Wanazuoni mbalimbali wakiwemo Greenberg (1957), Hymes (1974), Dik (1978) nk wanaiangalia lugha kwa mitazamo miwili: mtazamo wa kiisimu na ule wa kiisimujamii.
Katika mtazamo wa kwanza (wa kiisimu), lugha inaelezwa kuwa ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamadu i unaofanana ili kuwasiliana. Mtazamo huu unachukulia lugha kuwa kitu halisi amba ho kinaweza kuainishwa katika vipande sauti vidogo vidogo ambavyo kwa pamo huunda mfumo wa lugha wa mawasiliano.
Chomsky (1957) aliunga mkono mtazamo huu. Katika kuifafanua lugha, alitofautisha hali ya umilisi na utendaji. Umilisi ni kile ambacho mzungumzaji anafahamu kuhusu lugha yake. Uwezo huu humwezesha kuelewa na kutoa sentensi nyingi jinsi anavyotaka kuwasiliana. Huku ni kufahamu kanuni zinazoitawala lugha husika na uwezo huu umo akilini mwake.
Utendaji ni jinsi mzungumzaji anavyoitumia lugha.
Kutokana na maelezo haya ni kama Chomsky anatueleza kwamba tusiichunguze lugha katika matumizi yake, au hata jinsi tunavyojifunza lugha, bila kwanza kufahamu lugha ni nini. Anaona kuwa kazi ya mwanaisimu ni kuandika au kutunga sarufi na kukuza uelewa wetu wa lugha.
Kuna wataalamu ambao wamepinga msimamo huu. Kwa mfano, Labov anaiona sarufi kama mali ya kikundi/jamii au jumuia lugha na wala si mali ya kisaikolojia ya mtu binafsi. Hudson (1980:19) anaona kuwa mtazamo wa lugha usiohusisha jamii una upungufu. Nadharia fika ya lugha lazima itaje matumizi ya lugha hiyo. Anasema kuwa unweza kuitenga lugha na jinsi ya kwa nini inatumiwa.
Kwa hivyo lugha ni sehemu ya jamii.
Umilisi wa kimawasiliano hauhusu tu kufahamu mfumo wa lugha, bali pia ni nini unachosema na kwa nani, na namna utakavyokisema katika muktadha fulani. Unashughulikia ujuzi wa kijamii na kitamaduni ambao hudhaniwa kuwa wazungumzaji wanao unaowawezesha kufasiri mifumo ya kiisimu.
Fonolojia, sintaksia na msamiati ni sehemu tu ya vipashio vinavyotumiwa katika mawasiliano. Pamoja na hivyo lazima kuwepo semantiki, muktadha na kwa jumla mtazamo wa kijamii wa lugha.
Hivyo basi ufafanuzi wa Chomsky wa lugha una upungufu kwani unaichukulia lugha kama kitu kinachojitosheleza. Unaiondoa lugha kutoka kwenye jamii. Hapa ndipo isimujamii inapoingilia ili ilete kipengele cha jamii katika lugha.
Mtazamo wa pili wa lugha ni wa kiisimujamii. Mtazamo huu unaangalia lugha kama sehemu ya utamaduni wa jamii ulio na ruwaza ambazo hurithishwa na watu wenyewe kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mtazamo huu unaichukulia lugha kama mali ya jamii. Wanaisimujamii wanakubaliana na fasiri hii ya pili ya lugha.
Zoezi
Isimu jamii ni nini
Taja mikabala mitatu ya isimujamii na uoneshe kwa kutoa mifano jinsi inavyoingiliana na kutofautiana.
Eleza uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
Isimujamii ni taaluma inayoingiliana na taaluma nyingi katika jamii.
Fafanua kauli hii.
Muhtasari
Katika somo hili, tumeeleza maana ya isimu jamii na mambo haya
yamezingatiwa;
Tumeonesha mikabala mitatu ya isimujamii.
Tumeonesha uhusiano uliopo kati ya lugha na jamii.
Tumeonyesha jinsi isimujamii inavyoingiliana na taaluma nyingine. Tumeeleza mitazamo miwili ya lugha kwa kuzingatia maoni ya wataalamu mbalimbali.
Dik, S.C. (1978) Functional Grammar. North. Holland Linguistics Series North Holland Publishing Company. New York.
Fishman, J.A. (1967) Sociolinguistics and the Language Problems of Developing Countries katika Fishman, J.A. et.al. (eds.) Language Problems of Developing Nations.
John Wiley and Sons. Inc. London. (1972) Domains and the Relationship between Micro and Macro Sociolinguistics katika Gumperz, John & Dell Hymes (eds.)
Directions in Sociolinguistic: The Ethnography of communication. Basil Blackwell.oxford.
Greenberg, J.H. (1957) Essays in Linguistics, Chicago: Phoenix Boo.
Hudson, R. (1980) Sociolinguistics: Cambrdige, University Press, Cambridge.
Hymes, D. (1974) Foundations in Sociolinguistics: University of Pennyslavania Press, Philadelpia.
Labov (1980) (Mhr.) Locating Language in Time and Space. Academic Press. New York.
Mesthrie, R. et.al. (2000) Introducing Sociolinguistics. Edinburgh University Press, Edinburgh.
Msanjila, Y.P. (1995) Mawanda ya Isimu Jamii katika Mbogo, E. na McOnyango,O. (wahariri) Baragumu Juzuu la 2 Nam.1 & 2 Uk. 65-71, Chuo Kikuu Maseno.
Pride, J. G. & Holmers J. (eds.) (1972) Sociolinguistics Harmondsworth: Penguin.
Wardhaugh, R. (1992) An Introduction to Sociolinguistics. Blackwell.
Whorf, B.L. (1956), Language, Thought and Reality: Selected Writings, J.B. Carroll (ed). Cambridge, MA:MIT press