisitiza kwamba maendeleo vijijini hayana budi kuzingatia nafasi ya wanawake katika kuleta maendeleo ya wanaume. Kuna haja ya kuchambua mfumo wa jamii za vijijini na hali ya wanawake kiuchumi na kijamii jinsi inavyobadilika. Mwandishi anataja mada za uchunguzi zitakazosaidia mipango bora ya mabadiliko vijijini.
13. PALA, ACHOLA OKEYO 1981 “Reflections on Development Myths” (“Maoni juu ya Hadithi za Maendeleo”) African Report 26 (2) March – April: 7 – 10.
Makala haya yanatoa hoja ya kwamba pote duniani watu wanatambua kwamba hali ya wanawake ni ya chini na inazidi kushuka, na kwamba hali hii inaathiri vibaya maendeleo. Hivi sasa, wataalam wanaanza kutafuta mbinu za uchunguzi na ukusanyaji wa data ambazo zitafafanua vizuri zaidi kutokuwepo kwa usawa kati ya wanawake na wanaume. Kwa mfano mwandishi anasisitiza umuhimu wa kuacha mbinu ya kutotofautisha shughuli za uzalishaji wa chakula cha kuuza na cha matumizi ya nyumbani. Wakati huohuo lazima wanawake wote watafute mbinu za kutatua matatizo. Matatizo ya wanawake Waafrika yamefasiriwa “kwa nje”, yaani kwa kuzingatia mgawanyo wa kazi wa kimataifa na kusisitiza itikadi ya hali ya kiuchumi – jamii.
Mwandishi anapinga uchambuzi unaosisitiza utamaduni, kwa sababu uchambuzi huo unatenga utamaduni na siasa na uchumi na una fikra potevu kwamba mabadiliko ya utamaduni hauathiriwi na mambo mengine yaliyo nje ya utamaduni. Pia inapotosha kwa kutenga uchambuzi wa wanawake na uchambuzi wa hali ya kiuchumi-jamii na wa uchumi wa kimataifa. Msimamo wa wanawake wa nchi za magharibi ni kwamba mwanaume ni adui. Msimamo huo unatokana na hali halisi huko ambayo mwanamke hana maana. Hapa Afrika hali ni tofauti kwa sababu tangu zamani wanawake walizalisha mali. Kwa hiyo wanawake wa Kiafrika hawafikiri kwamba mwanaume ni tatizo. Isitoshe, wanawake wanapojaribu kuleta maendeleo, wanafanya hivi si kwa manufaa yao peke yao, bali kwa ajili ya familia zao. Hii haina maana ya kwamba wanaume hawapo katika maisha yao. Kwa hiyo ni kosa kusema kwamba “mipango ya wanawake inaweza kuleta mgogoro kati ya wanawake na wanaume”.
14. SCANDANAVIAN INSTITUTE OF AFRICAN STUDIES 1978 Women in Africa and Development Assistance (Wanawake katika Afrika na Msaada wa Maendeleo). Ripoti ya Semina iliyoandaliwa na Scandanavian Institute of African Studies, Uppsala, 20 – 21 Agosti, 1978 uk. 55.
Semina hii ilisisitiza maswala yafuatayo:
Misaada ya nje inaathirije wanawake? Wanawake wanahitaji msaada gani kujiendeleza? Ni Mbinu gani ambazo zingeweza kutumiwa ili misaada inayotolewa iwasaidie zaidi wanawake? Semina ilisisitiza haja ya kufanya uchunguzi unaoendelea kuhusu hali ya wanawake, ambao vilevile utalenga utekelezaji. Uchunguzi uliofanyika katika mazingira ya ukoloni mamboleo na mgawanyo wa kazi kimataifa unaonyesha kuwa wanawake wanafanya kazi kwa mshahara mdogo mno. Wanasemina vilevile walijadili dhana ya mgawanyo wa kazi za uchunguzi ambapo wachunguzi wagem na wachunguzi Waafrika wangetenganishwa. Wengine walitetea dhana hii na baadhi waliona kwamba “uchunguzi na matokeo yake ni muhimu zaidi kuliko swala la nani anaufanya”.
Uchunguzi na mipango ya msaada inayosisitiza zaidi “sera ya kuku” na kusaidia mahitaji ya kimsingi tu yanayombagua mwanamke mkulima na kumkandamiza kiuchumi. Wanawake wanahitaji mafunzo na kushirikishwa katika sekta zile za uchumi zilizoendelea sana.
15. IRENE TINKER 1981 “Policy Strategies for Women in the 1980’s” (“Mbinu za Sera ya Wanawake kwa Kipindi cha Miaka 10, 1980 – 1990”) African Report 2 (2) Machi – Aprili, uk. 11 – 16.
Makala hii inatoa maelezo ya historia ya dhana ya wanawake katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Ingawa inatoa uhakiki muhimu wa msimamo wa “Wanawake katika Maendeleo” haikuchambua kiini cha matatizo ya maendeleo yanayosababisha uonevu wa wanawake. Mwandishi anatoa hoja kwamba vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa vimepitisha maazimio yanayolazunisha kila mradi kujumuisha wanawake kama watendaji na wapokeaji wa msaada. Mwandishi anataja kwamba mambo hayo hayakubadilisha hali halisi. Labda jambo la maana lililofanywa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ni ukusanyaji wa data na ukuzaji wa miradi midogo ya wanawake. Uchunguzi unadhihirisha kwamba wanawake wanafanya kazi kwa bidii, na kila inapowezekana wanafanya kazi kupata hela. Uchunguzi wa matumizi ya hela na muda wa kazi una data juu ya nani anatawala hela za matumizi nyumbani na takwimu nyingine za mapato. Kwa mfano, katika USA imeonekana kwamba wanawake wanalipwa senti 59 kwa kila dola anayolipwa mwanaume. Hii ni kwa sababu ya ubaguzi wa wanawake kazini. Wanawake wanapewa kazi za mshahara mdogo wa kima cha chini kama vile, wanawake Watanzania wanaofanya kazi viwandani.
Katika nchi zinazoendelea, ujima (kwa mfano baina ya majirani) umefifia. Hivi sasa familia, kwa mfano, mama na watoto pamoja na vibarua, wanafanya kazi hizi. Kazi hizi hazihesabiwi katika uchambuzi wa wafanyakazi. Kazi hizi ni pamoja na kutayarisha chakula, kuchota maji, kufuma mikeka. Kazi hizi hazihesabiwa kama shughuli za kiuchumi ingawa zinasaidia kuendeleza familia na mara nyingme huleta mapato. Mashine zinazoweza kufanya kazi hizi ni kama masbine ya kusagisha au jiko la mafuta ya taa. Mashine hizi ni ghali mno na wengi hawawezi kuzinunua. Kwa hiyo, wanawake wanarudishwa nyuma kwa kupewa kazi nyingi za kila siku, kazi ambazo zinaweza kuitwa “kazi bila ya mapato”. Mwelekeo wa kupanga miradi ya wanawake umetenga jitihada za wanawake na mipango ya maendeleo. Ni kama wanawake wanapewa msaada wa ustawi wa jamii tu. Isitoshe, kwa kawaida miradi hiyo ni midogo mno na kiuchumi haiwezi kufanikiwa. Kwa hiyo kwa kipindi cha miaka 10 cha 1980 – 1990, tuwe na msimamo wa kuandaa miradi inayolenga mambo ambayo ni muhimu kwa wanawake na mahitaji yao, na kuwashirikisha katika kupanga na utekelezaji. Vilevile, miradi izingatie mpango wa maendeleo ya kijiji au taifa zima. Miradi ya vyama vya wanawake bado ina umuhimu katika kujenga tabia ya kujiamini na ya uongozi, na kufanya majaribio ya mradi unaofikiriwa. Mwandishi anataja vilevile kwamba ‘vyama’ vya wanawake havijitangazi vya kutosha, pia vinashmdwa kuleta umoja utakaoathiri sera. Bado wanawake wanalazimishwa kupeleka maswala yao kwenye “dunia ya wanaume” kama wanataka kusikilizwa.
16. UMOJA WA MATAIFA 1979 Convention on the Elimination of all Forms of Discrimination Against Women (Mkutano wa Kufuta Ubaguzi wote wa Wanawake) New York, uk. 15. Inapatikana bure kutoka Ofisi ya UNDPDar es Salaam na Arusha, pamoja na makala mengine za Umoja wa Mataifa.
Mnamo Desemba 1979, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulikubali kuitisha Mkutano wa Kufuta Ubaguzi wa Wanawake. Ripoti hii inaeleza kisheria mwongozo uliokubalika kimataifa na hatua za kuleta haki za usawa kwa wanawake. Zipo ibara 30 zinazopendekeza sheria za kimataifa za kupiga marufuku ubaguzi wa aina zote. Kwa mfano, ubaguzi uliopo katika siasa, uchumi, jamii, utamaduni na serikali. Vilevile inapendekeza hatua za muda za kubadilisha mifumo ya kijamii au kiutamaduni inayoendeleza ubaguzi. Hatua maalumu ni pamoja na nafasi sawa za elimu na kufuta ubaguzi katika mihtasari ya masomo. Kwa mfano wasichana wanasoma sayansi kimu na wavulana wanasoma ufundi. Hatua nyingine ni kufuta ubaguzi katika uajiri kuhusiana na mshahara na usalama wa kazi; mwanamke akiolewa au akipata mimba. Ripoti inasisitiza vilevile kwamba wanaume na wanawake wana wajibu sawasawa wa kutunza familia na kufanya kazi za nyumbani. Kuna haja ya huduma za jamii kama vituo vya watoto, kuhakikisha kwamba wazazi wote wanaweza kutekeleza wajibu wa kazi, kutunza familia, na kushiriki katika siasa.
Sasa vyombo vya kimataifa vinatayarishwa ili kukagua mapendekezo hayo yaliyokubaliwa na mataifa. Lakini ni wajibu wa kila nchi kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa dhidi ya ubaguzi wa wanawake, na ni wajibu kupigania sheria zinazohitajiwa ili zipitishwe Bungeni. Data zilizopo katika bibliografia hii zinaonyesha kwamba upo ubaguzi wa wanawake hapa Tanzania, na kuna mambo mengi ya kufanya ili kuufutilia mbali. Ubaguzi huu utafutwa ikiwa wanawake na wanaume watachunguza matatizo yanayozuia ushirikiano baina yao, hasa yale malatizo yanayosababisha wanawake kunyimwa haki zao.
17. UNECA, African Training and Research Centre for Women 1976 “The Education and Training of Rural Women for National Development” (“Elimu na Mafunzo ya Wanawake wa Vijijini kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa”). Makala iliyowasilishwa kwenye “International Workshop on Education for Rural Women” iliyofanyika Lushoto, Tanzania (PMO/UNICEF) uk. 14.
Makala haya yanaeleza hali ya wanawake vijijiini. Yanaeleza kwa nim hawapati elimu au mafunzo, hata mafunzo ya kilimo na kwa hiyo wanakuwa raia wa daraja la pili. Kwa hiyo lazima mafunzo yatolewe kwa wanawake wakulima na wanawake maofisa kilimo, na kuongeza shule za sekondari hasa zile zinazotoa masomo ya kilimo. Hapa Tanzania kuna shule 36 za sekondari zinazotoa masomo ya kilimo. Kati ya hizo 3 tu ni za wasichana. Wanawake wanahitaji mafunzo ya mifugo, biashara, viwanda vidogo na sanaa za mikono (ufinyanzi, ususi). Mafunzo yatasisitiza udhibiti wa ubora wa bidhaa, uongozi, mbinu ya kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali badala ya aina moja, matumizi ya vifaa, namna ya kutayarisha na kuhifadhi vyakula, kuongeza kiasi cha ubora wa vyakula. Vilevile mafunzo yatasaidia kuelimisha upya wakunga wa vijijini, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa vituo vya watoto wadogo na kliniki za kina mama na watoto wadogo na kuongeza huduma za kisomo cha manufaa.
18. UNECA 1977 The New International Economic Order, What Roles for Women? (Mfumo Mpya wa Uchuni wa Dunia una Nafasi Gani kwa Wanawake?) Addis Ababa, E/CN. 14/ATRCW/77/Wd3 uk. 54
Kitabu hiki kinachambua jinsi mapendekezo yalivyozingatia nafasi ya wanawake katika miradi hii. Vilevile kinapendekeza njia mbalimbali za kuangalia mchango wa wanawake na uwezo wao wa kupata nyenzo za kimsingi za maendeleo. Mapendekezo hayo ni pamoja na matumizi ya data iliyopo tayari na haja ya ukaguzi zaidi kupata data inayohitajika. Kinajadili matumizi ya jedwali za aina mbalimbali za data: uajiri (asilimia ya wafanyakazi wanawake, jinsi mishahara inavyolingana, saa za kazi za wanawake katika kazi zisizo na mkataba rasmi) elimu na mafunzo: (asilimia ya wanawake katika shule za msingi, sekondari na vyuo na masomo yao; ushirikiano wa wanawake katika mafunzo yasiyo ya shule kwa mfano, kilimo, mifugo, na kadhalika); afya na uzazi: (ushirikiano wa wanawake katika k.m. kuleta maji safi, zahanati); sheria (kumiliki ardhi, mikopo); teknolojia vijijini nafasi yao katika kutoa uamuzi.
19. UNITED NATIONS PROTEIN ADVISORY GROUP 1979 Women ni Food Production, Food Handling and Nutrition, with Special Emphasis on Africa. (Wanawake katika Uzalishaji wa Chakula, Utayarishaji wa Chakula na Lishe hasa katika Afrika). Ripoti ya Protein – Calorie Advisory Group (PAG) ya Umoja wa Mataifa, Roma, FAO, uk. 223.
Ripoti hii inasisitiza hali ya wanawake katika sehemu mbalimbali za Afrika, pamoja na Tanzania, kwa sababu wanawake ndio msingi wa uzalishaji mali katika Afrika. Inatumia utaalam wa masomo mbalimbali k.m. historia, chakula bora, sosiolojia, anthropolojia ya kijamii na vilevile makala za uchunguzi na za Umoja wa Mataifa. Ripoti matumia data hizo kutathmini: (1) nafasi ya wanawake katika uzalishaji mali, utayarishaji mali na utayarishaji wa chakula na lishe katika Afrika, na (2) kadiri mazingira ya kazi na maisha ya wanawake yanavyoathiri upatikanaji wa chakula na ubora wa chakula cha familia najamii zao. Ripoti iliona kwamba kuongeza chakula bora na uhaba wa vyakula vingine; lazima tuwe na ugawaji mzuri zaidi wa vyakula. Pia kama familia inaanza kupata hela zaidi, haina maana kwamba ubora wa chakula chao utaongezeka. Chakula kitakuwa bora zaidi ikiwa mama ndiye anayeamua kuhusu matumizi ya fedha hizo.
20. WORLD BANK (BENKI YA DUNIA) 1979 “Recognizing the ‘Invisible’ Woman in Development: The World Baok’s Experience” (“Kumtambua Mwanamke ‘Asiyeonekana’ katika Maendeleo: Uzoefu wa Benki ya Dunia”) Washington, d.C. uk. 31.
Utangulizi wa makala haya uliandikwa na Robert S. McNamara ambaye alikuwa Rais wa Benki ya Dunia kwa wakati ule. Kutokana na utangulizi huu, Benki ya dunia imeanza kutambua haja ya kuzingatia kwa makini athari za miradi yake kwa wanawake. Kwa hiyo mwaka 1977, Benki hii ilitenga nafasi moja ya kazi kwa Mshauri wa Wanawake katika Maendeleo, ambaye kazi yake ni “kukagua na kutoa ushauri juu ya athari za miradi na athari zinazoweza kutokana na miradi kwa hali ya wanawake”. Kwa mujibu wa McNamara, “kukiuka mipaka ya nafasi za jadi za wanawake wakiwa wazazi na wafanyakazi wa nyumbani na kuongeza nafasi zao za kiuchumi, kisiasa na kijamii, kutawawezesha kujishughulisha na kutumiwa uwezo wao katika uwanja mpana zaidi”.
Makala yenyewe inaanza na maelezo juu ya mambo yanayozingatiwa na Mshauri wa Wanawake katika Maendeleo anapokagua miradi: Miradi itasaidaje mahitaji ya wanawake na kukuza uwezo wao? Je, zipo njia gani za wanawake kufaidi miradi hiyo? Nafasi ya kiuchumi-jamii ya wanawake ikoje huko mradi unapotekelezwa? Je, mradi utaathiri vibaya wanawake? Tunawezaje kutambua athari hizi na kizizuia? Ingawa ripoti inauliza maswali muhimu na kutoa muhtasari mzuri wa matokeo ya uchunguzi, inatumia dhana ya kibepari ya maendeleo. Dhana hii inatenga wanawake na matnuiano ya kijamii na mifumo ya mabadiliko yanayotokea katika mazingira yao.
21. MARCIA WRIGHT 1975 “Women in Peril: A Commentary on the Life Stories of Captives in Nineteenth Century East-Central Africa” (“Wanawake Hatarini: Maoni juu ya Masimulizi ya Maisha ya Mateka wa Afrika ya Kati na ya Mashariki katika Karne ya 19”) African Social Research 20 (Desemba, uk. 800 – 819).
Makala hii inatokana na uchunguzi wa tawasifu zilizoandikwa na wanawake watatu na mwanaume mmoja waliokuwa watumwa. Hawa waliishi katika karne ya 19, wakati wa mabadiliko ya uchumi na jamii. Masimulizi ya kila mmoja yanachambuliwa ili kupata picha ya mabadiliko yaliyotokea katika hali ya wanawake kwa jumla.
Watu walibadilishana wanawake kwa kutumia njia mbalimbali. Njia mojawapo ilikuwa ni mahari au malipo ya kazi ya mwanamke. Wanawake vilevile walitumiwa kam’a malipo ya faini au fidia. Walitekwa katika vita na waliuzwa kwenye soko la biashara ya utumwa. Watoto wa watumwa walikuwa hawana hadhi – hawakuhesabiwa katika ukoo, hata kama wazazi (mzazi) walipewa hadhi katika ukoo kutokana na ndoa. Mifano inaonyesha kuwa nafasi mbalimbali za kazi za kuajiriwa na nyinginezo zilipatikana katika misheni au miji. Kazi hizo ziliwawezesha wanawake kutoroka maisha ya utumwa ili wajitegemee wakiwa wakuu wa kaya. Hata hivyo, katika hali zote wanawake walilazimishwa kuwa chini ya wanaume wenye hadhi iliyotambuliwa na sheria na jamii. Zaidi ya hapo, wanawake ndio waliotekwa na kufanywa watumwa kwa urahisi. Wanawake walikuwa na thamani kubwa sana kwa sababu ya nafasi zao kama “wazazi, wafanyakazi na bidhaa inayoweza kuuzwa au kurithishwa”.
Mwl Maeda